Category Archive Mafundisho

Nyongeza ya majina ya watu katika biblia

Tunaona kuna baadhi ya watu ambao majina yao yameongezwa vionjo kwa mbele, kwa mfano Simoni Petro, Yuda Iskariote, Tomaso pacha, Simoni mkananayo, Yohana Mbatizaji n.k

Watu hawa ambao majina yao yanaonekana kuongezewa vionjo mbele yake ni kwa lengo la kuwatofautisha na watu wengine wenye majina kama ya kwao. Na vionjo hivyo vilivyokuwa vinawekwa ni aidha kulingana na mahali (miji) wanayotokea, au majina ya wazazi wao, au matendo/huduma  wanazozifanya.

Wafuatao ni baadhi ya majina ya watu yaliyoongezewa vionjo kulingana na Matendo waliyokuwa wanayafanya;

  1. Yohana Mbatizaji – Ili kumtofautisha na Yohana wengi ambao walikuwepo Israeli, aliitwa hivyo Yohana Mbatizaji kutokana na kazi yake ya kubatiza watu aliyokuwa anaifanya, Hivyo palipotajwa Yohana mbatizaji wote walijua analengwa nani.
  2. Simoni Petro- Maana ya Petro ni ‘Jiwe’ dogo la kurusha, na si “mwamba” kama inavyoaminika na wengi. Bwana Yesu alimpa Simoni jina Petro, kutokana na jinsi Bwana atakavyomtumia katika huduma yake, katika kuzipiga nguvu za shetani.
  3. Yohana na Yakobo (Boanerge)- Maana ya Boanerge ni ‘Wana wa Ngurumo’ Marko 3:17. Bwana aliwaita hivi kufuatia huduma zao, na ili pia kuwatofautisha na wengine wenye majina kama yao.

Kulingana na Mahali walipotokea;

  1. Yuda Iskariote- Iskaritote maana yake ni mtu wa Keriote/Keriothi.. Na Keriothi ni mji uliokuwepo katika Nchi ya Moabu.
  2. Simoni Mkirene- Kirene ni mji uliokuwepo Kaskazini-kusini mwa nchi ya Libya, Ili kumtofautisha Simoni huyu aliyeubeba msalaba wa Bwana na Simoni aliyekuwa mwanafunzi wa Bwana, ndipo akatajwa kulingana na mji aliotokea ambao ni Kirene.
  3. Simoni Mkananayo- Aliitwa hivi kufuatia mji aliotokea ulioitwa ‘’KANA’’ ndio kule Bwana alipogeuza maji kuwa Divai (Mathayo 15:22) na pia ulikuwepo pia mji mwingine katika nchi ya Tiro ulioitwa hivyo ‘Kana’, ambapo aliishi yule mwanamke aliyemlilia Bwana amponye binti yake aliyepagawa na pepo (Soma Mathayo 15:21-22).Mtu aliyetokea Kana, aliitwa Mkananayo.. Lakini pia Huyu Simoni Mkananayo sehemu nyingine pia alijulikana kama Simoni Zelote (Luka 6:15, Matendo 1:13), maana ya Zelote ni “Mpigania dini”, hivyo watu waliokuwa wanaishindania na kuipigania dini ya kiyahudi wakati huo waliitwa Wazelote, na huyu Simoni kabla hajaitwa na Bwana alikuwa anajulikana hivyo
  4. Mariamu Magdalene- Magdalene ni mji uliokuwepo huko Galilaya.. hivyo ili kumtofautisha Mariamu mamaye Yesu na yule aliyetokwa na pepo saba, ndipo huyu akaitwa Mariamu Magdalene.

Kwahiyo ili kumtofautisha na Simoni Petro au Simoni  mwingine yeyote, ndipo huyu akaitwa Simoni Mkananayo au Simoni Zelote.

    Kulingana na majina ya Wazazi/ Ndugu

1 .Yakobo wa Alfayo:  Yakobo alikuwa ni mtoto wa Mtu aliyeitwa Alfayo, Aliitwa hivyo ili kumtofautisha na akina Yakobo wana wa Zebdayo na wengine waliokuwepo kwa wakati huo.(Marko 3:18).

2. Yuda mwana wa Yakobo: Huyu alikuwa ni mwanafunzi wa Bwana Yesu ambaye pia aliitwa kwa jina lingine “Thadayo”(Marko 3:18). Ili kumtofautisha na Yuda aliyemsaliti Bwana Yesu, ndipo kwa jina lingine akajulikana hivyo kama Yuda wa Yakobo au Thadayo.

3. Tomaso aitwaye Pacha (Yohana 20:2)– Ni kuonyesha Tomaso kuwa alikuwa na Pacha lakini hakutajwa katika maandiko huyo pacha wake alikuwa ni nani, ila aliitwa hivyo ili kumtofautisha na wakina Tomaso wengine waliokuwepo pale.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Je jina lako ni nani? Na linabeba ujumbe gani?… >>JINA LAKO NI LA NANI?

Maran atha

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

NI NANI ATAKAYEUCHUKUA MSALABA WA YESU?

MAANA YA MAJINA NA TAFSIRI ZAKE.

Kwanini mtu afanye miujiza na bado asiende mbinguni?

Yeremia alikuwa na umri gani alipoitwa?

NGUVU YA UPENDO WA KRISTO.

Rudi nyumbani

Print this post

SISI TU MANUKATO YA KRISTO.

(Masomo maalumu kwa Wakristo, Je! Unajijua nafasi yako?.. je unajijua kuwa wewe ni manukato yanayokubalika na pia yasiyokubalika kwa upande mwingine?).

Manukato ni neno lingine la “Marashi”.. Na kazi ya manukato/Marashi ni kukifanya kitu kivutie, hakuna mtu anayejipaka marashi ili mtu amkimbie. Lakini changamoto ni kwamba haijalishi marashi yatakuwa ni mazuri kiasi gani, ni lazima kwa upande mwingine kuna mtu yatamtia kichefuchefu tu. (Si kila marashi yaliyo mazuri kwa mtu, yatakuwa mazuri kwa watu wote).. ni lazima upande mmoja utayakosoa tu.

Na siku zote, marashi yaliyokosolewa huwa yanatia kichefuchefu na hata wakati mwingine kumuumiza Yule anayeyasikia..

Kadhalika biblia inasema kuwa sisi ni Manukato ya Kristo. Na kama ni manukato ni lazima upande mmoja yatakubalika na upande mwingine yatakatalika.. Na siri ya manukato ya Kristo ni kwamba wengi wanayachukia zaidi ya wale wanayoyapenda..

2Wakorintho 2:14 “Ila Mungu ashukuriwe, anayetushangiliza daima katika Kristo, na kuidhihirisha harufu ya kumjua yeye kila mahali kwa kazi yetu.

15  KWA MAANA SISI TU MANUKATO YA KRISTO, mbele za Mungu, katika wao wanaookolewa, na katika wao wanaopotea;

16  katika hao wa pili harufu ya mauti iletayo mauti; katika hao wa kwanza harufu ya uzima iletayo uzima. Naye ni nani atoshaye kwa mambo hayo?

17  Kwa maana sisi si kama walio wengi, walighoshio neno la Mungu; bali kama kwa weupe wa moyo, kama kutoka kwa Mungu, mbele za Mungu, twanena katika Kristo”.

Wakristo wengi wanadhani kuwa wanapookoka bali wataanza kupendwa, na kukubalika na kupokea kibali kila mahali. Ni kweli hayo yanaweza kutokea kwasababu kwa Mungu yote yanawezekana.. Lakini fahamu kuwa wewe ni marashi mazuri lakini yenye kuleta harufu mbaya kwa wanaopotea..

Maisha ya usafi na ukamilifu unayoishi ni harufu nzuri kwa wanaookolewa, (Maana yake ni mfano mzuri wa kuigwa, kwa waongofu wapya na waaliookoka), kuomba kwako na kufunga kwako na kuhubiri kwako ni harufu nzuri kwa waliookoka kama wewe.

Lakini kwa wale ambao hawamtaki Yesu, fahamu kuwa maisha yako ni kichefuchefu kwao….ni lazima watakupinga tu, ni lazima watakuletea vita tu, ni lazima watakukosa tu, ni lazima watakurushia mishale tu..Kwasababu kwao wewe ni manukato yenye harufu mbaya, tena harufu inayoleta mauti kabisa…yaani maisha yako yanawahukumu..

Hili ni jambo la kufahamu wewe uliyempokea Kristo na kuokoka!.. Kamwe usifikiri kuwa utaendelea furaha yako ndani ya Kristo ni jambo linalovutia machoni pa wengine… Ukristo ni vita, unapoamua kuwa mkristo ni kama mtu aliyevaa kombati na kuingia vitani.. Kwahiyo tegemea kukumbana na maadui wa imani, watakaokukosoa na kukutatisha tamaa..

Yohana 15:18  “Iwapo ulimwengu ukiwachukia, mwajua ya kuwa umenichukia mimi kabla ya kuwachukia ninyi.

19  Kama mngekuwa wa ulimwengu, ulimwengu ungewapenda walio wake; lakini kwa kuwa ninyi si wa ulimwengu, bali mimi naliwachagua katika ulimwengu, kwa sababu hiyo ulimwengu huwachukia.

20  Likumbukeni lile neno nililowaambia, Mtumwa si mkubwa kuliko bwana wake. Ikiwa waliniudhi mimi, watawaudhi ninyi; ikiwa walilishika neno langu watalishika na lenu”.

Bwana akubariki.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

Marhamu ni nini? Na Manukato ni nini?

Je tunaruhusiwa kujipaka mafuta au kujipulizia marashi?

USICHELEWE KUMPAKA BWANA MARHAMU!

KWANINI NDOA NYINGI ZINAVUNJIKA? (Sehemu ya 1: Upande wa wanaume)

Nini tofauti ya Uwezo na Uweza kibiblia?

Rudi nyumbani

Print this post

USIJISIFIE KARAMA KWA UONGO.

Mithali 25:14 “Kama mawingu na upepo pasipo mvua; Ndivyo alivyo yeye ajisifiaye karama kwa uongo”.

Njia nyingine shetani anayoitumia kuwaangusha watu na kudanganya watu, ni kupitia “karama za uongo”.. Hii inatokea pale ambapo mtu anajipandikiza karama ambayo hana, na anajitangaza kuwa anayo kwa wote, jambo ambalo lina madhara makubwa sana kiroho.

Zifuatazo ni ishara za karama ya kweli ndani ya Mtu, maana yake mtu akikosa hizi ishara basi huenda hiyo karama hana au anayo lakini imeshambuliwa na kutumiwa na adui.

  1. KUWAKAMILISHA WATAKATIFU.

  Mtu mwenye karama ya kweli ya Mungu, ni lazima atakuwa na msukumo wa kuwafanya watu wazidi kukamilika katika Utakatifu, na kumcha Mungu…hata kufikia viwango ambavyo Mungu anataka (Waebrania 12:14), maana yake kila siku atakuwa anatafuta kutatua kasoro zinazofanya watu au yeye mwenyewe asiwe mkamilifu kwa Mungu..Lakini kama karama ya mtu inazidi kumfanya yeye mwenyewe asiwe mkamilifu, au kuwafanya watu wasiwe wakamilifu kwa Mungu, au wasihamasike kumtafuta Mungu zaidi, au kujitakasa… badala yake inawahamasisha kutafuta mambo ya kidunia, basi huyo mtu haijalishi anajiita Mchungaji au Mtume, au nabii kiuhalisia hana hiyo karama..

Utauliza tunalithibitisha vipi hilo kimaandiko… hebu tusome maandiko yafuatayo..

Waefeso 4:11  “Naye alitoa wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na waalimu; KWA KUSUDI LA KUWAKAMILISHA WATAKATIFU….”

2. IPO KWA LENGO LA KUWAHUDUMIA WATU NA SI KUJIHUDUMIA YENYEWE.

Karama yoyote ya kweli ni lazima iwe na HUDUMA, na huduma maana yake ni kutoa msaada kwa wengine, na msaada tulioagizwa sisi wakristo tu utoe ni ule wa kiroho na usio na gharama.. Maana yake hatujaagizwa kuwatoza watu vitu ili wapokee kutoka kwetu.

Hiyo ikiwa na maana kuwa kama mtu yeyote anajiita Mchungaji, au Nabii, au Mwinjilisti au Mwimbaji, au halafu huduma yake anaitoa kwa malipo, ni wazi kuwa hana hiyo karama, haijalishi anajua kuimba kiasi gani au anajua kuhubiri kiasi gani, au anatoa unabii kiasi gani… Kama hatakuwa mtu wa kutoa Huduma bila kutazamia malipo, huyo atakuwa anahudumu kwa roho nyingine ya adui.

Utasema tunalithibithisha vipi hili nalo  kimaandiko… Tuendelee na mstari ule wa 12..

Waefeso 4:11  “Naye alitoa wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na waalimu;

12  kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, HATA KAZI YA HUDUMA ITENDEKE….”

3. IPO KWA LENGO LA KUUJENGA MWILI WA KRISTO.

Mwili wa Kristo unajengwa kwa viungo vyote na si kimoja au viwili.. Kristo alipokuwa hapa duniani hakuwa mlemavu.. wala hata baada ya kufa hakuwa mlemavu (maandiko yanaonyesha mifupa yake haikuvunjwa pale msalabani).. Na sisi ni viungo vya Kristo, hivyo ili tuujenge mwili mkamilifu wa Yesu ni lazima tuwepo wote pamoja..

Mtu akijiona Nabii, au Mtume, au Mwalimu na hayupo katika ushirika na viungo vingine katika kanisa, ni yeye tu kama yeye, mtu huyo si kiungo cha Kristo, na hana hiyo karama anayojivunia..

1Wakorintho 12:14  “Kwa maana mwili si kiungo kimoja, bali ni vingi.

15  Mguu ukisema, Kwa kuwa mimi si mkono, mimi si wa mwili; je! Si wa mwili kwa sababu hiyo?

16  Na sikio likisema, Kwa kuwa mimi si jicho, mimi si la mwili; je! Si la mwili kwa sababu hiyo?

17  Kama mwili wote ukiwa jicho, ku wapi kusikia? Kama wote ni sikio ku wapi kunusa?

18  Bali Mungu amevitia viungo kila kimoja katika mwili kama alivyotaka.

19  Lakini kama vyote vingekuwa kiungo kimoja, mwili ungekuwa wapi?

20  Lakini sasa viungo ni vingi, ila mwili ni mmoja.

21  Na jicho haliwezi kuuambia mkono, Sina haja na wewe; wala tena kichwa hakiwezi kuiambia miguu, Sina haja na ninyi”.

Tunazidi kulithibitsha hili katika mstari ule ule wa 12..

Waefeso 4:11 “Naye alitoa wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na waalimu;

12 kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya huduma itendeke, HATA MWILI WA KRISTO UJENGWE”

Kama Karama haiujengi mwili wa Kristo ni karama ya uongo.

Kwahiyo ni lazima kila mtu mwenye karama Fulani ya Roho awe na sifa hizo, lakini kama hana hizo sifa basi huenda hana hiyo karama anayojivunia kuwa anayo au alikuwa nayo lakini sasa imeshambuliwa na inatumiwa na adui.

Na watu wote wanaojivunia karama za Uongo, biblia imesema ni kama mawingu yasiyo na maji.

Mithali 25:14 “Kama mawingu na upepo pasipo mvua; Ndivyo alivyo yeye ajisifiaye karama kwa uongo”.

Maana yake ni watu wanaotoa matumaini ya kusitawisha jambo lakini mwisho wao ni ukame tu.. Hivyo si wakuaminiwa.

Bwana atusaidie karama zetu ziwe za kweli.

Maran atha!

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Jiunge na kundi letu la mafundisho ya Biblia whatsapp kwa kubofya hapa > Group-whatsapp

Mada Nyinginezo:

Karama ya pili inayozungumziwa katika 2Wakorintho 1:15 ndio ipi?

ICHOCHEE KARAMA YAKO.

Nini tofauti kati ya Kipawa na Karama?

JIHADHARI NA UONGO WA SHETANI UNAOKARIBIANA NA UKWELI.

NA VIUNGO VYETU VISIVYO NA UZURI VINA UZURI ZAIDI SANA.

Rudi nyumbani

Print this post

ISHARA YA KANISA LA LAODIKIA

Karibu katika mafunzo ya biblia.

Kwanini tunasema kuwa hili ni kanisa la Mwisho la Laodikia?, Je ni viashiria gani vinavyotutambulisha kuwa hali ya kanisa la Laodikia lile la saba ambalo Mtume Yohana alionyeshwa kwenye Maono  katika kitabu cha Ufunuo ndio hali halisi ya kanisa letu la siku za mwisho?.

Awali ya yote hebu tujikumbushe historia ya yale makanisa saba, tunayoyasoma katika kitabu cha Ufunuo Mlango wa 2 na wa 3.

Makanisa saba tunayoyasoma katika kitabu cha Ufunuo ni makanisa ambayo yalikuwa katika miji 7 tofauti tofauti. (Efeso, Smirna, Pergano, Thiatira, Sardi, Filadelfia na Laodikia, Ufunuo 1:11).

Hivyo  na makanisa hayo yalijulikana kwa majina ya miji hiyo,  na Yote ilikuwa inapatikana katika eneo lijulikanalo kama “Asia Ndogo” ambapo kwasasa ni nchi ya “Uturuki”.

Sasa kila kanisa lilikuwa na tabia yake, kulingana na huo mji (unaweza kusoma tabia hizo katika Ufunuo 2-3). Na kanisa la Mwisho kabisa kutajwa ambalo ndio la saba lililoitwa Laodikia lilikuwa na tabia nyingine ya kipekee ambayo kwa hiyo ndiyo tutajua kuwa kanisa letu la sasa linafanana na kanisa la huo mji au la!.

Sasa kabla ya kwenda kusoma tabia za kanisa hilo katika kitabu cha Ufunuo, hebu kwanza tuweke msingi mwingine wa kuelewa jambo lingine, ambalo litatusaidia kuelewa hili vizuri.

Katika biblia maandiko yanatabiri kuwa dalili za siku za mwisho ni Maasi kuongezeka katika kiwango cha miji ya Sodoma na Gomora, au miji ya Nyakati za Nuhu (Soma Luka 17:26-28).

Maana yake ni kuwa kama hali ya maovu haijafikia kile kiwango cha maasi ya Sodoma na Gomora, basi bado ule mwisho utakuwa upo mbali, lakini kama hali ya mji itafikia kile kiwango cha maasi ya Sodoma na Gomora basi ni wazi kuwa ule mwisho umefika.

Kwahiyo ni sahihi kusema kuwa  Miji ya Sodoma na Gomora ni ishara au alama ya miji ya siku za mwisho, Hivyo tukitaka kujua kuwa tupo siku za mwisho basi tujilinganishe na miji ya Sodoma na Gomora. (2Petro 2:6 na Yuda 1:7).

Na sasa tunaona kabisa kuwa kizazi chetu ni kama kile cha Sodoma na Gomora na hata huenda kimepita, kwasababu katika miji ya Sodoma na Gomora kulikuwa na mwingiliano wa ndoa za jinsia moja..vile vile na sasa hali ni hiyo hiyo, ushoga upo kila mahali, mauaji, dhuluma n.k kwahiyo tupo siku za mwisho.

Vile vile na kanisa la Mji wa Laodikia, ambao ulikuwepo katika enzi  za kanisa la Kwanza,  lilikuwa ni Ishara ya kanisa la siku za mwisho. Maana yake ni kuwa tukitaka kujua kuwa tunaishi katika kanisa la mwisho, basi tunapaswa tujilinganishe kanisa letu na lile la Laodikia. Tukiona yanafanana kitabia basi tujue kuwa hili ndio kanisa la mwisho na unyakuo umekaribia.. lakini tukiona kuwa bado hatujafikia viwango vya kanisa lile basi tujue kuwa ule mwisho huenda bado sana.

Sasa hebu tusome tabia za kanisa la Laodikia katika biblia.

Ufunuo 3:14 “Na kwa malaika wa kanisa lililoko Laodikia andika; Haya ndiyo anenayo yeye aliye Amina, Shahidi aliye mwaminifu na wa kweli, mwanzo wa kuumba kwa Mungu.

15  NAYAJUA MATENDO YAKO, YA KUWA HU BARIDI WALA HU MOTO; INGEKUWA HERI KAMA UNGEKUWA BARIDI AU MOTO.

16  Basi, kwa sababu una uvuguvugu, wala hu baridi wala moto, nitakutapika utoke katika kinywa changu.

17  Kwa kuwa wasema, Mimi ni tajiri, nimejitajirisha, wala sina haja ya kitu; nawe hujui ya kuwa wewe u mnyonge, na mwenye mashaka, na maskini, na kipofu, na uchi”.

Umeona tabia za kanisa la Laodikia?..Biblia inasema ni kanisa ambalo lilikuwa vuguvugu, si moto wala si bariki.. mfano kamili wa kanisa la wakati huu. (Kumbuka hapa tunazungumzia kanisa na si watu wa ulimwengu, watu wa ulimwengu ishara yao ni miji ya Sodoma na Gomora na sisi kanisa ishara yetu ni kanisa la mji wa Laodikia).

Kanisa la wakati huu utaona mtu mguu mmoja nje mguu mmoja ndani, leo yupo kanisani kesho disco, leo anamwabudu Bwana kesho anasikiliza miziki ya kidunia, simu yake nusu ina nyimbo za injili nusu nyimbo za kidunia, kabati lake nusu lina nguo za kujisitiri nusu lina nguo za nusu uchi, maneno yake nusu ya heshima nusu ya kihuni, biashara yake nusu ni halali nusu ni haramu, duka lake nusu lina bidhaa njema nusu lina bidhaa haramu (pombe, na sigara), leo atatoa sadaka kesho anaonga/ anaogwa.n.k

Hiyo ndiyo ilikuwa hali ya kanisa la Laodikia na ndio hali ya kanisa la Sasa tulilopo.

Hiyo ndiyo alama pekee inayotutambulisha siku si nyingi unyakuo wa kanisa utatokea. Kwasababu hakutakuwa na kanisa lingine litakalotokea lenye tabia nyingine, hili la Laodikia biblia imetabiri ndio kanisa la Mwisho baada ya hapo ni unyakuo ndio maana utaona pale, baada ya ujumbe wake kumalizika kilichofuata ni Yohana kuchukuliwa juu mbinguni.

Ufunuo 4:1 “Baada ya hayo naliona, na tazama, mlango ukafunguka mbinguni, na sauti ile ya kwanza niliyoisikia kama sauti ya baragumu ikinena nami, ikisema, Panda hata huku, nami nitakuonyesha mambo ambayo hayana budi kuwako baada ya hayo”.

Wakati kanisa hili la Laodikia limechafuka hivi, Bwana analiandaa kundi lake dogo, na kuliambia litoke huko, kama vile alivyowaokoa Nuhu na Luthu..Vile vile kanisa la Laodikia litaingia katika dhiki kuu kwasababu ni kanisa vuguvugu lakini kundi dogo ambalo litakuwa safi na litakuwa Moto na si Vuguvugu hilo litaenda na Bwana katika unyakuo.

Ndugu unyakuo umekaribia sana, Yesu yupo Mlangoni kurudi, ondoka katika uvuguvugu, wa kidunia, kuwa Moto.. Ukiamua kumfuata Kristo basi mfuate kwelikweli, usiige desturi za kidunia, ukiamua kuwa mtu wa kujisitiri fanya hivyo kikweli kweli usiwe nusu nusu, ukiamua kumfuata Yesu basi jikane kweli kweli.

Uvuguvu Kristo anauchukia kuliko hata Yule mtu aliye baridi kabisa.. kwasababu yeye mwenyewe anasema ni heri mtu awe moto au baridi kuliko vuguvugu..

Bwana atusaidie.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Jiunge na kundi letu la mafundisho ya Biblia whatsapp kwa kubofya hapa > Group-whatsapp

Mada Nyinginezo:

AGENDA KUBWA YA SHETANI KWA KANISA HILI LA LAODIKIA.

SAUTI NI SAUTI YA YAKOBO, LAKINI MIKONO NI YA ESAU.

Babewatoto ni nani katika biblia?(Isaya 34:14).

Babeli ni nchi gani kwasasa?

JE NI KWELI SAMAKI NGUVA YUPO?

Rudi nyumbani

Print this post

ATAANGAMIZWA NA KUTENGWA NA WATU WAKE.

Karibu tujifunze biblia.

Matendo 3:22 “ Kwa maana Musa kweli alisema ya kwamba, Bwana Mungu wenu atawainulieni nabii, katika ndugu zenu, kama mimi; msikieni yeye katika mambo yote atakayonena nanyi.

23 Na itakuwa ya kwamba kila mtu asiyemsikiliza nabii huyo ataangamizwa na kutengwa na watu wake”

Unabii huo unamhusu Bwana Yesu Kristo, lakini swali la Msingi hapa, je! Ni wakati gani ambao “watu wataangamizwa na kutengwa” kwa kutomsikiliza huyu Masihi…Kwasababu ni wengi leo hawamsikilizi wala kumtii lakini hawaangamizwi wala kutengwa na watu wao.

Hapo kuna mambo mawili ambayo yatatimia kwa pamoja.. 1) KUANGAMIZWA, na 2) KUTENGWA.

Haya ni mambo mawili ambayo yatatimia kwa wakati mmoja kwa wote ambao hawatamsikiliza Masihi.
Sasa swali, ni hili unabii huo utatimia lini wa watu kuangamizwa na kutengwa?

Tusome,

2Wathesalonike 1:7 “na kuwalipa ninyi mteswao raha pamoja na sisi; WAKATI WA KUFUNULIWA KWAKE BWANA YESU kutoka mbinguni pamoja na malaika wa uweza wake

8 katika mwali wa moto; huku akiwalipiza kisasi wao wasiomjua Mungu, na wao wasioitii Injili ya Bwana wetu Yesu;

9 watakaoadhibiwa kwa MAANGAMIZI ya milele, KUTENGWA na uso wa Bwana na UTUKUFU WA NGUVU ZAKE;”

Umeona hapo?. Kumbe wote wasioitii injili, leo siku ya mwisho (ya kufunuliwa Bwana Yesu) wataangamizwa!, na sio tu kuangamizwa, bali pia “watatengwa na uso wa Mungu” na “kutengwa na utukufu wa nguvu zake”…Maana yake wataanza kwa kutengwa kutoka kwa ndugu zao (wakati wa kutenganishwa kondoo na mbuzi Mathayo 25:31-35) na pia watatengwa na vitu vyote Mungu alivyoviumba ikiwemo dunia na kila kitu…sawasawa na Mithali 2:21-22.

Mithali 2:21 “Maana wanyofu watakaa katika nchi, Na wakamilifu watadumu ndani yake.

22 Bali waovu watatengwa na nchi, Nao wafanyao hila watang’olewa”

Ni jambo baya sana kutengwa na uso wa Mungu na kuangamizwa!..
Wengi leo wanamkataa Yesu na kuikataa Injili wakidhani ipo njia nyingine ya kufika mbinguni.. Bwana Yesu yeye mwenyewe alisema kwa kinywa chake kuwa..

Yohana 14:6 “..Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi”.
Hakuna njia nyingine ya kumfikisha mtu mbinguni isipokuwa njia ya Msalaba!.. Usidanganyike kwa vyovyote vile.

Mwisho wa dunia unakuja, Mpokee Yesu leo, Itii injili yake inayosema… usizini, usiibe, usivae mavazi ya nusu tupu, usivae mavazi yapasayo jinsia nyingine, usijichore mwili, usitukane n.k

Bwana akubariki.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Jiunge na kundi letu la mafundisho ya Biblia whatsapp kwa kubofya hapa >> WHATSAPP-GROUP

Mada Nyinginezo:

Je mwanamke anaruhusiwa kupanda madhabahuni akiwa katika siku zake?

Ni kwa namna gani Kristo analitakasa kanisa kwa Maji katika Neno? (Waefeso 5:26)

Je Mungu ana njia ngapi za kuzungumza?

Wana wa Manabii walikuwa ni watu gani?

REKEBISHA YAFUATAYO ILI UCHUMI WAKO UKAE SAWA.

Rudi nyumbani

Print this post

IJUE FAIDA YA KUNENA KWA LUGHA MPYA!

Jina la Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo lihimidiwe daima, karibu tujifunze Biblia Neno la Mungu wetu lililo taa ya miguu yetu na Mwanga wa njia yetu (Zab.119:105).

Maandiko yanatuonyesha kuwa si lazima watu wote wanene kwa lugha (1Wakorintho 12:30 na  14:23), kana kwamba ndio uthibitisho pekee wa mtu kuwa wa kiroho…lakini pia kuna faida kubwa ya kunena kwa lugha ikiwa mtu atajaliwa hilo.

Na pia kunena kwa lugha si jambo  ambalo mtu anaweza kuamua, kwamba sasa naanza kunena, la! Kunena kwa lugha ni msukumo ambao Roho Mtakatifu anaushusha ndani ya mtu pasipo mtu kutaka au kupanga!.. Ni kama mtu anavyopokea unabii, au anavyopokea ndoto au maono.. hakuna mtu anayeweza kupanga unabii au maono au ndoto (labda awe nabii wa uongo)!.. kwani mambo hayo yanakuja tu yenyewe kutoka kwa Mungu, kwajinsi apendavyo Mungu… Na kunena kwa lugha ni hivyo hivyo, si lazima iwe kila siku au kila saa, bali ni wakati maalumu tu ambao Roho atalishusha jambo hilo ndani ya mtu.

Sasa zipo lugha za wanadamu, na vile vile za Malaika (Soma 1Wakorintho 13:1), Zozote kati ya hizo mtu aliyejazwa Roho anaweza kuzinena. Na zote zina faida katika kuzinena… Katika kunena lugha za wanadamu ni pale ambapo mtu haijui lugha Fulani ya jamii fulani ya watu, lakini ghafla anajikuta anaanza kuizungumza ile lugha vizuri sana.. Vile vile katika kunena lugha za malaika, ni pale ambapo anajikuta anazungumza lugha ambayo ni mpya kabisa isiyotumiwa na wanadamu mahali popote.

Na maneno anayoyazungumza yanakuwa aidha ni maneno ya unabii, au maonyo au ya kumsifu Mungu.. kwahiyo kama ni ujumbe kwa kanisa ni lazima awepo mfasiri..

Vile vile kama ni lugha Mpya inayozungumzwa, maana yake ambayo haitumiki na jamii yoyote ya wanadamu, na ni ujumbe kwa kanisa, basi anahitajika pia mfasiri, lakini kama mtu yupo katika maombi yake binafsi na lugha hiyo ikamjia ndani yake, basi hapo hahitaji mfasiri bali anakuwa ananena maneno ya siri na Mungu wake.

Na leo tutaangalia faida moja kubwa  ya kunena lugha mpya, uwapo wewe binafsi katika maombi yako ya faragha.

MAZUNGUMZA YAKO YANAKUWA NI YA SIRI.

Hii ndio faida kuu na ya kwanza. Kikawaida mazungumzo ya siri yanakuwa na upinzani mchache kuliko mazungumzo ya wazi!..  na njia mojawapo ya kuficha mazungumzo ni kutumia lugha nyingine!..

Kwamfano utaona Waarabu wawili, au Wachaga wawili, au wamasai wawili, au wasukuma wawili, wanapokutana mahali Fulani ili waongee kwa uhuru zaidi utaona wanatumia lugha zao  za asili , lengo ni kuficha mazungumzo na pia kuzungumza mambo yao yale mambo ya ndani kwa uhuru zaidi.. watu walio kando kando inakuwa ngumu kuelewa na hivyo wazungumzaji wanakuwa wamefunga milango mingi.

Na  sisi tunapozungumza na Mungu wetu, KUNA WAKATI TUNAHITAJI USIRI.. Maneno yetu tunayoyazungumza si lazima yaeleweke na watu wa kando yetu au na mapepo katika ulimwengu wa roho. Ili kuzuia vita visivyokuwa na msingi.

Shetani asipoelewa kile tunachoomba kwa Mungu, inamwia vigumu kwake kupanga mashambulizi, kwasababu hajui ni nini tunamwomba Mungu kwa wakati huo, hivyo anabaki tu hapo katikati, lakini akisikia unamwomba Mungu akupe Amani, au akupe riziki Fulani, tayari na yeye kashajua ni eneo gani aende kukupiga vita ili usipokee kile ulichomwomba Mungu. Ndio maana Mtume Paulo kwa ufunuo wa roho aliliona hilo na akawaandikia watakatifu..                                                                                                                                                   

1Wakorintho 14:2  “Maana yeye anenaye kwa lugha, hasemi na watu, bali husema na Mungu; maana hakuna asikiaye; lakini anena mambo ya siri katika roho yake”.

Hivyo usijizuie kunena kwa lugha kama umejaliwa hilo.. itakusaidia kuzuia vita vingi katika ulimwengu wa mwili na wa roho.

Bwana akubariki.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

Je kunena kwa Lugha mpya kukoje?

JE! UMEPOKEA KWELI ROHO MTAKATIFU?

SEMA KWA LUGHA NYINGINE.

MBINGU MPYA NA NCHI MPYA. (Sehemu ya 1)

USHIRIKA WA ROHO MTAKATIFU UKAE NANYI NYOTE.

Rudi nyumbani

Print this post

SI KWA MATENDO BALI NEEMA.

Ikiwa unafanya matendo mazuri yanayompendeza Mungu, basi mshukuru Mungu kwa hayo lakini USIJISIFU wala kujigamba hata kidogo kwa hayo. Kwasababu wakati unadhani kuwa umefanya 100 yanayompendeza Mungu kwa siku moja, yapo mengine 200 uliyoyafanya yasiyompendeza Mungu, kwa kutokujua.

Laiti tukifunguliwa macho na kuona makosa yetu yote tunayoyafanya bila sisi wenyewe kujua, tusingeendelea kujitamani hata kidogo, tusingeendelea kujivuna, tusingeendelea kujisifia vimema vichache vichache tunavyovitenda kwa siku!!!…Kwaufupi maisha yetu yamejaa makosa mengi kuliko mema!, hata kama tutajiona kama tuna mema mengi kuliko kasoro.. Lakini uhalisia utabakia pale pale kwamba makosa yetu yamezidi mema yetu..

Kwahiyo kama Mungu ni wa haki, basi ni haki yake atulipe mabaya mengi kuliko mema.

Kama ukimlazimisha Mungu akuhesabie haki ya kukubariki kwa sadaka yako uliyotoa  jumapili, vile vile anapaswa akuhesabie haki ya kuadhibiwa kwa mawazo yako ya kutamani na kwa hasira uliyomwonea ndugu yako siku hiyo hiyo ya jumapili. Na maandiko yanasema mtu amwoneaye ndugu yake hasira ni mwuaji, kwahiyo unapaswa uhukumiwe kama mwuaji..

Lakini kama hutaki Mungu atazame udhaifu wako huo na hutaki akuadhibu kwa makosa yako basi usilazimishe akulipe kwa matendo yako mazuri unayomfanyia. Bali kinyume chake nyenyekea!!!.. Fanya tu yakupasayo kufanya sawasawa na Luka 17:10.

Luka 17:10  “Vivyo hivyo nanyi, mtakapokwisha kuyafanya yote mliyoagizwa, semeni, Sisi tu watumwa wasio na faida; tumefanya tu yaliyotupasa kufanya”.

Na kama tukiingia mkataba huo na Mungu wa kupokea haki yetu kwa matendo yetu, basi tunazo sababu nyingi za kulipwa mabaya kuliko mema. Kwasababu Mungu siku zote ni  wa haki.

Lakini kama mara nyingi Mungu anatuvumilia kwa mabaya yetu tunayoyafanya sawasawa na Zaburi 130:3  “Bwana, kama Wewe ungehesabu maovu, Ee Bwana, nani angesimama? Lakini kwako kuna msamaha, Ili Wewe uogopwe”…basi na sisi hatuna budi kutoyatumainia mema yetu tunayoyafanya!.

Ndio hapa sasa panazaliwa kitu kinachoitwa NEEMA!... Neema tafsiri yake ni upendeleo maalumu usiokuwa na sababu. Kwamba unapokea tu kitu kutoka kwa Mungu pasipo matendo yako.. Yaani Mungu anapenda tu kukupa si kwasababu wewe ni mtenda mema, au ni mwombaji sana, au ni mfungaji sana, au ni mhubiri mzuri… La!, bali anakutendea tu mema bila kwa upendo wake tu!, na huruma zake na kupenda kwake.

Ndio maana hatuna budi kila siku KUOMBA NEEMA YA MUNGU ije juu yetu. Kwasababu tukiipata hiyo tumepata kila kitu.

Usijivune, bali omba neema kwasababu Mungu huwapinga wenye kiburi na kuwapa wanyenyekevu Neema yake (1Petro 5:5).

Afya uliyonayo ni kwa neema tu, Uzima ulio nao ni kwa Neema tu, karama uliyo nayo ni kwa neema tu, zaidi sana hata Wokovu ulio nao ni kwa Neema tu na wala si kwa matendo yako.

Waefeso 2:8 “Kwa maana mmeokolewa kwa neema, kwa njia ya imani; ambayo hiyo haikutokana na nafsi zenu, ni kipawa cha Mungu;

9  wala si kwa matendo, mtu awaye yote asije akajisifu”

Na zaidi ya yote pia Roho Mtakatifu tunampokea kwa Neema..

Wagalatia 3:2 “Nataka kujifunza neno hili moja kwenu. Je! Mlipokea Roho kwa matendo ya sheria, au kwa kusikia kunakotokana na imani”

Omba Neema!!.. omba Neema!, Omba Neema…usitumainie matendo yako..

Bwana akubariki.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

NINI TOFAUTI KATI YA MATENDO YA SHERIA NA MATENDO YA IMANI?

NEEMA YA MUNGU KWA MARIAMU.

FUNDISHO KUU LA NEEMA YA MUNGU KWETU.

Kama tunaokolewa kwa neema kwanini wokovu tuupate kwa nguvu?

Nini tofauti ya Uwezo na Uweza kibiblia?

Rudi nyumbani

Print this post

HISTORIA YA BIBLIA YA KING JAMES, INA FUNZO GANI KWETU?

Jina la Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo libarikiwe.

Karibu tujifunze biblia, leo tujikumbushe historia fupi ya tafsiri ya biblia ya King James.

King James au kwa Kiswahili “Mfalme Yakobo” wa Uingereza, alikuwa ni mmoja wa wafalme ambao hawakuwa maarufu sana kwa wakati wao. Lakini alikuja kufanya jambo la kishujaa ambalo mpaka leo yupo katika rekodi ya watu maarufu na wakihistoria waliowahi kutokea Uingereza.

Mwaka 1604 baadhi ya wanazuoni wa Kiprotestanti (Wapuriti) walipendekeza kuchapishwa kwa tafsiri mpya ya biblia, kuchukua nafasi ya ile iliyokuwepo ambayo ilijulikana kama tafsiri ya “Geneva”. Tafsiri ya Geneva ndio ilikuwa tafsiri ya kwanza kwa lugha ya kiingereza kuchapichwa huko Ulaya, iliyotumiwa na Waprotestanti.

Upungufu wa tafsiri hiyo ya Geneva, ni kwamba ilikuwa ina “maoni ya ziada” yaliyoongezwa ili kutilia mkazo kile kilichoelezwa katika biblia, na maoni hayo ya mkazo, yalilenga sana kuwakosoa viongozi wa kisiasa na kidini.

Hivyo baadhi ya waprotestanti hao, jamii ya Wapuriti, walitoa mapendekezo yao kuchapiswa biblia nyingine ambayo itaondoa hayo maoni ya watu na kuiacha yenyewe kama yenyewe, pasipo maoni ya watu. Na pia chapisho hilo litalenga pia kuitafsiri biblia nzima katika kingereza kizuri zaidi.

Wapuri hao baada ya kutoa hilo pendekezo, walilifikisha kwa Mfalme ambaye alikuwa anaitwa YAKOBO (King James).

Kikawaida wafalme wengi huwa hawajihusishi na masuala ya kiimani, zaidi sana huwa wanayapinga, lakini ikawa ni kinyume chake kwa huyu King James, badala ya kulipinga au kulikosoa wazo lao, yeye alikubali biblia mpya hiyo ichapishwe na tena akatoa sehemu kubwa ya hazina ya utajiri wake kusaidia zoezi zima la utafsiri mpya.

Tafsiri hiyo mpya ya Biblia hiyo mpya iliandaliwa kwa kipindi cha Miaka 7, na wanazuoni zaidi ya 47 kutoka kila mahali, Uingereza.  Walianza kuitafsiri biblia upya kutoka katika Lugha ya kigiriki kwa agano la kale, na kiaramu kwa agano jipya. Walipomaliza kuitafsiri biblia yote wakaiita biblia hiyo KING JAMES BIBLE, Yaani biblia ya Mfalme Yakobo.

Baada ya kumaliza kutafsiri, kazi ile ilionekana kama dhaifu sana, lakini muujiza ni kwamba ndani ya kipindi kifupi, tafsiri hiyo mpya ya King James, ilianza kupendwa na watu wengi, kwani haikuwa na mchanganyiko wa maoni ya watu, na ilikuwa na kiingereza kikamilifu na haikuongeza neno wala kupunguza Neno.

Kufikika Mwaka 1611, tafsiri ya King James ilikuwa imeshasambaa katika bara la Ulaya yote, na baadaye duniani kote. Na tangu mwaka huo wa 1611 mpaka leo karne ya 21 ndio kitabu kinachoongoza kwa kuuzwa kuliko vitabu vyote duniani, na kumfanya Mfalme James, kuendelea kushika nafasi za juu za watu maarufu waliowahi kutokea.

Ni nini tunajifunza katika Mfalme Yakobo (King James).

Ni Mfalme ambaye alikuwa na hofu ya Mungu, ingawa hakuwa mkamilifu sana, lakini alitii na kuheshimu pendekezo la watu wa Mungu, ambao walimshauri aridhie ombi la kukitakasa kitabu kitakatifu cha Bwana, kwa kuondoa maoni ya watu na kukiacha kisafi kama kilivyo.

King James, aliruhusu pendekezo hilo pasipo kujua kuwa litaenda kuubadilisha ulimwengu. Mpaka Leo hii tafisiri bora ya kiingereza inayosomwa na wengi ni tafsiri hiyo ya King James. Na kwa kufanya hivyo Bwana akampa King James kumbukumbu la daima.

Ni wafalme wengi na mamalkia wengi wamekuja na kupita, wameandika vitabu lakini vitabu vyao vimepita, lakini kazi ya James mpaka leo inadumu na itaendelea kudumu hivyo mpaka Kristo anarudi.

Na sisi tukitaka tupate kumbukumbu la kudumu hatuna budi kumfikiri Mungu kwanza katika maisha yetu, haijalishi ngazi tuliyopo tuwe maskini, matajiri, tuwe wafalme tuwe watu wa kawaida.. tukimjali Bwana kwa mioyo yetu yote, na akili zetu zote na nguvu zetu zote, bali tuna kumbukumbu kubwa mbele zake si tu katika maisha haya, bali hata yale yajayo.

Malaki 3:13 “Maneno yenu yamekuwa magumu juu yangu, asema Bwana. Lakini ninyi mwasema, Tumesema maneno juu yako kwa namna gani?

 14 Mmesema, Kumtumikia Mungu hakuna faida; na, Tumepata faida gani kwa kuyashika maagizo yake, na kwa kwenda kwa huzuni mbele za Bwana wa majeshi? 

15 Na sasa twasema ya kwamba wenye kiburi ndio walio heri; naam, watendao uovu ndio wajengwao; naam, wamjaribuo Mungu ndio waponywao.

 16 Ndipo wale waliomcha Bwana waliposemezana wao kwa wao. Naye Bwana akasikiliza, akasikia; na kitabu cha ukumbusho kikaandikwa mbele zake, kwa ajili ya hao waliomcha Bwana, na kulitafakari jina lake.

 17 Nao watakuwa wangu, asema Bwana wa majeshi, katika siku ile niifanyayo; naam, watakuwa hazina yangu hasa; nami nitawaachilia, kama vile mtu amwachiliavyo mwanawe mwenyewe amtumikiaye”.

Bwana atubariki.

Maran atha.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

Dina akatoka kuwaona binti za nchi. (Mwanzo 34:1)

Biblia inamaana gani iliposema “Dhambi ilipozidi, Neema ilizidi kuwa nyingi Zaidi”.

WHAT DOES IT MEAN TO BE A CHRISTIAN?

Je ni viatu gani Musa aliambiwa avivue?  Vya mwilini au vya rohoni? (Kutoka 3:5).

NI UTUKUFU WA MUNGU KUFICHA JAMBO.

Rudi nyumbani

Print this post

WANNE WALIO WAONGO.

Biblia imetuonya imetutahadharisha vitu vitatu vilivyo na udanganyifu kuliko vitu vyote.

1.MOYO

Moyo wa mtu ndio kitu kilicho kidanganyifu kuliko vyote..

Yeremia 17:9 “Moyo huwa mdanganyifu kuliko vitu vyote, una ugonjwa wa kufisha; nani awezaye kuujua?”

Hakukuwa na shetani mwingine mbinguni aliyemdanganya shetani, bali kilichomdanganya shetani ni moyo wake mwenyewe… Moyo wake ulimtuma kuamini kuwa anaweza kuwa kama Mungu. Na hivyo akaufuata moyo wake na mwisho akaangukia upotevuni.

Na mioyo yetu sisi wanadamu ni midanganyifu sana, na mara nyingi inatuongoza pabaya…Mithali 16:2 “Njia zote za mtu ni safi machoni pake mwenyewe…” Na maandiko yanatufundisha kulinda mioyo yetu kuliko vyote tulindavyo, kwasababu huko ndiko zinakotoka chemchemi za uzima (Mithali 4:23).

Na tunailinda kwa kuangalia yale tunayoyasikia au tunayojifunza, na biblia ndio kitabu pekee cha kutusaidia kupima mambo yote.

2. DHAMBI.

Dhambi ni adui wa pili wa kumwongopa kuliko “shetani”. Na dhambi siku zote inadanganya, (inavutia kwa nje lakini mwisho wake ni Mauti, Warumi 6:23). Ulevi unaonekana kama unavutia lakini mwisho wake ni Mauti, Anasa zinaonekana kama zinavutia, lakini mwisho wake ni Mauti, Vivyo hivyo na Zinaa, na usengenyaji, na wizi, na rushwa n.k Vyote hivyo vinavutia kwa nje lakini ndani yake ni Mauti.

Waebrania 3:13 “Lakini mwonyane kila siku, maadamu iitwapo leo; ili mmoja wenu asifanywe mgumu kwa UDANGANYIFU WA DHAMBI”.

3. SHETANI.

Maandiko yanasema wazi kuwa shetani ni baba wa Uongo.

Shetani atakuambia kuabudu sanamu si dhambi, kunywa pombe si dhambi, kuupenda ulimwengu si dhambi, kujiburudisha kwa anasa si dhambi n.k  Na kumbe anasema Uongo, kwasababu yeye ni baba wa huo, ndivyo alivyomdanganya Hawa na ndivyo anavyoendelea kudanganya watu mpaka leo.

Yohana 8:44 “Ninyi ni wa baba yenu, Ibilisi, na tamaa za baba yenu ndizo mpendazo kuzitenda. Yeye alikuwa mwuaji tangu mwanzo; wala hakusimama katika kweli, kwa kuwa hamna hiyo kweli ndani yake. Asemapo uongo, husema yaliyo yake mwenyewe; kwa sababu yeye ni mwongo, na baba wa huo”

4. MALI

Maandiko pia yanasema kuwa Mali zinadanganya!.. Mali zinasema ukizipata utaheshimika, ukizipata utapendwa, ukizipata utaishi vizuri.. jambo ambalo si kweli, Kristo pekee ndiye ukimpata mambo yote, yatakuwa sawa hata pasipo hizo mali… Kama alisema “mtu hataishi kwa mkate tu, bali Neno la Mungu”…si zaidi Mali???.

Lakini Mali zenyewe zinatuhubiria kinyume chake kuwa pasipo hizo, maisha yetu hayawezi kwenda au yatakuwa ya shida, maisha yetu yatakuwa ya tabu na mateso…

kwahiyo kama hatutaongeza umakini katika kumjua Mungu na uweza wake tutadanganyika na udanganyifu huo ambao Mali zinauhubiri.. tutajikuta tunatumia muda mwingi kuzisaka na kutumia muda mchache kumtafuta Mungu.. na hivyo kupotea..

Mathayo 13:22  “Naye aliyepandwa penye miiba, huyo ndiye alisikiaye lile neno; na shughuli za dunia, na UDANGANYIFU WA MALI hulisonga lile neno; likawa halizai”.

Mali zisikudanganye na kukupotezea muda wako mwingi, Mali zisikuambie kuwa usipoenda kuzisaka siku ya jumapili utakufa njaa!!, mali zisikudanganye kuwa usipotumia usipotumia muda mwingi kuzisaka basi zitakukimbia!!..  Jihadhari na udanganyifu huo.

Bwana atubariki na kutusaidia.

Maran atha!

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

MBINGUNI YUPO NANI SASA?

Kwanini Paulo aungane na wale watu wanne wenye nadhiri?

Heri walio maskini wa roho; Maana ufalme wa mbinguni ni wao.

KWA WALE WALIO NJE “YOTE” HUFANYWA KWA MIFANO.

Sadaka ya Moyo ipoje? (Walawi 22:21).

Rudi nyumbani

Print this post

MAJARIBU 10 WANA WA ISRAELI WALIYOMJARIBU MUNGU.

Hesabu 14:22 “kwa sababu watu hawa wote, ambao wameuona utukufu wangu na ishara zangu, nilizozitenda huko Misri, na huko jangwani, pamoja na haya WAMENIJARIBU MARA HIZI KUMI, wala hawakuisikiza sauti yangu; 

23 hakika yangu hawataiona hiyo nchi niliyowaapia baba zao, wala katika hao wote walionidharau hapana atakayeiona;

24 lakini mtumishi wangu Kalebu, kwa kuwa alikuwa na roho nyingine ndani yake, naye ameniandama kwa moyo wote, nitamleta yeye mpaka nchi hiyo aliyoingia; na uzao wake wataimiliki”

Maandiko yanaonyesha kuwa wana wa Israeli walimjaribu Mungu MARA KUMI, je ni wapi katika maandiko panaonyesha hayo?

1. JARIBU LA KWANZA: (Mkabala na bahari ya Shamu)

Kutoka 14:9 “Wamisri wakafuata nyuma yao, farasi zote na magari yote ya Farao, na askari zake wenye kupanda farasi, na jeshi lake, nao wakawapata hali wamepanga pale karibu na bahari, karibu na Pi-hahirothi, kukabili Baal-sefoni. 

10 Hata Farao alipokaribia, wana wa Israeli wakainua macho yao, na tazama, Wamisri wanakuja nyuma yao; wakaogopa sana; wana wa Israeli wakamlilia Bwana. 

11 Wakamwambia Musa, Je! Kwa sababu hapakuwa na makaburi katika Misri umetutoa huko ili tufe jangwani? Mbona umetutendea haya, kututoa katika nchi ya Misri?

12 Neno hili silo tulilokuambia huko Misri”

Hili ndio jaribu la Kwanza wana wa Israeli walilomjaribu nalo Mungu, ijapokuwa walishaona matendo yake makuu kwa Farao na Misri yote kwa ujumla jinsi alivyoipiga Misri na kuiharibu kwa ishara kubwa na maajabu mengi, lakini hapa wanamjaribu Mungu kuangalia kama atawapigania tena kinyume na Farao au la!.. jambo ambalo ni dhambi kwao kwani tayari wanaujua uweza wa Mungu na hivyo hakuna haja ya kumjaribu ili kuona atakachokifanya.

2. JARIBU LA PILI: (Maji ya Mara)

Kutoka 15:22 “Musa akawaongoza Israeli waende mbele kutoka Bahari ya Shamu, nao wakatokea kwa jangwa la Shuri; wakaenda safari ya siku tatu jangwani wasione maji.

 23 Walipofika mahali palipoitwa Mara hawakupata kuyanywa yale maji ya Mara, kwa kuwa yalikuwa machungu; kwa ajili ya hayo jina lake likaitwa Mara. 

24 Ndipo watu wakamnung’unikia Musa, wakisema, Tunywe nini?

25 Naye akamlilia Bwana; Bwana akamwonyesha mti, naye akautia katika hayo maji, maji yakawa matamu. Basi akawawekea amri na hukumu huko, akawaonja huko”

Hili ni jaribu la pili, baada ya kuona uweza wa Mungu wa kupasua bahari, lakini bado wakamjaribu Mungu kuangalia kama atawafanyia muujiza wa Maji au la.. Na Bwana akawapa maji kama walivyotaka lakini bado hawakuridhika…

3. JARIBU LA TATU: (Katika bara ya Sini, kutaka Nyama)

Kutoka 16:1 “Kisha wakasafiri kutoka Elimu, na mkutano wote wa wana wa Israeli wakafikilia bara ya Sini, iliyoko kati ya Elimu na Sinai, siku ya kumi na tano ya mwezi wa pili baada ya kutoka kwao nchi ya Misri

2 Na mkutano mzima wa wana wa Israeli ukawanung’unikia Musa na Haruni, huko barani; 

3 wana wa Israeli wakawaambia, Laiti tungalikufa kwa mkono wa Bwana katika nchi ya Misri, hapo tulipoketi karibu na zile sufuria za nyama, tulipokula vyakula hata kushiba; kwani mmetutoa huko na kututia katika bara hii, ili kutuua kwa njaa kusanyiko hili lote.”

Hili ni jaribu la tatu baada ya kumjaribu Bwana kwa maji ya Mara na sasa wanataka kumwangalia Bwana kama anaweza kuwafanyia muujiza wa Nyama katikati ya jangwa, na Bwana akawapa nyama, kama walivyotaka lakini bado hawakuchoka kumjaribu..

4. JARIBU LA NNE: (Kusaza kwa Mana).

Kutoka 16:19 “Musa akawaambia, Mtu awaye yote asikisaze hata asubuhi.

 20 Lakini hawakumsikiza Musa; wengine miongoni mwao wakakisaza hata asubuhi, nacho kikaingia mabuu na kutoa uvundo; Musa akawakasirikia sana”

Walipewa maagizo wasikisaze (yaani wasibakishe chochote mpaka asubuhi) lakini wao wakafanya kinyume chake kwa kusudi la kuchunguza ni nini kitatokea.

5. JARIBU LA TANO: (Ukusanyaji wa Mana siku ya Sabato)

Kutoka 16:26 “Siku sita mtaokota; lakini siku ya saba ni Sabato, siku hiyo hakitapatikana. 

27 Ikawa siku ya saba wengine wakatoka kwenda kukiokota, wasikione. 

28 Bwana akamwambia Musa, Mtakataa kuyashika maagizo yangu na sheria zangu hata lini? “

Mungu aliwaambia wasitoke kwenda kuokota Mana siku ya Sabato, bali wapumzike, kwasababu hiyo mana haitapatikana siku hiyo, lakini wenyewe wakatoka kwenda kuhakiki kama kweli haitapatikana?.. hivyo ikawa ni dhambi kwao.

6. JARIBU LA SITA: (Maji ya Refidimu).

Kutoka 17:1 “Mkutano wote wa wana wa Israeli ukasafiri, kutoka bara ya Sini kwa safari zao, kama Bwana alivyowaagiza, wakatua Refidimu; napo hapakuwa na maji, watu wanywe.

2 Kwa hiyo hao watu wakateta na Musa, wakasema, Tupe maji tunywe. Musa akawaambia, Kwani kuteta na mimi? Mbona mnamjaribu Bwana?

3 Watu wakawa na kiu huko; nao wakamnung’unikia Musa, wakasema, Mbona umetupandisha kutoka Misri, kutuua sisi na watoto wetu na wanyama wetu kwa kiu?”

Baada ya kumjaribu Bwana kule Mara, kwa kutaka maji, sasa wanarudia tena yale yale makosa.. ya kutaka watokezewe maji ya kimiujiza..Kulikuwa hakuna haja ya kumjaribu Mungu mara ya pili, kwani tayari walishaona uweza wake mara ya kwanza, lakini wao walitaka kuona tena na tena..

7. JARIBU LA SABA: (Sanamu ya Ndama).

Kutoka 32:7 “Bwana akamwambia Musa, Haya! Shuka; kwa maana watu wako uliowatoa katika nchi ya Misri wamejiharibu nafsi zao,

8 wamepotoka upesi kuiacha ile njia niliyowaamuru, wamejifanyizia ndama ya kuyeyusha wakaiabudu na kuitolea dhabihu, wakasema, Hiyo ndiyo miungu yako, Ee Israeli, iliyokutoa katika nchi ya Misri”

Wametoka kunywa maji kimiujiza katika Mwamba, na kuhakiki kwamba Bwana yupo katikati yao, lakini hapa wanafanya makusudi kutengeneza sanamu ya Ndama, kama ishara ya kumsusia Mungu, ambaye wanajua kabisa yupo..

8. JARIBU LA NANE: (Moto wa Tabera)

Hesabu 11:1 “Kisha hao watu walikuwa kama wanung’unikao, wakinena maovu masikioni mwa Bwana; Bwana aliposikia hayo, hasira zake zikawaka; na moto wa Bwana ukawaka kati yao, ukateketeza katika mipaka ya mwisho wa marago. 

2 Ndipo watu wakamlilia Musa; naye Musa akamwomba Bwana, na ule moto ukakoma.

3 Jina la mahali hapo likaitwa Tabera; kwa sababu huo moto wa Bwana ukawaka kati yao’

Manung’uniko haya ni yale ya kutafuta kuona kitu cha kimwujiza kutoka kwa Mungu, kwasababu walikuwa wameshajua kuwa Mungu anaweza kufanya lolote..

9. JARIBU LA TISA: (Tamaa ya Nyama)

 Hesabu 11:4 “Kisha mkutano wa wafuasi waliokuwa kati yao, wakashikwa na tamaa; wana wa Israeli nao wakalia tena, wakasema, N’nani atakayetupa nyama tule?

 5 Twakumbuka samaki tuliokula huko Misri bure; na yale matango, na matikiti, na mboga, na vitunguu, na vitunguu saumu;

 6 lakini sasa roho zetu zimekauka; hapana kitu cho chote; hatuna kitu cha kutumaini isipokuwa hii mana tu”

Wana wa Israeli wanataka nyama, si kwasababu walikuwa na njaa sana, bali kwasababu walikuwa wanataka kuona jambo jipya kutoka kwa Bwana..

10. JARIBU LA KUMI: (Wapelelezi wa Kaanani)

Hesabu 14:1 “Mkutano wote wakapaza sauti zao wakalia; watu wakatoka machozi usiku ule.

 2 Kisha wana wa Israeli wote wakamnung’unikia Musa na Haruni; mkutano wote wakawaambia, Ingekuwa heri kama tungalikufa katika nchi ya Misri, au, ingekuwa heri kama tungalikufa katika jangwa hili. 

3 Mbona Bwana anatuleta mpaka nchi hii ili tuanguke kwa upanga? Wake zetu na watoto wetu watakuwa mateka; je! Si afadhali turudi Misri?

4 Wakaambiana, Na tumweke mtu mmoja awe akida, tukarudi Misri”.

Hili ndilo jaribu la mwisho, wana wa Israeli walilomjaribu nalo Mungu, nalo ndilo likawa Muhuri wa wao kuipoteza ahadi ya kuiona ile nchi, isipokuwa watu wa wawili tu, ambao ni Yoshua na Kalebu.

Nasi pia tunachoweza kujifunza katika habari hiyo kuwa “KUMJARIBU MUNGU NI DHAMBI KUBWA SANA”.

Kama tumeshaujua uweza wake kwanini tumjaribu?.. kama tumeshajua kuwa Mungu anaweza kutuokoa na hatari kwanini tujiweke katika hatari??.. Kama tumeshajua kuwa Mungu anaweza kutuokoa na yule mwovu kwanini basi tujisogeze karibu na yule Mwovu??.. Kama tumeshajua kuwa “tutakapokula vitu vya kufisha, havitatudhuru, kwanini basi tuvile makusudi”, kama umeshajua kuwa Mungu ni mponyaji kwanini basi tunywe sumu makusudi?..

Kama umeshajua kuwa Bwana anakupenda kwanini ujiuze kwenye dhambi ili uujaribu upendo wake???.. unadhani utabaki salama?

Ndicho wana wa Israeli walichokuwa wanakifanya, pasipo kujua kuwa wanafanya dhambi kubwa sana, ambayo itawagharimu kukosa kuingia Kaanani.

Kumbuka Hili ndilo jaribu ambalo shetani anawaangusha nalo watu wengi hata siku hizi za mwisho, na ndilo hata alilolichagua kama moja kati ya majaribu yake matatu yenye nguvu kubwa, ili aweze kumwangusha Bwana Yesu lakini alishindwa!,

Mathayo 4:5 “Kisha Ibilisi akamchukua mpaka mji mtakatifu, akamweka juu ya kinara cha hekalu,

6  akamwambia, Ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu jitupe chini; kwa maana imeandikwa, Atakuagizia malaika zake; Na mikononi mwao watakuchukua; Usije ukajikwaa mguu wako katika jiwe

7  Yesu akamwambia, Tena imeandikwa, Usimjaribu Bwana Mungu wako.”

Na wewe usimjaribu Bwana, usiujaribu Msalaba.

Bwana akubariki.

Maran atha.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Mada Nyinginezo:

KWA MIOYO YAO WAKAREJEA MISRI.

JIHADHARI NA MKUTANO WA WATU WALIOCHANGANYIKANA.

MADHARA YA KUKOSA MAJI YA UZIMA BAADA YA KIFO.

Je Ni kweli haturuhusiwi kula nyama kulingana na Isaya 66:3?

UPEPO WA KUSI HULETA MVUA;

Rudi nyumbani

Print this post