TAZAMA KRISTO YUPO HAPA,AU YUKO KULE MSISADIKI.

TAZAMA KRISTO YUPO HAPA,AU YUKO KULE MSISADIKI.

Shalom, Jina la Bwana wetu Yesu Kristo libarikiwe.

Bwana Yesu alisema maneno yafuatayo…

Mathayo 24:23 “Wakati huo mtu akiwaambia, Tazama, Kristo yupo hapa, au yuko kule msisadiki.

24 Kwa maana watatokea makristo wa uongo, na manabii wa uongo, nao watatoa ishara kubwa na maajabu; wapate kuwapoteza, kama yamkini, hata walio wateule”.

Bwana Yesu anapomwita mtu, au anapomvuta mtu kwake kitu cha kwanza kumwonesha sio kanisa la kujiunga…bali Neno lake. Ni muhimu kulijua hilo ili tusidanganyike na roho zituambiazo..”tazama Kristo yupo hapa ama kule”

Zamani kidogo kuna mtu alitutumia ujumbe akatuambia… “Ameota ndoto, alikuwa ndani ya kanisa lake ambalo ndilo analokwenda siku zote…katika hiyo ndogo alijiona alikuwa anaimba na kuabudu kwa furaha pamoja na washirika wenzake…wakati anaabudu kwa nje ya kanisa akamwona mdada mwingine ambaye anamfahamu anamwangalia kama kwa kumhuzunikia hivi…Na alipoona anamwangalia sana na tena kwa huzuni…yeye kitu Fulani kikamjia kwenye kichwa chake, kwamba pengine hayupo sehemu salama…hivyo akaamua kutoka kule ndani alipokuwa anaimba na wenzake na akamfuata Yule dada aliyekuwepo kule nje!..Na huyo dada alipomfuata aligundua kuwa anasali kanisa Fulani analolijua kisha akashtuka usingizini” .

Baada ya ndoto hiyo akatutumia meseji kwamba anahisi Mungu anamwambia aondoke hilo kanisa alilopo sasa aende kwenye kanisa lingine…ambalo ni la Yule dada aliyemwona kwenye ndoto. Akatuhadithia na hiyo ndoto aliyoiota. Ikabidi tuanze kumhoji kanisa alilopo sasa hivi ni kanisa gani! Akatutajia..na hilo analotaka kwenda pia akatutajia.. Tulichokuja kugundua kuwa mahali anaposali sasa pana uafadhali mkubwa sana kuliko kule alikokuwa anataka kwenda…

Kwanza mahali anaposali panahubiriwa maonyo ya siku za mwisho kwa nguvu, na pia wanafundishwa utakatifu, pamoja na wanawake kujiheshimu kwa kujisitiri, ni mahali ambapo wanawake hawavai suruali, hawavai mawigi, hawaruhusiwi kuvaa vimini, hawapaki wanja na mambo yote ya kidunia hayaruhusiwi kanisani…Na huko anakotaka kwenda ni mahali ambapo mambo hayo yote ni ruksa…kuvaa suruali na kuingia nazo kanisani ni ruksa, kujipodoa na kuingia kanisani ni ruksa, na wala hakuna msisitizo wowote wa ujio wa pili wa Kristo.

Tukamwuliza huyu dada ni kitu gani ambacho unahisi hakiendi sawa katika kanisa ulilopo sasa?..akasema hakuna..kila kitu kipo sawa, kanisani hakuna tatizo lolote kuna amani na kuna upendo tu. Lakini naogopa hiyo ndoto niliyoiota isije kuwa Mungu ananionya niondoke halafu simtii?.

Tukamwambia hiyo ndoto sio ya Ki-Mungu…Mungu kamwe hawezi kumtoa mtu kwenye kanisa na kumwonyesha kanisa…kamwe hafanyi hivyo!..Atamtoa mtu kwenye kanisa na kumwonyesha Neno lake kwanza…hicho ndicho kitu cha kwanza kumwonyesha…Kwamfano mtu anaweza kuwa katika kanisa ambalo kunafanyika ibada za sanamu….Sasa Roho Mtakatifu akitaka kumwondoa mtu hapo..hatamwonyesha kanisa Fulani lingine labda la kiroho akajiunge…kamwe hatafanya hicho kitu…atakachofanya ni kumwonyesha kwanza yule mtu maandiko yanavyosema…Atamwonyesha kwanza Neno linasema “usijifanyie sanamu ya kuchonga wala mfano wa kitu chochote kilicho juu mbinguni, wala duniani, wala chini kuzimu usivisujudie wala kuvitumikia (Kutoka 20:4)”.

Hilo ndilo Neno la kwanza atakalomwonyesha…na kwa kupitia hilo neno sasa ndipo mtu atapata ufahamu kuwa hayupo sehemu salama…na kuondoka pale alipo kwenda kutafuta mahali pengine ambapo hataabudu sanamu kulingana na Neno lile….Lakini Mungu hawezi kuliruka Neno lake na moja kwa moja kukupeleka kwenye kanisa Fulani…kama ilivyokuwa kwa huyu dada..Lazima akuonyeshe kwanza kuna kitu hakipo sawa kulingana na Neno mahali ulipo ndipo uondoke…lakini kama huoni chochote halafu unasikia kitu kinakuambia uondoke hizo ni roho zidanganyazo zisemazo “Kristo yupo huku au kule..”

Sasa hiyo roho inamtoa huyu dada mahali ambapo wanawake wanajisitiri na kumpeleka mahali ambapo ataruhusiwa kuvaa vimini na kuingia navyo kanisani, ataruhusiwa kujipodoa, mahali ambapo hatakemewa dhambi wala kukumbushwa habari za ujio wa pili wa Bwana Yesu.

Ndugu usikimbilie kutafuta kanisa..tafuta kulijua Neno la Mungu…ukilifahamu hilo ndipo utakapoweza kujua mahali ulipo kama ni salama au sio salama..kadhalika sio kila ndoto unayoota inatoka kwa Mungu…Nyingine zinatoka kwa Ibilisi, hivyo hupaswi kuamini kila roho, bali unapaswa uijaribu…na huwezi kuijua kama hiyo ndoto inatoka kwa Ibilisi au kwa Mungu kama hulijui Neno (Hivyo Neno la Mungu litabaki kuwa msingi wa kila kitu)….Usipolijua Neno Siku zote utatii kila ndoto na kumbe zinakupeleka upotevuni..Na jambo la mwisho la kufahamu ni kwamba…Sio kila ndoto ina maana!..nyingine zinatokana na shughuli zetu za kibinadamu tu(Mhubiri 5:3)… Usitafute kujua tafsiri ya kila ndoto unayoota nyingine ziache zipite.

Kama ni Mungu anazungumza na wewe katika ndoto usiwe na papara!… yeye mwenyewe atakutengenezea njia rahisi tu ya kuielewa tafsiri ya hiyo ndoto kama imetoka kwake..inaweza isiwe siku hiyo hiyo au wiki hiyo hiyo, lakini itafika saa na siku itaijua tafsiri yake…Unachopaswa kufanya ni kudumu katika utakatifu na maombi na kusoma Neno lake.

Hivyo kwa kuhitimisha…Lijue sana Neno hiyo ndiyo silaha yetu..Na pia usihangaike huku na huko kutafuta ni kanisa gani lipo sahihi…hangaika usiku na mchana kujifunza Neno la Mungu, hangaika usiku na mchana kutafuta kuijua biblia inasema nini?…hangaika kumjua Yesu Kristo ni nani katika Maisha yako?,..kujua biblia inasema nini kuhusu uumbaji, kuhusu siku tunazoishi, kuhusu ubatizo kwanini uwepo?, kwanini tumeumbwa, kwanini tuanguke dhambini, na kwanini tuokolewe…isome sana kwasababu majibu yote yamo kwenye biblia…soma kitabu cha Matendo angalia kanisa la kwanza lilianzaje!..soma kitabu cha wakoritho angalia upendo unapaswa uweje, Soma kitabu cha Waebrania angalia tunaokolewaje kwa agano la damu.. tenga muda mrefu kusoma vitabu vyote taratibu na kwa umakini…na ufahamu utakaoupata huko kwa msaada wa Roho Mtakatifu ndipo utakaoamua ni wapi utulie,…Bwana atautumia huo kukuweka sehemu sahihi ya kumwabudu yeye.

Ubarikiwe sana.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe au piga namba hii 0789001312

Mada Nyinginezo:

MPINGA-KRISTO

MUUNGANIKO WA MADHEHEBU NI MPANGO WA MPINGA-KRISTO.

Nifanye nini ili niondokane na Hofu maishani mwangu?

Utii ni nini? na ni nani tunayepaswa kumtii au kutokumtii?

Nifanye nini ili niwe na uhakika nikifa naenda mbinguni?

MADHABAHU NI NINI?

MAANA YA RANGI KIBIBLIA.

USILALE USINGIZI WAKATI WA KUMNGOJEA BWANA.

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments