Swali: Je lile shauri la kupeleka wapelelezi Kanaani lilitoka kwa nani?..Maana sehemu moja katika biblia inasema lilitoka kwa Bwana (Hesabu 13:1-3) na sehemu nyingine inasema lilitoka kwa wana wa Israeli (Kumbukumbu 1:22-23). Je! lipi ni sahihi, na je biblia inajichanganya?.
Jibu: Turejee mistari hiyo, mmoja baada ya mwingine.
Hesabu 13:1 “Kisha Bwana akanena na Musa, akamwambia,
2 Tuma watu, ili waende wakaipeleleze nchi ya Kanaani, niwapayo wana wa Israeli; katika kabila ya baba zao mtamtuma mtu mmoja, kila mtu na awe mkuu kati yao.
3 Basi Musa akawatuma kutoka nyika ya Parani kama alivyoagizwa na Bwana; wote walikuwa ni watu walio vichwa vya wana wa Israeli”.
Hapa tunaona ni MUNGU ndiye anamwamuru Musa apeleke wapelelezi.
Kumbukumbu 1:22 “Nanyi mkanikaribia kila mmoja wenu, mkasema, Na tupeleke watu mbele yetu, ili watupelelezee nchi na kutuletea habari za njia itupasayo kuipandia, na za miji tutakayoifikia.
23 Neno hili likanipendeza sana; nikatwaa watu kumi na wawili, mtu mmoja wa kila kabila”
Na hapa tunasoma kuwa ni “Wana wa Israeli” ndio waliopendekeza kupeleka wapelelezi Kanaani. Sasa swali ni je!..biblia inajichanganga?.
Jibu ni La!.. Biblia haijichanganyi mahali popote, isipokuwa fahamu/pambanuzi zetu ndizo zinachojichanganya au kuchanganyikiwa.
Sasa ni kwanini hapo sehemu moja iseme ni Mungu na sehemu nyingine iseme wana wa Israeli? Ukweli ni upi?
Ukweli ni kwamba wazo la kupeleka wapelelezi wakaiepeleze Kanaani ni Wana wa Israeli ndio waliolitoa, kamwe Mungu asingeweza kuwaambia wana wa Israeli wapeleke wapelelezi kwasababu yeye ana nguvu nyingi na wala hahitaji utafiti wa wanadamu katika kuokoa au kuharibu!…Kama ndivyo angefanya kwanza kwa Farao, lakini tunasoma Farao alikuwa kama mnyoo tu mbele za Bwana, na Taifa la Misri kwa wakati huo lilikuwa na nguvu Zaidi hata ya Kanaani.
Hivyo kilichowasukuma wana wa Israeli kupeleka wapelelezi ni hali ya ugumu wa mioyo yao, ambayo baada ya kutoka Misri walianza kuusahau uweza wa Mungu na kumdharau Mungu, kiasi kwamba hawakuamini kwamba angeweza kuwashindania kama alivyowashindania walipotoka Misri, lakini kinyume chake wakaukataa uweza wa Mungu, mioyo yao ikawa migumu, wakajitwika silaha, na wakapanga mipango yao.
Hesabu 14:11 “Bwana akamwuliza Musa, Je! Watu hawa watanidharau hata lini? Wasiniamini hata lini? Nijapokuwa nimefanya ishara hizo zote kati yao”.
Sasa kwakuwa wana wa Israeli tayari walikuwa wameshamdharau Mungu na uweza wake, hivyo Mungu aliruhusu baadhi ya Mambo wayafanye, katika kiwango cha uweza walichompimia. Na mojawapo ya jambo ambalo aliliruhusu ni hilo la kwenda kupeleleza.
Hivyo Musa aliposikia mpango wa wana wa Israeli kwenda kuipeleleza, alienda kuuliza kwa Bwana, na Bwana akawapa ruhusa sawasawa na hiyo Hesabu 13:1-6. Na sio jambo hilo tu ambalo Mungu alitoa ruhusa bali yapo na mengine mengi ambayo wana wa Israeli walijiamulia na Mungu akaruhusu yaendelee katikati yao, lakini hayakuwa mapenzi makamilifu ya Mungu, baadhi ya mambo hayo ni yale ya wana wa Israeli kujitakia mfalme katika (1Samweli 8:5) na yale ya talaka ambayo Bwana YESU aliyasema katika Mathayo 19:3-8.
Mathayo 19:3 “Basi Mafarisayo wakamwendea, wakamjaribu, wakimwambia, Je! Ni halali mtu kumwacha mkewe kwa kila sababu?
4 Akajibu, akawaambia, Hamkusoma ya kwamba yeye aliyewaumba mwanzo, aliwaumba mtu mume na mtu mke,
5 akasema, Kwa sababu hiyo, mtu atamwacha babaye na mamaye, ataambatana na mkewe; na hao wawili watakuwa mwili mmoja?
6 Hata wamekuwa si wawili tena, bali mwili mmoja. Basi aliowaunganisha Mungu, mwanadamu asiwatenganishe.
7 Wakamwambia, Jinsi gani basi Musa aliamuru kumpa hati ya talaka, na kumwacha?
8 Akawaambia, MUSA, KWA SABABU YA UGUMU WA MIOYO YENU, ALIWAPA RUHUSA KUWAACHA WAKE ZENU; LAKINI TANGU MWANZO HAIKUWA HIVI.
9 Nami nawaambia ninyi, Kila mtu atakayemwacha mkewe, isipokuwa ni kwa sababu ya uasherati, akaoa mwingine, azini; naye amwoaye yule aliyeachwa azini”
Hii ikitufundisha kuwa, kuna mambo ambayo Mungu anaweza kuyaruhusu katika maisha yetu yatokee lakini yakawa si mapenzi makamilifu ya Mungu. Hivyo ni muhimu sana kutafuta kuyajua na kuyafanya mapenzi makamilifu ya MUNGU, na ndivyo tutakavyompendeza Mungu, na kuishi kama atakavyo yeye.
Bwana akubariki.
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618
Mafundisho mengine:
TUMEFANYIKA KUWA WANA WA MUNGU!
EPUKA KUPELELEZA KILA KITU MUNGU ANACHOKUAHIDIA.
Swali: Roho ya kukata tamaa ipoje na inatendaje kazi na inawezaje kumtoka mtu?
“Roho ya kukata tamaa” ni roho inayomwingia mtu na kumfanya asiweze kuendelea mbele Zaidi. Roho hii inapomwingia mtu inamfanya asiwe na nguvu ya kufanya au kutafuta jambo lolote lile lililo zuri. Ndio hapo utaona mtu anakata tamaa ya kuendelea kusubiri jambo Fulani au kuendelea kuomba au kuendelea kutafuta.
Roho hii inasababishwa na “shetani” kwasababu kamwe MUNGU hawezi kumkatisha mtu tamaa kwa jambo lolote jema mtu apangalo kulifanya au kulitafuta. Yeye (Mungu) anasema maneno yafuatayo..
Luka 18:1 “Akawaambia mfano, ya kwamba IMEWAPASA KUMWOMBA MUNGU SIKUZOTE, WALA WASIKATE TAMAA”.
Mathayo 7:7 “Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtaona; bisheni, nanyi mtafunguliwa;
8 kwa maana kila aombaye hupokea; naye atafutaye huona; naye abishaye atafunguliwa”
Lakini adui kazi yake ni kukatishata tamaa, aidha kwa njia ya mawazo, ndoto au maneno ya watu.
Zifuatazo ni njia za kushughulika na roho ya kukata tamaa.
1. MPOKEE YESU
Kama bado hujaokoka, fahamu kuwa wewe ni windo tosha la adui, na moyo wako ni malango ya maskani za roho zote chafu zikiwemo za kukatisha tamaa, hivyo maisha yako yatatawaliwa na kuvunjika moyo na kutokusonga mbele.
2. SOMA NENO.
Soma sana Neno la MUNGU (Biblia) kwasababu ndani yake limejaa maneno ya Faraja, ambayo yanaweza kukufaa na kukutia nguvu katika nyakati zote utakayopitia za kukatisha tamaa, Kama magonjwa ndiyo yaliyokukatisha tamaa ndani ya biblia ipo mistari mingi ya kutia moyo wa kuendelea mbele.
Kama ni Ndoa ndio iliyokukatisha tamaa, yapo maneno ya faraha na kutia nguvu yahusuyo ndoa ndani ya biblia, kama ni anguko Fulani limetokea na likakukatisha tamaa, ndani ya biblia ipo mistari ya kutia nguvu ya kukunyanyua tena katika hali unayopitia. N.k
3. MAOMBI
Fanya maombi kila siku, hii utakusaidia kukuweka katika lile joto la kiroho, na hivyo kufunga milango yote ya roho za adui za vitisho na kukatisha tamaa. Ukiwa mwombaji utakuwa katika usalama wa Roho daima.
Kwa njia hizo tatu basi waweza kujifungua na kila kifungo cha kukata tamaa, au kukatishwa tamaa.
Bwana akubariki.
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618
Mafundisho mengine:
NI JAMBO GANI LINALOMTAMANISHA SANA BWANA TUMWOMBE BILA KUKATA TAMAA?
Nini maana ya kupiga Kite! Katika biblia.
Maana yake nini, Mwe na hofu wala msitende dhambi? (Zaburi 4:4)
Swali: Roho ya umasikini ipoje na inatenda kazi kwa namna gani, na inawezaje kumtoka mtu?
“Roho ya umasikini” ni roho inayomshusha mtu kiuchumi, hata kumfanya asifike kule anakotaka kufika kimaendeleo.
Roho hii inapomvaa mtu inamfanya wakati mwingine awe katika hali ya mahitaji kupindukia na hata kuwa katika hali ya madeni mazito.
Kibiblia watu wa Mungu umasikini si sehemu yao.. Ingawa kuna vipindi ambavyo Mungu anaweza kumpitisha mtoto wake kuonja umasikini kwa muda ili kumfundisha baadhi ya mambo, ambayo yatamfaa baadaye atakapobarikiwa.
Na urefu wa kipindi hicho cha madarasa ya Mungu kinategemea mtu na mtu. Wapo ambao watadumu katika hiko kipindi kwa muda mrefu kidogo lakini baadaye watatoka huko, na wapo ambao watadumu katika kipindi kifupi na baadaye watatoka huko na kupewa pumziko la faraja ya Bwana.
Lakini kwa ujumla Mkristo hajapewa umasikini wa kudumu kama sehemu maisha yake…au labda mtu huyo atake mwenyewe kujifanya maskini kwa nafsi yake au kwaajili ya Bwana.
Mtu anayejifanya maskini kwa ajili ya Bwana ni yule ambaye Mungu anamfungulia milango ya kupata vingi lakini kila anachokipata anakitoa na hivyo muda wote anakuwa katika hali ya kutokuwa na vingi…(Mtu wa namna hii ni maskini ingawa ni tajiri).
Mtu huyu anakuwa hawezi kuona furaha au Amani akiwa na viwili wakati mwingine hana hata kimoja. Mtu wa namna hii anakuwa anajifanya mwenyewe maskini kwaajili ya Bwana na kwa taji yake mbinguni, ikiwa anafanya hivyo kwa dhamiri njema na si kama sheria.
Mfano wa watu waliojifanya wenyewe kuwa maskini ingawa wangeweza kuwa matajiri ni Yohana Mbatizaji na BWANA WETU YESU KRISTO.
2Wakorintho 8:9 “Maana mmejua neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, jinsi alivyokuwa maskini kwa ajili yenu, ingawa alikuwa tajiri, ili kwamba ninyi mpate kuwa matajiri kwa umaskini wake.
Na pia wapo ambao walikuwa matajiri na wakadumu na utajiri wao, mfano wa hao ni Ibrahimu na Ayubu..
Sasa hakuna agizo lolote maalumu katika biblia kuwa ni sheria tujifanye kuwa maskini, kama alivyokuwa Bwana au Yohana Mbatizaji, mtu akijifanya hivyo basi iwe kwa nafsi yake na Mungu wake, na si amri wala agizo.
Lakini pamoja na hayo, upo umaskini mwingine ambao hauletwi na Mungu bali unaletwa na adui shetani. Mara nyingi umasikini huu ni ule unaompata mtu anapokuwa nje ya KRISTO (Maana yake hajaokoka).. au aliyeokoka lakini amepungukiwa na baadhi ya Maarifa ambayo yangemsaidia kusogea kimaisha.
Sasa ni njia gani za kushughulika na roho ya umaskini unaoletwa na adui shetani?
1. KUOKOKA
Unapookoka kikweli kweli kwa kumaanisha, basi roho zote za adui zinazochochoe na kutengeneza umaskini maishani mwako zinaondoka, na hivyo maisha yako kutengenezeka upya kama yalikuwa yameshaharibiwa na pepo la umasikini.
2. KUOMBA
Maombi ni silaha tosha kwa kila mwamini, na maombi ni ULINZI, Kama umeshuhudiwa kuwa hali unayopitia sio ya kawaida na wala haitokani na MUNGU, basi ni wakati wa kuingia vitani katika maombi, kuvunja na kukemea kila roho yote inayotaka kujiinua kinyume na maendeleo yako.
3. PATA MAARIFA.
Kama umeshaokoka na tena ni mwombaji sana lakini bado unaona hali hiyo ya umasikini inadumu muda mrefu, basi huenda Mungu kashakufungulia milango mbele yako ili upige hatua, lakini milango hiyo huioni aidha kutokana na kupungukiwa na MAARIFA, sawasawa na Hosea 4:6.
Hivyo tia bidii katika kutafuta maarifa ya jinsi ya kujiendeleza mbele kupitia kanuni za kibiblia. (Soma sana biblia, na pia sikiliza mafundisho mbalimbali kutoka kwa watumishi wa kweli wa Mungu yahusuyo namna ya kujiendeleza, vile vile ongeza ujuzi katika kile ukifanyacho).
Kupitia njia hizo tatu basi utaweza kujifungua kutoka katika kifungo cha umasikini.
Bwana akubariki.
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618
Mafundisho mengine:
Heri walio maskini wa roho; Maana ufalme wa mbinguni ni wao.
Mbona ni maskini tu huwa ndio wanaolipuka mapepo, na sio matajiri?
UKITAKA KUMFUATA YESU NI SHARTI UACHE VYOTE!
Elewa maana ya Mithali 18:23 Maskini hutumia maombi; Bali tajiri hujibu kwa ukali.
Je kualikwa kwenye sherehe za watu ambao si wakristo ni dhambi?
Swali: Kwanini tutoe sadaka? Na Je ni lazima kutoa sadaka?..Na mtu asipotoa sadaka ni dhambi?
Jibu: “Utoaji” (uwe wa sadaka au wa kitu kingine chochote) ni wajibu wa kila “Mwamini”.. Mtu ambaye si mtoaji bado hana badiliko la kweli ndani yake!…na wala Mungu hayupo ndani yake.
Sasa kwanini tunatoa sadaka? Na kwanini mtu ambaye si mtoaji hana Mungu ndani yake?
Jibu, Tunatoa sadaka kwasababu Mungu naye ni Mtoaji (vyote tunavyonufaika navyo ni yeye katupa bure bila gharama). Na kwanini Mungu awe mtoaji na sisi tuwe watoaji?.. Ni kwasababu tumeumbwa kwa sura na Mfano wake! (Mwanzo 1:26).
Kama mtu hatoi maana yake ule mfano wa Uungu ndani yake haupo kwasababu Mungu sifa yake kuu ni utoaji!.. Ametoa uzima bure, ametoa maisha bure Zaidi sana ametupa uzima wa milele bure kupitia kumtoa mwanawe wa pekee (Yohana 3:16) na mambo mengine mengi.. Hivyo na sisi ni lazima tuwe kama yeye…ndivyo maandiko yanavyotuambia.
Mathayo 5:48 “Basi ninyi mtakuwa wakamilifu, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo mkamilifu”.
Na kutoa ni “Wajibu” Zaidi ya “Agizo”.. Mtu anayejua wajibu wake, hakumbushwi kumbushwi, halazimishwi lazimishwi wala hasukumwi sukumwi.. Anatimiza wajibu wake kwasababu anajua pia ni kwa faida yake.
Ukiona utoaji ni sheria ngumu kwako, kwamba unaona uchungu kumtolea Mungu.. au unaona kama unafilisika, au unaonewa au unadhulumiwa wahi kutafuta msaada kutoka kwa BWANA, Mlile mwambie aiondoe hiyo roho ndani yako kwasababu ndio roho ile ile iliyokuwa ndani ya Kaini alipoona kumtolea Mungu sehemu ya kwanza ya vitu vyake ni hasara kubwa!.. na kwasababu anasukumwa sukumwa na sheria ya utoaji, akalazimika kumtolea Mungu sehemu hafifu na sadaka zake na hivyo zikakataliwa.
Mungu anayekupa pumzi na maisha bure unaonaje uchungu kumtolea sehemu ya kumi tu! Na sehemu 9 zilizosalia zibaki kwako?.. Huoni kuna shida kama unaona uchungu kwa hicho kidogo?..
Mungu unayekanyaga ardhi yake bure, unayevuta hewa yake bure tangu umezaliwa, unayefurahia jua lake bure bila kulipia hata mia, na wakati huo huo unawalipa tanesco fedha nyingi kwa kukupatia tu kanuru kadogo wakati wa usiku.. Huyo Mungu akupaye hayo yote, unamwonea uchungu na hata kumwibia, na ukiambiwa kuhusu kumtolea unaona unafilisiwa na kudhulumiwa, utaachaje kuwa kama KAINI WEWE!!. Moyo wako hauwezi kuwa kwa MUNGU Kamwe!, haijalishi utakuwa unaomba sana wewe bado utakuwa mnafiki.
Usikwepe kumtolea Mungu na tena ifanye kuwa ni wajibu, na si Agizo wala Amri!. Na madhara ya kutomtolea Mungu (kukwepa wajibu) yanapatikana katika Mathayo 25:41-46
+255789001312 au +255693036618
Mafundisho mengine:
Kwanini Sadaka ya Kaini ilikataliwa? (Mwanzo 4:5).
SADAKA INAHARIBU NGUVU ZA MADHABAHU ZA MASHETANI.
Sadaka ya kinywaji ilikuwaje? Na inawakilisha nini?.
Chakula kilichotolewa sadaka kwa sanamu ndio kipi? (Matendo 21:25).
Swali: Kwanini sadaka ya Kaini ya Mazao ilikataliwa na ile ya Habili ya wanyama ilikubaliwa? Je ni kwamba “wanyama” ni bora kuliko “mazao” mbele za Mungu?
Jibu: Turejee,
Mwanzo 4:4 “Habili naye akaleta wazao wa kwanza wa wanyama wake na sehemu zilizonona za wanyama. Bwana akamtakabali Habili na sadaka yake;
5 bali Kaini hakumtakabali, wala sadaka yake. Kaini akaghadhibika sana, uso wake ukakunjamana”.
Sababu ya sadaka ya Kaini kukataliwa si kwasababu Mungu anapendezwa sana na wanyama kuliko mazao.. LA! Zaidi sana Mazao yanaweza kuwa bora kuliko wanyama kwasababu hayahusishi umwagaji wa damu.
Lakini sababu kuu ya Sadaka ya Kaini kukataliwa ni hiyo tunayoisoma katika mstari wa 3 na wa 4..
“Ikawa hatimaye Kaini akaleta mazao ya ardhi, sadaka kwa Bwana. Habili naye akaleta WAZAO WA KWANZA wa wanyama wake na SEHEMU ZILIZONONA za wanyama. Bwana akamtakabali Habili na sadaka yake;”
Habili alileta wazao wa kwanza wa wanyama wake na sehemu zilizonona… Lakini Kaini hakupeleka sehemu za kwanza za mazao yake!..bali alipeleka sehemu dhaifu, kama ni mahindi pengine alipeleka yale yaliyoharibika haribika, kama ni matikiti alipeleka yale yaliokaribia kuoza! N.k..na zile njema na nzuri aliona zinamfaa yeye na si Mungu anayempa pumzi, na uhai na maisha.
Hivyo alimfanya Mungu wapili katika mali zake, na Mungu naye akamfanya wa pili mbele ya ndugu yake Habili.
Lakini Mungu ni wa upendo, huwenda alifanya vile kwa kukosa maarifa.. hivyo alimwonya na kumfundisha njia iliyobora ya kutoa sadaka ili sadaka yake ikubaliwe kama ya nduguye, lakini kwa kiburi alishupaza shingo, na akaenda kumwua ndugu yake, ikawa dhambi kubwa sana kwake.
Mwanzo 4:3 “Ikawa hatimaye Kaini akaleta mazao ya ardhi, sadaka kwa Bwana.
4 Habili naye akaleta wazao wa kwanza wa wanyama wake na sehemu zilizonona za wanyama. Bwana akamtakabali Habili na sadaka yake;
5 bali Kaini hakumtakabali, wala sadaka yake. Kaini akaghadhibika sana, uso wake ukakunjamana.
6 Bwana akamwambia Kaini, Kwa nini una ghadhabu? Na kwa nini uso wako umekunjamana?
7 Kama ukitenda vyema, hutapata kibali? Usipotenda vyema dhambi iko, inakuotea mlangoni, nayo inakutamani wewe, walakini yapasa uishinde.
8 Kaini akamwambia Habili nduguye, [Twende uwandani]Ikawa walipokuwapo uwandani,Kaini akamwinukia Habili nduguye,akamwua.
9 Bwana akamwambia Kaini, Yuko wapi Habili ndugu yako? Akasema, Sijui, mimi ni mlinzi wa ndugu yangu? “
Ni jambo gani tunajifunza hapo?
Jambo kuu tunalojifunza ni kuwa Mungu anaziangalia sadaka zetu, na kupitia hizo anatuhukumu nazo!.. Maandiko yanasema “hazina ya mtu ilipo ndipo na moyo wake utakapokuwepo (Mathayo 6:21)”.. Kama hazina yako ya kwanza haipo kwa Mungu, na Moyo wako hauwezi kuwa kwa Mungu, na ndicho kilichokuwa kwa Kaini.. Hazina yake kamilifu haikuwa kwa Mungu ndio maana hata Moyo wake haukumwelekea Mungu baada ya pale.
Lakini kama sehemu ya kwanza ya Hazina yako (sadaka) ipo kwa Mungu hata moyo wako utakuwa kwa Mungu..
Na kama unataka kujipima kama moyo wako kweli upo kwa Mungu “jiangalie utoaji wako”..(Hicho ndio kipimo kirahisi sana cha kujitambua wewe ni mtu wa namna gani).. Kwasababu hiyo basi ni dhambi kubwa sana kukwepa matoleo, haihitaji elimu kubwa kufahamu hilo….mtolee Bwana Zaka, mtolee Bwana sehemu zilizonona wala usimwibie, na moyo wako utakuwa kwake na utabarikiwa pia.
Bwana akubariki.
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618
Mafundisho mengine:
Mtu wa kwanza kufa alikuwa nani?
Biblia inaposema Kaini akatoka mbele za uso wa Bwana, Inamaana gani?
SISI NI WINDO BORA SANA, LA DHAMBI.
DAMU YA YESU INANENAJE MEMA KULIKO YA HABILI?
Swali: Kwanini Mungu alimkataa Mfalme Sauli na tunapata funzo gani?
Jibu: Sauli alikataliwa na Mungu kwasababu ya mambo makuu mawili, 1) UASI na 2) UKAIDI WA MOYO.
Hayo ndio mambo mawili yaliyomkosesha Sauli, na biblia imeweka wazi..
1Samweli 15:22 “Naye Samweli akasema, je! Bwana huzipenda sadaka za kuteketezwa na dhabihu Sawasawa na kuitii sauti ya Bwana? Angalia, kutii ni bora kuliko dhabihu, Na kusikia kuliko mafuta ya beberu.
23 Kwani KUASI ni kama dhambi ya uchawi, Na UKAIDI ni kama ukafiri na vinyago; Kwa kuwa umelikataa neno la Bwana, Yeye naye amekukataa wewe usiwe mfalme”.
1. KUASI
Kuasi maana yake ni kuondoka katika njia sahihi na kuwa adui wa hiyo njia. Ndicho kilichomtokea Sauli, Moyo wake ulianza kuondoka kwa MUNGU kidogo kidogo, na akaanza KWENDA KINYUME na sheria ya MUNGU huku akijua kabisa kuwa anachokifanya si sawa.
2. UKAIDI
Dhambi ya pili ya Sauli ni “Ukaidi”. Mkaidi ni mtu asiyeshaurika wala hakubali kubadili mawazo yake…anachokiamini amekiamini!!,…anachokishikilia amekishikilia!..
Na Mfalme Sauli alikuwa mkaidi kwa BWANA!, Kwani utaona alipofanya kosa la kwanza la kutoa dhabihu kinyume na sheria ya Mungu katika 1Samweli 13:18 na kukemewa na Bwana, lakini utaona anakuja kurudia kosa linalofanana na hilo katika 1Samweli 15:14 pale alipoleta dhabihu haramu kutoka kwa waamaleki na kutaka kuzitoa kwa Bwana.
Alileta kondoo na Ng’ombe (walionona) kutoka Taifa la Amaleki, ili amtolee Mungu dhabihu… Kwa jicho la Haraka inaweza kuonekana kuwa alifanya jambo la busara…lakini kwa jicho la ndani SAULI alifanya machukizo makubwa sana.
Kwani kitendo cha kutwaa Ng’ombe za watu wanaoabudu miungu, ambao wanaitolea miungu yao, na tena hajui hizo ng’ombe zina historia gani..na kuzichukua hizo kisa tu zimenona kisha kumtolea Mungu, ilikuwa ni kitendo cha dharau kubwa sana (1Samweli 15:14-15)!!.. Ni sawa tu na kutwaa msharaha wa kahaba na kumletea Bwana ule alioukataza katika Kumbukumbu 23:18..
Kumbukumbu 23:18 “Usilete ujira wa kahaba, wala mshahara wa mbwa, katika nyumba ya Bwana, Mungu wako, kwa ajili ya nadhiri yo yote; kwani haya ni machukizo kwa Bwana, Mungu wako, yote mawili”.
Hivyo Sauli alikuwa mkaidi kwa Mungu.. kwani sheria inasema Usimchinjie Bwana Ng’ombe wala kondoo aliye na kilema au MWENYE NENO OVU! (Kumbukumbu 17:1)..Na hapa Sauli analeta Ng’ombe walionona lakini waliojaa maovu ya Waamaleki kama sadaka kwa Bwana. (1Samweli 15:14-15)!!.. Huo ni UKAIDI MKUU..
Na hata leo, Mambo haya mawili (UASI na UKAIDI) yanamchukiza Mungu.
Yeremia 5:22 “Je! Hamniogopi mimi? Asema Bwana; hamtatetemeka mbele za uso wangu; mimi niliyeweka mchanga kuwa mpaka wa bahari, kwa amri ya daima, isiweze kuupita? Mawimbi yake yajapoumuka-umuka, hayawezi kushinda nguvu; yajapovuma sana, hayawezi kuupita.
23 Lakini watu hawa wana moyo wa KUASI NA UKAIDI; wameasi, wamekwenda zao.
24 Wala hawasemi mioyoni mwao, Basi, na tumche Bwana, Mungu wetu, aletaye mvua, mvua ya mwaka, na mvua ya vuli, kwa wakati wake; na kutuwekea juma za mavuno zilizoamriwa.
25 Maovu yenu yameyageuza haya, na dhambi zenu zimewazuilia mema msiyapate”.
Maran atha!
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618
Mafundisho mengine:
DHABIHU ZA ROHO NI ZIPI? (1Petro 2:5)
Swali: Kwanini Mungu ametuumba? Na Sababu ya sisi kuwepo ni ipi?.. Na kwanini mmoja aumbwe hivi mwingine vile? kwa ujumla kwanini Mungu aliiumba dunia?
Jibu: Mungu katuumba sisi kwa “Kupenda kwake yeye (Mapenzi yake)”… Ili yeye afurahi kuwa pamoja nasi na sisi tufurahi kuwa pamoja naye!.
Ufunuo 4:11 “Umestahili wewe, Bwana wetu na Mungu wetu, kuupokea utukufu na heshima na uweza; kwa kuwa wewe ndiwe uliyeviumba vitu vyote, na KWA SABABU YA MAPENZI YAKO VILIKUWAKO, navyo vikaumbwa”.
Kwetu kuumbwa ni “faida kubwa”…kwasababu hakuna faida yoyote ya “kutokuwepo”.. tengeneza picha haupo au hatupo!..je ni faida gani unapata au tunapata?..Lakini kama tukiwepo na tukaishi maisha ya milele na furaha basi ni heri sana!.
Na Mungu mwenyewe ametuahidia uzima wa milele kupitia mwanae YESU KRISTO.
Yohana 3:16 “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele”
Lakini kama mtu hatapenda kuishi, na wala hataki maisha basi njia ya kupoteza maisha ni kumkataa YESU.
1Yohana 5:12 “Yeye aliye naye Mwana, anao huo uzima; asiye naye Mwana wa Mungu hana huo uzima”
swali la pili; kwanini mmoja aumbwe hivi mwingine vile?
Jibu rahisi ni kwasababu ndivyo ilivyompendeza yeye ili kututofautisha sisi kwa sisi (hajapenda wote tufanane kama sisimizi)…na hatuwezi kuhoji Zaidi!.
Warumi 9:20 “La! Sivyo, Ee binadamu; wewe u nani umjibuye Mungu? Je! Kitu kilichoumbwa kimwambie yeye aliyekiumba, Kwani kuniumba hivi?
21 Au mfinyanzi je! Hana amri juu ya udongo, kwa fungu moja la udongo kuumba chombo kimoja kiwe cha heshima, na kimoja kiwe hakina heshima?”
Lakini kwa vyovyote vile tulivyoumbwa tunapaswa tuutafute uzima wa milele na pia ni muhimu kufahamu kuwa kwa Mungu hakuna upendeleo wa mmoja Zaidi ya mwingine, wote tupo sawa mbele zake, pasipo kuangalia mwonekano, wala kimo, wala umri, wala jinsia.. Wote tunapendwa sawa, na tunapimwa sawa mbele zake .
Je unao uzima wa milele ndani yako?..Kumbuka uzima wa Milele upo kwa mmoja tu! YESU KRISTO!, Ikiwa bado hujampokea na unahitaji msaada katika kumpokea basi waweza wasiliana nasi kwa namba zetu..
Bwana akubariki.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618
Mafundisho mengine:
TAFUTA UZIMA WA MILELE NA SI UZIMA TU!.
UNATAKA KUBARIKIWA? BASI USIKWEPE GHARAMA ZAKE.
FAHAMU VIASHIRIA VYA MTU ALIYESAMEHEWA DHAMBI ZAKE.
Kwanini Yakobo alimshinda Mungu, Je! Mungu huwa anashindwa na wanadamu?
SWALI: Mimi kila nikilala, huwa kuna kitu kinanikaba koo, nakosa pumzi, kinanikandamiza naona kama nakwenda kufa au wakati mwingine ninaganda muda mrefu siwezi kusogea. Hata nikijaribu kukemea, natumia kushindana sana, baadaye kinaniachia, Je hili ni jinamizi?. Jambo hili limekuwa likijirudia mara kwa mara. Nimejaribu kufunga na kuomba zinaweza pita tu siku kadhaa halafu kikajirudia tena. Naomba msaada nifanye nini?
JIBU: Hayo ni mashambulizi ya adui ndotoni. Tufahamu kuwa adui hashambulii tu katika mwili, lakini wakati mwingine pia katika ndoto. Wapo watu wanaosumbuliwa na shetani husasani katika maeneo ya ndoto.
Utakuta kila anapolala, ni mfululizo tu wa ndoto za kipepo, labda anafukuzwa-fukuzwa, au anazini-zini na mapepo hayo, au yupo makaburini, anafanya mambo ya kichawi, zaidi wengine zinakuwa ni mwendelezo, yaani pale alipoishia jana, leo anaendelea nazo sehemu ya pili, kila anapolala hana raha, kwasababu anajua vitisho ni vilevile anakwenda kukutana navyo. Wengine mpaka inazidi wanasikia sauti kabisa za mapepo, zikiwasemesha, au wanaona vitu vya ajabu vikipita mbele yao, na hiyo yote hutokea pindi tu wanapopitiwa na usingizi kidogo, haijalishi mchana au usiku. Kundi lingine ndio hili ambalo wanaona kama wananaswa, na kitu Fulani pumzi haitoki, wanaishia kutaabika. N.k.
Sasa, unapokutana na mojawapo ya shida, hizo au mashambulizi hayo ndotoni. Jambo la kwanza ‘hupaswi kuogopa’ Fahamu suluhisho ni moja tu nalo ni YESU KRISTO. Lakini wengi hawajui ni kwa namna gani.
Mambo haya matatu (3), yaelewe yatakusaidia..
Unapojikuta kwenye mashambulizi hayo, usiwe tu bubu. Hakikisha unalitumia jina la YESU kukemea. Kuyadhibiti hayo mapepo na kazi zao. Kwasababu mamlaka hiyo umepewa.
Mathayo 10:19 Tazama, nimewapa amri ya kukanyaga nyoka na nge, na nguvu zote za yule adui, wala hakuna kitu kitakachowadhuru.
Lakini ukiona unasumbuliwa na hizo ndoto, halafu unapambana mwenyewe mwenyewe, huna silaha yoyote mkononi mwako, jiandae kukugeuza wewe kuwa ndio kijiwe chao. Vaa silaha za vita. Jina la Yesu ndio silaha yetu kuu, kutiisha nguvu zote za Yule mwovu.
Penda kuwa mwombaji kabla hujalala, usilale tu bila kumkabidhi Bwana usiku wako. Lakini pia hakikisha moyoni mwako, huna makunyanzi ambayo shetani atapata sababu ya kukushitaki. Unajua ni kwanini biblia inasema maneno haya?
Waefeso 4:26 Mwe na hasira, ila msitende dhambi; jua lisichwe na uchungu wenu bado haujawatoka; 27 wala msimpe Ibilisi nafasi
Ni kwasababu shetani hupenda mipenyo kama hiyo, kwamfano moyoni mwako una vinyongo na wenzako, una hasira na jirani zao, mambo kama hayo, husababisha adui kukushambulia kwa njia yoyote nyakati za usiku. Hivyo ukabidhi moyo wako kwa Bwana.
Ikiwa mambo hayo mawili unayafanya, lakini bado unaona mashambulizi, yanaendelea. Basi tatizo kubwa kwako lipo kwenye IMANI. Imani yako ni chache. Upo wakati mitume walipambana na mapepo wakashindwa kuyatoa. Baadaye wakamuuliza Bwana mbona sisi tulishindwa? Yesu akawaambia ni kwasababu ya upungufu wa imani yenu. Hata leo hii ukiona mkristo unasumbuliwa sana na vibwengo, na vipepo. Ujue pia imani yake bado haijawa imara.
Kwa namna gani?
Bado hujaamini vya kutosha nguvu iliyopo ndani ya JINA LA YESU. Na ushindi ulipoupata kupitia Kristo Yesu moyoni mwako. Unachopaswa kufanya ni kumwamini Yesu asilimia mia alimaliza yote msalabani, uwe jasiri, ondoa hofu, vipepo ni vinyago tu, havina chochote cha kukubabaisha wewe. Ukiona hiyo hali inakuja wewe kuwa ujasiri na Imani yote, usiope kitu. Kemea. “Sema wewe pepo, mimi nimekombolewa na Yesu, huna uwezo wa kushindana na Roho Mtakatifu aliye ndani. Na sasa nisikilize, kuanzia sasa hili sio hekalu lako. Kwa mamlaka ya kifalme iliyo ndani ya jina la Yesu Kristo mwokozi wangu, nakuamuru toka na kwamwe usirudi hapa tena”.
Ukiwa na ujasiri unaotokana na imani ya Bwana unayemtumikia. Nakuambia pepo hilo litabadili uelekeo mara moja, hata likija kujaribu mara nyingine likakukuta na msimamo wako huo huo, hakuna hofu ndani yako. Ndio bye! bye! Halitakaa lirudi tena itakuwa ni historia.
Kumbuka Samsoni alipokutana na Yule Simba, yeye alimwona kama ni “mzinga” tu uliomletea asali. Hivyo akalirarua, na ndio maana baadaye akaja akakuta asali ndani yake akala akaondoka. Kwasababu alijua nguvu zilizo ndani yake, zinatuliza pepo na bahari, na milima simbuse hichi kisimba-mbarara kinachonguruma hapa mbele yangu.
Na wewe vivyo hivyo, usiishi kinyonge-nyonge tu, unakubali kunyanyaswa nyanyaswa na hivyo vipepo ambavyo havina kitu kwako kama vile huna mtetezi hapa duniani.. KEMEA! KWA IMANI, na Ujasiri. KAZI ITAKUWA IMEISHA!. Wala usitafute maombezi.
Bwana akubariki.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Shalom.
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618
Mafundisho mengine
Kanuni ya kufunga na kuomba inafananishwa na kanuni ya Kuku kuyaatamia mayai yake mpaka kufikia hatua ya kutotoa vifaranga.
Ili mayai yaweze kuanguliwa na vifaranga kutokea ni lazima Kuku ayaatamie mayai kwa siku 21, na ili aweze kuyaatamia kwa mafanikio, basi hana budi kujizuia kula kwa kipindi kirefu ili asipoteze joto la mayai yale. Ndio hapo utaona itampasa atoke mara chache chache kwenda kutafuta chakula kisha kuyarudia mayai yake, na atafanya hivyo kwa siku zote 21.
Maana yake kama kuku hatajiingiza katika hiyo adhabu ya kuutesa mwili wake na kujizuia na milo kwa siku 21, hawezi kupata vifaranga!.
Vile vile kuna mambo ambayo yanahitaji “Joto la kiroho” kwa siku kadhaa za MIFUNGO na MAOMBI na KUJITESA. Ili tuweze kuyapata…Vinginevyo hayatatokea kabisa haijalishi tutayatamani kiasi gani!.
Bwana YESU alisema mambo mengine hayatoki pasipo Maombi na Mifungo..
Mathayo 17:21 “[Lakini namna hii haitoki ila kwa kusali na kufunga.]”
> Ukiona umejaribu kutafuta kitu na hujakipata, ingia kwenye mfungo!
> Ikiwa umeomba na bado hujapata, ongezea na mfungo juu yake!.
> Ikiwa umetafuta na hujapata ongezea na mfungo wa maombi juu yake!.
> Ikiwa unataka Amani, Furaha, au Nguvu za kuendelea mbele, usikwepe mfungo! N.k
Ukiwa ni mtu wa kuomba pamoja na kufunga, utakuwa ni mtu wa mafanikio kiroho na kimwili. Utaangua vingi kwa wakati.. Lakini ukiwa ni mtu wa kukwepa mifungo basi utatumia nguvu nyingi sana kupata baadhi ya mambo.
Danieli 9:2 “katika mwaka wa kwanza wa kumiliki kwake, mimi Danielii, kwa kuvisoma vitabu, nalifahamu hesabu ya miaka, ambayo neno la Bwana lilimjia Yeremia nabii, ya kuutimiza ukiwa wa Yerusalemu, yaani, miaka sabini.
3 Nikamwelekezea Bwana Mungu uso wangu, ili kutaka KWA MAOMBI, na dua, PAMOJA NA KUFUNGA, na kuvaa nguo za magunia na majivu.……………………….
21 naam, nilipokuwa nikinena katika kuomba, mtu yule, Gabrieli, niliyemwona katika njozi hapo kwanza, akirushwa upesi, alinigusa panapo wakati wa dhabihu ya jioni.
22 Akaniagiza, akaongea nami, akasema, Ee Danielii, nimetokea sasa, ili nikupe akili upate kufahamu.
23 Mwanzo wa maombi yako ilitolewa amri, nami nimekuja kukupasha habari; maana wewe unapendwa sana; basi itafakari habari hii, na kuyafahamu maono haya”.
Na kuna Toba nyingine zinahitaji Mfungo kabisa ili mtu aweze kufunguliwa.
Yoeli 2:12 “Lakini hata sasa, asema Bwana, nirudieni mimi kwa mioyo yenu yote, na kwa kufunga, na kwa kulia, na kwa kuombolea;
13 rarueni mioyo yenu, wala si mavazi yenu, mkamrudie Bwana, Mungu wenu; kwa maana yeye ndiye mwenye neema, amejaa huruma; si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa rehema, naye hughairi mabaya”.
Usikwepe mifungo!
Shalom.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618
Mafundisho mengine:
Je unaruhusiwa kufanya tendo la ndoa ukiwa katika mfungo?
HIZI NI NYAKATI ZA KUFUNGA NA KUOMBA.
Kuomba katika roho ni kupi? na je nifanye nini ili niweze kuomba hivyo?
Swali: Je mtu aliyeishi miaka mingi kwenye biblia alikuwa nani?..na Mtu aliyeishi miaka mingi duniani ni nani?.
Jibu: Katika biblia mtu aliyeishi miaka mingi kuliko wote, ni METHUSELA, mwana wa Henoko aliyetwaliwa na Mungu..Biblia inasema huyu Methusela aliishi miaka 969, na hakuna mwingine aliyerekodiwa kuishi miaka mingi kuliko yeye.
Mwanzo 5:25 “Methusela akaishi miaka mia na themanini na saba, akamzaa Lameki.
26 Methusela akaishi baada ya kumzaa Lameki miaka mia saba na themanini na miwili, akazaa wana, waume na wake.
27 Siku zote za Methusela ni miaka MIA KENDA NA SITINI NA KENDA, AKAFA”.
Wengine walioishi miaka mingi katika biblia ni pamoja na;
Baada ya “Gharika ya Nuhu” miaka ya wanadamu ilishushwa mpaka kufikia miaka 120.. Ambapo ni wachache sana walivuka miaka hiyo, wengi waliishi chini ya hiyo..
Mwanzo 6:3 “Bwana akasema, Roho yangu haitashindana na mwanadamu milele, kwa kuwa yeye naye ni nyama; basi siku zake zitakuwa miaka mia na ishirini”.
Lakini kwajinsi siku zinavyozidi kwenda Miaka ya mwanadamu kuishi duniani ilizidi kushuka.. kutoka 120 mpaka 80
Zaburi 90:9 “Maana siku zetu zote zimepita katika hasira yako, Tumetowesha miaka yetu kama kite.
10 Siku za miaka yetu ni MIAKA SABINI, NA IKIWA TUNA NGUVU MIAKA THEMANINI; Na kiburi chake ni taabu na ubatili, Maana chapita upesi tukatokomea mara”.
Lakini swali kuu ni hili; kwanini miaka ya wanadamu inazidi kupungua siku baada ya siku? Je ni kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa au mabadiliko ya vyakula?
Jibu rahisi ni kwasababu ya “kuongezeka kwa Maasi”. Wala si mabadiliko ya hali ya hewa! Bali ni DHAMBI!.. Kitu cha kwanza kilichopunguza miaka ya Adamu na Hawa kutoka kuishi MILELE mpaka kufikia kuishi miaka 930 si kingine Zaidi ya DHAMBI!.. wala si kwasababu walikuwa hawazingatii mazoezi au milo kamili!..La!! bali ni dhambi!..
Na kanuni hiyo hiyo ndiyo inayopunguza maisha ya mwanadamu inaendelea mpaka sasa… Na wakati huo huo upande wa pili shetani anajaribu kuwaaminisha watu kuwa ni “Milo wanayokula ndiyo inayopunguza miaka” kwamba wapunguze ulaji wa nyama, na mafuta, na wazingatie mazoezi wataishi miaka mingi.
Mambo hayo ni mazuri, na yanafaa..lakini hayafai katika kuongeza UREFU WA MAISHA YA MTU, Kwani kuna wengi ambao wamezingatia hayo yote lakini wamewahi kuondoka duniani!.. na kuna ambao hawajazingatia hayo yote lakini wanayo miaka mingi duniani.
Kanuni ya kuishi miaka mingi na ya heri NI KUMCHA MUNGU NA KUEPUKANA NA UOVU, hiyo tu… Zishike Amri, fanya mapenzi ya Mungu, maisha yako yatakuwa marefu, hapa na katika ulimwengu ujao.
Kutoka 20: 12 “Waheshimu baba yako na mama yako; siku zako zipate kuwa nyingi katika nchi upewayo na Bwana, Mungu wako”.
Bwana akubariki.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618
Mafundisho mengine:
Je! mwanadamu wa kwanza kuumbwa ni yupi?
MAANA YA KUISHI NA MKE KWA AKILI.
NIFANYE NINI ILI NISILALE NINAPOSOMA BIBLIA.
MWONGOZO WA MAOMBI YA WAHUDUMU/ WASIMAMAO MADHABAHUNI.