SWALI: Hapo Bwana wa mabwana anamaanisha nini kusema ‘ Ni rahisi zaidi ngamia kupenya tundu ya sindano ’..Je! ni sindano ipi hiyo inayozungumziwa? Maana kisasa tuna sindano za kushona nguo,sindano za kushonea mwili wa binadamu,sindano yakushonea viatu,sindano yakumchoma mtu (za madawa) Ni sindano ya Aina gani ameizungumzia hapo kwenye Mathayo19:23).
JIBU: Kama tunavyoifahamu habari hiyo ni kuwa mtu tajiri alimfuata Bwana Yesu, na kumuuliza atende jambo gani jema ili aurithi uzima wa milele, Ndipo Bwana akamwambia Umezishika Amri? Yule kijana akasema hizo nimezishika tangu utoto wangu ,nimepungukiwa na nini tena?. Bwana akampenda sana lakini akamwambia ukitaka kuwa mkamilifu nenda kauze vyote ulivyonavyo kisha unifuate, lakini Yule kijana aliposikia vile aliondoka kwa huzuni kwasababu alikuwa na mali nyingi..Ndipo Bwana akawaambia wanafunzi wake maneno haya.
Mathayo 19:23 “Yesu akawaambia wanafunzi wake, Amin, nawaambieni, ya kwamba itakuwa shida tajiri kuingia katika ufalme wa mbinguni.
24 Nawaambia tena, Ni rahisi zaidi ngamia kupenya tundu ya sindano, kuliko tajiri kuingia katika ufalme wa Mungu.”
Sasa tundu linalozungumziwa hapo, inaaminiwa na baadhi ya watafiti wa mambo ya kale kuwa ni mlango mdogo ambao ulijengwa katika kuta za Yerusalemu uliokuwa unafunguliwa wakati wa usiku muda ambao geti kubwa la mji limefungwa kwa usalama wa mji na ulinzi..…Mlango huo ulijulikana Kwa jina hilo TUNDU LA SINDANO.
Ulikuwa ni mdogo kiasi cha mtu na wanyama wadogo tu kupita, lakini kwa wanyama wakubwa kama ngamia haikuwa rahisi na kama ikitokea anapaswa apite basi ni lazima ngamia atolewe mizigo yake yote , na apitishwe kwa kupigishwa magoti kwa shida sana, haikuwa rahisi hata kidogo….
Lakini nadharia hiyo haina uthibitisho wa moja kwa moja kuwa kulishawahi kuwa na mlango kama huo Yerusalemu. Uwezekano mwingine ni kuwa Watafsiri na wachambuzi wa maandiko wamegundua kuwa Neno ngamia kwa lugha ya KIARAMU linakaribiana sana kufanana na neno UZI, Hivyo wanasema watafsiri wa kwanza wa vitabu vya Agano jipya, walipokuwa wanatafsiri baadhi ya maneno kutoka katika Lugha ya kiaramu kwenda kwenye lugha kiyunani, walilitafsiri tofuati neno hilo wakidhani ilimaanisha pale ngamia kumbe ni UZI mpana, na kwamba ingepaswa isomeke hivi… Nawaambia tena, Ni rahisi zaidi Uzi mpana kupenya tundu la sindano, kuliko tajiri kuingia katika ufalme wa Mungu.” Na hivyo sindano inayozungumziwa pale ni Sindano kama sindano halisi kabisa ile ya Kushonea..
Lakini kwa vyovyote vile, tunapaswa kufahamu kiini cha ujumbe ambacho tunakipata katika habari ile…Pale tunaona Bwana alikuwa anajaribu kutueleza ugumu uliopo kwa watu wenye kutegemea mali kuingia katika ufalme wa mbinguni ndipo akatumia mfano ule ili kutilia msisitizo zaidi…
Ni sawa tu na pale aliposema “toa boriti iliyo katika jicho lako, ndipo uone vema kutoa kibanzi kilicho katika jicho la ndugu yako…Lakini kiuhalisia kibanzi au boriti haviwezi kukaa katika macho ya mtu…Lakini ili kufikisha ujumbe kwa uzito zaidi ilimpasa Bwana atoe mifano ya namna hiyo, ambayo kiuhalisia haiingia akilini, kama mahali pengine aliposema, mnachuja mbu, na kumeza ngamia…
Na ndivyo ilivyo katika habari hii..hatushangai pia akimaanisha kama ilivyoandikwa pale ngamia kupenya katika sindano ya kushonea.
Ubarikiwe.
Mada Nyinginezo:
NJIA YA ‘UTAJIRI MKUU’ KWA KIJANA.
MADHARA YA KUKOSA MAJI YA UZIMA BAADA YA KIFO.
BWANA YESU ANAMAANISHA NINI KUSEMA “WALA MSIMWITE MTU BABA DUNIANI”?
TAFUTA KUMJUA MUNGU ZAIDI YA SHETANI
SWALI: Bwana wetu YESU ametuahidi tumuombe jambo lolote lile KWA JINA LAKE YESU naye atalifanya..Mahali pengine anatuambia maombi yetu Watakatifu ni harufu nzuri ya manukato mbele zake..(Sasa mfano mimi nanyi tunaye rafiki yetu mpendwa amefariki na kila siku tulikuwa tukimuomba Mungu amkumbuke kwenye ufalme wake wa mbinguni,unajua hili lipo ndani ya karibu binadamu wote kwamba mtu wako wa karibu akifa KITU FULANI kinakuwa kinaning’inia moyoni mwako KUMTAKIA HATIMA NZURI YA MAISHA YAKE MBELE ZA MUNGU..hivyo ukimtakia mpendwa wako wa karibu aliyefariki kwa KUMUOMBEA mbele za Mungu (aliyetuambia maombi yetu Watakatifu ni harufu nzuri ya manukato mbele zake hivyo tumuombe tu lolote kwa JINA LA YESU) AMUOKOE NA KUZIMU. Je! kuna ubaya gani hapo? ukimuombea mtu aliyefariki kila siku mbele za Mwenyezi Mungu amkumbuke kwenye ufalme wake wa mbinguni KWA JINA LA YESU?.
JIBU: NI kweli tunajua Mungu anaweza mambo yote, lakini sifa yake nyingine ni kuwa hafanyi mambo yote. Alivyotuumba sisi wanadamu hakutuumba kama Ma-robot kwamba lisipoongozwa na mwanadamu haliwezi kufanya jambo lolote lenyewe….Pale aliposema katuumba kwa mfano wake, alimaanisha kweli kweli kusema vile!!, ikiwa na maana kuwa kwa sehemu Fulani mtu anaweza akajiamulia mambo yake mwenyewe binafsi bila hata ya kuingiliwa na mtu yeyote kana kwamba kajiumba mwenyewe kama Mungu.. Na jambo kubwa ambalo Mungu kamuumbia mwanadamu ni uhuru wa MAAMUZI, ambayo hata yeye mwenyewe muumbaji, mwenye sifa ya kutoshindwa kufanya jambo lolote anayaheshimu, kiasi cha kutoyaingilia, au kuyaathiri MAAMUZI YA MTU ikiwa tu mtu anaridhika kuwa nayo.
Mfano leo hii mtu akiamua kuwa mchawi kwa matakwa yake mwenyewe, Mungu haji kumwambia ni Nani amekupa ruhusa ya kuwa hivyo?, atakachofanya ni kumshawishi atoke huko, ataugua moyoni mwake kila kukicha ili aiache dhambi hiyo atampelekea mpaka watumishi wake kila kukicha kumuhubiria madhara ya kuwa mchawi, kwamba mwisho wa siku watu wa namna hiyo wataishia katika ziwa la moto..Hivyo mtu Yule akikubali kuitii ile sauti na kugeuka, Mungu ndio anatembea naye na kumwongoza katika njia sahihi zaidi, lakini kama hatakubali Mungu haji kumlazimisha kwa nguvu aache, hiyo haijawahi kuwa kanuni yake tangu mwanzo kwa viumbe vyake vyote..Hata shetani na mapepo yote hakuyafanyia hivyo.
Hivyo maombi yetu hayawezi kuvuka maamuzi ya mtu binafsi, Kama tu vile uweza wa Mungu usivyoweza wa kugeuza maamuzi ya mtu binafsi, kwasababu Kumbuka biblia inasema pia si mapenzi ya Mungu watu wapotee, bali wote waifikie toba,(2Petro 3:9) lakini leo hii kwanini tunaona watu wanapotea, japo anao Uwezo wa kuwafanya wasipotee?..Ni kwasababu kuna mipaka kajiwekea hawezi kuivuka..
Kadhalika mtu aliyepo kwenye dhambi maombi yetu tunayomwombea sio kwamba yanakwenda moja kwa moja kutangua maamuzi yake ya kuacha dhambi hapana! Bali yanafanya kazi ya kuongeza ushawishi wa Roho Mtakatifu ndani ya mtu, na ushawishi unavyozidi kuwa mwingi..mtu yule ndipo anaamua kugeuka kwa hiyari yake na hivyo tunasema tumempata. Leo hii kama mtu kaamua kuwa mtumishi wa shetani kwa akili zake mwenyewe, anasema hamtaki Mungu, sisi tukimwombea Mungu atakachofanya ni kumshawishi ndani ya moyo wake..
Lakini zaidi ya hapo hafanyi..hivyo hata tumwombeeje, kama anazidi kuukataa ule ushawishi ndani yake hapo haiwezekani kumgeuza. Sasa mpaka mtu amefikia hatua ya kufa, na ameenda kuzimu, ni wazi kuwa tangu akiwa hai aliichagua mwenyewe njia ya upotevuni, na sasa maisha yake yamekwisha akiwa katika hali hiyo, amefikia wakati wa mavuno wa kuvuna alichokipanda..Haiwezekani tena sio tu kumwombea, hata yeye mwenyewe kuweka nia ya kutoka huko, kama tu vile waliokufa katika haki haiwezekani tena wao kutoka kule peponi na kushuka kuzimu.
Hivyo ni vizuri kuutumia wetu vizuri tukiwa hapa duniani, Kwani kuna baadhi ya Imani ikiwemo Imani ya kanisa Katoliki zinaamini kuwa watu waovu wanapitia TOHARANI, , ili kusafishwa kabla ya kwenda mbinguni, kwa maelezo marefu juu ya somo hilo nitumie ujumbe inbox nikutumie habari yake.. Lakini huo ni opotofu mkubwa wa shetani, kuwafanya watu wastarehe katika dhambi zao wakidhani kuwa ipo nafasi ya pili..Biblia inasema: Waebrania 9:27 “Na kama vile watu wanavyowekewa kufa mara moja, na baada ya kufa hukumu;” Hakuna tumaini lolote, kwa aliye kufa ikiwa, amekuta katika dhambi.
Ubarikiwe sana.
Mada Nyinginezo:
NI SAHIHI KWA MKRISTO MTAKATIFU KUMWAMBIA BWANA AILAZE ROHO YA MTU ALIYEKUFA MAHALI PEMA PEPONI?
BWANA ALIMAANISHA NINI KUSEMA “WAACHE WAFU WAZIKE WAFU WAO.(MATHAYO 8:21)?
AMEFANYIKA BORA KUPITA MALAIKA!
SWALI: Shalom Wapendwa Samahani Nilikuwa Nauliza Katika Kitabu Cha Yohana 2:1 Na Kuendelea Katika Harusi Ya Kana Yesu alitumia “MABALASI” ile Mitungi Ya Kujitawadhia kugeuza maji kuwa Divai, swali linakuja je? ilikuwa ni kawaida kutumia hiyo mitungi kuwekea divai au kulikuwa na vyombo vingine.
JIBU: Mabalasi vilikuwa ni vyombo maalumu vya kuhifadhia vitu…Ni kama leo tuseme mapipa!..unaweza kwenda mahali ukakuta nyumba moja pipa wanalitumia kuwekea maji ya kunywa, pengine wanawekea mbegu za mazao, mahali pengine wanatumia pipa kuhifadhia pombe wanazotengeneza, sehemu nyingine wanatumia kuwekea maji ya kwendea bafuni n.k Na hapo katika habari hiyo, Mabalasi ni kama mapipa, isipokuwa hapo yalitumika kwa kutawadhia. Na kutawadha kunakozungumziwa hapo, sio kule kwa chooni, bali ni kule mtu anapojisafisha sehemu baadhi za mwili kama mikono na miguu…kabla ya kuingia kwenye Ibada, hiyo ilikuwa ni desturi za Wayahudi,…Na ilikuwa mtu hajisafishi ndani ya hilo balasi, hapana! Bali anachota maji kutoka kwenye hilo balasi na kujisafisha kando…
kama Bwana Yesu alivyowatawadha wanafunzi wake miguu kabla ya kushiriki meza ya Bwana (soma Yohana 13:1-18)…Hivyo mabalasi hayo ya kutawadhia vilikuwa ni vyombo visafi na si vichafu. Na kwanini Bwana Yesu aliagiza yatumike hayo Mabalasi na si vyombo vingine?…Ni kwasababu ndio vyombo pekee vilivyokuwa karibu na pale alipo (maeneo yale) na vilikuwa tupu
Yohana 2:6 “Basi kulikuwako huko mabalasi sita ya mawe, nayo yamewekwa huko kwa desturi ya Wayahudi ya kutawadha, kila moja lapata kadiri ya nzio mbili tatu.
7 Yesu akawaambia, Jalizeni mabalasi maji. Nao wakayajaliza hata juu”.
Ni kama tulivyosema, pipa hilo hilo linaweza kutumika kuhifadhia pombe, na pipa hilo hilo linaweza kutumika kuhifadhia maji, au mazao au taka, n.k…. Hivyo kama biblia inavyotuambia hapo mabalasi hayo yalitumika kwa ajili ya kutawadhia…lakini Bwana Yesu alilyaona yanaweza kufaa pia kwa kuwekea divai, ndipo akageuza maji yale kuwa divai ndani ya mabalasi yale, na watu walikunywa bila kuona shida yoyote wala kinyaa..kwasababu pengine ilishazoeleka na ilikuwa inajulikana kuwa mabalasi pia yanatumikaga kwa shughuli za kuhifadhia Divai ..
Ubarikiwe!
Mada Nyinginezo:
MTEGEMEE MUNGU, NA SI MWANADAMU.
UNALITUMIA KWA HALALI NENO LA KWELI?.
SWALI: Habari mtumishi…, ninaswali hapa naomba uniweke sawa.
Matendo ya mitume 8:14 “ na Mitume waliokuwako Yerusalemu, waliposikia ya kwamba Samaria imelikubali neno la Mungu,wakawapelekea Petro na Yohana,
15.ambao waliposhuka, wakawaombea wampokee Roho Mtakatifu,
16. kwa maana bado hawajashukia hata mmoja wao, ila wamebatizwa tu kwa jina la Bwana Yesu.
17.Ndipo wakaweka mikono yao juu yao, nao wakampokea Roho Mtakatifu”..
Sasa swali langu limegawanyika katika vipengele 3..a) Je! unaweza kubatizwa na usimpokee Roho Mtakatifu kama hawa watu wa Samaria ilivyokua?. b) Je! unaweza mpokea Roho Mtakatifu kwa kuombewa kama Petro na Yohana walivyofanya?. c) Kwa jamii yetu ya kawaida ni kigezo gani kinatumika kwa mtu kuwabatiza wengine au awe na sifa zipi huyo mbatizaji ili tupate ubatizo sahihi?
JIBU: Shalom, Bwana akubariki kwa swali zuri, Kwanza ni muhimu kufahamu umuhimu wa ubatizo sahihi, Ubatizo sahihi ni kama Leseni ya Roho Mtakatifu kukaa ndani ya mtu, yaani mtu anapobatizwa katika ubatizo sahihi, amemhalalisha Roho Mtakatifu kuingia ndani yake na kuwa wake.
Hivyo Roho Mtakatifu anaweza kushuka juu ya mtu kabla au baada ya kubatizwa, lakini uhalali wa kukaa moja kwa moja ndani ya mtu unakuja baada ya mtu kubatizwa. Sasa tukirudi kwenye swali la kwanza linalouliza “a) Je! unaweza kubatizwa na usimpokee roho mtakatifu kama hawa watu wa Samaria ilivyokua?” Jibu ni ndio! Kama umeamini na kutubu dhambi zako kwa kudhamiria kuziacha, na ukaenda kubatizwa, lakini hujawahi kusikia lolote juu ya Roho Mtakatifu, hapo hawezi kuingia ndani yako, kwasababu Roho hawezi kuja juu ya mtu ambaye hajawahi kabisa kuzisikia habari zake, ni sharti kwanza mtu huyo ahubiriwe Roho Mtakatifu ni nini, ndipo ashuke juu yake, Hata Bwana Yesu hawezi kuingia ndani ya moyo wa Mtu kama mtu huyo hajahubiriwa kabisa, au hajawahi kusikia kabisa habari za Yesu…. hivyo Kwa mtu aliyeamini na kutubu na kubatizwa ipasavyo, Roho Mtakatifu mwenyewe atahakikisha anamletea mhubiri ambaye atamweleza kuwa kuna kitu kinachoitwa Roho Mtakatifu ndipo ashuke ndani yake. Ndicho kilichotokea kwa hawa watu wa Samaria na wale Wakorintho Paulo aliokutana nao..
Matendo 19:1 “Ikawa, Apolo alipokuwa Korintho, Paulo, akiisha kupita kati ya nchi za juu, akafika Efeso; akakutana na wanafunzi kadha wa kadha huko;
2 akawauliza, Je! Mlipokea Roho Mtakatifu mlipoamini? Wakamjibu, La, hata kusikia kwamba kuna Roho Mtakatifu hatukusikia.
3 Akawauliza, Basi mlibatizwa kwa ubatizo gani? Wakasema, Kwa ubatizo wa Yohana.
4 Paulo akasema, Yohana alibatiza kwa ubatizo wa toba, akiwaambia watu wamwamini yeye atakayekuja nyuma yake, yaani, Yesu.
5 Waliposikia haya wakabatizwa kwa jina la Bwana Yesu.
6 Na Paulo, alipokwisha kuweka mikono yake juu yao, Roho Mtakatifu akaja juu yao; wakaanza kunena kwa lugha, na kutabiri.
7 Na jumla yao walipata wanaume kumi na wawili”.
Na pia Roho Mtakatifu anaweza kushuka juu ya mtu kabla hajabatizwa endapo tu atakuwa ameshasikia kuwa kuna kitu kinachoitwa ROHO MTAKATIFU, kama mtu ameshasikia kuwa kuna kitu kinaitwa Roho Mtakatifu na jinsi anavyotenda kazi, basi Roho anaweza kushuka juu ya huyo mtu kabla hata hajabatizwa, lakini ili awe na uhalali wa kukaa ndani ya huyo mtu ni lazima mtu huyo akabatizwe ili kukamilisha wokovu wake…Ndicho kilichotokea kwa Kornelio akida wa Kirumi wakati Petro amekwenda nyumbani kwake..
Matendo : 10:44 “Petro alipokuwa akisema maneno hayo Roho Mtakatifu akawashukia wote waliolisikia lile neno
45 Na wale waliotahiriwa, walioamini, wakashangaa, watu wote waliokuja pamoja na Petro, kwa sababu Mataifa nao wamemwagiwa kipawa cha Roho Mtakatifu.
46 Kwa maana waliwasikia wakisema kwa lugha, na kumwadhimisha Mungu. Ndipo Petro akajibu,
47 Ni nani awezaye kuzuia maji, hawa wasibatizwe, watu waliopokea Roho Mtakatifu vile vile kama sisi?
48 Akaamuru wabatizwe kwa Jina lake Yesu Kristo. Ndipo wakamsihi azidi kukaa siku kadha wa kadha”.
Swali la pili linasema “Je! unaweza mpokea Roho Mtakatifu kwa kuombewa kama Petro na Yohana walivofanya?” Jibu ni ndio! Unaweza kupokea Roho Mtakatifu kwa kuwekewa mikono, lakini sio wakati wote!.. mara nyingi watu wanapokea Roho pasipo hata kuwekewe mikono, mfano siku ya Pentekoste mitume hawakuwekewa mikono na mtu yeyote, na hata wakati Petro yupo nyumbani kwa Kornelio kama tulivyosoma hapo juu, wale watu hawakuwekewa mikono na mtu yeyote lakini Roho alishuka juu yao..hivyo Roho anaweza kushuka juu ya mtu aidha kwa kuwekewa mikono na watiwa Mafuta wake au bila kuwekewa mikono. Ni kwa jinsi Roho atakavyopenda!..Na kwa jinsi Roho atakavyomuongoza yule anayehudumu. Swali la tatu … “kwa jamii yetu ya kawaida ni kigezo gani kinatumika kwa mtu kuwabatiza wengine au awe na sifa zipi huyo mbatizaji ili tupate ubatizo sahihi?”
Jibu: Vigezo vinavyotumika vya mtu kuwabatiza wengine ni vigezo vile vile vya mtu anayetaka kuwa mhubiri!..Mtu akitaka kuwa mhubiri, au mwalimu kwa wengine ni sharti kwanza awe mwanafunzi wa Kristo, pili awe na uwezo wa kufundisha wengine kitu ambacho yeye mwenyewe anakiishi, na awe na uelewa wa kutosha wa kitu anachokwenda kukifanya, Awe Ameitwa na Mungu kweli na anafahamu kuwa anafanya kazi ya Mungu na si ya mwanadamu…
Kadhalika mtu anayetakiwa kubatiza wengine anapaswa na yeye mwenyewe kwanza awe amebatizwa katika ubatizo sahihi, na awe na uelewa wa kutosha kuhusu ubatizo yaani faida za kubatizwa na hasara za mtu kutokubatizwa ili aweze kuwafundisha vyema wale ambao watakuja kubatizwa naye!. Mtu mwingine yoyote asiyekuwa na vigezo hivyo haruhusiwi kifanya kitendo hicho kitakatifu.
Bwana akubariki!
Mada Nyinginezo:
JINSI ROHO MTAKATIFU ANAVYOKUJA JUU YA MTU.
JE! NI LAZIMA WATU WOTE WANENE KWA LUGHA?
ROHO ZILIZO CHINI YA MADHABAHU:
AMIN! NAWAAMBIA KIZAZI HIKI HAKITAPITA.
JIBU: Tunapaswa tufahamu mistari hiyo ilikuwa inalenga katika Nyanja gani, mfano kama tukisoma huo wa Yakobo1:13 Unasema
“Mtu ajaribiwapo, asiseme, Ninajaribiwa na Mungu; maana Mungu hawezi kujaribiwa na maovu, wala yeye mwenyewe hamjaribu mtu.
14 Lakini kila mmoja hujaribiwa na tamaa yake mwenyewe huku akivutwa na kudanganywa.
15 Halafu ile tamaa ikiisha kuchukua mimba huzaa dhambi, na ile dhambi ikiisha kukomaa huzaa mauti.”
Unaona ukiangalia hapo kwa makini utagundua kuwa analenga katika mambo maovu, kwamfano uzinzi, au ulevi, uchawi, usengenyaji, wizi,n.k. Kwamfano utakuta mtu ni mkristo, na hapo mwanzo alikuwa hazini wala hanywi pombe, lakini pengine ghafla mbele yake kikapita kichocheo kimojawapo cha zinaa labda tuseme kahaba, au picha chafu za ngono, sasa yeye badala avikatae na avikimbie hivyo vichochezi yeye kidogo kidogo anavutiwa navyo na kuanza kuvifuatilia au kudokoa na kuvitazama, huko ndiko kuvutwa na kudanganywa kwenyewe kunakozungumziwa hapo, na kama akizidi kuendelea kuviendekeza hivyo vichocheo baadaye vinazaa dhambi hapo ndipo unakuta mtu wa namna hiyo anaingia katika uzinzi moja kwa moja, na anakuwa mbaya kuliko hata wale aliowakuta huko na mwisho wa siku anazaa mauti kwasababu ile dhambi ilisha komaa hapo hawezi kugeuka tena kilichosalia ni kwenda kwenye ziwa la moto.
Sasa mtu kama huyo hawezi kusema Mungu alikuwa anamjaribu,kumletea kahaba, kwasababu Mungu hashikamani na ouvu wa aina yoyote..bali ni tamaa ya mambo yake ndio iliyokuwa inamvuta huko. Yusufu alipojaribiwa na mke wa Potifa sio Mungu aliyekuwa anamjaribu pale, bali ni ouvu, lakini yeye aliishinda kwasababu hakuiendekeza hiyo roho.
Lakini pia ifahamike kuwa mtu yeyote anapoamua kumfuata Mungu, inamaanisha kuwa anakuwa mwanafunzi wa Kristo moja kwa moja, na tunajua kuwa hakuna mwanafunzi yeyote anayesoma tu bila kujaribiwa kwa mitihani, hiyo haipo?, Mwalimu atajuaje kuwa huyu mwanafunzi ameelewa au la, Vinginevyo shule itajikuta inaandaa watu wasiokuwa na uwezo wa kitaaluma, Vivyo hivyo kwa Mungu pia kuna mitihani,unajaribiwa kuangaliwa kama umekidhi vigezo au la! Na kujaribiwa huko hakuna lengo la kukuangusha, bali kukuimarisha. Mwalimu yoyote mwenye akili timamu hawezi kuwajaribu wanafunzi wake kwa kuwachanganya kwenye bweni moja wanafunzi wa kike na wa kiume walale humo humo, kwa lengo la kupima kiwango chao cha elimu..huko ni kuwapoteza na sio kuwafundisha, bali atawapa mitihani kulingana na wanachofundishwa darasani, Na ndivyo Mungu anavyofanya kwa watoto wake wote, hawajaribu kwa maovu, bali kwa yale waliyokuwa wanafundishwa na kuyapitia katika imani yao, na ndio yaliyomkuta Ibrahimu na ndiyo yaliyowakuta wana wa Israeli na ndiyo yatakayokukuta wewe ambaye unasema umeamua kumfuata Kristo..
Mwanzo 22:1 “Ikawa baada ya mambo hayo Mungu ALIMJARIBU Ibrahimu, akamwambia, Ee Ibrahimu! Naye akasema, Mimi hapa.
2 Akasema, Umchukue mwanao, mwana wako wa pekee, umpendaye, Isaka, ukaende zako mpaka nchi ya Moria, ukamtoe sadaka ya kuteketezwa huko juu ya mlima mmojawapo nitakaokuambia.”
Ukisoma tena habari ya wana Israeli walipokuwa jangwani utaona Mungu akiwaambia hivi…
Kumbukumbu 8:2 “Nawe utaikumbuka njia ile yote Bwana, Mungu wako aliyokuongoza miaka hii arobaini katika jangwa, ili akutweze, KUKUJARIBU kuyajua yaliyo moyoni mwako, kwamba utashika amri zake, au sivyo.
3 Akakutweza, akakuacha uone njaa, akakulisha kwa mana, usiyoijua wewe wala baba zako hawakuijua; apate kukujulisha ya kuwa mwanadamu haishi kwa mkate tu, bali huishi kwa kila litokalo katika kinywa cha Bwana.
4 Mavazi yako hayakuchakaa, wala mguu wako haukuvimba, miaka hiyo arobaini.”
Vivyo hivyo leo hii unaweza kusema umemfuata Yesu, lakini kusema hivyo tu haitoshi, Mungu ataipima imani yako kwake,..pengine anaweza kuruhusu ukachekwa kwa ajili ya wokovu wako, aangalie je! Utauacha?, ataruhusu uchukiwe na kutengwa na ndugu, aangalie je! Kweli ulimaanisha kumfuata?, ataruhusu upitie kupungukiwa aangalie je! Unampenda wakati wa raha tu, au hadi wakati wa mateso, ataruhusu upitie hiki au kile..Huko ndio kujaribiwa na Mungu. Lakini Mungu hawezi kukuletea pombe, au kahaba, au hirizi au pesa haramu, ukasema ni Mungu anakujaribu,,ukikutana na mambo ya namna hiyo maovu fahamu kuwa unajaribiwa kwa tamaa zako mwenyewe sio kwa ajili ya IMANI yako.
Ubarikiwe.
Mada Nyinginezo:
MAJARIBU MATATU YA YESU KRISTO.
AYUBU ALITESEKA KATIKA MAJARIBU KWA MIAKA MINGAPI?
TUTAWEZAJE KUMZALIA MUNGU MATUNDA?
FUATILIA NDOTO HII, UTAJIFUZA KITU.
KWANINI NABII ISAYA ALIAGIZWA KUHUBIRI UCHI?
SWALI: Shalom watumishi wa Mungu Leo nina swali nataka niulize maana linanitatiza jambo hili ni kutoka kitabu cha Isaya.
Isaya 54:9 “ Kwa maana jambo hili limekuwa kama maji ya Nuhu kwangu; maana kama nilivyoapa ya kwamba maji ya Nuhu hayatapita juu ya dunia tena, kadhalika nimeapa ya kwamba sitakuonea hasira, wala kukukemea.
10 Maana milima itaondoka, na vilima vitaondolewa; bali wema wangu hautaondoka kwako, wala agano langu la amani halitaondolewa; asema Bwana akurehemuye”
Je! swali lina kuja hivi mtumishi Leo hii kuna watu nimewaskia wakisema hakuna ghadhabu ya Mungu tena mana amekwisha sema maji ya Nuhu hayatapita tena na tunajua maji ya Nuhu ilikua ni siku ya mwisho ya dunia je! ni kweli Mungu hata shusha hasira yake tena? kuna watu wana sadiki kujitetea na maovu yao kupitia neno hli wakisema hakuna hukumu tena maana Mungu amekwisha apa!
JIBU: Shalom! Ni kweli Mungu hataingamiza dunia tena kwa maji, kama Neno lake hilo linavyosema hapo juu! Lakini hiyo haimaanishi kuwa dunia haitaangamizwa, itaangamizwa lakini sio kwa maji, bali na kwa kitu kingine, kwasababu Neno linasema kama zilivyokuwa katika siku za Nuhu, ndivyo itakavyokuwa katika siku za kuja kwake mwana wa Adamu (yaani siku za mwisho) kwahiyo kama siku za Nuhu ulimwengu uliangamizwa kwa maovu yake, kadhalika na siku hizi za mwisho ulimwengu utaangamizwa vile vile kwa maovu yake..lakini si kwa maji. Na kama si kwa maji basi ni kwa kitu gani?…Jibu lipo kwenye biblia hiyo hiyo..tusome:
2 Petro 3:5 “Maana hufumba macho yao wasione neno hili ya kuwa zilikuwako mbingu tangu zamani, na nchi pia, imefanyizwa kutoka katika maji, na ndani ya maji, kwa neno la Mungu;
6 kwa hayo dunia ile ya wakati ule iligharikishwa na maji, ikaangamia.
7 Lakini mbingu za sasa na nchi zimewekwa akiba kwa moto, kwa neno lilo hilo, zikilindwa hata siku ya hukumu, na ya kuangamia kwao wanadamu wasiomcha Mungu”
Kwahiyo siku sio nyingi dunia hii itakwenda kugharikishwa KWA MOTO!..Usidanganyike hata kidogo kuwa hakuna hukumu inayokuja!..Hukumu ni lazima ije kwasababu Mungu alishasema ni lazima ije!..Hivyo ni kuwa macho na kukesha katika roho ili siku hiyo isitujie kama mwivi.
Ubarikiwe.
Mada Nyinginezo:
SIKU YA BWANA INAYOTISHA YAJA!
Naomba kujua watakaoenda mbinguni je! ni wengi au wachache?
JIBU: Shalom, utaona katika mstari huo anatumia neno “Tupa” na sio hifadhi au weka, ikiwa na maana ya kupoteza kitu chako cha thamani, chakula chako, na hapo anaendelea kusema kitupe usoni pa maji, ukisoma tafsiri nyingine utaona anasema kwenye habari, au maji mengi, na tunafahamu sikuzote ukitupa kitu mtoni au ziwani au baharini hapo ni kuhesabu kuwa umekipoteza hutakipata tena, sembuse chakula, ambacho kinayenyuka na kuoza haraka..
Lakini kinyume chake mhubiri anatuambia, “maana utakipata baada ya siku nyingi”..Ili kuelewa vizuri huo mstari tusome mistari inayofuata baada ya hiyo, 1 Tupa chakula chako usoni pa maji; Maana utakiona baada ya siku nyingi.
(Mhubiri 11: 2 Uwagawie sehemu watu saba, hata wanane; Maana hujui baa gani litakalokuwa juu ya nchi.
Maji mengi kwenye biblia yanawakilisha “watu wengi au mataifa, au makutano (soma Ufun.17:15)”….Unaona, kumbe alimaanisha uwagawie watu sehemu ya fungu lako, bila kujali malipo au watakurudishia nini, unafanya kama unapoteza, Kwamfano unaweza ukawa unavi hazina kidogo kwenye mfuko wako na pengine anatokea mtoto wa ndugu yako anaomba msaada wa ada ya shule, huku mwingine anakuomba chakula, mwingine anakuomba nguo, mwingine anakuomba hifadhi, maadamu vipo ndani ya uwezo wako fanya kuwapa tu kama vile huna matumizi na hiyo fedha, kwasababu biblia inasema hujui mbeleni kutakuwaje, pengine huyo mtu unayemsaidia sasa anaweza akawa msaada mkubwa sana kwako au kwa watoto wako, au kwa ndugu zako.
Tajiri mmoja wa kidunia ambaye leo hii anajulikana duniani kote anayeitwa Bill Gates, zamani alipokuwa kijana mdogo, alipenda kwenda kusoma magazeti, lakini kwa bahati mbaya alikuwa hana pesa ya kununa gazeti lakini mahali hapo kulikuwa na mzee mmoja mwafrika mweusi, alimnunuliza magazeti, hilo lilimwingia sana moyoni, miaka mingi ikapita akaanza kufanikiwa na kuwa tajiri sana kwa ugunduzi wake wa Microsoft, akakumbuka wema aliofanyiwa na huyo mzee, alingarimika kumtafuta popote alipo, alipomwona alimpatia kiasi cha dolla milioni moja, ambayo kwa pesa yetu ni zaidi ya sh. Bilioni 2,.Unaona gazeti la sh.1000, linakuja kumzaliwa Bilioni 2. Miaka mingi baadaye.
Hivyo Mhubiri anatufundisha hekima ya maisha ya kawaida, kuna usemi unaosema “kinachokwenda nje ndicho kinachokurudia”, leo hii mtu ukiwa mbinafsi na kuwadharau wengine kwa mafanikio yako kidogo uliyopewa na Bwana, ziangalie pia siku za mbeleni kwa jinsi ya kibinadamu. Na ndio maana hapo anasema sehemu, uwagawie watu 7 hata nane,.Hii Ikimaanisha usichague aina Fulani tu ya watu, tupa kokote,poteza kokote utakuja kupata hicho ulichokipoteza baada muda Fulani, haijalishi itachukua miaka mingi, lakini mwisho wa siku utakipata tu. Hata chakula vyenye asili ya mbegu kama maharage au mahindi, ukivitupa mahali penye ardhi yenye asili ya maji maji baada ya muda Fulani vitakuja kukuwa na kuzaa, na hivyo kukipata kile ulichokipoteza na Zaidi.
Ubarikiwe.
Mada Nyinginezo:
KUWAHUDUMIA MALAIKA PASIPO KUJUA.
KAMA UNAPENDA MAISHA, NA KUTAKA SIKU YAKO IWE NJEMA.
NI JAMBO GANI LINALOMTAMANISHA SANA BWANA TUMWOMBE BILA KUKATA TAMAA?
FUATILIA NDOTO HII, UTAJIFUZA KITU.
MWINUE YESU KRISTO KATIKA MAISHA YAKO.
JIBU: Tukianzia mistari ya juu anasema:
Yohana 3:31 “Yeye ajaye kutoka juu, huyo yu juu ya yote. Yeye aliye wa dunia, asili yake ni ya dunia, naye anena mambo ya duniani. Yeye ajaye kutoka mbinguni yu juu ya yote.
32 Yale aliyoyaona na kuyasikia ndiyo anayoyashuhudia, wala hakuna anayeukubali ushuhuda wake.
33 Yeye aliyeukubali ushuhuda wake ametia muhuri ya kwamba Mungu ni kweli.
34 Kwa kuwa yeye aliyetumwa na Mungu huyanena maneno ya Mungu; kwa sababu hamtoi Roho kwa kipimo
.35 Baba ampenda Mwana, naye amempa vyote mkononi mwake.
36 Amwaminiye Mwana yuna uzima wa milele; asiyemwamini Mwana hataona uzima, bali ghadhabu ya Mungu inamkalia”.
Kama tukichunguza hapo tunaona ni Kristo pekee ndiye anayeshuhudiwa katika biblia nzima kuwa “aliyaona na kuyasikia” mambo yote ya Mungu, Na hiyo ni kwasababu yeye alitoka huko, na asili yake ni huko, tofauti na wanadamu wengine wote, hivyo hata kile atakachokishuhudia duniani ni lazima kitakuwa ni Ukweli mtupu usiokuwa na chembe chembe yoyote ya mapungufu, Na ndio maana kila kilichotoka katika kinywa chake kilikuwa ni Neno la Mungu halisi kabisa.. Tofauti na manabii wake na watu wengine wote ambao wakati mwingine iliwapasa watafiti, tafiti wachunguze chunguze,
1Petro 1:10 “Katika habari ya wokovu huo manabii walitafuta-tafuta na kuchunguza-chunguza, ambao walitabiri habari za neema itakayowafikia ninyi.
11 Wakatafuta ni wakati upi, na wakati wa namna gani ulioonywa na Roho wa Kristo aliyekuwa ndani yao, ambaye alitangulia kuyashuhudia mateso yatakayompata Kristo, na utukufu utakaokuwako baada ya hayo.
Matendo 17:26 “Naye alifanya kila taifa la wanadamu kutoka katika mmoja, wakae juu ya uso wa nchi yote, akiisha kuwawekea nyakati alizoziamuru tangu zamani, na mipaka ya makazi yao;
27 ili wamtafute Mungu, INGAWA NI KWA KUPAPASA-PAPASA, wakamwone, ijapokuwa hawi mbali na kila mmoja wetu”.
Vile vile mitume nao, japo walifunuliwa mambo yote na Roho mtakatifu lakini bado walikuwa hawana ufahamu wote wa mambo yote,
1Wakoritho 13.9 “Kwa maana tunafahamu kwa sehemu; na tunafanya unabii kwa sehemu;
10 lakini ijapo ile iliyo kamili, iliyo kwa sehemu itabatilika…….wakati wa sasa nafahamu kwa sehemu; wakati ule nitajua sana kama mimi nami ninavyojuliwa sana”.
Umeona, aliyefahamu mambo yote ni YESU KRISTO mwenyewe,ambaye hapo mwanzo alikuwapo kwa Mungu, yeye alikuwa ashuhudiwi kwanza na Roho ndipo aseme kama vile mitume walivyofanya, bali kilichokuwa kinatoka kwenye kinywa chake ni maneno ya ROHO mwenyewe akizungumza mbele za watu ndio maana aliwaambia mahali fulani, maneno yangu ni Roho tena ni uzima.
Yohana 6.63 “Roho ndiyo itiayo uzima, mwili haufai kitu; maneno hayo niliyowaambia ni roho, tena ni uzima.”Hivyo mtu yeyote akiyasikia maneno ya Kristo, na kuyashika, ni Roho wa Mungu mwenyewe ndio anayejaa ndani yake..
Na ndio maana Yohana akamshuhudui, kuwa hamtoi Roho kwa kipimo. Leo hii ukisikiliza maneno ya watumishi wote wa Kristo, utapata kipimo cha Roho wa Mungu, kwasababu maneno yanayotoka katika vinywa vyao hajakamilika yote, lakini ukisikiliza maneno ya Kristo, utapata kiwango kamili cha Roho wake, kwasababu ni Neno lililotakasika lisilo la chembe ya uchafu, lisilo na kipimo …Na maneno ya Kristo ndio BIBLIA TAKATIFU,..ukiisioma hiyo, na kuiishi hiyo utapokea kiwango kamili cha Roho wake, bila kipimo…Kwasababu maneno yake ni ROHO.
Ubarikiwe.
Mada Nyinginezo:
JE! HIZI ROHO SABA ZA MUNGU NI ZIPI? NA JE ZINATOFAUTIANA NA ROHO MTAKATIFU?
JE, KAMA HAUNA UBATIZO SAHIHI HAUWEZI KUWA NA ROHO MTAKATIFU?
ROHO I RADHI, LAKINI MWILI NI DHAIFU.
MUUNGANO WA DINI NA MADHEHEBU YOTE, UMEKARIBIA.
JIBU: Ndio ni halali, Tunapaswa tutofautishe kati ya yale maagano ya mwilini na yale ya rohoni. Tunapookoka na kubatizwa katika ubatizo halali, hapo ni sawa na tumefungishwa ndoa na kuwa mwili mmoja na Kristo, ni hiyo ni ndoa ya kimbinguni kwasababu haitambuliki katika mwili, hata karamu yake haifanyiki huku bali kule mbinguni, vivyo hivyo nacheti chake ni lazima kiwe cha kule, na cheti chenyewe ndio ule uzima wa milele, pale tunapojua majina yameandikwa katika kitabu cha uzima.
Lakini mtu anapooa, au anapoolewa, haowi mbinguni au haolewi mbinguni bali ni hapa hapa duniani, hivyo kuwa na ushahidi au uthibitisho wa uhalali wa ndoa hiyo ni muhimu kuwepo, ni moja ya vigezo vya kuzingatiwa katika hatua za mwisho za ndoa. Na sio lazima kiwe ni cheti kabisa lakini walau waraka wa makubaliano uliothibitishwa na mashahidi kanisani (Mchungaji wako na waumini). Ikiwa tu kitendo cha kuachana katika Israeli kilihitaji “hati/cheti” (Mathayo 19:7, Kumbu 24:1) si zaidi kukubaliana?.
Na Hiyo faida yake ipo katika mwili, mojawapo ni hii unaweza kwenda mahali ugenini na mkeo, mkashindwa kuruhusiwa kuingia, au kushirikiana katika mambo Fulani, au kulala pamoja kwa kuwa tu hamna cheti cha ndoa, hususani katika nyumba za wageni. Pili hata ikitokea mmojawapo amefariki, hatua za kimirithani, yaani urithishaji mali, kama hakuna cheti inamaanisha, Serikali ya kidunia inaweza kukuzuia usiwe na haki ya kumiliki mali za mwenza wako ambazo mlizichuma pamoja. Hivyo japo katika roho cheti kinaweza kisiwe na maana yoyote, Na wala biblia haijaagiza lolote kuhusu hilo, lakini katika mwili kina umuhimu mkubwa, na pia ili kuiheshimisha ndoa yako, na kuipa thamani yake, ni vizuri ukapewa hati ya ndoa kanisani kwako.(Waebrania 13:4).
Bwana akubariki.
Mada Nyinginezo:
MADHARA YA DHAMBI YA UASHERATI.
MTI UANGUKAPO, PAPO HAPO UTALALA.
JE! MBINGUNI KUTAKUWA NA KULA NA KUNYWA?.
SWALI:Kule katika kitabu cha KUTOKA 20:5-6.Mungu alisema”NAWAPATILIZA WANA MAOVU YA BABA ZAO.. Sasa hivi Baba wa Fulani akimwiba mke wa jirani yake na kumwua..Mungu Atawapatiliza adhabu hao watoto wa baba Fulani Kwa huo wizi na uuaji wake?? Shalom.
JIBU: Ukisoma mistari yote inasema hivi
Kutoka 20:4“Usijifanyie sanamu ya kuchonga, wala mfano wa kitu cho chote kilicho juu mbinguni, wala kilicho chini duniani, wala kilicho majini chini ya dunia”.
5 Usivisujudie wala kuvitumikia; kwa kuwa mimi, Bwana, Mungu wako, ni Mungu mwenye wivu; nawapatiliza wana maovu ya baba zao, HATA KIZAZI CHA TATU NA CHA NNE CHA WANICHUKIAO,
6 nami nawarehemu maelfu elfu wanipendao, na kuzishika amri zangu.
Mwishoni mwa mstari wa 5 inasema hata kizazi cha tatu na cha nne cha “wanichukiao”. Kumbe cha hao wamchukiao, na sio cha wampendao, kama baba yako alikuwa ni mwovu anaabudu sanamu, halafu na wewe mtoto kwa kulijua hilo unafanya yale yale ambayo baba yako alikuwa anayafanya, hapo laana ya baba yako pamoja na yako mwenyewe itakupata…
Na ndivyo ilivyokuwa kwa wana wa Israeli, enzi zile za wafalme, jambo kuu lililowafanya wachukuliwe utumwani, kupelekwa Ashuru na Babeli ni kutokana na kuwa walikuwa hawampendi Mungu, Kwani baada ya kuona Baba zao na wafalme wao wanatenda maovu wanasimamisha maashera na kuabudu miungu mingine, wao badala ya kutubu wakayaiga yale yale waliyokuwa wanayafanya, hivyo Mungu alikasirika akayaketa maovu ya Baba zao wote yakawapata hao, mpaka walipotawanywa katika mataifa yote..
Lakini pia ukisoma mstari wa 6 anasema “nami nawarehemu maelfu elfu wanipendao, na kuzishika amri zangu”. Ikiwa na maana kuwa hata kama Baba zako walikuwa ni waovu vipi, Hivyo Mungu akakusudia kuulaani uzao wao wote, ikatokea wewe (mtoto) anampenda Mungu na kumcha, basi rehema zake zinakuwa juu yake, kana kwamba hujazaliwa katika kizazi chenye laana. Hapo linatimia hili neno.
Ezekieli 18: 20 “Roho itendayo dhambi, ndiyo itakayokufa; mwana hatauchukua uovu wa baba yake, wala baba hatauchukua uovu wa mwanawe, haki yake mwenye haki itakuwa juu yake, na uovu wake mwenye uovu utakuwa juu yake”.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe au piga namba hii +255 789 001312.
jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
LILE TUMAINI LILILO NDANI YETU LINAPOULIZIWA.
JE! VIUMBE VINATAZAMIAJE KWA SHAUKU KUFUNULIWA KWA MWANA WA MUNGU?