Nini maana ya ‘Usimwekee mtu mikono kwa haraka’?

Nini maana ya ‘Usimwekee mtu mikono kwa haraka’?

SWALI: Andiko hili lina maana gani?..1Timotheo 5: 22 “Usimwekee mtu mikono kwa haraka, wala usizishiriki dhambi za watu wengine. Ujilinde nafsi yako uwe safi”


JIBU: Maana ya awali ya mstari huo sio ile inayodhaniwa na wengi ya “Mtumishi wa Mungu, kumwekea mikono mtu mwenye tatizo fulani au ugonjwa fulani” na kumwombea…Hiyo sio maana ya msingi ya mstari huo…inaweza kuwa maana ya pili ya mstari huo …lakini maana ya msingi kabisa ya mstari huo ni “kuwekewa mikono kwa ajili ya utumishi”.

Huu ni waraka ambao Mtume Paulo alimwandikia Timotheo ambaye alikuwa ni mtumishi wa Mungu…Paulo alimfundisha madaraka ya kuitumishi kwa uongozo wa Roho Mtakatifu, ambayo unaweza kuyasoma yote katika wakara huo (yaani kuanzia sura ya kwanza hadi ya mwisho). Na mojawapo ya madaraka aliyompa ni madaraka ya kuwawekea mikono watumishi wapya, wale ambao tayari karama zao zimeshaanza kuonekana katika kanisa hivyo wapo tayari kuifanya kazi ya ki-utumishi katika mwili wa Kristo..kama jinsi yeye alivyowekewa..

1Timotheo 4:14 “Usiache kuitumia karama ile iliyomo ndani yako, uliyopewa kwa unabii na kwa KUWEKEWA MIKONO YA WAZEE”

Kwahiyo hapa Timotheo naye anaagizwa wakati wa kuwawekea mikono watumishi wapya (mfano..maaskofu wapya, wachungaji wapya wa makanisa, waalimu, au manabii) asiwe na haraka!…bali achukue muda kumsoma mtu yule, tabia yake, mwenendo wake, je kama ni kweli kaitwa, ama ni kweli ana nia ya Kristo, kama ni kweli amekidhi vigezo vyote vya kimaandiko..Ndipo amtie mikono na kumbariki.

Kwasababu wale waliotiwa mikono ni kama wamehalalishwa kuwa wamestahili kulitumikia kundi la Mungu, na hivyo watu wengi ni rahisi kuwaamini, kwahivyo endapo akiwekewa mikono mtu ambaye si sahihi, ambaye hana nia ya Kristo, ni mtu wa kidunia tu, anawaza fedha au ukubwa tu…na kundi lote likimwamini, basi ni rahisi kuleta uharibifu mkubwa sana katika kanisa…Ndio maana hapo juu Mtume Paulo anamwagiza Timotheo na kumwambia “asiwe mwepesi kumwekea mtu mikono kwa haraka”, maana yake achukue muda kumchunguza..

Na hata sasa makanisani inapaswa iwe hivyo hivyo..Kabla ya mtu kuwekewa mikono kuwa mchungaji, au askofu, au shemasi, au nabii, au mwalimu ni lazima awe ameshajaribiwa na kuhakikiwa vya kutosha ili asije akaliharibu kundi, vigezo vya uaskofu vinapatikana katika hiyo hiyo 1Timotheo

1Timotheo 3:1 “Ni neno la kuaminiwa; mtu akitaka kazi ya askofu, atamani kazi njema.

2 Basi imempasa askofu awe mtu asiyelaumika, mume wa mke mmoja, mwenye kiasi na busara, mtu wa utaratibu, mkaribishaji, ajuaye kufundisha;

3 si mtu wa kuzoelea ulevi, si mpiga watu; bali awe mpole; si mtu wa kujadiliana, wala asiwe mwenye kupenda fedha;

4 mwenye kuisimamia nyumba yake vema, ajuaye kutiisha watoto katika ustahivu;

5 (yaani, mtu asiyejua kuisimamia nyumba yake mwenyewe, atalitunzaje Kanisa la Mungu?)

6 Wala asiwe mtu aliyeongoka karibu, asije akajivuna akaanguka katika hukumu ya Ibilisi

7 Tena imempasa kushuhudiwa mema na watu walio nje; ili asianguke katika lawama na mtego wa Ibilisi.”.

Hiyo ndio maana ya awali ya KUMWEKEA MTU MIKONO, iliyomaanishwa katika mstari huo…Maana ya pili ndio ile inayojulikana na wengi, ambayo ni ya kumfahamu mtu kwanza kabla ya kumwekea mikono kumwombea..

Wengi hususani watumishi mtu anapokuja ana tatizo fulani, au ugonjwa fulani ni wepesi kumwekea tu mikono pasipo kumjua mtu huyo kwa undani..ili tu mtu aonekane ni mtumishi wa Mungu…pasipo kujua ni hatari kufanya hivyo…Kwasababu unaweza kujikuta unalaani kilichobarikiwa au una bariki kilicholaaniwa.

Kwamfano mtu unaweza kukuta anafanya kazi ya madawa ya kulevya, au ujambazi, au ya ukahaba au uzaji pombe..na yeye anakuja kwako kuomba kazi zake ziende vizuri (mtu kama huyo alishawahi kunifuata mimi)..na wewe pasipo kufikiri, kwasababu kaja tu kutafuta msaada kutoka kwako, unamwekea mikono na kumbariki katika jina la Bwana…(hapo umebariki kilicholaaniwa.).

Badala yake ungepaswa umhoji kwanza shughuli anayoifanya, na kama akikiri ni ya madawa ya kulevya basi, unamhubiria kwanza atubu na kumpa Kristo Maisha yake, na kutafuta kazi nyingine ndipo umeombee baraka kwa Mungu wako na ndipo huyo mtu abarikiwe..

Wengine ni makahaba na hawajui kama katika ukahaba wao wanamkosea Mungu (nimewahi kukutana na kahaba ambaye katika ukahaba wake aliniambia anamwamini Mungu, na huwa Mungu anamleteaga wateja, na huwa anaiombeaga biashara yake mara kwa mara ili iende vizuri)..baada ya kumhubiria sana ndipo alipoelewa kwamba alikuwa anafanya makosa pasipo kujijua…Sasa mwanamke kama huyu, anapokwenda kanisani au kwa mtumishi ambapo hataulizwa maisha yake ni rahisi watu kuibariki kazi iliyo laaniwa na Mungu..Hivyo ni kuwa makini sana.

Na pia tumeonywa hapo! Tusizishiriki dhambi za watu wengine, unapomwekea mtu mikono kwa pupa ni rahisi kuzishiriki dhambi za yule mtu, kadhalika unaposhirikiana na watu waovu katika kanisa ambao wanajua kabisa mambo wanayoyafanya ni kinyume na maandiko lakini bado wanaendelea kuyafanya huko ni sawa na kuzishiriki dhambi zao..

Bwana atusaidie tuwe wakamilifu mbele zake daima.

Maran atha!

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312

Mada Nyinginezo:

VIFO VYA MITUME WA YESU/ JINSI MITUME WALIVYOKUFA.

Uasherati wa Kiroho maana yake nini?

HAKI HAIMWACHI KUISHI.

NA MTU MMOJA AKAVUTA UPINDE KWA KUBAHATISHA, AKAMPIGA MFALME

JIEPUSHE NA MASHINDANO YA DINI.

KUSUDI LA MIMI KUWEPO DUNIANI NI LIPI?

YA KALE YAMEPITA, TAZAMA YAMEKUWA MAPYA

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments