HIZI NI NYAKATI ZA KUJIINGIZA KWA NGUVU.

HIZI NI NYAKATI ZA KUJIINGIZA KWA NGUVU.

Luka 16:16 “Torati na manabii vilikuwapo mpaka Yohana; tangu wakati huo habari njema ya ufalme wa Mungu hutangazwa, na kila mtu hujiingiza kwa nguvu”.

Nataka uone hicho kifungu cha mwisho, “ Na kila mtu hujiingiza kwa nguvu”..

Bwana Yesu alipotoa habari hiyo, kulikuwa na sababu kubwa kwanini alianza kwanza na habari za agano la kale(Torati na manabii) kisha akaja kwenye agano jipya, na kumalizia kwa kusema, tangu huo wakati kila mtu atakawa anajiingiza kwa nguvu.

Alisema hivyo kuonesha kuwa hapo kabla, kulikuwa hakuhitaji bidii yoyote, au jasho lolote, au nguvu yoyote, kuijua torati, lakini kuanzia wakati wa Yohana, injili ya kweli ambayo inaleta ondoleo la dhambi, ilipoanza kuhubiriwa, injili ya kumfanya mtu awe na maarifa kamili kumuhusu Mungu ilipoanza kuhubiri, injili inayomfungua mtu kweli kweli, basi vipingamizi vikubwa sana vitanyanyuka kiasi kwamba, mpaka mtu aipate ni lazima atumie nguvu nyingi sana kuingia, tofauti na ilivyokuwa hapo mwanzo.

Kwamfano utaona wakati ule tu, kulikuwa na mafarisayo na waandishi, ambao wamesimama hapo, katikati kuhakikisha kuwa mtu yeyote atakayemkiri Yesu hadharani, moja kwa moja atatengwa na sinagogi, (Yohana 9:22)

Na kutengwa kwa zamani sio kama sasa, zamani ukitengwa na sinagogi ni jamii nzima ya Israeli imekutenga mpaka familia yako. Hata misaada ya kijamii ulikuwa hupati, Hivyo suala la kutengwa lilikuwa ni jambo zito sana.

Hivyo haikuwa ni rahisi, hata kidogo, ilibidi watu walazimishe, mambo kwa nguvu, wawe radhi kutengwa tu, wawe tayari kupoteza mahusiano yao tu, lakini wasiukose ufalme wa mbinguni.

Mambo hayo hayo hata sasa, yanaendelea, kuupata ufalme wa mbinguni, ni kujiingiza kwa nguvu nyingi, wapo viongozi wako wa dini wanakuzuia usiokoke, kisa tu imani yao haimini kile biblia inachosema, pengine Imani yao inafundisha kusujudia sanamu, haiamini katika karama za Roho, ndugu usiwaangalie hao, wewe jiingize kwa nguvu katika ufalme wa Mungu,.

Hao ni wale wana-sheria wa dini, ambao Bwana Yesu anasema, kazi yao ni kusimama pale mlango kushikilia funguo, kuwazuia watu wasiingie, na wao wenyewe hawauingii, wanataka mkae wote katika giza la milele pamoja..

Luka 11:52 “Ole wenu, enyi wana-sheria, kwa kuwa mmeuondoa ufunguo wa maarifa; wenyewe hamkuingia, na wale waliokuwa wakiingia mmewazuia”.

Hivyo usiwaangalie hao hata kidogo, achana na mapokeo ya dini, tubu dhambi uokoke, tafuta ubatizo sahihi wa kuzamishwa katika maji mengi (Yohana 3:23), na kwa jina la YESU KRISTO sawasawa na Matendo 2:38, na sio ule wa kunyunyiziwa ambao haupo katika maandiko.

Jiingize kwa nguvu, hata kama ndugu zako hawakuelewi, Jiingize kwa nguvu hata kama marafiki zako watakuona mshamba, jipenyeze kwa nguvu hata kama dunia itakuona umerukwa na akili..Iokoe roho yako, wakati huu jiepushe na mtu ambaye unaona kabisa anaizuia njia yako ya wokovu.

Wenyewe hawawezi kuona hilo, kwasababu bado wapo gizani, lakini wewe umeiona nuru, usijifananishe na wao, zidi jenga uhusiano wako binafsi ya Yesu. Hizi ni nyakati za mwisho na unyakuo upo karibu sana,

Mathayo 11:12 “Tangu siku za Yohana Mbatizaji hata sasa ufalme wa mbinguni hupatikana kwa nguvu, nao wenye nguvu wauteka.

13 Kwa maana manabii wote na torati walitabiri mpaka wakati wa Yohana”.

Isiishi kwa kuwapendezesha watu na huku umelisahau Neno, kwasababu kila mtu atalibeba furushi lake mwenyewe (Wagalatia 6:5). Dakika hizi za majeruhi, zinafananishwa na Sodoma na Gomora, ambazo tunajua ni watu 3 tu kati ya mamilioni waliokuwa katika miji ile ndio waliopona….Ndivyo itakavyokuwa siku hizi, litavuka kundi dogo tu, lililoweza kujiingiza kwa nguvu katika ufalme wa mbinguni bila kujali vizuizi vya mpito vya ibilisi.

Unadhani shetani, hajui kuwa mtu akiupata ufalme wa Mungu, amepata kitu cha thamani kubwa sana, anajua hilo, na ndio maana lazima akuletee ugumu ili usijaribu kuuingia, ubakie kwenye giza huko huko..Hivyo vitisho kutoka kwa viongozi wako wa dini na ndugu na marafiki, visikufanye usichukue uamuzi wa kumpokea Yesu.

Mathayo 10:34 “Msidhani ya kuwa nimekuja kuleta amani duniani; la! Sikuja kuleta amani, bali upanga.

35 Kwa maana nalikuja kumfitini mtu na babaye, na binti na mamaye, na mkwe na mkwe mtu;

36 na adui za mtu ni wale wa nyumbani mwake.

37 Apendaye baba au mama kuliko mimi, hanistahili; wala apendaye mwana au binti kuliko mimi, hanistahili.

38 Wala mtu asiyechukua msalaba wake akanifuata, hanistahili.

39 Mwenye kuiona nafsi yake ataipoteza; naye mwenye kuipoteza nafsi yake kwa ajili yangu ataiona”.

Kama bado hujafanya uamuzi huo basi anza sasahivi, wokovu unapatikana bure, lakini si rahisi si rahisi lakini inahitaji nguvu kujiingiza kwa huo, hivyo jiingize kwa nguvu bila kujali, na huko huko Bwana Yesu atajifunua kwako kwa namna ambayo hukuwahi kumjua hapo kabla, ndipo utakapomjua Mungu, na ndipo atakapotembea na wewe.

Maran Atha.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312


Mada Nyinginezo:

USIUZE URITHI WAKO.

Je! Kiongozi wa dini anaouwezo wa kusamehe dhambi?

KANUNI RAHISI YA KUFANIKIWA.

JIHADHARI NA KUOSHWA MIGUU ISIVYOPASWA.

MWANANCHI WA UFALME WA MBINGUNI

USIISHI BILA KUIFANYA KAZI YA MUNGU KABISA..

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments