Category Archive Mafundisho

IHUBIRI INJILI, KILA MAHALI KWASABABU AKUZAYE NI MUNGU.

Jina la Mwokozi wetu YESU KRISTO libarikiwe.

Agizo la Bwana Kuhusu Kuitangaza Injili (Mathayo 28:18-20)

Upo umuhimu wa kuhubiri injili mahali popote na katika mazingira yoyote kwasababu ni agizo la Bwana mwenyewe. Wapo wanaoamini kuwa injili ya mitaani na masokoni hazina faida yoyote kwasababu watu wanakuwa hawapo katika utulivu. Na pia wapo wanaoamini kuwa injili za kwenye mikutano au makanisani ndizo zilizo bora.

Lakini nataka nikuambie: Injili zote zina umuhimu. Za watu walio katika utulivu na utayari wa kusikiliza, na hata za wale ambao hawako tayari kabisa.


Biblia Inasema Je Kuhusu Kuwafikia Wote?

Mitume wa Bwana Yesu:

“Basi katika sinagogi akahojiana na Wayahudi na waliomcha Mungu, na wale waliokutana naye sokoni kila siku.”
(Matendo 17:17)

Yesu Mwenyewe:

“Ikawa baada ya hayo alikuwa akizunguka-zunguka katika miji na vijiji akihubiri na kuitangaza habari njema ya ufalme wa Mungu…”
(Luka 8:1)


Umuhimu wa Injili ya Mitaani kwa Wasio Tayari Kusikia

Kikawaida ni ngumu kumsimamisha mtu barabarani na kumwambia asikilize. Lakini unapohubiri bila hata ridhaa yake, Neno linaweza kuingia ndani yake hata kama hataki. Lile Neno linaweza kuwa mbegu njema itakayochipuka kwa wakati wake.

Kwahiyo ni heri asikie moja kuliko kutokusikia kabisa. Wengine hawaendi kanisani, wengine ni wa imani tofauti, wengine wamejitosheleza – lakini kwa kuhubiri, unawafikia.


Kundi Linalosaidika kwa Kusikia kwa Lazima

“Nawe utawaambia maneno yangu, kwamba watasikia, au kwamba hawataki kusikia; maana hao wanaasi sana”
(Ezekieli 2:7)

Hata kama ni mara ya mia, huenda Neno moja tu likamgusa. Au wewe ndiye umeanza safari ya wokovu ndani yake ambayo itakamilika baadaye.


Wengi Hawakoki Mara Moja – Ni Safari

Wapo wanaohitaji kusikia mara nyingi. Ndio maana Bwana alituma manabii kupiga kelele:

“Piga kelele, usiache, Paza sauti yako kama tarumbeta…”
(Isaya 58:1)

Kazi ya kuhubiri si nyepesi. Lakini matokeo yake ni makubwa sana:

“Kuna furaha mbele ya malaika wa Mungu kwa ajili ya mwenye dhambi mmoja atubuye”
(Luka 15:10)


Je! UMEOKOKA???

Pengine umesikia injili mara nyingi lakini bado hutaki kubadilika. Injili ya kurudia rudia si tangazo, ni ushuhuda dhidi yako.

“Tena habari njema ya ufalme itahubiriwa katika ulimwengu wote, kuwa ushuhuda kwa mataifa yote; hapo ndipo ule mwisho utakapokuja”
(Mathayo 24:14)

“Katika siku ile Mungu atakapozihukumu siri za wanadamu, sawasawa na injili yangu, kwa Kristo Yesu”
(Warumi 2:16)


Bwana Atusaidie

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea.

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, basi wasiliana nasi:

📞 +255789001312
📞 +255693036618

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya hapa:
👉 https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Mafundisho mengine:

IMANI NI NINI?

Je! Watu ambao hawajawahi kusikia injili kabisa siku ya mwisho watahukumiwa?

TUSIWE WAVIVU WA KUSIKIA.

INJILI YA MILELE NI IPI KATIKA BIBLIA?

KWANINI KILA MWAMINI ANAPASWA AWE MHUBIRI WA INJILI

Rudi Nyumbani

Print this post

VIGEZO VYA NEEMA YA MUNGU.

Tangu mwanzo mwanadamu alikuwa akijaribu kujiokoa kwa njia yake mwenyewe ikiwemo kuonyesha matendo yake mazuri, na mwenendo wake mkamilifu lakini hakuweza. Pengine aliweza kushinda wizi kikamilifu lakini uongo ukamshinda, aliweza kushinda uzinzi wote, lakini tamaa zikamtawala, aliweza kushinda ibada za sanamu na vinyago, lakini kusamehe kukamshinda. Alipoweza kushinda kimoja, nyuma yake kulikuwa na elfu vinavyo mhukumu.

 

Na hiyo ilimfanya asikidhi vigezo vya kuingia mbinguni, kwasababu watakaoiona mbingu na Mungu ni watakatifu asilimia mia wasio na doa lolote. Ndio maana maandiko yanasema wote wameoza,wamepotoka hakuna amtafutaye Mungu. Bali tunahesabiwa haki bure kwa neema ya Bwana Yesu Kristo.

 

Warumi 3:11  Hakuna afahamuye; Hakuna amtafutaye Mungu. 12  Wote wamepotoka, wameoza wote pia; Hakuna mtenda mema, la! Hata mmoja.

 

Ndio sababu ya Yesu kuja duniani, ili kwa kupitia kumwamini yeye tuipokee hiyo neema ya kuitwa watakatifu, bila kuonyesha kwanza kipimo chochote kwa Mungu. 

Maana yake ni kuwa mimi na wewe tunapomwamini Yesu Kristo, ni moja kwa moja tunaitwa watakatifu, tuliosamehewa dhambi zetu, na kuondolewa pia. 

 

Ikiwa umemwamini leo Yesu Kristo, moja kwa moja Mungu hakuhesabii tena dhambi yoyote kama mkosaji. Ijapokuwa utakuwa hujakamilika bado.  Hii ndio maana ya neema, yaani kukubaliwa kusikostahili. Ilikupasa kwanza uwe na matendo makamilifu asilimia 100 kama Bwana Yesu, ndio uitwe mtakatifu uliyestahili kumwona Mungu. Lakini sasa kwa kuupokea ukombozi wa Yesu Kristo, dhambi zako, zimefuta unaitwa mtakatifu, kabla hata ya ukamilifu wa utakatifu wenyewe kukufikia. Ndio maana sisi tulio ndani ya Kristo hatuna budi kuwa na amani, na furaha wakati wote. Kwasababu ule mzigo mzito wa kujitahidi sisi wenyewe kuingia mbinguni umeondolewa na Yesu Kristo Bwana wetu, kwa kifo chake pale msalabani.

 

 

Lakini sasa, katika nyakati hizi za mwisho suala hili la neema limetafsirika vibaya, kama tu nyakati zile za zamani, na hapo yatupasa  tuwe makini sana. Ni sawa na taifa litangaze neema kwa nchi yake na kusema, sasa huduma zote za maji ni bure, hakuna kulipia bili,matumizi ni kama unavyotaka. halafu uone watu wanatumia fursa hiyo kwenda kufungulia  mabomba yatiririshe maji kwenye mitaro na mabarabarani, kila mahali kuwe ni maji tu,  Bila shaka utasema hawa watu wamerukwa na akili, hawana sifa ya kupewa huduma hiyo tena.

 

Ndivyo ilivyo kwa jambo linaloitwa neema, tusijipojua kanuni zake, tutajikuta badala ya kupokea wokovu, tunapokea maangamizi. Badala ya kukazana kumpendeza Mungu, tunastarehe katika dhambi,  Na ndicho kinachoendelea sasa kwa sehemu kubwa miongoni watu na madhehebu.

 

Yafuatayo ni mambo ambayo ujiepushe nayo kwa nguvu zote, wewe uliyeipokea neema ya Mungu.

 

  1. Kuipokea neema bure,

2 Wakorintho 6:1

[1]Nasi tukitenda kazi pamoja naye twawasihi msiipokee neema ya Mungu bure.

Ukisoma vifungu vichache vya nyuma anasema mtu akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya, ya kale yamepita tazama yamekuwa mapya.

 

Mtu ambaye hataki geuko, baada ya kusamehewa dhambi zake, huyo ni mtu ambaye ameipokea neema bure, haithamini, ameitwa mtakatifu, halafu hataki kuishi maisha matakatifu, anaendelea na maisha yake yale yale ya kale.. Mtu kama huyo asijidanganye neema hiyo ni batili. Mtu yeyote aliyeokoka  wakati huo huo una wajibu wa kuanza kupiga hatua za mabadiliko, na unapaswa uithamini sana hiyo zaidi ya vyote, kwasababu ni Mungu ndiye akutakasaye baada ya hapo.

 

Lakini pia mtu ambaye amekaa muda mrefu hamzalii Mungu matunda, anahesabika kama aliyeipokea neema ya Mungu bure, na hivyo mwisho wake unakuwa ni kukatwa.

 

Tito 2:11  Maana neema ya Mungu iwaokoayo wanadamu wote imefunuliwa;12  nayo yatufundisha kukataa ubaya na tamaa za kidunia; tupate kuishi kwa kiasi, na haki, na utauwa, katika ulimwengu huu wa sasa; 

 

Je! Umeitii neema hii inayokufundisha kukataa machafu ya duniani?. Leo yapo madhehebu yanayosema, ukiokoka umekoka milele, kazi yako imeisha, hata usipoonyesha  bidii nyingine yoyote kwa Mungu,huwezi potea. Ndugu yangu kuwa makini sana na imani hizi. Neema haipokelewi bure.

 

  1. Kuipungukia Neema

Epuke pia  kuipungukia neema.

 

Waebrania 12:15-17

[15]mkiangalia sana mtu asiipungukie neema ya Mungu; shina la uchungu lisije likachipuka na kuwasumbua, na watu wengi wakatiwa unajisi kwa hilo. 

[16]Asiwepo mwasherati wala asiyemcha Mungu, kama Esau, aliyeuuza urithi wake wa mzaliwa wa kwanza kwa ajili ya chakula kimoja. 

[17]Maana mwajua ya kuwa hata alipotaka baadaye kuirithi baraka, alikataliwa (maana hakuona nafasi ya kutubu), ijapokuwa aliitafuta sana kwa machozi.

Kuipungukie neema Ni tabia ya kuishusha thamani neema, na kuilazimisha  itende kazi hata katika kiwango ambacho si chake.

 

Hii hasa huja kwa watu ambao wanazoelea kufanya dhambi mara kwa mara wakiamini kuwa kwasababu Mungu hawahesabii makosa basi hata wakifanya kosa lolote hawawezi kupotea.

Ndugu, neema si kuhalalisha maisha ya dhambi. 

Biblia inasema..

Warumi 6:1  Tuseme nini basi? Tudumu katika dhambi ili neema izidi kuwa nyingi? 2  Hasha! Sisi tulioifia dhambi tutaishije tena katika dhambi?

3  Hamfahamu ya kuwa sisi sote tuliobatizwa katika Kristo Yesu tulibatizwa katika mauti yake?

4  Basi tulizikwa pamoja naye kwa njia ya ubatizo katika mauti yake, kusudi kama Kristo alivyofufuka katika wafu kwa njia ya utukufu wa Baba, vivyo hivyo na sisi tuenende katika upya wa uzima.

Usitende dhambi za mazoelea, ukadhani neema itakuwa sikuzote kukufunika. Ukiifanyia jeuri neema, itaondoka kwako.

 

Waebrania 6:4  Kwa maana hao waliokwisha kupewa nuru, na kukionja kipawa cha mbinguni, na kufanywa washirika wa Roho Mtakatifu,

5  na kulionja neno zuri la Mungu, na nguvu za zamani zijazo, 6  wakaanguka baada ya hayo, haiwezekani kuwafanya upya tena hata wakatubu; kwa kuwa wamsulibisha Mwana wa Mungu mara ya pili kwa nafsi zao, na kumfedhehi kwa dhahiri.

 

  1. Kuibadili neema ya Mungu.

 

Yuda 1:4  Kwa maana kuna watu waliojiingiza kwa siri, watu walioandikiwa tangu zamani hukumu hii, makafiri, wabadilio neema ya Mungu wetu kuwa ufisadi, nao humkana yeye aliye peke yake Mola, na Bwana wetu Yesu Kristo.

 

Neema ya Mungu inaweza badilishwa ikamaanishwa kivingine kabisa. Kwamfano utaona leo hata mashoga, wanavyama vyao wakisema sisi tupo chini ya neema. Walevi nao, wenye dhambi nao wanasema neema ya Yesu ipo duniani sasa, kumwokoa kila mtu.

 

Hivyo watakuambia maneno kama usihukumu usije ukahukumiwa. Na wana amani na ujasiri katika hayo wanayoyafanya na wengine wanajiita maaskofu na wachungaji, wakihalalisha kila kitu kiovu kufanyika kwa kivuli cha neema.

 

Hao ndio waibadilishao neema ya Bwana Yesu kuwa ufisadi, hilo Neno ufisadi ni zaidi ya uasherati, Ni pamoja na matendo yote maovu kupita kiasi. Lakini neema ya Yesu,.haikuja kufunuki dhambi, bali ilikuja kuondoa dhambi ndani ya mtu. Usiwe mmojawapo aibadilishaye neema ya Mungu.

 

Hivyo kwa vifungu hivyo itoshe kusema kuwa NEEMA tunaipokea bure, lakini ili iweze kufanya kazi lazima tujue sifa zake,  kisha tuzikubali, vinginevyo tutajidanganya na kuangamia.  Ni sawa na mtu akupe gari bure, lakini usipoliweka mafuta, na kujua kuliendesha linakuwa halina tofauti na mdoli wa gari.

Lakini ukiithamini neema, itakutunza, itakuhifadhi na kuyaficha makosa yako yote, Hivyo utaendelea kuonekana mkamilifu asilimia mia mbele za Mungu, na hata ukifa, ni moja kwa moja mbinguni.

Shalom.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

JINSI YA KUITUMIA VYEMA NEEMA YA MUNGU ILIYO JUU YANGU.

MANENO YA MUNGU YANAPINDULIWAJE?

JINSI MWISHO ULIVYOKARIBIA.

Print this post

IFUATE KANUNI SAHIHI YA MUNGU

Zipo kanuni za ki-Mungu tunaweza kuzifuata na zikaleta matokeo kabisa halisi, lakini zisiwe na manufaa kwetu katika suala la wokovu.  Sasa kabla ya kuangalia ni kwa namna gani? 

chukulia mfano wa kawaida.

Mwanamke yeyote anaweza kubeba ujauzito katika mazingira mbalimbali, kwamfano anaweza akatwezwa nguvu (akabakwa), na akapata ujauzito, lakini pia anaweza kwenda kujiuza kama kahaba na bado akapata ujauzito, vilevile anaweza akasubiri aolewe kwanza katika ndoa halali ndipo apokee ujauzito na likafanikiwa vilevile tu, kuleta kiumbe duniani, kama angefanya hayo kabla ya ndoa, au atokapo nje ya ndoa yake.

Sasa unaweza jiuliza, katika njia zote hizo ambazo angepata ujauzito ni ipi iliyo halali inayokubalika mbele za Mungu na wanadamu. Bila shaka ni hiyo njia ya mwisho ambayo ni ya kuolewa kwanza, ndipo apokee ujauzito kutoka kwa mume wake mmoja wa halali. Na ndio mtoto huyo hujulikana kama halali sio haramu.

Lakini cha ajabu ni kuwa ijapokuwa njia halali ipo lakini feki pia huleta matokeo yaleyale mfano wa halali. Kwasababu gani? Kwasababu kanuni ya kupata mtoto, si kanuni ya uhalali. Hivyo ni vitu viwili tofauti, 

Hata Ibrahimu, alikuwa na watoto wengi, alitangulia Ishmaeli, kisha baadaye wakazaliwa na watoto wengine sita kwa suria mwingine, mbali na Isaka. Wote walikuwa wanadamu, viumbe wa Mungu, wenye akili na nguvu na baraka, wasio na hatia. Lakini lilipokuja suala la urithi, ndipo kubaguliwa  kulipokuja, Watoto wote wa masuria walifukuzwa wakapewa zawadi tu bali Isaka alipewa vyote.

Mwanzo 25:5-6

[5]Ibrahimu akampa Isaka yote aliyokuwa nayo. 

[6]Lakini wana wa masuria aliokuwa nao Ibrahimu, Ibrahimu akawapa zawadi, naye akawaondoa katika mahali alipokaa Isaka mwanawe, wakati wa uhai wake, waende pande za mashariki, mpaka nchi ya Kedemu. 

Hii ni kutufundisha nini hasaa katika maisha yetu ya wokovu.

Zipo kanuni nyingi sana za kiroho ambazo mtu yeyote, hata ambaye  hajamwamini Yesu anaweza zitumia na zikatoa matokeo yaleyale sawa tu na mtu ambaye ameokoka.

Kwamfano, kufanya miujuza na ishara kwa jina la Yesu. Watu hawajui kuwa jambo hili huhitaji imani tu, katika jina lake. Hivyo wale wafikiao kiwango hicho haijalishi ni mwizi, ni mpagani, anaweza pokea muujiza na akafanya pia muujiza sawa tu na yule aliyeokoka.

Kwasababu gani? kwasababu amefanikiwa kufuata kanuni ambayo ni Imani.

Akijua lile neno linalosema  ‘yote yawezekana kwake yeye aaminiye’’ (Marko 9:23). Ndio maana walikuwepo watu wengi wasiokuwa wayahudi kipindi kile cha Yesu walipokea miujiza mikubwa, zaidi ya wayahudi kwasababu tu ya ukubwa wa imani zao. Na sio haki zao.

Vivyo hivyo hata katika kuomba. Mtu yeyote aombaye hupokea. Ni kanuni ya asili ya rohoni, haijalishi ni nani.

Mathayo 7:8

[8]kwa maana kila aombaye hupokea; naye atafutaye huona; naye abishaye atafunguliwa. 

Watu hawajui hata kufanikiwa kwa shetani hutegemea maombi, na yeye pia huenda mbele za Mungu kuomba na hupewa..hajiamulii tu mambo yake ovyo ovyo bila idhini ya Mungu, kwasababu hii dunia si yake… utauliza kwa namna gani, ? unamkumbuka shetani kipindi cha Ayubu, yeye naye alikwenda kujihudhurisha mbele za Mungu, ndipo akaleta uharibifu. Akapeka haja zake akasikiwa, dua zake na magoti yake.

Ayubu 1:6

[6]Ilikuwa, siku moja ambayo hao wana wa Mungu walikwenda kujihudhurisha mbele za BWANA, Shetani naye akaenda kati yao. 

Watu wengi wanapoona wanamwomba Mungu wanajibiwa wanadhani, ndio wamekubaliwa na Mungu. Kumbe unaweza kuomba kama mwana-haramu usiyekuwa na urithi wa uzima wa milele, bali haki ya kupokea tu unachokiomba.

Unaweza ukafanya miujiza kama mwana-haramu. Lakini usiende mbinguni.

Mathayo 7:22-23

[22]Wengi wataniambia siku ile, Bwana, Bwana, hatukufanya unabii kwa jina lako, na kwa jina lako kutoa pepo, na kwa jina lako kufanya miujiza mingi? 

[23]Ndipo nitawaambia dhahiri, Sikuwajua ninyi kamwe; ondokeni kwangu, ninyi mtendao maovu. 

 Unaweza ukamwamini Yesu, na kumuhofu,  lakini ukaamini kama mashetani.

Yakobo 2:19

[19]Wewe waamini ya kuwa Mungu ni mmoja; watenda vema. Mashetani nao waamini na kutetemeka. 

unaweza ukawavuta watu kwa Kristo na wakaokoka, lakini ukawa mtu wa kukataliwa kama tu Paulo alivyosema katika; 

1 Wakorintho 9:27

[27]bali nautesa mwili wangu na kuutumikisha; isiwe, nikiisha kuwahubiri wengine, mwenyewe niwe mtu wa kukataliwa. 

Sasa kanuni sahihi ya Mungu ni ipi ili tuonekane kamili na halali?

Kanuni Mungu anayoitazama kwetu ni Wokovu uliokamilishwa kwa matendo yake.

Angalia mwishoni pale kwenye Mathayo 7:23 Bwana Yesu alichokisema;

“ondokeni kwangu, ninyi mtendao maovu”

Umeona je unaishi maisha gani?. hicho ndio kipimo cha ki-Mungu, 

Alisema pia.

Yakobo 2:24

[24]Mwaona kwamba mwanadamu huhesabiwa kuwa ana haki kwa matendo yake; si kwa imani peke yake. 

Hakikisha maisha yako yanaendana na ukiri wako, wa imani yako, usiishi tu kama mtu ambaye hajaamini ukijitumainisha, kuona maombi yako yanajibiwa, karama yako inafanya kazi, imani yako inatenda kazi..hizo ni kanuni za kupokea lakini sio kanuni za uhalali wa kuurithi uzima wa milele. Ishi kama mtu ampendezaye Bwana wake kimwenendo, ndipo hayo mengine yakifuata huna hasara.

Nyakati hizi za mwisho, adui anaweka uzito kwenye mioyo ya watu wasipende kutafuta maisha matakatifu, kinyume chake wabakie tu kwenye miujiza, uponyaji, utabiri…Siku ile hivyo vitu havitafuata na wewe ndugu, bali matendo yako.

Ufunuo wa Yohana 14:13

[13]Nikasikia sauti kutoka mbinguni ikisema, Andika, Heri wafu wafao katika Bwana tangu sasa. Naam, asema Roho, wapate kupumzika baada ya taabu zao; kwa kuwa matendo yao yafuatana nao. 

Tuanze sasa kujipima mienendo yetu. Kisha tutumie nguvu nyingi hapo kujirekebisha, sawasawa na imani tuliyoipokea, ili tuwe wana halali waliozaliwa kweli ndani ya Kristo, watakaorithi uzima wa milele.

Wokovu wa kweli hufunuliwa kwa mwenendo mzuri. Tuitazame sana kanuni hii.

Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >>

https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

KANUNI JUU YA KANUNI.

KANUNI YA KUOMBA NA KUPOKEA.

JE NI HALALI KUOA WAKE WENGI AU KUTOA TALAKA?

Print this post

Biblia inasema nini kuhusu mtu ‘Mwenye kujipendekeza (Mithali 29:5)

SWALI: Naomba kufahamu ujumbe ulio katika Mithali 29:5

‘Mwenye kujipendekeza kwa jirani yake, Hutandika wavu ili kuitega miguu yake’.

JIBU: Mithali hii inazungumzia madhara yanayoibuka katika tabia ya kujipendekeza.

Kujipendekeza ni kitendo cha mtu kumthaminisha mtu, hata kama alikuwa hastahili sifa hizo, ili tu upate kitu Fulani kutoka kwake. Kumthaminisha kunaweza kuwa kumsifia, au kumpongeza, au kumzungumzia mema yake kupita kiasi, au kueleza mabaya ya wengine kwa huyo mtu, n.k.

 Na yote hayo hayawi kwa lengo la kuuthamini kweli uzuri wa Yule mtu, hapana bali  ni aidha upate kupendwa wewe zaidi ya wengine, au usaidiwe, au upewe cheo,  au kipaumbele Fulani. Hata kama utaona mabaya yake huwezi kumwambia kwasababu, huna lengo la kusaidia bali upate matakwa yako tu.

Sasa  hilo ni kosa, matokeo ya hilo biblia inatuambia “unamtandikia wavu ili kuitega miguu yake”. Yaana unampeleka kwenye mtego au aungamivu wake kabisa.  Hii ni kweli, tunaona hata viongozi wengi wa nchi wameponzwa na wasaidizi wao wa karibu,na matokeo yake wakaiharibu  nchi, kwasababu tu ya kupokea sifa za uongo kutoka kwao, kwamba wanafanya vema, wanawajibiki vizuri n.k..  Kama ilivyokuwa kipindi kile cha Mfalme Sedekia na wale manabii wa uongo wajipendekezao, walimtabiria uongo, lakini Yeremia alimweleza mfalme ukweli  hawakutaka kumsikiliza. Matokeo yake Mfalme Sedekia akaingia katika matatizo makubwa ya kutobolewa macho na kupelekwa utumwani, hiyo yote ni kwasababu alikaa na manabii wajipendekezao (Yeremia 34-41), kama tu ilivyokuwa Kwa Mfalme Ahabu naye na manabii wake mia nne wa uongo.

Hii ni kutufundisha nini?

Hasaa biblia hailengi, tuwe makini na watu wajipendekezao. Hapana, kwasababu wakati mwingine si rahisi kuwatambua, inahitaji neema ya Mungu. Lakini inalenga hasaa katika upande wetu , kwamba sisi tujiepushe na ‘tabia ya kujipendekeza”. Kwasababu tunaweza kudhani tunatafuta faidi yetu tu wenyewe, lakini kumbe tunamsababishia madhara Yule mtu ambaye tunajipendekeza kwake. Tunategea wavu mbaya sana, aanguke na kupotea kabisa, na huo si upendo.

Itakusaidia nini akutendee mema, halafu yeye aangamie?

Hivyo, pastahilipo kweli kusifia tusifie, lakini si kwa lengo la kujipendekeza, kwasababu tukienda huko, tunatenda dhambi kubwa zaidi. Hiyo ndio maana ya hivyo vifungu, tufikiriapo kujipendekeza, tuone kwamba ni watu wasio na hatia tunawategea wavu waangamie.

Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >>https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

TUZIJARIBU HIZI ROHO.

UNAWAFAHAMU MANABII WA UONGO?

USIJISIFIE KARAMA KWA UONGO.

Rudi Nyumbani

Print this post

KWA KUWA FURAHA YA BWANA NI NGUVU ZENU. 

Nehemia 8:10

[10]Kisha akawaambia, Enendeni zenu, mle kilichonona, na kunywa kilicho kitamu, tena mpelekeeni sehemu yeye asiyewekewa kitu; maana siku hii ni takatifu kwa BWANA wetu; wala msihuzunike; KWA KUWA FURAHA YA BWANA NI NGUVU ZENU.

Ni habari ya kutafakarisha, lakini zaidi sana ya kuwafariji watu wote wampendao Mungu. Tukisoma katika biblia ile habari ya Ezra na Nehemia, katika juhudi zao wa kuwarejesha Israeli katika ibada na njia za Mungu Yerusalemu.

Tunaona wakati ule ukuta wa Yerusalemu ulipomalizwa kujengwa baada ya kurudi kwao utumwani Babeli, Ezra hakuwaacha tu hivi hivi, wafurahie kukamilika kwa majengo, bali alitaka wakamilishwe na mioyo yao hivyo, alikichukua kitabu cha Torati na kuanza kuwasomea wayahudi wote tangu asubuhi mpaka adhuhiri, ili wajue ni nini Bwana anataka kwao (Nehemia 8).

Na waliposikia waliona makosa yao mengi sana, na hukumu nyingi za Mungu, alizowatamkia kufuatana na makosa yao, yaliyowapelekea mpaka wakachukuliwa mateka. Ikumbukwe kuwa kitabu hicho cha torati hakikuwahi kusomwa tangu zamani walipochukuliwa utumwani, ndio ilikuwa mara yao ya kwanza kukisoma baada ya miaka mingi kupita.

Hivyo wayahudi kusikia vile wakaanza kulia sana na kujuta na kuomboleza. Lakini tunaona kuna jambo lilifanyika la kitofauti.

Nehemia, alitambua wazo la Mungu…Hivyo akawazuia watu kulia na kuomboleza kwa ajili ya makosa yao. Kinyume chake akawaambia leo ni siku takatifu kwa Bwana, hivyo mle ,.mnywe, mtoe sadaka, mfurahi mbele za Mungu wenu kwasababu “furaha ya BWANA ni nguvu zenu” 

Hivyo watu wakasheherekea, badala ya kulia, Sio kwamba Nehemia alisheherekea makosa yao, hapana, bali alipewa kujua kwamba  furaha ya mtu kwa Mungu wake, ndio chanzo cha nguvu ya kumtumikia yeye. 

Ndio hapo baada ya wayahudi kujua makosa yaowakimfurahia Mungu, siku hiyo, na wakapokea nguvu nyingi za kuishika sheria ya Mungu. 

Yaani kwa namna nyingine, Mungu kuwakemea makosa yao,lengo lake lilikuwa sio awahukumu, au wainamishe vichwa vyao wakidhani kuwa wao ni kichefu-chefu kwake. Hapana..Bali anawapenda na hivyo anatarajia wajue nia ya makemeo yake.

Nehemia 8:10 Kisha akawaambia, Enendeni zenu, mle kilichonona, na kunywa kilicho kitamu, tena mpelekeeni sehemu yeye asiyewekewa kitu; maana siku hii ni takatifu kwa Bwana wetu; wala msihuzunike; kwa kuwa furaha ya Bwana ni nguvu zenu.

11 Hivyo Walawi wakawatuliza watu wote, wakasema, Nyamazeni, kwa maana siku hii ni takatifu; wala msihuzunike. 

12 Na watu wote wakaenda zao kula na kunywa, na kuwapelekea watu sehemu, na kufanya furaha nyingi, kwa sababu walikuwa wameyafahamu maneno yale waliyohubiriwa

 

Ni hata sasa, unaposoma biblia na kuona inakushitaki, inakuambia usiibe, usisengenye, amchukiaye ndugu yake ni sawa na muuaji, wazinzi wote sehemu yao ni katika lile ziwa la moto, inapokukemea maovu yako ya siri.. Usiinamishe kichwa na kusema “mimi sifahi mbele za Mungu, mimi ni mkosefu sistahili kuitwa mwana wake”..Ukaacha kukisoma kabisa, ukawa unalia tu, umenyong’onyea, na kujihisi wewe ni wajehanamu tu, Mungu hakupendi, ameshakuacha, ona sasa unamkosea kosea kila siku… Fahamu kuwa hilo sio kusudi la Mungu.

Kusudi la Mungu sio usome biblia, ujawe na hisia za Mungu kukuhukumu, au kukulaumu, au kukushitaki, bali kusudi la Mungu ni ujue  upendo wake uliozidi sana kwako, kiasi cha yeye kuonyesha hisia zake kwako namna ambavyo unapaswa uwe kama yeye.

Hivyo ukitoka kuonywa na kukemewa, unapaswa utoke kwa kufurahi moyoni  na kuruka-ruka, na hapo ndipo utapokea nguvu ya kuishinda hiyo dhambi. Lakini ukitoka kinyonge na mashaka utashindwa kwasababu furaha ya Bwana ndio chanzo cha nguvu zetu. Ukilipenda hilo katazo, utalitenda, usipolipenda kamwe huwezi litenda.

Mtunga Zaburi alisema,

Zaburi 119:52

[52]Nimezikumbuka hukumu zako za kale, Ee BWANA, nikajifariji.

Bwana anataka tuone upendo wake kwetu katika makemeo yake, tufarijike tupokee nguvu ya kushinda. Pengine umetoka kufanya dhambi fulani ya makusudi na Roho Mtakatifu akakumbusha kuwa watu wa namna hii, huangukia katika mtego mbaya wa shetani bila kunasuka, Sasa hapo usianze kupoteza ladha na Mungu wako, au biblia, ukauchukia wokovu, kabisa,  maanisha kutubu, jifunze kutokana na makosa, kisha furahia mwambie Bwana asante kwa kunipenda,

hata wachezaji wa mpira, wafungwao kipindi cha kwanza, wanapotulia na kujihamasisha tena, hupokea nguvu ya kucheza vema kipindi cha pili, lakini wajilaumupo, hufanya vibaya zaidi

Na sisi pia tuiamshe furaha ya Bwana daima.Kila tusomapo Neno lake, tufurahi kwasababu ni barua ya upendo wa Mungu kwetu Ili tuweze kuwa na nguvu.

Kwasababu furaha ya Bwana ndio nguvu yetu.

Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

SHUKURU KWA KILA JAMBO.

Furaha ni nini?

Fahamu maana 1Wakorintho 14:20  “Ndugu zangu msiwe watoto katika akili zenu;

 

Print this post

USI..USI..USI.

Usi!.. Usi!.. Usi! na sio Msi!… Msi!.. Msi!..

Amri za Mungu zinasema Usiue, Usizini, Usiibe … na sio Msiibe, Msiue, Msizini… Ikifunua kuwa Mungu anaongea na mtu mmoja mmoja… Anasema na Mimi kivyangu, lakini pia anasema na wewe kivyako… Na hatuambii wote kwa pamoja.

Kutoka 20:13 “Usiue. 

14 Usizini. 

15 Usiibe. 

16 Usimshuhudie jirani yako uongo. 

17 Usiitamani nyumba ya jirani yako…”

Siku ya Hukumu, hatutahukumiwa kwa pamoja, kila mtu atasimama peke yake, na kila mtu atalichukua furushi lake mwenyewe..

Wagalatia 6:5 “Maana kila mtu atalichukua furushi lake mwenyewe”.

Na tena kila mtu atatoa habari zake mwenyewe na si pamoja na mwenzake..

Warumi 14:12 “Basi ni hivyo, kila mtu miongoni mwetu atatoa habari zake mwenyewe mbele za Mungu”

Sasa kama ni hivyo kwanini Boss wako akukoseshe?..kwanini Rafiki akukoseshe, kwanini wanadamu wakukoseshe??… Na ilihali utasimama peke yako siku ile.

Kumbuka unapofanya uzinzi, siku ile hutakuwa na yule aliyefanya naye uzinzi, badala yake utasimama wewe kama wewe (kwasababu ile amri  inakuhusu wewe, na Mungu alikuwa anazungumza na wewe kivyako na si wewe pamoja na mwenzako)..

Kama unaiba, siku ile hutasimama na aliyekushawishi ukaibe, au uliyekuwa unashirikiana naye katika wizi.. wewe utakuwa peke yako, na yeye peke yake….kwasababu Amri ya Usiibe, uliambiwa wewe, nimeambiwa mimi na si wewe pamoja na mimi… Hivyo kila mtu atatoa habari zake mwenyewe.

Kama unaua, ni hivyo hivyo, kama uwaheshimu wazazi ni hivyo hivyo, na amri zote ni hivyo hivyo..

Hukumu ya Mungu inatisha!.

Bwana atusaidie.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

Je! sisi kama watakatifu tunaowezo wa kuamuru hukumu?

WATAMTAZAMA YEYE AMBAYE WALIMCHOMA; NAO WATAMWOMBOLEZEA.

NI WAKATI GANI SHETANI ANAPENDA KUMSHAMBULIA MWAMINI?

Kwa maana yule mume asiyeamini hutakaswa katika mkewe;

CHUKUA MZIGO WA MWINGINE.

Rudi Nyumbani

Print this post

KUWA MAKINI NA MATANGO MWITU, SIKU HIZI NI ZA MWISHO!

Kuna wakati Elisha alifika Gilgali na mahali pale palikuwa na njaa kali, na watu wengi (manabii) pia walikuwa  wamekusanyika kusikiliza mashauri ya mtu wa Mungu.

Hivyo akawaambia waweke sufuria motoni waandae chakula.

Lakini mmojawao akatoka akaenda mashambani kutafuta mboga. Na huko akafanikiwa kweli kukusanya zilizo bora, lakini kwasababu hakuwa na maarifa ya kutosha jinsi ya kutambua mboga sahihi ziwafaazo wanadamu akaona huko matango mwitu, na bila kujua, akidhani ni matango halisi, akayachuma na kuyaleta sufuriani. Matango yale yalikuwa ni sumu.

Lakini walipoonja kwa neema za Mungu walijua kuna kitu ambacho sio sahihi kimewekwa sufuriani, hivyo waacha wote kula. Ndipo Elisha akataarifiwa, juu ya jambo hilo, kama kimwagwe lakini kile chakula hakikumwagwa, bali aliwaagiza watie unga mule (kwa Neno la Bwana), na chakula kitaponyeka.  Wakafanya hivyo, kikawa sawa, wakala wakashiba.

2 Wafalme 4:38-41

[38]Elisha akafika Gilgali tena; na kulikuwa na njaa katika nchi; na hao wana wa manabii walikuwa wakikaa mbele yake. Akamwambia mtumishi wake, Teleka sufuria kubwa, uwapikie wana wa manabii.

[39]Na mmoja wao akaenda nje kondeni ili kuchuma mboga, akaona mtango-mwitu, akayachuma matango-mwitu, hata nguo yake ikawa imejaa, akaja akayapasua-pasua sufuriani; kwa maana hawakuyajua.

[40]Basi wakawapakulia hao watu ili wale. Ikawa, walipokuwa katika kula chakula, wakapiga kelele, wakasema, Mauti imo sufuriani, Ee mtu wa Mungu. Wala hawakuweza kula.

[41]Lakini yeye akasema, Leteni unga. Naye akautupa ndani ya sufuria; akasema, Wapakulie watu, ili wale. Wala hakikuwamo kitu kibaya sufuriani.

Habari hiyo inafunua nini?

Inatueleza hali ya kiroho ya watu iliyopo sasa.

Palipo na njaa ni rahisi mtu kula kila kitu, ilimradi tu asife. si rahisi akae chini na kufikiria ubora wa kile anachokula. Leo hii njaa ya Neno la kweli la Mungu ni kubwa, hivyo kila mtu anaenda kondeni kuokota kitu kimfaacho, huko huko tunakutana na vizuri lakini pia tunakutana na vibaya..

shida ipo hapo, je tunaweza kupambanua?

Kwasababu ukila sumu, ile sumu haitakuambia ngoja nisikuletee madhara kwasababu hukukusudia kunila, au hukujua kuwa mimi ni sumu, utakufa tu  sawasawa na yule anayejua anachokifanya.Kumbe ujinga una gharama kubwa.

Bwana Yesu alisema..

Mathayo 7:15

[15]Jihadharini na manabii wa uongo, watu wanaowajia wamevaa mavazi ya kondoo, walakini kwa ndani ni mbwa-mwitu wakali.

Mafundisho yasiyomhubiri Kristo na utakatifu, ni kuwa makini nayo, ni heri usiyasikilize kabisa kwa usalama wako wa kiroho. Yanayokuambia tunaokolewa kwa neema tu, hivyo matendo yako ni kazi bure mbele za Mungu, ukiokolewa umeokolewa milele, hata ukiwa unatenda dhambi vipi huwezi potea, yapime sana hayo mafundisho.

Mafundisho ya kuzimu-kuzimu tu na majini na wachawi epukana nayo, Mafundisho ya sanamu ibadani, ni mauti chunguni. Mafundisho yanayopinga habari za mwisho wa dunia, ambayo hayana habari na unyakuo au kumfanya mtu atazame kurudi kwa pili kwa Kristo, kinyume chake ni kukuweka kidunia, ufikirie mafanikio ya mwilini ni matango mwitu.

Manabii wa uongo ni wengi, wapo wanaotenda kazi kwa uwazi, lakini  wapo wanaotenda kazi kwa siri.

Jifunze kusoma biblia, jinsi usomavyo Neno la Mungu utagundua kuwa mtu uliyeokoka  kwa wakati uwapo hapa duniani Bwana anakutana Utembee katika utakatifu (Waebrania 12:14). Lakini pia uelekeze macho yako mbinguni kwa yale mambo yajayo, ya mbingu mpya na nchi mpya.

Luka 12:35-36

[35] Viuno vyenu na viwe vimefungwa, na taa zenu ziwe zinawaka; [36]nanyi iweni kama watu wanaomngojea bwana wao, atakaporudi kutoka arusini, ili atakapokuja na kubisha, wamfungulie mara.

Jihadhari na matango mwitu.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii  >>>> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

UNAWAFAHAMU MANABII WA UONGO?

Kusanyiko la makini/ mkutano wa makini ni upi?

USIPOTEZWE NA MANENO YA MANABII WA UONGO.

 

Print this post

NYWELE ZAKO ZIKUFUNDISHE, SAUTI YA MUNGU.

Kwanini Mungu akuumbe hivyo ulivyo? Kwanini asingeweka pembe kichwani kwako, au kwanini asingekuwekea  vilemba vya nyama kama vile vya kuku kichwani, au antena mbili kama zile za konokono au mdudu, bali amekuwekea nywele kichwani pako.

Sauti ya Mungu ipo katika maumbile yetu. Sisi kujikuta hivi tulivyo sio kwamba, ndio umbile bora zaidi ya yote Mungu aliloona linamfaa mtu, hapana,  tungeweza kuumbwa vizuri zaidi hata ya mwonekano huo tulionao, lakini tumebuniwa hivi, kwa kusudi la kipekee ambalo tunapaswa tulijue, na sio kwa kusudi la urembo.

Kwamfano usipoweza kuelewa utendaji kazi wa mwili wako jinsi viungo vinavyoshirikiana huwezi kuelewa jinsi kanisa la Kristo linavyopaswa kufanya kazi likutanikapo, kwasababu sisi tunaitwa viungo mbalimbali ndani ya mwili wa Kristo.Umeona? Bwana akasema kiungo kimoja kikiumia, vyote vimeumia.

Hivyo tumeumbwa, kimalengo sio kimwonekano bora au kiuzuri,. Ni sawa na mtu aulizwe kati ya jiko, na maua kipi kina umuhimu zaidi kuwepo ndani mwako. Ni wazi kuwa atasema jiko,kwasababu litamsaidia kupika. Hakulichagua kwasababu lina mwonekano bora, lakini kwasababu lina matumizi muhimu zaidi ya vingine.

Vivyo hivyo na wewe ujitazamapo mwili wako, usijitazame kiuzuri kuliko  viumbe vingine, au wanadamu wenzako, bali fikiria tu katika picha ya matumizi ya kila kiungo ulichopewa, kinakufundisha nini kuhusu muumba wako au kinatimiza kusudi gani kwa Mungu wako. Hilo ndio lengo hasaa la wewe kubuniwa hivyo ulivyo.

Leo tutaanza na NYWELE, kisha wakati mwingine tutatazama na viungo vingine;

Utazamapo nywele zako Bwana anataka ujue yafuatayo;

  1. Mambo yako yote, yapo katika hesabu za Mungu.

Mathayo 10:30  lakini ninyi, hata nywele za vichwa vyenu zimehesabiwa zote. 31  Msiogope basi; bora ninyi kuliko mashomoro wengi

Ni kawaida  kudhani kuwa Mungu hathamini, au hajui kila kitu, au anasahau sahau. Lakini sivyo, ukimfuata Mungu, vitu vyako vyote vinavyotoka na kuingia vipo kimahesabu, hakuna kitu kinachotokea kwa ghafla tu, bila yeye kujua au kuruhusu, Hivyo mashaka yakija, kumbuka nywele zako zilivyo nyingi lakini zimehesabiwa, vivyo hivyo mambo yako yote yamehesabiwa.

  1. Huwezi epukana na maadui.

Zaburi 69:4 Wanaonichukia bure ni wengi Kuliko nywele za kichwa changu. Watakao kunikatilia mbali wamekuwa hodari, Adui zangu kwa sababu isiyo kweli. Hata mimi nalilipishwa kwa nguvu Vitu nisivyovichukua

Jinsi nywele zako zilivyo nyingi, maadui nao vivyo hivyo. Na maadui zetu sio wanadamu bali ni mapepo ambayo mara nyingine huweza pia yavaa wanadamu, kutudhuru. Hivyo usiwe mtu wa kunung’unika au kulamimika, ujue kila mwanadamu yupo vitani. Kama Bwana wetu Yesu Kristo hakuwa na dhambi hata mmoja lakini alikuwa na jopo la maadui kwanini wewe usiwe nao. Hivyo kuwashinda ni kuwa mwombaji daima, na kutembea katika njia za Bwana sikuzote. Ukikumbuka kuwa maadui ni jambo la kawaida, kama tu nywele zako zilipo hapo kichwani.

  1. Si kila kitu unaweza kufanya. hivyo kuwa na kiasi.

Mathayo 5:36  Wala usiape kwa kichwa chako, maana huwezi kufanya unywele mmoja kuwa mweupe au mweusi.

Wakati mwingine, tunajiaminisha na kujihakikishia mambo na kuweka na viapo juu yake kana kwamba mambo yote yapo ndani ya uwezo wetu. Kauli kama, “leo nife,kama sitakupa hiyo fedha” au “Mungu anipige hapa hapa kama ninalokuambia ni uongo” Kauli  kama hizi, za kuongezea hakikisho lingine juu, hazitokani na Mungu, maneno yetu tumeambiwa yawe ndio ndio, au sio sio, zaidi ya hapo yanatokana na Yule mwovu. Kwahiyo popote unapojiona unakaribia kuzidi mipaka kumbuka hizo nywele zilizo juu yako hujawahi kuzifanya ziwe hivyo ulivyo, Bwana ndiye azibadilishaye, hivyo jiwekee mipaka.

  1. Zithamini nguvu zako za rohoni.

Nywele zako hufunua nguvu zako za rohoni. Wanadhiri wote wa Mungu hawakuruhusiwa kukatwa nywele, Samsoni alipewa nguvu, kwa agano la kutokatwa nywele, kufunua kuwa watakatifu wote nywele zao za rohoni ndio nguvu zao. Lakini unapoacha mpango wa Mungu adui anazikata, kama ilivyokuwa kwa Samsoni. Lakini baadaye alipojua amefanya makosa ziliota tena lakini katika gharama za ‘kutoona’ tena.

Waamuzi 16:22 Lakini zile nywele za kichwa chake zikaanza kukua tena baada ya kunyolewa kwake.

Tunza nguvu zako, usiruhusu kiwembe chochote cha mwovu kikupitie. Kwasababu hata zikirejea tena, hutakuwa kama hapo mwanzo.

  1. Uwe na nyakati za maombolezo.

Yeremia 7: 29 Zikate nywele zako, Ee Yerusalemu, uzitupe, Ukafanye maombolezo juu ya vilele vya milima; Kwa maana Bwana amekikataa na kukitupa Kizazi cha ghadhabu yake.

Zamani, kukatwa nywele zote kuisha kabisa ilikuwa ni ishara ya kuingia kwenye maombolezo, kwasababu utukufu wako umeuvua.

Maombolezo, kwa agano jipya sio kulia kama msiba, hapana bali kuingia kwenye maombi ya ndani kabisa, ya kuutafuta uso wa Mungu, ambayo huambatana na mifungo. Na leo, ni kila mara tunakwenda saluni kukata nywele zetu. Tujue Bwana anatutaka kama vile tukatavyo nywele zetu mara kwa mara ndivyo tukumbuke maombi ya kujimimina sana mbele zake.

Je! Somo hilo unajifunza mwilini mwako?

Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

Je Bwana Yesu alikuwa na nywele ndefu?

ILI TUONEKANE WAKAMILIFU MBELE ZA MUNGU.

MWOMBENI BWANA WA MAVUNO APELEKE WATENDA KAZI.

Rudi Nyumbani

Print this post

NIONYESHE MARAFIKI ZAKO, NIKUAMBIE TABIA ZAKO.

Mithali 13:20 Enenda pamoja na wenye hekima, nawe utakuwa na hekima; Bali rafiki wa wapumbavu ataumia.

Tulipokuwa watoto wazazi wetu walitufundisha kubagua baadhi ya marafiki tuliokuwa nao, na cha ajabu vigezo walivyotumia  havikuwa hata rangi zao, au kimo chao, au afya zao, bali tabia zao na akili zao. Wale watoto waliokuwa na nidhani, na akili shuleni wazazi wetu walitushurutisha sana kukaa nao karibu, kwasababu waligundua kuwa na sisi tutaambukizwa tabia zao, lakini wale waliokuwa watukutu, hata tulipokutwa tunacheza nao tu, tuliadhibiwa, sisi tuliona kama ni uonevu usio kuwa na tija, lakini baadaye tulipokuwa watu wazima, na kuona hatma ya wale watoto, ndio tulijua ni nini wazazi wetu walikuwa wanakiona.

Vivyo hivyo katika maisha ya rohoni, tunaambiwa.

Enenda pamoja na wenye hekima, nawe utakuwa na hekima; Bali rafiki wa wapumbavu ataumia.

Mbele za Mungu wenye hekima ni watu gani?

Ni watu waliookoka, wenye hofu ya Mungu ndani yao.

Mtu yeyote aliyemwamini Yesu kama Bwana na mwokozi wa maisha yake, huku akiendelea katika kumcha Mungu kwelikweli, huyo ni wa kukaa karibu naye sana. Kwasababu na wewe utajifunza njia za wokovu, utaambukizwa kuomba, utaambukizwa mifungo, utaambukizwa upendo wa ki-Mungu, lakini pia na maarifa ya Neno la Mungu, pamoja na uinjilisti.

Watu hawafahamu kuwa hata hekima ya mwokozi wetu Yesu haikuja tu kwa kutegemea hekima kutoka juu kwa baba yake, hapana, ilichangiwa pia  na watu aliowachagua kukaa nao karibu, tangu alipokuwa mdogo, tunalithibitisha hilo pindi alipokuwa amekwenda Yerusalemu na wazazi wake kwa ajili ya kuila sikukuu, kama kijana angeweza kukaa na wenzake, kujifunza uchezaji wa kamari, au kutembea mitaani kutafuta wasichana, au kwenda kwenye dansi na sinema, na kujiunga na makundi ya wavuta bangi. Lakini, haikuwa hivyo kwake, yeye alichagua watu ambao wangekuwa ni wa muhimu kwake, ndio wale viongozi wa imani na waalimu waliotwa marabi, akawa akiwasikiliza hao na kuwauliza maswali, na ghafla akaambukizwa tabia zao, mpaka akawa yeye ndio RABI wao mkuu.

Luka 2:40  Yule mtoto akakua, akaongezeka nguvu, amejaa hekima, na neema ya Mungu ilikuwa juu yake. 41  Basi, wazee wake huenda Yerusalemu kila mwaka, wakati wa sikukuu ya Pasaka.

42  Na alipopata umri wake miaka kumi na miwili, walipanda kama ilivyokuwa desturi ya sikukuu;

43  na walipokwisha kuzitimiza siku, wakati wa kurudi kwao, yule mtoto Yesu alibaki nyuma huko Yerusalemu, na wazee wake walikuwa hawana habari.

44  Nao wakadhani ya kuwa yumo katika msafara; wakaenenda mwendo wa kutwa, wakawa wakimtafuta katika jamaa zao na wenzao;

45  na walipomkosa, wakarejea Yerusalemu, huku wakimtafuta. 46  Ikawa baada ya siku tatu wakamwona hekaluni, AMEKETI KATIKATI YA WAALIMU, AKIWASIKILIZA NA KUWAULIZA MASWALI.

47  Nao wote waliomsikia walistaajabia fahamu zake na majibu yake. 48  Na walipomwona walishangaa, na mama yake akamwambia, Mwanangu, mbona umetutenda hivi? Tazama, baba yako na mimi tulikuwa tukikutafuta kwa huzuni.

49  Akawaambia, Kwani kunitafuta? Hamkujua ya kuwa imenipasa kuwamo katika nyumba ya Baba yangu? 50  Nao hawakuelewa na neno hilo alilowaambia

Mambo mengine hutaweza kuyaacha, au tabia nyingine hutaweza kuziondoa ndani yako. Kama hutaweka machaguzi ya watu sahihi wa kuongozana nao. Utakuta ni mkristo analalamika ni mzito wa kuomba, au kushuhudia, au kufunga. Ukiangalia kampani ya watu wake muda wote, ni wafanyakazi wenzake wa ofisini, ni marafiki zake wa chuo, ni majirani zake hapo mtaani. Lakini wapendwa, au watumishi wa Mungu waaminifu, ni jumapili tu kukutana nao kanisani, hata anapotafutwa, kukumbushwa wajibu wake kiroho, anawakwepa. Na wakati huo huo anatumainia awe moto kiroho. Hapo ni kujidanganya.

Tunahitaji  kupashana moto, kamwe huwezi simama kipeke yako, haijalishi wewe ni nani, au unamjua Mungu kwa ukubwa kiasi gani. Tembea na waombaji  ili  uwe mwombaji, tembea na washuhudiaji ili uweze  kushuhudia, kaa na waalimu ili uwe mwalimu. Nje ya hapo utageuzwa na ulimwengu,.

 Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >>https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

Usimwache rafiki yako mwenyewe, wala rafiki ya baba yako.

NGUVU YA HEKIMA NA AKILI

IVUMBUE INJILI YA KRISTO KUTOKA KATIKA KILA JAMBO.

Rudi Nyumbani

Print this post

JINSI YA KUSHINDA VISULISULI(Mithali 10:25)

SWALI: Nini maana ya hii Mithali 10:25

Kisulisuli kikiisha pita asiye haki hayuko tena; Bali mwenye haki ni msingi wa milele.


JIBU: Mstari huo unajifafanua vizuri kwenye ule mfano Bwana Yesu aliutoa kuhusiana na watu wanaoyasikia maneno yake, halafu hawayatendi. Tusome.

Mathayo 7:24  Basi kila asikiaye hayo maneno yangu, na kuyafanya, atafananishwa na mtu mwenye akili, aliyejenga nyumba yake juu ya mwamba;

25  mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile, isianguke; kwa maana misingi yake imewekwa juu ya mwamba.

26  Na kila asikiaye hayo maneno yangu asiyafanye, atafananishwa na mtu mpumbavu, aliyejenga nyumba yake juu ya mchanga;

27  mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile, ikaanguka; nalo anguko lake likawa kubwa.

Hivyo tukirejea katika vifungu vile vya kwenye mithali. Unaweza kuelewa mtu asiye haki hasaa ni nani?

Ni Yule ambaye anaisikia injili, halafu hatii.  Mtu Yule anayesema ameokoka, lakini zao la wokovu halionekana ndani yake. Rohoni anaonekana hana tofauti na yule ambaye hajamjua Mungu kabisa. Wote hao huitwa wasio haki. Bado wapo dhambini, hawajakombolewa na damu ya Yesu Kristo.

Hawa wataonekana kwa nje kama vile ni watakatifu. Lakini kinapokuja tu kisulisuli  aidha  cha majaribu, shida, dhiki, udhia,au mapigo kwa ajili ya Kristo, mara ghafla wanarudi nyuma, wanakuwa kama watu ambao hawajawahi kumjua Mungu kabisa, kwasababu hakujikita katika mwamba. Wengine sio majaribu ya shida, bali yale ya mafanikio makubwa, ndio hapo anasa zinawazidi wanamsahau Mungu, wanaiaga imani, kwani walimfuata Yesu kwasababu ya shida tu. Wengine ndoa, elimu, vyeo wakishavipata, huwaoni tena kwa Yesu.

Lakini mtu anayeyasikia maneno ya Kristo na kuyatii, ni kinyume chake, huitwa msingi wa milele. Huyo hatikiswi na wimbi, kisulisuli au dhoruba yoyote. Kwasababu yupo juu ya mwamba.

Okoka, upokee msamaha wa dhambi, kisha ishi kufuata na toba yako, ili uhakika wa kusimama uwe nao wakati wote.

Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

MWAMBA WETU.

Mtu asiye na akili ni nani kibiblia?

TUNAHESABIWA HAKI BURE KWA NJIA YA IMANI.

TUNAHESABIWA HAKI BURE KWA NJIA YA IMANI.

Rudi Nyumbani

Print this post