Title 8 May 2020

UWEZO WA KIPEKEE.

Kuna kipindi tuliishi bila kutegemea pua zetu kupumua, kuna kipindi tuliishi bila kutegemea midomo yetu kulia chakula…Na kipindi hicho si kingine zaidi ya kile kipindi ambacho tuliishi tumboni mwa mama zetu, kwa miezi 9 tuliishi maisha ya kimiujiza ujiza.. Hakuna mwanadamu yoyote anayeishi sasa ambaye hajapitia kuishi maisha hayo ya kimiujiza.

Hivyo si ajabu Bwana alisema… “….Imeandikwa, Mtu hataishi kwa mkate tu, ila kwa kila neno litokalo katika kinywa cha Mungu (Mathayo 4:4).

Kama kuna wakati maisha hayo yaliwezekana…hata sasa kuna mambo yanaonekana kama hayawezekani lakini yanawezekana.

Inaweza kuonekana haiwezekani kabisa leo kuishi maisha makamilifu yanayompendeza Mungu…lakini nataka nikuambie hilo linawezekana kabisa..kwasababu Bwana mwenyewe alisema tutakuwa wakamilifu kama Baba yetu alivyo mkamilifu…(Mathayo 5:48). Hivyo Mungu asiyeweza kusema uongo, hawezi kuumba kiumbe ambacho anajua atakipa jukumu kubwa zaidi ya uwezo wake…Kwasababu hiyo basi jinsi alivyotuumba sisi, anajua kabisa kuna namna au mazingira ambayo tukijiweka tutakuwa wakamilifu kama yeye anavyotaka sisi tuwe.

Na ukamilifu na utakatifu tunaouzungumzia sio ule wa kujisifu na kujibeza kwamba ni mkamilifu au mtakatifu mbele za Mungu, wala sio ule wa kujihesabia haki kwamba sifanyi hichi wala kile kama mtu Fulani au watu Fulani wanavyofanya…bali ukamilifu na utakatifu unaozungumziwa ni ule wa roho ya unyenyekevu, na ya kumwogopa Mungu, ambao huo unaleta moyo wa toba siku zote mbele za Mungu na hofu ya Mungu…ambapo hofu hiyo itakuzuia wewe kutokufanya mambo yote yasiyompendeza Mungu, hofu hiyo itakufanya usidhubutu kwenda kuzini, mawazo ya uzinzi yanapokujia unayashinda ndani ya sekunde chache sana, pia hofu hiyo inakuzuia kwenda kuiba, kwenda kutoa mimba, kwenda kula rushwa, n.k..Na haikufanyi wewe kujilinganisha na wengine au kufurahia wengine wanapofanya mambo ambayo wewe huyafanyi na kujifanya bora kupita hao…Yaani unapomwona mwingine anajiuza, unapata hisia kama ni dada yako au ndugu yako wa damu ndio yupo vile, lakini sio kufurahia kana kwamba umemzidi utakatifu, na hivyo wewe ni heri kuliko yeye…Huo sio utakatifu bali ni kujibeza, ambako hakumpendezi Mungu.

Hivyo..huo uwezo wa kuwa mkamilifu kwa namna hiyo ya kumpendeza Baba…Tumeahidiwa kwenye Neno la Mungu kwamba “Unaweza ukashuka juu yetu na ni ahadi”..Tunauita ni uwezo kwasababu katika hali ya kawaida, ni ngumu kumpenda Yule mtu anayekuchukia, ni ngumu kumsamehe Yule mtu ambaye amekutendea ubaya mkubwa sana, ni ngumu kurudisha mali ya Yule mtu aliyekuibia, ni ngumu kuacha uasherati au ukahaba unaokuingizia kipato kizuri n.k…Hivyo inahitajika uwezo mwingine kushuka juu yetu. Na huo uwezo ukishuka ndio unatufanya tuishi kimiujiza kama tulivyokuwa tunaishi kipindi Fulani huko nyuma tulivyokuwa tumboni mwa mama zetu…

Tulikuwa na pua lakini tulikuwa huituitumii tumboni, tulikuwa na midomo lakini tulikuwa huutumii kula..lakini bado tulikuwa tunaishi na kukua…Hali kadhalika ukiupokea huu uwezo leo, watu watashangaa unawezaje kuishi bila kufanya uzinzi na hali una uwezo wa kufanya hayo yote, na mazingira yanakuruhusu…wewe mwenyewe utajishangaa umewezaje kuishi bila kulewa tena pombe na ilihali una fedha za kukutosha kufanya hayo yote n.k.

Sasa uwezo huo utashuka juu yako endapo tu, utakubali tu kuviacha hivyo vitu…Kitu kimoja ambacho unahitaji kufahamu wewe ambaye bado hujampokea Yesu, ni kwamba Nguvu ya Roho Mtakatifu haiwezi kuzidi nguvu ya maamuzi yetu…maana yake ni kwamba Mungu hatulazimishi kama ma-robot kufanya mapenzi yake ingawa anao uwezo wa kufanya hivyo, ila hajachagua kufanya hivyo…anachokifanya ni kutuwekea chaguzi mbili mbele yetu…tuchague UZIMA au MAUTI. Tunapochagua uzima basi ndipo anatupa Baraka zote za Uzima ikiwemo UWEZO wa kuwa kama yeye.. Lakini tukichagua mauti hatatulazimisha kutupa uzima…Hivyo uchaguzi ni wetu.

Sasa hatuchagui kwa midomo…bali kwa vitendo..Maana yake ni kwamba kama ulikuwa unafanya kazi ya Bar, unaiacha mara moja, kama ulikuwa ni msikilizaji wa miziki ya kidunia kupitia simu yako unaifuta hiyo miziki na hizo video za kidunia zote pasipo kubakiza hata moja..kama ulikuwa ni mwizi na umeiba, unamrudishia Yule mtu mali yake uliyomuibia kama bado unayo na unakusudia kuacha wizi..kama ulikuwa unajiuza unaiacha hiyo biashara, kama ulikuwa ni mlevi hivyo hivyo unaacha kwenda ile Bar, na vitu vingine vyote visivyompendeza Mungu unajilazimisha kuviacha katika maisha yako Sasa Baba wa mbinguni akiona kwamba kwa vitendo umeacha mambo hayo…Ule uwezo unaushusha juu yako wakati huo huo ulipoamua kuyaweka chini maisha ya kale…

Kwasababu umeingia gharama ya kuyavua maisha yako ya kale, na yeye Baba wa mbinguni anaingia gharama ya kukutuza wewe usirudi tena nyuma..na anakutunza kwa njia gani?..kwa njia hiyo ya kukupa UWEZO wa kushinda Dhambi, na kuwa mkamilifu.

Sasa ndani ya kipindi kifupi baada ya wewe kuamua kuacha maisha ya dhambi kwa vitendo, utaona ile kiu ya pombe inakata ghafla, ile kiu ya kufanya ukahaba inakata ghafla, hupambani vita vikali kuukataa uasherati tofauti na hapo kwanza…mpaka wewe mwenyewe utajishangaa umekuwaje?..zamani ulikuwa ukipitisha siku mbili bila kunywa pombe unasikia kuumwa, lakini utashangaa inapita wiki, mara mwezi, mara mwaka hata ile hamu haipo..ulikuwa haipiti siku bila kujichua lakini utajikuta imepita wiki, mwezi na mwaka bila hata kukikumbuka hicho kitendo…sasa ukishafikia hatua kama hiyo basi ule uwezo umeshamiminwa ndani yako…na uwezo huo utaambatana na mambo mengine ya muhimu kama tuliyoyataja hapo juu..utajikuta unakuwa na hofu ya Mungu, na mtu wa kumpenda Mungu na kuzidi kujitenga na ulimwengu, pamoja na kuwa msaada kwa wengine ambao hawajaingia ndani ya Neema hiyo.

Kwahiyo kama wewe bado hujamwamini Yesu Kristo na bado hujapokea huo uwezo, tambua kwamba bado nafasi unayo…nguvu hiyo ni kutubadilisha ni zawadi kwetu sote kutoka kwa Baba, endapo tu tukimwamini Yesu..Hivyo basi popote pale ulipo tenga muda kadhaa peke yako binafsi, mwombe Mungu rehema..kisha kusudia kuacha yale yote uliomwomba akurehemu…Kumbuka kutubu maana yake ni kugeuka!..Hivyo matendo yako yana maana sana mbele za Mungu Baba zaidi ya maneno yako..

Pia inawezekana umeshamwamini Yesu, lakini umeomba muda mrefu uwezo huu ushuke juu yako, lakini bado huoni chochote, bado unajikuta unafanya punyeto, bado unajikuta unarudi kwenye ulevi, uasherati na ushirikina…kama unapitia hali kama hiyo basi fahamu kuwa hukutubu vizuri…Uliomba tu rehema..kwamba Bwana akusamehe tu hiki na kile..lakini hukukusudia kuviacha vile vitu kwa vitendo..bado ulikuwa ni miziki kwenye simu yako, bado ulikuwa unatembelea zile site za pornograph bado ulikuwa umejiungamanisha na makundi yale ya ulevi na walevi, na ndani kwako kulikuwa na chupa za bia, bado ulikuwa unarudi kwenye kazi yako ya Bar n.k..Hiyo ndio maana ule uwezo haukushuka ndani yako..lakini leo bado unayo nafasi..Tubu tu kwa kuacha hayo mambo na Bwana atakushushia uwezo huo wa kuishi kimiujiza kama aliokupa wakati ule ulipokuwa tumboni mwa mama yako.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312

jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Mada Nyinginezo:

MUUNGANIKO WA MADHEHEBU NI MPANGO WA MPINGA-KRISTO.

NAMI NINAZO FUNGUO ZA MAUTI, NA ZA KUZIMU.

JE MOYO WAKO NI MNYOFU MBELE ZA MUNGU

Je ni sahihi kumtenga mtu anapofanya dhambi kanisani?

Mbona Mungu anaruhusu watu wapate shida, ilhali ana uwezo wa kutuepusha?

Kwanini Mungu alisema hakuna mtu awazaye kuuona uso wake akaishi?

Rudi Nyumbani:

Print this post

JINSI DHAMBI INAVYOMGHARIMU MTU SANA.

Mwanzo 47:9 “Yakobo akamjibu Farao, Siku za miaka ya kusafiri kwangu ni mia na thelathini; siku za miaka ya maisha yangu zimekuwa chache, TENA ZA TAABU, wala hazikufikilia siku za miaka ya maisha ya baba zangu katika siku za kusafiri kwao.”

Hakuna dhambi isiyokuwa na gharama. Unaweza ukajiuliza ni kwanini Yakobo alimwambia Farao siku zake za kusafiri duniani zimekuwa ni za taabu, zisizoweza kufananishwa na za baba zake..?..

Ni kwasababu ya ujanja alioufanya wa kumdanganya baba yake na kuchukua mbaraka wa ndugu yake, Japo ni kweli ndani yake kulikuwa na mpango wa Mungu uliobeba ujumbe uliomhusu Mesia, lakini kitendo alichokifanya bado kilikuwa ni uovu..Na hiyo haikuzuia kutumikia adhabu ya uovu wake.

Na ndio maana utaona Yakobo baada ya kufanya kitendo kile alikimbilia kwa mjomba wake, hata yule mama yake aliyependana naye na kupatana kutenda uovu, ndio ikawa mwisho wa kuonana kwao tena mpaka mwisho wa miaka 20 mbeleni, kuonyesha kuwa upendo wowote wenye makubaliano yasiyo makamilifu huwa haudumu..

Na alipofika kwa mjomba yake Labani, na kukaa huko, akimtumikia kwa ajili ya Raheli mke wake, kwa miaka saba, akidhani sasa ndio anakwenda kumpata Raheli, kumbe mjomba yake Labani akamfanyia hila kama ile ile aliyomfanyia ndugu yake Esau, matokeo yake akapewa dada yake Lea ndio awe mke wake badala ya Raheli, hivyo Labani akamwambia akimtaka na Raheli pia ni lazima amtumie miaka saba mingine..

Akaendelea kuwa mtumishi kwa muda mrefu mingine, mpaka wakati anaondoka, Na kwenda kule Kaanani nchi ya baba yake. Huko nako Watoto wake wawili Simeoni na Lawi, wakamfanyia hila kwa kudanganya, mpaka wakaenda kuwauwa watu wasiokuwa na hatia (Mwanzo 34),

Kama hiyo haitoshi, mwanawe wa kwanza Reubeni, akamzunguka baba yake, naye pia akamfanyia hila akaenda kulala na mke wake.

Tena Zaidi ya hayo, Watoto wake wakamfanyia hila kubwa Zaidi, kumdanganya kuwa mtoto wake Yusufu ampendaye ameliwa na mnyama mkali porini..Ikimfanya alie sana na kuomboleza kwa uchungu mwingi..

Kwahiyo unaweza kuona Maisha ya Yakobo, yalikuwa ni ya kudanganywa danganywa tu, na kufanyiwa hila kila kukicha, tofauti na ilivyokuwa kwa Ibrahimu na Isaka..

Kwasababu biblia inasema…

Mathayo 7:2 “Kwa kuwa hukumu ile mhukumuyo, ndiyo mtakayohukumiwa; na kipimo kile mpimiacho, ndicho mtakachopimiwa”.

Na ndio maana utaona anakiri kabisa Maisha yake yalikuwa ni ya taabu,..Lakini mwishoni kabisa Mungu alikuja kumpa faraja, kupitia mwanawe Yusufu.

Sasa huyo alikuwa ni Yakobo, mtu aliyebarikiwa na Mungu, lakini hakuachwa bila adhabu ya muda mrefu hapa duniani. Tujiulize sisi ambao tunaoendelea kuishi katika Maisha ya dhambi, Maisha yetu sikuzote ni ya dhuluma, tutawezaje kupona tusipouthamini wokovu mkuu namna hii?

Mithali 11:31 “Tazama, mwenye haki atalipwa duniani; Basi mwovu na mkosaji si mara nyingi Zaidi”

Adhabu hizi za mwilini zinafunua zile za rohoni..Wapo wanaodhani ukifa tu, ndio umekufa hakuna adhabu baada ya hapa…Adhabu ipo kwa wakosaji wote. Lakini Neema ya Mungu pia ipo kutukinga na adhabu hizo.

Na neema yenyewe ni kupitia YESU KRISTO. Tukimkabidhi Maisha yetu atatusamehe na kutugeuza na kutufanya kuwa wapya tena. Atafuta hata deni la dhambi na adhabu tulizostahili kuzipokea katika utoaji mimba wetu, katika uuaji wetu, katika rushwa zetu, katika uongo wetu, katika wizi wetu, katika uzinzi wetu, katika utapeli wetu n.k. Na hiyo ndio faida ya agano hili jipya la neema lililo katika damu ya YESU.

Hivyo kimbilia leo msalabani ikiwa bado hujaaokoka, tubu dhambi zako, ukabatizwe, usamehewe dhambi zako kisha upokee Roho Mtakatifu, atakaye kuwa na wewe hadi siku ile ya mwisho ya Unyakuo.

Bwana akubariki sana.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312

jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Mada Nyinginezo:

Amin, nawaambia, Kizazi hiki hakitapita, hata hayo yote yatakapotimia..!!

KWANINI UNAPASWA UJIWEKE TAYARI SASA, KABLA YA ULE WAKATI KUFIKA?.

USIJITAFUTIE KULAMBWA NA MBWA KWA DHAMBI YA KUTAMANI.

MAONO YA NABII AMOSI.

Je Mtu anaweza kusema uongo, Na Mungu akambariki?

MKUMBUKE MKE WA LUTU.

MPINGA-KRISTO

Rudi Nyumbani:

Print this post

Je ni sahihi kumtenga mtu anapofanya dhambi kanisani?

JIBU: Yapo makundi mawili kanisani..kundi la kwanza ni lile ambalo linahusisha washirika, ambalo ndani yake kuna wachungaji, waalimu, wainjilisti, mashemasi na waumini na wengineo…Kundi lote hili linahusisha washirika ambao tayari wameshamwamini Yesu Kristo, na kubatizwa na kupokea Roho Mtakatifu…hali kadhalika wameshajifunza Neno vya kutosha na kukolea katika maarifa ya ki-Mungu…hata kufikia kiasi cha kuweza kuwaelekeza na kuwaelekeza wengine katika njia ya wokovu.

Na kundi la pili ni lile la watu waliookoka karibuni, au walioingia katika Imani kipindi cha hivi karibuni..Wengi wa hawa unakuta ni wachanga kiimani, na mara nyingi wanakuwa ni wageni…Hivyo wanakuwa bado wanahitaji msaada katika kujifunza Imani na uweza wa Mungu..Na kwasababu wametoka katika ulimwengu bado kuna tabia baadhi baadhi wanakuwa hawajaziacha kutokana na kwamba pengine hawajajua Neno la Mungu linasemaje kuhusu mambo hayo wanayoyafanya.

Sasa katika lile kundi la kwanza ambalo linahusisha washirika ambao tayari wameshaijua kweli ya Mungu kwa utimilifu mkubwa…wameshajua na kufundishwa uasherati ni dhambi, wizi ni dhambi, ulevi ni dhambi n.k…Wakakengeuka na kurudia matapishi na kufanya mojawapo ya dhambi hizo ambazo tayari walishajifunza kuwa ni machukizo kwa Mungu…Mtu wa Namna hiyo kimaandiko ANAPASWA ATENGWE!!…Na endapo asipotengwa wale ambao wanapaswa wamtenge watakuwa WANAFANYA DHAMBI MBELE ZA MUNGU!!…Hivyo ni agizo la Mungu kwamba ni lazima atengwe…

Na kutengwa huko kunahusisha, yeye kutoonekana maeneo au mazingira ya kanisa kwa kipindi kirefu…Na washirika wengine hawatakiwi hata kumsalimia wala kushirikiana naye kwa lolote lile, hata hata kama atatubu…atakaa mwenyewe kwa kipindi chote hicho…mpaka wakati ambao Kanisa litasikia amani ya Roho kumrudisha…na wakati huo wa kutengwa huku akiwa katika hali ya toba na maombolezo, Mungu atakuwa anamrudi kwa aliyoyafanya. Hivyo hakuna raha yoyote katika kutengwa, kama kweli ni mtoto wa Mungu. Kwasababu asipotolewa katika kanisa, watu wote wataiga na hawatamwogopa Mungu..Hivyo ili kuzuia hilo, biblia imeruhusu kumwondoa mtu huyo ili kanisa zima lisiharibike…

Utauliza ni wapi maandiko yanasema hivyo?

1Wakorintho 5:1 “Yakini habari imeenea ya kuwa kwenu kuna zinaa, na zinaa ya namna isiyokuwako hata katika Mataifa, kwamba mtu awe na mke wa babaye.

2 Nanyi mwajivuna, wala hamkusikitika, ili kwamba aondolewe miongoni mwenu huyo aliyetenda jambo hilo.

3 Kwa maana kweli, nisipokuwapo kwa mwili, lakini nikiwapo kwa roho, mimi mwenyewe nimekwisha kumhukumu yeye aliyetenda jambo hilo, kana kwamba nikiwapo.

4 Katika jina la Bwana wetu Yesu, ninyi mkiwa mmekusanyika pamoja na roho yangu, pamoja na uweza wa Bwana wetu Yesu;

5 kumtolea Shetani mtu huyo, ili mwili uadhibiwe, ili na roho iokolewe katika siku ya Bwana Yesu.

6 Kujisifu kwenu si kuzuri. Hamjui kwamba chachu kidogo hulichachusha donge zima

9 Naliwaandikia katika waraka wangu, kwamba msichangamane na wazinzi.

10 Sisemi msichangamane kabisa na wazinzi wa dunia hii, au na wenye kutamani, au na wanyang’anyi, au na wenye kuabudu sanamu; maana hapo ingewalazimu kutoka katika dunia.

11 Lakini, mambo yalivyo, naliwaandikia kwamba msichangamane na mtu aitwaye ndugu, akiwa ni mzinzi au mwenye kutamani au mwenye kuabudu sanamu au mtukanaji au mlevi au mnyang’anyi; mtu wa namna hii msikubali hata kula naye.

12 Maana yanihusu nini kuwahukumu wale walio nje? Ninyi hamwahukumu hao walio ndani?

13 Lakini hao walio nje Mungu atawahukumu. Ninyi mwondoeni yule mbaya miongoni mwenu.”

Soma pia..

2Wathesalonike 3:14 “Na ikiwa mtu awaye yote halishiki neno letu la waraka huu, jihadharini na mtu huyo, wala msizungumze naye, apate kutahayari; 15 lakini msimhesabu kuwa adui, bali mwonyeni kama ndugu”.

Hivyo kuna hatari sana ya kufanya dhambi za makusudi baada ya kuujua ukweli..Tunakuwa tunakabidhiwa shetani ashughulike na sisi, Hivyo tujihakiki na Bwana atuepushe na hayo yote.

Maran atha!

jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Mada Nyinginezo:

Je! mtu aliyeokoka anaruhusiwa kumiliki Lodge ambayo ina Bar ndani yake?

Mahuru ndio nini?

Kwanini Mungu alisema hakuna mtu awazaye kuuona uso wake akaishi?

Je Mtu anaweza kusema uongo, Na Mungu akambariki?

Nini maana ya mstari huu: (Mtu ambarikiye mwenzake kwa sauti kuu asubuhi na mapema; Itahesabiwa kuwa ni laana kwake.Mithali 27:14 )?

https://wingulamashahidi.org/2019/09/01/maana-ya-huu-mstari-ni-ipi-mithali-144-zizi-ni-safi-ambapo-hapana-ngombebali-nguvu-za-ngombe-zaleta-faida-nyingi/

Rudi Nyumbani:

Print this post

NAMI NINAZO FUNGUO ZA MAUTI, NA ZA KUZIMU.

Ufunuo 1: 17 “…Usiogope, Mimi ni wa kwanza na wa mwisho,

18 na aliye hai; nami nalikuwa nimekufa, na tazama, ni hai hata milele na milele. Nami ninazo funguo za mauti, na za kuzimu”.

Hayo ni Maneno ya Bwana wetu Yesu Kristo, akiliambia kanisa.. Sasa ukiona mpaka Bwana Yesu anasema anazo funguo za mauti, na kuzimu, ni dhahiri kuwa hapo mwanzo hakuwa nazo, zilikuwa kwa mwingine..Na huyo si mwingine zaidi ya Ibilisi.

Kumbuka Tahadhari ya kwanza Mungu aliyowapa Adamu na Hawa pale Edeni, kuhusu kula Tunda, haikuwa kwamba matokeo yake watakuwa uchi, au watajua mema na mabaya au watakula kwa jasho, au watazaa kuwa uchungu . Hapana, bali tahadhari aliyowapa ya kwanza na ya mwisho ilikuwa ni kuwa WATAKUFA(‘KIFO’)..Siku watakapokula matunda ya mti ule watakufa..akimaanisha watakufa kweli kweli..sio kwamba watakufa halafu siku moja watafufuka hapana, bali watakufa moja kwa moja..

Kwasababu Mungu alimwona muhasisi wa kifo hicho pale Edeni, Lakini wazazi wetu hawakuzingatia hilo badala yake wakala, Na matokeo yake ndio yale tuliyoyaona yalifuata baada ya pale..watu wakawa na makao mengine, baada ya pale yaliyoitwa KUZIMU. Chini ya mungu wao mpya aliyeitwa Ibilisi.

Na ndio maana katika agano la kale, hakukuwa na mtu aliyekuwa na uhakika wa maisha baada ya kifo, ni waisraeli tu ndio walifahamu hilo, nao si wote, isipokuwa wale tu waliokuwa wanafuatailia masuala ya Mesiya, ambaye alitabiriwa kuwa huko mbele atakuja kuwafufua wafu, lakini wengine waliosalia hawakujua hilo…

Na ndio maana tena utaona kulikuwa na mapambano makali kati ya mafarisayo na masadukayo, wengine waliamini kuna ufufuo wa wafu, na wengine hawakuamini hicho kitu (Soma, Matendo 4;1-2,23:7-8, Marko 12:18)..Ni kwasababu gani? Ni kwasababu suala la wafu kufufuliwa lilikuwa si jambo lililoandikwa kwa uwazi sana katika maandiko kama wengi wanavyodhani.. isipokuwa tu waliotambua jambo hilo ni wale waliokuwa wanafuatilia habari za Mesiya kuwa atakuja kufanya jambo hilo.

Kwahiyo wakati wote huo watu walikuwa wametawaliwa na roho ya mauti ya ibilisi.

Warumi 5:14 “walakini mauti ilitawala tangu Adamu mpaka Musa, nayo iliwatawala hata wao wasiofanya dhambi ifananayo na kosa la Adamu, aliye mfano wake yeye atakayekuja”.

Unaona wakati huo wote shetani alikuwa na funguo hizo, alikuwa wakati mwingine anao uwezo hata wa kuwaendea wafu walio watakatifu na kuzungumza nao, soma habari za samweli(1Samweli 28)..

Lakini sasa Kristo alipokuja alipindua kila kitu,(majira yakageuka), kwanza aliiondoa hofu ya mauti ambayo ilikuwa imewatawala wanadamu kwa muda mrefu tangu zamani..

Waebrania 2:14 “Basi, kwa kuwa watoto wameshiriki damu na mwili, yeye naye vivyo hivyo alishiriki yayo hayo, ili kwa njia ya mauti amharibu yeye aliyekuwa na nguvu za mauti, yaani, Ibilisi,

15 awaache huru wale ambao kwamba maisha yao yote kwa hofu ya mauti walikuwa katika hali ya utumwa”.

Na pili akaiteka ile Kuzimu iliyokuwa chini ya shetani, ambayo ndio ilikuwa makao ya wafu wote…

Na ndio maana siku ile alipokufa tu, utasoma makaburi yalipasuka na watakatifu wengi wakatoka makaburini

Mathayo 27:51 “Na tazama, pazia la hekalu likapasuka vipande viwili toka juu hata chini; nchi ikatetemeka; miamba ikapasuka;

52 makaburi yakafunuka; ikainuka miili mingi ya watakatifu waliolala;

53 nao wakiisha kutoka makaburini mwao, baada ya kufufuka kwake, wakauingia mji mtakatifu, wakawatokea wengi”.

Tangu huo wakati hadi leo ibilisi hajui wafu wapo wapi na wanafanya nini saa hii, anachojua tu, ni kuwa wale watakatifu wapo upande wa PEPO(Paradiso) na wale waovu wapo sehemu ya mateso (Jehanum)..Hana uwezo wa kuleta mzimu wa mtu yeyote aliyekufa kwasababu sasahivi Kristo ndiye anayewamiliki walio hai na waliokufa soma Warumi 14:9. Kwahiyo hivyo vinavyoonekana na watu vyenye sura kama za wapendwa waliokufa..kiuhalisia sio wale watu wenyewe, bali ni roho tu za mapepo zilizovaa sura za watu waliokufa…

Kristo sasa ameshashikilia mamlaka yote, ya mbinguni, ya duniani na ya kuzimu..Haleluya.

Hivyo ikiwa wewe ni mtakatifu, kama utakufa leo basi ujue roho yako na nafsi yako itakwenda sehemu salama, yenye raha na pumziko la kweli, mahali pasipoelezeka panapoitwa Pepo, lakini wewe ambaye ni mwenye dhambi, ukifa leo, shetani hakuchukui bali utakayekuchuwa na Mungu mwenyewe na kwenda kukutupa katika jehanamu ya moto ukingoja hukumu ya siku ile ya mwisho..

Unatanga tanga nini kwa waganga wa kienyeji? Hao hawatakusaidia chochote, unawatafuta wanadamu, hao nao hawawezi kukuondolea hofu ya mauti na mashaka uliyonayo sasa, kwamba ukifa utakwenda wapi..Anayeweza kufanya hivyo ni Kristo tu peke yake, mwenye funguo za mauti na kuzimu.Yeye ndiye atakayeweza kukufanya uwe huru na hofu ya kifo, kiasi kwamba hata ikitokea unakufa leo, utakuwa na uhakika kuwa roho yako imekwenda sehemu salama. Ukingojea siku ile kuu ya kwenda mbinguni kwa Baba.

Hivyo leo mpe Kristo maisha yako kama bado hujampa, vivyo hivyo kama ni vuguvugu huu ni wakati wa kuwa moto!.. Tubu dhambi zao kwa kumaanisha kuziacha, hizi ni nyakati za mwisho, parapanda italia wakati wowote, na Yesu atawafufua kwanza wale waliokufa katika haki nao kwa pamoja na sisi tulio hai tutakwenda kumlaki mawinguni,..lakini jiulize wewe mwenye dhambi utakuwa wapi siku hiyo?..Au ukifa leo hii ni nani atayekusaidia huko uendako? Shetani anaivizia roho yako kwasababu anajua ukifa katika dhambi ni umepotea kwelikweli hata yeye mwenyewe hata kuona milele…Hivyo acha leo ulevi, wizi, rushwa, anasa, uasherati, vipodozi unavyopaka, vimini unavyovaa, matusi unayotukana na mambo yote yanayofanana na hayo..Na upokee Roho Mtakatifu ambaye ni ahadi kwetu tutakaomwamini Yesu.

Uamuzi ni wako, tafakari tena kisha chagua uzima. Wokovu ni bure kwa wote wanaouhitaji..Kristo anaokoa kweli.

Shalom.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312

jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Mada Nyinginezo:

TOFAUTI KATI YA HEKALU, SINAGOGI NA KANISA NI IPI?

Nifanye nini ili niondokane na Hofu maishani mwangu?

SI KWA FAIDA YA MWENYEZI, BALI KWA FAIDA YETU.

MWAKA WA BWANA ULIOKUBALIWA.

NAO WAKADHANI YA KUWA YUMO KATIKA MSAFARA;

Nini maana ya maneno haya ya Bwana? “Nami nikiinuliwa juu ya nchi,NITAWAVUTA WOTE KWANGU”(Yohana12:32).

Rudi Nyumbani:

Print this post