Title kuota unasafiri

KUOTA UNASAFIRI.

Napendelea kabla mtu hajakimbilia kutafuta tafsiri ya ndoto yake, ni vizuri kwanza apate  elimu juu  ya aina za ndoto, hiyo itamsaidia kujua ndoto yake inaangukia katika kundi la aina gani, hivyo atapata wepesi wa kuweza yeye mwenyewe kuzitafsiri ndoto pasipo hata kutegemea msaada wa mtu mwingine.

Ikiwa utapenda kujua aina hizi za ndoto bofya hapa >>  NITAJUAJE KAMA NDOTO NI YA MUNGU AU YA SHETANI?   ukishamaliza kusoma kisha tuendelee…

Sasa kama ndoto yako sio ile inayotokana na shughuli za kila siku au mazingira yanayokuzunguka na unaiota mara kwa mara, basi fahamu kuwa kuna jambo Mungu anazungumza na wewe hapo zingatia sana..Biblia inasema..

Ayubu 33:14 “Kwa kuwa Mungu hunena mara moja, Naam, hata mara ya pili, ajapokuwa mtu hajali.

15 Katika ndoto, katika maono ya usiku, Usingizi mzito uwajiliapo watu, Katika usingizi kitandani;

16 Ndipo huyafunua masikio ya watu, Na kuyatia muhuri mafundisho yao,”

Mungu anakukumbusha kuwa upo safarini hapa duniani, kwamba kila jambo unalolifanya ukumbuke kuwa upo safarini hakuna na chochote utashikamana nacho hapa duniani milele,..

Na kama tunavyojua safarini, hata mkishuka kupumzika pengine kula au kujisaidia basi  ni dakika chache tu 10 au 15 basi safari inaendelea, hakuna muda wa kuzurura zurura au kuanza kujihangaisha na mambo ya hapo mlipokuwa mnapita, utakuwa ni mjinga kama utawaza kuwekeza eneo hilo, au kwenda kufanya shughuli hapo, gari litaondoka na kukuacha, na mwisho wa siku kule ulipokuwa unatazamia kwenda hutafika..

Hivyo Mungu kukuonyesha hivyo ni kukuonya usiangalie sana mambo ya ulimwengu huu yanayopita bali angalia vya kule mbele vinavyodumu na ukumbuke kuwa upo safarini, inamaanisha kuwa kwa namna moja au nyingine ulishawahi kuyatazama mambo ya kule, ishi kama maisha ya mpitaji, kwasababu watu wote wa Mungu ndivyo wanavyoishi..

Isaya 35:8 “Na hapo patakuwa na njia kuu, na njia, nayo itaitwa, Njia ya utakatifu; wasio safi hawatapita juu yake; bali itakuwa kwa ajili ya watu hao; wasafirio, wajapokuwa wajinga, hawatapotea katika njia hiyo.”

Hivyo angalia ni vitu gani vinavyokusonga katika maisha yako, Je! Ni shughuli za ulimwengu huu mpaka hauna muda na Mungu? Je! Ni tamaa ya mambo ya ulimwenguni huu, Je ni anasa? Biblia inasema:

1Petro 2:11 “Wapenzi, nawasihi kama wapitaji na wasafiri, ziepukeni tamaa za mwili zipiganazo na roho.

12 Mwe na mwenendo mzuri kati ya Mataifa, ili, iwapo huwasingizia kuwa watenda mabaya, wayatazamapo matendo yenu mazuri, wamtukuze Mungu siku ya kujiliwa.”

Hivyo Fahamu kuwa Mungu anakupenda na ndio maana amekuonyesha ndoto za namna hiyo, basi usipuuzie sauti yake, anza sasa kumtazama YESU ikiwa bado upo mbali naye, Unachopaswa kufanya ni kutubu sasa mkabidhi yeye maisha yako upya, nenda kabatizwe kwa ajili ya ondoleo la dhambi zako, kisha yeye mwenyewe atakupa kipawa cha Roho Mtakatifu…nawe utakuwa na uhakika wa kuwa salama katika safari yako fupi iliyobakia hapa duniani… Aidha kama utakuwa upo tayari ndani ya Kristo na unajihisi huna kando lolote basi fahamu kuwa Mungu anataka uzidi kuiangalia safari yako zaidi kuliko kitu kingine chochote, kwasababu ipo thawabu kubwa amekuandalia mbele.

Ubarikiwe.

Group la whatsapp Kwa mgawanyo bora wa masomo download App hapa>> App wingu la mashahidi

Mada Nyinginezo:

NJIA KUU YA KUINGIA KATIKA ULE MJI.

TAZAMA, NASIMAMA MLANGONI.

MFALME ANAKUJA.

NINI MAANA YA KUISHI KWA KUUKOMBOA WAKATI?.

CHANZO CHA MAMBO.

UNYAKUO.

SIKU YA HUKUMU ITAKUWAJE?


Rudi Nyumbani:

Print this post

KUOTA UNAENDESHA GARI.

Awali ya yote ni vizuri kufahamu kuwa asilimia kubwa ya ndoto tunazoota kila siku au mara kwa mara huwa zinatokana na mawazo yetu wenyewe, naweza kusema hata asilimia 95 ya ndoto zote tuziotazo usiku hutokana na sisi wenyewe, na hizo zinakuja  aidha kwa shughuli tunazozifanya kila siku au mazingira yanayotuzunguka au kitu tunachokiwaza sana…

Hivyo ndoto kama hizi, huwa hazibebi ujumbe wowote wa rohoni, ikitokea umeota  wewe zipuuzie tu vinginevyo utajikuta unachanganyikiwa ukidhani kuwa kila ndoto unayoota ina maana, ikiwa bado hujaweza kuzitofautisha aina za ndoto katika makundi yake basi pitia kwanza somo hili ili upate msingi kisha tuendelee. >>>NITAJUAJE KAMA NDOTO NI YA MUNGU AU YA SHETANI?

Lakini kama ndoto unayoota haihusiani na mazingira uliyopo, na huwa inajirudia mara kwa mara, basi lipo jambo ambalo Mungu anataka kukuonyesha hapo.

Sasa Kuota unaendesha gari na wakati mwingine umewapakiza watu nyuma,  ni ishara kwamba wewe mwenyewe unayaongoza maisha yako au maisha ya wengine, kukufikisha mahali Fulani au kuwafikisha mahali fulani..Kama wewe umeokoka na unalifanya kusudi la Mungu au unaifanya kazi ya Mungu basi zidisha mwendo katika safari yako kwasababu lengo lako utalifikia, kama hutapunguza mwendo kama alivyofanya Yehu, pale alipokuwa anakwenda kumuua Yule mfalme muasi Yoramu na mama yake Yezebeli waliowakosesha Israeli mpaka kupelekea wakaingia kwenye uchawi na ibada za sanamu, na Kumkasirisha Mungu kwa viwango vya juu sana.

2Wafalme 9:20 Yule mlinzi akatoa habari, akasema, Amewafikilia wala harudi tena; na mwendo huu ni kama mwendo wa Yehu mwana wa Nimshi; MAANA ANALIENDESHA GARI KWA KASI.

Hivyo kama unalo kusudi la Mungu mkononi mwako,litimize bila kuogopa kipingamizi au mitazamo ya watu..

Lakini pia,

unapaswa uwe makini ni gari la aina gani unatumia kuliendesha kusudi la Mungu wakati Fulani mfalme Daudi alikuwa analitoa sanduku la Mungu kutoka kwa Abinadabu kwenda Yerusalemu, lakini alifanya makosa kuwatumia ng’ombe kama usafiri wa kulisafirisha kusudi la Mungu badala ya kutumia watu tena makuhani ambao ndio Mungu aliowaagiza walibebe wakati wote,  wao wakawaweka ng’ombe kama magudurumu ya gari lao na ikapelekea kifo cha mtu mmoja..soma 1Nyakati 13:7

1Nyakati 13:7 “Hivyo Wakalipandisha sanduku la Mungu juu ya gari jipya kutoka nyumba ya Abinadabu; na Uza na Ahio WAKALIENDESHA LILE GARI.

8 Wakacheza Daudi na Israeli wote, mbele za Mungu, kwa nguvu zao zote; na kwa nyimbo na kwa vinubi, na kwa vinanda, na kwa matari, na kwa matoazi, na kwa tarumbeta.

9 Hata walipofika penye uga wa Nakoni, Uza akaunyosha mkono wake alishike sanduku; kwa maana wale ng’ombe walikunguwaa.

10 Ndipo hasira ya Bwana ikawaka juu ya Uza, naye akampiga, kwa sababu alilinyoshea sanduku mkono wake, hata akafa pale pale mbele za Mungu.

Hivyo uwe makini unapolifanya kusudi la Mungu na wale unaowaongoza, zingatia vigezo cha maandiko . Na ndio maana wengine wanaota wanaendesha vyombo tofauti tofauti , wengine wanaota wanaendesha malori, wengine wanaota wanaendesha baiskeli, wengine wanaota wanaendesha pikipiki n.k. Vyovyote vile, kuendesha ni kuendesha tu, hiyo ni kulingana na kusudi Mungu alilokupa cha msingi hapo ni kutimiza kusudi hilo kwa ukamilifu wote, ili uepuke kulaumiwa huko mbeleni.

Lakini kama unajijua wewe bado ni mwovu na hadi sasa upo katika dhambi, Hiyo ni Ishara mbaya sana kwako, Aidha Unajiongoza mwenyewe katika mauti au unawaongoza wengine katika mauti, au vyote viwili kwa pamoja..

2Nyakati 21:12 “Likamjia andiko kutoka kwa Eliya nabii, kusema, Bwana, Mungu wa Daudi baba yako, asema hivi, Kwa sababu hukuziendea njia za Yehoshafati baba yako, wala njia za Asa mfalme wa Yuda;

13 lakini umeiendea njia ya wafalme wa Israeli, UKAWAENDESHA KATIKA UASHERATI Yuda na wenyeji wa Yerusalemu, kama walivyofanya nyumba ya Ahabu; tena umewaua ndugu zako wa nyumba ya baba yako, waliokuwa wema kuliko wewe;

14 tazama, Bwana atawapiga pigo kubwa watu wako, na watoto wako, na wake zako, na mali yako yote;

15 nawe utakuwa na ugonjwa mkuu kwa maradhi ya matumbo, yatakapotokea matumbo yako kwa sababu ya ugonjwa huo siku kwa siku.

Unaona hapo huyu mfalme Yehoramu, alikuwa mtu mwovu, alikuwa ni muuaji, na mwabudu sanamu, akawafanya na Israeli wote wote wawe kama yeye, au kwa lugha nyingine akawaendesha waisraeli mpaka kwenye uasherati wa kiroho, kwa sababu hiyo basi Mungu akampiga kwa mapigo yale..

Hata na wewe, unayaongoza maisha yako sasa ukidhani kuwa upo salama, lakini mwisho wake utakuwa ni mauti kama hutatubu, unawasababishia wengine mauti wale walio chini yako, au wanaokutegemea, au wanaokutazama kwa mwenendo wako na maisha yako..

Hivyo Bwana anakupenda na ndio maana anakuonya Leo hii, Utubu umgeukie yeye, ili uliendeshe gari la maisha yako katika njia sahihi ya kutimiza makusudi ya Mungu na sio makusudio ya Shetani.

Ubarikiwe.

Pia kwa Maombezi, Ushauri, Maswali au Ratiba za Ibada Wasiliana nasi kwa namba

+225693036618/ +225789001312

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Mada Nyinginezo:

KUOTA UNAFANYA MTIHANI.

KUOTA UPO UCHI.

KUOTA UNAPAA.

KUOTA UNASAFIRI.

TOFAUTI KATI YA NDOTO NA MAONO NI IPI?

JE! KUBET NI DHAMBI?

AGANO LAKO LINABEBWA NA NANI?.


Rudi Nyumbani:

Print this post

KUOTA UPO UCHI.

Ufunuo 16:15 “(Tazama, naja kama mwivi. Heri akeshaye, na kuyatunza mavazi yake, asiende uchi hata watu wakaione aibu yake.)”

Kipindi Fulani nyuma kabla sijampa Bwana maisha yangu, niliota ndoto moja ambayo hadi leo sitaisahau, niliota nimejikuta nipo uchi, halafu nakatiza barabarani mjini maeneo ya posta Dar es salaam, sasa nilipojiona nipo vile nikawa ninatafuta namna ya kujificha..

Nikawa ninajibanza banza kwenye vikona vya majengo, nikivizia watu wapungue kisha nikimbilie upande mwingine, hivyo hivyo hadi kigiza kingie nikimbilie nyumbani, na kweli nilifanikiwa kujificha ficha hivyo hivyo nisionekane na watu au marafiki zangu mpaka nilipofanikiwa kufika  nyumbani nikafurahi sana kwasababu nilijiona kama sijaoenekana  na watu wengi, hususani na wanaonijua, lakini muda kidogo nikashangaa marafiki zangu wa chuo, tena wa kike wananijia kwa mshangao, wakiniambia mbona tumeona picha zako na video zako zimezagaa mtandaoni ukiwa uchi unakatiza barabarani, kwa kweli wakati nikiwa huko huko kwenye ndoto niliishiwa nguvu, nilijiona nipo katika aibu na fedheha ya milele isiyoweza kufutika, nikawa nawaza ni heri nisingezaliwa, kwasababu jambo kama  lile halina tofauti na wale wanaoigiza mikanda ya video za zinaa, ambalo litaendelea kuwepo mitandaoni daima..

Sasa wakati nikiwa katika hali mbaya sana huko huko kwenye ndoto neno moja la kiingereza likaja mbele yangu, ambalo sikuwahi hata kulijua wala kulisoma mahali popote na hilo ndilo lililonifanya mpaka leo hii ninaikumbuka ndoto hiyo na neno lenyewe ni hili “NUDE”.. Muda huo huo nikashutuka,  nikafurahi kwa kuwa kwa kuwa ilikuwa ni ndoto lakini nikasema ngoja nilitazame kwenye kamusi ya kiingereza lile neno lina maana gani ndipo nikakuta lina maana ile ile ya UCHI kama nilivyokuwa katika ndoto.

Kwa kweli nilikaa muda mrefu sana bila kuelewa ndoto ile ilikuwa na maana gani. Lakini siku nilipokuja kumpa Kristo maisha yangu, ndipo Bwana aliponifundisha maana ya ile ndoto niliyoita.. Nataka nikuambie ukiota ndoto yoyote upo uchi, halafu upo katikati ya kadamnasi, au mahali popote pale iwe shuleni, au kazini, au stendi ya mabasi, au sokoni, basi fahamu kuwa ndivyo hali yako ya kiroho ilivyo kwa sasa.

Sikuzote UCHI unazaa ni Aibu, na Aibu inakupelekea mtu kwenda kujificha..Adamu na Hawa walipoasi pale Edeni, walijiona kuwa wapo uchi, ndipo aibu ikawaingia na hapo hakuna kingine zaidi ya kwenda kutafuta namna ya kujisitiri..

Mwanzo 3:8 “Kisha wakasikia sauti ya Bwana Mungu, akitembea bustanini wakati wa jua kupunga; Adamu na mkewe wakajificha kati ya miti ya bustani, Bwana Mungu asiwaone.

9 Bwana Mungu akamwita Adamu, akamwambia, Uko wapi?

10 Akasema, Nalisikia sauti yako bustanini, nikaogopa kwa kuwa mimi ni uchi; nikajificha”.

Hivyo unapoota ndoto hii moja kwa moja ujue  kuwa utukufu wa Mungu umeondoka juu yako, au upo mbioni kuondoka  kabisa juu yako kama hutataka kutubu dhambi zako, Na ndio maana Mungu anakuonyesha kwa jinsi hiyo hiyo unavyoweza kuona aibu ndivyo itakavyokuwa siku ile siri zako zote na dhambi zako zote unazofanya kwa siri zitakapowekwa wazi mbele ya malaika wake wote wa mbinguni

Warumi 2:16 katika siku ile Mungu atakapozihukumu siri za wanadamu, sawasawa na injili yangu, kwa Kristo Yesu.

Danieli 12:2 “Tena, wengi wa hao walalao katika mavumbi ya nchi wataamka, wengine wapate uzima wa milele, wengine aibu na kudharauliwa milele”.

Jiulize siku hiyo utakuwa katika aibu ya namna gani, utakuwa katika hali ya kudharauliwa kwa namna gani…ubaya zaidi aibu hiyo itakuwa ni ya milele..Mimi nilipokuwa katika dhambi Mungu aliniotesha hilo na haikuwa mara moja, ziliendelea kuja hivyo hivyo  mara kwa mara mpaka nilipompokea Bwana Yesu.

Vilevile ndoto hii haimuhusu aliye nje ya Kristo tu peke yake hapana hata Yule ambaye yupo ndani ya Kristo lakini bado ni vuguvugu, Kristo anamtaka na yeye ayatengeneze mambo yake sawa kabla ya siku za aibu ya milele hazijamfikia..

Ufunuo 3:14 “Na kwa malaika wa kanisa lililoko Laodikia andika; Haya ndiyo anenayo yeye aliye Amina, Shahidi aliye mwaminifu na wa kweli, mwanzo wa kuumba kwa Mungu.

15 Nayajua matendo yako, ya kuwa hu baridi wala hu moto; ingekuwa heri kama ungekuwa baridi au moto.

16 Basi, kwa sababu una uvuguvugu, wala hu baridi wala moto, nitakutapika utoke katika kinywa changu.

17 Kwa kuwa wasema, Mimi ni tajiri, nimejitajirisha, wala sina haja ya kitu; nawe hujui ya kuwa wewe u mnyonge, na mwenye mashaka, na maskini, na kipofu, NA UCHI.

18 Nakupa shauri, ununue kwangu dhahabu iliyosafishwa kwa moto, upate kuwa tajiri, NA MAVAZI MEUPE UPATE KUVAA, AIBU YA UCHI WAKO ISIONEKANE, na dawa ya macho ya kujipaka macho yako, upate kuona.

19 Wote niwapendao mimi nawakemea, na kuwarudi; basi uwe na bidii, ukatubu.

20 Tazama, nasimama mlangoni, nabisha; mtu akiisikia sauti yangu, na kuufungua mlango, nitaingia kwake, nami nitakula pamoja naye, na yeye pamoja nami.

21 Yeye ashindaye, nitampa kuketi pamoja nami katika kiti changu cha enzi, kama mimi nilivyoshinda nikaketi pamoja na Baba yangu katika kiti chake cha enzi.

22 Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo Roho ayaambia makanisa”.

Unaona? Mungu anakupenda na anahitaji siku ile uweze kuketi pamoja naye katika kiti chake cha enzi, lakini kama tu leo hii utakuwa tayari kununua kwake mavazi meupe ili aibu ya uchi wako isionekane ambayo hiyo inakuja kwa KUTUBU, yaani kuufungua tu mlango wa moyo wako aingie ndani yako..Fungua tu mlango naye ataingia, anakupenda ndio maana anakuonyesha ndoto kama hizo.

Ubarikiwe.

Group la whatsappJiunge na Group letu ya whatsapp, la masomo ya kila siku kwa kubofya hapa > Group-whatsapp


 

 

Mada Nyinginezo:

KUOTA UNAFANYA MTIHANI.

KUOTA NYOKA.

KUOTA UNASAFIRI.

MTETEZI WAKO NI NANI?

FUATILIA NDOTO HII, UTAJIFUZA KITU.

TOFAUTI KATI YA NDOTO NA MAONO NI IPI?


Rudi Nyumbani:

Print this post

JE NI LAZIMA MKRISTO AOE/AOLEWE?

Shalom karibu tujifunze biblia.

Mojawapo wa uhuru Mungu aliompa mwanadamu ni kuoa/kuolewa…Mtu yeyote anayeoa/kuolewa sawasawa na maagizo ya Mungu (yaani ndoa ya mume mmoja na mke mmoja) basi anabarikiwa.

Mathayo 19:4 “Akajibu, akawaambia, Hamkusoma ya kwamba yeye aliyewaumba mwanzo, aliwaumba mtu mume na mtu mke,

5 akasema, Kwa sababu hiyo, mtu atamwacha babaye na mamaye, ataambatana na mkewe; na hao wawili watakuwa mwili mmoja?”.

Lakini Pamoja na hayo sio lazima pia kuoa au kuolewa kwa sababu maalumu.

Kwamfano biblia inasema katika..

1Wakorintho 7:32 “Lakini nataka msiwe na masumbufu. YEYE ASIYEOA hujishughulisha na mambo ya Bwana, ampendezeje Bwana;

33 bali yeye aliyeoa hujishughulisha na mambo ya dunia hii, jinsi atakavyompendeza mkewe.

34 Tena iko tofauti hii kati ya mke na mwanamwali. YEYE ASIYEOLEWA HUJISHUGHULISHA NA MAMBO YA BWANA, APATE KUWA MTAKATIFU MWILI NA ROHO. Lakini yeye aliyeolewa hujishughulisha na mambo ya dunia hii, jinsi atakavyompendeza mumewe”.

Hivyo sababu kuu ya mtu kujizuia kuoa au kuolewa ni ili apate nafasi kubwa ya kujishughulisha na kazi ya Mungu.. Ni kweli Mume au Mke ni msaidizi mzuri pia katika kazi ya Mungu lakini…kuwa kumtumikia Mungu binafsi pia ni vizuri Zaidi.. Kwasababu ukiwa na mke/mume kuna mambo ya kidunia ambayo hautayakwepa…kwamfano vitakuwepo vipindi vya kutunza Watoto, vitakuwepo vipindi vya kutafuta sana vya kidunia ili kuitunza familia na mke au mume. Vitakuwepo vipindi vya kukaa pamoja faragha!..

Huwezi kusema unasafiri miezi 5 mbali na mke/mume wako umeenda kufanya huduma…ni lazima kwa sehemu Fulani utamkwaza tu mwenzako! au utakuwa hujamtendea haki. Na biblia inasema ukishaoa/ukishaolewa..mwili wako ni mali ya mwenzako, huna amri juu ya mwili wako(kasome 1Wakorintho 7:3-5)..Sasa hayo ndio baadhi ya mapungufu katika kuoa/kuolewa.

Lakini usipooa au usipoolewa…utakuwa huru Zaidi..unaweza kufunga safari muda wowote unaotaka kuifanya kazi ya Mungu, unaweza kufunga siku nyingi bila usumbufu, unaweza kwenda kusali mlimani kipindi kirefu au kuhubiri bila kukumbuka una jukumu Fulani umeliacha nyumbani …kadhalika, hutapata usumbufu wa Watoto wanahitaji hiki, wanahitaji kile.. kadhalika hutaishi kwa matakwa ya mtu Fulani, bali kwa kile Mungu anachokuongoza kila mara. Jambo ambalo lina faida katika ufalme wa mbinguni mara dufu kuliko hilo lingine.

Wa kwanza kabisa ambaye tunaona hakuoa na huduma yake iliikuwa na matokeo makubwa sana ni Bwana wetu Yesu. Mwingine ni Paulo ambaye ndiye aliyeandika mistari hiyo hapo juu kwa uwezo wa roho..Paulo hakuwa miongoni mwa Mitume 12 wa Bwana Yesu, lakini alifanya kazi kubwa kuliko hata mitume wa Yesu (kasome1Wakorintho 15:10), na wengine ni Yohana Mbatizaji na Eliya Mtishbi.

Lakini hilo sio lazima na wala sio amri, kwamba kila mtu ni lazima asiolewe/asioe. Ni jinsi mtu aonavyo yeye kwamba anaweza kujizuia au la!…Wapo wanaoweza kujizuia na wapo wasioweza!…Biblia inasema kama huwezi kujizuia ni afadhali uoe/uolewe kuliko kuwakwa na tamaa.

1Wakorintho 7:8 “Lakini nawaambia wale WASIOOA BADO, na wajane, Ni heri wakae kama mimi nilivyo. LAKINI IKIWA HAWAWEZI KUJIZUIA, NA WAOE; maana ni afadhali kuoa kuliko kuwaka tamaa”……

 

1Wakorintho 7:1 “Basi kwa habari ya mambo yale mliyoandika, ni heri mwanamume asimguse mwanamke. 2 Lakini kwa sababu ya zinaa kila mwanamume na awe na mke wake mwenyewe, na kila mwanamke na awe na mume wake mwenyewe”.

Bwana akubariki.

Kumbuka kama unaishi na mwanamke/mwanaume ambaye hamjafunga ndoa..basi mnaishi katika uzinzi!..haijalishi mmeishi miaka mingapi Pamoja, au mmezaa Watoto wangapi..Mnapaswa mkatubu na kufunga ndoa takatifu, mbele ya kanisa la Kristo, ndipo mbarikiwe (na ndoa sio sherehe na matarumbeta)..mmeshaishi miaka yote hiyo, sherehe ya nini tena?..hatua mliyopo ni ya kutubu tu, na kwenda mbele ya kanisa kufungishwa ndoa mbele ya mashahidi na kurudi nyumbani kuendelea na maisha basi haihitaji maandalizi kana kwamba ndio mmketana kwa mara ya kwanza!. Lakini msipofanya hivyo mkifa leo mtahukumiwa, hiyo ni kulingana na maandiko.

Na mwisho kama hujaolewa na unatafuta wa kukuoa..Ni vizuri ukamtafuta kwanza Mwokozi. Kwasababu ukifa leo bila mwokozi utapotea milele, na Zaidi ya yote mbinguni hakuna kuoa wala kuolewa, hayo mambo yataishia humu humu duniani..miili tutakayopewa tukifika kule haina hisia za kimwili. Huko tutaishi na Kristo milele. Hivyo Wokovu ni muhimu na wa kwanza katika Maisha, hayo mengine ndio yafuate.

Maran atha!

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312

Mada Nyinginezo:

Bwana alimaanisha nini kusema JIKANE mwenyewe?(Mathayo 6:24)

 MAVUNO NI MENGI

MAMBO YA KUJIFUNZA KATIKA WARAKA WA TATU WA YOHANA.

MJUMBE ASIYEKUWA NA UJUMBE.

KUOTA UNASAFIRI.

USIPOKUWA MWAMINIFU, NAFASI YAKO ITACHUKULIWA.

UNYAKUO.

Rudi Nyumbani:

Print this post