Title Devis

Kwa mpotovu utajionyesha kuwa mkaidi, maana yake nini? (Zab.18:26)

Swali: Je Mungu ni mkaidi kulingana na Zaburi 18:26, au kwanini Mungu aseme maneno hayo?


Jibu: Tuanzie kusoma ule mstari wa 24, ili tupate maana kamili..

Zaburi  18:24 “Mradi Bwana amenilipa sawasawa na haki yangu, Sawasawa na usafi wa mikono yangu mbele zake.

25 Kwa mtu mwenye fadhili UTAKUWA MWENYE FADHILI; Kwa mkamilifu utajionyesha kuwa mkamilifu;

26 KWAKE AJITAKASAYE UTAJIONYESHA KUWA MTAKATIFU; Na KWA MPOTOVU UTAJIONYESHA KUWA MKAIDI”

Hapo anasema kwa mtu mwenye fadhili Bwana atajionyesha mwenye fadhili kwake, na kwa ajitakasaye Bwana atajionyesha ni mtakatifu kwake, vile vile na kwa mpotovu atajionyesha mkaidi.

Sasa kwa maneno hayo haimaanishi kuwa Bwana ni MKAIDI..La! yeye ni mwema siku zote na hawezi kufananishwa na sisi wanadamu…Lakini sasa swali ni kwanini aseme hivyo?

Ili tuelewe vizuri tafakari mfano huu; Unaye mtoto halafu ukaanza kuona anaonyesha tabia za kukosa nidhamu, na anafanya mabaya mengi, na ulipomwonya haonyeki, kisha ukaamua kumwambia kuwa endapo akiendelea kuwa na tabia hiyo, utakuwa mbaya kwake!..na akibadilika kuwa mzuri basi utakuwa mzuri kwake…

Je kwa kauli hiyo utakuwa umemaanisha kuwa wewe ni ni MTU MBAYA na MWOVU?.. bila shaka hutakuwa umemaanisha hivyo, bali utakuwa umemaanisha kuwa endapo akiendelea kufanya mabaya, basi utambadilikia na kumwadhibu, jambo ambalo ni baya machoni pa huyo mtoto, na ndicho Bwana Mungu alichomaanisha hapo kuwa kwa “mtu mpotovu atajionyesha kuwa Mkaidi”… Na si kwamba MUNGU ni Mkaidi.

Kwamba kwa mtu anayefanya mabaya Bwana na maovu na hakubali kuonyeka basi atapata mabaya kutoka kwa Mungu, kwani BWANA atamwadhibu,…Na adhabu za Bwana ni za lengo la kuonya, na kumfanya mtu aache njia mbaya, na si za kumpoteza mtu.

Waebrania 12:10 “Maana ni hakika, hao kwa siku chache waliturudi kama walivyoona vema wenyewe; bali yeye kwa faida yetu, ili tuushiriki utakatifu wake.

11 Kila adhabu wakati wake haionekani kuwa kitu cha furaha, bali cha huzuni; lakini baadaye huwaletea wao waliozoezwa nayo matunda ya haki yenye amani.

12 Kwa hiyo inyosheni mikono iliyolegea na magoti yaliyopooza,

13 mkaifanyie miguu yenu njia za kunyoka, ili kitu kilicho kiwete kisipotoshwe, bali afadhali kiponywe.

14 Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote, na huo utakatifu, ambao hapana mtu atakayemwona Bwana asipokuwa nao”

Na kinyume chake ni kweli, kwa mtu ajitakasaye, yeye Bwana atajionyesha mtakatifu kwake, Maana yake ataona mema mengi kutoka kwa Bwana..

Hivyo hiyo ni tahadhari kwetu na pia ni faraja kwetu, kwamba tukae katika usafi na utakatifu, ili tuuone wema wa Mungu, na tusikae katika upotovu, tusije tukauona ukaidi wa MUNGU, kwani Bwana atajionyesha kwa kila mtu sawasawasa na matendo yake.

Zaburi  18:24 “Mradi Bwana amenilipa sawasawa na haki yangu, Sawasawa na usafi wa mikono yangu mbele zake.

25 Kwa mtu mwenye fadhili UTAKUWA MWENYE FADHILI; Kwa mkamilifu utajionyesha kuwa mkamilifu;

26 KWAKE AJITAKASAYE UTAJIONYESHA KUWA MTAKATIFU; Na KWA MPOTOVU UTAJIONYESHA KUWA MKAIDI”

Bwana atusaidie.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

ZIKUMBUKE FADHILI ZA MUNGU

Kama ulimwengu ujao utakuwa na watakatifu tu, sasa hao watakaotawaliwa watatoka wapi?

TAA YA MWILI NI JICHO

TULITAFUTE KWA BIDII TUNDA LA ROHO.

Mwandishi na Uchambuzi wa kitabu cha Wakorintho wa pili (2Wakorintho)

Rudi Nyumbani

Print this post

Uchambuzi na mwandishi wa kitabu cha pili cha  Petro (2Petro).

Kama kitabu kinavyojitambulisha, “Waraka wa pili wa Petro kwa watu wote”

Petro ndiye mwandishi. Ni waraka mfupi, aliouelekeza kwa watakatifu wote duniani.

Na haya ndio maudhui yake makuu; 

  1. Kuwahimiza wakristo kuendelea kukua katika Imani.
  2.  Kuwathibitishia watakatifu ushuhuda wao kwamba haukutokana na hadithi za kutungwa kwa werevu bali ushuhuda wa macho.
  3. Kuwaonya wajiepushe udhalimu wa  manabii wa uongo.
  4.  Halikadhalika kuwapa tumaini juu ya ujio wa Bwana Yesu Kristo.
  5.  Na Uthabiti wa nyaraka za mitume kwao.

Haya ndio maelezo ya kila kipengele kwa ufupi;

1) Himizo la Ukuaji wa kiroho.

Petro anawahimiza watakatifu wasikwamwe kiroho bali waendelee kukua, mpaka kufikia utimilifu wao ambao ni upendo, Na kwamba mtu asipojitahidi kufanya hivyo matokeo yake ni kuwa atakuwa mvivu, na hatimaye atajikwaa.

 

2 Petro 1:3-8

[3]Kwa kuwa uweza wake wa Uungu umetukirimia vitu vyote vipasavyo uzima na utauwa, kwa kumjua yeye aliyetuita kwa utukufu wake na wema wake mwenyewe. 

[4]Tena kwa hayo ametukirimia ahadi kubwa mno, za thamani, ili kwamba kwa hizo mpate kuwa washirika wa tabia ya Uungu, mkiokolewa na uharibifu uliomo duniani kwa sababu ya tamaa. 

[5]Naam, na kwa sababu iyo hiyo mkijitahidi sana kwa upande wenu, katika imani yenu tieni na wema, na katika wema wenu maarifa, 

[6]na katika maarifa yenu kiasi, na katika kiasi chenu saburi, na katika saburi yenu utauwa, 

[7]na katika utauwa wenu upendano wa ndugu, na katika upendano wa ndugu, upendo. 

[8]Maana mambo hayo yakiwa kwenu na kujaa tele, yawafanya ninyi kuwa si wavivu wala si watu wasio na matunda, kwa kumjua Bwana wetu Yesu Kristo. 

 

2) Uthibitisho wa ushuhuda wao.

Mtume Petro anatoa hakikisho la ushuhuda wao juu ya ujio wa Kristo, kwamba hawakuupokea katika hadithi zilizotungwa kwa werevu, bali walishuhudia wao wenyewe kwa macho, walipotokewa na Musa na Eliya juu ya mlima ule mrefu na kuisikia sauti ya Mungu mbinguni  moja kwa moja ikimshuhudia Yesu kuwa ndiye mwana wa Mungu, aliyependwa naye.

 

2 Petro 1:16-17

[16]Maana hatukufuata hadithi zilizotungwa kwa werevu, tulipowajulisha ninyi nguvu zake Bwana wetu Yesu Kristo na kuja kwake; bali tulikuwa tumeuona wenyewe ukuu wake. 

[17]Maana alipata kwa Mungu Baba heshima na utukufu, hapo alipoletewa sauti iliyotoka katika utukufu mkuu, Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye. 

[18]Na sauti hiyo sisi tuliisikia ikitoka mbinguni tulipokuwa pamoja naye katika mlima ule mtakatifu. 

 

3) Tahadhari dhidi ya manabii wa uongo.(2:1-22)

Lakini pia anawahimiza kujiepusha na manabii wa uongo, ili  wasije wakachukuliwa na makosa Yao, wakaangamia tena. Ambao sifa zake nyingi ameziorodhesha pale (kwenye sura yote ya pili), Sifa zao ni pamoja na tamaa na uzinzi, akiwataja kama watu wasiokoma kutenda dhambi, wasaliti wa Bwana, wenye uhodari wa kutunga maneno wenye werevu, ili wawavute watu kwao, wenye kupenda ujira wa udhalimu kama Balaamu, watoao maneno ya makufuru, watu wa kujikinai, wasio na hofu ya Mungu, watu wa anasa, wa kuhadaa watu waliosimama imara, ili wawaaungushe.

2 Petro 3:17

[17]Basi, wapenzi mkitangulia kujua hayo, jilindeni nafsi zenu, msije mkachukuliwa na kosa la hao wahalifu mkaanguka na kuuacha uthibitifu wenu. 

 

4) Tumaini juu ya ujio wa Yesu Kristo.

Petro pia anawahimiza watakatifu wawe na tumaini juu ya uthabiti wa kurudi kwa Bwana,

akiwatahadharisha juu ya kuibuka kwa kundi la watu wenye kudhihaki, wanaosema iko wapi ile ahadi,mbona muda mrefu umepita? lakini Petro analirekebisha kwa kulitolea maelezo kuwa Mungu hakawii kutimiza ahadi yake bali anavumilia ili watu wote wafikie toba. Lakini siku hiyo itakuja kama mwizi, na ulimwengu ukaliwao na waovu utaharibiwa.

2 Petro 3:9-13

[9]Bwana hakawii kuitimiza ahadi yake, kama wengine wanavyokudhani kukawia, bali huvumilia kwenu, maana hapendi mtu ye yote apotee, bali wote wafikilie toba. 

[10]Lakini siku ya Bwana itakuja kama mwivi; katika siku hiyo mbingu zitatoweka kwa mshindo mkuu, na viumbe vya asili vitaunguzwa, na kufumuliwa, na nchi na kazi zilizomo ndani yake zitateketea. 

[11]Basi, kwa kuwa vitu hivi vyote vitafumuliwa hivyo, imewapasa ninyi kuwa watu wa tabia gani katika mwenendo mtakatifu na utauwa, 

[12]mkitazamia hata ije siku ile ya Mungu, na kuihimiza; ambayo katika hiyo mbingu zitafumuliwa zikiungua, na viumbe vya asili vitateketea na kuyeyuka? 

[13]Lakini, kama ilivyo ahadi yake, mnatazamia mbingu mpya na nchi mpya, ambayo haki yakaa ndani yake. 

 

5) Uthibitisho wa nyaraka za mitume. (3:15-18)

Mwisho, mtume Petro anaeleza uthabiti wa yale anayowaeleza, akiwatolea mfano kwa kurejea pia nyaraka za mitume wengine (akimtaja Paulo).Kama pia anayaeleza mambo hayo hayo ayasemayo katika nyaraka zake.

Petro 3:15-16

15 Nanyi uhesabuni uvumilivu wa Bwana wetu kuwa ni wokovu, kama vile na ndugu yetu mpenzi
Paulo alivyowaandikia kwa hekima aliyopewa;
16 vile vile kama katika nyaraka zake zote pia, akitoa humo habari za mambo hayo; katika
nyaraka hizo yamo mambo ambayo ni vigumu kuelewa nayo; na mambo hayo watu wasio na elimu,
wasio imara, huyapotoa, kama vile wayapotoavyo na maandiko mengine, kwa uvunjifu wao
wenyewe.

Hivyo kwa ujumla maudhui ya waraka huu ni kuwahimiza watakatifu kufanya bidii katika ukamilifu na kujiepusha na manabii wa uongo, na kuchoka kungojea ahadi za Mungu. Bali waendelee mbele kutibitika katika ukamilifu bila wala wala hila hadi siku ya kutokea kwake Bwana Yesu mara ya pili.

Je wewe kama mkristo unayemngojea Bwana. Unafanya imara wito wako na uteule wako, kwa kukua kila siku katika neema kiasi cha kukufanya ujione huna mawaa wala aibu, katika siku ile ya Bwana? 

Kama sio, basi wakati ndio huu, Maanisha kugeukia kumfuata Kristo.

Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

Mwandishi na Uchambuzi wa kitabu cha kwanza cha Petro.(1Petro)

Fahamu Mwandishi wa kitabu cha Waebrania ni nani.

Mwandishi na uchambuzi wa kitabu cha Wakorintho wa kwanza (1Wakorintho)

Rudi Nyumbani

Print this post

Konstantino mkuu ni nani, na je anaumuhimu wowote katika ukristo?

SWALI: Konstantino mkuu ni nani, na je umuhimu wake katika ukristo ni upi?


JIBU: Konstantino mkuu ni Mmoja wa wafalme waliotawala chini ya dola ya Rumi, Kuanzia mwaka wa 306BK mpaka 337BK.

Dola hii ya Rumi ndiyo dola iliyokuwa na nguvu sana, zaidi ya zote zilizowahi kutokea katika historia, ilifanikiwa kutawala kikamilifu katika nyanja karibia zote, za kijeshi, kisiasi hadi kiuchumi, na ndio ngome iliyodumu kwa muda mrefu kuliko zote.

Itakumbukwa kuwa hata wakati Kristo anakuja duniani, dola hii ndio ilikuwa inatawala ulimwenguni kote na Kaisari ndiye aliyekuwa mfalme. Israeli wakati huo halikuwa taifa huru kama tunavyoliona sasa, bali ilikuwa koloni la Rumi, na watalawa na maliwali wake wote akiwemo, Pilato na Herode walikuwa ni Warumi.

Utawala huu ndio uliomsulubisha Kristo kwa shinikizo la wayahudi. Lakini tunaona katika historia, injili ilipoanza kuhubiriwa na jamii kubwa ya watu kugeuzwa kuwa wakristo duniani kote, Utawala huu ulianza kulitesa kanisa, na hata baadhi ya wafalme wao waovu waliotokea walitunga sheria kwamba ikionekana mtu yeyote anajiita mkristo, basi adhabu yake ilikuwa ni kifungo kama sio kifo.

Mfano wa watawala hawa alikuwa Nero, trajan, na Domitian, Na hiyo ilipelekea jamii kubwa sana ya wakristo kuuawa kikatili, wengine kuchomwa moto, wengine kusulubiwa, wengine kuwekwa katika viwanja vya mauaji na kuachiwa wanyama wakali wawaue, idadi ya mamilioni ya wakristo walipoteza maisha kwa njia hii. Historia hiyo utaipata vema katika kitabu maarufu kijulikanacho kama (Foxes book of martyrs). Kumbuka utawala uliohusika ulikuwa ni huu wa Rumi, chini ya watawala wao mbalimbali.

Hivyo kwa wakati wote huo ukristo ulionekana kama imani ya vikundi fulani vya wavuruga amani..

Wakati huo Rumi lilikuwa ni taifa la kipagani likiongozwa kisiasa, chini ya dini zao za miungu mingi.

Lakini alipokuja kutokea huyu mtawala mpya aliyeitwa Kostantino baada ya watawala 59 kupita nyuma yake,

Kwa mujibu wa ushuhuda wake anasema wakati anakwenda kupigana vita mojawapo kuu iliyomkabili, katika maono aliona..msalaba angani, akaambiwa kwa ishara hii utashinda. Hivyo Konstantino akaichukua nembo ya ukristo na kuipachika katika ngao za jeshi lake, na hivyo akashinda vita ile iliyokuwa inamkabili, ushindi huo ulimuimarishia sana ufalme wake.

Huo ndio ukawa mwanzo wake wa kuwa mkristo. Aliendelea kuupa sana kipaumbele ukristo, Kuanzia huo wakati ndio ukawa mwisho wa mauaji ya watakatifu. Na mwanzo wa dini ya Kikatoliki.

Lakini historia inaonyesha Konstantini hakuwa ameupokea ukristo katika ukamilifu wote, kama madhehebu baadhi yanavyoamini. Bali ukristo wake ulikuwa na msukumo wa kisiasi pia nyuma yake, ambao ulilenga kuwaunganisha wakristo na warumi wakipagani, kwasababu hakuacha pia kuabudu miungu yake ya kirumi. Ndio maana ibada gheni za miungu zilichanganywa na imani ya mitume, kwa kuzaliwa kanisa katoliki na kulipelekea kanisa kuingia katika kipindi kirefu sana cha ukimya kijulikanacho kama kipindi cha giza.

Pamoja na hayo ni kweli alifanikiwa kukomesha mateso kwa wakristo, na kuuthaminisha ukristo, na wakati mwingine kuruhusu mabaraza ya Wakristo, kuthibitisha vipengele kadha wa kadha vya imani, vilivyoleta msaada mwingi.

Lakini pia hakuuingiza Ukristo Katika misingi yake yote, ndio maana kanisa liliongia katika kipindi cha giza.

Je! ni nini tunajifunza kwa Mtawala huyu?

Hata hivyo kwa sehemu yake alisimama kuanzisha Imani ijapokuwa hakufanya katika utimilifu wote. Ilikuwa ni wajibu wa mabaraza Na wazee na watakatifu, Kuyatengeneza yaliyosalia, lakini hawakupiga hatua yoyote zaidi ya pale kwa miaka mingi.

Lakini ashukuriwe Mungu wakati wa matengenezo ulipofika (Karne ya 15)..Bwana aliwanyanyua watu wake mbalimbal8 mfano wa Martin Luther, Zwingli, Calvin na wengineo kulitengeneza upya kanisa kutoka katika misingi mibovu Mpaka wakati wa Pentekoste, ambapo kanuni zote za Kibiblia zilirejeshwa. Na mpaka sasa Kanisa linazidi kupanda katika utumilifu wake wote.

Hivyo ni wajibu wetu, sote kusoma biblia na kuifahamu kwa kina kwa mwongozo wa Roho Mtakatifu, lakini pia kuhubiri injili kwasababu kwa njia hiyo ndivyo tutakavyoujenga ufalme Wa Kristo Na kuufanya uenee duniani kote, kiufasaha.

Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

Naliupata wenyeji huu kwa mali nyingi, maana yake nini (Matendo 22:28)

UKristo Ni Nini?

Je! Mtume Paulo alikuwa ni Mrumi, Myahudi au raia wa Tarso?

Print this post

Mwandishi na Uchambuzi wa kitabu cha kwanza cha Petro.(1Petro)

Kichwa cha kitabu hichi kinasema “Waraka wa kwanza wa Petro kwa watu wote” Kutuonyesha kuwa Petro Ndiye mwandishi.

Waraka huu mfupi aliuelekeza kwa watakatifu wote waliotawanyika, na kuishi kama wageni maeneo ya Asia ndogo ambayo kwasasa ni nchi ya Uturuki.

Maudhui makuu ya waraka huu tunaweza kuyagawanya katika sehemu kuu nne(4):

1) Ni kuwafariji watakatifu kwa kuwaeleza juu ya utukufu walioandaliwa mbinguni utakaofunuliwa siku ya mwisho. Na kwamba kwa kulitambua hilo basi wafurahi Katika majaribu mbalimbali ya imani, yaliyo ya kitambo tu.

2) Lakini pia unalenga kuwahimiza kuishi maisha ya utakatifu ya kumpendeza Mungu katika wakati wao wa kuishi hapa duniani.

3) Vilevile wajibu wakuishi maisha ya nidhamu katika Jamii ya wasioamini inayowazunguka.

4) Halikadhalika wajibu wa viongozi kulichunga kundi la Kristo kwa uaminifu wotena wajibu wa kanisa lote kumpinga shetani.

Haya ni maelezo mafupi juu ya kila kipengele:

1) Faraja katika dhiki mbalimbali.

Petro anawahimiza watakatifu kwamba wafurahi katika majaribu mbalimbali (kuliko kuhuzunika) kwa sababu ya uthamani mkuu wa imani yao itakayolipwa siku ile ya mwisho ambayo Yesu atafunuliwa kwetu.

1 Petro 1:6-7

[6]Mnafurahi sana wakati huo, ijapokuwa sasa kwa kitambo kidogo, ikiwa ni lazima, mmehuzunishwa kwa majaribu ya namna mbalimbali;

[7]ili kwamba kujaribiwa kwa imani yenu, ambayo ina thamani kuu kuliko dhahabu ipoteayo, ijapokuwa hiyo hujaribiwa kwa moto, kuonekane kuwa kwenye sifa na utukufu na heshima, katika kufunuliwa kwake Yesu Kristo.

> Petro Anahimiza kuiga kielelezo cha Kristo ambaye yeye alikubali kuteswa ijapokuwa hakutenda Dhambi, hata alipotukanwa hakurudisha majibu. Vivyo hivyo na sisi tukubali teso lolote kwa ajili yake katika upole wote, uvumilivu na ustahimilivu.

1 Petro 2:19-21

[19]Maana huu ndio wema hasa, mtu akivumilia huzuni kwa kumkumbuka Mungu, pale ateswapo isivyo haki.

[20]Kwa maana ni sifa gani kustahimili, mtendapo dhambi na kupigwa makofi? Lakini kustahimili, mtendapo mema na kupata mateso, huu ndio wema hasa mbele za Mungu.

[21]Kwa sababu ndio mlioitiwa; maana Kristo naye aliteswa kwa ajili yenu, akawaachia kielelezo, mfuate nyayo zake.

1 Petro 4:12-16

[12]Wapenzi, msione kuwa ni ajabu ule msiba ulio kati yenu, unaowapata kama moto ili kuwajaribu, kana kwamba ni kitu kigeni kiwapatacho.

[13]Lakini kama mnavyoyashiriki mateso ya Kristo, furahini; ili na katika ufunuo wa utukufu wake mfurahi kwa shangwe.

[14]Mkilaumiwa kwa ajili ya jina la Kristo ni heri yenu; kwa kuwa Roho wa utukufu na wa Mungu anawakalia.

[15]Maana mtu wa kwenu asiteswe kama mwuaji, au mwivi, au mtenda mabaya, au kama mtu ajishughulishaye na mambo ya watu wengine.

[16]Lakini ikiwa kwa sababu ni Mkristo asione haya, bali amtukuze Mungu katika jina hilo.

2) Wito wa kuishi maisha matakatifu.

Sehemu hii ya pili Mtume Petro anawahimiza watakatifu, kuwa kwasababu wanatazamia neema itakayofunuliwa siku ya mwisho ya kuja kwake Yesu Kristo (1:13), hivyo hawana budi kuishi maisha ya kiasi na utakatifu hapa duniani.

1 Petro 1:13-16

[13]Kwa hiyo vifungeni viuno vya nia zenu, na kuwa na kiasi; mkiitumainia kwa utimilifu ile neema mtakayoletewa katika ufunuo wake Yesu Kristo.

[14]Kama watoto wa kutii msijifananishe na tamaa zenu za kwanza za ujinga wenu;

[15]bali kama yeye aliyewaita alivyo mtakatifu, ninyi nanyi iweni watakatifu katika mwenendo wenu wote;

[16]kwa maana imeandikwa, Mtakuwa watakatifu kwa kuwa mimi ni mtakatifu.

1 Petro 2:1-2

[1]Basi, wekeni mbali uovu wote na hila yote, na unafiki na husuda na masingizio yote.

[2]Kama watoto wachanga waliozaliwa sasa yatamanini maziwa ya akili yasiyoghoshiwa, ili kwa hayo mpate kuukulia wokovu;

> Petro anaendelea kuwasihi watakatifu waishi kama wapitaji duniani, kwa kuziepuka tamaa za mwili.

1 Petro 2:11

[11]Wapenzi, nawasihi kama wapitaji na wasafiri, ziepukeni tamaa za mwili zipiganazo na roho.

1 Petro 4:2-3

[2]Tangu sasa msiendelee kuishi katika tamaa za wanadamu, bali katika mapenzi ya Mungu, wakati wenu uliobaki wa kukaa hapa duniani.

[3]Maana wakati wa maisha yetu uliopita watosha kwa kutenda mapenzi ya Mataifa; kuenenda katika ufisadi, na tamaa, na ulevi, na karamu za ulafi, na vileo, na ibada ya sanamu isiyo halali;

> Anaeleza pia Wajibu wa kupendana kuhurumiana, kunyenyekeana, tuwe watu wasiolipa baya kwa baya, bali wenye kubariki(3:8-12, 4:7)

> Kadhalika pia anaeleza wajibu wa wanandoa. Kwamba wake wawatii Waume zao, na kujipamba kwao kunapaswa kuwe kwa mapambo ya rohoni, Lakini pia waume kuishi na wake zao kwa akili. (3:1-7)

3) Mwenendo wa nidhamu kwa watu walio nje

Katika sehemu hii ya tatu anahimiza watakatifu kuwa na mwenendo unaopasa kwa watu wasioamini, ili wakose nafasi ya kutushitaki au kutulaumu kwa lolote.

> Anagusia katika eneo la watumwa Kwamba wawatii bwana zao, si wale tu wapole bali pia wale wakali.(2:18)

> Lakini pia Watakatifu waitii kila kilichoamriwa na mamlaka.

1 Petro 2:13-15

[13]Tiini kila kiamriwacho na watu, kwa ajili ya Bwana; ikiwa ni mfalme, kama mwenye cheo kikubwa;

[14]ikiwa ni wakubwa, kama wanaotumwa naye ili kuwalipiza kisasi watenda mabaya na kuwasifu watenda mema.

[15]Kwa sababu ndiyo mapenzi ya Mungu, kwamba kwa kutenda mema mzibe vinywa vya ujinga vya watu wapumbavu;

> Lakini pia anahimiza watakatifu wawaheshimu watu wote(2:17)

4) Wito kwa viongozo wa kanisa.

Mwishoni Petro anatoa wito wa waangalizi wa kanisa la Mungu (wazee), kwamba walichunge kundi kwa hiari, sio kwa kulazimishwa au kutazamia malipo ya kifedha, bali kwa moyo.

1 Petro 5:1-3

[1]Nawasihi wazee walio kwenu, mimi niliye mzee, mwenzi wao, na shahidi wa mateso ya Kristo, na mshirika wa utukufu utakaofunuliwa baadaye;

[2]lichungeni kundi la Mungu lililo kwenu, na kulisimamia, si kwa kulazimishwa, bali kwa hiari kama Mungu atakavyo; si kwa kutaka fedha ya aibu, bali kwa moyo.

[3]Wala si kama wajifanyao mabwana juu ya mitaa yao, bali kwa kujifanya vielelezo kwa lile kundi.

> Pamoja na hayo anasisitiza watakatifu wote wawe na kiasi na kukesha, kwasababu adui yetu ibilisi ni mfano wa simba angurumaye akitafuta mtu ammeze, hivyo wana wajibu wa kumpinga sikuzote.(5:8-9)

Hitimisho: 

Hivyo kwa maelezo machache ni kwamba Petro analihimiza kanisa kutembea katika uvumilivu wote na uthabiti Wa imani, pamoja na utakatifu, na kutimiza wajibu wao katika utakatifu na adabu kwa wanadamu wote, katika wakati ambao kanisa linasubiria neema kuu itakayofunuliwa siku ya mwisho Yesu atakaporudi.

Na ndivyo ambavyo sote tunapaswa tuishi hivyo sasa.

Kama mkristo je unaendelea kufurahi katika majaribu? Unaishi maisha matakatifu? Unaishi vema na jamii yako? unaifanya kazi ya Mungu? Unampinga shetani kwa kudumu katika sala?

Ikiwa hayo, unayazingatia basi, wewe ni mshirika wa neema hiyo kuu ya Mungu itakayofunuliwa siku ya mwisho.

Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >>

https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

Mwandishi na uchambuzi wa kitabu cha Wakolosai

Mwandishi na uchambuzi wa kitabu cha Wakorintho wa kwanza (1Wakorintho)

MAANA YA KUISHI NA MKE KWA AKILI.

JINSI ITAKAVYOKUWA KATIKA SIKU ILE

Print this post

KUSUDI LA KWANZA LA KUCHAGULIWA NA MUNGU NI LIPI?

Je wewe ni miongoni mwa waliochaguliwa sawasawa na andiko hili?…

Waefeso 1:11 ”na ndani yake sisi nasi tulifanywa urithi, huku tukichaguliwa tangu awali sawasawa na kusudi lake yeye, ambaye hufanya mambo yote kwa shauri la mapenzi yake”.

Kama wewe ni miongoni mwa waliochaguliwa basi fahamu lengo/kusudi la kwanza la wito wa MUNGU kwako ni lipi?..

Hebu tuusome wito wa Mtumishi wa Mungu Paulo, tuweze kujua nia ya Kristo ipi…

Matendo 22:13 “Akanijia, akasimama karibu nami, akaniambia, Ndugu yangu Sauli, uone. Nikamwinulia macho yangu saa ile ile.

14 Akasema, Mungu wa baba zetu amekuchagua wewe upate KUJUA MAPENZI YA MUNGU, na kumwona yule Mwenye haki, na kuisikia sauti itokayo katika kinywa chake”.

Hapo anasema “Mungu wa baba zetu amekuchagua wewe upate kujua MAPENZI YAKE..”...Jiulize kwanini ataje jambo la kwanza “mapenzi ya Mungu”.

Kumbe lengo la kwanza la Mungu kumwita Paulo ni yeye “kuyajua mapenzi ya Mungu”. Na mengine ndiyo yafuate..

Na ni sahihi kabisa kwani Bwana YESU mwenyewe alituambia maneno yafuatayo…

Mathayo 7:21 “Si kila mtu aniambiaye, Bwana, Bwana, atakayeingia katika ufalme wa mbinguni; bali ni yeye AFANYAYE MAPENZI YA BABA YANGU ALIYE MBINGUNI”.

22 Wengi wataniambia siku ile, Bwana, Bwana, hatukufanya unabii kwa jina lako, na kwa jina lako kutoa pepo, na kwa jina lako kufanya miujiza mingi?

23 Ndipo nitawaambia dhahiri, Sikuwajua ninyi kamwe; ondokeni kwangu, ninyi mtendao maovu”

Umeona?..kwahiyo kumbe Bwana anataka tuyajue sana mapenzi yake na tuyafanye..

Je unayajua mapenzi ya Mungu??…na je unayafanya pia?.

Mapenzi ya MUNGU ni haya…

1 Wathesalonike 4:3 “Maana haya ndiyo mapenzi ya Mungu, kutakaswa kwenu, mwepukane na uasherati;

4 kila mmoja wenu ajue kuuweza mwili wake katika utakatifu na heshima;

5 si katika hali ya tamaa mbaya, kama Mataifa wasiomjua Mungu”.

 1. Utakaso ni sehemu ya mapenzi ya MUNGU kwako.

(Na unatakasika kwa maombi, mifungo, kusoma Neno, na kuhudhuria ibada).

 2. Pia Kuuweza mwili katika utakatifu na heshima ni sehemu ya mapenzi ya MUNGU kwako.

(Maana yake mwili wako kuuweka katika hali ya heshima, ikiwemo kuvaa mavazi ya heshima na staha, ikiwemo kutojichubua, na kutofanya uasherati na mambo yote yanayohusika kuuchafua mwili”.

Yajue mapenzi ya MUNGU, yafanye mapenzi ya MUNGU.

Kwa urefu zaidi kuhusu Mapenzi ya MUNGU fungua hapa》》MAPENZI YA MUNGU NI YAPI?

Bwana akubariki.

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

Rudi Nyumbani

Print this post

Ile Mizeituni mwili na wale wana wawili wa mafuta vinawakilisha nini? (Zekaria 4)

Sura hii inaeleza maono aliyoonyeshwa nabii Zekaria, kuhusu ujenzi wa hekalu la pili. Anaanza kwa kuonyeshwa na malaika kinara cha taa cha dhahabu, chenye taa saba juu yake. Ambacho pia  kina mirija saba, inayotoka katika matawi ya mizeituni miwili inayohusika kuleta mafuta katika kinara hiyo.

Hivyo nabii Zekaria kuona maono hayo, alitamani kuelewa tafsiri yake ni nini. Tusome.

Zekaria 4:1 Na yule malaika aliyesema nami akanijia mara ya pili, akaniamsha, kama mtu aamshwavyo katika usingizi wake.

2 Akaniuliza, Unaona nini? Nikasema, Nimeona, na tazama, kinara cha taa cha dhahabu tupu, nacho kinabakuli juu yake, na taa zake saba juu yake; tena iko mirija saba ya kuleta mafuta, kwa taa zote zilizo juu yake;

3 na mizeituni miwili karibu yake, mmoja upande wa kuume walile bakuli, na mmoja upande wake wa kushoto. 4 Nami nikajibu, nikamwambia yule malaika aliyesema nami, nikasema, Ee Bwana wangu, vitu hivi ni nini?

5 Ndipo malaika aliyesema nami akajibu, akaniambia, Hujui vitu hivi ni nini? Nikasema, La, Bwana wangu.

6 Akajibu akaniambia, akisema, Hili ndilo neno la Bwana kwa Zerubabeli, kusema, Si kwa uwezo, wala sikwa nguvu, bali ni kwa roho yangu, asema Bwana wa majeshi.

7 Nani wewe, Ee mlima mkubwa? Mbele ya Zerubabeli utakuwa nchi tambarare; naye atalileta lile jiwe lakuwekwa juu kabisa pamoja na vigelegele vya, Neema, neema, ilikalie.

8 Tena neno la Bwana likanijia, kusema,

9 Mikono yake Zerubabeli imeiweka misingi ya nyumba hii, na mikono yake ndiyo itakayoimaliza; nawe

utajua ya kuwa Bwana wa majeshi amenituma kwenu.

10 Maana ni nani aliyeidharau siku ya mambo madogo? Kwa kuwa watafurahi, nao wataiona timazi katika mkono wa Zerubabeli; naam, hizi saba ndizo macho ya Bwana; yapiga mbio huko na huko duniani mwote.

11 Ndipo nikajibu, nikamwambia, Ni nini mizeituni hii miwili iliyo upande wa kuume wa kinara cha taa kile na upande wake wa kushoto?

12 Nami nikajibu mara ya pili, nikamwuliza, Ni nini haya matawi mawili ya mizeituni, ambayo kwa njia ya ile mifereji miwili ya dhahabu hutoa mafuta yao?

13 Akanijibu, akasema, Hujui hivi ni nini? Nikasema, La, Bwana wangu.

14 Ndipo akasema, Hivi ni hao wana wawili wa mafuta, wasimamao karibu na Bwana wa dunia yote.

Tafsiri yake ni kuwa matawi yale mawili walimwakilisha Yoshua kuhani mkuu, na Zerubabeli liwawi wa Yuda. Hawa ndio wana wawili wa mafuta. Yoshua alisimama katika mambo yote yahusuyo dini na ibada na Zerubabeli katika mambo yote ya  kiutawala,

Na ile mizeituni miwili iliwakilisha Neno la Mungu lililowajia wao, kuwaongoza na kuwatia nguvu.  aidha kwa njia ya Torati au kwa Manabii. Maana yake ni kuwa Yoshua kama kuhani mkuu akiongozwa na Torati na Zerubabeli kama akida akiongozwa na manabii waliopokea ujumbe kutoka kwa Mungu ili walisimamie kusudi lake. Na manabii ambao walihusika hapa kuwatia nguvu walikuwa ni Hagai na Zekaria.

Katika ono hili Mungu alikuwa anamfunulia Zerubabeli uweza wake, kwamba si yeye atendaye hiyo kazi kubwa ambayo inaonekana kibinadamu haiwezekani, kutokana na hofu ya maadui zao, kupungukiwa fedha, na lile agizo lililotolewa na mfalme kuwa mji ule usiendelezwe. Bali ni Roho wa Mungu atendaye kazi yote, kwasababu si kwa uweza wao wala kwa nguvu.

Mungu akamuhakikishia Zerubabeli kuwa mikono yake ndiyo imetia msingi, na mikono yake ndiyo itakayoimaliza nyumba ile yote. Akimwonyesha kimaono jinsi wao wanavyosimama tu kama matawi ndani ya mzeituni (Zerubabeli na Yoshua), ambayo yanapokea mafuta na kutoa kuelekea kwenye mirija. Lakini hayahusiki katika kutengeneza mafuta au  kuwasha taa yoyote.

Na ndivyo ilivyokuwa kwao ujenzi huo ulienda ukakamilika bila taabu zao wenyewe walizozitarajia, bali Mungu alihakikisha anawapatia kibali, pamoja na vitendeakazi vyote(Mali) kiasi kwamba utukufu wa hekalu hilo la pili ukawa mkubwa sana kuliko ule wa kwanza, pamoja na udhaifu wao.

Vivyo hivyo hata sasa, ni lazima tufahamu kuwa jambo lolote kuu tunalotamani kumfanyia Mungu, aidha kujenga nyumba yake, kusapoti injili, kuhubiri injili sehemu za taabu na nguvu n.k. Tusifirie sana hali zetu, bali tumfikirie Roho Mtakatifu, kwasababu yeye mwenyewe aliahidi kuwa atatupa nguvu ya kuyatenda hayo yote, na kuyatimiliza.(Matendo 1:8), ili utukufu wote umrudie yeye.

Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

Amka, Ee upanga, juu ya mchungaji wangu (Zekaria 13:7-9)

DAMU YA ZAKARI BIN BARAKIA.

Mafuta mabichi ni mafuta ya aina gani? (Zaburi 92:10)

Rudi Nyumbani

Print this post

Aliyeungwa na Bwana ni roho moja naye maana yake nini?.

Swali: Neno la Mungu limemaanisha nini kusema aliyeungwa na Bwana ni roho moja naye? (1Wakorintho 6:17).


Jibu: Turejee…

1 Wakorintho 6:17 “Lakini yeye aliyeungwa na Bwana ni roho moja naye”.

Maana ya kuwa roho moja na Bwana ni kama maandiko yafuatayo yanavyoeleza..

Ufunuo 22:17 “Na Roho na Bibi-arusi wasema Njoo!…..”.

Hapa anasema Roho (yaani wa Roho wa Mungu) na bibi-arusi (yaani kanisa la Mungu)…Wasema Njoo!!…

Maana yake hawa wawili (Roho pamoja na bibi arusi) wote wanatoa Kauli moja!.. ya Njoo!..

Maana yake Bibi arusi akisema ni Roho wa Mungu kasema na Roho wa Mungu akisema ni  Bibi arusi kasema…kwanini?…kwasababu wameungwa pamoja.

Ndio sababu Bwana YESU alisema, tukiwapokea waliotumwa na yeye, tumempokea yeye, na tukiwakataa waliotumwa na yeye, tumemkataa yeye kwasababu wameungwa na yeye.

Mathayo 10:40 “Awapokeaye ninyi, anipokea mimi; naye anipokeaye mimi, ampokea yeye aliyenituma”.

Je umemwamini Bwana YESU?. Je unasubiri Bwana YESU mwenyewe akutokee ndio uamini?..

Kama ndicho unachosubiri basi upo hatarini, kwasababu YESU yupo anafanya kazi ndani ya watu wake, mtumishi wa MUNGU wa kweli kukujia na kukupa habari za uzima wa milele, tayari YESU ameshakutokea kwasababu maneno akuambiayo si yake bali ya Roho wa Mungu.

Na anapokuita uingie kwenye imani/wokovu si yeye bali ni Roho wa MUNGU ndani yake..

Ufunuo 22:17 “Na Roho na Bibi-arusi wasema Njoo! Naye asikiaye na aseme, Njoo! Naye mwenye kiu na aje; na yeye atakaye, na ayatwae maji ya uzima bure”

Shalom.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

VIASHIRIA VINGINE VYA ROHO MTAKATIFU KUWEPO NDANI YAKO.

NAFASI YAKO NI IPI KATIKA MWILI WA KRISTO?

Pale mwanandoa mmoja anaposhindwa kutimiza wajibu wake ufanyaje?

NDOA TAKATIFU NI MKE MMOJA/MUME MMOJA.

Biblia imemaanisha nini iliposema “hawezi mtu kusema, Yesu ni Bwana, isipokuwa katika Roho Mtakatifu”

Rudi Nyumbani

Print this post

Kwanini nguo za waliomwua Stefano ziwekwe miguuni mwa Sauli?.

Swali: Kulikuwa na sababu gani habari za nguo za waliomwua Stefano kuandikwa katika biblia? (Matendo 7:58).

Jibu: Turejee…

Matendo 7:58 “wakamtoa nje ya mji, wakampiga kwa mawe. Nao mashahidi WAKAWEKA NGUO ZAO MIGUUNI PA KIJANA MMOJA ALIYEITWA SAULI. 

59 Wakampiga kwa mawe Stefano, naye akiomba, akisema, Bwana Yesu, pokea roho yangu”.

Zipo tafiti zinasema kuwa zamani za biblia, akipatikana mtu na kosa la kustahili kuuawa kwa kupigwa mawe, basi wale mashahidi waliolishuhudia kosa la huyo mtu, kabla ya kutekeleza mauaji walivua nguo zao kama ishara ya kiapo walichokitoa/ushahidi kuwa ni kweli.

Lakini dhana hiyo haina marejeo yoyote ya biblia, hivyo si ya kusadikika.

Lakini sababu pekee yenye kuleta maana ya mavazi ya mashahidi kuwekwa miguuni mwa Sauli ni ili wawe wepesi katika kutekeleza zoezi hilo la mauaji.

Ni kawaida wana michezo au wapiganaji kupunguza mavazi yao kabla ya mchezo kuanza ili wawe wepesi, ndicho walichokifanya hawa mashahidi, walipunguza mavazi yao ya nje, na kumpatia kijana Sauli awahifadhie kwa muda na baadae wazichukue baada ya kumuua Stefano.

Na tunasoma Sauli (ambaye baadaye ndiye aliyekuja kuwa Paulo), alikubali kuwatunzia..

Matendo 22:20 “Na damu ya Stefano shahidi wako ilipomwagwa, mimi nami nilikuwa nikisimama karibu, nikikubali, na kuzitunza nguo zao waliomwua”.

Sasa ni kwanini Bwana MUNGU aruhusu mavazi ya wauaji yatunzwe na Sauli?.

Sababu kuu ni kwamba Bwana  MUNGU alijua Sauli atakuja kugeuka baadaye na kuwa mtumishi wake kwa watu wa Mataifa.

Hivyo kitendo cha zile nguo kuwekwa miguuni mwa Sauli ni kuweka sababu baadae ya Wayahudi pamoja na wakristo waliopo Yerusalemu kumkataa, ili aende kwa watu wa mataifa…

Kwani watakapokumbuka lile tendo la kushiriki kwake kumuua Stefano, wamkatae na kumwona hafai..

Matendo22:17 “Ikawa nilipokwisha kurudi Yerusalemu, nilipokuwa nikisali ndani ya hekalu, nikawa hali ya kuzimia roho, 

18 nikamwona, naye akiniambia, Hima, utoke Yerusalemu upesi, KWA SABABU HAWATAKUBALI USHUHUDA WAKO katika habari zangu. 

19 Nami nikasema, Bwana, wanajua hao ya kuwa mimi nalikuwa nikiwafunga gerezani wale wanaokuamini na kuwapiga katika kila sinagogi. 

20 Na damu ya Stefano shahidi wako ilipomwagwa, mimi nami nilikuwa nikisimama karibu, nikikubali, na kuzitunza nguo zao waliomwua. 

21 Naye akaniambia, Enenda zako; KWA KUWA NITAKUTUMA UENDE MBALI KWA WATU WA MATAIFA”.

Na utaona faida ya Paulo kuhubiri kwa watu wa Mataifa ndio mazao ya nyaraka zote za Paulo, ambazo mpaka leo zimekuwa msingi wa Neno la Mungu.

Tunachojifunza zaidi kuwa yapo makosa ambayo yalitokea zamani, na MUNGU aliyaruhusu yatokee kwasababu yamebeba kusudi kubwa mbeleni.

Makosa mengine yaliruhusiwa zamani ili yatuondolee viburi leo, mengine yaliruhusiwa ili tupate fursa njema leo, na mengine ni ushuhuda kwa wengine na maonyo kwa wengi e n.k

Hivyo kila jambo lina kusudi lake.

Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

Maziara ni nini? Je! Na Tunaruhusiwa kuyajenga kwenye makaburi yetu?

Ni sahihi kusema sikuitiwa kuhubiri ubatizo kama Paulo alivyosema (1Wakorintho 1:17)?

Nini maana ya “Heri kuchagua jina jema kuliko mali nyingi”?

ANTIPA SHAHIDI WANGU, MWAMINIFU WANGU.

MWOMBENI BWANA WA MAVUNO APELEKE WATENDA KAZI.

Rudi Nyumbani

Print this post

Mwandishi na Uchambuzi wa kitabu cha Wakorintho wa pili (2Wakorintho)


Kama kichwa cha waraka Huu kinavyosema… “Waraka wa pili wa Paulo Mtume kwa Wakorintho”

Kutuonyesha kuwa Paulo ndiye mwandishi wa kitabu hichi..

Tunaweza kukigawanya katika sehemu kuu tatu (3)

1) Utendaji kazi wa Mungu, na wajibu wa watakatifu katika huduma na maisha yao ( sura ya 1-7)

2) Utoaji bora kwa mkristo.(Sura ya 8-9)

3) Utetezi wa huduma ya Paulo (10-13)

Sehemu ya kwanza:

1) Utendaji kazi wa Mungu, na wajibu wa watakatifu katika huduma na maisha yao ( sura ya 1-7)

Katika sura hizi, Mtume anagusia maeneo kadha wa kadha, kama ifuatavyo.

i) Faraja ya Mungu

Paulo anatoa shukrani zake kwa jinsi Mungu anavyoweza kuwafariji watu wake katikati na dhiki na majaribu mazito. Akimtaja Mungu kama ni ndio mtoa faraja yote, katika dhiki zetu. (1-3-7)

2 Wakorintho 1:3-4

[3]Na ahimidiwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa rehema, Mungu wa faraja yote;

[4]atufarijiye katika dhiki zetu zote ili nasi tupate kuwafariji wale walio katika dhiki za namna zote, kwa faraja hizo, tunazofarijiwa na Mungu.

ii) Nafasi ya kutubu.

Sehemu inayofuata Paulo anaeleza sababu ya kutofika Korintho haraka, kama ilivyodhaniwa. Ni ili asilete tena huzuni zaidi kama akiwakuta bado hawajakamilika. Na hiyo ni kutokana na kuwa hawakuwa na mabadiliko ya haraka kwa agizo lake la kwanza, hivyo hakutaka afanye ziara ya ghafla bali wayatengeneze kwanza wao wenyewe ili ziara yake kwao, safari hii iwe ya raha na sio ya hukumu.(1:23-2:4)

 iii) Wajibu wa kusamehe. (2:5-11)

Paulo anawahimiza wakorintho kusamehe kwa wale watu wanaoleta huzuni ndani ya kanisa, Hususani waliomnenea vibaya utume wake. Anahimiza kuliko kusimamia adhabu ziwapasazo ambazo wana haki kweli ya kuzipokea. Kinyume chake wawasamehe ili wawapate tena wasipotee kabisa katika huzuni zao.

IV) Utukufu wa agano jipya.(sura ya 3-5)

Paulo Anaeleza jinsi gani, agano jipya utukufu wake ulivyo mbali na ule wa agano la kale. Kwasababu utukufu wa agano jipya umekuja Katika Roho atoaye uhuru.

Paulo anaeleza kwasababu hiyo hatupaswi kulegea kwa kuenenda kwa hila au kulichanganya Neno la Mungu na uongo. Au kwa kutohubiri injili. Bali kufanya yote bila kujali utu wetu wa nje kuchakaa. Tukijua kuwa ule wa ndani unafanywa upya siku baada ya siku na kwamba ipo siku tutasimama mbele ya kiti hukumu kutoa Hesabu ya mambo yetu yote tuliyoyatenda katika mwili.

Paulo anaeleza kwamba kama Kristo alivyopewa huduma ya upatanisho sisi pia tumepewa Neno Hilo hilo ndani yetu. Kuupatanisha ulimwengu na Mungu kupitia Yesu Kristo. Akionyesha kuwa ni wajibu wetu sote kuhubiri injili.

V) Maisha ya ukamilifu (sura ya 6-7)

Paulo anawasihi Wakoritho waikunjue mioyo yao na waishi maisha ya ukamilifu na ya uangalifu wasiwe kwazo la namna yoyote ili utumishi wao usije laumiwa siku ile ya Bwana

Lakini pia anawapa onyo wasiwe na ushirika na wasioamini.

Pamoja na hilo katika sura ya saba, Paulo anaeleza furaha yake kwa Wakorintho Kwa kuitii toba..kufuatana na waraka aliowaandikia hapo kabla wa huzuni ( Ambao haupo miongoni mwa nyaraka hizi zilizo kwenye biblia). Ambapo walipousoma walitubu na kugeuka, kwelikweli. Kuonyesha utii wa toba. Ambao unapaswa uonekane ndani ya makanisa hata sasa.

Sehemu ya Pili:

2) Utoaji bora kwa mkristo.(8-9)

Katika sura ya 8-9

Paulo anahimiza michango kwa ajili ya watakatifu walio Yerusalemu, Akitolea mfano watakatifu wa Makedonia jinsi walivyoweza kutoa kwa ukarimu hata katika umaskini wao, vivyo hivyo na wao anawahimiza wawe na moyo huo huo. Akiwaonyesha jinsi Bwana wetu Yesu alivyotupa kielelezo cha kukubali kuwa maskini ili sisi tuwe matajiri kwa umaskini wake.

2 Wakorintho 8:9

[9]Maana mmejua neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, jinsi alivyokuwa maskini kwa ajili yenu, ingawa alikuwa tajiri, ili kwamba ninyi mpate kuwa matajiri kwa umaskini wake.

Kwasababu utumishi wa namna hiyo sio tu unawapata watakatifu rizki lakini pia huleta matunda ya shukrani kwa Mungu.

2 Wakorintho 9:12

[12]Maana utumishi wa huduma hii hauwatimizii watakatifu riziki walizopungukiwa tu, bali huzidi sana kuwa na faida kwa shukrani nyingi apewazo Mungu;

Sehemu ya tatu:

3) Utetezi wa huduma yake (Paulo). Sura ya 10-13

Katika sura hizi Paulo anaitetea Huduma yake dhidi ya watu wengine wanaojitukuza mbele za watu, kana kwamba ni mtume wa kweli kumbe ni mitume wa uongo, ambao huwashawishi watu kwa majivuno ya nje na ukali, lakini si ya kazi.

2 Wakorintho 11:20

[20]Maana mwachukuliana na mtu akiwatia utumwani, akiwameza, akiwateka nyara, akijikuza, akiwapiga usoni.

Hivyo Paulo anawaeleza kwa upana uthabiti wa huduma yake, tangu asili ya kabila lake, mateso aliyopitia, akionyesha mpaka kusimama vile, hakukutokea hivi hivi tu, bali katika masumbufu mengi, anawaeleza pia maono aliyoyafikia mpaka kunyakuliwa mbingu ya tatu, hiyo yote ni kuwaonyesha wakorintho kama wanataka kuamini kwa watu wanaojisifia basi yeye anawazidi wao, lakini hatumii njia hiyo, bali ya udhaifu ili asihesabiwe zaidi ya vile watu wavionavyo Kwake.

Salamu za mwisho.

Anahimiza wakoritho wanie Mamoja, watimilike na wafarijike.

Hivyo kwa ufupi mambo haya makuu tunaweza kuyapata katika waraka huu;

  1. Faraja za Mungu katika majaribu
  2. Huduma ya Upatanisho tuliyopewa ndani yetu, kuwapatanisha waovu kwa Mungu.
  3. Utukufu bora wa agano jipya, jinsi ulivyo mbali na ule wa agano la lake
  4. Nguvu tulizonazo katika udhaifu
  5. Utoaji umpendezao Mungu, kwa kukubali sisi kupoteza kwa ajili ya wengine.
  6. Lakini pia Namna bora ya kuithibitisha huduma ya kweli, si katika majivuno bali katika matunda ya kazi

Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

Mwandishi na uchambuzi wa kitabu cha Wakorintho wa kwanza (1Wakorintho)

Fahamu maana ya 2 Wakorintho 8:9 alikuwa maskini ili sisi tuwe matajiri kwa umaskini wake.

Uchambuzi na mwandishi wa kitabu cha Waefeso.

Fahamu ni nani aliye mwandishi wa kitabu cha Mathayo.

Rudi Nyumbani

Print this post

Je ni sahihi kusema waraka fulani ni wa kanisa fulani tu?.

Swali: Je ni sahihi kusema waraka fulani wa Mtume Paulo ni kwaajili ya kanisa fulani tu?…Mfano waraka wa Wakorintho uliwahusu Wakorintho  tu peke yao hivyo si vitu vyote vya kuchukua huko… 

Vile vile waraka wa Waefeso uliwahusu waefeso peke yao? Na si makanisa yote ikiwemo sisi, hivyo kuna vitu si sahihi kuvibeba kutoka kwenye waraka huo?.


Jibu: Awali turejee salamu za kwanza za Paulo kwa baadhi ya makanisa…

Wakolosai 1:1 “Paulo, mtume wa Kristo Yesu kwa mapenzi ya Mungu, na Timotheo, ndugu yetu,

2 kwa ndugu watakatifu, waaminifu katika Kristo, WALIOKO KOLOSAI. Neema na iwe kwenu, na amani, zitokazo kwa Mungu Baba yetu”.

Ni kweli hapa anaonyesha kuwa waraka huu umekusudiwa kwa wakristo walioko KOLOSAI…

Lakini swali ni je?…ni wakristo walioko Kolosai tu ndio waliokusudiwa wasome huu waraka au hata makanisa mengine ya mahali pengine ikiwemo sisi tuishio wakati huu wa mwisho?.

Jibu la swali hili tutalipata katika waraka huu huu wa Wakolosai…

Wakolosai 4:16 “Waraka huu ukiisha kusomwa kwenu fanyeni kwamba usomwe katika kanisa la Walaodikia pia; na ule wa Laodikia usomwe na ninyi”.

Kumbe ulikuwepo waraka mwingine ulioandikwa wa kanisa la Laodikia ambao ungepaswa usomwe kwa Wakolosai, na huu wa Wakolosai ulipaswa ukasomwe kwa kanisa la Laodikia.

Ikiwa na maana kuwa nyaraka za Paulo, ijapokuwa alizipeleka katika kanisa husika lakini hakuzizuia zisisomwe katika makanisa mengine, kwasababu mambo aliyokuwa anayahubiri kanisa moja na kuyakemea ndio hayo hayo atakayoyafundisha na kuyakemea katika makanisa mengine, na ndio hayo hayo pia yanatufaa katika makanisa ya siku za mwisho.

Utaona pia salamu ya kwanza ya Paulo kwa Wagalatia, ilihusu makanisa yote yaliyopo Galatia na si kanisa moja tu….

Wagalatia 1:1 “Paulo, mtume, (si mtume wa wanadamu, wala kutumwa na mwanadamu, bali na Yesu Kristo, na Mungu Baba aliyemfufua kutoka kwa wafu),

2 na ndugu wote walio pamoja nami, kwa makanisa ya Galatia”.

Maana yake kama makanisa yaliyokuwepo Galatia yalikuwa mia (maana Galatia ilikuwa ni kubwa mno, tazama ramani)..basi makanisa yote yalisomewa huo waraka pasipo kujalisha tabia zao.

Pia utazidi kulithibitisha hilo katika kitabu cha waraka kwa Wakorintho, utaona Paulo anaelekeza kuwa si kwa Wakorintho peke yao bali na kwa watu wote wanaoliitia jina la Bwana kila mahali ikiwemo sisi..

1 Wakorintho 1:1 “Paulo, aliyeitwa kuwa mtume wa Yesu Kristo kwa mapenzi ya Mungu, na Sosthene ndugu yetu,

2 kwa kanisa la Mungu lililoko Korintho, wale waliotakaswa katika Kristo Yesu, walioitwa wawe watakatifu, pamoja na wote wanaoliitia jina la Bwana wetu Yesu Kristo kila mahali, Bwana wao na wetu”

Kwahiyo kwa hitimisho ni kwamba nyaraka zote za Mtume Paulo na biblia yote kwa ujumla yafaa kwa mafundisho kwa makanisa yote na vizazi vyote..

2 Timotheo 3:16 “Kila andiko, lenye pumzi ya Mungu, lafaa kwa mafundisho, na kwa kuwaonya watu makosa yao, na kwa kuwaongoza, na kwa kuwaadibisha katika haki”

Hivyo si sahihi kusema waraka huu waliandikiwa Wakorintho tu peke yao au Wagalatia bali unatuhusu hata sisi..

Mafundisho yaliyohusu utakatifu ikiwemo kujisitiri na kuishi maisha ya kuepuka dhambi yaliwahusu watu wa kanisa la kwanza na yanatuhusu sisi pia..

Mafundisho yanayohusu nafasi za wanawake na wanaume katika kanisa sawasawa na 1Wakorintho 14:34 na 1Timotheo 2:8-12, yanatuhusu hata sisi.

Kupunguza Neno lolote katika biblia ni kosa, Bwana atusaidie.

Shalom

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

ISHARA YA KANISA LA LAODIKIA

Mwandishi na uchambuzi wa kitabu cha Wakorintho wa kwanza (1Wakorintho)

Uchambuzi na mwandishi wa kitabu cha Waefeso.

VITABU VYA BIBLIA: Sehemu ya 1

Biblia inasema nini kuhusu mtu ‘Mwenye kujipendekeza (Mithali 29:5)

Rudi Nyumbani

Print this post