SWALI: Kwanini biblia sehemu moja inasema mtu aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi, na sehemu nyingine inasema tukisema hatuna dhambi tunajidanganya wenyewe?. Je! Ni lipi hapo lipo sahihi kati ya hayo mawili?.
JIBU: Tukisoma 1Yohana 3:9 inasema..
“Kila mtu aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi, kwa sababu uzao wake wakaa ndani yake; wala hawezi kutenda dhambi kwa sababu amezaliwa kutokana na Mungu”.
Tukisoma pia 1Yohana 1:8-10 inasema..
“Tukisema kwamba hatuna dhambi, twajidanganya wenyewe, wala kweli haimo mwetu.
9 Tukiziungama dhambi zetu, Yeye ni mwaminifu na wa haki hata atuondolee dhambi zetu, na kutusafisha na udhalimu wote.
10 Tukisema kwamba hatukutenda dhambi, twamfanya Yeye kuwa mwongo wala neno lake halimo mwetu”.
Hivyo ukisoma kwa juu juu mistari hiyo utaona kama inajichanganya yenyewe lakini ukweli ni kwamba haijichanganyi na yote miwili ipo sawa, isipokuwa tunapaswa tuelewe Mtume Yohana alikuwa anaizungumzia hiyo mistari katika Nyanja ipi?, kwamfano kama ukiutazama vizuri huo mstari wa pili unaosema,“Tukisema kwamba hatuna dhambi, twajidanganya wenyewe, wala kweli haimo mwetu.,” Utagundua kuwa Mtume Yohana alikuwa analenga katika eneo la mtu kujiona kuwa mkamilifu asilimia mia kama Mungu mwenyewe, suala ambalo halipo, hakuna mwanadamu ambaye ni mkamilifu kwa asilimia zote, anayesema hana chembe ya dhambi hata kidogo ndani yake, vinginevyo basi neema itakuwa ni bure…..yapo makosa madogo madogo ambayo mtu anayatenda pasipo hata yeye kujua kama ameyafanya sasa haya ndio yanayotufanya tusijigambe kuwa hatuna dhambi hata kidogo.
Na tukiwa na ufahamu huo kichwani mwetu basi, tutajinyenyekeza mbele zake, na kuungama makosa yetu kila siku kwa yale ambayo tunamkosea Mungu pasipo kujua na kwa yale tunayoyajua.
Lakini sasa tukirudi katika ule mstari wa kwanza unaosema.. “Kila mtu aliyezaliwa na Mungu hatendi dhambi, kwa sababu uzao wake wakaa ndani yake; wala hawezi kutenda dhambi kwa sababu amezaliwa kutokana na Mungu”.
Ni kwamba hakuna mtu yeyote anayesema amezaliwa mara ya pili kwa akili zake na kwa ufahamu wake akaenda kutenda dhambi…Hicho kitu hakiwezekani kabisa, kutokuwa wakamilifu asilimia 100 kama Mungu hakumaanishi kuwa ndio tufanye dhambi kwa makusudi, wanaoweza kufanya hivyo ni watu ambao hawajazaliwa mara ya pili, wao ndio wanaweza kutamani na muda huo huo wakaenda kuzini au kufanya mustarbation, au kutazama pornography, wanaweza wakakasirika na muda huo huo wakaleta madhara na wakati mwingine hata kuua, wanaweza wakatamani mali ya mwingine na muda huo huo wakaiba, wanaweza kuudhiwa na muda huo huo wakaporomosha matusi, au kulipiza kisasi..
Lakini kwa mtu aliyezaliwa mara ya pili jambo hilo haliwezekaniki kabisa, ni kwasababu gani?. Ni kwasababu biblia inasema,uzao wake wakaa ndani yake, (yaani Uzao wa Mungu) na kama uzao wake wakaa ndani yake, basi mtu huyo ataonyesha tabia za yule aliyemzaa, ataonyesha tabia za YESU ndani yake..Kwamfano haiwezekani, mtoto akazaliwa na mtu halafu siku hiyo hiyo akaanza kula majani kama ng’ombe,tutajiuliza ni nini kimetokea,.. lakini tukimwona ndama aliyezaliwa leo anakula majani hatushangai kwasababu uzao wa ng’ombe upo ndani yake..Vivyo hivyo na sisi tuliozaliwa mara ya pili, hatuwezi sisi wenyewe kutenda dhambi kwa makusudi halafu tukasema tumezaliwa na Mungu, huo ni uongo…
Ukiona mtu anakwenda kuzini halafu anasema nimepitiwa huyo bado hajazaliwa mara ya pili, ukiona mtu anafanya mustarbation halafu anasema ameokoka huyo bado hajazaliwa mara ya pili, ukiona anakwenda disko bado hajazaliwa mara ya pili..ukiona mtu ni mlevi, au mvutaji sigara au mvaaji vimini, mzinzi, mtukanaji, na bado anasema amezaliwa mara ya pili fahamu kuwa huyo bado yupo ulimwenguni. Uzao wa Mungu haupo ndani yake. Hivyo anahitaji kutubu na kuzaliwa mara ya pili.
Ubarikiwe.jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Mada Nyinginezo:
DHAMBI YA MAUTI
DHAMBI ISIYO NA MSAMAHA.
IELEWE SAUTI YA MUNGU.
Katika Yakobo 1:13 Biblia inasema Mungu hamjaribu mtu, lakini tukirudi kwenye kitabu cha Mwanzo 22:1 tunaona Mungu alimjaribu Ibrahimu. Hapo naomba mwanga zaidi.
Tumaini ni moja ya nguzo tatu kuu katika Ukristo, Ya kwanza ikiwa ni UPENDO, Ya pili ni IMANI na ya tatu ni Tumaini. (1Wakorintho 13:13). Sasa hivi viwili vya mwisho vinatabia ya kwenda sambamba, kwani biblia inatumbia Imani ni kuwa na uhakika wa mambo YATARAJIWAYO, ni bayana ya mambo yasiyoonekana…(Waebrania 11:1)
Lakini kibiblia tumaini ni tarajio, au tazamio Fulani ambalo tayari unao uhakika nalo. Tofauti na tafsiri za kawaida kwamba tumaini ni tarajio la jambo ambalo pengine unaweza ukawa hata huna uhakika nalo, kwamfano, mtu anayeishi na virusi vya ukimwi, ipo kauli inayosema, watu wa namna hiyo huwa wanaishi kwa matumaini…Wakiwa na maana kuwa wanatumainia siku moja dawa itatokea, na kwamba isipotekea ndio basi tena…kwasababu wapo katika tarajio lisilo na uhakika.
Lakini katika ukristo ni kinyume chake, hatusemi tunatumainia tukifa tutakwenda mbinguni, kana kwamba hatuna uhakika huo kuwa tutakwenda mbinguni au la, hapana…Au hatusemi tunatumai Bwana Yesu atakuja hapana bali tunaamini kuwa atakuja, uhakika huo tunao kabisaa na hiyo ndio inayoitwa Imani…sasa katika kuamini huko ndipo tumaini halisi linazaliwa hapo ndipo tunaweza kusema tunatumai moja ya hizi siku tutamwona Bwana Yesu akitokea mawinguni…Unaona hapo tunaamini kuwa ni lazima aje, isipokuwa tunatazamia atakuja hivi karibuni, na kama asipokuja leo wala kesho, basi ni sawa lakini mwisho wa siku ni lazima aje tu…
Kila mkristo ni lazima awe na kiwango kikubwa cha Tumaini ndani yake, katika safari hii ngumu na ya majaribu mengi hapa duniani ni lazima TUMAINI liumbike ndani yetu kwamba siku si nyingi Bwana wetu atatuokoa…Na ndio maana tunaimba..’’Ni salama rohoni mwangu, Bwana Himiza siku ya kuja,’’ ..tunatumai siku moja hayo yote yatakwisha, tunapopitia misiba ya ndugu zetu tunatumai siku moja tutawaona tena utukufuni uso kwa uso, na hivyo hiyo inatupa nguvu ya kuendelea mbele tusikate tamaa, tunapopitia mateso, na njaa na kuchukiwa na kutengwa, na kudharauliwa tunajua ni kwa muda tu tunatumai siku moja tutafutwa machozi na BWANA na hayo yote hatutayaona tena…Hilo ndilo tumaini hasaa linalotoka katika uhakika Fulani…ambao bado hatujaufikia maadamu tupo hapa duniani.
Bila tumaini, katika safari hii hatuwezi kufika mbali kama vile tu, bila Imani na Upendo, hakuna chochote tunachoweza kufanya.Kwasababu tumaini linavutwa na subira na uvumilivu.
Warumi 5:1 Basi tukiisha kuhesabiwa haki itokayo katika imani, na mwe na amani kwa Mungu, kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo,
2 ambaye kwa yeye tumepata kwa njia ya imani kuifikia neema hii ambayo mnasimama ndani yake; na kufurahi katika tumaini la utukufu wa Mungu.
3 Wala si hivyo tu, ila na mfurahi katika dhiki pia; mkijua ya kuwa dhiki, kazi yake ni kuleta saburi;
4 na kazi ya saburi ni uthabiti wa moyo; na kazi ya uthabiti wa moyo ni tumaini;
5 na tumaini halitahayarishi; kwa maana pendo la Mungu limekwisha kumiminwa katika mioyo yetu na Roho Mtakatifu tuliyepewa sisi.
Wagalatia 5:5 Maana sisi kwa Roho tunalitazamia tumaini la haki kwa njia ya imani.
Wafilipi 3:20 Kwa maana sisi, wenyeji wetu uko mbinguni; kutoka huko tena TUNAMTAZAMIA Mwokozi, Bwana Yesu Kristo;
21 atakayeubadili mwili wetu wa unyonge, upate kufanana na mwili wake wa utukufu, kwa uweza ule ambao kwa huo aweza hata kuvitiisha vitu vyote viwe chini yake.
2Petro 3:13 Lakini, kama ilivyo ahadi yake, MNATAZAMIA mbingu mpya na nchi mpya, ambayo haki yakaa ndani yake. 14 Kwa hiyo, wapenzi, kwa kuwa mnatazamia mambo hayo, fanyeni bidii ili mwonekane katika amani kuwa hamna mawaa wala aibu mbele yake.
Hivyo kwa ufupi tumaini ni matarajio au matazamio ya ahadi tulizoahidiwa, Lakini Imani ni uhakika wa matarajio hayo. Au tunaweza kusema uhakika wa tumaini letu.
Ubarikiwe sana. jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Mada Nyinginezo:
UPENDO NI NINI NA JE! KUNA AINA NGAPI ZA UPENDO?
PENGINE MUNGU ALISHASEMA NAWE KWA NJIA HII.
UMEPATANISHWA NA MAADUI ZAKO?
Biblia inamaanisha nini kusema Yeye aliye na sikio, na asikie?
Kutahiriwa kibiblia ni kitendo cha Sehemu ya nyama ya mbele ya uume wa mwanamume kukatwa. Mtoto yeyote wa kiume anapozaliwa anakuwa na sehemu ya nyama iliyozidi katika uume wake. Sehemu hiyo ya nyama ndiyo inayoitwa GOVI na ndiyo iliyokuwa inakatwa.
Katika Biblia Mungu alimpa Ibrahimu maagizo ya kufanya Tohara yake (Yaani kuiondoa hiyo sehemu ya nyama iliyozidi katika kila mtoto wa kiume) kuanzia yeye binafsi na wazao wake pamoja na wote waliokuwepo katika malango yake. Na Tohara hiyo Mungu aliiruhusu ifanyike kama Ishara ya Agano Mungu aliloingia nao.
Mwanzo 17:9 “Mungu akamwambia Ibrahimu, Nawe ulishike agano langu, wewe na uzao wako kwa vizazi vyao baada
yako.10 Hili ndilo agano langu utakalolishika, kati ya mimi na wewe, na uzao wako baada yako, Kila mwanamume wa kwenu atatahiriwa.
11 Mtatahiriwa nyama ya magovi yenu, na jambo hilo litakuwa ishara ya agano kati ya mimi na ninyi.
12 Mtoto wa siku nane atatahiriwa kwenu, kila mwanamume katika vizazi vyenu, mzaliwa nyumbani, na mnunuliwa kwa fedha, kila mgeni asiyekuwa wa uzao wako.
13 Mzaliwa nyumbani mwako, na mnunuliwa kwa fedha yako, lazima atahiriwe; na agano langu litakuwa katika mwili wenu, kuwa agano la milele.
14 Na mwanamume mwenye govi asiyetahiriwa nyama ya govi lake, mtu yule atatengwa na watu wake; amelivunja agano langu”
Hivyo Tohara ilikuwa ni Ishara ya Agano la Mungu katika miili ya wana wa Israeli.
Jibu ni kwamba sehemu ya uzazi, ni sehemu ya siri na ya muhimu sana kwa mtu.Ni sehemu ambayo inafunikwa kwa mavazi mengi. Jambo hilo linafunua kitu fulani katika Tohara ya pili ambayo tutakwenda kuiona hapo mbele.
Lakini sasa tukirudi katika Agano jipya la Yesu Kristo. Tohara ya mwilini sio tena ISHARA YA AGANO Mungu aliloingia nasi. Ipo tohara nyingine ya Rohoni ambayo ndiyo ya Muhimu kuliko zote. Ambayo ndio ISHARA Pekee ya Agano la Mungu. Na hiyo si nyingine zaidi ya TOHARA YA MOYONI.
Warumi 2:29 “bali yeye ni Myahudi aliye Myahudi kwa ndani, na tohara ni ya moyo, katika roho, si katika andiko; ambaye sifa yake haitoki kwa wanadamu bali kwa Mungu”.
Tunapoisikia Injili na kuitii, Roho Mtakatifu anaondoa kile kipande cha nyama kilichozidi katika mioyo yetu. Kiburi kilichozidi ni govi, Uongo ambao haukupaswa uwepo ndani yako ni govi, hivyo Roho Mtakatifu anaukata. Kadhalika uasherati, ulevi, wizi na mambo mengine yote mabaya. Yanaondolewa na Roho Mtakatifu mwenyewe.
Wakolosai 2:10 “Na ninyi mmetimilika katika yeye aliye kichwa cha enzi yote na mamlaka.
11 Katika yeye mmetahiriwa kwa tohara isiyofanyika kwa mikono, kwa kuuvua mwili wa nyama, kwa tohara ya Kristo”
Matendo 7:7.51 Enyi wenye shingo gumu, msiotahiriwa mioyo wala masikio, siku zote mnampinga Roho Mtakatifu; kama baba zenu walivyofanya, na ninyi ni vivyo hivyo.
Hivyo kutahiriwa kibiblia ni kuondolewa sehemu isiyostahili kuwepo katika moyo wa mtu. Na kama vile jinsi ilivyofanyika kwenye viungo vya uzazi vilivyojificha. Kadhalika inafanyika pia katika MOYO ambao ndio umeficha mambo yote ya siri za mtu.
Je! Umetahiriwa moyoni mwako?..ulevi umeondolewa? rushwa imeondolewa?.. uasherati umeondolewa?. Kumbuka Tohara ya kwanza ilikuwa inawahusu wanaume tu..Lakini hii ya pili inahusu jinsia zote!.
Kama wewe bado unatoa mimba bado hujatahiriwa. Kama wewe mwanamke unasengenya na kuishi na mwanamume ambaye hamjafunga ndoa hapo bado unahitaji tohara ya moyoni.
Hivyo kama hujampa Yesu Kristo maisha yako. Ni wazi kuwa bado hujapokea Tohara hii ya moyoni yenye umuhimu mkubwa sana. Maana hiyo ndio ishara ya Agano la Mungu kwako. jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Mada Nyinginezo:
Bwana Yesu alisema sehemu fulani maneno haya ” walakini siku ile na saa ile”..akiwa na maana kuwa Kuna siku inayokuja huko mbeleni, yenye Tarehe yake na mwezi wake, na mwaka wake. Siku hiyo itaitwa tarehe Fulani ya Mwezi Fulani na mwaka Fulani.
Siku hiyo upande mmoja wa dunia utakuwa ni mchana na mwingine usiku, siku hiyo watu watakuwa wanapika, wengine wanafanya biashara, wengine wanajenga, wengine wapo katikati ya harusi, wengine watakuwa safarini, wengine watakuwa misibani, wengine mashuleni, Wengine watakuwa wamelala, wengine wapo kanisani, wengine watakuwa mahospitalini, wengine mahakamani, wengine wanacheza mpira, wengine wapo disko. Wengine bungeni, wengine magerezani,wengine wanapanga mipango na mikakati ya namna ya kuimarisha vipato vyao na kazi zao n.k…Siku hiyo ndio itakuwa mwisho wa utendaji kazi wa Roho Mtakatifu duniani kwa watu wa mataifa…siku hiyo utapita kitu kinachoitwa UNYAKUO.
Wakati watu wengi watakuwa hawaelewi chochote, kufumba na kufumbua baadhi ya watu watatoweka, wachache sana…Tetesi tetesi chache zitasikika huko na huko kwamba kuna baadhi ya watu wamepotea katika mazingira ya kutatanisha, lakini kutokana na kwamba dunia imelewa na kulemewa na mambo mengi, wengi watasema ni habari za kuzusha, kwani imezoeleka kusikika unyakuo umepita na unakuta hakuna lolote lililotokea. Watasema mwaka 2000 ilikuwa hivyo hivyo, walitabiri na hakuna kilichotokea…mwaka 2002 ikawa hivyo hivyo, wakasema unyao umepita na hakuna lolote, kadhalika mwaka 2012…Na leo tena uzushi mpya umezuka.
Wakati mamia na maelfu ya watu wanapuuzia habari hizo na kuona ni habari za uzushi, upande wa pili kutakuwa na uchungu na vilio kwa wale waliowashuhudia wenzao wakinyakuliwa mbele ya macho yao, wale waliokuwa wanalima pamoja ghafla jirani anatoweka mbele yake, wale ambao walikuwa wamelala na wenzao katika chumba kimoja ambacho kilifungwa na makomeo kwa ndani, na walipoamka kwa ghafla wakakuta hawapo, huku milango bado imefungwa vile vile kwa ndani, wale ambao walikuwa wapo ibadani pamoja kanisani na ghafla wenzao wamepotea, wale ambao wamemwona mtu Fulani kaketi mahali Fulani na kufumba na kufumbua katoweka. Hao ndio watakaoelewa uchungu wa kuachwa. Watalia sana na kuomboleza lakini haitasaidia.
Siku hiyo utakapoona mwanao hayupo, dada yako aliyekuwa ameokoka hayupo, mchungaji wako hayupo, na wewe umeachwa! Itakuwa ni uchungu kiasi gani?. Ukitazama ni masaa machache tu nyuma umetoka kupokea rushwa, ukitazama ni masaa machache tu nyuma umesikia mahubiri ya kukuonya na ulimwengu ukakataa. Ukitazama ni wiki chache tu nyuma uliota ndoto inayokuonya kwamba hizi ni siku za mwisho ukapuuzia. Masaa machache tu ulisikia mahali panazungumziwa habari za unyakuo.
Ukitazama ni siku chache tu nyuma ndio ulianza kupoa, utajisikiaje? Ukitafakari sasa wenzako wanafutwa machozi mbinguni na wewe umebaki ukingojea dhiki kuu na chapa ya mnyama na ziwa la moto milele?, ukitafakari ni disko ndio iliyokuponza, mke au mume unayeishi naye ndio aliyekuponza, binti/kijana unayetembea naye ndiye aliyekuponza, utafutaji mali uliopindukia ndio iliyokuponza, miziki ya kidunia, na tamaa ndivyo vilivyokuponza kuikosa mbingu, utakuwa katika huzuni kubwa kiasi gani.
Ndugu hiyo siku inafika, labda ni leo, au kesho au kesho kutwa hakuna aijuaye! Lakini ipo karibuni sana biblia inasema hivyo…
Mathayo 24:36 “Walakini habari ya siku ile na saa ile hakuna aijuaye, hata malaika walio mbinguni, wala Mwana, ila Baba peke yake.
37 Kwa maana kama vile ilivyokuwa siku za Nuhu, ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu.
38 Kwa kuwa kama vile siku zile zilizokuwa kabla ya Gharika watu walivyokuwa wakila, na kunywa, wakioa na kuolewa, hata siku ile aliyoingia Nuhu katika safina,
39 wasitambue, hata Gharika ikaja, ikawachukua wote, ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Adamu.
40 Wakati ule watu wawili watakuwako kondeni; mmoja atwaliwa, mmoja aachwa;
41 wanawake wawili watakuwa wakisaga; mmoja atwaliwa, mmoja aachwa.
42 Kesheni basi; kwa maana hamjui ni siku ipi atakayokuja Bwana wenu
43 Lakini fahamuni neno hili; kama mwenye nyumba angaliijua ile zamu mwivi atakayokuja, angalikesha, wala asingaliiacha nyumba yake kuvunjwa.
44 Kwa sababu hiyo ninyi nanyi jiwekeni tayari; kwa kuwa katika saa msiyodhani Mwana wa Adamu yuaja.”
Kukesha kunakozungumziwa hapo na Bwana Yesu, sio kujizuia kulala usingizi wa mwilini wakati wa usiku hapana!…Bali maana yake kujizuia kulala usingizi wa rohoni…kwasababu duniani sasahivi ni giza! Ni Giza Nene kutokana na matendo ya giza yanayotendeka, Na sikuzote tabia ya giza ni kusababisha usingizi, siku zote usiku ndio watu wanalala! Sio mchana wakati wa Nuru, Kwahiyo giza lililopo duniani leo linasababisha usingizi mkali wa kiroho, na hivyo tunapaswa tuushinde huo usingizi na kukesha! Kwasababu Bwana atakapokuja hatawachukua watu waliolala bali walio macho!
Waefeso 5:14 “Hivyo husema, Amka, wewe usinziaye, Ufufuke katika wafu, Na Kristo atakuangaza.
15 Basi angalieni sana jinsi mnavyoenenda; si kama watu wasio na hekima bali kama watu wenye hekima;
16 mkiukomboa wakati kwa maana zamani hizi ni za uovu”.
Bado unaendelea na uasherati? Unaendelea na utoaji mimba? Unaendelea na uvaaji mbaya na ibada za sanamu? Tubu na kumgeukia mwokozi, kabla siku ile na saa ile haijafika. Kwasababu Bwana hapendi kumwona mtu yeyote aangamie, bali ni atubu, vilevile anataka watu wote waingie katika karamu ya mwana wake aliyowaandalia siku ile..Sasa Kwanini uikose?, tubu angali muda unao, na Bwana atakupokea na kukukaribisha katika ufalme wake.
Bwana akubariki! jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Mada Nyinginezo:
TUUTAZAME PIA MWISHO WA UJENZI WETU.
SADAKA YA MALIMBUKO.
HATARI YA KUHUBIRI INJILI TOFAUTI NA ILIYOANDIKWA KWENYE BIBLIA.
JISHUSHE ILI MUNGU AKUHUDUMIE.
ROHO HUTUOMBEA KWA KUUGUA KUSIKOWEZA KUTAMKWA!
Timazi ni nini?
Ni kifaa kidogo kilichokuwa kinatumika zamani katika Ujenzi na hata sasa bado kinaendelea kutumika…kifaa chenye umbo la PIA. Kinakuwa kimetengenezwa kwa chuma kizito kidogo. Na kinafungwa kamba, na kuwa katika hala ya kuning’inia. Na kinaning’inizwa kutokea juu ya ukuta kwenda chini.
Katika Biblia kifaa hichi kimetajwa mara kadhaa (Soma 2Wafalme 21:13, Isaya 28:19-17 na Zekaria 4:10,). Na kifaa hiki kimekuwa kikiwakilisha Upimwaji wa Taifa la Israeli. Bwana alipotaka kutumia lugha ya kupima kiwango cha maovu au wema, mara nyingi alitumia lugha ya kijenzi.
Ndio maana utaona Mfalme Nebkadneza baada ya kumchukiza Mungu aliambiwa “Amepimwa katika Mizani na kuonekana umepunguka” (Danieli 5:27). Kiuhalisia mtu hawezi kuwekwa kwenye mizani ya nafaka na kupimwa!..Hapana bali utaona hiyo ni lugha tu ya kuonesha kiwango cha maovu cha mtu huyo. Mfano mwingine tunaona kwa Nabii Amosi.
Amosi 7:6 “Bwana akaghairi katika jambo hili pia. Jambo hili halitakuwa, asema Bwana MUNGU.
7 Haya ndiyo aliyonionyesha; na tazama, Bwana alisimama karibu na ukuta uliojengwa kwa timazi, mwenye timazi mkononi mwake.
8 Bwana akaniambia, Amosii, unaona nini? Nikasema, Naona timazi. Ndipo Bwana akasema, Tazama, nitaweka timazi kati ya watu wangu Israeli; sitawapita tena kamwe”
Hata sasa Bwana ameshika TIMAZI juu ya mtu mmoja mmoja, na juu ya Ulimwengu kwa Ujumla..Anayapima matendo ya kila mtu, aangalie kama yamepunguka! au la!. Kama yanampendeza basi mtu huyo atapata rehema na thawabu kutoka kwa Mungu na kupendwa sana, lakini kama yamepunguka basi kuna hatari ya kuhukumiwa kama Mfalme Nebkadneza alivyohukumiwa.
Je matendo yako yanastahili hukumu au thawabu?. Jibu unalo. Kama hujampa Yesu Kristo maisha yako. Mlango wa Neema upo wazi, fanya hima uingie, kabla siku muda wako wa kuishi duiniani haujaisha.
Bwana akubariki.
jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Mada Nyinginezo:
KAMA MUNGU ANABORESHA KAZI ZAKE, KWANINI WEWE USIBORESHE ZA KWAKO?.
KUACHA KUVUTA SIGARA.
KUOTA UPO UCHI.
KUOTA UNAPAA.
KUSAMBAA KWA ROHO YA MPINGA-KRISTO.
Biblia inasema katika Zaburi 119:105 “Neno lako ni taa ya miguu yangu, Na mwanga wa njia yangu.” Hivyo Neno la Mungu ni Taa!
Maisha ya Mtu aliyeokoka yanafananishwa na Mtu asafiriye (Waebrania 11:13 na 1Petro 2:11). Na safari mtu aliyeokoka asafiriyo ni safari ya USIKU na si Mchana.
Hatari ya Kwanza: ni kukutana na wanyama wakali: Wanyama wote wararuao na wadhuruo huwa wanatembea Usiku, wanyama kama chui, simba, fisi, mbweha pamoja na nyoka huwa wanatafuta mara nyingi mawindo yao wakati wa Usiku.
Na viumbe vyote vinavyotembea usiku vinafunua viumbe vya rohoni vilivyo viovu ambayo ni mapepo..Ndio maana wanaojihusisha na uchawi wanatumia viumbe kama popo, bundi, fisi, chui, nyoka na viumbe vyote vinavyotembea gizani kufanya shughuli zao.
Wakati wa Usiku ni rahisi kupungukiwa umakini kutokana na Usingizi, au giza. Siku zote giza linaleta usingizi, wanaosafiri na magari usiku ni rahisi kupata ajali kuliko wanaosafiri mchana.
Hivyo ili kuzuia hatari zote hizi Msafiri asafiriye usiku anahitaji kuiongeza umakini sana anapotembea usiku na pia anahitaji TAA ITAKAYOMWONGOZA NJIA YAKE. Hakuna namna yoyote anaweza kukwepa matumizi ya Taa. Awe anatembea kwa miguu au kwa Gari, Taa ni Lazima.
Na sisi wakristo tupo safarini. Dunia ndio NJIA yetu. Na dunia yote sasa ni giza Kutokana na matendo ya giza yanayoendelea ulimwenguni kote. Uzinzi ni matendo ya giza, ulevi ni matendo ya giza. Kadhalika uchawi, rushwa, utoaji mimba, ulawiti, uvutaji sigara. Mauaji, usagaji na uchafu wa kila aina..Mambo hayo yanakoleza giza lililopo ulimwenguni.
Na sisi hatuna budi kupita katikati ya hilo giza ili tutokezee ng’ambo ya pili, hakuna kuingia mbinguni pasipo kupitia duniani!. Kwasababu hiyo basi tunahitaji Mwanga katika hili giza Nene!. Na Mwanga si kingine bali ni NENO LA MUNGU, Lililovuviwa na Roho Mtakatifu.
Neno la Mungu linaposema Usizini, ni kwa faida yetu! Neno hilo ni mwanga wa njia zetu, maana yake tukizini tumeizimisha taa. Na hivyo ni rahisi kupotea. Na kushambuliwa na wanyama wakali. Kadhalika na maneno mengine yote ambayo Biblia imekataza kama rushwa, usengenyaji, chuki, wivu, hasira, faraka, uchungu, wizi, uuaji, ulevi n.k hayo yote ni matendo yanayozima taa zetu na hivyo kutuweka hatarini katika safari yetu.
Zaburi 119:9 “Jinsi gani kijana aisafishe njia yake? Kwa kutii, akilifuata neno lako”.
Hivyo ukitaka kuisafisha njia yako!. Utaisafisha tu kwa kulitii na kulifuata Neno la Mungu ambalo hilo ndilo Taa yetu.
Kumbuka Bwana Yesu anakuja, na wala hatakawia. Hivyo kama hujaoshwa dhambi zako kimbilia Kalvari haraka kabla mlango wa Neema haujafungwa. Na Bwana atakuokoa.
Bwana akubariki. jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Mada Nyinginezo:
BARAGUMU NI NINI?
USIPOLITENDEA KAZI NENO LA MUNGU.
JE KUJIUA NI DHAMBI?
Wakatoliki wanaabudu sanamu?
SWALI: Huyu Yeshuruni ni nani kwenye biblia?. Na kwanini alinenepa na kumdharau mwamba wa wokovu wake (Kumb.32:15)?.
JIBU: Yeshuruni ni jina lingine la Taifa la Israeli lililotumika katika biblia ya kiyahudi hususani katika mashahiri,..Neno hili linaonekana mara 4 katika biblia soma (Kumbukumbu 32:15, 33:26, 33:5 na Isaya 44:2).
Hivyo tukirudi pale kwenye Kumbukumbu 32:15-18
Inasema..
Kumbukumbu 32:15 “Lakini Yeshuruni alinenepa, akapiga teke; Umenenepa, umekuwa mnene, umewanda; Ndipo akamwacha Mungu aliyemfanya, Akamdharau Mwamba wa wokovu wake
16 Wakamtia wivu kwa miungu migeni, Wakamkasirisha kwa machukizo.
17 Walitoa sadaka kwa pepo, si Mungu, Kwa miungu wasiyoijua, Kwa miungu mipya iliyotokea siku zilizo karibu, Ambayo baba zenu hawakuiogopa.
18 Humkumbuki Mwamba aliyekuzaa, Mungu aliyekuzaa umemsahau,”
Maneno hayo aliyazungumza Musa akiwa jangwani, kama unabii, kuonyesha jinsi Israeli watakavyokuja kumsahau Mungu wao huko mbeleni watakapofika katika nchi yenye maziwa na na asali, kwa kufanikiwa kwao, kwa nchi kuwazalia, kwa kutokuwa tena na jangwa, wala kula chakula cha aina moja, kwa kufanya biashara na kufanikiwa na kuwa matajiri, watamsahau Mungu wao aliyewatoa katika ile nchi ya Misri, watamsahau yule Mungu ambaye walikuwa wanamtumainia walipokuwa jangwani kwenye shida, watamdharau na kugeukia miungu mingine. Na unabii huo ulikuja kutimia vilevile kama Musa alivyotabiri katika shahiri lile walipofika nchi ya ahadi.
Hivyo ukikutana na Neno hilo Yeshuruni ni nani, basi ufahamu hilo ni jina lingine la Israeli.
Hata leo hii ni kawaida ya watu kumtafuta Mungu wakati wa shida, tu, lakini pale wanapofanikiwa, au pale ambapo hawana haja ya kitu chochote, wana afya, wana mali basi Mungu kwao si kimbilio tena,..wapo tayari hata kuutakana wokovu na kuona kama ni ushamba.Ndio maana Bwana Yesu alisema ni rahisi ngamia kupenya katika tundu la sindano kuliko Tajiri kuingia katika ufalme wa Mungu..
Utajiri wa aina yoyote ile ni ukweli usiopingika kuwa ni kikwako kikubwa sana katika ufalme wa mbinguni, kama vile umaskini uliopindukia ulivyo. Haimaanishi kuwa tusiwe matajiri lakini tunapaswa tutumie hekima katika kumwomba Mungu atupe kile ambacho ni sawasawa na uwezo wetu, tusije tukanenepa na kuwanda kama Yeshuruni na kumsahau Mungu, kama Aguri bin yake alivyotushauri katika Mithali 30:9.
Mithali 30:8“…………Usinipe umaskini wala utajiri; Unilishe chakula kilicho kadiri yangu.
9 Nisije nikashiba nikakukana, Nikasema, Bwana ni nani? Wala nisiwe maskini sana nikaiba, Na kulitaja bure jina la Mungu wangu.”
Ubarikiwe,jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Mada Nyinginezo:
SADAKA YA MALIMBUKO.
JE! UNAYO NAFASI MBINGUNI?
Ni sahihi kumuita Mariamu mama wa Mungu?
JISHUSHE ILI MUNGU AKUHUDUMIE.
2Wakorintho 6:1 “Nasi tukitenda kazi pamoja naye twawasihi msiipokee neema ya Mungu bure.
2 (Kwa maana asema, Wakati uliokubalika nalikusikia, Siku ya wokovu nalikusaidia; tazama,wakati uliokubalika ndiyo sasa; tazama siku ya wokovu ni sasa)”
Saa ya Wokovu ni sasa na sio kesho! Leo ndio wakati uliokubalika, dakika hii ndio wakati uliokubalika wa kupoekea Wokovu, usiseme kesho! Kwasababu kesho huwa inajipangia yenyewe mambo yake. Jambo ambalo wengi hawalijui ni kwamba Siku ndiyo inayotengeneza matukio na sio mtu anayetengeneza matukio ya siku.
Utapanga kesho ufue na kuanika nguo zako, lakini hiyo kesho mvua ikanyesha kubwa hata ikakuzuia wewe kufua. Umepanga kesho usafiri lakini hali ya hewa ikakuzuia. Umepanga kesho usafiri kwenda mashariki lakini ghafla ukajikuta unakwenda kusini kwenye mazishi.
Hivyo kesho si ya kuitumainia kabisa kwasababu imejaa mambo ya kushtukiza. Biblia inasema..
Mithali 27:1 “Usijisifu kwa ajili ya kesho; Kwa maana hujui yatakayozaliwa na siku moja”.
Mathayo 6:34 “Basi msisumbukie ya kesho; kwa kuwa kesho itajisumbukia yenyewe. Yatosha kwa siku maovu yake”.
Hivyo hakuna Tarehe, wala Mwezi wala Mwaka uliopangwa kwa wokovu…SAA YA WOKOVU NI SASA! na WAKATI ULIOKUBALIKA NDIYO SASA, na SIKU YA WOKOVU NI SASA.
Je! Umeokoka? na kama Bado unasubiri nini? Unajitumainisha na ya kesho? je wewe una hekima kulika Mungu anayekuambia kuwa usijisiu kwa ajili ya kesho? Hivyo ni kama hujampa Yesu Kristo maisha yako, na Roho Mtakatifu anaugua ndani yako sasa juu ya dhambi zako. Usikawie, hapo ulipo piga magoti, nyosha mikono yako juu!. Tubu kwa kumaanisha kabisa kuhitaji rehema kutoka kwa Bwana.
Bwana anakuona moyo wako naye atakuokoa sasa! kwasababu amesema mwenyewe saa ya wokovu ni sasa! Hivyo leo leo utakuwa umeokoka kama umedhamiria kutubu!
Sema Bwana Yesu!, ninakuja mbele zako. Mimi ni mwenye dhambi! naomba unisamehe dhambi zangu zote, Naahidi kutokuzifanya tena! Nisaidide Bwana. Niondoe kutoka katika mstari wa wanaokwenda Jehanamu niingize katika orodha ya wanaokwenda mbinguni. Nipe moyo safi leo! naomba Roho wako Mtakatifu aingie ndani yangu sasa! niwe Mtakatifu. Nakiri kwamba wewe ndiye Mwokozi wangu, na Bwana wangu na Mungu wangu, katika Jina la Yesu.
Kama umefuatiliza sala hiyo. Basi umeshaokoka sasa! katika saa hii hii, kwasababu yeye anasema “Wakati uliokubalika nalikusikia“. Hivyo ameshakusikia. Kwahiyo sasa Chukua hatua ya kiimani kutafuta kanisa la kiroho ambalo utaweza kubatizwa ubatizo sahihi wa maji tele na kwa jina la Yesu kama hujabatizwa! Hiyo yote ni ili kuutia muhuri wokovu ambao umeshaupata moyoni mwako leo.
Kama utapata shida katika kutafuta kanisa, unaweza kuwasiliana nasi tutakusaidia kukuelekeza kanisa karibu na mahali ulipo ambapo utaweza kupata huduma hiyo ya ubatizo na ya kufanya ushirika na watu wenye Imani moja na wewe. Tutumie ujumbe mfupi kwa kupitia namba hizi 0789001312.
Bwana akubariki. jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Mada Nyinginezo:
Nini tofauti ya haya maneno. 1) KUOKOKA, 2) WOKOVU, 3) KUONGOKA.?
Jina la Bwana wetu Yesu Kristo libarikiwe, karibu tujifunze Neno la Mungu ambalo ndio mwanga wa njia zetu na taa ya miguu yetu. Zab 119:105..Leo tutajifunza kwa ufupi sana juu ya kulipa Zaka, Kimaandiko Zaka ni fungu la 10, yaani sehemu ya 10 ya mapato ya mtu anayatoa kwa Mungu. Kwahiyo zaka ni mojawapo ya aina ya sadaka.
Kabla hatujaenda kujifunza kuhusu umuhimu wa kulipa zaka, kama ina ulazima au la! Hebu tujifunze kidogo historia ya ZAKA.
Zaka kwa mara ya Kwanza ilianza kutolewa na mtu anayeitwa Ibrahimu, ambaye anajulikana kama Baba wa Imani.
Mwanzo 14:17 “Abramu aliporudi kutoka kumpiga Kedorlaoma na wale wafalme waliokuwa pamoja naye, mfalme wa Sodoma akatoka amlaki katika bonde la Shawe, nalo ni Bonde la Mfalme.
18 Na Melkizedeki mfalme wa Salemu akaleta mkate na divai, naye alikuwa kuhani wa Mungu Aliye juu sana.
19 Akambariki, akasema, Abramu na abarikiwe na Mungu Aliye juu sana, Muumba mbingu na nchi.
20 Ahimidiwe Mungu Aliye juu sana, aliyewatia adui zako mikononi mwako. ABRAMU AKAMPA FUNGU LA KUMI LA VITU VYOTE”.
Ibrahimu alimpa fungu la 10 huyu Melkizedeki, huyu Melkizedeki alikuwa ni Mungu aliyekuja katika Mwili wa kibinadamu… na pia anajulikana kama Kuhani Mkuu, mfano wa Mwana wa Mungu (Yesu Kristo) hana baba, wala mama, wala hana mwanzo wa siku wala mwisho wake. Kwahiyo alikuwa ni Mungu mwenyewe aliyekuja katika mwili wa kibinadamu.
Sasa wakati Abramu ametoka kumwokoa ndugu yake Lutu ambaye alikuwa ametekwa yeye pamoja na wanawe, njiani wakati anarudi akakutana na Huyu Melkizedeki, na huyu Melkizedeki alikuwa amebeba Divai na Mkate, akampatia Abramu na kwasababu Abramu alimpenda sana Mungu, hakuona vyema kupokea bure bila kutoa chochote…zaidi ya yote Mungu amemwonekania na kumfanikisha katikati ya maadui zake na kuwashinda! Hivyo ndani yake kuna kitu cha kipekee kikamgusa akaona si vyema kutomrudishia chochote Mungu wake, hivyo akaamua mwenyewe pasipo kuambiwa na mtu yeyote kumtolea Mungu wake sehemu ya 10 ya vitu vyake!!! O huo ni moyo wa namna gani? Kumbuka hakuambiwa hata na Mungu afanye vile, ni yeye mwenyewe tu kuna kitu ndani yake kilimfanya ajisikie vibaya endapo angemwona Mungu wake anaondoka mikono mitupu, na hicho si kingine zaidi ya Roho Mtakatifu.
Sasa wakati huo kulikuwa hakuna sheria yoyote, wala amri 10 na Mungu hakuingia Agano na Ibrahimu kuhusu zaka, Miaka kama 400 hivi baadaye ndipo wana wa Israeli, walikuja kupewa sheria na Mungu! Na miongoni mwa hizo sheria ilikuwa ni pamoja na kulipa zaka!, ilikuwa ni lazima kulipa zaka, mtu asipolipa zaka ilikuwa inahesabika kwake kuwa ni dhambi!, na mbele za Mungu ni kama mwizi (Malaki 3:8-9).
Lakini sasa hatuishi kwa sheria bali kwa Imani, na Imani tunayoizungumzia ni Imani ile ile ya kwanza kama ya Ibrahimu, yaani Imani ya kufanya mambo bila ya kusukumwa sukumwa, na Imani hiyo ndio kama hiyo ya Ibrahimu, ya kumtolea Mungu fungu la 10 pasipo masharti!..Ibrahimu alitoa pasipo masharti, wala sheria, wala torati kwasababu Torati hata bado ilikuwa haijaja, wala kulazimishwa, wala kusukumwa wala kuombwa, wala kumwuliza Mungu, wala kuhubiriwa na mtu yeyote bali alitoa kwa Imani na kwa moyo, akitafakari kwamba vyote vimetoka kwa Mungu, na Mungu ndiye mpaji wangu (Yehova-YIRE), hivyo kama yeye amenipa sehemu kubwa ya vitu hivi, basi mimi nitamrudishia walau sehemu ya 10 ya vitu alivyonipa. Na akajiwekea hiyo kuwa ndio sheria yake daima! Kila sehemu ya 10 anayopata anamrudishia Mungu.
Ndugu, Ibrahimu alikutana na Melkizedeki, na hata sasa huyu Melkizedeki yupo naye si mwingine bali ni Bwana wetu Yesu Kristo, maandiko yanalithibitisha hilo katika…
Waebrania 6:20 “alimoingia Yesu kwa ajili yetu, mtangulizi wetu, amekuwa kuhani mkuu hata milele kwa mfano wa Melkizedeki”.
Waebrania 7:1 “Kwa maana Melkizedeki huyo, mfalme wa Salemu, kuhani wa Mungu aliye juu, aliyekutana na Ibrahimu alipokuwa akirudi katika kuwapiga hao wafalme, akambariki;
2 ambaye Ibrahimu alimgawia sehemu ya kumi ya vitu vyote; (tafsiri ya jina lake kwanza ni mfalme wa haki, tena, mfalme wa Salemu, maana yake, mfalme wa amani;
3 hana baba, hana mama, hana wazazi, hana mwanzo wa siku zake, wala mwisho wa uhai wake, bali amefananishwa na Mwana wa Mungu); huyo adumu kuhani milele.
4 Basi, angalieni jinsi mtu huyo alivyokuwa mkuu, ambaye Ibrahimu, baba yetu mkuu, alimpa sehemu ya kumi ya nyara”.
Waebrania 5:5 “Vivyo hivyo Kristo naye hakujitukuza nafsi yake kufanywa kuhani mkuu, lakini yeye aliyemwambia, Ndiwe mwanangu, Mimi leo nimekuzaa.
6 kama asemavyo mahali pengine, Ndiwe kuhani wa milele Kwa mfano wa Melkizedeki”.
Umeona Kristo amefananishwa na Melkizedeki, na kama Melkizedeki alipewa sehemu ya 10 na Ibrahimu, kadhalika Kristo naye anastahili sehemu ya 10, kwasababu yeye ndiye Melkizedeki wa Agano letu, na kama Melkizedekia alivyompigania Ibrahimu ndivyo Kristo anavyotupigania sisi sasa hivi,
Na kama Ibrahimu alimpa Melkizedeki fungu la 10 pasipo masharti, wala pasipo torati, wala pasipo sheria yoyote, wala pasipo kuhubiriwa na mtu, wala pasipo kushauriwa na mtu, wala pasipo kusukumwa na mtu yeyote ndivyo hivyo hivyo leo hii tunapaswa tumtolee YESU KRISTO fungu la 10 pasipo sheria yoyote, wala pasipo masharti yoyote, wala pasipo mahubiri yoyote, wala pasipo kusukumwa na mtu..Linapaswa liwe ni jambo linalotoka moyoni kwamba tunatambua uwepo wa Yesu Kristo katika maisha yetu na hivyo tunamheshimu kwa kumtolea fungu la 10, yeye hana shida na fedha! Lakini anaitazama mioyo yetu!. Na Bwana Yesu mwenyewe aliruhusu hilo katika (Mathayo 23:23).
Ukiona mtu anapinga kulipa ZAKA!(Na huku ameshaujua ukweli) Na anapinga kumtolea Mungu, Huo ni uthibitisho kuwa hana ROHO MTAKATIFU ndani yake! Ni moja ya uthibitisho wa mtu aliyekosa Roho Mtakatifu ndani yake!..Kwasababu ni wazi kuwa hampendi Mungu, kwasababu hawezi kumshukuru kwa kutoa hata sehemu ya 10 ya mali zake na kumrudishia yeye, ingawa anavuta pumzi bure, anakanyaga ardhi ambayo sio yake bure, anakula chakula ambacho hajui kimetengenezwaje tengenezwaje! Hathamini hata Kristo aliyeotoa uhai kwa ajili yake bure..Kwa ufupi ni mtu asiye na shukrani.
Na mtu wa namna hiyo atawezaye kumshukuru Mungu kwa kutoa sehemu ya 10 ya maisha yake kuhubiri Injili?, atawezaje kutoa kutoa hata uhai wake kwaajili ya Injili?, au atawezaje kuifia Imani? Kama tu sehemu ya 10 ya fedha yake hawezi kuitoa?. Huyo Mtu atawezaje hata kuacha vyote na kumfuata Kristo kama tu sehemu ya 10 kutoa ni vita?..Atawezaje kumtolea Mungu katika vyote alivyonavyo kama Yule mwanamke aliyetoa senti mbili na Bwana akamsifia? Tafakari tu!
Hivyo ZAKA sio kitu cha kukwepa kabisa! Hakitolewi kwa sheria wala kwa torati, wala kwa imeandikwa wapi kwenye biblia, bali kwa moyo kama vile Ibrahimu!..Kama huna kazi yoyote inayokupatia kipato hapo upo huru!, lakini chochote unachokipata tofauti na kazi kitolee sehemu ya 10 katika hicho na kumrudishia Mungu, huna kazi lakini umepewa zawadi kiasi Fulani cha fedha kitolee sehemu ya 10, na utoe kwa moyo pasipo kulazimishwa, kwasababu Mungu sio mkusanyaji mapato! Anataka tumtolee kwa Moyo na kwa furaha, huku tukielewa umuhimu wa kumtolea yeye kama Ibrahimu alivyofanya.
Kitakachompeleka mtu kuzimu sio kitendo cha kukiuka kulipa zaka au kuzini, au kuiba, au kutukana hapana kitakachompeleka mtu kuzimu ni kumkosa Kristo moyoni mwako, akaaye kama Roho Mtakatifu, ambapo sasa matokeo ya kutokuwa na Roho Mtakatifu ndio hayo sasa atakuwa mwizi, mwasherati, mtukanaji, atakuwa ni mtu asiyekuwa na Moyo wa Utoaji kabisa, likija suala la utoaji ni vita, anakuwa hawezi kuwasaidia wengine, na pia hawezi kuchangia chochote katika ufalme wa mbinguni katika utoaji wake, pia anakuwa mtu asiyesamehe Kwasababu Mtu aliye na Roho Mtakatifu hawezi kufanya mojawapo ya hayo mambo kwasababu Roho Mtakatifu atakuwa anaugua ndani yake kuhusu dhambi na atakuwa anaugua pia kuhusu ni kwanini hamtolei Mungu, hivyo hawezi kukwepa kulipa zaka kama vile asivyoweza kukwepa kuwasaidia wengine au kusali.
Upo usemi unaosema kwamba, mimi ni mkamilifu katika kila kitu! Isipokuwa ni zaka tu ndio sitoi!
Bwana akubariki jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Mada Nyinginezo:
JE! UNAYO NAFASI MBINGUNI?
KUWA MAKINI NA MITANDAO, NI SHIMO REFU.
JISHUSHE ILI MUNGU AKUHUDUMIE.
UNATAKA KUBARIKIWA? BASI USIKWEPE GHARAMA ZAKE.
Kumbukumbu 22:8 “Utakapojenga nyumba mpya, fanya ukuta kando-kando ya dari lako, usije ukaleta damu juu ya nyumba yako, mtu akianguka huko”.
Bwana Yesu alisema, mtu yeyote anayeyasikia maneno yangu na kuyatenda anafananishwa na mtu aliyejenga nyumba yake juu ya mwamba…(Mathayo 7:24), Hii ikiwa na maana kuwa kumbe Maisha ya kila mtu aliyeokoka ni sawa na nyumba inayoijenga yeye mwenyewe,..Hivyo kila mtu anapaswa awe makini anapoijenga nyumba yake sio tu pale anapoujenga msingi wake bali pia mpaka pale anapomalizia…
Kwamfano tutaona hapa Bwana Yesu alikuwa anasisitiza juu ya msingi, ambao ndio mwanzo wa ujenzi wa maisha ya mtu, kwamba ukitaka nyumba yako(Maisha yako) yasiwe kazi bure basi zingatia ni ardhi gani unayoijengea nyumba yako, kama ni mwamba (ambao ndio maneno ya Yesu Kristo yenyewe) basi fahamu kuwa msingi wako nyumba yako utakuwa salama na nyumba yako itasimama imara milele lakini kama ni nje ya Kristo basi ujue Maisha yako unayoyaishi sasa hivi ni kazi bure kwasababu yatafikia mwisho yatakoma na utakuwa umepata hasara kubwa..
Lakini Sio tu kufanikiwa kuijenga nyumba yako juu ya mwamba imara, unapaswa pia uzingatie umaliziaji wa nyumba yako ili iwe katika ujenzi bora na salama..Kama tunavyosoma hapo juu enzi za agano la kale Mungu alitoa amri kwa waisraeli wote, pindi tu wanapomaliza kujenga nyumba zao, hawapasi kuzifunika tu kwa sakafu au matofali na kuziacha hivyo hivyo bila uzio wowote kama ujenzi mwingi unavyofanyika sikuhizi wa kuweka mabati, hapana bali Mungu aliwapa maagizo wahakikishe kuwa wanaweka ukuta kando-kando ya dari zao, ulionyanyuka, kusudi kwamba ikitokea mtu amepanda kule, na akateleza bahati mbaya, basi ule ukuta ulio kando kando ya dari umzuie asianguke mpaka chini, tofauti na ujenzi mwingi wa sasa hivi ulivyo, mtu akiteleza kwenye bati basi moja kwa moja ni mpaka chini, na pengine kumsababishia majeraha ya kudumu au mauti kabisa. Angalau baadhi ya magorofa marefu yana uzio huo kule juu kabsia, ingawa si yote.
Hivyo nyumba zote, na majengo yote ya kiyahudi ndivyo yalivyojengwa enzi zile. Na kama mtu asipofanya hivyo na ikatokea mtu akaanguka darini kwake, basi damu ya huyo mtu, Mungu ataitaka juu ya huyo mwenye nyumba.
Kama tulivyoona mkristo kweli anaweza akawa ameanza vizuri katika ujenzi wake, ameokoka, amemwamini Yesu Kristo, amepokea uzima wa milele, lakini hazingatii kuchukua tahadhari katika nyumba yake anayoijenga, haweki kuta, hajiwekei mipaka ya njia zake, hajui kuwa wapo watu wanamwangalia, wapo watu wanayatambelea Maisha yake kila siku, wanapanda mpaka juu ya dari lake, mahali ambao anadhania watu hawawezi kufika,Sasa kwa kutolijua hilo wale watu wanapofika, na kukutana na kikwazo kidogo tu, pengine wanamwona ni mvaaji wa vimini, unatembea nusu uchi barabarani halafu unasema umeokoka, ni rahisi wao kuanguka, na kusema kama wokovu ndio huu, ni heri niendelee kuwa kahaba milele…Hajui kuwa ameshamkosesha yule mtu na damu yake itatakwa juu yake.
Unakwenda disko, unatukana , na bado unasema umeokoka, unacheza kamari, una-bet na huku bado unasema umeokoka, wale watu wanaokutazama, wakiona mapungufu kama hayo, umewasababishia wao kuanguka mara mbili Zaidi. Ni heri ungesema sijaokoka wasingekuwa na la kujikwaa, na hiyo yote ni kwasababu hujiwekei kuta za kuilinda nyumba isiwe ya lawana.
Unasikiliza miziki ya kidunia, muda huo huo unamwimbia Mungu, wale watu wanaokuzunguka watakuonaje? Watasema kuna wokovu kweli hapo? unakula rushwa, unaongea matusi hivyo vyote ni vikwazo, unawasengenya wengine, hatujui kuwa sisi ni barua inayosomwa na watu wote. Ujenzi wetu wa mwisho unapaswa uthaminiwe kama ulivyokuwa ule wa kwanza.
Vinginevyo tutajikuta tunakwenda kulaumiwa kwa kuwakosesha wengine,. Na adhabu ya kuwakosesha wengine ni kubwa Zaidi, Bwana Yesu alitoa mfano wake na kusema ni heri mtu wa namna hiyo angefungiwa jiwe la kusagia na kutupwa baharini, kuliko kumkosesha mmojawapo wa wadogo hao.
Hivyo kama tumedhamiria kweli kumfuata Kristo, basi kila siku tujiangalie, tujiwekee mipaka, tuhakikishe ndani yetu hakuna mahali popote pa kumkwaza asiye amini..kuvaa vizuri ni mipaka!, kutokushiriki usengenyaji ni mipaka, kutoshiriki mazungumzo ya mizaha na kujiheshimu ni mipaka…Bwana atusaidie sote katika hilo.
Ubarikiwe. Tafadhali “Share” Ujumbe huu na kwa wengine.jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Mada Nyinginezo:
NYAKATI SABA ZA KANISA NA WAJUMBE WAKE.
HAMJAFAHAMU BADO?
NILIMWONA SHETANI, AKIANGUKA KUTOKA MBINGUNI.
NGUVU YA UPOTEVU.
http://wanatai.wingulamashahidi.org/