Karibu tujifunze biblia, Neno la Mungu wetu, lililo taa na mwanga wa njia zetu.
Je unajua ni kwanini tunapaswa kwenda kuihubiri injili kwa ujasiri wote, tena pasipo woga wowote?.. na tena sio kwa watu baadhi tu, bali kwa watu wote wa dunia yote na katika kila mtaa, na wilaya, na mkoa, na Taifa, na kila bara?.. Ni lazima tukijue kitu kinachotupa ujasiri wa sisi kufanya hivyo!, tusipokujua hicho tutakuwa waoga wa kuhubiri.
Sasa hebu tusome maandiko yafuatayo..
Mathayo 28:18 “Yesu akaja kwao, akasema nao, akawaambia, NIMEPEWA MAMLAKA YOTE MBINGUNI NA DUNIANI.
19 Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu;
20 na kuwafundisha kuyashika yote niliyowaamuru ninyi; na tazama, mimi nipo pamoja nanyi siku zote, hata ukamilifu wa dahari”
Hicho ni kipindi ambacho Bwana Yesu aliwatokea wanafunzi wake baada ya kufufuka kwake.. Na siku hiyo alipowatokea alikuja na agizo maalumu kwao!.. Na agizo lenyewe ni hilo la “KWENDA KUHUBIRI INJILI DUNIANI KOTE”.
Lakini agizo hilo ni gumu na zito!.. Yaani kwenda ulimwenguni kote kusema habari za Masihi, kwenda katika jamii za watu wabaya, na wakatili na wauaji, kwenda katika jamii za wasomi na watawala, na tena ulimwenguni kote?, hilo jambo si jepesi hata kidogo!.
Sasa Bwana Yesu alijua hilo jambo sio dogo wala sio lepesi, hivyo akatanguliza kwanza SABABU za kwanini awaagize kwenda duniani kote, katika mitaa yote, na miji yote na vijiji vyote na kwa watu wote wakawahubirie watu..
Na sababu yenyewe ndio tunayoisoma katika mwanzoni mwa mistari hiyo.. hebu tusome tena mstari wa 18..
Mathayo 28:18 “Yesu akaja kwao, akasema nao, akawaambia, NIMEPEWA MAMLAKA YOTE MBINGUNI NA DUNIANI.
19 Basi, enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa wanafunzi, mkiwabatiza kwa jina la Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu”
Hiyo sentensi ya kwanza kwamba “amekabidhiwa mamlaka yote mbinguni na duniani” ndio iliyowapa ujasiri Mitume wake kwenda kuhubiri injili kila mahali.
Hebu tafakari leo hii umetumwa kupeleka ujumbe kwa watu Fulani katika mkoa Fulani, halafu aliyekupa huo ujumbe ni mtu tu wakawaida..bila shaka itakuwa ni ngumu kwako kupeleka ujumbe kwa jamii ya hao watu kwasababu kwanza huenda wana nguvu kuliko wewe, hivyo ukiwapelekea vitu tofauti na itikadi zao au jamii zao ni rahisi kujitafutia madhara.. lakini hebu tengeneza picha ni Raisi ndio anakupa ujumbe uwapelekee watu Fulani, ni dhahiri kuwa mashaka yatapungua na ujasiri utaongezeka…kwanini?.. Kwasababu unajua kuwa Raisi amepewa mamlaka yote juu ya hii nchi!..
Vivyo hivyo na kwa mitume…waliposikia tu hayo maneno ya kwanza ya Bwana Yesu kwamba “amepewa mamlaka yote ya mbinguni na duniani” ikawa ni sababu tosha ya wao kuwa na ujasiri wa kwenda kila mahali, kwasababu wanajua kila mahali waendapo tayari ni milki ya Kristo, kwamba Kristo ana nguvu juu ya hilo eneo… na maana akawaambia waende kwasababu yeye atakuwa pamoja nao hata mwisho wa Dahari (yaani mwisho wa Nyakati). Na sasa tupo karibia na Mwisho wa Nyakati, Kwahiyo Kristo yupo na sisi pale tunapokwenda kuieneza injili.
Ndugu usisubiri Bwana Yesu akutokee na kukuambia nenda kahubiri!.. Tayari agizo lilishatoka miaka zaidi ya elfu 2 iliyopita… kwamba nenda kahubiri injili.
Wengi leo hii wanaogopa kwenda kuhubiri injili, kwasababu hawana vitu vya kuhubiri.. Bwana Yesu hakuwaambia wanafunzi wake wakanunue vyombo vya miziki kwanza, au spika au wapate nguo nzuri ndipo wakahubiri injili..hapana! kinyume chake aliwaambia wasibebe chochote kwasababu huko waendako watavipata vyote.
Na wewe unasubiri nini usiende kuhubiri injili? Ni wito gani unaoungoja?, ni sauti gani unayoingoja?.. na upako gani unaoungoja?…ni ujuzi gani unaousubiri?.. ukisubiri ufikie ujuzi Fulani au maarifa Fulani hutayafikia kwasababu kila siku tunakua kutoka utukufu hadi utukufu, hakuna siku tutasema tumeshajua!!.. kila siku tunajifunza..hivyo usiseme ngoja nifikia levo Fulani ndipo nikahubiri, hizo ni akili za kichanga!.. Nenda kahubiri injili..
Sasa unaanzia wapi kuhubiri injili?
Kabla ya kwenda mbali anza kuhubiri injili hapo hapo ulipo, kabla ya kufikiri kwenda nje ya mtaa anza katika mtaa wako, anza katika nyumba yako, anza katika ofisi yako, anza katika shule yako.. hakikisha hapo umemaliza kwanza na watu wameitii injili ndipo uende nje!.. na katika hatua hiyo ya awali kumbuka kuwa Kristo yupo na wewe, na kumbuka kuwa yeye amekabidhiwa mamlaka yote ya mbinguni na duniani, kwahiyo hakuna nguvu zozote wala mamlaka yoyote unayoweza kushindana na hilo agizo la Bwana Yesu.
Bwana Yesu akubariki.
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
Mada Nyinginezo:
ENZI NA MAMLAKA AMEZIFANYA KUWA MKOGO
NI KWA NAMNA GANI SHETANI ANAIZUIA INJILI?
Ni kweli Paulo alipuuzia maonyo aliyopewa ya kwenda Yerusalemu?
Ni sahihi kusema sikuitiwa kuhubiri ubatizo kama Paulo alivyosema (1Wakorintho 1:17)?.
Jibu: Tusome kuanzia mstari wa kwanza..
Matendo 23:1 “Paulo akawakazia macho watu; wa baraza, akasema, Ndugu zangu, mimi kwa dhamiri safi kabisa nimeishi mbele za Mungu hata leo hivi.
2 Kuhani Mkuu Anania akawaamuru wale waliosimama karibu naye wampige kinywa chake.
3 Ndipo Paulo akamwambia, Mungu atakupiga wewe, UKUTA ULIOPAKWA CHOKAA. Wewe umeketi kunihukumu sawasawa na sheria, nawe unaamuru nipigwe kinyume cha sheria?”
Makaburi ya zamani sio kama ya zama hizi.. Haya ya wakati yanachimbwa kuelekea chini, na mtu anawekwa kwenye jeneza na kisha kufukiwa chini, lakini makaburi ya zamani hayakuwa hivyo.. Bali yalikuwa katika mfumo wa pango, ambayo linafunguliwa na watu wanawekwa ndani ya hayo mapango, na kisha kwa nje yanarembwa kwa kupakwa chokaa au rangi nyingine ya kuvutia.
Sasa Bwana Yesu alitumia mfano wa makaburi hayo yaliyopakwa chokaa, ambayo kwa nje yanaonekana ni mazuri na kuvutia kana kwamba kuna kitu cha thamani ndani, kumbe ndani yake ni mifupa tu imejaa. Alitumia mfano huo kuwalinganisha na watu ambao kwa mwonekano wa nje wanaonekana wanafaa, wanaonekana na wacha Mungu, wanaonekana ni Watumishi wazuri, wanaonekana ni waimbaji wazuri, ni wakristo wa zuri, kumbe ndani yao ni MIFUPA TU!.. Ni wanafiki.. Bwana alisema Ole wa hao!!.
Mathayo 23;27 ‘Ole wenu, waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mmefanana na MAKABURI YALIYOPAKWA CHOKAA, nayo kwa nje yaonekana kuwa mazuri, bali ndani yamejaa MIFUPA YA WAFU, na uchafu wote.
28 Vivyo hivyo ninyi nanyi, kwa nje mwaonekana na watu kuwa wenye haki, bali ndani MMEJAA UNAFIKI NA MAASI’.
Hizo ndizo tabia walizokuwa nazo makuhani na mafarisayo wa wakati huo, walikuwa wamejaa unafiki ndani yao, na wana maasi mengi ingawa kwa nje wanasifiwa na watu wote!!.
Na katika siku hizi zetu tunazoishi, mambo haya haya yanajirudia katikati ya watu wa Mungu.. tunaonekana kwa nje ni wakristo wazuri, ni wahubiri wazuri, ni waimbaji wazuri…lakini ndani tuna unafiki uliopitiliza.. Ndani tumejaa viburi, uongo, kutokusamehe, vinyongo, visasi na kila aina ya uchafu!
Bwana Yesu atusaidie tusiwe kuta zilizopakwa chokaa, bali tuwe wakamilifu nje na ndani..
1Wathesalonike 5:22 “jitengeni na ubaya wa kila namna.
23 Mungu wa amani mwenyewe awatakase kabisa; nanyi NAFSI ZENU NA ROHO ZENU NA MIILI YENU mhifadhiwe mwe kamili, bila lawama, wakati wa kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo”.
Shalom.
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
Mada Nyinginezo:
MAKABURI YAKAFUNUKA; IKAINUKA MIILI MINGI YA WATAKATIFU WALIOLALA;
HAPAKUWA NA NAFASI YA KUPITA KWA YULE MNYAMA ALIYEKUWA CHINI YANGU.
EZEKIELI, ITABIRIE MIFUPA MIKAVU.
SWALI: Nini maana ya huu mstari?
Mithali 18:8 “Maneno ya mchongezi ni kama vitoweo; Nayo hushukia pande za ndani za tumbo”.
JIBU: Mchongezi kibiblia ni mtu anayesambaza habari mbaya za wengine, au msengenyaji, na mlalamikiaji wa wengine. Jambo ambalo Mungu kalionya tangu zamani, hata kipindi wana wa Israeli wakiwa jangwani.
Walawi 19:16a “Usiende huko na huko katikati ya watu wako, kama mchongezi;..”
Usengenyaji ni dhambi iliyostahili adhabu kali ya ukoma, kama yaliyomkuta Miriamu alivyofanya kwa Musa. Kwasababu hapo maandiko yanaeleza kuanza kwake ni kama kitoweo, yaani ni kama chakula kizuri sana kinachovutia mdomoni mwa anayekisikia.. Lakini madhara yake ni kwamba kinashuka mpaka pande za ndani za tumbo, ikiwa na maana kuwa huingia ndani kabisa ya moyo wa msikiaji, na kuzaa maumivu makali, Ni heri kingekuwa kinaishia pale mdomoni.
Ni jambo la kuwa nalo makini sana katika kanisa, kwasababu wengi wameacha imani kwasababu ya maneno, wengine wamewekeana chuki kwasababu ya kupokea taarifa zao Fulani kutoka kwa wengine. Vita vya chini chini baina ya mshirika na mshirika, upendo umepoa kwasababu tu ya uchongezi.
Pale mtu anapokufuata na kukwambia.. “nimesikia Fulani na Fulani”…”Unahabari Yule amefanya hivi au vile”…Taarifa kama hizi ngumu kukataa kuzisikia, zinakuja kama kitoweo kizuri sana, kinachovutia kukisikia, lakini hutoa chuki na hasira na uchungu ndani. Kwa mtoaji anaweza kuona kaleta habari njema, lakini kwa mpokeaji, au atakayekuja kusikia baadaye huchimbua matatizo mengi sana.
Hivyo hatupaswi kuruhusu minong’ono yoyote katikati yetu, hata kama tutaona haina madhara yoyote makubwa. Ni kudhibiti huo mnyororo haraka sana, tukiona taarifa Fulani zinaletwa kwetu zenye maudhui ya masengenyo ni kuzipinga muda huo huo, ili tuepuke madhara zaidi. Roho Mtakatifu alilionya kanisa juu ya jambo hili, hususani kwa wanawake akasema;.
Tito 2:3 “Vivyo hivyo na wazee wa kike wawe na mwenendo wa utakatifu; wasiwe wasingiziaji..”
1Timotheo 5:13 “Tena, pamoja na hayo, hujifunza kuwa wavivu, wakizunguka-zunguka nyumba kwa nyumba; wala si wavivu tu, lakini ni wachongezi na wadadisi, wakinena maneno yasiyowapasa”.
Soma 1Timotheo 3:11, 2Timotheo 3:1-3.
Kama mkristo, ni jambo la kujiepusha sana, kuulinda ulimi wako.
Shalom.
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
Mada Nyinginezo:
WAMWENDEA YESU KWA KUSAFIWA lyrics na historia
LEO WOKOVU UMEFIKA NYUMBANI HUMU
Kuwaogopa wanadamu huleta mtego,(Mithali 29:25)
Aibusu midomo atoaye jawabu la haki (Mithali 24:26)
SWALI: Mimi nimeokoka lakini nakuwa na hasira nyingi sana, nifanyaje ili niweze kuzizuia hasira zangu?
JIBU: Hasira zipo za aina mbili,
Kuna hasira zenye malengo chanya, na kuna hasira zenye malengo hasi.
Hasira zenye malengo chanya, zinakuwa na shabaha ya kujenga na sio kubomoa, upendo na sio uadui. Mfano wa Hasira hizi ni kama alizokuwa nazo Bwana Yesu..
Marko 3: 1-5
‘1 Akaingia tena katika sinagogi; na palikuwako huko mtu mwenye mkono uliopooza;
2 wakamvizia ili kuona kama atamponya siku ya sabato; wapate kumshitaki.
3 Akamwambia yule mtu mwenye mkono uliopooza, Simama katikati.
4 Akawauliza, Ni halali siku ya sabato kutenda mema, au kutenda mabaya? Kuponya roho au kuiua? Wakanyamaza.
5 Akawakazia macho pande zote kwa hasira, akiona huzuni kwa ajili ya ugumu wa mioyo yao, akamwambia yule mtu, Nyosha mkono wako. Naye akaunyosha; mkono wake ukawa mzima tena’.
Halikadhalika alizidhihirisha pale alipoingia Hekaluni na kupindua meza za wafanyabiashara (Marko 11:15-18). Hata sasa hasira kama hizi za ki-Mungu zinahitajika..Pale ambapo mzazi unamwona mtoto wako, anatukana watu, halafu hudhihirishi hasira yako, kwa kumwadhibu na kumkemea hapo humpendi. Mungu aliwakasirikia mara nyingi watoto wake (Wayahudi), na kuwapa adhabu nyingi ikiwemo kuwapeleka utumwani, na kuwaweka chini ya maadui zao, n.k. Lakini lengo lake likiwa ni kuwafanya wasipotee, sio awatese (Yeremia 29:11 )
Lakini ipo hasira ambayo haitokani na Mungu bali inazalika katika wivu, kushindwa, majivuno, uchoyo. ambayo inapelekea kuleta madhara, au visasi kwa wengine. Kwa ufupi haina zao lolote la huruma au upendo ndani yake.. Mfano wa hasira kama hizi ni ile aliyokuwa nayo Kaini kwa ndugu yake, alipoona sadaka ya mwenzake imekubaliwa yake haijakubaliwa, akakasirika na kumuua.
Ni ile aliyokuwa nayo Yule mwana mkubwa, katika habari ya mwanampotevu, baada ya kuona ndugu yake aliyepotea anafanyiwa karamu yeye hafanyiwi (Luka 15:28), Ni ile aliyokuwa nayo Yona juu ya mtango, baada kuona Mungu anawarehemu watu 120,000, hawaui (Yona 4:9-11). Ndio ile iliyomfanya Simoni na Lawi kuwaua watu wasiokuwa na hatia kwa taarifa za kubakwa dada yao. Na ndio pia aliyokuwa nayo Sauli kwa Daudi.
Hasira hii, huzaa, mauaji, vinyongo na uchungu, masengenyo visasi n.k.
Lakini pia hasira hii inaweza ikazuka tu ghafla..kufuatana na asili ya dhambi ya kibinadamu.. Kwamfano, unapodharauliwa, unapopuuziwa, unapopigwa, unapoibiwa, unapodhulumiwa, unaposemwa vibaya, ghafla tu huzuka..panapofanyika kitu kinyume na ulivyotaka, unapotelekezwa, unaposalitiwa, unaponyimwa kitu, unapoelezwa ukweli n.k. Hasira hizi huwa zinawaka zenyewe katika mazingira kama haya..
Hivyo ni lazima ujue namna ya kupambana nazo, kwasababu maandiko yanasema..
Yakobo 1:20 “kwa maana hasira ya mwanadamu haiitendi haki ya Mungu”.
Sikuzote inakinzana na mpango wa Mungu. Hivyo uonapo hasira imekujia kutokana na mojawapo ya sababu hizo, huna budi kuishinda..
Hivyo hizi ni njia zitakazokusaidia kuishindana nayo.
Kujifunza kukaa kimya. Ni tiba madhubuti ya hasira.
Yakobo 1:19 “Hayo mnajua, ndugu zangu wapenzi. Basi kila mtu na awe mwepesi wa kusikia, bali si mwepesi wa kusema; wala kukasirika;”
Hapo anasema tusiwe wepesi wa “kusema wala kukasirika” mambo mawili, Maana yake ni kuwa Pale unapoudhiwa, ni rahisi, kurudisha majibu, aidha kwa “maneno au matendo”. Kama hutarudisha jibu la kipumbavu, basi utaonyesha kwa vitendo kama vile kurudisha rusha mkono, kusonya, kuguna, kuzira, kununa, kuzomea N.k
Haya ni mambo unapaswa ujitahidi kuyashinda. Ikitokea hii hali ndani yako, kaa kimya, adui wako wa kwanza awe ni hiyo hasira yako na sio aliyekukasirisha..Na baada ya muda itaondoka.
Bwana Yesu alisema..
Luka 6:36 “Basi, iweni na huruma, kama Baba yenu alivyo na huruma.
37 Msihukumu, nanyi hamtahukumiwa; msilaumu, nanyi hamtalaumiwa; achilieni, nanyi mtaachiliwa”.
Kuna kuudhiwa kweli kwenye msingi, ambapo unakuwa na sababu zote za kuwa na hasira ya kulipiza kisasi, kwamfano umeibiwa mali zako. Lakini biblia inatushauri tusiruhusu jua lichwe, bado uchungu huo upo mioyoni mwetu.
Waefeso 4:26 “Mwe na hasira, ila msitende dhambi; jua lisichwe na uchungu wenu bado haujawatoka”;
Ikifika kesho yawaze ya siku hiyo. Yale ya jana yaache yapite.
Tunaposoma Neno maana yake tunaisoma tabia ya Kristo. Hivyo katika Neno utajifunza mambo mengi, ikiwemo uvumilivu, unyenyekevu, upendo, amani, kujitoa sadaka n.k. Ukiwa msomaji mkubwa sana utajijengea wigo wa kudhibiti hasira yako, kwamfano pale unaposoma maneno kama haya ya Bwana Yesu anayosema.
Mathayo 5:38 “Mmesikia kwamba imenenwa, Jicho kwa jicho, na jino kwa jino;
39 Lakini mimi nawaambia, Msishindane na mtu mwovu; lakini mtu akupigaye shavu la kuume, mgeuzie na la pili.
40 Na mtu atakaye kukushitaki na kuitwaa kanzu yako, mwachie na joho pia.
41 Na mtu atakayekulazimisha mwendo wa maili moja, nenda naye mbili”.
Maombi hufukuza majaribu ya ibilisi, maombi hukuwekea wigo na mipaka rohoni. Maombi hukaribisha utukufu wa Mungu nafsini mwako. Hivyo unavyojifunza kudumu sana uweponi maana yake, uso wako unafanana na ule wa Mungu, kama vile Musa alivyokaa uweponi mwa Mungu muda mrefu siku 40, uso wake uling’aa kama malaika.
Halikadhalika ukiwa ni mtu wa maombi, ibada, mifungo, utabeba tabia za Kristo ndani yako, na hivyo utaweza kudhibiti hasira zako kiwepesi sana, lakini ukiwa ni mtu wa mwilini, hutaweza kushinda matendo ya mwili kama haya ya hasira.
Wagalatia 5:19 “Basi matendo ya mwili ni dhahiri, ndiyo haya, uasherati, uchafu, ufisadi,
20 ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi,
Kuliko kutazama vile vitendo 99 viovu ulivyofanyiwa, au vilivyokuudhi.. Jijengee tabia kutazama kimoja tu chema, kisha kitafakari hicho muda wote. Matokeo yake itakuwa ni kuishinda hasira. Kwamfano mzazi wako anaweza kukuudhi, ukasema kamwe sitakaa niongee naye. Lakini unasahau alishawahi kukunyonyesha katika matiti yake. Unapaswa ulifikirie hilo limoja wakati wote, bila kujali yale mengine mengi mabaya aliyokutendea. Ukifanya hivi utakuwa ni mtu wa kutokukasirika pia mapema. Lakini tukiwa ni wa kutazama tu sikuzote makosa, hasira haitaondoka.
Kibinadamu, ni ngumu sana kuona mapungufu yaliyopo ndani yako, lakini ni rahisi kuona yale yaliyo kwa wengine, Hivyo tukijifunza kupambana na hali zetu wenyewe, itatujengea unyenyekevu. Kwasababu zao mojawapo la hasira ni majivuno, kuona kwamba kila unachowaza wewe ndio bora kuliko kile.
Wafilipi 2:3 “Msitende neno lo lote kwa kushindana wala kwa majivuno; bali kwa unyenyekevu, kila mtu na amhesabu mwenziwe kuwa bora kuliko nafsi yake.
4 Kila mtu asiangalie mambo yake mwenyewe, bali kila mtu aangalie mambo ya wengine”.
Bwana Yesu alipokuwa anaudhiwa msalaba, aliwaona kama ni watu wasiojua wayatendayo, laiti wangejua wasingefanya vile. Kuna kuudhiwa, lakini anayekuudhi huwenda kasema kwa akili zake tu, lakini hakujua kinaweza kuleta madhara kwa mwingine,. Hivyo ni wajibu wako wewe ulipokeaye, kuwa na fikra hizo kama za Bwana, hutakuwa mtu wa kukasirika kiwepesi uonapo mambo hayajaenda kama utakavyo.
Hivyo kwa kuzingatia kanuni hizo basi utaweza kuishinda hali ya hasira kiwepesi. Bwana akubariki.
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
Mada Nyinginezo:
SHINA LA UCHUNGU, LISICHIPUKE NDANI YETU.
BWANA SI MWEPESI WA HASIRA, LAKINI BWANA NI MWINGI WA HASIRA.
NENO LA MUNGU KATIKA UTIMILIFU WOTE.
Jibu: Ili tuelewe vizuri tofauti ya haya maneno mawili “kipawa na karama” hebu tuutafakari mfano ufuatao;
Watu wawili wamepewa zawadi ya magari ya kutembelea, tena yanayofanana, kila mmoja la kwake.. Ila wa kwanza akalitumia lile gari kwa faida yake yeye, yaani kumrahisishia usafiri, na kwa matumize yake binafsi…..na wa pili akalichukua lile gari alilopewa na kwenda kulifanya kuwa gari la kuwasaidia wagonjwa mahospitalini (ambulance) tena bure…
Sasa kibiblia Magari waliyopewa hawa watu wawili ndiyo yanayofananishwa na VIPAWA vya Mungu, lakini huyo wa pili aliyelifanya gari lake kuwa gari la huduma (msaada kwa wengine), gari lake hilo ndilo linalofananishwa na KARAMA, kwasababu alilitoa kwaajili ya kuwasaidia wengine na si kwa faida yake yeye… Yeye alikuwa radhi atembee kwa miguu, lakini si wagonjwa wasifie nyumbani kwa kukosa usafiri wa haraka kufika katika vituo vya huduma..
Kwahiyo kwa hitimisho ni kwamba Kipawa ni zawadi ya kipekee kwa Mtu anayopewa na Mungu , lakini karama imeenda mbali zaidi;ni zawadi ya kipekee kwa Mtu kutoka kwa Mungu yenye lengo la kuwasaidia wengine (kuwanufaisha wengine).
Kwamaana hata asili ya neno lenyewe karama ni “kukirimu” na kukirimu maana yake ni kusaidia..na mtu anayekirimu ndio anaitwa Mkarimu.
Na leo hii kuna watu wengi wenye vipawa makanisani lakini hawana karama!… Wengi leo wana vipawa vya kuimba lakini hawana karama ya kuimba…
Wana vipawa vya kunena kwa lugha lakini hawana karama ya kunena, wana vipawa vya kutabiri lakini hawana karama za kutabiri..
kwasababu gani?…Ni kwasababu vile vipawa wanavitumia kwa faida zao wenyewe na si kwa faida ya mwili wa Kristo…wanavitumia kwaajili ya umaarufu wao na kwa matumbo yao, na si kwaajili ya kuujenga mwili wa Kristo.
1 Wakorintho 14:12 ”Vivyo hivyo na ninyi, kwa kuwa mnatamani sana kuwa watu wenye karama za roho, takeni kwamba mzidi sana kuwa nazo ili kulijenga kanisa”.
Hapo anasema “ili kulijenga kanisa”, na si kwaajili yetu…
Jitazame!..Je kipawa ulichonacho ni kwa kukunufaisha wewe au wengine?..
Je kipawa ulichonacho cha kuimba, kufundisha au kuhubiri au kuimba au unabii.. je kinafanya kazi ya kuujenga mwili wa Kristo au kujenga umaarufu wako na kujaza tumbo lako?..na kujiongezea utukufu?.
Kama kipawa chako kinakunufaisha wewe zaidi ya wengine, kama hakilitukuzi jina la Yesu, bali kinakutukuza wewe zaidi….basi tambua ya kuwa bado hauna Karama yoyote!…haijalishi unafanya miujiza kiasi gani, haijalishi unajua kuimba kiasi gani au unasifiwa na watu wote duniani..bado huna karama ya Roho.
Kifanye kipawa chako kuwa Karama!!.
Na madhara ya kutokuwa na karama yoyote maana yake hutakuwepo “karamuni” siku ile!!…Kwasababu watakaoalikwa katika karamu ya Mwanakondoo ni wale waliokuwa na karama na walizitumia vizuri kwa manufaa ya mwili wa Kristo…Kwasababu hata mzizi wa neno hilo karamu ni “karama”.
Je unataka karama za Rohoni basi Kifanye kipawa chako kuwa baraka kwa wengine..
1 Wakorintho 12:4 “Basi pana tofauti za karama; bali Roho ni yeye yule.
5 Tena pana tofauti za huduma, na Bwana ni yeye yule.
6 Kisha pana tofauti za kutenda kazi, bali Mungu ni yeye yule azitendaye kazi zote katika wote.
7 Lakini kila mmoja hupewa ufunuo wa Roho KWA KUFAIDIANA”.
Nataka tuutazame huo mstari wa mwisho unaosema “KWA KUFAIDIANA”.
Hapo mwisho anasema “kwa kufaidiana”
Siku zote kuwa mtu mwenye Nia ya kuujenga mwili wa Kristo, kuwa na nia ya kuwasaidia wengine pasipo kutegemea faida wala malipo!..na Kipawa chako Bwana atakigeuza kuwa KARAMA.
Bwana akubariki.
Maran atha!
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
Mada Nyinginezo:
Je! Ni kweli ubatizo wa maji hatuuhitaji tena?
Karama ya pili inayozungumziwa katika 2Wakorintho 1:15 ndio ipi?
Wakati ni “kipindi cha Muda” kwa kusudi Fulani, Kwamfano ukipanga kesho saa 7 mchana uende sokoni kununua bidhaa.. sasa huo muda wa “Saa 7 mchana” ndio unaoitwa “wakati wa kwenda kununua bidhaa”
Lakini “Majira” ni kipindi cha Muda ambacho ni cha “Msimu” Kwamfano Msimu wa mvua za masika hayo ni “majira ya masika”..msimu wa matunda ya maembe “hayo ni majira ya maembe”.. Msimu wa baridi, unaitwa “Majira ya baridi”.. Msimu wa joto huo unaitwa “majira ya joto”.
Mwanzo 8:22 “Muda nchi idumupo, MAJIRA YA KUPANDA, na mavuno, wakati wa baridi na wakati wa hari, wakati wa kaskazi na wakati wa kusi, mchana na usiku, havitakoma”
Sulemani alizidi kuliweka hili vizuri kitabu cha Mhubiri..
Mhubiri 3:1 “Kwa kila jambo kuna MAJIRA YAKE, Na WAKATI kwa kila kusudi chini ya mbingu.
2 Wakati wa kuzaliwa, na wakati wa kufa; Wakati wa kupanda, na wakati wa kung’oa yaliyopandwa;
3 Wakati wa kuua, na wakati wa kupoza; Wakati wa kubomoa, na wakati wa kujenga;
4 Wakati wa kulia, na wakati wa kucheka; Wakati wa kuomboleza, na wakati wa kucheza”
Unaweza kusoma zaidi juu ya Majira na Nyakati katika Mwanzo 7:21, Zaburi 1:3, Walawi 15:25, na Ayubu 39:1.
Lakini pia yapo majira na nyakati katika makusudi ya Mungu. Na kusudi kuu ambalo ni muhimu kulijua majira yake ya kurudi kwa BWANA YESU MARA YA PILI!.. Hatuwezi kujua “Wakati” lakini “majira” ya kurudi kwake, tunaweza kuyajua… Ni kama vile hatuwezi kujua siku au wakati mvua itanyesha, lakini tunajua msimu, kuwa tukishaufikia huo msimu basi tunajua siku yoyote mvua itaanza kunyesha.
Vile vile Bwana Yesu hakutoa wakati wa kurudi kwake, lakini alitoa “MAJIRA” Kwamba tuyafikiapo hayo majira basi tutajua kuwa WAKATI wowote atatokea mawinguni.
Marko 13:32 “Walakini habari ya siku ile na saa ile hakuna aijuaye, hata malaika walio mbinguni, wala Mwana, ila Baba.
33 Angalieni, kesheni, [ombeni], kwa kuwa hamjui WAKATI ule utakapokuwapo”
Sasa Majira ya kurudi kwake ni yapi, ambayo tukiyatazama tutajua kuwa yupo mlangoni?.
Si mengine zaidi ya yale tunayoyasoma katika Mathayo 24, Luka 21 na Marko 13... kwamba kutatokea “Tauni” mahali na mahali, kutasikika tetesi za vita mahali na mahali, kutatokea na magonjwa mfano wa Tauni mahali na mahali, vile vile kutatokea na manabii wengi wa uongo ambao watawadanganya wengi na upendo wa wengi utapoa na maasi yataongezeka.
Hivyo tukishaona hizo dalili basi tunajua kuwa tayari tumeingia katika MAJIRA YA KURUDI KWAKE…na kwamba wakati wowote atatokea mawinguni, na hivyo tunapaswa tuchukue tahadhari… Na majira yenyewe ndio haya tuliyopo mimi na wewe..
Ndugu yangu Yesu anarudi wakati wowote!!, na yeye mwenyewe alituonya tuwe macho!, tukeshe katika roho kila siku, ili siku ile isije ikatujia ghafla..
Lakini tukifumba macho yetu na kukataa kuyatazama haya majira na kuchukua tahadhari.. basi tutaangukia katika like kundi la wanafiki Bwana Yesu alilolitaja katika Luka 12:54-56 na siku ile itatujia ghafla na hatutapona.
Luka 12:54 “Akawaambia makutano pia, Kila mwonapo wingu likizuka pande za magharibi mara husema, Mvua inakuja; ikawa hivyo.
55 Na kila ivumapo kaskazi, husema, Kutakuwa na joto; na ndivyo ilivyo.
56 Enyi wanafiki, mwajua kuutambua uso wa nchi na mbingu; imekuwaje, BASI, KUWA HAMJUI KUTAMBUA MAJIRA HAYA?”
Bwana akubariki.
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
Mada Nyinginezo:
WAKATI ULIOKUBALIKA NALIKUSIKIA
Mtu wa kwanza kufa alikuwa nani?
KUNA NGUVU YA ZIADA KATIKA KULING’ANG’ANIA KUSUDI LA MUNGU.
Swali: Hawa wadudu, tunaowasoma katika Yoeli 2:25 (Nzige,Parare, madumadu na tunutu) ni wadudu gani na wanabeba ujumbe gani kiroho?
Tusome,
Yoeli 2:25 “Nami nitawarudishia hiyo miaka iliyoliwa na NZIGE, NA PARARE, NA MADUMADU, NA TUNUTU, jeshi langu kubwa nililotuma kati yenu”.
Hizi ni jamii za wadudu waharibifu wanaokula mazao hususani ya nafaka!.(Tazama picha juu)
1. NZIGE.
Hii ni jamii ya Panzi, ambayo ndio jamii kubwa kimaumbile kuliko jamii zote za panzi, Nzige wanasifa ya kutembea kimakundi na wanahama kutoka ukanda mmoja kwenda mwingine, na wanapotua mahali wanaharibu mazao ndani ya muda mfupi sana. Sifa ya nzige ni kwamba hawana kiongozi kama walivyo wadudu wengine kama Nyuki au Mchwa. (Soma Mithali 30:27).
Mfano wa hao Nzige ni wale Wamisri walioletewa na Mungu, ambapo walitua na kula kila mmea uliopo juu ya uso wa nchi yote ya Misri kasome (Kutoka 10:12-15), Na pia jamii ya mfano wa Nzige ni wale waliotua katika sehemu ya ukanda wa Afrika mashariki, wajulikanao kama Nzige wa Jangwani.
Lakini Nzige wanatabia ya kula Matawi ya Nafaka na kubakisha mapengo mapengo na kisha kuondoka.
2. PARARE.
Parare ni jamii nyingine ya Panzi, ambayo yenyewe inakula sehemu zile Nzige (walizobakisha/walizosaza). Parare kimaumbile ni wadogo kuliko Nzige, na kimwonekano wanayo miiba katika Miguu.. Parare si waharibifu kama Nzige, ingawa kwa nafaka ambazo tayari zimeshaharibika basi wenyewe wanaongezea uharibifu kwa kula vile vilivyosalia.
3. MADUMADU.
Madumadu ni jamii ya Panzi wadogo, wale (wanaokaa katika Nyasi)..Hii ndio jamii ya panzi wadogo kuliko wote, na sifa yao kubwa ni kula sehemu za majani zilizo ndogo sana, ambazo Nzige wala Parare hawawezi kula.
4. TUNUTU.
Tunutu ni vimelea vidogo kabisa vya wadudu, ambavyo vipo kama minyoo. Wadudu wengi warukao kabla ya kufikia hatua ya kukomaa huwa wanapitia hii hatua, ambapo wanakuwa kama viminyoo vidogo ambayo huwa vinakula mabua au sehemu ya majani ambayo Nzige, Parare, au Madumadu hawawezi kula. (Tazama picha chini)
Sasa tukirudi katika hiyo Yoeli 2 kwanini Bwana awataje wadudu hao?
Ili tuelewe vizuri hebu tusome tena kuanzia mstari wa 1.
Yoeli 1:1 “Neno la Bwana lililomjia Yoeli, mwana wa Pethueli.
2 Sikieni haya, enyi wazee; Sikilizeni, enyi wenyeji wote wa nchi. Je! Mambo haya yamekuwako katika siku zenu, Au katika siku za baba zenu?
3 Waarifuni watoto wenu habari yake, Watoto wenu wakawaambie watoto wao, Na watoto wao wakakiambie kizazi kingine.
4 YALIYOSAZWA NA TUNUTU YAMELIWA NA NZIGE; NA YALIYOSAZWA NA NZIGE YAMELIWA NA PARARE; NA YALIYOSAZWA NA PARARE YAMELIWA NA MADUMADU.
5 Levukeni, enyi walevi, mkalie; Pigeni yowe, ninyi nyote mnywao divai; Kwa sababu ya divai mpya; Maana umekatiliwa mbali na vinywa vyenu”
Umeona hapo?.. Bwana anamwonesha Yoeli hali ya kimwili ya wana wa Israeli jinsi alivyowapiga kwa Hawa wadudu Nzige, Parare, Madumadu, na Tunutu kutokana na Makosa yao. (Ambapo janga hili lilitokea dhahiri kabisa katika Israeli kwa miaka kadhaa, wakaishiwa chakula mpaka sadaka za unga zikakoma kutolewa katika nyumba ya Mungu kutokana na upungufu wa chakula).
Sasa wadudu hawakuishia kuwa wa kimwili tu, bali waliendelea kuwa hadi wa kiroho.. Maana yake ni kwamba Bwana kawaletea Nzige katika roho, Parare katika roho, Madumadu katika roho, na Tunutu katika roho, na kuyaharibu maisha yao. Na hiyo ikasababisha maisha yao kupukutika hata vile vichache walivyobakiwa navyo pia vikapukutika kama vile madumadu wanavyokula hata vile vidogo kabisa visivyoonekana.
Maana yake ni kwamba Mungu aliyaharibu maisha yao hata hawakubakiwa na kitu.. aliwaletea mikosi, na maafa na hasara, na wakaishiwa kabisa..kwasababu walimwacha!.
Hiyo ikifunua kuwa Na sisi tukimwacha Mungu, basi atalituma jeshi hili kuyaharibu maisha yetu, Utajikuta unafanya kazi kweli unapata pesa nyingi au faida nyingi, lakini itakapoishia hutajua, utajikuta tu hujasalia na chochote, utajikuta mara hili limezuka mara lile.. Ukiona hali kama hiyo basi jua kuwa ni Mungu kalituma jeshi hilo la Nzige, parare, madumadu na tunutu katika roho kula kila kitu ulicho nacho, na hata kukufanya usibakiwe na chochote.
Hagai 1:5 “Basi sasa, Bwana wa majeshi asema hivi, Zitafakarini njia zenu.
6 Mmepanda mbegu nyingi mkavuna kidogo; mnakula lakini hamshibi; mnakunywa lakini hamkujazwa na vinywaji; mnajivika nguo lakini hapana aonaye moto; na yeye apataye mshahara apata mshahara ili kuutia katika mfuko uliotoboka-toboka.
7 Bwana wa majeshi asema hivi, Zitafakarini njia zenu”.
Hivyo kama hujaokoka!..Fahamu kuwa maisha yako ya kimwili na kiroho kila siku yatazidi kuharibika, lakini kama leo hii ukiamua kumgeukia Mwokozi Yesu, kwa kutubu na kumaanisha kugeuka na kuacha dhambi kwa matendo, basi Bwana Yesu mwenyewe atakupa kipawa cha Roho wake mtakatifu na zaidi ya yote, atairejesha ile miaka yote ambayo imeliwa na Parare na Nzige, na Madumadu sawasawa na Neno lake katika Yoeli 2:25
Yoeli 2:22 “Msiogope, enyi wanyama wa kondeni; maana malisho ya jangwani yanatoa miche, na huo mti unazaa matunda yake, mtini na mzabibu inatoa nguvu zake.
23 Furahini, basi, enyi wana wa Sayuni, mkamfurahie Bwana, Mungu wenu; kwa kuwa yeye huwapa ninyi mvua ya masika, kwa kipimo cha haki, naye huwanyeshea mvua, mvua ya masika, na mvua ya vuli, kama kwanza.
24 Na sakafu za kupepetea zitajaa ngano, na mashinikizo yatafurika kwa divai na mafuta.
25 Nami nitawarudishia hiyo miaka iliyoliwa na NZIGE, NA PARARE, NA MADUMADU, NA TUNUTU, jeshi langu kubwa nililotuma kati yenu.
26 Nanyi mtakula chakula tele na kushiba, na kulihimidi jina la Bwana, Mungu wenu, aliyewatendea mambo ya ajabu; na watu wangu hawatatahayari kamwe”.
Bwana akubariki.
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
Mada Nyinginezo:
kwanini Yakobo amefananishwa na mdudu?(Isa 42:14)
Nondo ni nini kama tunavyosoma katika biblia?
Kula uzao wa tumbo lako maana yake nini? (Kumbukumbu 28:53)
Silaha moja shetani anayoitumia kuharibu maisha ya kiroho ya watu wengi, hususani vijana ni MAKUNDI!..
Na mtu mkamilifu ni Yule anayeweza kuchagua aina ya watu wa kutembea naye. Biblia inatufundisha kuwapenda watu wote, lakini si kuambatana na watu wote.
2Wakorintho 6:14 “Msifungiwe nira pamoja na wasioamini, kwa jinsi isivyo sawasawa; kwa maana pana urafiki gani KATI YA HAKI NA UASI? Tena pana shirika gani kati ya nuru na giza?”
Umeona?..maana yake ni kwamba kama unaambatana na mtu ambaye si wa aina yako, basi unajiharibu mwenyewe!, Baada tu ya kumkiri Yesu, jambo lingine la muhimu linalopasa kufuata ni KUCHAGUA AINA YA WATU, utakaoanza kuwa nao karibu, kuanzia huo wakati na kuendelea.
Wengi wanalikwepa hili na mwisho wa siku wanajikuta wameurudia ulimwengu tena kwa kasi kubwa.. Ndugu ukishaokoka yale makundi ya walevi uliyokuwa unashinda nayo, ni sharti uyaache!, ukishaokoka zile saluni ulizokuwa unaenda ambazo kutwa kuchwa ni kuzungumzia mambo ya watu wengine, unaziacha.. Ukishaokoka wale watu uliokuwa unakula nao rushwa, au unaiba nao unawaacha!
Sasa unawaachaje?
Awali ya yote unapaswa uwaambie na uikiri imani yako mbele yao, na endapo wakikusikia na wao wakakubali kubadilika na kuwa kama wewe basi utakuwa umewapata, lakini kama hawataki kubadilika na zaidi sana njia zao ni zile zile, basi hapo UNAPASWA UWAACHE!!, Kwa usalama wa roho yako, anza kutafuta marafiki wengine wa imani moja na wewe, hao panga ratiba mara chache chache kwenda kuwatembelea na utakapowatembelea habari utakazowapelekea ni za injili kuanzia mwanzo wako hadi mwisho wako.
Na kamwe usijaribu kuwaza kuwa unaweza kuwa shujaa na kwamba hawataweza kukurudisha nyuma endapo utashikamana nao..Ni kweli katika siku za mwanzo unaweza kujiona wewe ni mshindi, lakini nataka nikuambie kwa kadiri siku zitakavyozidi kwenda tabia yako njema kidogo kidogo itaanza kuathirika, na baada ya kipindi fulani, utajioni umepoa kabisa na kufanana na hao, au kuishia kuwa mkristo vuguvugu tu!.
Ukitaka ukristo wako uimarike siku baada ya siku, watafute wakristo wa kweli ungana nao!..na iache kampani mbaya!.. binti ukitaka udumu katika kuvaa vizuri na kwa heshima, na katika usafi watafute mabinti wenzako wa imani kama yako hiyo, dumu nao hao!.. utautunza utakatifu wako kwa viwango vya juu.. lakini ukitaka kuanza na moto na kuishia baridi, basi endelea na makundi yale yale uliyonayo baada ya kuokoka. (Maisha yako ya wokovu hayatafika mbali).
Vile vile ukitaka kudumu katika eneo la Maombi, yaani uzidi kuwa mwombaji, na mtu wa ibadani na mtu wa kumpenda Mungu, sharti uwatafute watu wa namna yako!.. ambao ni wacha Mungu tena wanaopenda maombi, lakini kama hutawatafuta hao na ukasema mimi ninaweza kuendelea kuwa mwombaji hata nikiwa na makundi yangu yale yale, nataka nikuambie ndugu yangu, unapoteza muda.. mwisho wako utakuwa mbaya sana, na hautajua ni saangapi umepoa kiroho au umeanguka kabisa.
Sasa tunazidi kulithibitisha vipi hili kimaandiko?
Tusome,
2Timotheo 2:22 “Lakini zikimbie tamaa za ujanani; ukafuate haki, na imani, na upendo, na amani, PAMOJA NA WALE WAMWITAO BWANA KWA MOYO SAFI”.
Hapo anasema tuzikimbie tamaa za ujanani, tukatafute “haki, imani, upendo na amani.” Lakini sasa tunatafuta hii haki, imani, upendo na amani pamoja na watu gani???..je! pamoja na walevi?, au pamoja na wazinzi?, au pamoja na watu wenye mizaa? Au pamoja na wahuni?..jibu ni la! Bali pamoja na WALE WAMWITAO BWANA KWA MOYO SAFI!!... Na wanaomwita Bwana kwa moyo safi si wengine zaidi ya wale wakristo waliosimama kikweli kweli, ambao Bwana kawapanda kila mahali.
Ukidhani kuwa unaweza kulirekebisha hilo andiko na kwamba wewe unaweza kwenda kutafuta Imani pamoja na walevi, unapoteza muda!, ukidhani unaweza kuitafuta amani na kuipata pamoja na wazinzi, au wahuni, au wauaji, au watu wa masengenyo basi nataka nikuambia kuwa unapoteza muda wako mwingi..Hata mwanafunzi hawezi kupata maarifa yoyote ya darasani endapo akikaa na wanafunzi wasiopenda shule, lakini akikaa na wenzake wapendao shule basi atapata faida anayoitafuta.
Vile vile na wewe leo hii, punguza makundi ya watu wa kidunia, na ongeza makundi ya watu wamwitao Bwana kwa moyo safi.
Maran atha!
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
Mada Nyinginezo:
NI LIPI KATI YA MAKUNDI HAYA, WEWE UPO?
EPUKA KUUNDA MATARAJIO YAKO, KWENYE AHADI ZA MUNGU.
Bwana Yesu atukuzwe daima. Karibu tena tuyasogelee maneno matukufu ya Mungu wetu Yehova;
Maandiko yanasema hivi;
Waefeso 2:1-2
[1]Nanyi mlikuwa wafu kwa sababu ya makosa na dhambi zenu;
[2]ambazo mliziendea zamani KWA KUIFUATA KAWAIDA YA ULIMWENGU HUU, na kwa kumfuata mfalme wa uwezo wa anga, roho yule atendaye kazi sasa katika wana wa kuasi;
Kumbe hii dunia ina “kawaida yake”..yaani kwa ufupi ina desturi yake ambayo imeshajizoesha tangu enzi na enzi, tangu Adamu alipoasi hata sasa, kuendana nayo.
Kwamfano leo ukienda nchi nyingi za magharibi au Asia kama vile Japan na Nepal, utakuta wanaume na wanawake sehemu za umma wanashea vyoo . Tofauti na huku kwetu, jambo hilo halikubaliwi kabisa na ni ajabu sana ukikutwa mtu unatumia choo cha jinsia tofauti.
Hivyo huku kwetu ni jambo lisilo na heshima lakini kwao ni “la kawaida”..ndio desturi yao.
Mataifa mengine kama Jamaika kuvuta bangi, ni haki kisheria lakini kwetu sisi, ni kosa..kwao ni “kawaida” kwetu sisi ni kosa la jinai..
Vivyo hivyo na hii dunia ina kawaida yake ambayo inakinzana na kanuni za ufalme wa mbinguni, Na sisi kama wakristo hatupaswi kuiiga, hata kidogo…japokuwa tutaonekana ni watu wa ajabu sana, kama mtume Petro alivyosema katika;
1 Petro 4:3-5
[3]Maana wakati wa maisha yetu uliopita watosha kwa kutenda mapenzi ya Mataifa; kuenenda katika ufisadi, na tamaa, na ulevi, na karamu za ulafi, na vileo, na ibada ya sanamu isiyo halali;
[4]MAMBO AMBAYO WAO HUONA KUWA NI AJABU YA NINYI KUTOKWENDA MBIO PAMOJA NAO katika ufisadi ule ule usio na kiasi, wakiwatukana.
[5]Nao watatoa hesabu kwake yeye aliye tayari kuwahukumu walio hai na waliokufa.
Mwanamke mmoja alinifuata na kuniambia mwanaume kama huna mojawapo ya starehe hizi yaani; 1) Ushabiki wa mpira, 2) wanawake, 3) pombe.. Wewe sio mwanaume kamili, una mapungufu. Nikasema ni kweli kwasababu kawaida ya ulimwengu huu, inalazimisha watu wawe na tabia hizo.
Binti unaambiwa usipokuwa na boyfriend, usipotumia kidogo mkorogo, usipovaa visuruali na visketi vifupi vifupi utaitwa mama/mbibi.. Wala usishangae kwasababu kawaida ya ulimwengu huu ni lazima utaonekana hivyo.
Lakini sisi kama wapitaji, makao yetu yaliyo mbinguni wala sio hapa duniani, hatuna ruhusu ya kuifuata, haijalishi itaonekana ni njema mbele ya dunia nzima..Sisi tunaifuata ‘kawaida ya mbinguni’..ambayo inatufundisha kuishi maisha ya utakatifu na usafi, kama Mungu mwenyewe na malaika zake walivyo watakatifu.
Hatuna desturi ya kuzini kabla ya ndoa, hatuna desturi ya kutembea na vimini, na mavazi ya utupu barabarani, hatuna ruhusa ya kuzifurahia anasa za ulimwengu huu, miziki, disco, kamari, pombe.
Warumi 12:2
[2]WALA MSIIFUATISHE NAMNA YA DUNIA HII; bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate kujua hakika mapenzi ya Mungu yaliyo mema, ya kumpendeza, na ukamilifu.
Hivyo ndugu uliyeokoka, kamwe usitake kumpendeza mtu, ukafaraka na Mungu. Mambo mengi ya ulimwengu huu yamefaraka na Mungu..Huo ndio ukweli, Ukiupenda ulimwengu ukasema unampenda na Mungu pia hapo unajidanganya.
1 Yohana 2:15-17
[15]Msiipende dunia, wala mambo yaliyomo katika dunia. Mtu akiipenda dunia, kumpenda Baba hakumo ndani yake.
[16]Maana kila kilichomo duniani, yaani, tamaa ya mwili, na tamaa ya macho, na kiburi cha uzima, havitokani na Baba, bali vyatokana na dunia.
[17]Na dunia inapita, pamoja na tamaa zake, bali yeye afanyaye mapenzi ya Mungu adumu hata milele.
Chagua leo ni kawaida ipi, unasimama nayo..Je! ile ya mbinguni au ya duniani hii. Kamwe usijaribu kuwa hapo katikati, yaani vuguvugu..una hatari kubwa sana ya kutapikwa..kumchanganya Mungu na udunia, ni hatari kubwa sana.
Bwana akubariki
Shalom.
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
Mada Nyinginezo:
Biblia inamaanisha nini iliposema “wakidhania kuwa ulevi wakati wa mchana ni anasa;?
ZIFAHAMU KAZI TATU ZA ROHO MTAKATIFU KATIKA ULIMWENGU.
Kutazama Nyakati mbaya ni kufanyaje?.
Vitabu vya Deuterokanoni ni vya kiMungu?
Biblia inamaana gani iliposema “Dhambi ilipozidi, Neema ilizidi kuwa nyingi Zaidi”.
Swali: Katika 1Timotheo 2:8 tunaona Mtume Paulo akiwataja wanaume kuwa wanaposalisha wanyanyue mikono iliyotakata, sasa hii mikono iliyotakata ndio mikono ya namna gani?
Jibu: Tusome,
1Timotheo 2:8 “Basi, nataka wanaume wasalishe kila mahali, huku wakiinua mikono iliyotakata pasipo hasira wala majadiliano”
Mikono iliyotakata ni mikono isiyo na “Dosari”..Sasa ili tuelewe mikono isiyo na Dosari ni mikono ya namna gani, hebu tuangalie mikono yenye Dosari ni ipi. Tusome Isaya 1:15-17.
Isaya 1:15 “Nanyi mkunjuapo mikono yenu, nitaficha macho yangu nisiwaone; naam, mwombapo maombi mengi, sitasikia; mikono yenu imejaa damu.
16 Jiosheni, jitakaseni; ondoeni uovu wa matendo yenu usiwe mbele za macho yangu; acheni kutenda mabaya;
17 jifunzeni kutenda mema; takeni hukumu na haki; wasaidieni walioonewa; mpatieni yatima haki yake; mteteeni mjane”.
Umeona Mikono yenye dosari ni ipi?.. Ni ile inayomwaga damu, inayoonea wanyonge, inayokula rushwa, mikono inayoabudu sanamu…kwaufupi mwenye dhambi yoyote Yule mikono yake ni michafu, na ina dosari mbele za Mungu.
Kwahiyo tukirudi kwenye biblia hapo maandiko yanaposema kuwa “..wanaume wasalishe kila mahali, huku wakiinua mikono iliyotakata..” imemaanisha kuwa wawapo katika ibada, au kanisani wakiabudu au kuomba, au kumtolea Mungu wahakikishe mikono yao haina hila..sio watu wa kumwaga damu, sio watu wa kula rushwa, sio watu wa kuonea watu n.k Soma pia Zaburi 58:1. Isaya 37:1 na Isaya 59:3, utaona jambo hilo hilo.
Hivyo huo ni ujumbe kwetu wote, kwamba tuitakase mikono yetu.. sio tunakwenda kumfanyia Mungu ibada au kumtolea matoleo na huku mikono yetu ni michafu..Bwana hatazitakabari sadaka zetu kama alivyozikataa zile za Kaini, vile vile tunaponyosha mikono yetu ambayo ina visasi, au ina vinyongo, au ina rushwa, na kumwabudu Mungu kwayo, kibiblia ni machukizo mbele zake.
Yakobo 4:8 “Mkaribieni Mungu, naye atawakaribia ninyi. ITAKASENI MIKONO YENU, enyi wenye dhambi, na kuisafisha mioyo yenu, enyi wenye nia mbili”.
Je umempokea Yesu katika maisha yako?.. Fahamu kuwa Yesu ndiye Njia, Kweli na Uzima.. wala hakuna mtu atakamwona Mungu, pasipo kupitia kwake yeye. Hivyo tubu leo kwa kumaanisha kuziacha dhambi zako na tafuta ubatizo sahihi ambao ni wa maji mengi (Yohana 2:23) na kwa jina la Bwana Yesu Kristo (Matendo 2:38), na Roho Mtakatifu atakuongoza na kukutia katika kweli yote sawasawa na ahadi yake (Yohana 16:13).
Marana atha!
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
Mada Nyinginezo:
Biblia inapotumia neno “Bila kazi ya mikono”, ina maana gani?
UTAKAPOKUWA MZEE, UTAINYOSHA MIKONO YAKO. NA MWINGINE ATAKUFUNGA
USIZISHIRIKI DHAMBI ZA WATU WENGINE.