Zaburi 34:15 Macho ya Bwana huwaelekea wenye haki, Na masikio yake hukielekea kilio chao. 16 Uso wa Bwana ni juu ya watenda mabaya, Aliondoe kumbukumbu lao duniani.
JIBU: Andiko hili lilinukuliwa tena na mtume Petro katika 1Petro 3:12-13 linasema;
“12 Kwa kuwa macho ya Bwana huwaelekea wenye haki, Na masikio yake husikiliza maombi yao; Bali uso wa Bwana ni juu ya watenda mabaya. 13 Naye ni nani atakayewadhuru, mkiwa wenye juhudi katika mema?
Kama tunavyojua Macho kazi yake ni kutazama, lakini uso, ni kueleza taswira ya mtu/ kitu fulani.
Na kimsingi macho huona vyote, vilivyo vyema na vilivyo vibaya. Isipokuwa jicho lolote hupendelea zaidi kutazama vilivyo vyema zaidi ya vile vibaya. Ndivyo ilivyo kwa Mungu wetu pia, anaona yote, maandiko yanasema hivyo katika;
Mithali 15:3 “Macho ya Bwana yako kila mahali; Yakimchunguza mbaya na mwema”.
lakini zaidi anaelekeza macho yake zaidi kwa walio wema ili awape mema.
Na ndio maana ya hiyo sehemu ya kwanza ya andiko hilo inayosema ‘Macho ya Bwana huwaelekea wenye haki, Na masikio yake hukielekea kilio chao’ Lakini haimaanishi kuwa macho yake pia hayawaoni watenda mabaya.
Vivyo hivyo katika sehemu ya pili inayoeleza juu ya Uso wa Bwana. Kama tulivyoona Uso kazi yake ni kueleza taswira ya mtu. Kwa mfano mtu akifurahi, au akiwa na huzuni au akiwa na hasira ni rahisi kumtambua kwa kuutazama uso wake. Na Vivyo hivyo, kwa Mungu wetu ukiitambua tabia yake, basi ni sawa na umeuona uso wake.
Sasa uso wake pia upo katika pande mbili; 1) Wa Rehema, 2) na wa Hasira (Nahumu 1:2-3)
Maana yake ni kuwa ukimtafuta Bwana, na kumpenda, utaona uso wake mwema, utaona upendo wake, utaona fadhili zake, utaona ukarimu wake, huruma yake, na rehema zake sikuzote. Na ndio maana maandiko yanatuasa tupende kuutafuta Uso wa Bwana. Ili tuujue uzuri wake.
Zaburi 105:4 ‘Mtakeni Bwana na nguvu zake, Utafuteni uso wake sikuzote’.
Zaburi 143:7 “Ee Bwana, unijibu hima, roho yangu imelegea; Usinifiche uso wako, Nisifanane nao washukao shimoni’
Lakini pia kinyume chake ni kweli ukiwa mwovu, ukiwa mkaidi, ukiwa mbaya, unajiandaa kuuna uso wa Mungu wenye ghadhabu,na hasira, na mapigo na matokeo yake utakumbana na adhabu kali kutoka kwake. Ndio hapo, anasema.
‘Uso wa Bwana ni juu ya watenda mabaya, Aliondoe kumbukumbu lao duniani’.
Hivyo kwa ufupisho ni kwamba jicho la Mungu linaona wote, waovu na wema, vilevile uso wa Bwana unawaelekea wote waovu na wema. Lakini katika vifungu hivyo, na vingine baadhi, vinapozungumzia macho ya Bwana huwa vinalenga sana sana kwa wema. Na vinaposema Uso wa Bwana, huwa vinalenga sana sana kwa upande wa waovu.
Kwahiyo usichanganyikiwe, bali fahamu muktadha, wa habari hiyo katika sehemu husika. Ili ujue alimaanisha nini hapo, kwa msaada wa Roho wa Mungu. Kwasababu hutumika kotekote
Bwana akubariki.
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618
Mada Nyinginezo:
UNAVYOZIDI KUWA MWENYE HAKI, NDIVYO KUJITAMBUA KWAKO KUNAVYOPUNGUA.
ANDALIZI LA MWISHO LA UJIO WA MPINGA KRISTO.
JIFUNZE KUDUMU UWEPONI MWA MUNGU.
Biblia inaposema Kaini akatoka mbele za uso wa Bwana, Inamaana gani?
Ni kweli hakuna mtu aliyewahi kuuona uso wa Mungu Zaidi ya Bwana Yesu?
Je Paulo na Petro walishindania nini? (Wagalatia 2:11).
Karibu katika mfululizo ya masomo yahusuyo matoleo!
(Ifahamu Nguvu iliyopo katika Sadaka)
Tangu Adamu aanguke ardhi ilianza kulaaniwa; kila siku laana ilikuwa inajiongeza juu ya laana, ndio maana utaona Mungu alimwambia Adamu ardhi imelaaniwa kwaajili yake yeye na uzao wake (Mwanzo 3:17), lakini ukizidi kusoma utaona tena ardhi inalaaniwa mara ya pili kwa Kaini (Mwanzo 4:11).
Na desturi hiyo iliendelea juu ya wanadamu, (Maana yake kila kukicha ardhi ilikuwa inalaaniwa juu ya wanadamu, kutokana na maasi).
Lakini tunasoma alipozaliwa Nuhu maandiko yanamtaja kama mwana wa Faraja, atakayeikomesha laana iliyo juu ya ardhi.
Mwanzo 5:28 “Lameki akaishi miaka mia na themanini na miwili, akazaa mwana.
29 Akamwita jina lake Nuhu, AKINENA, HUYU NDIYE ATAKAYETUFARIJI KWA KAZI YETU NA KWA TAABU YA MIKONO YETU KATIKA NCHI ALIYOILAANI BWANA”
Sasa unaweza kujiuliza ni wakati gani ambao Nuhu alileta faraja katika Nchi aliyoilaani Bwana?
Tusome Mwanzo 8:20-22.
Mwanzo 8:20 Nuhu akamjengea Bwana madhabahu; akatwaa katika kila mnyama aliye safi, na katika kila ndege aliye safi, akavitoa sadaka za kuteketezwa juu ya madhabahu.
21 Bwana akasikia harufu ya kumridhisha; Bwana akasema moyoni, SITAILAANI NCHI TENA BAADA YA HAYO KWA SABABU YA WANADAMU, MAANA MAWAZO YA MOYO WA MWANADAMU NI MABAYA TANGU UJANA WAKE; WALA SITAPIGA TENA BAADA YA HAYO KILA KILICHO HAI KAMA NILIVYOFANYA.
22 Muda nchi idumupo, majira ya kupanda, na mavuno, wakati wa baridi na wakati wa hari, wakati wa kaskazi na wakati wa kusi, mchana na usiku, havitakoma”
Umeona hapo? Baada ya Nuhu kumjengea Bwana madhabahu na kumtolea Bwana sadaka nzuri na ya kumridhisha, ndipo akaikomesha ile laana yote iliyokuwa inaendelea juu ya ardhi, kukawa hakuna tena kulaaniwa kwa nchi baada ya hapo!, ndio maana mpaka leo tunaona misimu ya mvua ipo, misimu ya kiangazi cha mavuno ipo, majira ya kuvuna na kupanda bado yapo, kama isingelikuwa ile sadaka Nuhu aliyoitoa huenda leo tungekuwa dunia ingekuwa mahali pabaya.
Lakini siri ya KUIKOMESHA HIYO LAANA!, Nuhu alifahamu ni kwa NJIA YA MATOLEO TU!..Na ni kanuni gani Nuhu aliyoitumia kutoa sadaka mpaka kufikia kuvunja misingi ya laana ya ardhi?
1.Alijenga Madhabahu.
Na sisi ni lazima tujenge madhabahu kwanza, na Madhahabu ya sasa, Agano jipya si ile ya mawe bali ni MIOYO YETU, Hiyo inapaswa iwe misafi kabla ya kufikiri kumtolea BWANA sadaka. Kwasababu maandiko yanasema sadaka ya mtu mbaya ni machukizo kwa Bwana (Mithali 15:8).
2. Kutoa vilivyo safi.
Baada ya Nuhu kutoka kwenye safina alitwaa wanyama walio safi tu na kumtolea Mungu, Na sisi ni lazima tumtolee Mungu vitu vilivyo visafi, hatupaswi kumtolea Mungu vitu vilivyopatikana kwa njia haramu kama ukahaba, dhuluma, rushwa, wizi, utapeli, na njia nyingine zote zinazofanana na hizo.
Kumbukumbu 23:18 “Usilete ujira wa kahaba, wala mshahara wa mbwa, katika nyumba ya Bwana, Mungu wako, kwa ajili ya nadhiri yo yote; kwani haya ni machukizo kwa Bwana, Mungu wako, yote mawili.”
3. Kutoa katika KILA kilicho safi!
Hii ni kanuni ya mwisho na ya muhimu sana, Ni lazima kutoa katika “KILA” kilicho safi, na si katika “BAADHI ya vilivyo safi”. Nuhu hakutoa tu Ng’ombe pekee yake kama sadaka, na kuwahifadhi mbuzi kwaajili ya chakula chake na biashara yake, au hakutoa kondoo pekee yake, na kuwaacha kuku na mbuzi…bali alitoa katika vyote vilivyo safi, ikiwemo kondoo, mbuzi, ng’ombe, njiwa, kuku na vinginevyo.. kila kimoja kwa sehemu yake..Hiyo ikafanya sadaka yake kumridhisha Mungu, na hivyo kufuta laana zote zilizokuwepo juu ya nchi, ambapo mpaka leo tunakula matunda yake.
Na wewe una vitu gani vilivyo safi mbele za Mungu?, je katika vyote unavyovifanya huwa unafikiri kumtolea Mungu katika hivyo?, Je katika zawadi unazopewa ulishawahi kufikiri kumtolea Mungu sehemu ndogo katika hiyo?, au unafiki ni sehemu ya mshahara tu ndio Mungu anaitaka?!
Je katika mifugo yako yote ulishawahi kufikiri kumtolea Mungu sehemu ya hiyo? Usimtolee Mungu kuku na kuacha Mbuzi!.. Jaribu siku moja kumtolea mbuzi na kuku kwa pamoja, na uone matokeo yake, (Mungu ameruhusu tumjaribu kwa njia hiyo, Malaki 3:10).
Utaona laana zinavyoondoka juu yako!!.
Bwana akubariki.
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
Mada Nyinginezo:
Sadaka ya Moyo ipoje? (Walawi 22:21).
Chakula kilichotolewa sadaka kwa sanamu ndio kipi? (Matendo 21:25).
Kwanini Nuhu alimlaani Kaanani badala ya mtoto wake Hamu,
UTAYAFIKIAJE MANENO SAFI YA MUNGU?
Biblia inaposema Kaini akatoka mbele za uso wa Bwana, Inamaana gani?
Nakusalimu katika jina la Bwana wetu Yesu Kristo. Karibu tuyasikilize maagizo ya Mungu.
Kuna wakati Bwana alipokutana na mafarisayo alisema maneno haya;
Mathayo 23:25-26
[25]Ole wenu waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnasafisha nje ya kikombe na chano, na ndani yake vimejaa unyang’anyi na kutokuwa na kiasi.
[26]Ewe Farisayo kipofu, safisha kwanza ndani ya kikombe, ili nje yake nayo ipate kuwa safi.
Tengeneza picha ya kikombe. Kiuhalisia ili kifae Kwa matumizi ni lazima kiwe kisafi pande zote, yaani nje na ndani. Huwezi kutumia kikombe ambacho nje ni kisafi lakini ndani kina matope, vilevile huwezi tumia kikombe ambacho ndani ni kisafi lakini nje kina matope,. Bado uchafu ni ule ule..Hivyo ili kifae Kwa matumizi hakina budi kisafishwe kotekote ndani na nje.
Leo hii tunakosa shabaha kudhani, ni upande mmoja tu Mungu anautazama. Ndivyo walivyofanya mafarisayo Kwa nje walionekana wanyenyekevu, wafanya ibada, Wana staha, waalimu wazuri wa torati lakini ndani walijaa wivu, mashindani, majivuno, tamaa n.k.
Lakini vilevile wapo watu ambao Kwa ndani wanadai Wana upole, Upendo, amani, lakini Kwa nje, hawana ushuhuda wowote, Hawa ndio wale ambao wanasema Mungu anaangalia vya rohoni haangalii vya nje.
Ndugu ili utumiwe na Bwana, safisha kikombe kotekote. Rohoni na Mwilini
Sasa haya ni baadhi ya mambo ambayo unapaswa uyafanye kotekote. Tukiangazia mifano kwa Bwana Yesu.
Yesu aliishi maisha ya kumpendeza Mungu, lakini alijua kwamba kabla ya kumpendeza Mungu ni lazima niwapendeze kwanza wanadamu. Hivyo akafanya bidii kuwa na sifa njema katika jamii pia, na kwa Mungu.
Luka 2:52
[52]Naye Yesu akazidi kuendelea katika hekima na kimo, akimpendeza Mungu na wanadamu.
Umeona? Hakuwa mtu wa kusema Mimi ni Mungu tu, lakini alitafuta sifa nzuri pia Kwa wanadamu ili Mungu wake atukuzwe, hivyo aliishi vizuri na wanadamu, alikuwa mtiifu, mwaminifu, mwenye utu, mwenye adabu kwa watu. Vivyo hivyo na wewe kama mkristo kama sifa zako nje zinavuma vibaya.. hata kama ni mtu mzuri kiibada hapo ni sawa na umesafisha kikombe Kwa ndani lakini nje ni kichafu. Hivyo bado hujakamilika. Safisha pande zote, mbinguni na ulimwenguni.
Maandiko yanasema, Mpende Bwana Mungu wako Kwa moyo wako wote, na Kwa Roho yako yote na Kwa nguvu zako zote..lakini kabla hayajasema maneno hayo, Mungu alitangulia kusema kwanza mpende jirani Yako,ili Upendo wako kwake ukamilike.
1 Yohana 4:20-21
[20]Mtu akisema, Nampenda Mungu, naye anamchukia ndugu yake, ni mwongo; kwa maana asiyempenda ndugu yake ambaye amemwona, hawezi kumpenda Mungu ambaye hakumwona.
[21]Na amri hii tumepewa na yeye, ya kwamba yeye ampendaye Mungu, ampende na ndugu yake.
Kabla hujampenda Mungu mpende mwanadamu. Safisha kikombe nje na ndani.
Mungu anatutaka tuwe wasafi moyoni moyoni.(Mathayo 5:8)..Lakini usafi wa ndani unakamilishwa na ule wa nje.
Soma
2 Wakorintho 7:1
[1]Basi, wapenzi wangu, kwa kuwa tuna ahadi hizo, na tujitakase nafsi zetu na uchafu wote wa mwili na roho, huku tukitimiza utakatifu katika kumcha Mungu.
Umeona kumbe Kuna uchafu wa mwili na pia wa roho. Ule wa Roho ndio wivu, kiburi, uongo n.k. lakini ule wa mwili ndio ulevu, uvaaji mbovu, uchoraji mwili, utukanaji, mazungumzo mabaya.n.k
Ikiwa unajiita Mtakatifu halafu unatembea na vimini barabarani, Binti unatembea na suruali, na nguo za mgongo wazi, huna tofauti na yule mhudumu wa pale bar.Fahamu kuwa huo usafi wako wa roho ni kazi bure. Kijana unatembea na suruali za milegezo, unafuga Rasta na viduku, huna tofauti na yule msanii wa kidunia.halafu unasema wewe ni msafi wa moyo fahamu kuwa hapo unayo dosari mbele za Bwana.
UWE KIKOMBE SAFI.
Shalom
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
Mada Nyinginezo:
KIKOMBE CHA GHADHABU YA MUNGU KINAJAA.
UPENDO NI NINI NA JE! KUNA AINA NGAPI ZA UPENDO?
UTAYAFIKIAJE MANENO SAFI YA MUNGU?
Njia zote za mtu ni safi machoni pake mwenyewe;(Mithali 16:2)
AINA SABA (7) ZA UNAFIKI, AMBAZO UNAPASWA UJIEPUSHE NAZO.
Maziara ni nini? Je! Na Tunaruhusiwa kuyajenga kwenye makaburi yetu?
Mathayo 9:14 “Wakati ule wanafunzi wake Yohana wakamwendea, wakasema, Kwa nini sisi na Mafarisayo twafunga, BALI WANAFUNZI WAKO HAWAFUNGI?
15 Yesu akawaambia, Walioalikwa arusini wawezaje kuomboleza, muda bwana arusi akiwapo pamoja nao? Lakini siku zitakuja WATAKAPOONDOLEWA BWANA ARUSI; NDIPO WATAKAPOFUNGA”.
Wanafunzi walipokuwa na Bwana Yesu katika mwili, chochote walichokihitaji walikipata kirahisi kwasababu Neema walikuwa naye katika mwili, walipohitaji uponyaji Kristo alikuwepo kuwaponya, walipohitaji kuona ishara na miujiza kama ile ya mikate mitano kulisha elfu tano, waliiona kirahisi.
Kila walichokihitaji walikipata, kwasababu Mtenda miujiza walikuwa wanamwona dhahiri na kumshika. Lakini ulipofika wakati wa Kristo kuchukuliwa juu, mambo yalibadilika!!, ile hali ya kusubiria kufanyiwa mambo na Bwana ikapotea, ikawabidi waanze kutafuta wenyewe namna ya kufanya mambo!. Ni kama tu kifaranga cha kuku kilichoachwa na mama yake, kikawaida kinaanza kujitafutia chenyewe, kitatembea huku na kule kama mama yake kutafuta chakula.
Ndicho kilichowatokea Mitume Bwa Yesu, ulipofika wakati wanakutana na wagonjwa na yule Bwana Yesu wa kukimbiziwa wagonjwa hayupo!!!.. ndipo ufahamu wa kutafuta nguvu alizokuwa nazo Bwana Yesu ukawajia!.
Ndipo wakaanza kutafiti ni vitu gani vilivyokuwa vinampa nguvu Bwana Yesu, kufanya miujiza ile na kuishi maisha yale!, ndipo wakaanza kutafakari maisha yake na kugundua kuwa muda mwingi Bwana aliutumia KUFUNGA na KUKESHA MILIMANI KUOMBA.
Na wao ikawabidi wabadilike na kuanza kuwa WAFUNGAJI NA WAOMBAJI kama Bwana Yesu ili baadhi ya mambo yawezekanike kama yalivyowezekanika kwa Bwana, vinginevyo baadhi ya mambo yasingeenda sawa, Ndio maana utaona akina Petro walipokuwa na Bwana ni kama walikuwa wanavutwa vutwa katika suala la uombaji (Utaona kuna mahali Bwana Yesu alikuja kuwaamsha Zaidi ya mara 2 waombe lakini wakarudi kulala).
Marko 14:34 “Akawaambia, Roho yangu ina huzuni nyingi kiasi cha kufa; kaeni hapa mkeshe.
35 Akaendelea mbele kidogo, akaanguka kifudifudi, akiomba ya kuwa, ikiwezekana, saa hiyo imwepuke. 36 Akasema, Aba, Baba, yote yawezekana kwako; uniondolee kikombe hiki; walakini, si kama nitakavyo mimi, bali utakavyo wewe.
37 AKAJA AKAWAKUTA WAMELALA USINGIZI, AKAMWAMBIA PETRO, JE! SIMONI, UMELALA? Hukuweza kukesha saa moja? 14.38 Kesheni mwombe, msije mkaingia majaribuni, roho i radhi ila mwili ni dhaifu.
39 Akaenda zake tena, akaomba, akisema neno lilo hilo.
40 AKAJA TENA AKAWAKUTA WAMELALA, maana macho yao yamekuwa mazito, wala hawakujua la kumjibu.
41 Akaja mara ya tatu, akawaambia, Laleni sasa, mpumzike; yatosha, saa imekuja; tazama, Mwana wa Adamu anatiwa mikononi mwao wenye dhambi”.
Hapa tunaona akina Petro wakiwa wanavutwa vutwa katika suala la uombaji, lakini tunaona mambo yanabadilika baada ya Bwana Yesu kuondoka, walianza kufunga na kukesha katika maombi mengi,.. Kuna mahali Petro anaonekana kufunga kwa kuomba mpaka anazimia kwa njaa.
Matendo 10:9 “Hata siku ya pili, walipokuwa wakisafiri na kuukaribia mji, Petro alipanda juu darini, kwenda kuomba, yapata saa sita ya mchana;
10 AKAUMWA NA NJAA SANA, AKATAKA KULA; LAKINI WALIPOKUWA WAKIANDAA, ROHO YAKE IKAZIMIA,
11 akaona mbingu zimefunuka, na chombo kikishuka kama nguo kubwa, inatelemshwa kwa pembe zake nne hata nchi”
Hii ikifunua nini?
Kristo mpaka sasa hayupo nasi katika Mwili, hivyo na sisi pia tupo katika Nyakati za KUFUNGA na KUOMBA.
Ndugu Hizi ni nyakati za “Kufunga na kuomba”. Bwana Yesu alisema mambo mengine hayawezekaniki isipokuwa kwa kufunga na kuomba/kusali.
Mathayo 17:21 “[Lakini namna hii haitoki ila kwa kusali na kufunga]”
Je Unataka kumwona Mungu katika maisha yako?..Funga na kuomba!..je unataka kuongezeka viwango vya kumjua Mungu?..Funga na kuomba!…Je Unataka Neema iongezeke juu yako! Na mambo mengine mengi yaliyo mazuri uyaone??, basi funguo ni Mifungo na Maombi. (Na kumbuka hapa biblia inazungumzia Maombi na sio maombezi). Usifunge na kwenda kutafuta kuombewa na mtumishi!.. Bali funga na omba mwenyewe!.
Maran atha!
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
Mada Nyinginezo:
HATUA ZA ROHO MTAKATIFU KATIKA KUTUONGOZA.
Kutazama Nyakati mbaya ni kufanyaje?.
NYAKATI SABA ZA KANISA NA WAJUMBE WAKE.
Kwa utamaduni wa sasa mtu anapokufa, huwa anafukiwa chini ardhini, na juu huwekewa kiashirio Fulani cha kawaida kuonesha eneo hilo lipo kaburi. Lakini watu wengine hupenda kuyapa thamani makaburi ya watu wao, hivyo kwa juu hujengea, kichumba Fulani kinachopambwa kwa vito au mawe ya thamani , wengine wanaweka mnara Fulani n.k. Sasa vitu hivi vyote vinavyojengewa juu ndio huitwa Maziara.
Kwamfano katika picha hii, ni mfano wa Ziara ambalo lilijengwa na wenyeji wa Marekani kama kumuenzi raisi wao wa kwanza wa taifa hilo aliyeitwa George Washington.
Hata katika agano la kale, enzi za biblia, yapo makaburi yaliyokuwa ya kawaida, lakini pia yapo yaliyokuwa yamejengewa maziara. Na hayo yalikuwa hususani ya wafalme na manabii wakubwa waliotokea Israeli, ambao waliuliwa kikatili mfano wa hao ni Zekaria, Hagai na Malaki. Na waliohusika sana kutengeneza maziara haya walikuwa ni hawa waandishi na mafarisayo(Watu wa kidini). Wakidai kuwa wanawa-enzi manabii wao, lakini tunaona Yesu akiwakemea kwa dhambi ya unafki waliyokuwa wanaifanya kwa tendo hilo.
Tusome.
Mathayo 23:29 Ole wenu, waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnayajenga makaburi ya manabii, na kuyapamba maziara ya wenye haki, 30 na kusema, Kama sisi tungalikuwako zamani za baba zetu, hatungalishirikiana nao katika damu ya manabii. 31 Hivi mwajishuhudia wenyewe, ya kwamba ninyi ni wana wao waliowaua manabii. 32 Kijazeni basi kipimo cha baba zenu. 33 Enyi nyoka, wana wa majoka, mtaikimbiaje hukumu ya jehanum? 34 Kwa sababu hiyo, angalieni, mimi natuma kwenu manabii na wenye hekima na waandishi; na wengine wao ninyi mtawaua na kuwasulibisha, na wengine wao mtawapiga katika masinagogi yenu, na kuwafukuza mji kwa mji; 35 hivyo ije juu yenu damu yote ya haki iliyomwagika juu ya nchi, tangu damu ya Habili, yule mwenye haki, hata damu ya Zakaria bin Barakia, mliyemwua kati ya patakatifu na madhabahu. 36 Amin, nawaambieni, Mambo hayo yote yatakuja juu ya kizazi hiki.
Soma pia (Luka 11:47-48).
Jibu ni hapana, Bali walichokuwa wanakifanya nje, hakikuendana na kile kilichokuwa mioyoni mwao na ndio maana akawaita wanafiki. Kwasababu walikuwepo pia manabii wa Mungu na watu wenye haki wakati wao, mfano wa Yohana, pamoja na yeye mwenyewe lakini walikuwa wanataka kuwaua. Na ndivyo walivyokuja kufanya kwa Bwana, pamoja na mitume wako na watakatifu wa kanisa la kwanza kama vile wakina Stefano.
Jibu ni la, Endapo tu hatutashirikisha ibada yoyote ya wafu mahali pale. Lakini kama ni kwa kumbukumbu, au kumu-enzi marehemu wako, hakuna shida kuweka ziara (kupamba kaburi lako kwa jinsi upendavyo). Lakini fahamu tu hilo halitakuongezea jambo lolote rohoni. Wala halimfaidii kwa lolote Yule marehemu kule alipo.
Kutunza kaburi lolote, yaani kulisafisha, kulirepea, kulipandia bustani, kulilinda.. Si kosa kibiblia, kwasababu tunaona katika biblia makaburi yalitunzwa kwa bustani, soma (Yohana 20:15), pia yalilindwa, Na zaidi yalihifadhiwa yasiharibiwe. Soma
2Wafalme 23:16 Naye Yosia alipogeuka, aliyaona makaburi yale yaliyokuwako huko, juu ya mlima; akatuma watu, akaitoa ile mifupa katika yale makaburi, akaiteketeza juu ya madhabahu, akainajisi, sawasawa na lile neno la Bwana, alilolinena yule mtu wa Mungu, aliyetamka mambo hayo. 17 Kisha akasema, Ni kumbukumbu la nani, hili ninaloliona? Na watu wa mji wakamwambia, Ni kaburi la yule mtu wa Mungu, aliyetoka Yuda, akayanena mambo hayo uliyoyatenda wewe juu ya madhabahu ya Betheli. 18 Akasema, Mwacheni; mtu awaye yote asiiondoe mifupa yake. Basi wakaiacha mifupa yake, pamoja na mifupa ya yule nabii aliyetoka Samaria.
Hivyo, upendapo kutunza kaburi la mpendwa wako, aliyefariki hufanyi kosa.
Zipo ibada za wafu, ambazo ndizo zinazofanyika mara nyingi katika makaburi ya marehemu, ibadani hizo, zinahusianisha kuwaombea wafu hao, n.k. Ibada hizi ni za kipagani, na mkristo hapaswi kuzifanya ni ibada za miungu. Au wengine wanakwenda kuzungumza na kaburi wakiamini Yule mtu yupo pale makaburini anawasikia. Huo ni uchawi.
Hivyo hakuna mahusiano yoyote ya kiibada katika makaburi. Endapo imetokea unakwenda kufanya maziara (yaani kukarabati au kupamba), basi unachofanya ni kufungua kwa maombi na kufunga kwa maombi, kisha mnaendelea na kazi yenu, ili kutimiza hili andiko
Wakolosai 3:17 “Na kila mfanyalo, kwa neno au kwa tendo, fanyeni yote katika jina la Bwana Yesu, mkimshukuru Mungu Baba kwa yeye”.
Na kama mmeguswa kutafakari maneno ya Mungu mahali pale, kama mfanyapo sehemu nyingine zozote, mfano kazini, shuleni, chini ya mwembe n.k.. Basi iwe ni kwa Mungu na sio kwasababu ya makaburi. Epuka Ibada za wafu.
Shalom.
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
Mada Nyinginezo:
Pango la Makpela ni lipi, je lina umuhimu wowote kwetu?
MAKABURI YAKAFUNUKA; IKAINUKA MIILI MINGI YA WATAKATIFU WALIOLALA;
MAUTI NA KUZIMU ZIKAWATOA WAFU WALIOKUWAMO NDANI YAKE.
Wenye kubatizwa kwa ajili ya wafu ni wakina nani?
Praitorio ni nini? Na Kwanini ilikuwa ni najisi kwa wayahudi kuingia humo? (Yohana 18:28)
Je unajua kuwa roho ya mpinga-kristo imeshaanza kutenda kazi na inaendelea kutenda kazi hata sasa?
1 Yohana 4:3 “Na kila roho isiyomkiri Yesu haitokani na Mungu. Na hii ndiyo roho ya mpinga Kristo ambayo mmesikia kwamba yaja; NA SASA IMEKWISHA KUWAKO DUNIANI”.
Andalizi la mwisho la Mpinga Kristo kabla ya chapa yake kuanza kufanya kazi ni hili “MUNGU HAANGALII MWILI BALI ROHO”.
Roho ya Mpinga-kristo inawaandaa sasa watu na hiyo saikolojia, kwamba waamini Mungu haangalii mwili bali roho tu.
Na kwanini anafanya hivyo?.. ni ili iwe vyepesi kwake siku ile kuwatia watu CHAPA mwilini (Usoni na mikononi)
Kwasababu asipowaandaa na hiyo saikolojia itakuwa kwake ni ngumu sana kuwashinikiza waipokee chapa katika vipaji vya nyuso na katika mwili siku zile baada ya unyakuo wa kanisa kupita.
Kwahiyo anaanza na saikolojia ndogo tu kwamba kuvaa hereni sio kosa, kutoboa pua sio kosa, kujichora tattoo na hina sio kosa na kupaka lipstick midomoni na wanja machoni sio dhambi.. ( kwamba Mungu hawezi kumhukumu mtu kwa vitu vinavyowekwa mwilini)
Ndugu usidanganyike, je! Umewahi kujiuliza kwanini Mungu atawahukumu watu wote watakaoipokea ile chapa ya mnyama katika VIPAJI vya nyuso zao na katika MIKONO yao siku ile?..
Kama Mungu haangalii mwili kwanini chapa ya 666 itiwe katika mwili na Mungu awahukumu wale wote watakaoipokea chapa hiyo?, maana maandiko yanasema watu wote watakaoipokea chapa hiyo katika vipaji vya nyuso zao au katika mikono basi watahukumiwa katika lile ziwa la moto (Ufunuo 14:9-10).
Sasa kama tu alama ya kishetani katika kipaji cha uso au katika sehemu ya mkono, inaweza kuwa sababu ya mtu kukataliwa na Mungu milele!, vipi hizo tattoo unazochora mwilini, vipi hizo hina unazozipaka na wanja unaoupaka machoni?, vipi hizo lipstick unazopaka mdomoni na rangi unazopaka kwenye kucha?… Vipi hizo hereni unazozining’iniza masikioni?.
Kama tu leo ni ngumu kuelewa kuwa kupaka wanja ni kosa kibiblia, utashawishikaje siku ile kuamini kuwa kuandikwa alama ya 666 kwenye kipaji cha uso wako ni kosa?..nataka nikuambie kuwa siku ile utaipokea tu chapa kama kawaida. Kama tu leo kutoboa masikio na kuweka hereni na kutoboa pua na kuweka pini huoni shida, utaonaje shida siku ile utakapotobolewa katika mkono wako na chipu kuwekwa mwilini mwako?.
Tafakari sana dada!!… tafakari sana kaka!! Tafakari sana Mama, tafakari sana Baba…Usiwe mwepesi kuiga mambo yanayoendelea na kuonekana ulimwenguni, hususani yanayofanywa na watu wengi!…(Mengi ya hayo yanaongozwa na roho ya mpinga kristo)…Ni kweli unajipenda, na ni vizuri kufanya hivyo, ni kweli unapenda uonekane vizuri na maridadi mbele za watu, ni vizuri pia kufanya hivyo lakini vipi na roho yako? Je itaendelea kubaki salama?.
Shetani amewafunga wengi macho siku hizi za mwisho wasiyaelewe maandiko! Na kuwaaminisha kuwa Mungu haangalii mwili bali anaangalia roho.
Dada usidanganyike! Kwasababu udanganyifu upo leo.. na utaendelea kuwepo mpaka wakati wa chapa ya mnyama.
Tupa hereni zote, kachome mawigi, ondoa pistick, na wanja machoni.
Bwana akubariki.
Maran atha!
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
Mada Nyinginezo:
UTENDAJI KAZI MWINGINE WA ROHO MTAKATIFU USIOUFAHAMU.
JE CHANJO YA KORONA NI ALAMA YA MNYAMA?
KUSAMBAA KWA ROHO YA MPINGA-KRISTO.
NIMEAZIMIA KUWAKUSANYA MATAIFA. NIPATE KUWAMWAGIA GHADHABU YANGU
Mithali 29:21 “Amtunduiaye mtumwa wake tangu utoto, Mwisho wake atakuwa ni mwanawe”.
Kutundua ni kujali mtu kupita kiasi, au kuonyesha wema uliopitiliza.
Hivyo hapo anaposema amtunduiaye mtumwa wake tangu utotoni, mwisho wake atakuwa ni mwanawe. Anamaanisha amjalie mtumwa wake, kupita kiasi, yaani kuishi naye kama sio mtumwa kwake, (kumdekeza), na kama mfano ikiendelea hivyo kwa kipindi kirefu, mwisho wake utakuwa ni kumfanya mwanawe, yaani mrithi.
Zamani enzi za biblia, watu walikuwa aidha wananunua watumwa, au wanawazalisha majumbani kwao, ikiwa na maana kama mtu huyo alikuwa na mtumwa, kisha mtumwa Yule akazaa, sasa wale watoto wanakuwa pia ni watumwa wa Yule bwana.
Na kulikuwa na sheria kwamba kila baada ya miaka 7, mbiu ilipigwa ya kuwafanya watumwa wote huru, hivyo waliotaka kuondoka waliondoka, lakini waliotaka kuendelea, basi waliendelea kwa mkataba mwingine wa miaka saba. Na hivyo mtumwa huyo aliwajibika kutumika ipasavyo muda wote huo wa mkataba wake (Kumbukumbu 15:1-18).
Sasa hapa, biblia inaeleza tabia ya bwana ambaye moyo wake ni wa kitofauti. Bwana ambaye, anatabia ya kumjali sana mtumwa wake kuliko uhalisia, huwenda anamuhurumia, kumwona anafanya kazi nyingi, hivyo anampa kidogo tu, au anapokwenda kwenye sherehe hamwachi nyumbani anakwenda naye pia, hata akiwa nyumbani majukumu anapewa machache sana, anakaa naye mezani pamoja wanacheka n.k… Sasa katika hali kama hiyo, ikiwa mtumwa huyo, atadumu kubaki kwa bwana wake, kwa kipindi kirefu, Yule bwana, atamfanya tu kuwa kama mmojawapo wa mwanawe, maana yake siku atakapotoa urithi, na huyu lazima apewe, kwasababu ameishi kama mtoto wake kwa kipindi kirefu.
Na hii ni kweli, hata katika kipindi hichi, labda mfanyakazi kaajiriwa kwenye nyumba fulani, kisha mwenye nyumba akampenda, akawa naye kwa kipindi cha miaka mingi, mwishowe, atamfanya tu kama mwanafamilia, na hatimaye atapata kitu kama mmojawapo wa watoto wake.
Hii ni Tabia aliyokuwa nayo Mungu kwetu sisi watu wa mataifa.
Tulipokwenda kwake, hatukuwa wana wake, au warithi, bali warithi walikuwa ni wayahudi tu, lakini kwa ukarimu wake, akatutoa katika utumwa na kutufanya WANA, jambo ambalo si kawaida kwa bwana yoyote, kutenda kwa kijakazi aliyezaliwa kusikojulikana. Ndicho alichokuja kukifanya Yesu;
Yohana 15:15 Siwaiti tena watumwa; kwa maana mtumwa hajui atendalo bwana wake; lakini ninyi nimewaita rafiki; kwa kuwa yote niliyoyasikia kwa Baba yangu nimewaarifu.
Yohana 8:35 “Wala mtumwa hakai nyumbani sikuzote; mwana hukaa sikuzote. 36 Basi Mwana akiwaweka huru, mtakuwa huru kweli kweli”.
Hivyo mimi na wewe tunafanyika, WANA na WARITHI, wa Mungu kwa njia ya Bwana Yesu. Haleluya. Utukufu na heshima ni kwa Bwana wetu Yesu!! milele na milele.
Ni kukubali tu kudumu katika nyumba yake. Kama vile mtumwa Yule ambaye aliamua kudumu tangu UTOTONI. Hivyo na wewe umepewa neema, dumu katika neema, dumu katika wokovu, acha kutanga tanga huku na kule. Mungu akaghahiri mema kwako. Ulimwengu hauwezi kukupa unafuu wowote, ni kwa Kristo tu ndio utapata raha nafsini, Hakuna mateso kwa Kristo, Utumwa wake ni mwepesi sana alisema hivyo. Soma (Mathayo 11:28-30).
Ikiwa hujaokoka unasubiri nini sasa? Embu fanya uamuzi wa haraka sana umgeukie Kristo akuokoe. Hizi ni siku za mwisho, anakaribia kurudi kuwanyakua wateule wake. Kama upo tayari kutubu leo dhambi zako, basi fungua hapa kwa ajili ya mwongozo wa sala ya toba.>>> KUONGOZWA SALA YA TOBA
Bwana akubariki.
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
Mada Nyinginezo:
Nini tofauti ya Mtumwa, Mjakazi na kijakazi?
Maana ya Mithali 9:17 “Maji yaliyoibiwa ni matamu, Na mkate ulioliwa kwa siri hupendeza”
Miimo ni nini na kizingiti ni nini?
Ni kwa namna gani haki huinua taifa? (Mithali 14:34)
AKAPITA KATIKA LILE SHAMBA AMBALO YAKOBO ALIMPA YUSUFU MWANAWE
Nini maana ya Mithali 27:6 “Jeraha utiwazo na rafiki ni amini;
Karibu tujifunze biblia, Neno la Mungu wetu lililo hai (Zab.119:105)
Je unaijua nguvu ya kinywa chako? Biblia inasema kuwa MAUTI na UZIMA huwa katika uwezo wa ULIMI. Na mtu awezaye kuutumia vizuri ulimi wake atakula matunda yake.
Mithali 18:21 “Mauti na uzima huwa katika uwezo wa ulimi; Na wao waupendao watakula matunda yake”.
Sasa ULIMI una matunda mawili tu!, ambayo ni “Uzima na Mauti”. Maana yake mtu anaweza kuutumia ulimi wake ukamletea UZIMA, lakini pia anaweza kuutumia na ukamletea MAUTI.
Yule kijana aliyempelekea Daudi habari za kifo cha Sauli, kinywa chake mwenyewe kilimletea “Mauti” (2Samweli 1:16) hali kadhalika Mfalme Yehoshafati alipokuwa katika hatari ya kufa, kwa kinywa chake mwenyewe alijiokoa. (2Nyakati 18:31).
Lakini leo nataka tuangalie faida za kutumia ULIMI katika eneo la MAOMBI.
Wengi tumezoea kuomba kimoyomoyo, jambo ambalo ni zuri lakini si wakati wote linafaa!!.. kuna mazingira ni lazima utumie kinywa chako kutoa maneno dhahiri yanayosikika!..Kuna ngome zinahitaji kusikia sauti ndipo zitii!, Kuna ngome zinahitaji kuamrishwa na kukemewa ndipo zitii (Kuta za Yeriko zilihitaji kelele nyingi ili zianguke)….Hali kadhalika katika imani inahitajika sauti ya kinywa ili kuthibitisha wokovu mtu alioupata…
Warumi 10:9 “Kwa sababu, ukimkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu, utaokoka.
10 Kwa maana kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu”.
Kwa hiyo si kila wakati maombi ya ukimya yanafaa… Ni lazima ujifunze kubadili gear unapoingia katika maombi ya vita, hata motokaa haisafiri kwa gear moja tu, ikienda hivyo itakwamaa mahali Fulani.
Sasa biblia inatufundisha kuwa “Mauti na Uzima” huwa katika uwezo wa kinywa. Maana yake ni kwamba tukitumia vizuri ndimi zetu wakati wa kuomba tunauwezo wa kuvihuisha vitu vingi vilivyokufa, na pia kuviua baadhi ya vitu visivyofaa maishani mwetu.
Tunaviuaje vitu visivyofaa?.. Tunaviua kwa “kuvitamkia kifo” kwa mfano ule ule wa Bwana Yesu alivyoutamkia ule Mtini, na ukafa wakati ule ule.
Mathayo 21:18 “Hata asubuhi alipokuwa akienda mjini, aliona njaa.
19 Akaona mtini mmoja kando ya njia, akauendea, asione kitu juu yake ila majani tu; AKAUAMBIA, YASIPATIKANE MATUNDA KWAKO TANGU LEO HATA MILELE. MTINI UKANYAUKA MARA.
20 Wanafunzi walipoona, walistaajabu, wakisema, Jinsi gani mtini umenyauka mara?
21 Yesu akajibu, akawaambia, Amin, nawaambia Mkiwa na imani, msipokuwa na shaka, mtafanya si hilo la mtini tu, lakini hata mkiuambia mlima huu, Ng’oka, ukatupwe baharini, litatendeka.
22 Na yo yote mtakayoyaomba katika sala mkiamini, mtapokea”.
Mstari wa 19 unasema “..akauambia, yasipatikane matunda kwako tangu leo hata milele, mtini ukanyauka mara.” Hapo Bwana Yesu aliuua huo mtini kwa kutumia kinywa chake. (Aliutumia ulimi wake na akala matunda yake), na anatuambia tukiwa na Imani tunaweza kufanya kama hayo na hata Zaidi ya hayo.
Hivyo na sisi ni lazima tujifunze kutumia Ndimi zetu kuua baadhi ya vitu ambavyo shetani kavipanda katika maisha yetu.
Unapoamka kusali Ua kazi za giza katika siku yako, unapotembea zihukumu kazi za giza kwa kutumia kinywa chako.. kwasababu unapotamka na kuamini moyoni mwako basi fahamu kuwa ni lazima yatokee hayo uliyoyasema.
Zitamkie mauti kazi za shetani katika utumishi wako, katika familia yako, katika watoto wako, katika shughuli zako, katika vitu vyako unavyomiliki, Usiishie tu kuomba kimya kimya pasipo kutoa maneno yoyote.. Paza sauti kwasababu kuna nguvu Mungu kaiweka katika ulimi wa mwanadamu.
Wachawi na mawakala wote washetani wanajua nguvu iliyopo katika ulimi, ndio maana wanautumia kuleta madhara makubwa katika maisha ya watu.. sasa na watu waliookoka ni lazima kutumia ulimi kutangua maneno yote yaliyonenwa au yanayonenwa kinyume na maisha yetu ya kiroho na kimwili.
Vile vile ni lazima tutumie Ndimi zetu kutamka UZIMA wa vitu vilivyokufa katika maisha yetu. Nabii Ezekieli aliambiwa aitabirie mifupa mikavu ili iweze kuwa na uhai tena, na katika maono yale aliitabiria mifupa ile kwa kinywa chake na ikarudia uzima na likaamka jeshi kubwa sana (soma Ezekieli 37:1-8).
Sehemu zote Bwana Yesu alipoenda kuponya wagonjwa alitumia kinywa chake kutamka, na sisi ni lazima tutumie vinywa vyetu kutamka uzima juu ya vitu viliyokufa ndani yetu. Ikiwa ni huduma, ikiwa ni karama, ikiwa ni shughuli unayoifanya, ikiwa ni watoto, au kitu kingine chochote kilicho chema ni sharti kipate uzima kupitia kinywa chako!. Fanya hivyo daima, usiache hata siku moja hata kama unaona kwa nje ni pakavu, endelea kwasababu vita vya kiroho si vita vya kimwili, na ukiwa na bidii kufanya hivyo mwisho utakula matunda ya ulimi wako.
Mithali 18:21 “Mauti na uzima huwa katika uwezo wa ulimi; Na wao waupendao watakula matunda yake”
Maran atha!
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
Mada Nyinginezo:
KWANINI MTINI KATIKATI YA MIZABIBU?
KAMA UNAPENDA MAISHA, NA KUTAKA SIKU YAKO IWE NJEMA.
Tofuati kati ya kifo na mauti ni ipi?
Jina la Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo libarikiwe, karibu tujifunze biblia Neno la Mungu wetu lililo taa ya miguu yetu na Mwanga wa njia yetu (Zab.119:105).
Ni muhimu kujua kanuni kadhaa za kuomba ili maombi yetu yawe na majibu.
Tumewahi kujifunza kanuni kadhaa huko nyuma na leo imempendeza Bwana tujifunze kanuni nyingine.
Neno la Mungu linasema yafuatayo katika kitabu cha Yakobo 4:2-3.
Yakobo 4:2 “ Mwatamani, wala hamna kitu, mwaua na kuona wivu, wala hamwezi kupata. Mwafanya vita na kupigana, wala hamna kitu kwa kuwa hamwombi!
3 Hata mwaomba, wala hampati kwa sababu mwaomba vibaya, ili mvitumie kwa tamaa zenu”.
Kumbe sababu ya kutopata yale tunayoyaomba ni jinsi tunavyoomba!.. (kwamba tunaomba vibaya!).
Na kuomba vibaya kunakozungumziwa hapo si kukosea kupangilia maneno wakati wa kuomba, bali ni kuomba kusikompendeza Bwana, ambako ni nje na mapenzi ya Mungu, mfano wa maombi hayo ni yale mtu anaomba Bwana ampatie fedha ili awe nazo awakomeshe wanaomdharau. (Maombi ya namna hii ni maombi mabaya, na mara nyingi hayana majibu)
Hivyo unapoomba zingatia mambo yafuatayo.
1.Kuwa na Nia Njema:
Nia njema, maana yake ni kusudi jema… Kama unahitaji Bwana akupe mafanikio Fulani ya kiroho au ya kimwili, hakikisha Nia yako ni njema, kwamba utokane tu na ugumu unaoupitia, na pia upate kitu cha kuwasaidia wengine, na si kwa lengo la kuwakomesha wanaokudharau. Ukiwa na Nia ya kupata vitu ili wengine waone, maombi hayo yanaweza yasijibiwe kabisa.
2. Mwombe Mungu mahitaji na si Fedha.
Wengi wetu tunapenda kupeleka maombi ya kupata fedha kutoka kwa Mungu.. Lakini kiuhalisia hayo si maombi bora. Tunasahau kuwa tunachokihitaji sana ni mahitaji yetu kama chakula, mavazi, makazi, afya na mengineyo, ambayo hayo Mungu anaweza kukutimizia pasipo fedha.
Ukiwa na haja ya chakula, mwambie Bwana naomba chakula na yeye anajua namna ya kukupatia hicho chakula kama kwa njia ya kukupatia fedha ukanunue, au kwa kukuletea mtu atakayekupa hicho chakula, (usikimbilie moja kwa moja kumwambia Bwana akupe fedha ya chakula), kwani yeye anazo njia nyingi za kukulisha wewe, si lazima kwa kutumia fedha.
Vile vile ukitaka mavazi, makazi, biashara, afya n.k Mwambie Bwana akupe vitu hivyo, na wala usiombe fedha za kupata mavazi, au za kupata makazi, au za kufanya biashara.. wewe mwambie naomba mavazi, yeye anajua jinsi ya kukupatia kama kupitia mlango huo wa fedha au kupitia watu yeye anajua, vile vile usiombe mtaji kwa Mungu, badala yake iombe ile kazi kwasababu wakati wewe unawaza kupata mtaji kwanza kumbe pengine Mungu amekuandalia mahali utakapoanza kufanya kazi pasipo mtaji.
Ukihataji Bwana akupe kifaa cha kazi au chombo za kukurahisishia usafiri, usimwambie Bwana akupe Pesa za kununua chombo hicho, badala yake mwombe Bwana akupe hicho chombo, kwa njia anayoijua yeye.
Ukitaka kusafiri usimwombe Bwana fedha za kusafiri, wewe mwombe akusafirishe, yeye atajua njia atakayotumia kukufikisha kule unakotaka kwenda, kama atanyanyua mtu na kukusafirisha kwa gharama zake au bure, au atafungua mlango wa wewe kupata fedha hizo, ila usijifunge kwa kanuni ya fedha.
Vile vile unapoumwa usimwombe Mungu pesa za matibabu, mwombe afya, yeye anajua njia atakayotumia kukupa hiyo afya, na mambo mengine yote, epuka Kutaja “Pesa” mbele za Mungu!!.. bali taja lile hitaji!.
Kwanini maombi mengi ya kuomba Pesa hayajibiwi?
Kwasababu kuna roho nyuma ya pesa, inayowasukuma watu katika tamaa mbaya za kidunia, na kuwatoa wengi kwenye Imani, ndivyo maandiko yanavyosema.
1Timotheo 6:10 “Maana shina moja la mabaya ya kila namna ni kupenda fedha; ambayo wengine hali wakiitamani hiyo wamefarakana na Imani, na kujichoma kwa maumivu mengi”
Ndio maana utaona asilimia kubwa ya watu waliopata pesa wanakuwa na kiburi!. Lakini waliopewa na Bwana ni wanyenyekevu. Mtu aliyezawadiwa baiskeli na yule aliyenunua baiskeli kwa fedha, utaona yule aliyenunua anakuwa na kiburi Zaidi ya yule aliyepewa. Ingawa wote wana baiskeli!.
Yule aliyezawadiwa nyumba na yule aliyejenga kwa fedha yake, utaona yule aliyejenga anakuwa na kiburi Zaidi ya yule aliyezawadiwa. Na mapenzi ya Mungu ni sisi tuwe wanyenyekevu na si watu wenye viburi, hivyo kamwe hawezi kukupa kitu ambacho baadaye kitakuja kukupa kiburi.
Ni wachache sana ambao Mungu anawabariki kwa fedha, kwasababu anajua tayari ameshawatengeneza mioyo yao, hawawezi kuwa na kiburi hata wawe na kiasi gani cha fedha, na hiyo naweza kusema ni asilimia 1% lakini wengi Mungu hawapi hizo fedha wanazozihitaji kwasababu anajua tamaa tulizo nazo. Na ukiona mtu ana fedha nyingi na ana kiburi (hizo fedha hajapewa na Mungu!!).
Kama mkristo biblia inatufundisha tusiwe watu wa kupenda fedha, wala kuzisifia wala kuzitukuza, badala yake tumtukuze Mungu na tumfanye Mungu siku zote kuwa MPAJI WETU (YEHOVA YIRE)!!. Kwamba fedha ziwepo au zisiwepo bado tutaishi, bado tutavaa, bado tutakula, bado tutamiliki vitu.. Tuliookoka tuna uwezo wa kuishi bila fedha wala vitu vilivyotukuzwa na wanadamu na bado tukawa na maisha bora kuliko watu wenye mambo hayo.
Mhubiri 5:10 “Apendaye fedha hatashiba fedha, Wala apendaye wingi hatashiba maongeo. Hayo pia ni ubatili”.
Bwana atusaidie.
Maran atha!
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
Mada Nyinginezo:
JE UMEJIANDAA KUTIMIZA UNABII UPI?
Ni kwa namna gani haki huinua taifa? (Mithali 14:34)
Ni lini na wapi Ibrahimu aliioona siku ya Bwana akashangilia?.
Alani ni kifuko cha kuhifadhia upanga ambacho huvaliwa kiunoni na askari hususani wakati wa vita. Tazama picha juu.
Neno hilo utalisoma katika vifungu hivi;
1Samweli 17: 51 “Ndipo Daudi akapiga mbio, akasimama juu ya Mfilisti, akautwaa upanga wake, akaufuta alani mwake, akamwua, akamkata kichwa kwa upanga huo. Nao Wafilisti walipoona ya kuwa shujaa wao amekufa, wakakimbia”
1Nyakati 21:27 “Bwana naye akamwamuru malaika; naye akaurudisha upanga wake alani mwake tena”.
Yohana 18:11 “Basi Yesu akamwambia Petro, Rudisha upanga alani mwake; je! Kikombe alichonipa Baba, mimi nisikinywee?”
Soma pia, Ezekieli 21:3, 5
Kama tujuavyo upanga na alani, ni kama pochi na pesa, havitengani. Na upanga, kibiblia ni Neno la Mungu (Waefeso 6:17, Waebrania 4:12). Hivyo Neno la Mungu halihifadhiwi penginepo zaidi ya kwenye moyo. Pale linapohitajika kutumika hutolewa moyoni na sio penginepo. Kwahiyo chombo hichi kijulikanacho kama Alani, kinauwakilisha moyo wa Mtu.
Na kama tunavyojua upanga hutumiwa na mtu yoyote, unaweza hata kumwangamiza mwenye nao, ukitumiwa na adui. Ndivyo alivyojaribu kufanya shetani alipomjaribu Bwana na kumwambia ‘imeandikwa’, Lakini kwasababu Yesu alikuwa amejaa ‘Kweli yote’. Aliweza kumpokonya upanga huo huo na kummaliza nao.
Hivyo ni muhimu pia kujaa ‘Kweli yote’ sio Neno tu peke yake, yaani kuufahamu ukweli wa Neno la Mungu. Kwasababu ibilisi anaweza kulitumia kukuangusha ikiwa hutakamilishwa katika hilo, kwamfano anaweza kuja kukwambia kuoa wake wengi si dhambi, kwani Yakobo, alioa wake wengi, Daudi alioa wake wengi, Sulemani alioa wake wengi, na wote hawa walikubaliwa vizuri na Mungu, vivyo hivyo na wewe ukifanya hivyo utakubaliwa tu, hamna shida,. Lakini je! Hiyo ni kweli yote? Kweli yote inasema Mungu alimuumba mtu mke na mume, na hao wawili watakuwa mwili mmoja.(Mathayo 19:4-9), hakuumba Adamu mmoja, Hawa wengi. Hivyo usipojua kuligawanya vema Neno la Mungu kwa msaada wa Roho ni rahisi shetani kukupiga.
Na ndio maana maandiko yanatusihi tuivae ‘kweli’ kiunoni.
Waefeso 6:13 “Kwa sababu hiyo twaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kushindana siku ya uovu, na mkiisha kuyatimiza yote, kusimama. 14 Basi simameni, hali mmejifunga kweli viunoni, na kuvaa dirii ya haki kifuani,”
Bwana akubariki.
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
Mada Nyinginezo:
JE UPANGA UMEINGIA MOYONI MWAKO?
Silaha za Mkono wa kuume na za mkono wa kushoto ni zipi
Kwanini Bwana Yesu aliwaagiza wanafunzi wake wakanunue upanga?
Nini maana ya Dirii, Chapeo na Utayari?
Kwanini Mungu aseme “Alaaniwe azuiaye upanga wake usimwage damu” (Yeremia 48:10).