Title Devis

Nini maana ya “SAA INAKUJA” na “SASA IPO” (Yohana 4:23).

Jibu: Turejee,

Yohana 4:19  “Yule mwanamke akamwambia, Bwana, naona ya kuwa u nabii!

20  Baba zetu waliabudu katika mlima huu, nanyi husema ya kwamba huko Yerusalemu ni mahali patupasapo kuabudia.

21  Yesu akamwambia, Mama, unisadiki, saa inakuja ambayo hamtamwabudu Baba katika mlima huu, wala kule Yerusalemu.

22  Ninyi mnaabudu msichokijua; sisi tunaabudu tukijuacho; kwa kuwa wokovu watoka kwa Wayahudi.

23  Lakini SAA INAKUJA, NAYO SASA IPO, ambayo waabuduo halisi watamwabudu Baba KATIKA ROHO NA KWELI. Kwa maana Baba awatafuta watu kama hao wamwabudu”.

Maana ya kumwabudu Baba katika roho na kweli, ni KUMFANYIA MUNGU IBADA, KATIKA ROHO MTAKATIFU NA KATIKA KWELI YA NENO LAKE.

Yohana 16:13 “Lakini yeye atakapokuja, huyo ROHO WA KWELI, ATAWAONGOZA AWATIE KWENYE KWELI YOTE…”

Sasa BWANA YESU aliposema kuwa “SAA INAKUJA”, alimaanisha kuwa kuna kipindi kinakuja  mbeleni, ambacho waabuduo halisi watamwabudu Baba katika roho na kweli, na wakati huo si mwingine Zaidi ya ule wa Pentekoste. Kipindi ambacho Roho Mtakatifu atamwagwa juu ya kanisa kwa mara ya kwanza, baada ya BWANA YESU kuondoka!.

Huo ndio uliokuwa mwanzo wa watu kumwabudu Baba katika roho na kweli. (Matendo 2:1-15)

Lakini pia aliposema kuwa..“NA SASA IPO”…. maana yake hata huo wakati tayari Baba ameshaanza kuabudiwa katika roho na kweli. Na aliyekuwa anamwabudu baba katika ROHO NA KWELI ni yeye mwenyewe BWANA YESU KRISTO. Kwasababu tayari alikuwa na Roho Mtakatifu ndani yake, ambaye alipoondoka ndipo akammwaga juu ya kanisa.

Yohana 16:7 “Lakini mimi nawaambia iliyo kweli; yawafaa ninyi mimi niondoke, kwa maana mimi nisipoondoka, huyo Msaidizi hatakuja kwenu; bali mimi nikienda zangu, nitampeleka kwenu”.

Na hata sasa tupo kipindi ambacho Neema ya Roho Mtakatifu bado ipo duniani kwa kila anayemwitaji sawasawa na Matendo 2:38, Na kumbuka Roho Mtakatifu pekee ndiye funguo za mtu kumwabudu Mungu katika roho na kweli, na pasipo yeye haiwezekani kumwabudu Mungu katika roho.

Kwa somo refu lihusuyo jinsi ya kumwabudu Mungu katika roho na kweli fungua hapa >>Nini maana ya kumwabudu Mungu katika Roho na kweli?

Bwana akubariki.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618

Mafundisho mengine:

NI SAA KUMI NA MBILI (12) TU, ZA KRISTO KWAKO.

Bwana Yesu alimaanisha nini kusema “Saa yangu haijawadia?”

Ni muda gani Bwana Yesu alisulibiwa. Je! Ni saa 3 au saa 6?

JINSI MUNGU ATAKAVYOTOA THAWABU ZAKE, NA VIGEZO ATAKAVYOTUMIA. (Sehemu ya 5)

UWEZO WA KIPEKEE.

Rudi nyumbani

Print this post

MAOMBI MAALUMU YA WA-WAMAMA / WANAWAKE WA KANISANI.

Kama mwanamke uliyeokoka. Fahamu kuwa una wajibu wa kujiombea wewe, kuombea jinsia yako, na kuliombea Kanisa la Kristo kwa ujumla. Huu ni mwongozo wa kipengele muhimu vitakavyokusaidia katika maombi yako. ambavyo kama utakuwa ni mwombaji wa mara kwa mara katika maeneo hayo, basi unajijengea mazingira ya kuwa  mwanamke bora, mama bora, na zaidi sana mtumishi bora wa Bwana katika mwili wa Kristo.

Mwongozo huu unaweza kuutumia pia muwapo wanawake wawili au watatu katika kikundi chenu cha maombi, au kanisani. Na hivyo kila kipengele tenga muda wa kutosha kuomba.

  • Omba Bwana akufanye kuwa shujaa wa injili, pia omba Bwana anyanyue jeshi la wanawake watetea injili, watumike vema katika nafasi zao kanisani,na nje ya Kanisa, kuwaokoa wenye dhambi. Katika maandiko Mfano wa Hawa ni Prisila Matendo 18:18, 26. 

NANGA: Zaburi 68:11 “Bwana analitoa neno lake; Wanawake watangazao habari ni jeshi kubwa;”

  • Omba Bwana akupe uwezo wa kuirithisha imani kwa vizazi vijavyo, Pia awanyanyue wanamwake  vijana/wazee wengi wa namna hiyo, wenye uwezo wa kuirithisha imani ya Kristo kwa vizazi vingi mbeleni. Imani isiishie kwao tu, bali hata kwa vijukuu na vitukuu vyao.

Mfano wa wanawake  hawa alikuwa ni Loisi.

NANGA: 2Timotheo 1:5  nikiikumbuka imani uliyo nayo isiyo na unafiki, ambayo ilikaa kwanza katika bibi yako Loisi, na katika mama yako Eunike, nami nasadiki wewe nawe unayo

  • Omba Bwana aamshe kwako na kwa wanawake wote Roho ya uombolezaji(kuugua ndani) mtakaosimama katika mahali palipo bomoka kwa ajili ya kulinyanyua kanisa na wenye dhambi.

NANGA: Yeremia 9:17 Bwana wa majeshi asema hivi, Fikirini ninyi, mkawaite wanawake waombolezao, ili waje; mkatume na kuwaita wanawake wenye ustadi, ili waje;  18 na wafanye haraka na kutuombolezea, ili macho yetu yachuruzike machozi, na kope zetu zibubujike maji.  19 Maana sauti ya maombolezo imesikiwa toka Sayuni, Jinsi tulivyotekwa! tulivyofadhaika sana! Kwa sababu tumeiacha nchi, kwa kuwa wameangusha makao yetu.

  • Omba Bwana aamshe Kiu ya kupenda kujifunza Neno, ndani yako na kwa wanawake wengine wote wamchao Mungu. Mfano wa Hawa alikuwa ni Mariamu Dada yake Martha.

NANGA:  Luka 10:39  Naye alikuwa na umbu lake aitwaye Mariamu, aliyeketi miguuni pake Yesu, akasikiliza maneno yake.

  • Omba Bwana akupe Roho ya upole na utulivu; Sio ya vurugu au  kutanga-tanga huku na huko kiroho, au kimwili. Sawasawa na Agizo Mtume Petro aliloliandika kwa kanisa (1Petro 3:1-6).

NANGA: 1Petro 3:4  bali kuwe utu wa moyoni usioonekana, katika mapambo yasiyoharibika; yaani, roho ya upole na utulivu, iliyo ya thamani kuu mbele za Mungu.

  • Bwana aweke Roho ya utii, wewe na kwa Wanawake wote wamchao Bwana ndani ya Kanisa. Mfano wa ile iliyokuwa ndani ya Sara, ambayo aliweza kumtii Mungu, lakini pia mume wake.

NANGA:  1Petro 3:6 Kama vile Sara alivyomtii Ibrahimu, akamwita Bwana; nanyi ni watoto wake, mfanyapo mema, wala hamkutishwa kwa hofu yo yote

  • Bwana akupe Roho ya kupenda kujisitiri, na kuvaa mavazi ya jinsia yako, vilevile awape na wanawake wote watakatifu moyo huo.  (Kumbu 22:5)

NANGA:  1Timotheo 2:9  Vivyo hivyo wanawake na wajipambe kwa mavazi ya kujisitiri, pamoja na adabu nzuri, na moyo wa kiasi; si kwa kusuka nywele, wala kwa dhahabu na lulu, wala kwa nguo za thamani

  • Bwana akuumbie Roho ya kujitoa kwake Bwana, kwa mali zako, na kwa nguvu zako. ( Mfano wa hawa alikuwa ni Mariamu magdalena, Mshunami (Yohana 12:3, 2Wafalme 4:8-18))

NANGA: Luka 8:3  na Yoana mkewe Kuza, wakili wake Herode, na Susana, na wengine wengi, waliokuwa wakimhudumia kwa mali zao

  • Bwana aiamshe Roho ya ‘usaidizi’ katika huduma, pia iumbike katikati ya wanawake. Kumbuka wewe kama mwanamke umepewa karamu kubwa sana ya usaidizi tangu kuumbwa kwako. Ombea itende kazi vema ili iifaidie kanisa na familia.

NANGA:  Mwanzo 2:18  Bwana Mungu akasema, Si vema huyo mtu awe peke yake, nitamfanyia msaidizi wa kufanana naye

  • Bwana akuumbie Roho ya uaminifu hata pale ambapo hujapata kitu chochote. Usimwache Bwana.

NANGA: Luka 1:6  Na wote wawili walikuwa wenye haki mbele za Mungu, wakiendelea katika amri zote za Bwana na maagizo yake bila lawama. 7  Nao walikuwa hawana mtoto, maana Elisabeti alikuwa tasa, na wote wawili ni wazee sana

  • Akupe Roho ya kumwimbia Mungu kwa moyo wote wa furaha na kuchangamka Mfano wa wanawake mashujaa waliomcha Mungu zamani, ambao hawakuona aibu kumwimbia Bwana kwa mioyo yao yote.

 NANGA: Kutoka 15:20 Na Miriamu, nabii mke, ndugu yake Haruni, akatwaa tari mkononi mwake; wanawake wakatoka wote wakaenda nyuma yake, wenye matari na kucheza.  21 Miriamu akawaitikia,Mwimbieni Bwana ,kwa maana ametukuka sana;Farasi na mpanda farasi amewatupa baharini

  • Omba Bwana akuumbie Nguvu ya “maombi ya kung’ang’ania” mpaka ipatikane ichipushwe pia miongoni mwa kundi Mfano wa Hawa alikuwa ni Rispa binti aya ambaye aliweza kukesha milimani kufunga na kuombeleza kwa miezi mingi mpaka mfalme akasikia habari zake, akatoa agizo juu yake

NANGA: Soma – 2Samweli 21, yote

  • Bwana akupe Roho ya Uwazi na kusaidiana kwa umoja na wanawake wenzako wacha Mungu ndani ya kanisa na pia iwepo  kwa wanawake wote.

NANGA: Luka 24:22  tena, wanawake kadha wa kadha wa kwetu walitushitusha, waliokwenda kaburini asubuhi na mapema, 23  wasiuone mwili wake; wakaja wakasema ya kwamba wametokewa na malaika waliosema kwamba yu hai

PIA OMBA…

  • Bwana akuumbie Roho ya uangalizi na ulezi kwa watoto, na vijana katika maadili ya kumcha Bwana

NANGA: 2Yohana 1:1  Mzee, kwa mama mteule na watoto wake niwapendao katika kweli; wala si mimi peke yangu, bali na wote waijuao ile kweli;

  • Upewe Roho ya huruma na ya kutunza uhai. Mfano wa hawa ni  (yehosheba). Aliuhifadhi uzao wa kifalme katika  Israeli kwa kumficha mtoto asiuawe.  (2Wafalme 11:2). Ilikuwa pia kwa mama yake Musa, lakini pia kwa Shifra na Pua wazalisha wa kiebrania

NANGA:  (Soma Kutoka 1:15-19)

  • Roho ya unyenyekevu na ya kujiachilia kwa Bwana moja kwa moja, bila kigugumizi chochote cha rohoni. Mfano wa Ruthu kwa Naomi, ambaye alijitoa kwa mkwewe katika hali zote bila kujali ujana wake, au umaskini wa mkwewe.

NANGA: Ruthu 1:16 Naye Ruthuu akasema, Usinisihi nikuache, Nirejee nisifuatane nawe; Maana wewe uendako nitakwenda, Na wewe ukaapo nitakaa. Watu wako watakuwa watu wangu, Na Mungu wako atakuwa Mungu wangu;  17 Pale utakapokufa nitakufa nami, Na papo hapo nitazikwa; Bwana anitende vivyo na kuzidi, Ila kufa tu kutatutenga wewe name

  • Akupe Moyo wa ujakazi mwema wenye manufaa, utakaowaleta wengine kwa Kristo ikiwa wewe ni mwajiriwa mahali fulani (Mfano wa hawa alikuwa ni Roda, &  Yule kijakazi wa Naamani) – 2 Wafalme 5:1-19, Matendo 12:13
  • Bwana akupe moyo wa kupenda kudumu hekaluni mwa Bwana. Vivyo hivyo na wanawake wote kanisani. Mfano ni Ana binti Fanueli.

NANGA: Luka 2:36  Palikuwa na nabii mke, jina lake Ana, binti Fanueli, wa kabila ya Asheri, na umri wake ulikuwa miaka mingi, alikuwa amekaa na mume miaka saba baada ya uanawali wake. 2.37  Naye ni mjane wa miaka themanini na minne; haondoki katika hekalu, ila huabudu usiku na mchana kwa kufunga na kuomba

  • Bwana akupe ufahamu wa kuyatunza Maneno ya Mungu moyoni wako. Usiwe wa kutokuzingatia kile Mungu anachosema na wewe. Mfano bora ni  (Mariamu mamaye Yesu)

NANGA: Luka 2:51  Nao hawakuelewa na neno hilo alilowaambia. 51  Akashuka pamoja nao mpaka Nazareti, naye alikuwa akiwatii; na mamaye aliyaweka hayo yote moyoni mwake

  • Roho ya kupenda kujitaabisha kwa Bwana katika hekima yote ya ki-Mungu itokee ndani yako na kwa wanawake wengine. (Martha)-

NANGA: Luka 10:40  “Lakini Martha alikuwa akihangaika kwa utumishi mwingi;..”

  • Bwana akujalie wewe na wanawake wote Roho ya nguvu na ya ujasiri ya kuweza hata kuliamua taifa. Mfano wa Debora, katika nafasi yako kama mama.

NANGA: Waamuzi 4:4 Basi Debora, nabii mke, mkewe Lapidothi, ndiye aliyekuwa mwamuzi wa Israeli wakati ule.  5 Naye alikaa chini ya mtende wa Debora, kati ya Rama na Betheli, katika nchi ya vilima vilima ya Efraimu; wana wa Israeli wakakwea kwake, awaamue

  • Roho ya kuthamini, Bwana alivyoviweka mkononi mwako, kuvilinda na kuvitafuta pindi vipoteapo.

NANGA: Luka 15:8  Au kuna mwanamke gani mwenye shilingi kumi, akipotewa na moja, asiyewasha taa na kufagia nyumba, na kutafuta kwa bidii hata aione? 15.9  Na akiisha kuiona, huwaita rafiki zake na jirani zake, akawaambia, Furahini pamoja nami, kwa kuwa nimeipata tena shilingi ile iliyonipotea.

  • Bwana akupe Roho ya kuridhika na hali, na mwonekano wako, kutoongeza mapambo mwilini. Usiwe kama Yezebeli-2Wafalme 9:30
  • Bwana awajalie wanawake wote wakue kiroho, ili wasichukuliwe mateka na watu wadanganyifu (2Timotheo 3:6)
  • Bwana awafariji wajane wote, lakini pia awape moyo wa kupenda kutoa na kutumika (Mfano wa Yule aliyetoa senti mbili, Yule aliyetembelewa na Eliya)-

NANGA: Soma (Marko 12:42, 1Wafalme 17:12, Luka 7:11)

OMBA PIA…

  • Roho ya kuwajibika kwa wanawake, Bwana aiamshe kwako na  katika kanisa (kupenda kushughulika Mithali 31:10-31
  • Bwana awajalie wanawake wote Wajawazito kujifungua salama.(Kutoka 1:15-17, Isaya 66:9)
  • Mabinti/ wanawake katika kanisa wanaotaka kuolewa, Bwana awape wenzi sahihi (Abigaili aliolewa na Nabali mume asiyestahili. -1Samweli  25)  Jambo hilo lisitokee ndani ya kanisa.
  • Magonjwa yanayoishambulia jinsia ya kike. Bwana ayafute mbali na wewe na ndani ya kanisa la Mungu (Marko 5:25-34)

PIA OMBA HIZI TABIA ZIONDOKE NDANI YAKO NA WANAWAKE WOTE…

  • Roho ya kujichanganya na makundi yasiyofaa/ kutokuwa na mipaka, itoweshwe (Dina hakuwa na mipaka,  akahadaiwa na watu wa kidunia – Mwanzo 34:1).
  • Roho ya utoaji mimba, ipotelee mbali kwa wanawake wacha Mungu na kwa jamii yetu (Kutoka 20:13, Ayubu 3:3-12).
  • Bwana aifutilie mbali tabia ya kupuuzia maono: Mke wa Herode alisemeshwa kwa ajili ya haki ya Yesu lakini hakuchukua hatua stahiki, kama Bwana alivyotaka (Mathayo 27:19)
  • Wanawake wa kikristo wanaonyanyaswa kijinsi agh. Kulazimishwa kuolewa, kukeketwa, kubakwa, kupigwa, kunyimwa haki za elimu, na kumcha Mungu n.k. Bwana afutilie mbali hiyo roho; > Mfano ni Kisa cha Tamari na amnoni (2Samweli 13)
  • Nguvu za giza zinazowavaa wanawake kiwepesi, zisipate nafasi ndani ya kanisa la Kristo.( Marko 16:9)
  • Roho ya udanganyifu wa nyoka, (kushawishwa) Bwana aifukuzie mbali na kanisa lake takatifu (Mwanzo 3:1)
  • Roho ya uuaji ya Yezebeli na Athalia, na herodia  isipate nafasi ndani ya Kanisa la Bwana –, (2Wafalme 11:1, Mathayo 14:8)
  • Roho ya kiburi isitokee miongoni mwa kundi (Vashti –Esta 1:12)
  • Roho ya masengenyo, na udadisi ifutwe katikati ya kundi la Kristo (1Timotheo 5:13)
  • Roho za ndoa kuvunjika, na magomvi zisitoe mzizi ndani ya kanisani.  (Waefeso 5:33)
  • Roho ya kukufuru kama ya Mke wa Ayubu Bwana aifutilie mbali. (Ayubu 2:9)
  • Roho ya kupenda ulimwengu na mambo ya kidunia, iondoshwe (Mke wa Lutu) –Mawnzo 19:26
  • Roho ya tamaa ya kuiba vya Mungu, isichipuke ndani ya kundi la wanawake ( mkewe Safira) Matendo 5:1
  • Roho ya uzinzi ife iyeyushwe kabisa (mke wa potifa)- Mwanzo 39:7
  • Roho ya ushirikina na uchawi isipate nafasi miongoni mwa wanawake (mganga wa Sauli)-Samweli 28:11
  • Roho ya mashindano itoweke miongoni mwa wanawake (Lea na Raheli, wanawake hao)-Mwanzo 29:30
  • Roho ya kuzira/ kukwazika mapema hata kutaka kuacha kutumika ifitwe miongoni mwa wanawake (Hajira- Mwanzo 16:9)
  • Roho ya kutumiwa na adui (u-agent), ili kuliangusha kundi ifutwe (Delila –Waamuzi 16)
  • Roho ya kusema uongo/  kutumia hila,  isionekane ndani ya kundi (Mama yake Yakobo – Rebeka- Mwanzo 27:6)
  • Roho ya uchungu usiokoma moyoni, vinyongo, visasa, kutokuachilia, kutokusamehe, iyeyuke ndani ya wanawake.(Yakobo 3:14)
  • Roho ya matabaka, ndani ya Kanisa ipotelee mbali(Wafilipi 4:2). Sintike na Euodia
  • Roho ya udhuru isisimame ndani ya kundi la wanawake kanisani. – (Matendo 1:14)
  • Roho ya kudharau, watu wa Mungu, au kazi ya Mungu, isiwe na sehemu miongoni mwa wanawake( Mfano wa Mikali, binti Sauli. 2Samweli 6:16

Kwa ushauri/ Msaada/ Maombezi /Ratiba za ibada, wasiliana nasi kwa mawasiliano haya;

Na, Mwl Denis & Devis Julius

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618

Mafundisho mengine:

KANUNI YA KUOMBA NA KUPOKEA.

MWONGOZO WA MAOMBI YA WAHUDUMU/ WASIMAMAO MADHABAHUNI.

Kwanini wanawake wengi huwa wanalipuka mapepo?

NIFANYE NINI ILI MUNGU AYAJIBU MAOMBI YANGU?

MWANAMKE, BINTI, MAMA.( Sehemu ya 1)

Rudi nyumbani

Print this post

Nini maana ya  Mithali 21:1 Moyo wa mfalme huwa katika mkono wa Bwana;

SWALI: Nini maana ya  Mithali 21:1

“Moyo wa mfalme huwa katika mkono wa Bwana; Kama mifereji ya maji huugeuza po pote apendapo”.


JIBU: Kuna mithali inayosema “maji hufuata mkondo”. Ikiwa na maana, palipo na mfereji kule kule unapoelekea ndipo maji nayo huelekea. Mfano ukielekeza mrefeji shambani mwako, basi maji yale yataelekea huko si kwingineko, ukielekezea mfereji nyumbani mwako, basi maji yatakuja ndani mwako. Kamwe maji  hayajiamulii  pa kuririkia.

Vivyo hivyo na Mungu, ndivyo anavyofananisha mamlaka yake juu ya wafalme na wakuu wa dunia hii. Kwamba mashauri yao, hawajiamulii tu peke yao kwa kujitakia. Kwamfano utakumbuka kuna wakati  Mungu alimnyanyua Moyo Koreshi mtawala wa Uajemi ili awape ruhusu wayahudi warudi katika nchi yao wakamjengee nyumba.

Ezra 1:1 Ikawa katika mwaka wa kwanza wa Koreshi, mfalme wa Uajemi, ili kwamba neno la Bwana alilolisema kwa kinywa cha Yeremia lipate kutimizwa, Bwana akamwamsha roho yake Koreshi, mfalme wa Uajemi, hata akapiga mbiu katika ufalme wake wote, akaiandika pia, akisema,  2 Koreshi, mfalme wa Uajemi asema hivi;  3 Basi kila mtu katika ninyi nyote mlio watu wake, Bwana, Mungu wake, na awe pamoja naye, na akwee mpaka Yerusalemu, ulioko Yuda, akaijenge nyumba ya Bwana, Mungu wa Israeli, (yeye ndiye Mungu), iliyoko Yerusalemu.  4 Na mtu awaye yote aliyesalia mahali po pote akaapo hali ya ugeni, na asaidiwe na watu wa mahali pake, kwa fedha, na dhahabu, na mali, na wanyama, zaidi ya vitu vitolewavyo kwa hiari ya mtu, kwa ajili ya nyumba ya Mungu, iliyoko Yerusalemu

Mungu huyo  huyo ndiye aliyemfanya mfalme Nebukadreza kuwa na moyo mkatili ili awachukue watu wake utumwani kwasababu ya makosa yao.(Yeremia 27:6, 43:10)

Mungu anaweza kuwatumia watawala kuadhibu taifa, au kuwabariki watu wake. Hii ni kuonyesha kuwa hakuna tawala yoyote katika hii dunia inamilikiwa na fikra za mwanadamu asilimia 100, bali mengi ya mashauri ya wakuu hutoka juu mbinguni, au yameruhusiwa na Mungu. Wao ni kama maji tu yanayofuata mkondo wa kusudi la Mungu.

Ndio jambo ambalo Mungu alimwambia Mfalme Nebukadreza kwamba “aliye juu ndiye anayetawala”(Danieli 5:21) lakini yeye alidhani ni uongo, mpaka siku alipoondolewa kwenye ufalme wake kwa miaka 7, na kurudishwa baadaye.

Hivyo, jambo hili, sio tu la viongozi wa kidunia, lakini pia hata wa kanisani. Ikiwa kanisa ulilopo linasimamia kweli na utakatifu na Kristo Yesu ndio kiini cha fundisho lao, basi waheshimu sana viongozi wako, kwasababu si kila shauri linalotoka kwenye vinywa vyao, ni wao wamefikiria. Wao ni kama maji tu yaliyomwagwa kwenye mfereji, ili kukuongoza wewe. ukishandana nao, au ukipuuzia kuongozwa nao, wakati mwingine unapingana na maamuzi ya Mungu wako bila kujijua.

Waheshimu viongozi wako wanaokulea kiroho, kama vile unavyowaheshimu watawala ya kidunia.

Bwana akubariki.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Shalom

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618

Mafundisho mengine:

Fahamu maana ya Mithali 29:4 “Mfalme huithibitisha nchi kwa hukumu; Bali yeye apokeaye rushwa huipindua.

Ni kwa namna gani Kristo analitakasa kanisa kwa Maji katika Neno? (Waefeso 5:26)

MADHARA YA KUKOSA MAJI YA UZIMA BAADA YA KIFO.

NDIPO HUENDA AKACHUKUA PEPO WENGINE SABA.

ITAMBUE KARAMA YA MUNGU.

Rudi nyumbani

Print this post

Mabibi wastahiki walikuwa ni watu gani? (Esta 1:18).

(Mada maalumu kwa wanawake)

Jibu: Mabibi Wastahiki ni “wanawake wa heshima”.. kundi hili la wanawake lilihusisha wake za Wafalme, Maliwali au Maakida au Majumbe..

Wakati mfalme Ahasuero alipowafanyia maakida wake na maliwali wake karamu, biblia inatuambia kuwa Malkia Vashti (mke wa mfalme), yeye naye aliwafanyia wanawake (ambao ni wake wa hao maakida na maliwali) karamu.

Esta 1:2 “siku zile mfalme Ahasuero alipoketi katika kiti cha enzi cha ufalme wake, huko Shushani ngomeni;

3 mwaka wa tatu wa kumiliki kwake, ikawa aliwafanyia karamu maakida wake wote na majumbe wake; wakuu wa Uajemi na Umedi, watu wenye cheo na maakida wa majimbo, wakihudhuria mbele zake. 

4 Akawaonyesha utajiri wa ufalme wake mtukufu, na heshima ya enzi yake bora siku nyingi, maana siku mia na themanini……………………..

9 Tena Vashti, malkia, naye akawafanyia karamu WANAWAKE NDANI YA NYUMBA YA KIFALME YA MFALME Ahasuero”.

Sasa hao wanawake waliokuwa wake za “maliwali na maakida” ndio waliojulikana kama “mabibi wastahiki”.. wakiongozwa na Malkia Vashti.

Lakini tunachoweza kujifunza ni kuwa ile karamu ya hawa wanawake haikuwa na utukufu wowote, kwani iliishia kuleta aibu kubwa katika ufalme wote wa Uajemi. Kwani Malkia Vashti alikosa utii kwa Mfalme alipoitwa, na zaidi sana alionyesha dharau hizo mbele ya Mfalme na maliwali wake wote.

Na huenda pia kiburi hicho kilichochewa na jopo la wale wanawake wengine wastahiki waliohudhuria karamu hiyo ya Malkia Vashti. Hiyo ikifunua kuwa hakuna cha maana walichokuwa wanakizungumza au kukipanga katika hiyo karamu Vashti aliyowaandalia, huenda yaliyokuwa yanazungumziwa kule ni UMBEA TU na kusema mapungufu ya waume zao!

Hiyo ikamfanya Vashti apoteze umalkia wake, na hata hao wanawake wengine ambao wastahiki kuzidi kutawaliwa na waume zao.

Esta 1:16 “Basi Memukani akajibu mbele ya mfalme na maakida, Huyu Vashti, malkia, hakumkosa mfalme tu peke yake, ila na maakida wote, na watu wote pia walioko katika majimbo yote ya mfalme Ahasuero. 

17 Kwa maana tendo hilo la malkia litajulikana na wanawake wote, hata waume zao watadharauliwa machoni pao, itakaponenwa ya kuwa mfalme Ahasuero aliamuru Vashti, malkia, aletwe mbele yake, bali hakuja. 

18 Hata na leo hivi mabibi wastahiki wa Uajemi na Umedi waliokwisha kuzisikia habari za tendo lake malkia watawaambia vivi hivi maakida wote wa mfalme. Hivyo kutatokea dharau nyingi na ghadhabu tele.

 19 Basi mfalme akiona vema, na itoke kwake amri ya kifalme, nayo iandikwe katika sheria za Waajemi na Wamedi isitanguke, ya kwamba Vashti asifike tena mbele ya mfalme Ahasuero; na umalkia wake mfalme ampe mwingine aliye mwema kuliko yeye.

 20 Basi mbiu ya mfalme atakayoipiga itakapotangazwa katika ufalme wake wote, nao ni mkubwa, wake wote watawaheshimu waume zao, wakubwa kwa wadogo.

 21 Basi neno hili likawapendeza mfalme na maakida; naye mfalme akafanya sawasawa na neno lake Memukani.

 22 Kwa maana alipeleka nyaraka katika majimbo yote ya mfalme, kila jimbo kwa mwandiko wake, na kila taifa kwa lugha yake, ya kwamba kila mwanamume atawale nyumbani mwake, na kuitangaza habari hii kwa lugha ya watu wake”.

Tabia kama hii inaendelea mpaka leo kwa baadhi ya wanawake walioolewa!, ambao baada ya kuolewa wanawaona waume zao kama si kitu tena, na hata kupoteza UTII kwao!. Pasipo kujua kuwa kwa kufanya hivyo wanazidi kujipotezea nafasi zao ndani ya familia zao, kwani badala ya kuwa kichwa Mungu anawaweka kuwa wa mwisho.

Neno la Mungu linasema wanawake na wawatii waume zao.

1Petro 3:1 “Kadhalika ninyi wake, watiini waume zenu; kusudi, ikiwa wako wasioliamini Neno, wavutwe kwa mwenendo wa wake zao, pasipo lile Neno;

2  wakiutazama mwenendo wenu safi, na wa hofu.

3  Kujipamba kwenu, kusiwe kujipamba kwa nje, yaani, kusuka nywele; na kujitia dhahabu, na kuvalia mavazi;

4  bali kuwe utu wa moyoni usioonekana, katika mapambo yasiyoharibika; yaani, roho ya upole na utulivu, iliyo ya thamani kuu mbele za Mungu.

5  Maana hivyo ndivyo walivyojipamba wanawake watakatifu wa zamani, waliomtumaini Mungu, NA KUWATII WAUME ZAO”

Soma tena Waefeso 5:24 na Tito 2:5 utaona jambo hilo hilo, sasa mwana-mama unatolea wapi kiburi!!!. Badilika, na anza kuwa mtii, ikiwa haupo ndani yako, na hiyo ni kwa faida yako na familia yako. Kitabu cha Esta, huenda kingepaswa kiitwe kitabu cha Vashti, lakini kwa kiburi chake, umalkia wake akapewa Esta.

Bwana akubariki.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618

Mafundisho mengine:

ESTA: Mlango wa 5, 6 & 7

LITANIA YA BIKIRA MARIA JE! NI SALA YA KIMAANDIKO?

YESU ANAKWENDA KUIBADILISHA OFISI YAKE.

NI KIJIJI CHA AINA GANI UPO?

MAJESHI YA PEPO WABAYA.

Rudi nyumbani

Print this post

Kipuli ni nini, na kimebeba ujumbe gani?.(Mithali 25:12).

Jibu: Turejee,

Mithali 25:12 “KIPULI CHA DHAHABU, na pambo la dhahabu safi; Ndivyo alivyo mwonyaji mwenye hekima kwa sikio lisikialo”

“Kipuli” ni jina lingine la “hereni za masikioni”.

Neno hili limeonekana mara moja tu katika biblia, katika kitabu cha Mithali 25:12.

Na mwandishi wa Mithali (Sulemani) kwa hekima ya roho alipata kuelewa vipuli (hereni) sahihi wanazopaswa wavae watu, tofauti na hizi tuzijuazo.

Anasema… “KIPULI CHA DHAHABU, na pambo la dhahabu safi; Ndivyo alivyo MWONYAJI MWENYE HEKIMA KWA SIKIO LISIKIALO”.

Maana yake ni kuwa sikio linalosikia hekima kutoka kwa wenye hekima, linafananishwa na sikio lililovishwa hereni ya dhahabu au pambo la dhahabu.

Kwa lugha nyingine ni kwamba, kama tukitaka kupamba masikio yetu kwa vitu vya thamani, basi tuwe wasikilizaji wa maneno ya hekima. (Kwani maneno hayo yataonekana kama mapambo ya thamani katika masikio yetu).

Na maneno ya hekima hatuyapati pengine isipokuwa katika biblia takatifu (Humo ndimo tutakapopata lulu na mapambo ya thamani ya masikio yetu)..

Mithali 2:1 “Mwanangu, kama ukiyakubali maneno yangu, Na kuyaweka akiba maagizo yangu;

2 HATA UKATEGA SIKIO LAKO KUSIKIA HEKIMA, UKAUELEKEZA MOYO WAKO UPATE KUFAHAMU;

3 Naam, ukiita busara, Na kupaza sauti yako upate ufahamu;

4 Ukiutafuta kama fedha, Na kuutafutia kama hazina iliyositirika;

5 Ndipo utakapofahamu kumcha Bwana, Na kupata kumjua Mungu”

Soma tena  Mithali 4:20, Mithali 5:1, na  Mithali 22:17 utaona maneno yanayopatana na hayo..

Mithali hizi zinalingana kabisa na ujumbe wa Roho Mtakatifu tunaousoma katika kitabu cha 1Petro 3:3. Na 1 Timotheo 2:9.

1 Petro 3:3 “Kujipamba kwenu, kusiwe kujipamba kwa nje, yaani, kusuka nywele; na kujitia dhahabu, na kuvalia mavazi;

4 BALI KUWE UTU WA MOYONI USIOONEKANA, KATIKA MAPAMBO YASIYOHARIBIKA; YAANI, ROHO YA UPOLE NA UTULIVU, ILIYO YA THAMANI KUU MBELE ZA MUNGU.

5 Maana hivyo ndivyo walivyojipamba wanawake watakatifu wa zamani, waliomtumaini Mungu, na kuwatii waume zao.

6 Kama vile Sara alivyomtii Ibrahimu, akamwita Bwana; nanyi ni watoto wake, mfanyapo mema, wala hamkutishwa kwa hofu yo yote”.

Mstari wa 4 unasema… “ BALI KUWE UTU WA MOYONI USIOONEKANA, KATIKA MAPAMBO YASIYOHARIBIKA; YAANI, ROHO YA UPOLE NA UTULIVU, ILIYO YA THAMANI KUU MBELE ZA MUNGU”.

Je ni vipuli gani vipo masikioni mwako?…vya chuma au vya maneno ya hekima?.

Bwana atusaidie.

Shalom.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Mafundisho mengine:

Rudi nyumbani

Print this post

WALAWI WALIKUWA WENYE MIOYO YA ADILI KWA KUJITAKASA KULIKO MAKUHANI.

2Nyakati 29:34 Lakini makuhani walikuwa wachache, wasiweze kuchuna sadaka zote za kuteketezwa; basi ndugu zao Walawi wakawasaidia, hata ilipokwisha kazi, na hata makuhani walipojitakasa; kwa kuwa Walawi walikuwa wenye mioyo ya adili kwa kujitakasa kuliko makuhani.

Nakusalimu katika jina la Bwana Yesu.

Fundisho hili linawahusu sana sana viongozi wa kiroho / Watumishi wa Mungu wanaohudumia kundi la Mungu. Mfano wachungaji au maaskofu.

Kuna wakati wale walioteuliwa kuwa viongozi wa juu kabisa wanaweza wasiwajibike ipasavyo katika nafasi zao, je! Wewe kama mwangalizi wao ufanye nini?

Mfano tukirejea habari hiyo tunaona Mfalme Hezekia alipokusudia kulitakasa hekalu la Mungu, ambalo lilikuwa limefungwa na kusahauliwa, na baba yake.

Alitafuta makuhani wa kuhudumu upya katika nyumba ya Mungu. Ikumbukwe kuwa makuhani tu ndio walioruhusiwa kufanya shughuli zote za madhahabuni, ikiwemo kuvukiza uvumba na kuandaa zile sadaka zilizoletwa mbele ya nyumba ya Bwana.

Lakini hapo biblia inatuambia, Makuhani walikuwa wachache!. Utajiuliza ni kwanini? Sio kwamba hawakuwepo kabisa, walikuwepo, lakini biblia inatuambia waliokuwa na mioyo ya adili ya kuipenda kazi ya Mungu ndio walikuwa wachache.

Pengine, wengine walikuwa na udhuru zao, wakiona kuahirisha shughuli zao, na kwenda kuhudumu madhabahuni  ni kuvurugiwa ratiba ni kazi ya kuchosha, haina faida, wengine hawakuwa tayari kujitakasa, kwa kuacha mambo mabovu yasiyowapasa makuhani, wengine wakawa wazito, wanavutwa vutwa sana, kazi ambayo inapaswa ifanyike haraka n.k..

Hivyo hiyo ikapelekea kundi la viongozi wa juu kabisa likawa chache sana. Na kimsingi ni lazima wawepo wahudumu wa kutosha katika kazi hiyo ya madhabahuni. Sasa wafanyaje. Ndipo hapo utaona Walawi ambao kazi zao ni za nje, ya hema kama vile usimamizi wa malango, kulinda hekalu, na kuimba. Ikabidi sasa waingizwe ndani kwa ajili ya kusaidia kazi za kikuhani.

Na sababu ya kufanya hivyo biblia inasema, wenyewe walikuwa ni “wenye mioyo ya adili kwa kujitakasa kuliko makuhani”.

Walikuwa na moyo wa kumtumikia Mungu zaidi hata ya wale wanaostahili. Hivyo wakapewa kazi za juu zisizowastahili na wakafanya vizuri na Mungu akawabariki, ijapokuwa ilikuwa ni kinyume na taratibu.

Hata sasa katika kanisa, ni rahisi kuona wenye ngazi za chini, ni wepesi na wenye mioyo ya uaminifu katika nyumba ya Bwana kuliko wale viongozi wa juu. Utaona ni kiongozi wa wakina mama, lakini kwenye maombi haudhurii, kuwafuatilia wanawake wenzake haangahiki. Lakini hapo hapo utaona kabinti kadogo, kanajibidiisha, haachi maombi yapite, anawapigia simu yeye kuwakumbusha kana kwamba ndio kiongozi mkuu, anatoa taarifa za maboresho na changamoto kwa kiongozi wake, mambo  ambayo hata huyo kiongozi hajui.

Sasa katika mazingira kama haya? Unadhani kiongozi ni nani? …Uongozi sio cheo, uongozi ni MOYO, uaminifu na kujitoa. Ikiwa wewe ni mwangalizi, hakikisha huyu aliye na MOYO ndio unampa wajibu na majukumu yote ya uongozi katika nafasi hiyo. Hata kama hajawekewa mikono, au hana uzoefu wowote, au hajatambulika rasmi.

Huyo huyo ndiye Mungu aliyemchagua, hao wengine ni makapi.

Kwani Bwana Yesu alishatangulia kusema maneno haya.

Mathayo 19:30  “Lakini wengi walio wa kwanza watakuwa wa mwisho, na walio wa mwisho watakuwa wa kwanza”.

Sio kwamba Mungu anao upendeleo.. Lakini alisema.. “ walioalikwa hawakustahili”(Mathayo 22:8).

Halidhalika hata katika ngazi nyingine zote, ikiwa mchungaji msaidizi haipendi kazi yake, usione vibaya, kumpa kazi hiyo shemasi mwenye MOYO wa kuwahudumia watu. Mungu atamtengeneza mwenyewe. Lakini ikiwa wewe ni kiongozi-mlegevu, tubu geuka, ipende nafasi yako, hudumu hapo kwa uaminifu kwasababu umepewa dhamana ambayo utakuja kuitolea hesabu yake siku ile ya hukumu.

Bwana awe nawe.

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618

Mafundisho mengine:

Uadilifu ni nini kibiblia?

Kwa namna gani tumefanyika Makuhani na Ufalme?.(Ufunuo 1:6)

Kwanini Yesu aliwaambia wale wakoma wakajionyeshe kwa makuhani?

VITABU VYA BIBLIA: Sehemu ya 1

Sadaka ya unga na sadaka ya kinywaji zilikuwaje?

Rudi nyumbani

Print this post

Kwa namna gani tumefanyika Makuhani na Ufalme?.(Ufunuo 1:6)

Swali: Biblia inasema katika Ufunuo 1:6 kuwa kupitia Bwana Yesu tumefanyika kuwa ufalme na makuhani, je tumefanyikaje kuwa hivyo?

Jibu: Awali ya yote tusome maandiko yafuatayo,

1 Yohana 4:17 “Katika hili pendo limekamilishwa kwetu, ili tuwe na ujasiri katika siku ya hukumu; kwa kuwa, KAMA YEYE ALIVYO, NDIVYO TULIVYO NA SISI ULIMWENGUNI HUMU”.

Hapo anasema “kama yeye alivyo ndivyo na sisi tulivyo”. Ikiwa na maana kuwa katika roho sisi tunafanana na Kristo kwa kila kitu.

Maana yake kama Kristo ni mwana wa Mungu basi na sisi ni wana wa Mungu sawasawa na Warumi 8:16.

Warumi 8:16 “Roho mwenyewe hushuhudia pamoja na roho zetu, ya kuwa sisi tu watoto wa Mungu”.

Vile vile kama Kristo alikufa na kufufuka na kuketi katika kiti cha enzi, vile vile na sisi katika roho tulikufa pamoja naye kwa njia ya ubatizo (sawasawa na Warumi 6:4 na Warumi 6:8) kwa njia ya ubatizo

Warumi 6:4 “Basi tulizikwa pamoja naye kwa njia ya ubatizo katika mauti yake, kusudi kama Kristo alivyofufuka katika wafu kwa njia ya utukufu wa Baba, vivyo hivyo na sisi tuenende katika upya wa uzima”.

Na vile vile kama Kristo alifufuka na sisi pia tulifufuka  pamoja naye na sasa tumeketi pamoja naye katika ulimwengu wa roho.

Waefeso 2:6 “Akatufufua pamoja naye, akatuketisha pamoja naye katika ulimwengu wa roho, katika Kristo Yesu”.

Kwahiyo kwa ufupi ni kwamba watu waliookoka kikamilifu wanafanana na Kristo kwa kila kitu, na hii ndio sababu kwanini shetani pamoja na mapepo yake yanawaogopa watu wa YESU KRISTO, ni kwasababu yanamwona Yesu Kristo ndani yao.

Sasa nafasi nyingine ya YESU iliyo kuu ni nafasi ya “ukuhani” na tena si kuhani tu, bali “KUHANI MKUU”.

Waebrania 8:1 “Basi, katika hayo tunayosema, neno lililo kuu ndilo hili: Tunaye kuhani mkuu wa namna hii, aliyeketi mkono wa kuume wa kiti cha enzi cha Ukuu mbinguni”.

Na kama Kristo alivyokuwa Kuhani, vile vile na sisi ni makuhani.

Na kumbuka kazi ya Makuhani ilikuwa ni kuwapatanisha watu na Mungu wao kwa njia ya SADAKA NA MAOMBI NA MAFUNDISHO.

Mfano Samweli, alifanya kazi ya kuwapatanisha Israeli kupitia sadaka zao , vilevile na kuwaombea na kuwafundisha njia iliyo sahihi..

1 Samweli 12:23 “Walakini mimi, hasha! Nisimtende BWANA dhambi kwa kuacha kuwaombea ninyi; lakini nitawaelimisha katika njia iliyo njema, na kunyoka”

Na Kristo ni hivyo kama Kuhani amesimama kutupatanisha na baba kwa njia ya kutuombea..

1 Yohana 2:1 “Watoto wangu wadogo, nawaandikia haya ili kwamba msitende dhambi. Na kama mtu akitenda dhambi tunaye Mwombezi kwa Baba, Yesu Kristo mwenye haki”.

Soma pia Warumi 8:34, utaona jambo hilo hilo.

Na pia Yesu anatupatanisha kwa Baba kwa njia ya sadaka ya mwili  wake alioutoa kwaajili yetu.

Na sisi pia kwakuwa tunafanana na yeye katika roho sawasawa na hiyo 1 Yohana 4:1, basi na sisi ni makuhani kama yeye na tunaweza kuzifanya kazi zile zile anazozifanya yeye sasa za kikuhani.

Na kazi hizo ni kuwapatanisha watu na Baba kwa njia ya MAOMBI, MAFUNDISHO NA SADAKA. Hivyo tumepewa na sisi huduma ya upatanisho kama aliyonayo Bwana wetu YESU KRISTO.

Utauliza tunalithibitisha vipi hilo kibiblia?…Tusome maandiko yafuatayo..

2 Wakorintho 5:18 “Lakini vyote pia vyatokana na Mungu, aliyetupatanisha sisi na nafsi yake kwa Kristo, naye ALITUPA HUDUMA YA UPATANISHO;

19 yaani, Mungu alikuwa ndani ya Kristo, akiupatanisha ulimwengu na nafsi yake, asiwahesabie makosa yao; NAYE AMETIA NDANI YETU NENO LA UPATANISHO”

Ndio maana tunaweza kuombeana na Mungu akasikia (Yakobo 5:16) kwasababu na sisi ni makuhani kama yeye, Vile vile kwa kujitoa miili yetu na vitu vyetu kama sadaka tunaweza kujipatanisha na kuwapatanisha wengine na Mungu.

Na hiyo yote ni kwasababu Kristo ametufanya na sisi kuwa makuhani kama yeye sawasawa na Ufunuo 1:6.

Tofauti ya Kristo na sisi ni kwamba Kristo yeye ni KUHANI MKUU, na sisi tunabaki kuwa makuhani, (yeye ni mkuu wa makuhani, utukufu na heshima zinabaki kwake, Bwana wa mabwana, mwamba imara!!!).

Na ni kwa namna gani sisi ni UFALME?.

Ni kwa namna ile jinsi Kristo alivyo…Yeye ni Mfalme, na tena si mfalme tu, bali Mfalme wa wafalme.

Ufunuo 19:16 “Naye ana jina limeandikwa katika vazi lake na paja lake, MFALME WA WAFALME, NA BWANA WA MABWANA”

Na kama yeye ni Mfalme wa wafalme, maana yake anao wafalme anaowatawala ambao nao pia ni wafalme na hao si wengine zaidi ya wale wanaomwamini..  (Kwamaana hawezi kuitwa mfalme wa wafalme kama hana wafalme chini yake anaowatawala).

Na utukufu wa ufalme tulionao sasa utakuja kudhuhirika zaidi katika ule utawala wa amani wa miaka 1000 wa YESU KRISTO.

Ufunuo 20:6 “Huo ndio ufufuo wa kwanza. Heri, na mtakatifu, ni yeye aliye na sehemu katika ufufuo wa kwanza; juu ya hao mauti ya pili haina nguvu; BALI WATAKUWA MAKUHANI WA MUNGU NA WA KRISTO, NAO WATATAWALA PAMOJA NAYE HIYO MIAKA ELFU”

Je umeziona faida za kuwa ndani ya Kristo?.. Tunakuwa makuhani na tena wafalme…

Je! Tayari Umemwamini yeye?.

Kama bado unasubiri nini?..kumbuka tunaishi majira ya kurudi kwa Yesu mara ya pili.

Bwana akubariki.

Shalom..

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618

Mafundisho mengine:

Rudi nyumbani

Print this post

Uadilifu ni nini kibiblia?

Uadilifu ni neno pana linalomaanisha, nidhamu, utu, auminifu, yaani kutenda kile ambacho jamii husika inataka wewe ukitende.

Kibiblia uadilifu ni utiifu katika sheria ya Mungu. Vilevile uaminifu na nidhamu katika mambo yote ya ki-Mungu.  Mtu wa namna hiyo anaitwa mwadilifu, au mcha Mungu.

Kwamfano watu ambao walikuwa waadilifu katika biblia ni kama Yusufu, Ayubu, Danieli pamoja na wengine, ambao waliweza kutembea katika sheria za Mungu bila lawama yoyote.

Baadhi ya vifungu ambavyo utakutana na Neno hilo ni hivi;

2Nyakati 26:3 Uzia alikuwa na umri wa miaka kumi na sita alipoanza kutawala; akatawala huko Yerusalemu miaka hamsini na miwili; na jina la mamaye aliitwa Yekolia wa Yerusalemu.  4 Akafanya yaliyo ya adili machoni pa Bwana, sawasawa na yote aliyoyafanya Amazia babaye

Zaburi 64: 10 “Mwenye haki atamfurahia Bwana na kumkimbilia, Na wote wenye moyo wa adili watajisifu”

Zaburi 112: 2 Wazao wake watakuwa hodari duniani; Kizazi cha wenye adili kitabarikiwa.  3 Nyumbani mwake mna utajiri na mali, Na haki yake yakaa milele.  4 Nuru huwazukia wenye adili gizani; Ana fadhili na huruma na haki

Soma pia 2Nyakati 27:2,29:2 Zaburi 140:13.

Lakini cha kujua kuhusu tabia hii, ni kwamba Bwana Yesu alisema ni wajibu pia wa kila kiongozi wa kiroho/ Mhubiri kufundisha mafundisho ya adili, zaidi ya mafundisho ya utoaji.

Luka 11:42  Lakini, ole wenu, Mafarisayo, kwa kuwa mwatoa zaka za mnanaa na mchicha na kila mboga, na huku mwaacha mambo ya adili, na upendo wa Mungu; iliwapasa kuyafanya hayo ya kwanza, bila kuyaacha hayo ya pili.

Mafundisho ya adili, ni kama vile, utakatifu, uaminifu, haki, utu wema, amani, umoja na kiasi, uvumilivu, fadhili, upole, unyenyekevu. na yote yanayofanana na hayo. Kwasababu ndicho Bwana anataka kukiona ndani ya mioyo ya watu wake, wawe waadilifu kama yeye alivyo mwadilifu (Zaburi 25:8).

Je! Wewe ni mwadilifu? Kumbuka huwezi kuwa hivyo kama upo nje ya Kristo. Yeye ndio pekee anayeweza kukupa nguvu ya kutenda mema. Hivyo ili uitwe mwadilifu sharti kwanza umpokee Yesu akuokoe, akusamehe dhambi zako. Ndipo Bwana akupe nguvu ya kumcha yeye.

Ikiwa upo tayari leo kuokoka, basi fungua hapa kwa mwongozo wa Sala ya Toba. >> KUONGOZWA SALA YA TOBA

Bwana akubariki.

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618

Mafundisho mengine:

IMANI YENYE MATENDO;

NINI TOFAUTI KATI YA MATENDO YA SHERIA NA MATENDO YA IMANI?

JE KUHUDUMU KWA NYIMBO ZA INJILI KUKOJE?

MWIMBIE BWANA ZABURI KATIKA NYAKATI ZA FURAHA.

NYAKATI SABA ZA KANISA NA WAJUMBE WAKE.

Rudi nyumbani

Print this post

Ebenezeri / Ebeneza maana yake ni nini?

Maana ya Neno Ebenezeri ni jiwe la msaada.

Wakati ule Israeli wanamlilia Bwana awarudie, Wafilisti walipata taarifa wakakusanyika pamoja ili wawaangamize, Israeli walivyoona hivyo wakaogopa sana, wakamsihi Samweli awalilie kwa Bwana ili wasaidiwe kwasababu wanakwenda kuangamia. Na Mungu akasikia kilio chao, akawatetea, kwa kutoa ngurumo kubwa sana, zilizowadhoofisha wafilisti, hivyo wakapigwa na kuharibiwa, mpaka miji ambayo wafilisti walikuwa wameiteka ikarudishwa yote kwa Israeli. Ndipo Samweli akachukua jiwe kubwa akalisimamisha Kati ya Mispa na Sheni, akaliita Ebenezeri, akasema hata sasa Bwana ametusaidia.

1Samweli 7:12 Ndipo Samweli akatwaa jiwe, na kulisimamisha kati ya Mispa na Sheni, akaliita jina lake Eben-ezeri, akisema, Hata sasa Bwana ametusaidia.

Lakini la kujiuliza kwanini Samweli anyanyue jiwe, na sio kitu kingine labda nguzo au bendera? Na pia alikuwa na maana gani kusema “Hata sasa Bwana ametusaidia”? Na sio maneno mengine?

JIBU: Alinyanyua jiwe kwasababu alipata ufunuo wa aliyemsaidia, na huyo si mwingine zaidi ya  Kristo ambaye ndio jiwe letu (Warumi 9:33). Alitambua ni yeye ndiye aliyewapigania vita kwa kunguruma, Kwasababu ndiye simba wa Yuda.

Lakini pia kwanini aseme “Hata sasa Bwana ametusaidia” ni kwasababu alitambua kuwa Mungu ni msaada wao sikuzote, hadi ule wakati walioufikia bado alikuwa ni msaada wao, ndio maana akasema “Hata sasa Bwana ametusaidia”, yaani sio tu jana, au zamani bali hata sasa Bwana yupo pamoja nasi.

Ikiwa na maana kuwa hata na sisi tukiwa ndani ya Kristo wakati wote atatulinda,  sio jana tu peke yake, hadi leo na hata kesho. Ni furaha iliyoje kuwekwa chini ya huu mwamba Yesu Kristo?

Je! Kristo ni jiwe lako? Je! Ni Ebenezeri wako? Kama sio, embu mkaribishe leo maishani mwako akuokoe, upate uzima wa milele. Akulinde mbali na Yule mwovu. Ikiwa upo tayari kutubu na kumpokea Yesu basi fungua hapa kwa msaada wa sala ya Toba >>> KUONGOZWA SALA YA TOBA

Bwana akubariki.

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618

Mafundisho mengine:

CHAGUA NI JIWE LIPI LITAKALO KUFAA KWA UJENZI.

BASI, IWENI NA HURUMA, KAMA BABA YENU ALIVYO NA HURUMA

LIONDOE JIWE.

Usimwache rafiki yako mwenyewe, wala rafiki ya baba yako.

Rudi nyumbani

Print this post

Mganda ni nini kama itumikavyo katika biblia?

Neno hili utalisoma katika vifungu kadha wa kadha,

Hivi ni baadhi ya vifungu hivyo ambavyo utakutana nalo;

Mwanzo 37:6 “akawaambia, Tafadhalini, sikieni ndoto hii niliyoiota.  7 Tazama, sisi tulikuwa tukifunga miganda shambani, kumbe! Mganda wangu ukaondoka ukasimama, na tazama, miganda yenu ikazunguka ikainama mbele ya mganda wangu.  8 Ndugu zake wakamwambia, Je! Kweli wewe utatumiliki sisi? Nawe utatutawala sisi? Wakazidi kumchukia kwa ajili ya ndoto yake, na kwa maneno yake”.

Walawi 23: 10 Nena na wana wa Israeli, uwaambie, Hapo mtakapokuwa mmekwisha ingia hiyo nchi niwapayo, na kuyavuna mavuno yake, ndipo mtakapomletea kuhani mganda wa malimbuko ya mavuno yenu;  11 naye atautikisa mganda mbele za Bwana ili kwamba ukubaliwe kwa ajili yenu; siku ya pili baada ya Sabato kuhani atautikisa.  12 Na siku hiyo mtakayoutikisa mganda, mtamsongeza mwana-kondoo wa kiume mkamilifu wa mwaka wa kwanza awe sadaka ya kuteketezwa kwa Bwana.

Tafsiri ya Neno mganda, ni matita ya mazao yoyote yaliyovunwa ambayo yamefungwa pamoja. Kwamfano ngano zilipovunwa, katika mashamba, zilifungwa kwanza katika matita matita, baadaye zikakusanywa zote pamoja, ndipo zikaenda kukobolewa na kusagwa. Sasa hayo matita matita ndio huitwa miganda. (Tazama picha juu)

Kwamfano katika vifungu vifuatavyo utaelewa biblia ilimaanisha nini;

Kumbukumbu 24: 19 Uvunapo mavuno yako katika shamba lako, ukasahau mganda shambani, usirudi kuuchukua; na uwe wa mgeni, au yatima, au mjane; ili Bwana, Mungu wako, akubariki katika kazi yote ya mikono yako.

Maana yake ni kuwa ikitokea, umeenda shambani kuvuna, ukafanikiwa kukusanya miganda kumi, sasa wakati unaondoka ukasahau mmoja, Ilikatazwa kurudi nyuma na kuuchukua, bali uuache kwa ajili ya mayatima na wageni. Kwasababu maskini waliruhusiwa kuingia kwenye mashamba kuokota vile vinavyosalia.

Hii inatufundisha nini?

Wakati mwingine Mungu ataruhusu usichukue kila kitu ulichonacho / ulichokikusanya, ikawa umesahau  fahamu kuwa ni Mungu ametaka, ili wengine wafaidike, usipende kukomba kila kitu, wakati mwingine utajiepusha na Baraka zako. Ukisafiri usiondoke na kabati lote la nguo, ulikuwa unakwenda mahali Fulani umebeba vingi, na kwa bahati mbaya ukakisahau kimoja, usiwe mwepesi kukirudia  kukichukua, hujui ni kwanini Mungu amekusahaulisha.

Wewe ni boss, umeona, vichenji vimebaki, si lazima uvikombe vyote, waachie waajiriwa wako. Itakuwa ni Baraka kwako.

Lakini pia ni kutuelekeza mioyo yetu imtegemee yeye zaidi ya miganda yetu. Utakumbuka mitume wa Kristo, walipofanyiwa miujiza ya mikate, wakaagizwa wakusanye vipande, kisipotee hata kimoja, lakini baadaye walipoondoka, wakakumbuka wamesahau,wakaanza kulalamikiana wao kwa wao watakula nini. Lakini Yesu akawaambia mmesahau miujiza Mungu aliyowafanyia kama hiyo? Mna wasiwasi gani? Mungu anaweza kuwapa na vingine.

Mathayo 16:5  Nao wanafunzi wakaenda hata ng’ambo, wakasahau kuchukua mikate. 6  Yesu akawaambia, Angalieni, jilindeni na chachu ya Mafarisayo na Masadukayo. 7  Wakabishana wao kwa wao, wakisema, Ni kwa sababu hatukuchukua mikate. 8  Naye Yesu akafahamu, akawaambia, Mbona mnabishana ninyi kwa ninyi, enyi wa imani chache, kwa sababu hamna mikate? 9  Hamjafahamu bado, wala hamkumbuki ile mikate mitano kwa wale elfu tano, na vikapu vingapi mlivyoviokota?

Hivyo na sisi pia tusiwe na tabia ya kubeba miganda yote.

Bwana akubariki.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618

Mafundisho mengine:

Mofa ni nini? na inafunua nini kiroho?(1Samweli 28:24).

Mashonde ni nini? (Ezekieli 4:15).

YEYE ATAWABATIZA KWA ROHO MTAKATIFU NA KWA MOTO.

TUYATENDE MAMBO YOTE KWA UZURI NA UTARATIBU.

VIACHENI VYOTE VIKUE HATA WAKATI WA MAVUNO.

Rudi nyumbani

Print this post