Category Archive Uncategorized @sw-tz

Mwandishi na uchambuzi wa kitabu cha Wakolosai

Kama kinavyoanza kwa utambulisho wake, ‘Waraka wa Paulo mtume kwa Wakolosai’.

Paulo ndiye mwandishi wa waraka huu.

Madhumuni makuu ya waraka huu ulikuwa ni kuwasisitiza Wakolosai  jinsi Yesu alivyo UTOSHELEVU WOTE, ambaye kwa kupitia yeye Uumbaji wote umekamilishwa ndani yake, lakini si hilo tu bali na  utimilifu  wote wa ki-Mungu unapatikana ndani yake, pamoja na hazina zote za hekima na maarifa.

Akiwa na maana kuwa mtu akimpata Kristo, hahitaji kitu kingine cha pembeni kumkamilisha yeye, Utoshelevu wote upo kwake.

Hivi ni vifungu mama,

1:15-17

“15 naye ni mfano wa Mungu asiyeonekana, mzaliwa wa kwanza wa viumbe vyote. 16 Kwa kuwa katika yeye vitu vyote viliumbwa, vilivyo mbinguni na vilivyo juu ya nchi, vinavyoonekana na visivyoonekana; ikiwa ni vitu vya enzi, au usultani, au enzi, au mamlaka; vitu vyote viliumbwa kwa njia yake, na kwa ajili yake. 17 Naye amekuwako kabla ya vitu vyote, na vitu vyote hushikana katika yeye”.

2:3

ambaye ndani yake yeye hazina zote za hekima na maarifa zimesitirika.

 

2:9

 “Maana katika yeye unakaa utimilifu wote wa Mungu, kwa jinsi ya kimwili”.

Lakini Sababu ya kusisitiza jambo ni ipi?

Anaeleza kwa undani katika sura ile ya pili, kwamba ni kutokana na uwepo wa watu waliolivamia kanisa na kuwadanganya kwa maneno ya ushawishi, nia zao ni kuwafanya mateka kwa elimu isiyo na matunda, ya mapokeo ya kibinadamu, yasiyo ya Kristo (2:8). Kwamba mtu akishika hayo, ndio utimilifu wote unapatikana.

Vilevile kuonekana kwa baadhi ya desturi za kiyahudi ndani ya kanisa, kama vile kushika sikukuu, tohara,  sabato, na mwandamo wa mwezi. Vikidhaniwa kuwa vitu hivyo vinaweza kuleta ukamilifu wote pamoja na Kristo (2:11-23)

Na pia kuzuka kwa ibada bandia za kuabudu viumbe vya rohoni (malaika), kwa mawazo kuwa mtu ataupokea ukamilifu.(2:18)

Paulo anaeleza yote hayo hayana wokovu, isipokuwa kwa njia ya haki tuliyoipokea kwa msalaba wake uliofuta hati ya mashtaka yetu, kwa mateso yake pale msalabani ambayo kwa kupitia njia hiyo tumepokea msamaha wa dhambi, pale tu tunapoamini na kubatizwa (2:12-17)

Maisha mapya ndani ya Kristo.

Sehemu ya tatu Paulo anaeleza kwamba kuamini ni pamoja na kuuvaa utu upya wa Kristo. Hivyo huyu mtu hatarajiwi kuendelea kuishi hivi hivi tu, kisa Kristo amemkamilisha kwa kila kitu, bali anapaswa aenende kwa Kristo mwenyewe, ayafikiri yaliyo juu, (3:1-17),

Kwa namna gani?

Kwa kuzifisha tabia za mwilini, kama uasherati, uchafu, kutamani, mawazo mabaya, ghadhabu, matusi. Lakini pia kujivika utu wema, moyo wa rehema, unyenyekevu, upole, uvumilivu, kusameheana, upendo, ibada. Vilevile si tu katika mambo ya rohoni , bali mpaka kwenye ngazi za kifamilia, kwamba wake kuwatii waume zao, na waume kuwapenda wake zao, na watoto kuwatii wazazi. Hizo ndio tabia za utu mpya.

Katika sura ya 4.

Bado Paulo aendelea kueleza huo mwenendo ndani ya Kristo, unapaswa uonekane mpaka kwa mabwana, kwa watumwa wao. Kwamba mabwana wawape watumwa haki zao, Lakini pia watakatifu wote, wanapaswa kudumu katika maombi, na kuenenda kwa hekima kwa watu wasioamini, katika usemi bora, na kujifunza kuukomboa wakati.

Na mwisho.

Paulo anawasilisha salamu za washirika wenzake wa injili, kwa Wakolosai ikiwemo, Epafra, Luka, Dema, marko, Aristarko, Yusto.

Hitimisho.

Kwa ufupi waraka huu, hueleza kwamba utoshelevu wote upo ndani ya Kristo tu na sio zaidi ya hapo, hatuhitaji kitu kingine cha pembeni kutukamilisha sisi, Lakini ni wajibu wa huyu mkristo kutembea katika maisha mapya ndani yake. Kwasababu mambo yote mawili yanakwenda sambamba hayatengani. Kristo huokoa na kutakasa wakati huo huo. Unapookolewa, saa hiyo hiyo umevikwa utu upya. Huwezi kuendelea katika dhambi.

Ni kipi cha ziada tunachoweza kujifunza katika waraka huu?.

Maombi ya Paulo na Eprafa yasiyokoma kwa kanisa hili(1:3, 9, 4:12):

Hatuna budi kujijengea desturi ya sikuzote kuliombea kanisa la Bwana, hususani mahali tulipo, pamoja na watakatifu wengine tuwajuao. Kwasababu kusimama kwa kanisa hutegemea sana maombi yasiyokoma.

                                        Bwana akubariki.                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                     ||kiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii. Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

Nini maana ya kuabudu malaika? (Wakolosai 2:18)

Nijapokuwa sipo kwa mwili, lakini nipo pamoja nanyi kwa roho,

Tafsiri ya Wakolosai 2:18 Mtu asiwanyang’anye thawabu yenu,

Epafra ni nani katika biblia? (Wakolosai 1:7)

Uchambuzi na Mwandishi wa kitabu cha Wagalatia

Rudi Nyumbani

Print this post

Kwanini biblia iwasifu wenye kutumia shoto zaidi ya wanaotumia kulia? (Waamuzi 20:16).

Kwanini biblia iwasifu wenye kutumia shoto zaidi ya wanaotumia kulia? (Waamuzi 20:16).


Swali: Je kuna jambo gani la ziada katika mkono wa kushoto hata watajwe kama mahodari katika vita?.

Jibu: Turejee…

Waamuzi 20:16 “Katika watu hao wote walikuwako watu waume mia saba waliochaguliwa, wenye shoto; kila mmoja alikuwa anaweza kuutupia unywele mawe kwa teo, wala asikose”.

Ni kweli zipo tafiti zinazoonyesha kuwa mkono wa kushoto una nguvu (uwezo) kuliko ule wa kuume (kulia).

Lakini hiyo si sababu biblia iliyoitumia kuusifiia mkono huo(wa kushoto) zaidi ya ule wa kulia…kwasababu pia walikuwepo mahodari waliotumia mikono yote miwili na walionekana sawa tu..

1Nyakati 12:2 “Walikuwa wenye kupinda upinde, nao walikuwa hodari wa kutumia mkono wa kuume na wa kushoto, kwa kutupa mawe ya teo, na kwa kupiga mishale ya upinde; walikuwa wa nduguze Sauli, wa Benyamini”.

Sasa ni sababu gani inayowafanya wanaotumia shoto kuonekana mashujaa zaidi?.

Jibu, Sababu kuu ni mbinu za upiganaji.

 Kawaida ni kuwa idadi ya askari wanaotumia mkono wa kulia (kuume)…ni kubwa kuliko ile ya wanaotumoa shoto.

Sasa kikawaida inakuwa ni ngumu sana kupambana na mtu anayetumia mfumo mwingine tofauti na wa kwako, lakini mfumo unaofanana na wewe ni rahisi kumsoma, na kumwingia.

Ni rahisi sana mashoto kupambana na mashoto wenzake na kulia kupambana na kulia mwenzake..lakini inapotokea kinyume na hapo, basi vita vinakuwa vigumu kwasababu ni mifumo miwili tofauti.

Na kwasababu mashoto ni wachache na wengi wanaokutana nao wakati wa vita ni watu wanaotumia mkono wa kuume (kulia), basi wanapata mzoefu mkubwa wa kupambana na watu wa tofauti na mikono yao, na kuwafanya kuwa hodari zaidi..

Lakini wale wanaotumia kulia, wanakuwa na uhodari hafifu kwasababu ni mara chache sana wanakutana na wasiotumia mashoto, hiyo inawafanya uzoefu wa kupigana na jamii hiyo ya watu kuwa mdogo, na kuwafanya kuanguka (kupigwa) wanapokutana na watu wanaotumia mashoto, hiyo ndio sababu kuu…

Na sababu nyingine inayowafanya watu wanaotumia mashoto kuwa hodari zaidi katika biblia, ni uwezo wa kuficha jambo bila kujulikana..

Kikaiwaida askari anajulikana kwa kuhifadhi upanga wake upande wa paja lake la kushoto, lakini wale wanaotumia mashoto huficha panga zao upande wa kuume, jambo linalowafanya wasifahamike kwa haraka kama ni maaskari..

Jambo hilo tunaliona kwa Ehudi aliyekuwa mwamuzi wa Israeli.

Waamuzi 3:14 “Wana wa Israeli walimtumikia Egloni mfalme wa Moabu muda wa miaka kumi na minane.

15 Lakini wana wa Israeli walipomlilia BWANA, BWANA akawainulia mwokozi, Ehudi, mwana wa Gera, Mbenyamini, mtu aliyekuwa mwenye shoto; nao wana wa Israeli walimpelekea Egloni mfalme wa Moabu tunu mkononi mwa huyo Ehudi.

16 Ehudi alijifanyia upanga uliokuwa na makali kuwili, urefu wake ulipata dhiraa moja; akaufunga huo upanga ndani ya nguo yake katika paja lake la MKONO WA KUUME…………

20 Basi Ehudi akamwendea; naye alikuwa anaketi peke yake katika chumba chake cha baridi. Ehudi akasema, Mimi nina ujumbe utokao kwa Mungu kwako wewe. Basi akainuka katika kiti chake.

21 Ehudi akaunyosha mkono wake wa kushoto, akaushika huo upanga kuutoa hapo katika paja lake la kuume, akamtia tumboni mwake;

22 hicho kipini nacho kikaingia ndani pamoja na huo upanga wenyewe; nayo mafuta yakashikamana tena juu ya upanga, kwani hakuutoa tena upanga tumboni; nao ukatokea kwa nyuma”

Bwana atupe kutumia mashoto mbele ya adui wetu ibilisi, tupiganapo vita vya kiroho.

Waefeso 6:14 “Basi simameni, hali mmejifunga kweli viunoni, na kuvaa dirii ya haki kifuani……..

17 tena ipokeeni chapeo ya wokovu, na upanga wa Roho ambao ni neno la Mungu”

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

LIPO LA KUJIFUNZA KWA WALE MASHUJAA 37 WA DAUDI.

Nini maana ya Dirii, Chapeo na Utayari?

Amka, Ee upanga, juu ya mchungaji wangu (Zekaria 13:7-9)

MAANA ROHO HUCHUNGUZA YOTE, HATA MAFUMBO YA MUNGU.

TUTAMPIGA KWA NDIMI ZETU.

Rudi Nyumbani

Print this post

Mwandishi na uchambuzi wa kitabu cha Warumi.

Kitabu hichi kama kinavyojitambulisha, “Waraka wa Paulo kwa Warumi” mwandishi wake ni Mtume Paulo.

Kitabu hiki alikiandika akiwa Korintho mahali palipoitwa Kenkrea (Warumi 16:1)

Tofauti na nyaraka nyingine ambazo Paulo aliziandika kwa makanisa ambayo alikuwa tayari ameshayatembelea/ameyapanda hapo nyuma. Waraka huu tunaonyeshwa Paulo hakuwahi kufika Rumi. Lakini alisikia mwitikio wao wa injili, hivyo likawa ni tamanio lake pia awafikie na wao, lengo likiwa sio kupanda juu ya msingi wa watu wengine bali wajengane kiimani.(1-18),

Na kweli tamanio lake tunaona lilikuja kutimia baadaye, kama tunavyosoma kwenye kitabu cha matendo ya mitume, katika ile ziara yake ya mwisho kama mfungwa, alifika Rumi, na huko akafanikiwa kuhubiri injili sawasawa na tamanio lake (Matendo 27-28).

Hichi ni kitabu kinachoeleza misingi ya imani  ki-mpangilio . Kuanzia asili ya wokovu wetu, haki ya Mungu, na mwenendo wa kikristo. Hivyo kuna umuhimu mkubwa sana kwa mkristo yoyote kukielewa vema kitabu hichi.

Migawanya mikuu ya kitabu hichi.

     1) Nguvu ya injili? (1: 1-17)

Baada ya Paulo, kueleza tamanio lake la kuwafikia katika utangulizi wake, tunaona katika mistari hiyo anasisitiza kwanini afanye hivyo? Ni kwasababu ya ‘Nguvu ya Injili yenyewe’, Akisema Injili ni uweza wa Mungu uuletao wokovu. Na hivyo haionei haya kuihubiri kwa watu wote..kwa wayahudi na watu wa mataifa pia.

  1. Hatia kwa wanadamu wote (1:18- 3:20)

Sehemu ya pili Paulo anaeleza jinsi wanadamu wote walivyopungikiwa na utukufu wa Mungu kuanzia watu wa mataifa ambao wameshindwa kuitii kweli ya Mungu iliyofunuliwa kwao kwa mambo yake yaliyo dhahiri kabisa yanayotambulika hata pasipo sheria, kwamba mambo ya asili yanafundisha haki ya Mungu, lakini walikataa kutii. Vilevile na wayahudi  pia ambao walikuwa na sheria lakini walishindwa kuyatenda yote kulingana na yaliyoandikwa. Hivyo hakuna hata mmoja mwenye haki,  wote wamewekwa chini ya hukumu ya ghadhabu ya Mungu, kwa kushindwa kutenda haki yote.

  1. Haki kwa Imani (3:21-5:21)

Kwa kuwa wanadamu wameshindwa kuwa wakamilifu, Paulo anaeleza njia ambayo Mungu ameitoa kwa  mwanadamu kuweza  kuhesabiwa haki. Ni njia ambayo inadhihirishwa bila matendo ya sheria, tunayoipata kwa kumwamini tu Yesu Kristo. Yaani pale mtu anapomwamini Bwana Yesu kwamba kifo chake kimeleta ukombozi wa roho yake, basi mtu huyo anakuwa amehesabiwa haki kuwa ni Mtakatifu mbele za Mungu.

Kulithibitisha hilo Paulo akaendelea kueleza  kwa mfano wa Ibrahimu jinsi Mungu alivyomhesabia haki bila sheria yoyote, na kwamba sisi pia tutahesabiwa kwa njia hiyo hiyo.

  1. Maisha mapya ndani ya Kristo (6:1-8:39)

Katika sehemu hii Paulo anaeleza maisha baada ya kuhesabiwa haki, kwamba mkristo anapaswa aendelee kutakaswa na kuwa kama Kristo. Lakini kutokana na mashindano kati ya mwili na roho. Ili aweze kuushinda mwili anapaswa ajifunze kuishi kwa Roho, kwa kuruhusu utendaji kazi wake ndani yake. Maneno hayo ameyarudia pia katika waraka wake kwa Wagalatia (Wagatia 5:16). Kwamba mtu anayeenenda kwa Roho kamwe hawezi kuzitimiza tamaa za mwili.

Lakini mbele kidogo anaendelea kuhimiza upendo wa milele wa Mungu, uliodhihirishwa kwetu kupitia Yesu Kristo, ambao hauwezi kutenganishwa na kitu chochote tukijuacho duniani au mbinguni.

  1. Uhuru wa Mungu wa kuchagua, na kusudi lake kwa Waisraeli (9:1- 11:36)

Kwenye sura hizi, Paulo anaeleza uhuru wa Mungu wa kuchagua, na siri iliyokuwa nyuma ya Israeli kukataa injili. Anaeleza mpango wake wa wokovu kwa mataifa na waisraeli, kwamba iliwapasa wao wakatae injili ili sisi watu wa mataifa tuipokee injili. Na hivyo anaeleza sisi pia tunapaswa tuupokee wokovu kwa unyenyekevu wote kwasababu tusipokaa katika kuamini tutakatwa, kama wao walivyokatwa.

  1. Tabia ya maisha mapya katika Kristo (Warumi 12:1- 15:3 )

Paulo anaeleza jinsi tunavyopaswa kuitoa miili yetu kama dhabihu iliyo hai takatifu yenye kumpendeza Mungu, tunawajibu wa kupendana sisi kwa sisi, tusiwe watu wa kulipa kisasi, tuishi kwa heshima, tuhudumiane katika karama mbalimbali tulizokirimiwa na Mungu, tutii mamlaka zilizowekwa, vinywa vyetu vitoe baraka, tumtumikie Mungu kwa bidii, tudumu katika sala, tuishi kwa amani sisi kwa sisi, pia tuweze kuchukiliana katika viwango mbalimbali vya imani bila kuhukumiana.

Kwa ufupi sura hizi zinaeleza tabia zetu zinapaswa ziweje baada ya wokovu.

  1. Hitimisho  (15:14- 19:27)

Paulo anaeleza mpango wake wa kuwafikia Warumi pindi atakapokuwa anasafiri kwenda Spania kuhubiri injili. Akiomba akumbukwe katika maombi dhidi ya watu wabaya, na mwisho anatoa salamu kwa watakatifu wote walio Rumi, pamoja na angalizo kwa watu waletao fitna katika injili waliyoipokea wajiepushe nao

KWA UFUPI.

Kitabu hichi kinaeleza

Haki ya Mungu ikoje, ambapo hapo mwanzo ilidhaniwa inapatikana kwa sheria au matendo ya mwanadamu, kumbe sio, hayo yalishindwa bali kwa njia ya Yesu Kristo, lakini pia kinaeleza namna ambavyo tunaupokea wokovu huo kwa neema kwa njia ya Imani, na pia jinsi Mkristo anavyopaswa aishi kulingana na wokovu alioupokea. Kwamba sio kwasababu amehesabiwa haki bure bila matendo, basi aishi maisha kama atakayo, hapana vinginevyo atakufa.

Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

NJIA/BARABARA YA WOKOVU NDANI YA KITABU CHA WARUMI.

Fahamu Mwandishi wa kitabu cha Waebrania ni nani.

Uchambuzi na Mwandishi wa kitabu cha Wagalatia

Je Kauli ya Mungu katika Warumi 11:4 na 1Wafalme 19:18 inajichanganya?.

Rudi Nyumbani

Print this post

TUTAMPIGA KWA NDIMI ZETU.

Silaha ya Mwisho mwisho kabisa ya adui  kumshambulia Mtu ni “ULIMI WA UOVU”.. Ukiona Maneno ya uongo kuhusu wewe, au ya vitisho au ya uchonganishi yanatembea huku na huko basi fahamu kuwa adui ndio yupo katika hatua za mwisho mwisho, kukuacha!..(Ni wakati wa kumaliza jaribu).

Na kama ukiweza kusimama katika hiko kipindi bila hofu, wala kutetereka wala kurudi nyuma, basi shetani unaweza usimwone tena baada ya hapo, kwa kipindi kirefu sana.

Mfano katika biblia tunamwona Nabii Yeremia,

Adui alimtafuta mara nyingi kwa njia mbalimbali ili amnyamazishe asitoe unabii, lakini kila alichojaribu ili kumzuia Yeremia asitoe unabii, kilishindikana, na ndipo akatumia silaha yake ya mwisho ya NDIMI ZA UOVU, ili yamkini amtishe Yeremia, lakini pia haikusaidia,

Yeremia 18:18 “Hapo ndipo waliposema, Njoni na tufanye mashauri juu ya Yeremia; maana sheria haitampotea kuhani, wala shauri halitampotea mwenye hekima, wala neno halitampotea nabii. Njoni, na TUMPIGE KWA NDIMI ZETU, wala tusiyaangalie maneno yake yo yote.

19 Niangalie, Ee Bwana, ukasikilize sauti ya wanaoshindana nami”.

Wakati huo kilitokea kikundi kiovu na kuanza kumtisha Yeremia kwa maneno mengi, na pia kumzushia mambo mengi na zaidi ya yote, ya uchonganishi na kumchafua mbele ya Mfalme, ili tu Yeremia akamatwe asiendelee kutoa unabii.

Yeremia 38: 4 “Ndipo wakuu wakamwambia mfalme, Twakuomba, mtu huyu auawe, kwa kuwa aidhoofisha mikono ya watu wa vita, waliobaki katika mji huu, na mikono ya watu wote, kwa kuwaambia maneno kama hayo; maana mtu huyu hawatafutii watu hawa heri, bali shari.

5 Naye mfalme Sedekia akasema, Tazama, yu mikononi mwenu; maana mfalme siye awezaye kufanya neno lo lote kinyume chenu”.

Mtu mwingine aliyepigwa kwa NDIMI  OVU ni nabii Danieli, soma Danieli 6..

Sasa kwanini Adui, aiweke hii silaha ya ulimi kama chaguo lake la mwisho?… Ni kwasababu anajua ulimi wa mtu unaweza kuwasha moto mkubwa, na kama mtu hatakuwa na Imani ya kutosha basi anaweza kuanguka kabisa…

Yakobo 3:6 “Nao ulimi ni moto; ule ulimwengu wa uovu, ule ulimi, umewekwa katika viungo vyetu, nao ndio uutiao mwili wote unajisi, huuwasha moto mfulizo wa maumbile, nao huwashwa moto na jehanum”

Hivyo shetani anaweza kukuwashia tu moto kupitia ulimi wa mtu au ndimi za watu, na moto huo ukawa mkubwa sana, kiasi kwamba kama huna imani na ujasiri wa kutosha, unaweza kurudi nyuma kabisa.

Shedraka, Meshaki na Abednego walijikuta wapo katika tanuru la Moto, kwasababu tu ya baadhi ya watu waliotumia ndimi zao kupeleka mashitaka kwa mfalme kuwa hawataki kuisujudia ile sanamu.(Danieli 3:8-12).

Danieli naye alijikuta katika tundu la simba kwasababu tu ya vinywa vya watu, na Yeremia naye alijikuta katika lile shimo refu lenye giza lililojaa matope kwasababu ya maneno ya watu(Yeremia 38:6)..

Lakini wote hao walishinda, kwani moto ule uliokusudiwa juu yao uliwala maadui zao, na mashimo yale na matundu yale yaliyokusudiwa juu yao yaliwaharibu maadui zao, lakini kama wangetetemeka na kuogopa na kurudi nyuma bila shaka wangepotea kwa kuharibiwa na ibilisi!.

Na sisi hatuna budi kusimama Imara bila hofu, kwa ujasiri mwingi pale ambapo adui anatumia NDIMI za watu kama silaha yake…

Hiko ni kipindi cha kuwa na imani na ujasiri….mipango inapopangwa ya vitisho au uchonganishi, havitasimama endapo wewe utasimama.

Ni wakati kusimama na kuamini huku tukiomba, na silaha za ndimi zao zitaanguka, na Bwana atatukuzwa.

Ifuatayo ni mistari inayozungumzia hatari ya NDIMI ZA UOVU…

Zaburi 57:4 “Nafsi yangu i kati ya simba, Nitastarehe kati yao waliowaka moto. Wanadamu meno yao ni mikuki na mishale, Na ndimi zao ni upanga mkali.”

Zaburi 64: 2 “Utanificha mbali na shauri la siri la watenda mabaya, Mbali na ghasia ya watu wafanyao maovu;

3 Waliounoa ulimi wao kama upanga, Wameielekeza mishale yao, maneno ya uchungu,

4 Wapate kumpiga mkamilifu faraghani, Kwa ghafula humpiga wala hawaogopi.

5 Walijifanya hodari katika jambo baya; Hushauriana juu ya kutega mitego; Husema, Ni nani atakayeiona”

Zaburi 140:1 “Ee Bwana, uniokoe na mtu mbaya, Unihifadhi na mtu wa jeuri.

2 Waliowaza mabaya mioyoni mwao, Kila siku huondokesha vita.

3 Wamenoa ndimi zao kama nyoka, Sumu ya fira i chini ya midomo yao”.

Lakini pamoja na kwamba adui anatumia ndimi kutushambulia, vile vile na sisi tunaweza kutumia ndimi hizo hizo, kumharibu.

Mithali 18:21 “Mauti na uzima huwa katika uwezo wa ulimi; Na wao waupendao watakula matunda yake”

Tunampiga shetani kwa ndimi zetu, kwa njia ya KUOMBA, na hususani maombi yanayohusisha mfungo.

Bwana atubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

Rudi Nyumbani

Print this post

Kughafilika ni nini? (Wagalatia 6:1)

Swali: Kughafilika maana yake nini?


Jibu: Turejee…

Wagalatia 6:1  “Ndugu zangu, mtu akighafilika katika kosa lo lote, ninyi mlio wa Roho mrejezeni upya mtu kama huyo kwa roho ya upole, ukijiangalia nafsi yako usije ukajaribiwa wewe mwenyewe.

2  Mchukuliane mizigo na kuitimiza hivyo sheria ya Kristo”

Kughafilika maana yake ni  “Kuchukuliwa na jambo fulani baya”.. Mtu aliyeghafilika anakuwa amezama katika Uovu na anakuwa haoni tena kama ni kosa kufanya uovu ule  (kiasi kwamba ufahamu wake unakuwa kama umefungwa)..

Kwamfano mtu aliyezama katika anasa ambao hapo kwanza alikuwa anaukataa, mtu huyo anakuwa “Ameghafilika katika anasa za dunia” n.k

Biblia inatufundisha kuwa watu kama hawa ni kuwarejesha kwa roho ya upole, Maana yake kwa kuwafundisha taratibu na kuwaombea mpaka watakaporudi katika mstari, na hiyo ndiyo tafsiri ya kuchukua mzigo wa mwingine, (yaani  ni kumrejesha katika kweli, mtu aliyekengeuka, na si kumwombea baada ya kufa!)

Mtu aliyekufa hakuna mtu anayeweza kuuchukua mzigo wake wa dhambi, bali atasimama nao mbele ya kile kiti cha hukumu..

Wagalatia 6:5 “Maana kila mtu atalichukua furushi lake mwenyewe”

Na sio tu mtu, bali hata Bwana mwenyewe hatamchukulia mtu mzigo wa dhambi, baada ya kifo….

Yohana 8:21  “Basi akawaambia tena, Mimi naondoka, nanyi mtanitafuta; NANYI MTAKUFA KATIKA DHAMBI YENU; mimi niendako ninyi hamwezi kuja…….

24  Kwa hiyo naliwaambieni ya kwamba MTAKUFA KATIKA DHAMBI ZENU; kwa sababu msiposadiki ya kuwa mimi ndiye, MTAKUFA KATIKA DHAMBI ZENU”.

Je umeokoka?.. una uhakika Bwana YESU akirudi leo utakwenda naye?.

Maran atha..

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

Uchambuzi na Mwandishi wa kitabu cha Wagalatia

WALIPO WAWILI AU WATATU KWA JINA LANGU

Je, kama hauna ubatizo sahihi hauwezi kuwa na Roho Mtakatifu?

Ni uchafu gani unaozungumziwa katika Wagalatia 5:19?

je! Paulo aliwalaani Wagalatia na Wakorintho?

Rudi Nyumbani

Print this post

MHESHIMU MCHUNGAJI WAKO.

Kila mahali pana mamlaka yake, na mamlaka hizo huwa ni  wajibu kwa walio chini yake kuzitii. Kwamfano katika familia Mungu ameweka mamlaka, Baba awe kichwa, na mama msaidizi wake, hivyo ni wajibu wa watoto kuwatii wazazi wao . Familia haiwezi kusimama,.kama mtoto atataka nafasi ya baba, kwamba yeye ndio atoe maamuzi ya mwisho, au ajiamulie la kufanya, awapangie wazazi wake majukumu ya ndani. hilo haliwezekani.

Vilevile katika ngazi ya utawala wa kidunia, Mungu kaziweka mamlaka na anataka watu wote wazitii, kwasababu hazijaamuriwa na mwanadamu bali yeye Mungu mwenyewe..

Warumi 13:1-2

[1]Kila mtu na aitii mamlaka iliyo kuu; kwa maana hakuna mamlaka isiyotoka kwa Mungu; na ile iliyopo umeamriwa na Mungu.

[2]Hivyo amwasiye mwenye mamlaka hushindana na agizo la Mungu; nao washindanao watajipatia hukumu.

Tito 3:1-2

[1]Uwakumbushe watu kunyenyekea kwa wenye uwezo na mamlaka, na kutii, na kuwa tayari kwa kila kazi njema; [2]wasimtukane mtu ye yote, wasiwe wagomvi, wawe wema, wakionyesha upole wote kwa watu wote.

Sasa hizi ni mamlaka za kidunia. Zipi kuhusu Mungu, unadhani hana mamlaka?

Mungu pia ameweka mamlaka yake duniani, ambayo ni kuu kupita hizo zote, na kupitia hiyo huwahudumia watu wake. Na anataka tuitii na kuitetemekea kwasababu ni yeye mwenyewe atendaye kazi kupitia hiyo.

Je mamlaka hiyo kaiweka kupitia nani?

Bila shaka kupitia wachungaji wetu/waangalizi wetu, ndani ya kanisa

Ni vema kufahamu kuwa kiongozi yoyote wa kiroho (anayeisimamia kweli). Hakujiteua mwenyewe kwenye nafasi hiyo.  Mitume wa Yesu hawakujichagua wao. Bali walichaguliwa na Mungu mwenyewe.

Mtu yeyote aliyepewa maono ya kuanza kanisa, na ukajikuta upo chini yake, au kateuliwa na Roho Mtakatifu mwenyewe ndani ya kanisa (Matendo 14:23), Huyo ni wa kumtii sana. Kama vile unavyowatii watawala au mazazi wako kwenye familia, haijalishi atakuwa na mapungufu kiasi gani, au umri wake ni mdogo au mkubwa kiasi gani, awe mwenye uwezo au asiye na uwezo kiasi gani.

Kwanini uwaheshimu.

1) Wanajitaabisha kwa ajili yako kukuchunga, kukuonya na kukuombea.

Hivyo wajibu ni wako kurudisha moyo wa upendo, na kuwasikiliza.

1 Wathesalonike 5:12-13

[12]Lakini, ndugu, tunataka mwatambue wale wanaojitaabisha kwa ajili yenu, na kuwasimamia ninyi katika Bwana, na kuwaonyeni; [13]mkawastahi sana katika upendo, kwa ajili ya kazi zao. Iweni na amani ninyi kwa ninyi.

2) Watasimama mbele ya kiti cha hukumu siku ya mwisho kutoa hesabu juu yako.

Hivyo ni wajibu kuonyesha moyo wa kunyenyekea kwao.

Waebrania 13:17

[17]Watiini wenye kuwaongoza, na kuwanyenyekea; maana wao wanakesha kwa ajili ya roho zenu, kama watu watakaotoa hesabu, ili kwamba wafanye hivyo kwa furaha wala si kwa kuugua; maana isingewafaa ninyi.

Madhara ya kutowasikiliza/ kutowatii.

i) Watafanya kazi ya Mungu kwa kuugua.

Hapo kwenye Waebrania 13:17b anasema..

..ili kwamba wafanye hivyo kwa furaha wala si kwa kuugua; maana isingewafaa ninyi

Na matokeo yake utendaji kazi ndani ya kanisani utakuwa hafifu. Ukishaanza kuonyesha tabia ya kutosikiliza unachoelekezwa, unapewa jukumu hutekelezi, hurudishi mrejesho, unafanya tofauti na wengine, yeye anataka uende kulia wewe unaenda kushoto, , yeye anafundisha hiki wewe unafundisha kile. Fahamu kuwa jambo hilo litamhuzunisha kiongozi wako. Na hivyo kupelekea hamasa ya kuhudumu kupungua. Na madhara yake ni kuwa Mungu kukata utendaji kazi wake mahali hapo,

ii) Dhara lingine ni kuwa utajisababishia adhabu kwa Mungu.

Wakati ule Haruni na Miriamu dada yake. walimnenea Musa maneno mabaya kwasababu na mke wake ambaye hakuwa myahudi. Mungu aliwaadhibu kwa kumpiga ukoma Miriamu kwasababu tu hiyo ya kutoonyesha adabu kwa mtumishi wake.

Hesabu 12:7-8

[7]Sivyo ilivyo kwa mtumishi wangu, Musa; Yeye ni mwaminifu katika nyumba yangu yote;

[8]Kwake nitanena mdomo kwa mdomo, Maana, waziwazi wala si kwa mafumbo; Na umbo la BWANA yeye ataliona. Mbona basi ninyi hamkuogopa Kumnenea mtumishi wangu, huyo Musa?

Ni kosa kumnenea vibaya mchungaji wako. Epuka masengenyo na uasi na matabaka ndani ya kanisa. Uonapo kosa mwombee, au mfuate mweleze  uwapo naye peke yake. Hilo litamjenga zaidi ya kutoa malaumu na manung’uniko. Adui hutumia sana njia hii kuleta mafarakano na magomvi, na mapigo kanisani.

Mheshimu mchungaji wako, zaidi ya raisi wa nchi kwasababu yeye ni balozi wa mbinguni na Mungu atakuinua (1Petro 5:1-6)

Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

TEMBEA NDANI YA SUKOTHI YAKO.-Maafundisho maalumu kwa watumishi

Ipi tofauti kati ya KUHANI na MCHUNGAJI.

VITABU VYA BIBLIA: Sehemu ya 1

Rudi Nyumbani

Print this post

JINSI YA KUMFANYA MUNGU MWONGO.

Wazia jambo hili, raisi amepewa taarifa na wataalamu wake wa hali ya hewa kwamba kuna kimbunga kikubwa kinatokea bahari. 

Hivyo akachukua hatua ya kuwatahadharisha wananchi wake wasifike maeneo yote ya pwani. akawaelekeza na namna ya kujilinda, na mazingira yote hatarishi, akawajuza na madhara ambayo tayari kimbunga hicho kimeshaleta, akawaonya sana wakae ndani mpaka hicho kipindi chote cha hatari kitakapokwisha.

Lakini cha kushangaza kesho yake wakaonekana watumishi wa raisi na mawaziri , pamoja na watumishi wote wa serikalini wakiwa ufukweni wakiogolea na kufurahi na kustareheka..kana kwamba hakuna hatari yoyote mbeleni.

Unadhani ni wazo gani litajengeka kwa wananchi juu ya raisi wao?

Watasema raisi ni mwongo. Ametulaghai, mbona mamlaka yake haichukui hatua ya janga lililotangazwa?

Lakini heri na hapo, unadhani raisi naye atajisikiaje moyoni, kwa wale watu waliomtendea hivyo?

Sasa hilo ndilo watu wanalolifanya kwa Mungu sasa mpaka anaonekana ni mwongo.

Neno la Mungu linasema…

1 Yohana 5:10-12

[10]Yeye amwaminiye Mwana wa Mungu anao huo ushuhuda ndani yake. Asiyemwamini Mungu amemfanya kuwa mwongo, kwa kuwa hakuuamini huo ushuhuda ambao Mungu amemshuhudia Mwanawe.

[11]Na huu ndio ushuhuda, ya kwamba Mungu alitupa uzima wa milele; na uzima huu umo katika Mwanawe.

[12]Yeye aliye naye Mwana, anao huo uzima; asiye naye Mwana wa Mungu hana huo uzima.

Mungu alimtuma Yesu duniani, kuushuhudia ulimwengu kuwa una dhambi, Na mwana wake kuja duniani ni kwa lengo hilo kuu la kuwaokoa watu dhambini.

Hivyo Mungu akamshuhudia kwa sauti kutoka mbinguni, kwa ishara na miujiza mingi,.kwa Roho Mtakatifu aliyetuachia, lakini bado watu wakapuuzia, wakaendelea na mambo yao. Sasa huko ndiko kumfanya Mungu mwongo. Yaani kufikiri kuwa sisi hatukutenda dhambi, tunamfanya yeye kuwa mwongo.

1 Yohana 1:10

[10]Tukisema kwamba hatukutenda dhambi, twamfanya Yeye kuwa mwongo wala neno lake halimo mwetu.

Hivyo mtu yeyote anayekataa injili, ni kwamba anamfanya yeye aonekane mwongo. Ushuhuda wake ni uongo, kazi aliyoifanya ni bure, ni kuthibitisha mtu anaweza kuishi tu mwenyewe apendavyo na akawa na maisha ya milele?

Je! umempokea Yesu, kama Bwana na mwokozi wa maisha yako. Kama ni La! ndugu Kamwe usimfanye Mungu mwongo.

Amini ushuhuda wake kupitia mwana wake kwasababu ni kweli usipookolewa na yeye. Uzima wa milele haupo ndani yako. Dhambi ipo, na bado itaendelea kuwepo juu yako, hata kama utakuwa na matendo mazuri kiasi gani.

Fanya uamuzi sasa ya kuokoka. Hukumu ipo mbele na inatisha.

Shalom.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >>

https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

JINSI YA KUUHARIBU UJANA WAKO.

NI NJIA GANI MTU AITUMIE AWEZE KUSHINDA TAMAA NA VISHAWISHI?

NINYI AKINA BABA MSIWACHOKOZE WATOTO WENU

Rudi Nyumbani

Print this post

Je! Paulo, alikuwa na injili yake tofauti na wengine?(Warumi 2:16)

SWALI: Je! Paulo, alikuwa na injili yake, tofauti na wengine?  sawasawa na (Warumi 2:16)

Warumi 2:16 katika siku ile Mungu atakapozihukumu siri za wanadamu, sawasawa na injili yangu, kwa Kristo Yesu.


JIBU: Katika habari hiyo mtume Paulo hakumaanisha kwamba anayo injili nyingine ya kipekee tofauti na mitume wengine wa Kristo, na kwamba ya kwake tu  ndiyo Mungu atakayoitumia kuzihukumu siri za wanadamu.

Hapana mitume wote walikabidhiwa “injili moja”. Nayo ni kushuhudia wokovu ulioletwa duniani na mtu mmoja tu, ambaye ni YESU KRISTO, kwa lile tendo la kufa na kukufuka kwake kama fidia ya dhambi za ulimwengu, ambapo mtu akiamini basi amepokea ondoleo la dhambi na uzima wa milele. Na mtu yeyote ambaye hatamwamini huyu basi hukumu ya Mungu inakuwa juu yake.

Kwahiyo Paulo kama mmoja wa hao waliokabidhiwa injili hiyo, alikuwa na ujasiri kuwaeleza watu wale wa Rumi, kwamba kupitia injili yake hiyo sahihi, Mungu atawahukumu wanadamu, kwasababu anayehubiriwa ni Yesu Kristo. Ni sawa tu na Petro, au Yohana, au Yakobo, wangesema maneno kama hayo, wasingewezeka kupingana na Paulo kwasababu wanachokishuhudia wote ni kitu kimoja. Ndio maana tunaona maneno ya mitume wote, yameunganishwa katika kitabu kimoja kinachoitwa BIBLIA.

Lakini kwa nini Paulo aliongeze Neno hilo “sawasawa na injili yangu” Na asingeishia kwenye injili tu?.

Ni kwasababu wakati ule kulikuwa na watu waliomhubiri Yesu mwingine na injili nyingine, tofauti na ile waliyoihubiri mitume wa kweli.  Na hawa watu, wengi wao walikuwa ni  wayahudi wa tohara, Hivyo ilimbidi aliweke wazi hilo ili watu wabakie kwenye injili sahihi ya kweli.

Injili hizo Paulo aliziona kwenye makanisa kadha wa kadha kama tunavyosoma katika vifungu hivi;

2Wakorintho 11:4 Maana yeye ajaye akihubiri Yesu mwingine ambaye sisi hatukumhubiri, au mkipokea roho nyingine msiyoipokea, au injili nyingine msiyoikubali, mnatenda vema kuvumiliana naye!

Na..

Wagalatia 1:6 Nastaajabu kwa kuwa mnamwacha upesi hivi yeye aliyewaita katika neema ya Kristo, na

kugeukia injili ya namna nyingine. 7 Wala si nyingine; lakini wapo watu wawataabishao na kutaka kuigeuza injili ya Kristo.

Umeona, hiyo ndio sababu ya Paulo na kule Rumi kuitamka kauli hiyo, “sawasawa na injili yangu”. Ili kuwapa ufahamu kuwa hizo nyingine wanazozisikia huko nje, hazina uhai wowote wa kumwokoa mtu, au kumtetea siku ile ya hukumu.

Hata sasa, mambo ni yale yale, kumekuwa na madhehebu mengi, imani nyingi, ambazo zote zinadai ni za kikristo, lakini ukiangalia uhalisia wake humwoni Kristo ndani yake, wala injili ya Kristo. Fundisho lililo mule ndani sio fundisho la mitume. Watu hawahubiriwi  tena toba ya kweli na kumwangalia Kristo kama kiini cha wokovu wao. Wanafundishwa mambo mengine kabisa wengine mafanikio, wengine  uchawi, wengine  miujiza n.k kama ndio utimilifu wa ukristo. Sasa mambo kama hayo, hayaweza kumtetea mtu siku ya hukumu.

Bali injili ya Yesu Kristo, kupitia mitume wake. Ambayo ni hii biblia tuliyonayo, ndio tunayopaswa tuiegemee, kwasababu katika hiyo ndio tutakayohukumiwa.

Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

je! Paulo aliwalaani Wagalatia na Wakorintho?

Maana ya ‘Usimjibu mpumbavu sawasawa na upumbavu wake’

Kama wakitenda mambo haya katika mti mbichi, itakuwaje katika mkavu?

Rudi Nyumbani

Print this post

Silwano  ni nani,kama tunavyomsoma kwenye biblia?(1Petro 5:12)

Silwano ni matamshi mengine ya jina la Sila. Kwa kiyunani ni Sila, lakini kwa kilatino ni silwano. Hivyo Silwano ndio Sila yule tunayemsoma kwenye maandiko.

Habari ya Silwano/Sila hasaa tunaipata katika kitabu cha matendo ya mitume, huyu ni mmoja wa manabii wawili walioteuliwa na wazee wa kanisa la Yerusalemu kuambatana na Paulo na Barnaba katika kupeleka waraka wa makubaliano kwa makanisa ya mataifa.(Matendo 15:22).

Tunaona Sila na Yuda walipofika Antiokia, na kumaliza huduma yao, Yuda alirejea Yerusalemu, lakini Sila aliamua kuungana na Paulo katika ziara zake za kupeleka injili kwa mataifa.

Tunafahamu nini kuhusu Silwano/sila?

> Sila alipigwa na kufungwa pamoja na Paulo kule Filipi (Matendo 16:19-25).

> Sila anatajwa kama mwandishi mwenza wa kitabu cha Wathesalonike pamoja na Paulo(1&2 Wathesalonike 1:1).

 “Paulo, na Silwano, na Timotheo, kwa kanisa la Wathesalonike, lililo katika Mungu Baba, na

katika Bwana Yesu Kristo. Neema na iwe kwenu na amani.”

> Sila alihudumu Beroya.

Matendo ya Mitume 17:10

[10]Mara hao ndugu wakawapeleka Paulo na Sila usiku hata Beroya. Nao walipofika huko wakaingia katika sinagogi la Wayahudi.

> Alihudumu pia   Makedonia,  na Korintho pamoja na Paulo na wakati mwingine Timotheo (Matendo 15-18)

> Silwano anatajwa kama mjumbe wa mtume Petro, kama mwandishi wa ile barua yake ya kwanza,

> Lakini pia anatajwa kama mtu mwaminifu.

1 Petro 5:12

[12]Kwa mkono wa Silwano, ndugu mwaminifu kama nionavyo, nimewaandikia kwa maneno machache, kuonya na kushuhudia ya kuwa hii ndiyo neema ya kweli ya Mungu. Simameni imara katika hiyo.

Tunajifunza nini kwa Sila?

Uaminifu  aliokuwa nao ambao ulionekana na kutajwa mpaka kwa mitume, ni uaminifu wa kuwa tayari kujitoa maisha yake kwa ajili ya kuitetea injili bila kujali gharama yoyote.

Sila tunamfananisha na Ruthu, ambaye alipoambiwa arejee nyumbani kwake akakataa , akajilazimisha kwenda na Naomi katika hali ya ajane, katika nchi ya ugenini.

Ndivyo ilivyokuwa kwa Sila alikuwa na uwezo wa kurudi Yerusalemu pamoja na Yuda, kuhudumu kule lakini akakubali kwenda kwenda katika dhiki na Paulo mataifani. Lakini taabu yake haikuwa bure, bali kazi yake inatambulika mpaka leo.

Sila amekuwa kama kiungo wa kanisa la kwanza pamoja na mitume , tangu wazee wa kanisa Yerusalemu, mpaka Petro hadi Paulo anaonekana akihudumu nao tofauti na washirika wengine wa mitume, walikuwa wakiambatana na mtume Fulani maalumu, mfano tukimwona Timotheo hatuoni popote akihudumu pamoja na Petro, lakini Sila alikuwa kiungo kotekote.

Bwana atupe moyo kama wa Sila. Tupelekwapo, tunajitoa kikamilifu kabisa kwa kufanya zaidi ya tunavyoagizwa..

Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

Timotheo alikuwa wapi wakati anaandikiwa nyaraka zake na mtume Paulo?

ORODHA YA MITUME.

Mwandishi wa kitabu cha Matendo ya mitume.

Rudi Nyumbani

Print this post

BWANA, SISI TUNATAKA KUMWONA YESU.

SWALI: Kwanini wale wayunani, walimfuata Filipo na kumwambia tunataka kumwona Yesu, maudhui  ya tukio lile ni nini, mpaka lirekodiwe?


JIBU: Kipindi cha Bwana Yesu hadi kipindi chote cha mitume, yalikuwepo makundi mawili ya watu ambayo yalijikita kwa umakini sana katika kutafuta uhalisia na ukweli wote kuhusu masuala ya Mungu.

kundi la kwanza lilikuwa ni wayahudi, na kundi la pili ni wayunani. Tofauti ya wayahudi na wayunani ni kwamba. Wayahudi walijikita kuthibitisha kwa njia ya ishara. Lakini wayunani kwa hekima.

1 Wakorintho 1:22-23

[22]Kwa sababu Wayahudi wanataka ishara, na Wayunani wanatafuta hekima;  [23]bali sisi tunamhubiri Kristo, aliyesulibiwa; kwa Wayahudi ni kikwazo, na kwa Wayunani ni upuzi;

Hivyo Yesu ambaye ni jibu lao wote alipokuja, baadhi ya hawa wayahudi walipomwona Kristo wakaanza kumthibitisha kwa ishara kwa walivyotarajia, kwamba ndiye masihi na mkombozi waliyemtarajia la!.(wakitaka wafanyiwe matendo fulani ya ajabu mbele ya macho yao, waamini)

Ijapokuwa Mungu hathibitishwi kwa ishara, bado Kristo aliwapa ishara.. Na ishara hiyo ilikuwa ni ile ya Yona. kukaa katika moyo wa nchi siku tatu, usiku na mchana na hatimaye kutoka mzima.

Mathayo 12:38 Hapo baadhi ya waandishi na Mafarisayo wakamjibu, wakasema, Mwalimu, twataka kuona ishara kwako.

39 Akajibu, akawaambia, Kizazi kibaya na cha zinaa chatafuta ishara, wala hakitapewa ishara, ila ishara ya nabii Yona.

40 Kwani kama vile Yona alivyokuwa siku tatu mchana na usiku katika tumbo la nyangumi, hivyo ndivyo Mwana wa Adamu atakavyokuwa siku tatu mchana na usiku katika moyo wa nchi.

Hilo lilipokuja kutimia…tunaona wayahudi wengi waliamini, ikiwemo mitume (akina Tomaso). Na ndio ukawa mwanzo wa kumuhubiri Yesu aliyefufuka.

Lakini wale waliotazamia ishara walizoziwaza kwa akili zao, mfano  za kushusha moto, kama Eliya, na kusahau ile ya kufufuka ambayo imezidi zote, bado Kristo akabakia kikwazo kwao.

Halikadhalika na kwa wayunani. Walimtafuta Mungu kwa njia ya hekima, ya elimu, ya maarifa, walimtafuta Mungu mwenye siri zote za uumbaji, na ujuzi, na utashi zaidi ya wanadamu wote na viumbe vyote.Ambaye atawazidi wanafalsa wao kama Plato, Socrates, Aristotle.

Kwa muda mrefu hawakufanikiwa mpaka baadhi yao, wakaishia kumwabudu tu, huku wakikiri hawamjui.

Matendo  17:22-23

[22]Paulo akasimama katikati ya Areopago, akasema, Enyi watu wa Athene, katika mambo yote naona ya kuwa ninyi ni watu wa kutafakari sana mambo ya dini.

[23]Kwa sababu nilipokuwa nikipita huko na huko na kuyaona mambo ya ibada yenu, naliona madhabahu iliyoandikwa maneno haya, KWA MUNGU ASIYEJULIKANA. Basi mimi nawahubirini habari zake yeye ambaye ninyi mnamwabudu bila kumjua.

Yaani wakiwa na maana tunasikia miungu mingi,.lakini katika hiyo yote bado hatujaona mwenye hekima ya kuitwa Mungu wa ulimwengu. Wote akili zao ni kama za kibinadamu tu.

Sasa tukirudi kipindi cha Yesu, tunaona tukio jipya linajitokeza,

sio tu wayahudi walimwamini, bali hadi hawa wayunani watafuta-hekima wengi wao waliposikiliza maneno ya Yesu, na kupima kwa jicho la hekima, wakaona hakika hajawahi tokea anayeweza kuelezea ukweli wote wa uumbaji kama Yesu.

Hilo liliwashawishi na kuwafanya kukiri kuwa huyu ndiye suluhisho la utata wetu kuhusu Mungu na elimu.

Hivyo wakaamini, ndio sababu ya wao kumfata Filipo kumwomba wamwone Yesu. Hiyo ilikiwa ni heshima kubwa sana kwa Yesu  (kidini) mbele ya macho makuhani na mafarisayo wote, kwamba Mungu kathibitishwa kifalsafa. Kumbuka wayunani hawa waliokwenda hawakuwa watu tu wa kawaida. Bali ni watu wenye heshima ya juu sana na hadhi.

Hiyo ndio sababu Bwana Yesu  kusema saa imefika mwana wa  Adamu atukuzwe.

Yohana 12:20-26

[20]Palikuwa na Wayunani kadha wa kadha miongoni mwa watu waliokwea kwenda kuabudu kwenye sikukuu.

[21]Basi hao walimwendea Filipo, mtu wa Bethsaida ya Galilaya, wakamwomba, wakisema, Bwana, sisi tunataka kumwona Yesu.

[22]Filipo akaenda, akamwambia Andrea; kisha Andrea na Filipo wakamwambia Yesu.

[23]Naye Yesu akawajibu, akasema, Saa imefika atukuzwe Mwana wa Adamu.

[24]Amin, amin, nawaambia, Chembe ya ngano isipoanguka katika nchi, ikafa, hukaa hali iyo hiyo peke yake; bali ikifa, hutoa mazao mengi.

[25]Yeye aipendaye nafsi yake ataiangamiza; naye aichukiaye nafsi yake katika ulimwengu huu ataisalimisha hata uzima wa milele.

[26]Mtu akinitumikia, na anifuate; nami nilipo, ndipo na mtumishi wangu atakapokuwapo. Tena mtu akinitumikia, Baba atamheshimu.

Ni nini cha tunafundishwa katika habari hii ya wayunani?

Hata leo, Yesu anathibitika katika mambo yote endapo tu tutamaanisha kumwona katika namna hizo. Ndio maana katika makundi yote ya watu ni lazima utakuta waamini.

Katika ya wanasayansi utawaona, katikati ya wanajeshi utawaona, katikati ya watawala utawaona,katikati ya mamajusi utawaona, katikati ya  matajiri utawaona, katikati ya maskini utawaona, kati ya wanazuoni utawaona, kati ya madaktari utawaona,

Ukiuliza imekuwaje katika hali zao/ nafasi zao ambazo ni mbaya, na nyingine zenye majaribu, au zenye kumkana Mungu waziwazi, lakini wao wamemwamini Mungu?.

Ni kwasababu YESU anathibitika kila mahali.

Mtu kutokuamini ni yeye mwenyewe kataka. Hakuna atakayekuwa na udhuru siku ya mwisho, kwasababu Yesu amefunuliwa kila mahali.

Swali ni je! umemwamini Kristo?  kama ni la! unasubiri nini. Mwamini leo kwa kuikubali kazi aliyoikamilisha juu yako ya kuondoa dhambi kwa kifo na kufufuka kwake. Ambayo hiyo huambatana na toba ya kweli na ubatizo.

Baada ya hapo utakuwa umepokea ondoleo la dhambi zako bure, mpokee Yesu sasa

Mungu akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

Nawiwa na Wayunani na wasio Wayunani.

Utawanyiko wa Wayunani ulikuwaje?

ALIYOKUTANA NAYO YESU, YERIKO.

SAUTI NYUMA YA ISHARA.

Rudi Nyumbani

Print this post