Nakusalimu katika jina kuu la mwokozi wetu Yesu Kristo. Karibu tuyatafakari maneno ya uzima.
Tukimtafakari Yesu, jinsi alivyopendwa na Mungu kiasi cha kukabidhiwa vyote na Baba, jinsi alivyojaliwa kutenda miujiza mikubwa ambayo hata vitabu vyote duniani vingeandika habari zake visingetosha kueleza biblia inasema hivyo, tunatamani sana kuwa kama yeye. Yesu ni mtu pekee ambaye alikuwa akimwomba Mungu kitu chochote anapewa saa hiyo hiyo, Lakini mwisho wa siku anakuja kutoa siri ya kukubaliwa kwake..Siri ambazo anasema manabii wengi na wafalme walitamani kuyafahamu hayo wasiyafahamu(Luka 24:10). Lakini mimi na wewe tunazifahamu.
Na siri mojawapo ni hii inayohusiana na namna ya kudili na maadui zetu na wale wanaotuudhi. Alisema hivi,
Mathayo 5:44 “lakini mimi nawaambia, Wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi”,
Mwanzoni nilipokuwa nasoma huu mstari nilidhani nimeulewa vizuri, lakini baadaye nilikuja kujua kimatendo kuwa nipo mbali sana nao, nilipotafakari matukio ambayo niliudhiwa na watu, Na muda niliotenga kuwaombea hao watu walioniudhi na kunichukia.. Nikagundua kuwa sijawahi kufanya hivyo.
Ni kweli nilisamehe, lakini kusamehe kwangu kuliishia tu katika ‘kusamehe’ na baada ya hapo ikawa ni kujiepusha naye ili asiniudhi tena. Lakini kwa Mungu huo bado sio ukamilifu, Ukamilifu ni kumwombea huyo anayekuudhi.. Na Zaidi sana kumpenda yule ambaye unahisi ni adui kwako.
Bwana wetu Yesu Kristo ni mtu aliweza kuishi kile alichokisema, Vinginevyo angekuwa ni mnafki.. Yeye ni mtu ambaye aliweza kuishi na mmoja wa maadui zake hatari sana. Adui aliyemuuza mbele ya macho yake. Na huyo si mwingine Zaidi ya Yuda. Yesu alimjua tangu mwanzo kuwa ndiye atakayemsaliti, Lakini hakuwahi kumfukuza, hakuwahi kumnenea mabaya, Zaidi sana alimwita RAFIKI, na pale alipokula chakula kizuri alimchagua Yuda kula naye(Yohana 13:18).. Na tunajua Yesu si mnafki, alipomwita Yuda rafiki(Mathayo 26:50), alimaanisha kweli, kwamba yule alikuwa ni rafiki yake tena hata Zaidi ya mitume wengine.
Tengeneza picha Japo Yesu alijua unafiki wake, lakini ndani yake hakukuwa na sababu ya kutomwona kama yeye ni rafiki tu. Aliweza kuishi naye miaka yake yote ya kiutumishi, akamwongezea na neema juu ya kutoa Pepo na kufanya miujiza. Alipopanda kuwaombea wanafunzi wake, alimwombea na Yuda pia, japokuwa alijua kuwa huyo ndiye msaliti wake. Yuda hakuwahi kumrudishia fadhili Yesu wakati wowote, hata kipindi kile yule mwanamke anamwagia marahamu, yeye bado alipinga. Lakini Yesu alimpenda.
Tujiulize na sisi tuliookoka tunaweza kuwa kama mwana wa Mungu Yesu Kristo. Kuishi na maadui zetu tunaojua wanakwenda kutuchinja na Zaidi sana tunawaombea na kuwabariki? Huo ndio ukamilifu ambao Mungu anataka kuuona kwetu.
Hii ndio sababu kwanini Yesu anasema tuwe watu wa namna hiyo na si vinginevyo anasema..
Mathayo 5:45 “ili mpate kuwa wana wa Baba yenu aliye mbinguni; maana yeye huwaangazia jua lake waovu na wema, huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki”.
Umeona? Kwasababu tabia ya Mungu ndio hiyo, anawarehemu watu wote, wanaomshukuru na wasiomshukuru, hata maadui zake, anawapa chakula. Kwasababu anajua huwenda siku moja watatubu. Hata sisi pia kabla ya kuokolewa, tulikuwa katika dhambi, tulimkosea sana yeye, lakini hakututendea jambo lolote baya, akatusamehe,. Vivyo hivyo anataka na sisi tufanye kwa maadui zetu, na kwa wale wanaotuchukia.
Ikiwa ni mfanyakazi wako anakuudhi, chukuliana naye tu..Hamna namna, mwombee, mbariki, usiwe mwepesi kumfukuza kazi. Ikiwa ni mpendwa mwenzako anakukwaza mara kwa mara, hupaswi kumsamehe tu na kujiepusha naye mbali, bali umwombee, na Zaidi umwite rafiki yako.
Tabia kama hii, haitokani na sisi wanadamu bali na Mungu, kwa nguvu zetu hatutaweza, lakini tukiwa na Neno la Mungu sana mioyoni mwetu, atatusaidia kuidhihirisha tabii yake hii ya kiMungu. Na kama tukifaulu kushinda, Basi tujue ndivyo Baba atakavyotukaribia, na kujifunua kwetu. Kwasababu tunafanya yanayompendeza.
Hivyo, tumwombe Bwana atusaidie, na sisi tuonyeshi bidii katika kudhihirisha jambo hilo, ili tuwe wakamilifu kama yeye alivyomkamilifu.
Tahadhari:
Epuka mahubiri, unayoambiwa walete maadui zako hapa tuwapige kwa moto wa Roho Mtakatifu wafe. Epuka sana, hayo hayakusaidii kitu Zaidi sana yanakuongezea chuki na visasi moyoni mwako. Ambayo ni zao la shetani na sio Roho Mtakatifu. Bali penda ushauri wa Bwana Yesu, kisha uutende hata kama ni mgumu, lakini ndio njia yenyewe ya kumfikia Mungu, hakuna nyingine.. Wapende maadui zako, kisha waombee
Bwana akubariki.
Shalom.
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp: Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
Mada Nyinginezo:
RACA
UMUHIMU WA KUBATIZWA.
USIMPELEKEE BWANA MASHITAKA, YA MAADUI ZAKO.
YAFAHAMU MAPENZI KAMILI YA MUNGU KWA MAADUI ZAKO.
MPENDEZE MUNGU ZAIDI.
BWANA UNIJULISHE MWISHO WANGU.
FAHAMU MAISHA YA YESU KABLA YA HUDUMA.
Mimbari ni nini? Je tofauti kati ya Mimbari na madhabahu ni ipi?
Rudi nyumbani
Print this post