Wakati mwingine kuna mambo unasoma kwenye biblia unaishia kuogopa sana, hususani pale unapoona mtu Mungu anafanya mambo ambayo hata mwenye dhambi si rahisi ayafanye. Kwamfano embu tuwaangalie hawa watu wawili, [Daudi na Yuda]. Hawa wote tunajua walikuwa ni watiwa mafuta wa Mungu, tukianzana na Daudi, tunajua alikuwa ni shujaa sana, na katika ushujaa wake, aliweza kuchagua mashujaa wake wengine 37 waaminifu ili kumsaidia katika vita, na kuipigania Israeli.
Lakini katikati ya mashujaa hao kulikuwa na mwingine ambaye alikuwa mwaminifu sana pengine hata Zaidi ya mashujaa wengine wote, na huyo aliitwa Uria. Uaminifu wake tunausoma jinsi ulivyokuwa.. hakuwa tayari kwenda kujiburudisha nafsi yake wakati kazi ya vita haijamalizika, na wenzake wapo bado mapambanoni, haijalishi kuwa ni mfalme ndiye aliyempa ruhusu ya kuondoka, hakuwa tayari kuondoka.
2Samweli 11:8 “Daudi akamwambia Uria, Haya, shuka nyumbani kwako, ukanawe miguu yako. Basi Uria akatoka katika nyumba ya mfalme, na tunu ya vyakula ikamfuata, iliyotoka kwa mfalme.
9 Lakini Uria akalala mlangoni pa nyumba ya mfalme, pamoja na watumishi wote wa bwana wake, wala hakushuka nyumbani kwake.
10 Watu walipomwambia Daudi ya kwamba, Uria hakushuka nyumbani kwake, Daudi akamwambia Uria, Je! Hukutoka safarini? Mbona hukushuka nyumbani kwako?
11 Naye Uria akamwambia Daudi, Sanduku, na Israeli, na Yuda, wanakaa vibandani; na bwana wangu Yoabu, na watumishi wa bwana wangu, wamepiga kambi waziwazi uwandani; nami niende nyumbani kwangu, kula na kunywa, na kulala na mke wangu? Uishivyo, na kama roho yako iishivyo, mimi sitafanya jambo hili. 12 Basi Daudi akamwambia Uria, Ngoja hapa leo tena, na kesho nitakuacha kwenda zako. Basi Uria akakaa Yerusalemu siku ile, na siku ya pili yake.
13 Naye Daudi akamwalika, akala, akanywa mbele yake; naye akamlevya; hata wakati wa jioni akatoka kwenda kulala kitandani mwake pamoja na watumishi wa bwana wake, lakini hakushuka nyumbani kwake.”
Unaweza ukajiuliza, mtu kama huyu, labda ndio angependwa kipekee na Daudi, na kupewa zawadi nyingi kwa moyo wake huo wa uaminifu na Upendo, lakini kinyume chake Daudi ndio akampangia njama za kumwangamiza. Tena kumwangamiza katika huo huo uaminifu wake.. Na akafanikiwa, akamuua kwenye vita, pale alipowaambia mashujaa wake wamwache mwenyewe auawe.
Huyo ndio Daudi mtiwa mafuta wa Bwana, Lakini ni nini kilichompelekea afanye vile, hakufanya vile kwasababu alipenda, bali kwasababu ya shinikizo la dhambi lililokuwa nyuma yake. Na dhambi yenyewe ilianzia pale, alimuona mke wa Uria, akamtamani, kisha akamchukua alale naye, akadhani itaishia pale pale tu, hakujua kuwa madhara Zaidi yanaweza kuja, matokeo yake akapata mimba yule mwanamke, Na Daudi alipoona hivyo akataka kumbambikizia Uria mimba ambayo si yake , ili tu kusitiri aibu, ndio maana akampa likizo ya ghafla, ili akalale na mkewe, lakini Uria alikuwa mwaminifu hakukwenda kulala na mke wake, alibaki kambini, ndipo Daudi ikambidi abuni mbinu nyingine ya kusitiri uovu wake, ndipo akaamua kukiua kiungo chake kiteule, kisichokuwa na hatia yoyote. Hilo ndio shinikizo la dhambi.
Mwingine ni Yuda, huyu naye alianza dhambi kidogo kidogo tu, ya wizi, hakujua tamaa hiyo itampelekea kuisaliti damu isiyokuwa na hatia, akadhani ni mambo rahisi rahisi tu, akaendelea kuwa mwizi, mpaka ikafikia hatua ile dhambi iliyokuwa ndani yake ikamshinikiza, kupata hela nyingi Zaidi na njia pekee ambayo ingempelekea kuipata ni kwa kumsaliti Bwana wake, Mtakatifu ili wale wakuu wa makuhani wampe Hela.
Sasa usidhani kwamba kumsaliti Bwana wake ambaye alijua anampenda upeo, na kumweshimu ilikuwa ni jambo analolifurahia sana, hapana, bali lile shinikizo la dhambi ndio lililompelekea kuchukua maamuzi ambayo yalimletea majuto ya milele.
Yuda alimsaliti Bwana wake, alimsaliti jemedari wake, alimsaliti mwokozi wake aliyependa, kwa dhambi ndogo tu ya kupenda fedha na wizi.
Huoni leo hii watu wanawatoa ndugu zao kafara kwa waganga wa kienyeji, unadhani hawawapendi ndugu zao, wanawapenda lakini lile shinikizo la dhambi ambalo lilianza zamani kama tamaa tu ya mali ndilo lililowafikisha mahali ambapo inawagharimu wafanye hivyo, wasipofanya ndio wamekwisha.
Huoni leo hii mabinti wengi, wanatoa mimba ovyo, kama vile si kitendo cha uuaji wanachokifanya. Usidhani hawawapendi watoto wao, lakini lile shinikizo la dhambi pengine la kukwepa aibu, kukwepa kutengwa, kukwepa kufukuzwa shule, kukwepa majukumu, linawafanya watende vitendo hivyo vya kinyama kila kukicha.
Hata wewe leo hii usidhani huwezi kumuua mtu kwa kumpiga risasi, usidhani huwezi kufanya mambo ya ajabu kupindukia, usiseme hivyo kama ni mtendaji wa dhambi hizo ambazo unaziona za kawaida tu, unaweza kutenda tena na ukawa ni mnyama kuliko hata magaidi wenyewe, kama utaivumilia dhambi ndani yako, Haijalishi utajiita ni mtumishi wa Mungu.
Dhambi ni ya kuiogopa sana, usiseme yule ni mke wa mtu ngoja nikazini naye leo tu basi, hakutakuwa na shida yoyote, usijaribu kufanya hivyo ndugu, usiseme ngoja niibe kile kidogo kwenye kampuni, hakitaniletea madhara yoyote, usifanye hivyo.. Dhambi inashinikizo kubwa sana, inakupeleka mahali ambapo huwezi kuchomoka mpaka ufanye kufuru mbaya sana. Laiti Daudi au Yuda angelijua tangu mwanzo kuwa watasababisha damu zisizo na hatia kumwagika wasingedhubutu kufanya mambo kama yale.
Lolote unaloliona ni dogo maadamu ni dhambi jiepushe nalo tu, kwa usalama wa maisha yako ya rohoni.
Shalom.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255693036618 au +255789001312
jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Mafundisho mengine
Mada Nyinginezo:
Je mtu anayeua anabeba dhambi zote za yule aliyemuua?
USIINGIE MKATABA NA DHAMBI.
ROHO ANENA WAZIWAZI
Swali: Kurushwa upesi kunakozungumziwa katika Danieli 9:21 ndio kupi?
IFAHAMU HUZUNI NA FURAHA YA MALAIKA.
Shalom..Jina la Bwana wetu Yesu Kristo libarikiwe.
Neno la Mungu linasema katika…
1 Timotheo 4:1 “Basi Roho anena waziwazi ya kwamba nyakati za mwisho wengine watajitenga na imani, wakisikiliza roho zidanganyazo, na mafundisho ya mashetani”
Maana ya kunena waziwazi ni kwamba…“ananena pasipo maficho yoyote wala pasipo siri yoyote”..yapo mambo ambayo Roho Mtakatifu akiyanena yanahitaji ufunuo mpana kutoka kwake..kwamfano utaona katika kitabu cha ufunuo sehemu kadha wa kadha, anasema “yeye aliye na sikio na asikie neno hili ambalo Roho ayaambia makanisa”. Au kwa lugha rahisi ni sawa na kusema “yeye mwenye akili na aweze kuyajua haya yanayozungumzwa maana yake ni nini”..kwamaana inahitajika ufunuo kuyajua.
Kwamfano tunaweza kujifunza mfano mmoja, ambapo Roho hajanena waziwazi.
Ufunuo 2:26 “Na yeye ashindaye, na kuyatunza matendo yangu hata mwisho, nitampa mamlaka juu ya mataifa,
27 naye atawachunga kwa fimbo ya chuma, kama vyombo vya mfinyanzi vipondwavyo, kama mimi nami nilivyopokea kwa Baba yangu.
28 Nami nitampa ile nyota ya asubuhi.
29 Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo Roho ayaambia makanisa”
Hapo Roho kanena..lakini si wazi..kwasababu atakayesoma hajaambiwa nyota ya asubuhi hapo ni nini, wala hajaambiwa hao mataifa atakaowachunga ni wakina nani…maana yake mambo hayo yote yanahitaji ufunuo wa Roho kuyaelewa…hayajanenwa waziwazi..
Lakini katika hiyo 1Timotheo 4 biblia inasema Roho anena waziwazi..kwamba nyakati za mwisho wengine watajitenga na Imani, wakisikiliza roho zidanganyazo….na mafundisho ya mashetani..
Hapo anasema wakizisikiliza roho zidanganyazo…na si wakizitazama au wakiziabudu..bali wakizisikiliza..maana yake hizo roho zinazungumza na zipo nyingi.
Sasa hizo zinazungumzaje?
Roho hizi zinazungumza kwa njia kuu mbili.
1. Katika nafsi ya mtu
2. Kupitia watumishi wa shetani, ambao wamevaa mavazi ya kondoo.
1. Katika nafsi ya mtu ni pale mtu anaposikia sauti au msukumo wa kwenda kufanya jambo lililo kinyume na mapenzi ya Mungu.. Kwamfano kama mtu atasikia sauti ikimwambia akatoe mimba, au akaue, au akaibe, akaabudu sanamu au akafanye uasherat, ukavae nguo za nusu uchi, ukapake lipatick, ukavae suruali kwa mwanamke, ukaende kwa waganga, ukaachane na mke wako/mume wako wa ndoa..n.k.kama akiisikiliza hiyo sauti na kwenda kufanya mojawapo ya hayo tayari atakuwa kasikiliza roho hiyo idanganyayo.
2. Vile vile kama atamsikia mtu au mhubiri akimshawishi kufanya mojawapo ya mambo hayo hapo juu tayari, na kwenda kufanya kama alivyosikia kutoka kwa huyo mtu au mhubiri, tayari atakuwa ameisikiliza roho hiyo na imeshamdanganya, aidha kwa kujua au kwa kutokujua..kupitia huyo mhubiri.
Hivyo Roho anatuambia waziwazi kuwa nyakati za mwisho ambazo ndizo hizi watu wengi sana watakuwa wanazisikiliza hizi roho..na si wachache bali ni wengi..Hivyo ni wajibu wetu kuwa macho,na kuwa makini sana ili tusiwe miongoni mwa hao “wengi”…ndio maana ametuambia waziwazi ili tujue hali halisi, na tuweze kujilinda.
Huu ni wakati wa kuzichunguza sana roho..niliwahi kukutana na mtu akaniambia ameokoka na anaamini sana sauti yoyote inayomjia ndani yake ni ya roho mtakatifu..Nikamuuliza anatumia nini kuipima hiyo sauti.. akasema anatumia hisia tu…hivyo hawezikudanganyika.
Ndugu hata uwe mhubiri mkubwa kiasi gani, hata uwe unanena kwa lugha, hata uwe unatabiri, au unaona maono, hata uwe kila siku unatembelewa na malaika..roho za yule adui yetu shetani hazichunguzwi kwa ujuzi au utaalamu au uzoefu fulani au kwa hisia..hapana!! bali zinachunguzwa kwa Neno la Mungu tu..
Maana yake ni kwamba hata kama nimeokoka sio kila sauti inayokuja ndani yangu ni ya kuiamini, bali ni lazima ipimwe na neno la Mungu..kama inakubaliana na Neno hiyo ni sauti kutoka kwa Mungu..lakini kama inapingana na Neno, haijalishi imekuja kwa nguvu kiasi gani, au umekuja na amani kiasi gani, au imekuja na hisia nzuri kiasi gani…hiyo si ya kuifuata ni sauti kutoka kwa yule adui. Biblia inasema..
2 Wakorintho 11:14 “Wala si ajabu. Maana Shetani mwenyewe hujigeuza awe mfano wa malaika wa nuru”.
Na neno la Mungu tunalijua kwa kusoma biblia kwa bidii sana…hiyo ndiyo silaha.
Kumbuka tena usisahau neno hili… Roho anena waziwazi, kuwa nyakati za mwisho wengi watajitenga na Imani, na kusikiliza roho zidanganyazo… ni maombi yangu kuwa mimi na wewe hatutakuwa miongoni mwa hao “wengi”.
Kama hujampokea Yesu mpaka sasa, kwasababu fulani fulani, unazozijua wewe, fahamu kuwa umeshasikiliza roho hizo na zimekudanganya…Hivyo fungua leo macho yako na mgeukie Kristo uanze upya, naye atakupokea na kukusaidia kwasababu anatamani wewe uwe na uzima kuliko wewe unavyotamani.
Maran atha.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255693036618 au +255789001312
jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Mafundisho mengine
Mada Nyinginezo:
Ulishawahi kujiuliza ni kwanini Roho Mtakatifu alicheleweshwa kushuka juu ya mitume ikawachukua muda mrefu kidogo, Na hata baada ya Yesu kufufuka tunaona iliwapasa tena kungojea kwa muda wa siku 50? Ulishawahi kujiuliza ni kwanini? Sio kwamba walikuwa hawastahili kupokea Roho Mtakatifu tangu zamani, hapana lakini ndio tabia ya Roho Mtakatifu aliyojiwekea, na anafanya hivyo kwasababu zake maalumu.
Hawi mwepesi sana kushuka juu ya mtu kwa haraka kwasababu anajua akishashuka huwa hashuki kwa kipimo au nusunusu, au kuchunguza chunguza. Na ndio maana Bwana Yesu alisubiri kwanza, wanafunzi wake wakamilishwe katika madarasa yake, ili kusudi kwamba watakaposhukiwa na Roho kile kilicho ndani yao kitendeke kwa ufasaha ziadi kama kilivyokusudiwa.
Roho Mtakatifu anafananishwa na MVUA, Na kama tunavyojua mvua sikuzote ikishuka huwa haichagui hapa kuna ngano au magugu, au mboga, au bangi, au mbigili kazi yake ni kwenda kustawisha tu, hiyo ndio kazi yake. Hivyo ni wajibu wa mwenye shamba kuhakikisha kitu alichokipanda shambani kwake ni chenye manufaa, ahakikishe shamba lake amelipalilia vya kutosha, kwamba hakuna mbegu za magugu chini ya ardhi,vinginevyo itakuwa ni kwa hasara yake mwenyewe pale mvua itakaponyesha na kustawisha magugu badala ya chakula.
Na ndivyo Roho Mtakatifu alivyo, anaposhuka juu ya mtu au kanisa, huwa anakuza au kukiwezesha kile ambacho kimeshapandwa ndani yake. Na ndio maana anaitwa msaidizi, Sasa Kama ulitubu dhambi zako, ukawa unaishi maisha matakatifu, ukawa unabidii katika kumtafuta Mungu, basi Roho akija juu yako, anaikuza hiyo mbegu iliyopo ndani yako, kuwezesha kumjua Mungu zaidi na kuishi hayo maisha kwa viwango vingine vya juu sana.
Na ndio hapo atakuongezea vipawa na karama ili kuhakikisha unafikia pale ambapo umepakusudia na Mungu ufike na hata zaidi. Lakini pale atakaposhuka juu yako, na bado haujajiweka tayari kwa Mungu, kinyume chake, ni mzinzi, au unayo mambo yako ya kidunia, na bado unasema ni mkristo, atakuja kweli na akija hatakufanya uwe mtakatifu bali atakufanya uwe mwovu zaidi. Hapo ndipo wengi wetu hatujui. Tendo hili katika biblia sehemu nyingine imeitwa “nguvu ya upotevu” itokayo kwa Mungu.. Soma 2Wathesalonike 2:10-12
Utajiuliza ni wapi tena jambo hilo tena utalipata katika biblia, Embu vitafakari hivi vifungu, hususa ni hivyo vilivyo katika herufi kubwa.
Waebrania 6.4 “Kwa maana hao waliokwisha kupewa nuru, na kukionja kipawa cha mbinguni, na kufanywa washirika wa Roho Mtakatifu,
5 na kulionja neno zuri la Mungu, na nguvu za zamani zijazo,
6 wakaanguka baada ya hayo, haiwezekani kuwafanya upya tena hata wakatubu; kwa kuwa wamsulibisha Mwana wa Mungu mara ya pili kwa nafsi zao, na kumfedhehi kwa dhahiri.
7 MAANA NCHI INAYOINYWA MVUA INAYOINYESHEA MARA KWA MARA, NA KUZAA MBOGA ZENYE MANUFAA KWA HAO AMBAO KWA AJILI YAO YALIMWA, HUSHIRIKI BARAKA ZITOKAZO KWA MUNGU;
8 BALI IKITOA MIIBA NA MAGUGU HUKATALIWA NA KUWA KARIBU NA LAANA; AMBAYO MWISHO WAKE NI KUTEKETEZWA”.
Embu jiulize upo katika kanisa muda mrefu, unasema umeokoka, unasali, unafanya ushirika, unaimba kwaya n.k. lakini bado una maisha ya dhambi ya siri unayoyajua wewe.. Unatazamia nini pale Roho Mtakatifu atakaposhuka juu yako au juu ya kanisa, upaliliwe kitu gani?
Roho Mtakatifu anaposhuka ndani ya kanisa lake kulinyeshea mvua, halafu anakukuta, wewe ni gugu umepandwa ndani yake, ujue kuwa mvua hiyo itaistawisha gugu, lizidi kustawi zaidi ili siku ya kuteketezwa na kutupwa motoni likapate adhabu iliyokubwa zaidi. Ili kutimiza andiko hili;
Mathayo 13:24 “Akawatolea mfano mwingine, akisema, Ufalme wa mbinguni umefanana na mtu aliyepanda mbegu njema katika konde lake;
25 lakini watu walipolala, akaja adui yake akapanda magugu katikati ya ngano, akaenda zake.
26 Baadaye majani ya ngano yalipomea na kuzaa, yakaonekana na magugu.
27 Watumwa wa mwenye nyumba wakaenda wakamwambia, Bwana, hukupanda mbegu njema katika konde lako? Limepata wapi basi magugu?
28 Akawaambia, Adui ndiye aliyetenda hivi. Watumwa wakamwambia, Basi, wataka twende tukayakusanye?
29 Akasema, La; msije mkakusanya magugu, na kuzing’oa ngano pamoja nayo.
30 Viacheni vyote vikue hata wakati wa mavuno; na wakati wa mavuno nitawaambia wavunao, Yakusanyeni kwanza magugu, myafunge matita matita mkayachome; bali ngano ikusanyeni ghalani mwangu”.
Kumbuka kilichomfanya mfalme Sauli ashukiwe na Roho mbaya kutoka kwa Mungu, ni tabia yake ya wivu na ile ya kudharau maagizo ya Mungu, hivyo ile Roho njema ya Mungu iliposhuka juu yake na kukutana na tabia yake mbaya, ndio ikamfanya awe mbaya, kutaka kumwangamiza Daudi. Lakini kama angekuwa ni mtiifu kwa Mungu na mwenye upendo, Roho ya Mungu ingekutana na tabia hiyo njema na kumfanya kuwa mfalme Hodari zaidi na mshupavu kama alivyokuwa hapo mwanzoni. Hiyo ndio sababu kwanini biblia ilikuwa inasema “Roho mbaya kutoka kwa Mungu” ilikuwa inamjia Sauli..Hizi ndio sababu.(1Samweli 16:14-23)
Hata sasa, tunapaswa tujiangalie sana mienendo yetu katika kanisa, wapo watu baada ya kukaa kanisani ndio wamezidi kuwa wabaya zaidi, wanafanya mambo ambayo hata watu wa kidunia hawafanyi, kama ulikuwa hujui sababu ndio hii. Sasa usidhani mtu kama huyo alianza tu kuwa mbaya, hapana, bali alidharau maagizo ya Mungu, akawa anafanya mambo yasiyofaa kidogo kidogo hivyo hivyo, na mwisho wa siku akajikuta anayafanya kwa nguvu zaidi,..Hajui kuwa tayari kashapotea milele, Na biblia inasema mtu akishafikia hatua hiyo, hawezi kufanywa upya tena atubu, anasubiria kwenda tu katika ziwa la moto. Kwahiyo tujitathimini ni mbegu za aina gani zipo ndani yetu. Ili tuwe na amani pale Roho anaposhuka juu yetu, kutuwezesha zaidi.
Tukipanda mbegu njema katika utakatifu, Roho Mtakatifu atatufanya kuwa watakatifu zaidi, tukipanda katika imani,atatuongezea imani zaidi, tukipanda katika upendo vivyo hivyo, katika kulitafakari Neno lake, atatuongezea mafunuo mengi zaidi n.k. Huo ndio uzuri wa Roho Mtakatifu, ndio maana anaitwa msaidizi.
Yohana 16:13 Lakini yeye atakapokuja, huyo Roho wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote; kwa maana hatanena kwa shauri lake mwenyewe, lakini yote atakayoyasikia atayanena, na mambo yajayo atawapasha habari yake.
Hivyo katika hili eneo tunapaswa tuwe makini sana, hata Bwana Yesu alituonya hivyo. Ni heri ukafanya mizaha katika mambo ya kidunia, lakini sio ndani ya kanisa la Kristo. Kwasababu huko ndani Roho Mtakatifu yupo kuwezesha watu, kwahiyo angalie zisije zikawa ndio dhambi zako zinawezeshwa huko.
Bwana akubariki.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255693036618 au +255789001312
jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Mafundisho mengine
Mada Nyinginezo: