Je unajua kuwa roho ya mpinga-kristo imeshaanza kutenda kazi na inaendelea kutenda kazi hata sasa?
1 Yohana 4:3 “Na kila roho isiyomkiri Yesu haitokani na Mungu. Na hii ndiyo roho ya mpinga Kristo ambayo mmesikia kwamba yaja; NA SASA IMEKWISHA KUWAKO DUNIANI”.
Andalizi la mwisho la Mpinga Kristo kabla ya chapa yake kuanza kufanya kazi ni hili “MUNGU HAANGALII MWILI BALI ROHO”.
Roho ya Mpinga-kristo inawaandaa sasa watu na hiyo saikolojia, kwamba waamini Mungu haangalii mwili bali roho tu.
Na kwanini anafanya hivyo?.. ni ili iwe vyepesi kwake siku ile kuwatia watu CHAPA mwilini (Usoni na mikononi)
Kwasababu asipowaandaa na hiyo saikolojia itakuwa kwake ni ngumu sana kuwashinikiza waipokee chapa katika vipaji vya nyuso na katika mwili siku zile baada ya unyakuo wa kanisa kupita.
Kwahiyo anaanza na saikolojia ndogo tu kwamba kuvaa hereni sio kosa, kutoboa pua sio kosa, kujichora tattoo na hina sio kosa na kupaka lipstick midomoni na wanja machoni sio dhambi.. ( kwamba Mungu hawezi kumhukumu mtu kwa vitu vinavyowekwa mwilini)
Ndugu usidanganyike, je! Umewahi kujiuliza kwanini Mungu atawahukumu watu wote watakaoipokea ile chapa ya mnyama katika VIPAJI vya nyuso zao na katika MIKONO yao siku ile?..
Kama Mungu haangalii mwili kwanini chapa ya 666 itiwe katika mwili na Mungu awahukumu wale wote watakaoipokea chapa hiyo?, maana maandiko yanasema watu wote watakaoipokea chapa hiyo katika vipaji vya nyuso zao au katika mikono basi watahukumiwa katika lile ziwa la moto (Ufunuo 14:9-10).
Sasa kama tu alama ya kishetani katika kipaji cha uso au katika sehemu ya mkono, inaweza kuwa sababu ya mtu kukataliwa na Mungu milele!, vipi hizo tattoo unazochora mwilini, vipi hizo hina unazozipaka na wanja unaoupaka machoni?, vipi hizo lipstick unazopaka mdomoni na rangi unazopaka kwenye kucha?… Vipi hizo hereni unazozining’iniza masikioni?.
Kama tu leo ni ngumu kuelewa kuwa kupaka wanja ni kosa kibiblia, utashawishikaje siku ile kuamini kuwa kuandikwa alama ya 666 kwenye kipaji cha uso wako ni kosa?..nataka nikuambie kuwa siku ile utaipokea tu chapa kama kawaida. Kama tu leo kutoboa masikio na kuweka hereni na kutoboa pua na kuweka pini huoni shida, utaonaje shida siku ile utakapotobolewa katika mkono wako na chipu kuwekwa mwilini mwako?.
Tafakari sana dada!!… tafakari sana kaka!! Tafakari sana Mama, tafakari sana Baba…Usiwe mwepesi kuiga mambo yanayoendelea na kuonekana ulimwenguni, hususani yanayofanywa na watu wengi!…(Mengi ya hayo yanaongozwa na roho ya mpinga kristo)…Ni kweli unajipenda, na ni vizuri kufanya hivyo, ni kweli unapenda uonekane vizuri na maridadi mbele za watu, ni vizuri pia kufanya hivyo lakini vipi na roho yako? Je itaendelea kubaki salama?.
Shetani amewafunga wengi macho siku hizi za mwisho wasiyaelewe maandiko! Na kuwaaminisha kuwa Mungu haangalii mwili bali anaangalia roho.
Dada usidanganyike! Kwasababu udanganyifu upo leo.. na utaendelea kuwepo mpaka wakati wa chapa ya mnyama.
Tupa hereni zote, kachome mawigi, ondoa pistick, na wanja machoni.
Bwana akubariki.
Maran atha!
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
Mada Nyinginezo:
UTENDAJI KAZI MWINGINE WA ROHO MTAKATIFU USIOUFAHAMU.
JE CHANJO YA KORONA NI ALAMA YA MNYAMA?
KUSAMBAA KWA ROHO YA MPINGA-KRISTO.
NIMEAZIMIA KUWAKUSANYA MATAIFA. NIPATE KUWAMWAGIA GHADHABU YANGU
Karibu tujifunze biblia, Neno la Mungu wetu lililo hai (Zab.119:105)
Je unaijua nguvu ya kinywa chako? Biblia inasema kuwa MAUTI na UZIMA huwa katika uwezo wa ULIMI. Na mtu awezaye kuutumia vizuri ulimi wake atakula matunda yake.
Mithali 18:21 “Mauti na uzima huwa katika uwezo wa ulimi; Na wao waupendao watakula matunda yake”.
Sasa ULIMI una matunda mawili tu!, ambayo ni “Uzima na Mauti”. Maana yake mtu anaweza kuutumia ulimi wake ukamletea UZIMA, lakini pia anaweza kuutumia na ukamletea MAUTI.
Yule kijana aliyempelekea Daudi habari za kifo cha Sauli, kinywa chake mwenyewe kilimletea “Mauti” (2Samweli 1:16) hali kadhalika Mfalme Yehoshafati alipokuwa katika hatari ya kufa, kwa kinywa chake mwenyewe alijiokoa. (2Nyakati 18:31).
Lakini leo nataka tuangalie faida za kutumia ULIMI katika eneo la MAOMBI.
Wengi tumezoea kuomba kimoyomoyo, jambo ambalo ni zuri lakini si wakati wote linafaa!!.. kuna mazingira ni lazima utumie kinywa chako kutoa maneno dhahiri yanayosikika!..Kuna ngome zinahitaji kusikia sauti ndipo zitii!, Kuna ngome zinahitaji kuamrishwa na kukemewa ndipo zitii (Kuta za Yeriko zilihitaji kelele nyingi ili zianguke)….Hali kadhalika katika imani inahitajika sauti ya kinywa ili kuthibitisha wokovu mtu alioupata…
Warumi 10:9 “Kwa sababu, ukimkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu, utaokoka.
10 Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu”.
Kwa hiyo si kila wakati maombi ya ukimya yanafaa… Ni lazima ujifunze kubadili gear unapoingia katika maombi ya vita, hata motokaa haisafiri kwa gear moja tu, ikienda hivyo itakwamaa mahali Fulani.
Sasa biblia inatufundisha kuwa “Mauti na Uzima” huwa katika uwezo wa kinywa. Maana yake ni kwamba tukitumia vizuri ndimi zetu wakati wa kuomba tunauwezo wa kuvihuisha vitu vingi vilivyokufa, na pia kuviua baadhi ya vitu visivyofaa maishani mwetu.
Tunaviuaje vitu visivyofaa?.. Tunaviua kwa “kuvitamkia kifo” kwa mfano ule ule wa Bwana Yesu alivyoutamkia ule Mtini, na ukafa wakati ule ule.
Mathayo 21:18 “Hata asubuhi alipokuwa akienda mjini, aliona njaa.
19 Akaona mtini mmoja kando ya njia, akauendea, asione kitu juu yake ila majani tu; AKAUAMBIA, YASIPATIKANE MATUNDA KWAKO TANGU LEO HATA MILELE. MTINI UKANYAUKA MARA.
20 Wanafunzi walipoona, walistaajabu, wakisema, Jinsi gani mtini umenyauka mara?
21 Yesu akajibu, akawaambia, Amin, nawaambia Mkiwa na imani, msipokuwa na shaka, mtafanya si hilo la mtini tu, lakini hata mkiuambia mlima huu, Ng’oka, ukatupwe baharini, litatendeka.
22 Na yo yote mtakayoyaomba katika sala mkiamini, mtapokea”.
Mstari wa 19 unasema “..akauambia, yasipatikane matunda kwako tangu leo hata milele, mtini ukanyauka mara.” Hapo Bwana Yesu aliuua huo mtini kwa kutumia kinywa chake. (Aliutumia ulimi wake na akala matunda yake), na anatuambia tukiwa na Imani tunaweza kufanya kama hayo na hata Zaidi ya hayo.
Hivyo na sisi ni lazima tujifunze kutumia Ndimi zetu kuua baadhi ya vitu ambavyo shetani kavipanda katika maisha yetu.
Unapoamka kusali Ua kazi za giza katika siku yako, unapotembea zihukumu kazi za giza kwa kutumia kinywa chako.. kwasababu unapotamka na kuamini moyoni mwako basi fahamu kuwa ni lazima yatokee hayo uliyoyasema.
Zitamkie mauti kazi za shetani katika utumishi wako, katika familia yako, katika watoto wako, katika shughuli zako, katika vitu vyako unavyomiliki, Usiishie tu kuomba kimya kimya pasipo kutoa maneno yoyote.. Paza sauti kwasababu kuna nguvu Mungu kaiweka katika ulimi wa mwanadamu.
Wachawi na mawakala wote washetani wanajua nguvu iliyopo katika ulimi, ndio maana wanautumia kuleta madhara makubwa katika maisha ya watu.. sasa na watu waliookoka ni lazima kutumia ulimi kutangua maneno yote yaliyonenwa au yanayonenwa kinyume na maisha yetu ya kiroho na kimwili.
Vile vile ni lazima tutumie Ndimi zetu kutamka UZIMA wa vitu vilivyokufa katika maisha yetu. Nabii Ezekieli aliambiwa aitabirie mifupa mikavu ili iweze kuwa na uhai tena, na katika maono yale aliitabiria mifupa ile kwa kinywa chake na ikarudia uzima na likaamka jeshi kubwa sana (soma Ezekieli 37:1-8).
Sehemu zote Bwana Yesu alipoenda kuponya wagonjwa alitumia kinywa chake kutamka, na sisi ni lazima tutumie vinywa vyetu kutamka uzima juu ya vitu viliyokufa ndani yetu. Ikiwa ni huduma, ikiwa ni karama, ikiwa ni shughuli unayoifanya, ikiwa ni watoto, au kitu kingine chochote kilicho chema ni sharti kipate uzima kupitia kinywa chako!. Fanya hivyo daima, usiache hata siku moja hata kama unaona kwa nje ni pakavu, endelea kwasababu vita vya kiroho si vita vya kimwili, na ukiwa na bidii kufanya hivyo mwisho utakula matunda ya ulimi wako.
Mithali 18:21 “Mauti na uzima huwa katika uwezo wa ulimi; Na wao waupendao watakula matunda yake”
Maran atha!
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
Mada Nyinginezo:
KWANINI MTINI KATIKATI YA MIZABIBU?
KAMA UNAPENDA MAISHA, NA KUTAKA SIKU YAKO IWE NJEMA.
Tofuati kati ya kifo na mauti ni ipi?
Jina la Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo libarikiwe, karibu tujifunze biblia Neno la Mungu wetu lililo taa ya miguu yetu na Mwanga wa njia yetu (Zab.119:105).
Ni muhimu kujua kanuni kadhaa za kuomba ili maombi yetu yawe na majibu.
Tumewahi kujifunza kanuni kadhaa huko nyuma na leo imempendeza Bwana tujifunze kanuni nyingine.
Neno la Mungu linasema yafuatayo katika kitabu cha Yakobo 4:2-3.
Yakobo 4:2 “ Mwatamani, wala hamna kitu, mwaua na kuona wivu, wala hamwezi kupata. Mwafanya vita na kupigana, wala hamna kitu kwa kuwa hamwombi!
3 Hata mwaomba, wala hampati kwa sababu mwaomba vibaya, ili mvitumie kwa tamaa zenu”.
Kumbe sababu ya kutopata yale tunayoyaomba ni jinsi tunavyoomba!.. (kwamba tunaomba vibaya!).
Na kuomba vibaya kunakozungumziwa hapo si kukosea kupangilia maneno wakati wa kuomba, bali ni kuomba kusikompendeza Bwana, ambako ni nje na mapenzi ya Mungu, mfano wa maombi hayo ni yale mtu anaomba Bwana ampatie fedha ili awe nazo awakomeshe wanaomdharau. (Maombi ya namna hii ni maombi mabaya, na mara nyingi hayana majibu)
Hivyo unapoomba zingatia mambo yafuatayo.
1.Kuwa na Nia Njema:
Nia njema, maana yake ni kusudi jema… Kama unahitaji Bwana akupe mafanikio Fulani ya kiroho au ya kimwili, hakikisha Nia yako ni njema, kwamba utokane tu na ugumu unaoupitia, na pia upate kitu cha kuwasaidia wengine, na si kwa lengo la kuwakomesha wanaokudharau. Ukiwa na Nia ya kupata vitu ili wengine waone, maombi hayo yanaweza yasijibiwe kabisa.
2. Mwombe Mungu mahitaji na si Fedha.
Wengi wetu tunapenda kupeleka maombi ya kupata fedha kutoka kwa Mungu.. Lakini kiuhalisia hayo si maombi bora. Tunasahau kuwa tunachokihitaji sana ni mahitaji yetu kama chakula, mavazi, makazi, afya na mengineyo, ambayo hayo Mungu anaweza kukutimizia pasipo fedha.
Ukiwa na haja ya chakula, mwambie Bwana naomba chakula na yeye anajua namna ya kukupatia hicho chakula kama kwa njia ya kukupatia fedha ukanunue, au kwa kukuletea mtu atakayekupa hicho chakula, (usikimbilie moja kwa moja kumwambia Bwana akupe fedha ya chakula), kwani yeye anazo njia nyingi za kukulisha wewe, si lazima kwa kutumia fedha.
Vile vile ukitaka mavazi, makazi, biashara, afya n.k Mwambie Bwana akupe vitu hivyo, na wala usiombe fedha za kupata mavazi, au za kupata makazi, au za kufanya biashara.. wewe mwambie naomba mavazi, yeye anajua jinsi ya kukupatia kama kupitia mlango huo wa fedha au kupitia watu yeye anajua, vile vile usiombe mtaji kwa Mungu, badala yake iombe ile kazi kwasababu wakati wewe unawaza kupata mtaji kwanza kumbe pengine Mungu amekuandalia mahali utakapoanza kufanya kazi pasipo mtaji.
Ukihataji Bwana akupe kifaa cha kazi au chombo za kukurahisishia usafiri, usimwambie Bwana akupe Pesa za kununua chombo hicho, badala yake mwombe Bwana akupe hicho chombo, kwa njia anayoijua yeye.
Ukitaka kusafiri usimwombe Bwana fedha za kusafiri, wewe mwombe akusafirishe, yeye atajua njia atakayotumia kukufikisha kule unakotaka kwenda, kama atanyanyua mtu na kukusafirisha kwa gharama zake au bure, au atafungua mlango wa wewe kupata fedha hizo, ila usijifunge kwa kanuni ya fedha.
Vile vile unapoumwa usimwombe Mungu pesa za matibabu, mwombe afya, yeye anajua njia atakayotumia kukupa hiyo afya, na mambo mengine yote, epuka Kutaja “Pesa” mbele za Mungu!!.. bali taja lile hitaji!.
Kwanini maombi mengi ya kuomba Pesa hayajibiwi?
Kwasababu kuna roho nyuma ya pesa, inayowasukuma watu katika tamaa mbaya za kidunia, na kuwatoa wengi kwenye Imani, ndivyo maandiko yanavyosema.
1Timotheo 6:10 “Maana shina moja la mabaya ya kila namna ni kupenda fedha; ambayo wengine hali wakiitamani hiyo wamefarakana na Imani, na kujichoma kwa maumivu mengi”
Ndio maana utaona asilimia kubwa ya watu waliopata pesa wanakuwa na kiburi!. Lakini waliopewa na Bwana ni wanyenyekevu. Mtu aliyezawadiwa baiskeli na yule aliyenunua baiskeli kwa fedha, utaona yule aliyenunua anakuwa na kiburi Zaidi ya yule aliyepewa. Ingawa wote wana baiskeli!.
Yule aliyezawadiwa nyumba na yule aliyejenga kwa fedha yake, utaona yule aliyejenga anakuwa na kiburi Zaidi ya yule aliyezawadiwa. Na mapenzi ya Mungu ni sisi tuwe wanyenyekevu na si watu wenye viburi, hivyo kamwe hawezi kukupa kitu ambacho baadaye kitakuja kukupa kiburi.
Ni wachache sana ambao Mungu anawabariki kwa fedha, kwasababu anajua tayari ameshawatengeneza mioyo yao, hawawezi kuwa na kiburi hata wawe na kiasi gani cha fedha, na hiyo naweza kusema ni asilimia 1% lakini wengi Mungu hawapi hizo fedha wanazozihitaji kwasababu anajua tamaa tulizo nazo. Na ukiona mtu ana fedha nyingi na ana kiburi (hizo fedha hajapewa na Mungu!!).
Kama mkristo biblia inatufundisha tusiwe watu wa kupenda fedha, wala kuzisifia wala kuzitukuza, badala yake tumtukuze Mungu na tumfanye Mungu siku zote kuwa MPAJI WETU (YEHOVA YIRE)!!. Kwamba fedha ziwepo au zisiwepo bado tutaishi, bado tutavaa, bado tutakula, bado tutamiliki vitu.. Tuliookoka tuna uwezo wa kuishi bila fedha wala vitu vilivyotukuzwa na wanadamu na bado tukawa na maisha bora kuliko watu wenye mambo hayo.
Mhubiri 5:10 “Apendaye fedha hatashiba fedha, Wala apendaye wingi hatashiba maongeo. Hayo pia ni ubatili”.
Bwana atusaidie.
Maran atha!
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
Mada Nyinginezo:
JE UMEJIANDAA KUTIMIZA UNABII UPI?
Ni kwa namna gani haki huinua taifa? (Mithali 14:34)
Ni lini na wapi Ibrahimu aliioona siku ya Bwana akashangilia?.
Mara nyingi tunapojikuta tumelala tunaposoma biblia, huwa moja kwa moja tunamsingizia shetani. Lakini ukweli ni kwamba shetani anahusika kwa sehemu ndogo, sehemu kubwa ni hali zetu za kimwili ndio zinakuwa adui katika jambo hili. Mazingira ambayo ni mashambulizi kutoka kwa adui mfano wake yanakuwa ni kama haya; pengine mtu akianza tu kusoma biblia anasikia maumivu makali kwenye kichwa, au mwili, lakini akiacha tu kusoma hali yake inarudia kama kawaida, au anaona giza au vitu kama mianga mianga kwenye macho na hivyo inamfanya asiweze kuisoma biblia, au kila anapotaka kusoma anapoteza hapo hapo kumbukumbu zote kwamba alikuwa anasoma biblia, na hatimaye anajikuta yupo usingizini, au anafanya mambo mengine kabisa, hiyo ndio mfano ya mashambulizi.. Na inahitaji kuombewa, au kushindana na hiyo roho hadi ikutoke.
Lakini ukijiona unaposoma biblia usingizi mzito umekukamata, unasinzia sinzia, unapiga piga miayo, huyo sio adui huo ni mwili wako, usiopenda mambo ya rohoni. Hivyo ni lazima uushinde huo.
Wagalatia 5:17 “Kwa sababu mwili hutamani ukishindana na Roho, na Roho kushindana na mwili; kwa maana hizi zimepingana, hata hamwezi kufanya mnayotaka”
Hivyo hizi ni njia ambazo zitakusaidia usilale pale unaposoma biblia.
Usipende kufungua biblia kama kitabu cha riwaya, unasoma tu utakavyo. Kumbuka yale ni maneno ya ROHO, na hivyo inahitaji umkaribishe Roho akusaidie. Hivyo usiwe mvivu wa kuomba, pata dakika, kadhaa za kufanya hivyo. Ni jambo ambalo nimejifunza sana, wakati nasoma biblia bila kuomba, na pale ninapoomba kisha nikaisoma, kuna tofauti kubwa sana ya kiuelewa na kiutulivu. Maombi pia yanasaidia kama kuna mashambulizi yoyote, basi yanatowekea hapo.
Ikiwa umechoka sana, si lazima usome biblia muda huo huo. Pendelea kuruhusu mwili wako upumzike vizuri, kwamfano umetoka kazini, umeshughulika kutwa nzima, ni rahisi sana kukabwa na usingizi muda huo huo usomapo biblia peke yako. Hivyo tumia busara, wahi kulala, kisha amka usiku. Ukilala hata masaa 3, mwili unapokea taarifa kuwa huyu mtu tayari alishapumzika. Hivyo ukiamka ukajimwagia maji, ukaketi utajiona unafuu mkubwa, na utapata kitu kikubwa kuliko kulizimisha mwili wakati umechoka.
Tafuta meza ukae, mwili wako uwe kama mtu aliye darasani, sio kama aliye hospitalini mgonjwa unasubiriwa kuhudumiwa. Kaa kwenye meza, kisha ndio usome biblia yako
Luka 12:35 Viuno vyenu na viwe vimefungwa, na taa zenu ziwe zinawaka
Kusoma kwa kuandika na kwa sauti, huwa kuna matokeo makubwa kuliko, kutumia tu macho yako. Hivyo andiko vifungu unavyovisoma, na ufunuo unaopata, itakuongezea umakini katika usomaji wako, na hivyo Roho Mtakatifu atapata nafasi ya kukufindisha kwa urahisi zaidi.
Ukiona huwezi kujiwekea ustaarabu wa kuzingatia ratiba yako ya usomaji, pendelea kujifunza na wengine. Kaa na familia yako, au ndugu zako, au rafiki yako katika Bwana jiwekeeni ratiba ya usomaji wa biblia pamoja, kisha mnachambua kile mlichojifunza, kwa namna hiyo itakusaidia sana kuielewa ..
Mathayo 18:20 “Kwa kuwa walipo wawili watatu wamekusanyika kwa jina langu, nami nipo papo hapo katikati yao”
Kusoma biblia sio mashindano kwamba ni lazima uimalize yote kwa siku moja, soma vifungu kadhaa, kisha tumia muda mwingi, kuvitafakari hivyo vilimaanisha nini. Roho Mtakatifu anapenda kutufundisha taratibu sana, hataki tuvuke madarasa ya juu wakati ya chini bado hatujayamaliza. Hivyo zingatia kusoma kwa muktadha wa kuelemishwa na Roho Mtakatifu, sio kumaliza silabasi. Kusoma vifungu vitano kwa dakika mbili, kisha ukavifakari kwa masaa 2, ni bora kuliko kusoma vifungu elfu kwa saa2, halafu hakuna tafakari yoyote.
Mfungo ni jambo zuri ambalo huupa mwili wepesi, kwasababu mwili unapotaabika kwa kunyimwa haja zake kwa kawaida roho yako huwa inakuja juu. Hivyo ukiwa katika kipindi cha mfungo, utaona wepesi Fulani wa kuisoma biblia kwa masafa marefu kidogo, kuliko kipindi kingine. Fungu mara kwa mara, au ukiwa unatamani wiki hiyo kuitumia vizuri usiku katika kusoma Biblia, basi hakikisha wiki hiyo yote unafunga, utajiona mwepesi sana hususani wakati wa usiku unapotulia.
Si kila jambo utaweza kulitatua tu peke yako mengine, utahitaji msaada, hivyo hakikisha maendeleo yako ya kiusomaji, kiongozi wako anayafahamu, hatua zako unamshirikisha mchungaji wako, itakusaidia sana, kupata ushauri au maombi , au ushuhuda kwa yale ambayo pengine usingeyafahamu uwapo peke yako. Na hiyo itakupa hamasa zaidi na shauku ya kusoma.
Bwana akubariki.
Hakikisha unasoma BIBLIA kila siku.
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
Mada Nyinginezo:
Jinsi ya kuandaa Somo la kufundisha
Tirshatha ni nini? (Ezra 2:63)
HEKIMA YA KIMUNGU, INAINGIAJE MIOYONI MWETU?
UFUNUO NI NINI, NA NITAPOKEAJE UFUNUO KUTOKA KWA MUNGU?
Biblia inamaana gani inaposema tutoapo unabii tutoe kwa kadiri ya imani?
Ni kanuni gani ya kuzingatia wakati wa kuhubiri/kufundisha ili usimzimishe Roho?.
Kuna vita vikubwa sana vya kiroho vinavyoinuka muda mchache kabla ya kusimama kufundisha/kuhubiri ambavyo ni lazima mkristo avijue na ajue jinsi ya kuvishinda ili injili ya Bwana isizuilike.
Baada ya kuandaa somo kwa kuongozwa na Roho Mtakatifu, hatua inayofuata ni wewe kwenda kuwasilisha ujumbe ulioupokea mbele ya mtu au watu. Sasa ni muhimu kujua kanuni za kuwasilisha ujumbe ili usije ukamzimisha Roho, kwasababu Roho Mtakatifu pia anaweza kuzimishwa ndani ya mtu na mtu mwenyewe, na shetani ndicho anachokitafuta hicho, lengo lake Injili isiwafikie wengine.
(Kumbuka shetani mwenyewe hawezi kumzimisha Roho Mtakatifu, kwasababu Roho Mtakatifu ana nguvu kuliko yeye), anachokifanya shetani ni kuzikoroga hisia za mtu ili zisiruhusu Roho Mtakatifu kufanya kazi ndani yake. Na neno linatuambia kuwa “tusimzimishe Roho”
1Wathesalonike 5:19 “Msimzimishe Roho”.
Wengi huwa wanamzimisha Roho Mtakatifu wakati wa kusimama kufundisha/kuhubiri pasipo wao kujijua..unakuta wakati wanaandaa somo/mahubiri wanakuwa katika uwepo mkubwa sana lakini wakati wa kufundisha au kuhubiri ule uwepo au ile hali ya kutiririka inapotea, na hivyo kumfanya huyu mtu ajihisi Mungu hayupo naye au kamwacha.
Kiuhalisia huyu mtu hajaachwa na Roho Mtakatifu, isipokuwa hali yake ya ndani imezuia utendaji kazi wa Roho Mtakatifu.
Sasa yafuatayo ni mambo ya kuzingatia ili Roho asizime ndani yako, (kule kutiririka kusikome), na ule ujumbe wa Roho Mtakatifu ulioupokea ufike kwa walengwa kama Roho alivyokufunulia.
1.Usijipange kwa maneno mengi.
Epuka kujipanga kwa maneno mengi; Maneno mengi yanazuia kutiririka kwa Roho Mtakatifu, wengi wanadhani kuwa na maneno mengi ndiko kueleweka, pasipo kujua kuwa anayewagusa watu na kuwafanya waelewe ni Roho Mtakatifu, hivyo ukifuata kanuni ya Roho Mtakatifu utaeleweka tu na utakuwa na matunda.
Unapojiandaa kwa maneno mengi, utajikuta unategemea yale maneno yako, na hivyo wakati Roho Mtakatifu anataka kuingiza mada nyingine katika akili yako wakati wa kufundisha ule ukuta wa maneno uliojiwekea unazuia kinywa cha Roho Mtakatifu kifanye kazi, na hivyo utajikuta unafundisha kwa akili zako, na yale maneno uliyoyaandaa yanapokwisha unajikuta na wewe umekauka, huna cha kusema Zaidi.
Kwahiyo jiandae kwa maneno machache tu!, hata kama unaona somo litakuwa ni fupi sana, Roho Mtakatifu ndio anataka iwe hivyo, ili hayo maneno mengine ayajazie yeye, ukiweka desturi hiyo siku zote utaona muda hautoshi, utaona daftari lako lina maneno machache uliyoyaandaa, lakini muda uliofundisha ni madakika mengi au masaa mengi, ukiona hiyo hali imekutokea jua sio wewe uliyekuwa unafundisha bali ni Roho Mtakatifu ndani yako.
2. Usifikiri fikiri.
Kufikikri fikiri ni nini utaenda kusema au kuhubiri, kunazima kinywa cha Roho Mtakatifu. Unapofika wakati wa kwenda kufundisha wengi huwa wanapaniki na kuwaza mara nyingi nyingi ni nini wataenda kusema, na hivyo kujikuta kulazimisha kupanga maneno ya kuzungumza kuanzia mwanzo hadi mwisho. Ukiona hiyo hali inakujua ndani yako dakika chache kabla ya kusimama kufundisha au kuhubiri ikatae!. Kwani ni adui anataka kutumia fikra zako kumzimisha Roho ndani yako.
Siku zote usijiangalie hali uliyonayo kifikra wakati wa kwenda kufundisha, hata kama hukumbuki chochote, wewe tulia mpaka wakati utakapofika wa kusimama, funga fikra zako kufikiri ni nini utaenda kufundisha au kuhubiri, ukiona mawazo hayo yanakujia hamisha fikra zako kwa kutafakari mambo mengine ya kiMungu au soma Neno, kwasababu wakati huo ndio wakati wa vita vikali, shetani anatumia nguvu kubwa sana kumshambulia mtu katika hii hatua.
Hivyo funga fikra zako na subiri ule wakati wa kufundisha Roho Mtakatifu atakupa cha kusema wakati ule ule utakaposimama kufundisha.
Kanuni kama hii Bwana Yesu aliwafundisha wanafunzi wake wakati wakipelekwa mbele ya watu wa Mataifa, akawaambia wasifikiri fikiri watakavyojibu kwani watapewa kinywa saa ile ile watakaposimamishwa.
Mathayo 10:19 “ Lakini hapo watakapowapeleka, msifikiri-fikiri jinsi mtakavyosema; maana mtapewa saa ile mtakayosema
20 Kwa kuwa si ninyi msemao, bali ni Roho wa Baba yenu asemaye ndani yenu”.
Kwahiyo na wewe usiwe mtu wa kufikiri fikiri utakavyosema, subiri ule muda utakapofika utapewa kinywa cha kusema, ambacho hata wewe mwenyewe utajishangaa.
3. Usijiangalie udhaifu wako na Jiachilie
Usijipime kwa kujiangalia udhaifu wako, kama unajua kuhubiri au la!, kama una kigugumizi au la!, kama una uzoefu au la!..Kwani kinywa chochote kilichovuviwa na Roho Mtakatifu kina nguvu kwasababu kimebeba ujumbe wa Roho Mtakatifu.
Hivyo kabla ya kwenda kufundisha weka kando udhaifu wako, weka kando kumbukumbu za nyuma ambazo unahisi uliwahi kukosea, weka kando hisia kwamba husikilizwi au hueleweki, au unapotezea watu muda.
Zungumza kile kinachokuja kinywani mwako muda ule kwa ujasiri wote, (achilia moyo wako na fikra zako), wala usijilinganishe na yeyote wala usitafute kufundisha kama mtu Fulani unayemjua, hapo utaona Roho Mtakatifua atakavyokutumia na utakavyomhisi akitenda kazi ndani yako kwa viwango vingine.
4. Usiongozwe na muda.
Ukiona hofu ya kuwahi kumaliza inaingia ndani yako, ikatae hiyo hali!.. Kwasababu ni mbinu nyingine ya shetani kumzimisha Roho Mtakatifu ndani yako (Kumbuka tena shetani mwenyewe hawezi kumzimisha Roho Mtakatifu, kwasababu Roho Mtakatifu ana nguvu kuliko yeye), anachokifanya shetani ni kuzikoroga hisia zako ili zisiruhusu Roho Mtakatifu kufanya kazi ndani yako.
Kwahiyo hofu ya muda ikatae. Kama umepewa lisaa la kufundisha, usianze kuwaza utasema nini kwenye hilo lisaa lote (hiyo sio kazi yako) ni kazi ya Roho Mtakatifu, ukianza kuwaza utasema nini muda wote huo wakati utakapofika hofu iliyopo ndani yako itamzuia Roho Mtakatifu kusema kupitia wewe. Wewe anza kufundisha kana kwamba utamaliza dakika tano zijazo, na utaona Roho Mtakatifu atakachokifanya!.. Kama atapenda umalize ujumbe kwa dakika hizo hizo tano, wala usiogope!, ndivyo alivyotaka yeye, na kama atakusudia ufundishe kwa kwa lisaa au masaa mawili, atakupa maneno na utashangaa yametoka wapi.. Kwahiyo ondoa hofu ya muda!.
5. Wahusishe watu katika kufundisha kwako
Hii ni njia nyingine ya kuendeleza uwepo uwepo wa Roho Mtakatifu usikatike ndani yako, tumia muda kuwauliza maswali unaowafundisha kama unaweza kufanya hivyo, au kuwapa jukumu la kusoma mistari ya biblia n.k
Hizi ni baadhi ya njia chache utakazoweza kuzitumia ili Kile Roho Mtakatifu alichokufunulia kiweze kuwafikia walengwa.
Kwahiyo kwa hitimisho ni kwamba kabla ya kwenda kusimama kufundisha ZILINDE SANA FIKRA ZAKO!.. Kwasababu hizo ndizo shetani anashughulika nazo kuharibu mambo.
Bwana akubariki.
Ikiwa hukupata somo la “Jinsi ya kuandaa somo basi wasiliana nasi kwa njia ya inbox”
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
Mada Nyinginezo:
Jinsi ya kuandaa Somo la kufundisha
Wanikolai ni watu gani? Katika biblia?
Je biblia inatufundisha wakristo kuwa na desturi?.
Jibu ni Ndio!, Biblia inatufundisha kuwa na desturi, ikiwa na maana kuwa desturi ina nyongeza kubwa sana katika Imani ya mkristo.
Sasa desturi ni nini?
Desturi ni kitu chochote mtu anachokifanya kwa kurudia rudia.(Ni Kanuni ya daima ya mtu)
Sasa si kila desturi ni nzuri lakini zipo chache zilizo nzuri, na leo tutaenda kutazama moja ambayo kila mkristo lazima awe nayo.
Hii ni desturi ya kwanza na ya msingi tunayopaswa kuwa nayo, ambayo biblia imeihakiki!
Kukusanyika katika ibada, semina, na mikutano ni jambo ambalo linapaswa liwe desturi ya kila mkristo (maana yake mtu akilala akiamka anapaswa ajue kuwa kukusanyika ni sehemu ya maisha yake) na si jambo la kuamua leo kukusanyika na kesho kutokukusanyika. Biblia inatufundisha kuwa ni lazima liwe desturi kwetu,…sasa utauliza hilo tunalisoma wapi katika biblia..
Waebrania 10:25 “WALA TUSIACHE KUKUSANYIKA PAMOJA, kama ilivyo DESTURI YA WENGINE; bali tuonyane; na kuzidi kufanya hivyo, kwa kadiri mwonavyo siku ile kuwa inakaribia”.
Umeona?
Kumbe kukusanyika ilikuwa ni desturi ya kundi Fulani la watu wa Mungu, na hapa biblia inatufundisha hayo hayo, kwamba na sisi tusiache kukusanyika KAMA ILIVYO DESTURI YA WENGINE. Maana yake inapaswa iwe desturi yetu na sisi, liwe jambo endelevu.
Kukusanyika ibadani hakupaswi kuwa tendo la leo kuamua na kesho kutoamua, bali linapaswa liwe desturi, iwe unajisikia au hujisikii, kukusanyika ni lazima iwe desturi yako, shetani amewafumba watu macho wasione kama kukusanyika ni desturi badala yake waone kama ni tendo kujisikia au kutojisikia, na hivyo kuwanyonyea Baraka zao!
Hivyo atakachokifanya ni kuwatengenezea udhuru na vijisababu kwenye vichwa vyao ili awawafanye wasikusanyike na wengine.
Zifuatazo ni sababu kuu nne (4) za kuzikataa na kuzikimbia ambazo zitaharibu desturi yako njema ya kukusanyika na wengine.. kwasababu zinatoka kwa shetani.
1.Nimechoka:
Hii ni sababu ya kwanza ya kuikataa kwasababu hata siku nyingine za wiki unakuwa umechoka lakini huachi kwenda kwenye majukumu yako. Kwahiyo kama ilivyo desturi yako kwenda kazini, basi na kwenda kanisani kufanye kuwa desturi yako.
2.Naumwa:
Hii ni sababu ya pili yenye nguvu inayotoka kwa shetani, hata kama unasikia kuumwa kiasi gani usiache kukusanyika ibadani, kwasababu huko huendi kuongeza ugonjwa bali kuuondoa, kwasababu ugonjwa uliopata umetoka kwa shetani na kanisani shetani hayupo!.
Kama utakuwa na uwezo wa kuamka na kwenda hospitali pamoja na kwamba ni mgonjwa, kwanini usiamke na kwenda kanisani mahali penye uponyaji wa kiungu?
3.Mvua:
Hii ni sababu ya tatu ya shetani, ambayo inaharibu desturi ya wengi ya kwenda ibadani. Mvua isikuzuie kwenda ibadani.. bali nunua mwavuli na makoti ya mvua, na dhamiria kuwa iwe jua au mvua ni lazima ufike ibadani, kama mvua haiwezi kukuzuia kwenda kutafuta riziki za kimwili kwanini ikuzuie kwenda kutafuta riziki za kiroho?
4.Dharura
Dharura ni kitu chochote kinachonyanyuka wakati wa wewe kwenda ibadani, na hizo zinaweza kuwa ni za kikazi, familia, na nyinginezo.. Utakuta mtu anapigiwa simu na kuombwa ahudhurie mahali Fulani, na pasipo aibu ya uso anakubali na ilihali anajua kabisa siku hiyo ni maalumu kwa Mungu wake kukusanyika na wengine, lakini mtu huyo huyo akipokea simu siku za kazi yupo radhi kukataa kuvunjiwa ratiba zake za kazini na kuiheshimu kazi yake, lakini Nyumbani kwa Mungu kwake si kitu, Ukatae huo udhuru utaharibu desturi yako iliyo njema.
Na zipo sababu nyingine nyingi, hizi ni chacche tu, lakini katika hizo zote kataa visababu lakini jenga Desturi.. Huenda Desturi yako leo imeharibiwa na shetani, lakini Bwana Yupo kukusaidia ndio maana unayasikia haya leo.
Unachopaswa kufanya kuanzia leo ni kuomba rehema na kisha kutendea kazi hiki unachokisikia kuanzia leo, weka ratiba ambayo haibadiliki. Kwasababu desturi ya kwenda kanisani imehakikiwa na Roho Mtakatifu kuwa ni desturi njema. Hatuhitaji kuongozwa na Roho Mtakatifu au kupokea maono ya kwenda kanisani au la! Biblia tayari imeshatuelekeza kuwa inapaswa iwe desturi yetu.
Maran atha!
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
Mada Nyinginezo:
Je ni kweli ilikuwa desturi ya Bwana kuishika sabato?(Luka 4:16)
TUSIIFUATISHE KAWAIDA YA ULIMWENGU HUU.
KATAA KUWA EUTIKO, WA KUSINZIA IBADANI.
SWALI: Nini maana ya huu mstari?
Mithali 14:23 “Katika kila kazi mna faida; Bali maneno ya midomo huleta hasara tu”
JIBU: Kitabu cha Mithali na Mhubiri ni vitabu vilivyobeba mafunzo mengi sio tu yale ya kiroho bali pia hata ya maisha ya kawaida. Mstari huo unaelezea uzito wa kitu kinachotendewa kazi zaidi ya kile kinachozungumzwa tu. Kwamfano hapo anaanza kwa kusema “katika KILA KAZI mna faida”.. Maana yake ni kuwa katika kazi yoyote (iliyonjema), inafaida nyuma yake,. Iwe ni ya kudharaulika au yenye heshima, iwe ni ngumu iwe ni rahisi, iwe ni ya kipato kikubwa au kidogo, maadamu kazi fulani inatendeka ni lazima faida tu itaonekana nyuma yake.
Lakini mtu akiwa ni wa mipango mikubwa, mikakati mingi, akili nyingi za kubuni namna ya kutenda kitu Fulani, vikao vingi, halafu hakitendei kazi, Bwana anasema, badala ya faida kinyume chake ni hasara tu atapata..
Vivyo hivyo na katika roho. Bwana anataka tuwe watendaji wa Neno lake, Sio kusikia tu au kuomba tu peke yake. Unaweza ukaomba usiku kucha lakini kama sio mtendaji wa Neno lake uliombalo, ni unapoteza nguvu tu.
Kwamfano unaomba Bwana akusaidie uushinde uasherati, lakini bado unashikamana na vichocheo vyake vyote, una picha chafu kwenye simu yako, kinywa chako kinazungumza mambo ya kizinzi na vijana wenzako, unachati na watu wa jinsia tofauti muda wote, unatazama tamthilia zenye maudhui hayo, unasikiliza miziki ya kidunia, unaishi na boyfriend/girlfriend. Unategemea vipi tamaa zisikutawale? Utaomba usiku kucha na hutaona matokeo yoyote, kwasababu hukitendei kazi kile unachokiomba.
Bwana alisema kama vile mwili bila roho umekufa, vivyo hivyo imani bila matendo imekufa ndani yake.(Yakobo 2:17). Kukitendea kazi kile kimoja ukiombacho, kina nguvu sana kuliko maneno elfu unayoweza kumwomba Mungu mwaka mzima.
Yakobo 1:22 “Lakini iweni watendaji wa neno, wala si wasikiaji tu, hali mkijidanganya nafsi zenu. 23 Kwa sababu mtu akiwa ni msikiaji wa neno tu, wala si mtendaji, mtu huyo ni kama mtu anayejiangalia uso wake katika kioo. 24 Maana hujiangalia, kisha huenda zake, mara akasahau jinsi alivyo”.
Shalom.
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
Mada Nyinginezo:
Nini maana ya “katika wingi wa hekima mna wingi wa huzuni”.
Nini maana ya huu mstari? “Yeye mwenyewe ataokolewa lakini ni kama kwa moto”
Mithali 14:4 ‘Zizi ni safi ambapo hapana ngombe;
Marijani ni nini katika biblia(Ayubu 28:18,Mithali 8:11)?
Nini maana ya mhubiri 9:11? si wenye mbio washindao katika michezo?
Isaya 46:3 “Nisikilizeni, enyi wa nyumba ya Yakobo, ninyi mlio mabaki ya nyumba ya Israeli, mliochukuliwa nami tangu tumboni, mlioinuliwa tangu mimbani;
4 na hata uzee wenu mimi ndiye, na hata wakati wenu wa mvi nitawachukueni; nimefanya, nami nitachukua; naam, nitachukua na kuokoa”.
Mstari huu wa faraja unatuonyesha fadhili za Mungu jinsi zilivyo nyingi kwa watu wake, Anaonyesha jinsi asivyoweza kuwaacha watu wake, tangu wakiwa tumboni mwa mama zao hadi kufikia uzee wao. Kila hatua ya maisha yupo nao, kila pito liwe rahisi au liwe gumu yupo nao, wakiwa watoto, wakafikia ujana, kisha nguvu zikaisha wakiwa wazee, Mungu yupo nao. Haleluya.
Daudi alilitambua hilo pindi alipoishiwa nguvu zake, akaandika…
Zaburi 37:25 “Nalikuwa kijana nami sasa ni mzee, Lakini sijamwona mwenye haki ameachwa Wala mzao wake akiomba chakula”.
Hivyo huna haja ya kuhofu kesho yako itakuwaje au uzee wako utaishaje, maadamu upo na Bwana, maadamu unamtumikia, siku hizo zikifika, atakuhifadhi Mungu wako. Mwingine anasema mpaka sasa sina mfuko wa mafao, na nguvu zangu zinakaribia kuisha, ni nani atakayenisaidia, ni nani atakayekuwa karibu na mimi? Jibu ni kuwa Bwana ndiye atakayekuwa karibu na wewe. Kwasababu tangu zamani ulimtumainia. Lakini hata kama utakuwa na mali, huwezi kuwa na raha moyoni wakati huo endapo Kristo hayupo nafsini mwako sasa.
Hivyo wekeza maisha yako kwa Bwana sasa, ili kesho yako pia iwe na matumaini na raha tele. Ikiwa wewe ni kijana wakati huu uliopo, mtafute muumba wako, upokee WOKOVU kwa kumaanisha kabisa kuuacha ulimwengu, mtumikie Mungu, kimbia kweli kweli tamaa za ujanani, kabla zile nyakati mbaya za hatari hazijafika, Kwasababu maandiko yanasema kuna siku-mbaya mbeleni zitawakumba watu ambao hawakumcha Mungu tangu zamani.
Mhubiri 12:1 “Mkumbuke Muumba wako siku za ujana wako, Kabla hazijaja siku zilizo mbaya, Wala haijakaribia miaka utakaposema, Mimi sina furaha katika hiyo”.
Ikiwa upo tayari kutubu dhambi zako leo , na kumkaribisha Bwana Yesu maishani mwako, basi bofya hapa kwa mwongozo wa sala hiyo ya toba >>>> KUONGOZWA SALA YA TOBA
Bwana akubariki.
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
Mada Nyinginezo:
TUTAMKARIBIA MUNGU KWA IDADI YA MVI ZETU ROHONI.
Je! Wana wenu huwatoa kwa nani? maana yake ni nini?
NINYI AKINA BABA MSIWACHOKOZE WATOTO WENU
UFANYE WEMA WAKO KATIKA MAARIFA.
Praitorio ni nini? Na Kwanini ilikuwa ni najisi kwa wayahudi kuingia humo? (Yohana 18:28)
Ayubu 5:6 “Kwani taabu haitoki mchangani, Wala mashaka hayachipuki katika nchi;”
Watu wengi tumekuwa tukilaumu mazingira, tukilaumu wanyama, tukilaumu ardhi, na vitu vingine vya asili kuwa ndio chanzo cha matatizo yetu, chanzo ya shida zetu na mashaka yetu rohoni. Lakini maandiko yanatupa uhalisia kwamba taabu na mashaka havichupuki ardhini, kama vile mchicha umeavyo, bali vinatoka ndani yetu wenyewe.
Makosa yetu ndio zao la kila aina ya matatizo yetu. Asili ya migogoro katika ndoa, sio ule m-buyu uliokaribu na nyumba zetu. Unaweza kuhama hata nchi ukakaa chini ya mizeituni na mizabibu mizuri, na maua, lakini bado ndoa yako ikaendelea kuwa na matatizo tena makubwa zaidi hata yale ya mwanzo.
Sababu ya kuteswa na mapepo, sio Yule paka mweusi wa jirani anayekuja kulala batini kwako kila siku usiku. Bali ni kwasababu Kristo hayupo ndani yako.
Sababu ya kutokupiga hatua kiroho, sio hiyo ardhi unayoishi, au unayoimiliki, usihangaike na maombi ya kufungua/ kukomboa ardhi, hangaika na vifungo vilivyomo ndani yako. Ambavyo vinatokana na aidha kutolielewa Neno la Mungu, au kuwa nje ya wokovu.
Biblia inasema..
Yohana 8:36 Basi Mwana akiwaweka huru, mtakuwa huru kweli kweli.
Na tena inasema…
Yohana 8:32 “tena mtaifahamu kweli, nayo hiyo kweli itawaweka huru”.
Rekebisha mwenendo wako, pokea wokovu wa kweli, kisha liishi Neno la Kristo kila siku. Hakika utaona jinsi tatizo lako linavyotalika kirahisi, ndipo utaacha kuyalaumu mazingira ya nje.
Ayubu 5:6 “Kwani taabu haitoki mchangani, Wala mashaka hayachipuki katika nchi;”
Je! Umeokoka? Kama bado unasubiri nini? Je! Unatambua kuwa hizi ni siku za mwisho, na Kristo yupo mlangoni kurudi, tunaishi katika muda wa nyongeza tu, siku yoyote unyakuo wa kanisa unapita, watakatifu kuchukuliwa mbinguni na wenye dhambi kwenda motoni?. Fanya uamuzi sahihi sasa, ikiwa upo tayari kuokoka leo, basi fungua hapa kwa mwongozo huo >>> KUONGOZWA SALA YA TOBA
Bwana akubariki.
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
Mada Nyinginezo:
MTU MWENYE KUSITA-SITA KATIKA MAWAZO MAWILI.
LAKINI WAKATI WA TAABU WATASEMA, SIMAMA UKATUOKOE.
Rafiki hupenda sikuzote; Na ndugu amezaliwa kwa siku ya taabu.
VITABU VYA BIBLIA: Sehemu ya 9 (Kitabu cha Ayubu).
Shalom, nakusalimu katika jina la Yesu Kristo mwokozi wetu. Karibu tujifunze maneno ya uzima maadamu siku ile inakaribia.
Katika siku hizi za mwisho ni lazima uwe makini sana na mahali ulipo, kwasababu zama zimebadilika, si kila jambo la kuliamini, vilevile si kila jambo la kutoliamini. Unamuhitaji Roho Mtakatifu sana kukusaidia kuchagua kilicho sahihi.
Bwana anatufananisha sisi na kama kondoo, na yeye kama mchungaji. Na sikuzote, mchungaji mwema, huwa anawapeleka kondoo wake katika maji ya mito-salama. Na si kila mto ilimradi mto tu anawapeleka kondoo zake kunywea maji hapana, bali pale tu palipo na maji ya utulivu ndipo anapowapeleka kondoo zake.
Ndio maana katika Zaburi ya 23 Inasema;
Zaburi 23:1 ‘Bwana ndiye mchungaji wangu, Sitapungukiwa na kitu. 2 Katika malisho ya majani mabichi hunilaza, Kando ya maji ya utulivu huniongoza’.
Ni kwanini maji ya utulivu, kwasababu maji yenye mvurugano, au yaliyotibuliwa yana hatari nyingi, huwenda ni makao ya viboko na mamba na hivyo kutembea kwao huko ndio kunafanya maji Yale yawe na mvuragano, kwahiyo kondoo akinywa maji pale yupo hatarini kuvutwa na mamba, akafanyika kitoweo.
Au huwenda maji hayo ni mkondo wa mafuriko, hivyo kitu chochote kitakachotelezea kule mtoni, si rahisi kupona kinyume chake ni kitasombwa na kupotelea mbali.
Hivyo maji yasiyotulia, si salama kwa mifugo. Na mchungaji apendaye kondoo huwa hawapeleki mifugo yake hapo.
Ndivyo ilivyo kwa Kristo, anapotuokoa, anatuongoza kwa Roho wake malipo na maji ya utulivu tukae hapo tunywe. Lakini tatizo linakuja ni sisi kuyakataa maji ya utulivu, tunayatafuta maji ya mivurugano.
Ndugu usiangalie ukubwa wa mto, au ukubwa wa Bwawa, haikuhitaji wewe kunywa mto mzima ndio ukate kiu yao. Naamanisha usiangalie wingi wa watu, au ukubwa wa jengo na madhabahu iliyopambwa, au utajiri wa kanisa ndio ufikiri kuwa hapo ni salama kwa roho yako. Bali tazama palipo na utulivu wa kiroho. Hapo ndipo utulize nafsi yako. Kwasababu unaweza kwenda mahali kwa lengo la kuikata kweli kiu yako kwa Bwana lakini kinyume chake ukakutana na mamba wakali wakakumaliza kabisa.
Palipo na maji salama ni wapi?
Kwanza ni pale Palipo na fundisho la Yesu: Yesu ndio maji yenyewe tulivu ya uzima, na sio nabii au mtume au askofu, au kanisa, au pesa, au umaarufu.. Hivyo angalia kiini cha fundisho unalofundishwa mahali ulipo, je yote yanalenga kukukuza kumjua Yesu au linakupeleka katika mambo mengine? Fikiri Tangu umekaa hapo, ni nini umeongeza katika kulijua Neno la Kristo katika kweli yote. Lakini Kama umejazwa maarifa ya ki-mwili tu zaidi yale ya Kristo, yaani ya ki-ndoa, ki-uchumi, uchawi, biashara,pesa, hiyo ni injili nyingine, ni mafuriko ya adui, hakuna maji tulivu hapo, utazombwa na kuangamia kabisa.
Yohana 4:13 “Yesu akajibu, akamwambia, Kila anywaye maji haya ataona kiu tena; 14 walakini ye yote atakayekunywa maji yale nitakayompa mimi hataona kiu milele; bali yale maji nitakayompa yatakuwa ndani yake chemchemi ya maji, yakibubujikia uzima wa milele”
Palipo na Upendo: Hicho ni kigezo cha pili.
Yakobo 3:16 “Maana hapo palipo wivu na ugomvi ndipo palipo machafuko, na kila tendo baya”.
Katika mkusanyiko wowote, fundisho la tendo la upendo wa ki-ndugu linapuuziwa, au halihimizwi, ndani kuna vita visivyokoma kati ya washirika, pengine huwenda na viongozi kwa viongozi, hiyo ni ishara kuwa utulivu wa Roho haupo hapo, hivyo ni hatari pia kwa maisha yako ya kiroho.
Tujitahidi sana kuwa na vipimo hivi vya kiroho katika kuchagua mahali tukusanyakapo kupata maji ya uzima, vitakusaidia sana, kwasababu hizi ni siku za mwisho, na manabii wengi na makristo wa uongo na madhehebu na dini za uongo zimezuka kila pembe ili kuwatoa watu kwenye mstari.
Yajali maisha yako ya kiroho. Mpende Kristo na Agizo lake.
Shalom.
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
Mada Nyinginezo:
MAFUNDISHO MAALUMU KWA WAONGOFU WAPYA.
JINSI YA KUMSIKIA MUNGU, NA KUPOKEA MAFUNUO AU JUMBE KUTOKA KWAKE.
MWENGE WAKO WA UHURU UPO WAPI?
MADHARA YA KUKOSA MAJI YA UZIMA BAADA YA KIFO.
WALIKUWA WAMECHOKA NA KUTAWANYIKA KAMA KONDOO WASIO NA MCHUNGAJI.