Ni mistari ipi shetani anapenda kuitumia kuwaangusha watu waliosimama?
Shetani akitaka kumwangamiza mtu aliye mwamini Mungu, anachofanya ni anamchukua na kumpeleka juu sana,.. hamwachi pale alipo, kwasababu anajua mtu aliye chini hata akinguka, ataumia kidogo tu, lakini bado akawa na uwezo wa kusimama na kuendelea mbele tena..Badala yake anachokifanya yeye ni anamchukua na kumpelekea juu sana kwenye kilele cha mnara, mahali ambapo anajua akifanya kosa kidogo tu, na kuteleza basi habari yake ndio inakuwa imeishia pale pale…
Ndivyo alivyofanya kwa Bwana wetu Yesu, alimnyanyua na kumpeleka juu sana kwenye kilele cha hekalu,..Na wakati anampandisha, akaanza kumuhubiria Zaburi ya 91 moyoni mwake (Hii ndio zaburi shetani anayoitumia sana kama silaha yake)…
Inayozungumzia jinsi Mtu yule aliyekubaliwa na Mungu anavyopokea ulinzi wa kipekee kutoka kwa Mungu, haijalishi itakuwa ni wakati wa mchana au wa usiku, haijalisha atakuwa anazungukwa na magonjwa ya hatari kiasi gani ambayo ni tuishio katika dunia yaliyowaangamiza watu makumi elfu, lakini kwake yeye hayatamgusa hata moja..Jinsi mtu huyo anavyofunikwa chini ya mbawa zake ili mabaya yasimpate.. jinsi atakavyowekwa mahali pa juu..jinsi atakavyowakanyaga simba na majoka, na jinsi Mungu atakavyomtumia malaika zake wamlindie njia zake zote, asiteleze….
Kwa muda wako pitia zaburi yote ya 91, uone jinsi inavyouzungumzia ulinzi wa kipekee anaoupokea Mtu yule aliyekubalika na Mungu..lakini hapa tutatazama tu vifungu vichache..
Zaburi 91:10 “Mabaya hayatakupata wewe, Wala tauni haitaikaribia hema yako. 11 KWA KUWA ATAKUAGIZIA MALAIKA ZAKE WAKULINDE KATIKA NJIA ZAKO ZOTE. 12 MIKONONI MWAO WATAKUCHUKUA, USIJE UKAJIKWAA MGUU WAKO KATIKA JIWE. 13 Utawakanyaga simba na nyoka, Mwana-simba na joka utawaseta kwa miguu. 14 Kwa kuwa amekaza kunipenda Nitamwokoa; na kumweka palipo juu, Kwa kuwa amenijua Jina langu. 15 Ataniita nami nitamwitikia; Nitakuwa pamoja naye taabuni, Nitamwokoa na kumtukuza; 16 Kwa siku nyingi nitamshibisha, Nami nitamwonyesha wokovu wangu”.
Zaburi 91:10 “Mabaya hayatakupata wewe, Wala tauni haitaikaribia hema yako.
11 KWA KUWA ATAKUAGIZIA MALAIKA ZAKE WAKULINDE KATIKA NJIA ZAKO ZOTE.
12 MIKONONI MWAO WATAKUCHUKUA, USIJE UKAJIKWAA MGUU WAKO KATIKA JIWE.
13 Utawakanyaga simba na nyoka, Mwana-simba na joka utawaseta kwa miguu.
14 Kwa kuwa amekaza kunipenda Nitamwokoa; na kumweka palipo juu, Kwa kuwa amenijua Jina langu.
15 Ataniita nami nitamwitikia; Nitakuwa pamoja naye taabuni, Nitamwokoa na kumtukuza;
16 Kwa siku nyingi nitamshibisha, Nami nitamwonyesha wokovu wangu”.
Unaona? sasa Wakati anampandisha juu sana, alikuwa anamthibitishia mistari hiyo kichwani pake..Na kweli shetani alichokuwa anamwambia Bwana ni sahihi kabisa, lakini sio katika mazingira yale..Na alipomfikisha pale juu sasa, ndipo akamwambia huu ni wakati wa wewe kujitupa chini kwasababu Bwana Mungu wako amekupenda na kukuthibitisha, hakuna baya lolote litakaloweza kukupata …. Hivyo usiogope kujitupa chini kwasababu malaika zake wapo kila mahali ili Wakulinde katika njia zako zote. Na Mikononi mwao watakuchukua, Usije ukajikwaa mguu wako katika jiwe
Unaweza kudhani alimaanisha jitupe tu chini kikawaida peke yake, La, sio hivyo tu.. shetani alimaanisha pia dondoka, kutoka katika msimamo wako wa Imani kidogo tu. Ukifanya hivyo Mungu wa mbinguni hatakuacha uangamie kabisa kwani atakutumia malaika zake ili kukurudisha pale ulipokuwa.
Lakini shetani alijua kitakachofuata baada ya pale ni nini..kwasababu alishawahi kuwaangusha watu wengi kwa njia hiyo hiyo akadhani itakuwa hivyo pia na kwa Bwana wetu Yesu Kristo.
Lakini Bwana alimwambia Neno fupi tu..Imeandikwa “Usimjaribu Bwana Mungu wako”.
Kama wewe ni umesimama katika wokovu, nataka nikuambie, katika mahali ambapo unapaswa uwe napo makini basi ni hapa..
Kwenye mahubiri yanayokuaminisha kwamba wewe umekubaliwa na Mungu wakati wote.., na hivyo unaoulinzi wa kipekee kutoka kwake.. kama hujui hiyo ndio mistari shetani anayoipenda kuitumia kuliko mistari mingine yeyote ili kukuangusha wewe uliyesimama..
Ni kweli Mungu ameahidi kufanya hivyo lakini ni kwanini aje kukuhubiria hivyo hivyo kila siku , hakuhubirii habari nyingine za kumcha Mungu? …Jiulize kwanini shetani hakumwambia Bwana, kwa maana imeandikwa mpende Bwana Mungu wako, kwa moyo wako wote, kwa akili zako zote, na kwa nguvu zako zote…Badala yake anamwambia kwa kuwa imeandikwa atakuagiza malaika zake wakulinde, usiteleze….Utaona Ni mistari ya kusifiwa tu, na kufarijiwa tu na ya kutoa sifa tu ili ujione wewe ni kitu Fulani mbele za Mungu…hata kama utakuwa katika mahusiano mabaya na Mungu, atakuletea tu hiyo mistari..
Na kibaya Zaidi siku hizi za mwisho mafundisho ya namna hii ndio yanapewa kipaumbele, pale tunapohubiriwa kwamba Mungu ametukubali, Mungu ametuweka juu, hatutakwenda chini, maadui zetu watashindana wala hawatashinda, watakuja kwa njia moja lakini watatoweka kwa njia saba….mahubiri kama haya tunayapenda, ni kweli ni maneno ya Mungu lakini kumbuka hayo ndiyo yanayokupeleka katika kilele cha hekalu ili kukuangamiza kama hutakuwa makini..
Sasa ukiwa katika kilele cha mahubiri kama hayo, hutaki kusikia kingine chochote, hapo ndipo ibilisi anakuletea mambo maovu, kwasababu shetani alishakujaza ujasiri wote kuwa wewe ni mteule wa Mungu, huwezi kupotea?, Inakuwa ni rahisi kwako wewe kwenda kufanya uzinzi, kwasababu shetani ndani anakuhubiria na kukwambia Mungu anaelewa, bado anakupenda, ulishaokoka,atakulinda..Mungu haangalii mavazi yako, haangalii vimini vyako, anaangalia moyo wako, wewe ni mshindi tayari usikubali kushindwa…hata ukiendelea tu kuvaa uchi uchi na kutembea barabarani, haina shida wewe ni mtoto wa Mungu.
Kumbe hujui ndio ndio unaukaribia mwisho wako..Ukiingia huko ndio moja kwa moja, utakuwa umeshateleza na kuanguka kama yeye alivyoanguka alivyoasi zamani, Na mpaka utakapofika chini tayari umeshakuwa mfu rohoni..hufai tena.
Hizi ni siku za mwisho. Utakatifu hauhubiriwi, bali maneno ya kututia faraja tu, ya kutufanya tujione kuwa sisi tumekubaliwa na Mungu, ili kwamba tuendelee kustarehe katika dhambi zetu..
Waebrania 12:14 “Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote, NA HUO UTAKATIFU, ambao hapana mtu atakayemwona Bwana asipokuwa nao”
Bwana atusaidie.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312
Mada Nyinginezo:
JINSI WATU WANAVYOZAMA KATIKA USHIRIKINA NA UCHAWI.
JE! UMEFANYIKA KUWA MWANAFUNZI WA BWANA?
VITABU VYA BIBLIA: Sehemu ya 6
MJUMBE WA AGANO.
NIFANYE NINI ILI NILITIMIZE KUSUDI LA MUNGU.
Rudi Nyumbani:
Print this post