Title namna ya kuomba

Fahamu Namna ya Kuomba.

Wengi wa wanaompa Yesu Kristo maisha yao kwa mara ya kwanza, ndio maswali ya kwanza kwanza kujiuliza…nitaombaje! namna gani ya kuomba ili Mungu anisikie!

Kiuhalisia hakuna fomula fulani maalumu ya kuomba wala chuo fulani maalumu cha kujifunzia kuomba, Kwasababu Mungu wetu si mwanadamu wala hana udhaifu wa kutuelewa…Sehemu nyingine katika maandiko inasema “Baba yetu wa mbinguni anajua tujayohitaji hata kabla sisi hatujamwomba”

Unaona? kwa sentensi tu hiyo inaonesha kuwa Mungu si dhaifu wa kutuelewa sisi, kiasi kwamba tunahitaji course fulani tukasome ndipo atuelewe au kutusikia. Kitendo cha Kuwa mwanadamu tu! tayari Mungu anakuelewa kuliko unavyojielewa.

Hivyo mbele za Mungu, hatuendi na mpangilio mzuri wa Maneno kama tunavyoandaa hotuba kwenda kuisoma mbele za Mkuu wa Nchi…Isipokuwa tunakwenda na hoja zenye nguvu...Na hoja hizo ndio zile Bwana alizotufundisha wakati wa kuomba..katika Mathayo 6

“9 Basi ninyi salini hivi; Baba yetu uliye mbinguni, Jina lako litukuzwe, Ufalme wako uje,

10 Mapenzi yako yatimizwe, hapa duniani kama huko mbinguni.

11 Utupe leo riziki yetu.

12 Utusamehe deni zetu, kama sisi nasi tuwasamehevyo wadeni wetu.

13 Na usitutie majaribuni, lakini utuokoe na yule mwovu. [Kwa kuwa ufalme ni wako, na nguvu, na utukufu, hata milele. Amina”.

Kwamba tuombapo tuhakikishe tunaomba toba, na pia tuhakikishe nawasamehe wengine ili na sisi pia tusamehewe…Kadhalika tunapoomba tuhakikishe tunalitukuza jina la Yesu, na pia tunaomba ufalme wake uje…Na pia tusisahau kusema mapenzi yake yatimizwe…kwasababu sio kila kitu tunachokiomba ni mapenzi ya Mungu…Pia tunapaswa tumwombe Mungu atupe riziki zetu za kila siku, kama chakula, mavazi, malazi pamoja na fursa.

Kadhalika tunamwomba asitutie majaribuni hiyo inahusisha kumwomba Bwana atuepushe na yule mwovu katika maisha yetu, imani yetu, familia zetu, kazi zetu, huduma zetu za kila siku za kuwaleta watu kwa Kristo, tunazungukwa na nguvu za yule adui kila mahali, hivyo ni muhimu kumwomba Bwana atuepushe na mitego yake yote.

Na bila kusahau kurudisha utukufu, na kutambua kuwa uweza, nguvu na mamlaka vina yeye milele na milele…Hivyo hakuna kama yeye, na yeye ndiye mwanzo na mwisho.

Hizo ndio hoja zenye nguvu…usitazame ni maneno kiasi gani umekosea kuongea, wala ni lugha gani umezungumza wakati wa kuomba, hakikisha tu maombi yako yanahusisha hivyo vipengele.

Kwa mawasiliano/mafundisho zaidi kwa njia ya whatsapp, tutumie ujumbe kwenye
namba hizi: +255789001312/ +255693036618


Mada Nyinginezo:

FAIDA ZA MAOMBI YA USIKU

FAIDA ZA MAOMBI.

SALA YA BWANA. (Namna ya kuiomba)

TUMEAMBIWA TUNAPOSALI TUSIPAYUKE-PAYUKE, JE! HUKO KUPAYUKA PAYAUKA NDIO KUPI?

NI KWA NAMNA GANI SHETANI ANAIZUIA INJILI?

KUTUBU SIO KUOMBA REHEMA.

Ni kwa namna gani malaika wa mbinguni wanaweza kutuhubiria sisi injili?


Rudi Nyumbani:

Print this post

Maandiko yanasema Eliya aliomba kwa bidii hadi akasimamisha mvua kunyesha kwa MUDA wa miaka 3 na nusu.(Yakobo5:17) Je! kuomba kwa bidii ni kuomba kwa namna gani?

JIBU: Tusome:

Yakobo 5:17 “Eliya alikuwa mwanadamu mwenye tabia moja na sisi, akaomba kwa bidii mvua isinyeshe, na mvua haikunyesha juu ya nchi muda wa miaka mitatu na miezi sita.

18 Akaomba tena, mbingu zikatoa mvua, nayo nchi ikazaa matunda yake.” 

Kwakuwa habari hii inamzungumzia Eliya hivyo ili kuelewa vizuri hiyo bidii aliyokuwa nayo ni vizuri tukarejea kwenye tukio halisi lenyewe ili tuone ni jinsi gani aliomba. Sasa ukiangalia vizuri utaona biblia haijatoa maelezo mengi juu ya maombi aliyoyaomba siku ile alipozuia mvua. Inaonyesha tu Eliya akitokea kwenye tukio na kuzungumza maneno yale na kuondoka,

 1Wafalme 17:1 “Basi Eliya Mtishbi, wa wageni wa Gileadi, akamwambia Ahabu, Kama Bwana, Mungu wa Israeli, aishivyo, ambaye ninasimama mbele zake, hakutakuwa na umande wala mvua miaka hii, ila kwa neno langu.

2 Neno la Bwana likamjia, kusema,

3 Ondoka hapa, geuka, uende upande wa mashariki, ujifiche karibu na kijito cha Kerithi kinachokabili Yordani.

 Lakini siku ile anarudi, ili kuifungua tena mbingu kwa Neno la Mungu, tunaona halikuwa ni jambo la kutamka na kuondoka tu kuna vitu viliendelea pale embu Tusome:

1Wafalme 18:41 “Naye Eliya akamwambia Ahabu, Haya! Inuka, ule, unywe; kwani pana sauti ya mvua tele.

42 Basi Ahabu akainuka ili ale na kunywa. Naye Eliya akapanda juu mpaka kilele cha Karmeli; akasujudu kifudifudi, akainama uso mpaka magotini.

43 Akamwambia mtumishi wake, Kwea sasa, utazame upande wa bahari. Akakwea, akatazama, na kusema, Hakuna kitu. Naye akanena, Enenda tena mara saba.

44 Ikawa mara ya saba akasema, Tazama, wingu linatoka katika bahari, nalo ni dogo kama mkono wa mtu. Akanena, Enenda, umwambie Ahabu, Tandika, ushuke, mvua isikuzuie.

45 Ikawa, muda si muda, mbingu zikawa nyeusi kwa mawingu na upepo, ikanyesha mvua nyingi. Ahabu akapanda garini, akaenda zake Yezreeli.” 

Hapo unaweza ukajifunza mambo kadhaa, cha kwanza Eliya kabla hata hajamwomba Mungu, alishaamini kuwa mvua inakwenda kunyesha siku hiyo katika nchi, na ndio maana alikuwa na ujasiri wa kumwambia Mfalme Ahabu inuka unywe kwani pana sauti ya mvua tele.

Pili alipoonenda magotini sasa ili kumwomba Mungu jibu lake halikuja ndani ya wakati alioutazamia pengine aliomba lisaa la kwanza, akitazamia kabla hata hajamaliza juu kutakuwa kumeshafunga, lakini Yule mtumishi wake alipoenda alirudisha repoti kuwa juu hakuna dalili yoyote ya mvua kunyesha, lakini aliendelea kukaa uweponi mwa Bwana akimshukuru kwa matendo yake makuu, lisaa lingine likapita akamwambia mtumishi wake haya nenda katazame tena, akarudi akasema hakuna kitu, ikaendelea hivyo hivyo lisaa la tatu, la nne, mpaka lisaa la 7 pengine, akamwambia nenda katazame usichoke, ndipo Yule mtumishi wake akarudi akasema ninaona kawingu kadogo kama cha mkono wa mtoto mchanga, Ndipo Eliya alipoacha kuomba akijua kuwa tayari imekwisha kuwa..

Na kama ingetokea hakuna kitu chochote kilichotokea ni wazi kuwa angeendelea hivyo hivyo hata mara 20 au 50, au 100 kwa nguvu ile ile akijua kuwa Mungu ameshamsikia..Huko ndiko kuomba kwa BIDII ambapo hata sisi tunapashwa tuwe nako, Ni rahisi kumwamini Mungu tunapompelekea mahitaji yetu lakini kudumu uweponi Mwake hatuwezi pale tunapoona majibu yanachelewa kidogo, hayajaja ndani ya wakati tuliotuzamia..Tunaanza kumtilia Mungu mashaka pengine hajatusikia. Lakini tukiendelea kushikilia na kumwamini Mungu kuwa ameshatenda, hata kama itapita siku, wiki, mwezi, miaka, ukizidi kushikilia nakwambia milango yote itafunguka mbele yetu. Hivyo kwa ufupi kuomba kwa bidii kunakozungumziwa hapo ni Kukaza kumwamini Mungu mpaka majibu yanapotokea. 

Ubarikiwe sana.


Mada Nyinginezo:

ROHO YA ELIYA KATIKA AGANO JIPYA INATENDAJE KAZI?

UFUNUO: MLANGO WA 11

KUNA TOFAUTI GANI KATI YA SALA NA DUA?

NJIA SAHIHI YA KUFUNGA.

“WOKOVU WETU U KARIBU NASI KULIKO TULIPOANZA KUAMINI”

VITA DHIDI YA MAADUI

TUMEPEWA, SI KUMWAMINI TU KRISTO, ILA NA KUTESWA KWA AJILI YAKE;


Rudi Nyumbani:

Print this post

Je! Petro na wenzie walitambuaje kuwa wale walikuwa ni Musa na Eliya?

Swali: Katika kitabu cha Mathayo 17:4 Mtume Petro na wenzie waliwezaje kufahamu kuwa wale ni Musa na Eliya?


Jibu: Turejee habari hiyo kuanzia ule mstari wa kwanza..

Mathayo 17:1 “Na baada ya siku sita Yesu akawatwaa Petro, na Yakobo, na Yohana nduguye, akawaleta juu ya mlima mrefu faraghani;

2 akageuka sura yake mbele yao; uso wake ukang’aa kama jua, mavazi yake yakawa meupe kama nuru.

3 Na tazama, wakatokewa na Musa na Eliya, wakizungumza naye.

4 Petro akajibu akamwambia Yesu, Bwana, ni vizuri sisi kuwapo hapa; ukitaka, nitafanya hapa vibanda vitatu, kimoja chako wewe, na kimoja cha Musa, na kimoja cha Eliya”.

Biblia haijaeleza kama Musa na Eliya walijitambulisha katika maono yale, ikiwa na maana kuwa kuna njia nyingine iliyowafanya Petro na wenzie kujua kuwa wale ni manabii Musa na Eliya na si wengine.

Sasa njia Pekee iliyomfanya Petro na wenzie kufahamu kuwa wale walikuwa ni Musa na Eliya na si wengine, ni UFUNUO WA ROHO MTAKATIFU.

Kama vile ufunuo wa Roho Mtakatifu ulivyomjia Petro kumhusu YESU.

Mathayo 16.15 “Akawaambia, Nanyi mwaninena mimi kuwa ni nani?

16 Simoni Petro akajibu akasema, Wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai.

17 Yesu akajibu, akamwambia, Heri wewe Simoni Bar-yona; kwa kuwa mwili na damu havikukufunulia hili, bali Baba yangu aliye mbinguni”.

Umeona hapo?, aliyemwambia Petro kuwa YESU ni KRISTO tena ni MWANA WA MUNGU aliye juu sio YESU mwenyewe!, bali ni ufunuo wa alioupokea kutoka kwa Baba.

Na hiyo sio ajabu kwani walikuwa wameenda mlimani kuomba.. ni kawaida kwa watumishi wa MUNGU kupokea mafunuo ya mambo yaliyopo, au yajayo wanapokuwa katika maombi, hususani kama hayo ya mlimani.

Kwahiyo Mtume Petro na wenzie walipata ufunuo wa ujio au uwepo wa manabii hao wawili wakiwa katika maombi, utaona jambo kama hilo lilishatokea tena kwa Petro wakati yupo kwa Yule Simoni mtengenezaji wa ngozi wa kule Yafa, wakati ambapo Roho Mtakatifu alimfunulia alipokuwa katika maombi kuwa kuna watu watatu wanamwulizia, hivyo aende nao asiogope!, na kweli ikawa hivyo..

Matendo 10:17 “Hata Petro alipokuwa akiona shaka ndani ya nafsi yake, maana yake ni nini maono hayo aliyoyaona, wale watu waliotumwa na Kornelio, wakiisha kuiulizia nyumba ya Simoni, wakasimama mbele ya mlango,

18 wakaita; wakauliza kwamba Simoni aitwaye Petro anakaa humo.

19 Na Petro alikuwa akiyafikiri yale maono. Roho akamwambia, Wako watu watatu wanakutafuta.

20 Basi ondoka ushuke ufuatane nao, usione tashwishi, kwa maana ni mimi niliyewatuma.

21 Petro akawashukia wale watu, akanena, Mimi ndiye mnayemtafuta. Mmekuja kwa sababu gani?”

Kwa namna hiyo hiyo, huenda Petro na wenzake walipokea ufunuo kuwa wale ni Musa na Eliya, labda walipokea ufunuo huo muda mchache kabla hawajawatokea, au wakati ule ule walipotokea.

Kikubwa tunachoweza kujifunza ni kuwa tuwapo katika uwepo wa MUNGU kama katika maombi, ni rahisi kupokea ufunuo wa Roho Mtakatifu kwani tunakuwa tupo katika roho, na mtu anapokuwa katika roho anayatambua mambo yote ya rohoni pasipo kuambiwa!

Hivyo ni muhimu sana kuwa waombaji, na wasomaji wa Neno la MUNGU, endapo akina Petro wangekuwa si watu wa kusoma maandiko, ni dhahiri kuwa wasingemjua Musa wala Eliya na hiyo ingezuia Roho kuwafunulia watu hao, kwani Roho Mtakatifu anamfunulia mtu kitu ambacho kinahusiana na Neno la MUNGU.

Je na wewe ni mtu wa kudumu uweponi mwa MUNGU? Je KRISTO YESU?..Je unao uhakika kwamba akirudi unaenda naye?

Maran atha!

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

Kwanini Eliya afunge Mbingu miaka mitatu na nusu? (1Wafalme 17:1)

TUKIO LA MUSA NA ELIYA KUMTOKEA BWANA, LIMEBEBA UJUMBE GANI?

Je! Tutatambuana tukifika mbinguni?

Je Mariamu alikuwa na umri gani alipochukua mimba ya Bwana YESU?

Kwanini Mungu alimchagua Musa, na si mtu mwingine?

Print this post

OMBA JAMBO KATIKA MAJIRA YAKE.

Zekaria 10:1 “Mwombeni Bwana mvua wakati wa masika, naam, Bwana afanyaye umeme, naye atawapa manyunyu ya mvua, kila mtu atapewa nyasi kondeni”.

Umewahi kujiuliza kwanini hapo maandiko yanasema “Mwombeni Bwana mvua WAKATI WA MASIKA” na si wakati mwingine wowote kama kiangazi?..

Ni kwasababu msimu wa masika ni msimu wa mvua, hivyo inapotokea hakuna mvua si jambo la kawaida, kwahiyo tukiomba mvua msimu huo ni hoja yenye nguvu, lakini tunapoomba mvua msimu wa kiangazi zinakuwa si hoja zenye nguvu!.. Ndicho maandiko yanachokimaanisha hapo.

Maombi ya kuomba kwa wakati ni mazuri na yana majibu ya haraka kuliko yale ya kuomba nje ya msimu/majira.

Unaomba mume/mke  na bado ni mwanafunzi, unaomba mali na bado unasoma, unaomba umtimikie MUNGU na bado hujaokoka!, maombi ya namna hiyo ni nadra sana kujibiwa!.. ni wachache sana wanaojibiwa hayo maombi!!.. sio kwamba ni maombi mabaya au vinavyoombwa ni vitu vibaya!. La! Ni vizuri lakini vinaombwa nje ya majira yake.

Hapo maandiko yanasema “Mwombeni Bwana Mvua wakati wa Masika”..  Maana yake ni lazima ujue uhusiano wa kile unachomwomba MUNGU na majira uliyopo. Kama kitu bado majira yake usitumie nguvu kubwa kuomba, shughulika na vile ambavyo sasa ndio majira yake.

Kama wewe ni mwanafunzi usiombe MUNGU akupe hela kwa sasa….badala yake mwombe akufanikishe katika masomo ufaulu, uwe kichwa, hayo mengine bado msimu wake!..

Kama wewe ni binti/kijana na bado upo chini ya wazazi unawategemea, usiombe MUNGU akuonyeshe mume wako/mke wako, badala yake mwombe ulinzi juu ya tabia yako mpaka utakapofika wakati wa wewe kujitegemea na kufikiri kuingia katika ndoa.

Lakini kama umeshaingia katika msimu basi ni haki yako kumwomba BWANA!, Na unapomwomba Bwana jambo sahihi katika msimu sahihi, MUNGU ni mwenye huruma atakupa unachokihitaji haraka sana, na hata kikichelewa atakupa sababu kwanini kinachelewa, na sababu za BWANA zote ni Bora na wala si za kumwumiza Mtu, kwasababu yeye kamwe hawezi kuruhusu tujaribiwe kupita tuwezavyo.

Vumilia tu ukiona umeshaingia kwenye msimu na bado matokeo hujayaona!, yatakuja tu!..usikate tama a wala kuishiwa nguvu, mwamini MUNGU na mngojee, naye atakupa nguvu mpya kila siku.

Jambo la mwisho la kujua ni kwamba wokovu pia unao msimu wake, na msimu wa Wokovu ndio sasa..

Huu ndio wakati wa MUNGU kutupa wokovu na kutusikia maombi yetu, kwani utafika wakati ambapo hakutakuwa tena na wokovu wala maombi kusikiwa, ndivyo maandiko yanavyosema..

2Wakorintho 6:1 “Nasi tukitenda kazi pamoja naye twawasihi msiipokee neema ya Mungu bure.

2 (Kwa maana asema, Wakati uliokubalika nalikusikia, Siku ya wokovu nalikusaidia; tazama,wakati uliokubalika ndiyo sasa; tazama siku ya wokovu ni sasa)

Sasa kama  siku ya Wokovu ndio sasa, unasubiri nini usimpokee YESU?.. je unadhani itakuwa hivi siku zote?.. utafika wakati mlango wa Neema utafungwa, na hakutakuwa tena na msamaha wa dhambi wala ondoleo la dhambi, mti ulipoangukia huko huko utalala (Mhubiri 11:3).

Sasa unayadharau mahubiri na mafundisho ya uzima, unayoyapokea kila mahali yanayokuonya kuhusu dhambi, je unadhani hali itakuwa hivyo kila siku?…Majira yatabadilika ndugu, utafika wakati kutakuwa hakuna kuponywa tena mwili na roho!.

2Nyakati 36:15 “Naye Bwana, Mungu wa baba zao, akatuma kwao kwa mikono ya wajumbe wake, akiondoka mapema, na kutuma; kwa sababu aliwahurumia watu wake, na makao yake;

16 lakini waliwadhihaki wajumbe wa Mungu, na kuyadharau maneno yake, na kuwacheka manabii wake, HATA ILIPOZIDI GHADHABU YA BWANA JUU YA WATU WAKE, HATA KUSIWE NA KUPONYA”.

Bwana atusaidie.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

Nzige, Parare, madumadu na tunutu ni wadudu gani? (Yoeli 2:25)?

MAASI KUONGEZEKA NI ISHARA YA NINI?.

JIFUNZE JAMBO KWENYE UKOO WA YESU, UWE NA AMANI

Kwanini madhabahu zilitengenezwa kwa mawe yasiyochongwa?

Kwanini Mungu auweke Mti wa Mema na Mabaya katikati ya bustani?

Print this post

IFAHAMU NGUVU YA MAOMBI (Sehemu ya pili)

Maombi ya shabaha kwaajili ya Kazi/kibarua/shughuli/biashara/elimu.


UTANGULIZI: Ni muhimu kujua hili: lengo kuu au kiini cha Wokovu ulioletwa na BWANA YESU KRISTO sio sisi tuwe matajiri au tupate mafanikio ya huu ulimwengu!.

Mafanikio ya dunia hii ni moja ya faida za mwisho mwisho kabisa za kusudi la msalaba wa Bwana YESU kwasababuwalikuwepomatajiri kabla ya Bwana YESU kuja duniani, hivyo KRISTO asingeweza kuja kutegua mtego aukutatua tatizo ambalo lilishatatuliwa huko nyuma.

Ingekuwa lengo lake ni ili tufanikiwe tuwe matajiri, angetuambia tu tusikilize hekima za Sulemani na tungefanikiwa, hakukuwa na haja ya kuja kumwaga damu yake.

Lakini suala la ondoleo la dhambi hilo halikuwahi kufanyika huko nyuma, hakuna aliyewahi kuondolewa dhambi, kwani dhambi zilikuwa zinafunikwa tu! (Soma Waebrani 10:3-4)..

Sasa hiko ambacho kilishindikana kutendeka huko nyuma (katika Agano la kale) ndicho kilichokuwa cha kwanza na cha msingi kilichomleta BWANA YESU duniani, na kitu hiko si kingine zaidi ya ONDOLEO LA DHAMBI.…kiasi kwamba mtu akikosa ondoleo la dhambi hata awe na vitu vyote ulimwenguni bado anayo hasara kubwa soma (Mathayo 16:26).

Kwahiyo ni muhimu kujua msingi huu, ili tunapokwenda kujifunza juu ya MAOMBI JUU YA KAZI au BIASHARA, Usiweke moyo wako wote huko!.. Yatumie tu maarifa haya kama sehemu ya maisha, lakini jali zaidi hatima ya roho yako, kupitia damu ya YESU na UTAKATIFU.

Sasa tukirudi katika kiini cha somo!.. Ikiwa unafanya kazi za mikono, labda tuseme biashara, tumia kanuni hii ya Maombi kupata FAIDA YA KILE UNACHOKIFANYA!!.

Badala ya kuombea bidhaa zako, kama sabuni unazouza, au dawa unazouza, au kingine chochote kwamba kiwe na mvuto, kuanzia leo punguza kuomba maombi ya namna hiyo, badala yake omba maombi yafuatayo.

– Kila mteja anayekuja kwako mwombe neema ya Wokovu, ikiwa bado hajampokea YESU, maombi ya namna hiyo yanamtoa yule mtu kutoka katika vifungo vya ibilisi na hatimaye kumfungua kabisa, na anapofunguliwa aweza kuwa mteja wako wa ajabu sana, au akawaleta na wengine wengi mahali ulipo.

– Ikiwa tayari ameshampokea YESU mwombee azidi kusimama katika imani, na mwombee akawe Nuru kwa wengine wengi, ombea na familia yake kama unaijua, hiyo ndio njia bora ya kuombea kazi yako au biashara yako..

– Unafanya biashara ya chakula, na wateja wako ni watu wa kidunia, badala ya kuombea madishi na chakula unachokipika kwamba wakipende, hebu waombee wampende YESU, halafu uone kama hiko chakula chako hawatakipenda, zaidi ya vyakula vya wengine wote.

– Pale ofisini acha kuombea uso wako kwamba upate kibali, sawa waweza kuomba hivyo, lakini isizidi sana kiasi kwamba hujui kitu kingine cha kuomba zaidi ya hicho, badala yake anza kuomba watu wa ofisini kwako wamjue MUNGU, wakimjua MUNGU wewe utapata kibali tu!, wala hutatumia nguvu nyingi.

– Pale shuleni acha kuombea walimu wakupende, hebu waombee wamjue YESU na kumpenda, halafu uone kama hawatakupenda na wewe.

– Unauza bidhaa, waombee wateja wako wamjue YESU na kumpenda zaidi ya bidhaa zako, halafu uone matokeo.

Ukitaka kufunga kwaajili ya biashara yako!, Funga kwa maombi ya kuwaombea wateja wako wokovu na Neema zaidi, kama unayo list, anza mmoja baada ya mwingine, wapatanishe na KRISTO hivyo uone kama KRISTO pia hatakupatanisha nao, utaona kazi zako zinaenda, shule yako inaenda, biashara yako inaenda, kazi yako inaenda.

Lakini ukijikita tu kuziombea bidhaa kama vile waganga wanavyotoa dawa za kwaajili ya biashara, matokeo yake yatakuwa ni madogo sana.

Hivyo OMBA lakini omba kwa shabaha/target.

Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

IFAHAMU NGUVU YA MAOMBI:

MWONGOZO WA MAOMBI YA FAMILIA

KWANINI MUNGU HAJIBU MAOMBI?

Mistari ya biblia kuhusu maombi.

MWONGOZO WA MAOMBI YA WAHUDUMU/ WASIMAMAO MADHABAHUNI.

Print this post

IFAHAMU NGUVU YA MAOMBI.

Sehemu ya kwanza.

Zaburi 66:20 “Na ahimidiwe Mungu asiyeyakataa maombi yangu, Wala kuniondolea fadhili zake”.

Maombi ni zaidi ya silaha yoyote ile yenye ubora inayofahamika, leo nataka tujifunze kupitia mfano mdogo sana wa simu ya mkononi.

Kawaida ili uweze kuongeza uwezo wa simu yako, huna budi kujiunganisha na internet..

Internet ni mtandao usiookana kwa macho, unaoratibu mawasiliano ya haraka na taarifa za haraka.

Sasa simu yako inapoungwa na internet ndipo unapoweza kupakua (kudownload) vichocheo vya simu vinavyoitwa application.

Applications zile zinasaidia kuongeza uwezo wa simu yako..

Kama unataka simu yako iweze kusoma baadhi ya makala unahitaji kichocheo husika cha kusomea makala hizo.

Vile vile kama unahitaji simu yako iwe na uwezo wa kucheza nyimbo kwa mpangilio, itakugharimu kupakua (download) vichocheo hivyo n.k

Simu zenye vichocheo (applications) nyingi mbalimbali ndizo zenye uwezo mkubwa..na zile zisizo na vichocheo kabisa huwa zina uwezo mdogo na changamoto nyingi.

Sasa na mwili wa Mtu ni hivyo hivyo, kuna mambo hatuwezi kufanya wala kuwa nayo pasipo hivi vichocheo vinavyoongeza uwezo.

Kwamfano huwezi kusoma biblia na kuielewa kama hujaongezewa nguvu.. Utakuwa ukishika tu unalala!.

Huwezi kuhubiri kama hujaongezewa nguvu, utakuwa unaona aibu tu!.

Huwezi kuishi maisha masafi kama hujaongezewa nguvu utajaribu lakini utashindwa…n.k.

Sasa kazi ya Roho Mtakatifu ni kutuunganisha sisi na mtandao wa kimbinguni, kama vile simu inavyoungwa na internet.

Na tunapoungwa na mtandao wa kimbinguni basi tunaweza kupakua (download) vichocheo vya kimbinguni..

Na tunavipakua vichocheo hivyo kwa njia moja tu ya MAOMBI!.

Unapoomba maana yake unapakua (download) visaidizi vya kimbunguni, ambavyo vinakuongezea nguvu katika utu wa ndani.

KUMBUKA: Maombi hayakupi kitu! Balia YANAKUONGEZEA NGUVU YA KUFANYA NA KUPATA KITU.

Ndio maana baada ya maombi utaona ile nguvu ya kusoma Neno inaongezeka, ile nguvu ya kuhubiri inaongezeka, ile nguvu ya kushinda dhambi inaongezeka, ile nguvu ya kuendelea na wokovu inaongezeka..

Utaona ile nguvu ya kuendeleza maono yako inaongezeka,..ukiona hivyo jua ni vichochezi vya kimbinguni vimeingia ndani yako vinafanya kazi..HIYO NDIO NGUVU YA MAOMBI!!.

Na kawaida hata vichochezi vya simu (application) vinakuwa updated mara kwa mara, vivyo hivyo na mwombaji huwa haombi mara moja na kuacha, bali anakuwa na desturi ya kuomba mara kwa mara ili kuimarisha vichochezi vyake.

Lakini usipokuwa mwombaji, utabaki, hutaona mabadiliko yoyote katika eneo lolota la kiroho na kimwili…kila kitu kitakuwa kigumu hakiendi..

Na kama ulikuwa mwombaji na ukapunguza kuomba, na vile vichocheo pia vinapungua nguvu.

Anza kuwa mwombaji, kuna mambo hayawezekaniki pasipo maombi hususani yale ya mfungo.

Mathayo 17:21 “Lakini namna hii haitoki ila kwa kusali na kufunga”.

Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

Print this post

Biblia inaposema sisi ni ukuhani wa kifalme, maana  yake nini?

1Petro 2:9 Bali ninyi ni mzao mteule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, watu wa milki ya Mungu, mpate kuzitangaza fadhili zake yeye aliyewaita mtoke gizani mkaingie katika nuru yake ya ajabu;


JIBU: Katika vifungu hivyo biblia inaeleza kwa ukubwa sifa zetu sisi tuliomwamini Yesu Kristo, jinsi zilivyo kuu, anasema sisi ni mzao mteule, na pia watu wa milki ya Mungu. Lakini sifa nyingine ndio hiyo ya ukuhani wa kifalme.

Angeweza kusema sisi ni  ukuhani wa kisomi, au ukuhani wa kiroho, au ukuhani ki-mbingu, au ukuhani wa kitajiri. Lakini anatumia Neno ukuhani wa kifalme. Ikiwa na maana kuwa tunao ukuhani lakini si ukuhani tu bali wenye asili ya kifalme.

Sifa kuu ya kuhani, ni kuweza kumkaribia Mungu kusema naye, na kufanya upatanisho kwa ajili ya watu wengi. Mfano wa Haruni na uzao wake. Tunaona hawa tu ndio waliopewa neema ya kuweza kumkaribia Mungu katika kiti chake che rehema, kuzungumza naye na kuomba rehemu kwa taifa zima. Wengine wote walikaa nje ya hema.

Lakini pia sifa ya mfalme ni uweza, mamlaka, nguvu, na utajiri.  Mfalme anatawala, mfalme ana nguvu ya kijeshi, mfalme ni lazima awe tajiri na mwenye utiisho.

Sasa tukirudi kibiblia, Haruni na walawi wote ambao waliopewa sifa ya kikuhani, hawakuwa na ukuhani wa kifalme ndani yao. Waliishia tu kukaa hemani, na sio ni makuhani na wakati huo huo ni wafalme, lakini pia wafalme wengi (Mfano wa Daudi, Sulemani n.k.)hawakuwa na ukuhani pia ndani yao.. Hivyo waliishia tu kutawala lakini sio kuingia hekaluni kuvukiza uvumba. Alitokea mfalme mmoja kujaribu kufanya kazi hizo mbili kwa wakati mmoja, aliishia kupata ukoma kwasababu hakukuwahi kutokea mtu mwenye uwezo huo wa kutembea katika vyeo vyote viwili kwa wakati mmoja (2Nyakati 26:16-21).

Lakini yupo aliyetabiriwa na manabii kuwa atakuwa kuhani mkuu lakini pia mfalme. Na huyo si mwingine zaidi ya Bwana wetu Yesu Kristo. (Waebrania 7:11-17), Yeye alikuwa kuhani lakini pia alitokea katika kabila la kifalme la Yuda, kwa jinsi ya mwili.

Na mpaka sasa anatawala kama kuhani mkuu wetu, lakini pia mfalme wetu. Amewazidi makuhani wote, amewazidi wafalme wote.

Hivyo na sisi tuliozaliwa na yeye, tunarithi vyote alivyonavyo, maandiko yanasema hivyo (1Petro 1:3-4), Tunafanyika sio tu makuhani, ambao tunamkaribia Mungu kusema naye ana kwa ana, na kuwapatanisha wengine na yeye, lakini pia  tunafanyika wafalme wenye mamlaka yote, na nguvu, na utajiri.

Sisi tumepewa mamlaka ya kukanyaga nge na nyoka, na nguvu zote za Yule mwovu, mamlaka ya kupooza kila aina ya magonjwa na madhaifu, mamlaka ya kufungua na kufunga jambo lolote. Vilevile tumepewa na utajiri wote wa hekima na maarifa ndani ya Yesu Kristo (Waefeso 1:3).

Na zaidi mamlaka ya ufalme tuliyonayo itakuja kudhihirika vema mbeleni kwenye utawala wa miaka 1000 wa amani wa Yesu Kristo duniani. Jinsi tutakavyo milika na kutawala na yeye kama wafalme, na yeye akiwa kama mfalme wa wafalme. (Ufunuo 19:16)

Ufunuo 5:10 ukawafanya kuwa ufalme na makuhani kwa Mungu wetu; nao wanamiliki juu ya nchi.

Je!, umeipokea neema hii?

Ni nini unachosubiri usimpe Kristo maisha yako? Tafakari ahadi kubwa namna hii unapewa bure, ni nani anayeweza kufanya hivyo? Saa ya wokovu ni sasa, na wakati uliokubaliwa na Mungu ndio huu, okoka leo, usamehewe dhambi zako, jina lako liandikwe katika kitabu cha uzima.

ikiwa upo tayari kumpokea Yesu, basi fungua hapa kwa mwongozo wa sala ya Toba >>>> KUONGOZWA SALA YA TOBA

Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

Nini maana ya “Uweza wa kifalme utakuwa begani mwake” (Isaya 9:6)?.

HERI YULE ATAKAYEKULA MKATE KATIKA UFALME WA MUNGU.

Ulimwengu wa Roho ni nini? Na mtu anawezaje kuwa wa rohoni?

Print this post

Msingi wa imani ya kikristo ni upi?

Msingi ni chimbuko, au mwanzo au kiini cha kitu fulani.

Ni wazi kuwa kila jambo lina msingi wake. taifa lina msingi wake, taasisi ina msingi wake, kabila lina msingi wake vilevile pia imani ina msingi wake.

Hivyo tukirudi katika ukristo. Msingi wa imani yake ni upi?

Msingi wa ukristo ni YESU KRISTO mwenyewe, na kazi yake aliyoikamilisha ya kufa na kufufuka kwake. Na sio kanisa, au dhehebu, au mapokeo fulani, au kikundi fulani cha wanaharakati.

Pasipo Yesu hakuna ukristo.

Yeye anafananishwa na lile jiwe kuu la pembeni, ambalo hakuna mjenzi aliyeweza kusimamisha jengo bila kuliweka hilo.

1 Petro 2:6

[6]Kwa kuwa imeandikwa katika maandiko Tazama, naweka katika Sayuni jiwe kuu la pembeni, teule, lenye heshima, Na kila amwaminiye hatatahayarika. 

Habari kamili za Yesu, na kazi yake aliyokuja kuifanya duniani unaipata katika kitabu kimoja tu kiitwacho BIBLIA. Hivyo huwezi kutenganisha biblia na Yesu Kristo.

Ili mtu ashawishwe kuipokea imani, ni sharti, aisikie kwanza injili yake ambayo hiyo utaipata katika Neno la Mungu yaani biblia..(Warumi 10:17)

Mpaka mtu aitwe mkristo ni lazima amtambue kwanza Kristo ni nani, na nini amekileta duniani, vinginevyo hawezi kuwa mkristo, hata kama atajiunga na kanisa, au dhehebu na kuyashika mapokeo yote aliyoyakuta huko, au kuisoma biblia yote, huyo bado hajawa mkristo.

Ni muhimu sana kumtambua Yesu ni nani kwetu. Kumtambua Yesu kama mwana wa Mungu bado inaweza isikupe wokovu, hata kumtambua Yesu kama Mungu bado inaweza isikupe wokovu (ijapokuwa vyote hivyo ni vyeo vyake). Lakini vyeo hivyo sio kiini cha ukristo.

 Yesu ni nani na ni nini alikileta duniani?

Yesu ni MKOMBOZI, kama tafsiri ya jina lake linavyojieleza( Mathayo 1:21)

mkombozi wa nini?

Alikuja kutukomboa roho zetu, nafsi zetu na miili yetu, Na kama ilivyo kanuni ya kiroho ili jambo hilo liweze kukamilika ilipasa itolewe kafara isiyo na kasoro yoyote(yaani dhambi). Na aliyeweza kukidhi vigezo hivyo ni Yesu pekee.

Ndio maana ilimgharimu afe, kama fidia ili sisi tupokee ondoleo la dhambi na msamaha wa dhambi kwa kifo chake. Hivyo yoyote anayeamini(yaani anayeupokea wokovu huo aliouleta).

kwa toba ya kweli na ubatizo, Basi anakuwa ameokoka, hivyo ile ghadhabu ya Mungu kwa wenye dhambi wote haiwi tena juu yake, tangu huo wakati anaitwa mbarikiwa, au mkristo, kwasababu dhambi zake zinakuwa zimefutwa kabisa.

Na zaidi ya hayo mtu huyu moja kwa moja anapewa zawadi ya Roho Mtakatifu, ambaye tangu huo wakati na kuendelea anakuwa ndani yake kama msaidizi, kumsaidia madhaifu yake, katika kuomba, kuijua kweli, kumkumbusha aliyoyasema Yesu, kumpasha habari ya mambo yajayo, na kumtia nguvu ya kumtumikia Mungu, pamoja na kumpa nguvu ya kushinda dhambi.

Huyu ndiye mkristo.

Swali ni je! umemwamini ipasavyo? au umempokea kwa namna ile ya kidini?

Usifikiri kuhama dini, wewe ni Kristo, au kuzaliwa kwenye familia ya kikristo wewe ndio mkristo, au kusomea theolojia, hapana hizo ni kampeni tu, ukristo halisi huja kwa kumwelewa Kristo ni nani na ni nini amekifanya kwako.

Ikiwa bado hujaokoka na unataka kumpokea leo ili upate ondoleo la dhambi zako. Basi uamuzi huo ni bora sana kwako. Wasiliana nasi namba uzionazo chini  kwa mwongozo wa sala ya toba.

Ubarikiwe.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

 +255693036618/ +255789001312

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >>https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

YESU NI NANI?

UKOMA NA UJANE ULIO NDANI YAKO, UMEUPATIA TIBA?

Je huduma za mitume na manabii, zinaendelea kufanya kazi hadi sasa?

Rudi Nyumbani

Print this post

MAANA ROHO HUCHUNGUZA YOTE, HATA MAFUMBO YA MUNGU.

Wakorintho 2:10  Lakini Mungu ametufunulia sisi kwa Roho. Maana Roho huchunguza yote, hata mafumbo ya Mungu.

11  Maana ni nani katika binadamu ayajuaye mambo ya binadamu ila roho ya binadamu iliyo ndani yake? Vivyo hivyo na mambo ya Mungu hakuna ayafahamuye ila Roho wa Mungu

Sifa mojawapo ya Roho Mtakatifu, ni kuchunguza, na tunajua mpaka kitu kichunguzwe ni lazima tu kitakuwa kimesitirika, kwa lugha nyingine tunaweza kusema kipo katika mafumbo. Hivyo Roho Mtakatifu anafanya kazi ya  kuyachunguza “YOTE”. Akiwa na maana Mafumbo yote, si tu yale yaliyo chini bali pia hata yaliyo kule juu Mungu mwenyewe alipo.

Na leo tutanyambua aina hizo za mafumbo kwa upana, ili tuelewe ni kwa jinsi gani Roho Mtakatifu alivyomsaada mkubwa sana kwetu.

Mafumbo yamegawanyika katika sehemu kuu tatu (3)

  1. Mafumbo ya wanadamu
  2. Mafumbo ya shetani
  3. Mafumbo ya Mungu

Mafumbo ya Wanadamu:

Ukipokea Roho Mtakatifu,  moja kwa moja unaongezewa hekima, ya kuweza kupambanua, na kuhukumu, akili zote za kibinadamu. Wala hakuna litakalokushinda, kwamfano Bwana Yesu alipowekewa mitego mingi na wayahudi ili watafute kosa ndani yake, wapate kumshitaki, hawakuweza kumshinda kwasababu saa ile ile, alielewa vema mawazo yao kwa Roho Mtakatifu aliyekuwa ndani yake.

Kwamfano katika ile habari ya kulipa kodi walipomjaribu, walishindwa kabisa kabisa.

Mathayo 22:15  Ndipo Mafarisayo wakaenda zao, wakafanya shauri, jinsi ya kumtega kwa maneno.

16  Wakatuma kwake wanafunzi wao pamoja na Maherodi, wakasema, Mwalimu, twajua ya kuwa wewe u mtu wa kweli, na njia ya Mungu waifundisha katika kweli, wala hujali cheo cha mtu awaye yote, kwa maana hutazami sura za watu.

17  Basi utuambie, Waonaje? Ni halali kumpa Kaisari kodi, ama sivyo? 18  Lakini Yesu akaufahamu uovu wao, akasema, Mbona mnanijaribu, enyi wanafiki?

19  Nionyesheni fedha ya kodi. Nao wakamletea dinari. 20  Akawaambia, Ni ya nani sanamu hii, na anwani hii?

21  Wakamwambia, Ni ya Kaisari. Akawaambia, Basi, mlipeni Kaisari yaliyo ya Kaisari, na Mungu yaliyo ya Mungu. 22  Waliposikia, walistaajabu, wakamwacha, wakaenda zao

Wakati mwingine walimletea mwanamke aliyefumaniwa katika uzinzi, ili wamnase wakashindwa pia, kwasababu Yesu alikuwa na Roho wa Mungu ndani yake(Yohana 8:1-11). Ndio maana Yesu naye akatupa hakikisho hilo kwamba katika kuenenda kuhubiri kwetu,  tusihofu watakapotaka kutushitaki, na kutupeleka mabarazani, au mahakamani, kutuhukumu, kwani yeye mwenywe atatupa kinywa cha hekima ambacho watesi wetu hawatatuweza.

Yohana 21:12  Lakini, kabla hayo yote hayajatokea, watawakamata na kuwaudhi; watawapeleka mbele ya masinagogi, na kuwaua magerezani, mkipelekwa mbele ya wafalme na maliwali kwa ajili ya jina langu.

13  Na hayo yatakuwa ushuhuda kwenu.

14  Basi, kusudieni mioyoni mwenu, kutofikiri-fikiri kwanza mtakavyojibu;

15  kwa sababu mimi nitawapa kinywa na hekima ambayo watesi wenu wote hawataweza kushindana nayo wala kuipinga.

Lakini pia Roho achunguzaye mafumbo hutupa hekima sio tu ya kutambua lakini pia ya kufanya hukumu sahihi.

Utakumbuka kisa kile cha Sulemani na wale wanawake wawili makahaba, ambao kila mmoja alikuwa ana mng’ang’ania mtoto Yule mmoja wakisema ni wake. Lakini Sulemani alipewa hekima ya kutoa hukumu vema, kwa kuwaambia nileteeni upanga, nimgawanye, ili kila mtu achukue nusu yake. Yule ambaye mtoto si wake akasema na iwe hivyo, lakini Yule mwingine akamwonea huruma. Ndipo Sulemani akatambua kuwa mtoto ni wa Yule mama aliyemwonea huruma (1Wafalme 3:16-28)

Sasa hiyo yote ni kazi ya Roho Mtakatifu ya kuchunguza mafumbo ya wanadamu, na kutupasha habari.

Lakini pia hutumia  njia ya maono au  ndoto kutufahamisha. Mafumbo yaliyositirika mioyoni mwa watu. Mfano wa Yusufu kwa Farao, na Danieli kwa ile ndoto ya Nebukadreza, Mambo ambayo hata walioziota ndoto zenyewe hawakuzikumbuka wala kujua maana zao, lakini Roho Mtakatifu aliwafunulia.

Hivyo ndivyo Roho Mtakatifu anavyotusaidia kuchunguza mafumbo ya wanadamu.

Mafumbo ya shetani:

Si kawaida ya shetani kujidhihirisha kwa wazi kama wengi wanavyodhani, bali huja kama malaika wa nuru, hivyo kama hujajazwa Roho Mtakatifu vema kamwe huwezi yajua mafumbo yake. Ndicho walichokikosa baadhi ya watakatifu wa kanisa la Thiatira.

Ufunuo 2:24  Lakini nawaambia ninyi wengine mlioko Thiatira, wo wote wasio na mafundisho hayo, wasiozijua fumbo za Shetani, kama vile wasemavyo, Sitaweka juu yenu mzigo mwingine.

25  Ila mlicho nacho kishikeni sana, hata nitakapokuja.

Swali ni je haya Mafumbo ya shetani yanakujaje?

Yapo Manabii wa Uongo:

Manabii hawa wa uongo wamegawanyika katika makundi mawili.

Kundi la watumishi wa Mungu: Hawa ni ambao hawajasimama vema, hivyo wakati mwingine shetani hutumia vivywa vyao au mafundisho yao kupotosha wengine, bila hata ya wao kukusudia wakati mwingine. Mfano wa hawa alikuwa ni Petro, wakati ule aliposimama mbele ya Yesu na kuanza  kumkemea kwamba hatakwenda msalabani. Lakini Yesu palepale alitambua si Petro anayezungumza bali ni shetani, akamkea na kumwambia nenda nyuma yangu shetani (Mathayo 16:23).

Mfano wa hawa pia ni wale manabii 400 wa Ahabu. Ambao walimtabiria mfalme kuwa akienda vitani atashinda, kumbe ni pepo la uongo liliwaingia vinywani mwao likawaonyesha maono feki. Matokeo yake yakawa ni mfalme kufa (1Wafalme 22).

Mfano wa watumishi wa namna hii wanaompa shetani nafasi kuwatumia ni wengi sana. Hivyo si kila neno ambalo utaambiwa na kila anayeitwa mtumishi ulipokee tu au uliamini, ukijawa Roho vema utaweza yapambanua vizuri mafumbo haya ya shetani katikati ya vinywa vyao. Atakupa upambanuzi, kwa mafuta aliyoyaweka ndani yako.

Kundi la watumishi wa shetani: Hawa wanajijua kabisa kuwa ni watumishi wa ibilisi, ni wachawi wanaovaa suti na majoho, na kusimama madhabahuni, hawana hata ushirika na Kristo. Kuwatambua hawa Roho alitufundisha, ni kutazama matunda yao. (Mathayo 7:15-20), asilimia kubwa ya hawa wanajigamba kwa vitu, ukubwa. Na mafundisho yao ni ya mwilini. lakini pia kwasababu wana mapepo ya utambuzi hupendelea sana kujitii manabii. Ni wengi leo wanawafuata kwasababu ya kazi hiyo, wakidhani wanatabiriwa na Roho Mtakatifu kumbe ni mizimu. Ukijawa Roho vema utaweza kuzitambua hizo Roho. Kwasababu hazina ushirika hata kidogo na jina la Yesu, au mambo ya rohoni.

Mafumbo ya Mungu.

Mungu pia ana mafumbo yake, ambayo kama huna Roho Mtakatifu huwezi yatambua. Kwamfano Kristo anatembea leo duniani, akiwa na kiu, na njaa na uchi, na anagonga kwenye milango ya watu..Sasa kwasababu wewe hujui unadhani akija kwako atakutokea amevaa mavazi meupe na uso unaong’aa kama jua,  hujui kuwa amekuja kama watumishi wa Mungu wa kweli wanaojitaabisha kwa ajili ya roho yako, kukulea na kukulisha neno la Mungu. Lakini wewe unasema hawa ni matapeli, omba omba.

Mathayo 25:31  Hapo atakapokuja Mwana wa Adamu katika utukufu wake, na malaika watakatifu wote pamoja naye, ndipo atakapoketi katika kiti cha utukufu wake;

32  na mataifa yote watakusanyika mbele zake; naye atawabagua kama vile mchungaji abaguavyo kondoo na mbuzi;

33  atawaweka kondoo mkono wake wa kuume, na mbuzi mkono wake wa kushoto.

34  Kisha Mfalme atawaambia wale walioko mkono wake wa kuume, Njoni, mliobarikiwa na Baba yangu, urithini ufalme mliowekewa tayari tangu kuumbwa ulimwengu;

35  kwa maana nalikuwa na njaa, mkanipa chakula; nalikuwa na kiu, mkaninywesha; nalikuwa mgeni, mkanikaribisha;

36  nalikuwa uchi, mkanivika nalikuwa mgonjwa, mkaja kunitazama; nalikuwa kifungoni, mkanijia.

37  Ndipo wenye haki watakapomjibu, wakisema, Bwana, ni lini tulipokuona una njaa, tukakulisha, au una kiu tukakunywesha?

38  Tena ni lini tulipokuona u mgeni, tukakukaribisha, au u uchi, tukakuvika?

39  Ni lini tena tulipokuona u mgonjwa, au kifungoni, tukakujia?

40  Na Mfalme atajibu, akiwaambia, Amin, nawaambia, kadiri mlivyomtendea mmojawapo wa hao ndugu zangu walio wadogo, mlinitendea mimi.

Umeona hao wanaozungumziwa hapo, sio wale maskini unaowaona barabarani, au omba-omba, bali ni watendakazi wa Mungu. Hivyo watu wanaoonyosha mikono yao, kuwatengemeza watumishi na madhabahu za kweli za Mungu, wamejaliwa kuyajua mafumbo haya ya Mungu.

Mafumbo ya Mungu yapo mengi sana, ndio siri za ufalme wa mbinguni ambazo zipo ndani ya Yesu Kristo. Ambazo Yesu mwenyewe alizizungumza pia katika Mathayo 13.

Vilevile ukitaka umwone Mungu fumbo lake ni upendo, Ukitaka upewe na Mungu, fumbo lake ni utoe, ukitaka ukwezwe na Mungu fumbo lake ni unyenyekevu.

Kwanini leo utaona mtu anasema sijawahi kumsikia Mungu, na angali Mungu anasema nasi kila siku? Sijawahi kukutana na Mungu, na angali Mungu anakutana nasi kila siku? Sijawahi kuziona nguvu za Mungu, na wakati zipo nasi kila kitu? Ni kwasababu hajajawa vema Roho Mtakatifu, ambaye atamjalia kuujua moyo wa Mungu upo wapi.

Hivyo kwa hitimisho ni kuwa, tunahitaji  kujazwa Roho na hiyo inakuja tutengapo muda wetu mwingi kila siku kutafakari sana Neno, pamoja na kuomba kila siku kwa muda usiopungua saa moja , hiyo itakupelekea kujazwa vema Roho, na hatimaye tutaweza kuyachunguza yote, na kuyatambua yote. Na wala hatutashindwa aidha na mwanadamu au shetani.

Ubarikiwe.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

JINSI ROHO MTAKATIFU ANAVYOKUJA JUU YA MTU.

Roho Mtakatifu ni nani?.

ZIFAHAMU KAZI KUU (10) ZA SHETANI DUNIANI.

Rudi Nyumbani

Print this post

IFUATE KANUNI SAHIHI YA MUNGU

Zipo kanuni za ki-Mungu tunaweza kuzifuata na zikaleta matokeo kabisa halisi, lakini zisiwe na manufaa kwetu katika suala la wokovu.  Sasa kabla ya kuangalia ni kwa namna gani? 

chukulia mfano wa kawaida.

Mwanamke yeyote anaweza kubeba ujauzito katika mazingira mbalimbali, kwamfano anaweza akatwezwa nguvu (akabakwa), na akapata ujauzito, lakini pia anaweza kwenda kujiuza kama kahaba na bado akapata ujauzito, vilevile anaweza akasubiri aolewe kwanza katika ndoa halali ndipo apokee ujauzito na likafanikiwa vilevile tu, kuleta kiumbe duniani, kama angefanya hayo kabla ya ndoa, au atokapo nje ya ndoa yake.

Sasa unaweza jiuliza, katika njia zote hizo ambazo angepata ujauzito ni ipi iliyo halali inayokubalika mbele za Mungu na wanadamu. Bila shaka ni hiyo njia ya mwisho ambayo ni ya kuolewa kwanza, ndipo apokee ujauzito kutoka kwa mume wake mmoja wa halali. Na ndio mtoto huyo hujulikana kama halali sio haramu.

Lakini cha ajabu ni kuwa ijapokuwa njia halali ipo lakini feki pia huleta matokeo yaleyale mfano wa halali. Kwasababu gani? Kwasababu kanuni ya kupata mtoto, si kanuni ya uhalali. Hivyo ni vitu viwili tofauti, 

Hata Ibrahimu, alikuwa na watoto wengi, alitangulia Ishmaeli, kisha baadaye wakazaliwa na watoto wengine sita kwa suria mwingine, mbali na Isaka. Wote walikuwa wanadamu, viumbe wa Mungu, wenye akili na nguvu na baraka, wasio na hatia. Lakini lilipokuja suala la urithi, ndipo kubaguliwa  kulipokuja, Watoto wote wa masuria walifukuzwa wakapewa zawadi tu bali Isaka alipewa vyote.

Mwanzo 25:5-6

[5]Ibrahimu akampa Isaka yote aliyokuwa nayo. 

[6]Lakini wana wa masuria aliokuwa nao Ibrahimu, Ibrahimu akawapa zawadi, naye akawaondoa katika mahali alipokaa Isaka mwanawe, wakati wa uhai wake, waende pande za mashariki, mpaka nchi ya Kedemu. 

Hii ni kutufundisha nini hasaa katika maisha yetu ya wokovu.

Zipo kanuni nyingi sana za kiroho ambazo mtu yeyote, hata ambaye  hajamwamini Yesu anaweza zitumia na zikatoa matokeo yaleyale sawa tu na mtu ambaye ameokoka.

Kwamfano, kufanya miujuza na ishara kwa jina la Yesu. Watu hawajui kuwa jambo hili huhitaji imani tu, katika jina lake. Hivyo wale wafikiao kiwango hicho haijalishi ni mwizi, ni mpagani, anaweza pokea muujiza na akafanya pia muujiza sawa tu na yule aliyeokoka.

Kwasababu gani? kwasababu amefanikiwa kufuata kanuni ambayo ni Imani.

Akijua lile neno linalosema  ‘yote yawezekana kwake yeye aaminiye’’ (Marko 9:23). Ndio maana walikuwepo watu wengi wasiokuwa wayahudi kipindi kile cha Yesu walipokea miujiza mikubwa, zaidi ya wayahudi kwasababu tu ya ukubwa wa imani zao. Na sio haki zao.

Vivyo hivyo hata katika kuomba. Mtu yeyote aombaye hupokea. Ni kanuni ya asili ya rohoni, haijalishi ni nani.

Mathayo 7:8

[8]kwa maana kila aombaye hupokea; naye atafutaye huona; naye abishaye atafunguliwa. 

Watu hawajui hata kufanikiwa kwa shetani hutegemea maombi, na yeye pia huenda mbele za Mungu kuomba na hupewa..hajiamulii tu mambo yake ovyo ovyo bila idhini ya Mungu, kwasababu hii dunia si yake… utauliza kwa namna gani, ? unamkumbuka shetani kipindi cha Ayubu, yeye naye alikwenda kujihudhurisha mbele za Mungu, ndipo akaleta uharibifu. Akapeka haja zake akasikiwa, dua zake na magoti yake.

Ayubu 1:6

[6]Ilikuwa, siku moja ambayo hao wana wa Mungu walikwenda kujihudhurisha mbele za BWANA, Shetani naye akaenda kati yao. 

Watu wengi wanapoona wanamwomba Mungu wanajibiwa wanadhani, ndio wamekubaliwa na Mungu. Kumbe unaweza kuomba kama mwana-haramu usiyekuwa na urithi wa uzima wa milele, bali haki ya kupokea tu unachokiomba.

Unaweza ukafanya miujiza kama mwana-haramu. Lakini usiende mbinguni.

Mathayo 7:22-23

[22]Wengi wataniambia siku ile, Bwana, Bwana, hatukufanya unabii kwa jina lako, na kwa jina lako kutoa pepo, na kwa jina lako kufanya miujiza mingi? 

[23]Ndipo nitawaambia dhahiri, Sikuwajua ninyi kamwe; ondokeni kwangu, ninyi mtendao maovu. 

 Unaweza ukamwamini Yesu, na kumuhofu,  lakini ukaamini kama mashetani.

Yakobo 2:19

[19]Wewe waamini ya kuwa Mungu ni mmoja; watenda vema. Mashetani nao waamini na kutetemeka. 

unaweza ukawavuta watu kwa Kristo na wakaokoka, lakini ukawa mtu wa kukataliwa kama tu Paulo alivyosema katika; 

1 Wakorintho 9:27

[27]bali nautesa mwili wangu na kuutumikisha; isiwe, nikiisha kuwahubiri wengine, mwenyewe niwe mtu wa kukataliwa. 

Sasa kanuni sahihi ya Mungu ni ipi ili tuonekane kamili na halali?

Kanuni Mungu anayoitazama kwetu ni Wokovu uliokamilishwa kwa matendo yake.

Angalia mwishoni pale kwenye Mathayo 7:23 Bwana Yesu alichokisema;

“ondokeni kwangu, ninyi mtendao maovu”

Umeona je unaishi maisha gani?. hicho ndio kipimo cha ki-Mungu, 

Alisema pia.

Yakobo 2:24

[24]Mwaona kwamba mwanadamu huhesabiwa kuwa ana haki kwa matendo yake; si kwa imani peke yake. 

Hakikisha maisha yako yanaendana na ukiri wako, wa imani yako, usiishi tu kama mtu ambaye hajaamini ukijitumainisha, kuona maombi yako yanajibiwa, karama yako inafanya kazi, imani yako inatenda kazi..hizo ni kanuni za kupokea lakini sio kanuni za uhalali wa kuurithi uzima wa milele. Ishi kama mtu ampendezaye Bwana wake kimwenendo, ndipo hayo mengine yakifuata huna hasara.

Nyakati hizi za mwisho, adui anaweka uzito kwenye mioyo ya watu wasipende kutafuta maisha matakatifu, kinyume chake wabakie tu kwenye miujiza, uponyaji, utabiri…Siku ile hivyo vitu havitafuata na wewe ndugu, bali matendo yako.

Ufunuo wa Yohana 14:13

[13]Nikasikia sauti kutoka mbinguni ikisema, Andika, Heri wafu wafao katika Bwana tangu sasa. Naam, asema Roho, wapate kupumzika baada ya taabu zao; kwa kuwa matendo yao yafuatana nao. 

Tuanze sasa kujipima mienendo yetu. Kisha tutumie nguvu nyingi hapo kujirekebisha, sawasawa na imani tuliyoipokea, ili tuwe wana halali waliozaliwa kweli ndani ya Kristo, watakaorithi uzima wa milele.

Wokovu wa kweli hufunuliwa kwa mwenendo mzuri. Tuitazame sana kanuni hii.

Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >>

https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

KANUNI JUU YA KANUNI.

KANUNI YA KUOMBA NA KUPOKEA.

JE NI HALALI KUOA WAKE WENGI AU KUTOA TALAKA?

Print this post