Jina la Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo libarikiwe, karibu tujifunze biblia.
Leo nataka tujifunze umuhimu wa kuchunguza mambo, kwani tusipokuwa watu wa kuchunguza mambo basi tunaweza tusiuelewe uweza wa Mungu.
Asilimia kubwa ya watu wanaobarikiwa hawajui kuwa mafanikio yao ni kutokana na maombi ya watu wengine (ambao wanawaombea wao pasipo kujua), hivyo ni muhimu sana kufikiri wakati wa kufanikiwa.
Hebu tujifunze katika ile habari ya Kana ya Galilaya pale Bwana Yesu alipofanya muujiza wake wa kwanza wa kugeuza maji kuwa divai.
Maandiko yanasema baada ya Bwana Yesu kubadili yale maji kuwa divai, yule Mkuu wa meza, aliyeteuliwa kuandaa vinywaji vya wageni wa kawaida na mgeni rasmi, hakujua kama ile divai mpya imetoka kwa Bwana, badala yake alidhani mwenye sherehe ndiye aliyeinunua, na ndipo akaenda kumfuata mwenye sherehe (Bwana harusi) na kumpongeza akidhani kuwa yeye ndiye kainunua ile divai mpya na kuwapa watu wote wanywe.
Na yule Bwana harusi naye akashangaa kupewa sifa ambazo si zake, huenda na yeye akadhani kuna mtu tu katikati ya sherehe kajitokeza na kujitolea kununua divai mpya ili kuimeza aibu.. kwamaana divai kuisha katikati ya sherehe na bado kuna watu wa muhimu hawajapata, ilikuwa ni aibu kubwa sana kwa wenye sherehe. Hivyo mpaka mwisho wa sherehe ni wachache sana ndio waliojua siri ya ile divai, kuwa na Bwana Yesu ndiye aliyeitoa.
Tusome,
Yohana 2:1 “Na siku ya tatu palikuwa na arusi huko Kana, mji wa Galilaya; naye mama yake Yesu alikuwapo.
2 Yesu naye alikuwa amealikwa arusini pamoja na wanafunzi wake.
3 Hata divai ilipowatindikia, mamaye Yesu akamwambia, Hawana divai.
4 Yesu akamwambia, Mama, tuna nini mimi nawe? Saa yangu haijawadia.
5 Mamaye akawaambia watumishi, Lo lote atakalowaambia, fanyeni.
6 Basi kulikuwako huko mabalasi sita ya mawe, nayo yamewekwa huko kwa desturi ya Wayahudi ya kutawadha, kila moja lapata kadiri ya nzio mbili tatu.
7 Yesu akawaambia, Jalizeni mabalasi maji. Nao wakayajaliza hata juu.
8 Akawaambia, Sasa tekeni, mkampelekee mkuu wa meza. Wakapeleka.
9 Naye mkuu wa meza alipoyaonja yale maji yaliyopata kuwa divai, (wala asijue ilikotoka, lakini watumishi walijua, wale walioyateka yale maji), yule mkuu wa meza alimwita bwana arusi,
10 akamwambia, Kila mtu kwanza huandaa divai iliyo njema; hata watu wakiisha kunywa sana ndipo huleta iliyo dhaifu; wewe umeiweka divai iliyo njema hata sasa”.
Sasa nataka tuone nyuma ya Baraka hizo alikuwa nani?, Nyuma ya muujiza huo alikuwa nani, na nyuma ya aliyetoa aibu alikuwa ni nani?.. kisha na sisi tutapata akili wakati wa kufanikiwa.
MWOMBAJI/ WAOMBAJI.
Kulipoonekana tatizo, Marimu alienda kumwomba Bwana na kumsihi sana. Huyu ndiye aliyekuwa mwanzo wa muujiza wa divai. Kama sio Mariamu watu wangeabika kwenye sherehe hata kama sherehe hiyo Kristo alikuwepo ndani.
Vile vile hata leo, ukiona jambo Fulani la heri limetokea mbele yako lililoziba aibu yako, hebu tafakari sana, usijivune wala usikimbilie kusema wewe ni mwenye bahati, huna bahati yoyote, hayo ni matokeo ya wengine kuomba kwaajili yako..haijalishi Kristo yupo na wewe.. Hata katika ile harusi Kristo alikuwepo ndani, alikuwa ni mwalikwa, lakini bado kama pasingekuwepo mwombaji, hakuna kitu kingefanyika.
Ukiona umebarikiwa kwa jambo Fulani au mambo yako fulani fulani yameenda sawa usikimbilie kujisifu, wala kujivuna, kwamba una bahati!!…fahamu kuwa hayo ni matokeo ya wengine kuomba kwaajili yako, na hao huenda unawajua au huwajui.
Mtoto ukifanikiwa jua wakati mwingine ni matokeo ya maombi ya wazazi wako na si kwasababu wewe una akili sana au una ujanja mwingi, kijana ukifanikiwa jua ni matokeo ya maombi ya ndugu zako, au wapendwa wenzako wanaokesha kwaajili yako pasipo wewe kujua.
Unapoona unapiga hatua kimaisha au kiroho, fahamu kuwa ni matokeo ya wanaokuongoza kiroho kukuombea, wala usidhani ni kwa nguvu zako au una bahati..
Waebrania 13:17 “Watiini wenye kuwaongoza, na kuwanyenyekea; maana wao wanakesha kwa ajili ya roho zenu, kama watu watakaotoa hesabu, ili kwamba wafanye hivyo kwa furaha wala si kwa kuugua; maana isingewafaa ninyi”
Ukilifahamu hili siku zote utakuwa mnyenyekevu na kumshukuru Mungu kwa kila jambo na pia kufikiri sana kuwaheshimu wanaokuombea na hata wewe kutenga muda kuwaombea!.. Laiti yule mkuu wa Meza na yule Bwana arusi wangejua kitu Mariamu alichowafanyia, kwenda kuwaombea kwa Bwana wangeshangaa sana, na kunyenyekea sana.
Laiti ungejua mambo watu wanayomwambia Bwana kuhusu wewe, usingebaki kama ulivyo..
Amani ya familia yako, Amani ya jamii yako, Amani ya nchi yako, ni matokeo ya maombi ya watu wengine wa Mungu wanaolia mbele zake usiku na mchana.. wala si kwasababu nyingine?, kama si hao ni kitambo sana mambo ya ulimwengu yangeshaharibika..(2Thesalonike 2:7).
Bwana akubariki.
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
Mada Nyinginezo:
SABATO ILIFANYIKA KWAAJILI YA MWANADAMU NA SI MWANADAMU KWAAJILI YA SABATO!
Je! Siku ilihesabiwaje kabla ya jua na mwezi kuumbwa?
Je! Karamu za ‘Idi’ ndio zipo hizo tunazozisoma katika Hosea (12:9)
Ni lini na wapi Ibrahimu aliioona siku ya Bwana akashangilia?.
Nakusalimu katika jina kuu sana na lenye nguvu la Bwana wetu Yesu Kristo. Karibu tujifunze maneno ya uzima ya Mungu wetu.
Sisi kama Wanadamu Kila mmoja wetu haijalishi ameokoka au hajaokoka, ndani yake ameumbiwa kiwango cha “kusahau”. Hii ni karama ya Mungu na ni vizuri kumshukuru Mungu Kwa jambo hili, kwasababu kama tungeikosa wanadamu wote tusingeishi hivi tulivyo Leo.
Lakini kusahau kukisimama Mahali pasipo-papasa, inageuka kuwa hatari kubwa sana, Tena dhambi yenye matokeo mabaya sana rohoni.
Kuna aina ngapi za kusahau?
Sasa kusahau kunaweza kuwa aidha kupoteza kumbukumbu ya lile jambo au tukio, Moja Kwa Moja akilini mwako, uwe kana kwamba hujawahi kulipitia.
Au kunaweza kuwa kulipoteza tu Kwa muda katika kumbukumbu lakini utakapokumbushwa unalikumbuka Tena.
Kusahau kwenye madhara ni kupi?.
Kabla ya kutazama ‘kusahau’ kwenye hasara tuone kusahau kwenye faida kukoje.
Kusahau kwenye faida kunatimia katika mambo yasiyo na maana, au yenye maudhui hasi kwako. Kwa mfano pale mtu unapotukanwa, au unapopigwa kikumbo barabarani na mtu usiyemjua, unaposikia miziki isiyokufaidia huko nje, unapofiwa, unapodhulumiwa, unaposemwa, unapovunjiwa heshima, unapoaibishwa, unaposingiziwa n.k… Mazingira kama haya ambayo ni hasi…kusahau Kunahitajika sana na ni lazima ujifunze kuruhusu jambo hili liumbike ndani Yako ili uponyeke kwa haraka,.maana ndio sehemu yake hiyo inapopaswa itumike.
Lakini kusahau kusikokujenga ni pale unaposahau Matendo mema, au mambo chanya yakupasayo kutenda. Kwamfano Sheria inasema ” usitupe taka hapa” Halafu inapita wiki Moja umesahau agizo hilo, unarudia tena kutupa taka pale pale ulipokatazwa..Hapo utakuwa hujitafutii jambo lingine zaidi matatizo?
Vivyo hivyo katika Neno la Mungu pale unaposahau sahau Neno la Mungu hapo ndio pabaya sana. Wakristo wengi hatujui kuwa Mungu “anayorudia kutuambia ni mengi kuliko Yale mapya anayotaka kusema nasi”..Ni Kwanini? ni kwasababu tumekuwa wepesi wa kusahau Sheria zake.
Mambo yamekuwa kinyume chake, badala tusahau yaliyo mabaya tukumbuke yaliyo mema, tunasahau mema tunakumbuka mabaya sikuzote.
Ni shambuliko kubwa sana ambalo ibilisi amelipanda mioyoni mwa wanadamu. Ndio sababu uchungu haukomi, masengenyo hayaishi, vita vinazuka Kila siku, fitna, unafki, na uongo havina mwisho ni kwasababu Hali Ile Ile tuliyokuwa nayo nyuma mpaka sasa tunairuhusu ikae kwenye akili zetu.
Wakati nguvu hiyo tungepaswa tuitumie kulihifadhi Neno la Mungu mioyoni mwetu ili Matendo chanya yaendelea kutokea ndani yetu, hatufanyi hivyo.. maandiko yanasema..
Yakobo 1:22-25
[22]Lakini iweni watendaji wa neno, wala si wasikiaji tu, hali mkijidanganya nafsi zenu.
[23]Kwa sababu mtu akiwa ni msikiaji wa neno tu, wala si mtendaji, mtu huyo ni kama mtu anayejiangalia uso wake katika kioo.
[24]Maana hujiangalia, kisha huenda zake, mara akasahau jinsi alivyo.
[25]Lakini aliyeitazama sheria kamilifu iliyo ya uhuru, na kukaa humo, asiwe msikiaji msahaulifu, bali mtendaji wa kazi, huyo atakuwa heri katika kutenda kwake.
Tuweke mfano, tunaweza kusoma kwenye biblia kwamba Upendo hauhesabu mabaya, Wala haujivuni, Wala hauoni uchungu n.k(1Kor 13).. Sasa wakati uliposoma hili neno, moyoni mwako unasema nitaliishi hili Neno, lakini inapita siku mbili unashangaa umerudia kule kule, unaanza ishi maisha ya namna Ile ya kwanza,. Tatizo lipo hapo kwenye kusahau. Laiti.hilo Neno lingekuwa limeganda viizuri kwenye moyo wako, ingekuwa breki pale tu mambo mabaya yanapojaribu kuvuka mipaka.
Sasa tunawezaje kuishinda Hali hii ya kusahau sahau?
Ni kama vile mwanafunzi darasani, mara nyingi anakuwa ni mtu wa.kurudia rudia kusoma na kufanyia sana mazoezi kile alichofundishwa..lengo la kufanya vile ni kulazimisha akili yake inakili Yale mafundisho kwa muda mrefu ili atakapoingia kwenye mtihani asisahau chochote…Lakini kama akisema Mimi ni ‘genius’ sina muda wa kurudia nilivyofundishwa..ni wazi kuwa mambo mengi yatamruka, na atafeli.
Hivyo na sisi sote ni wanafunzi wa Biblia. Soma biblia Kila siku ifanye kuwa rafiki Yako, usiwe mtu wa kusoma Leo, Tena wiki ijayo au mwezi ujao, ndio unakuja kusoma tena..SoMo tafakari mambo uliyoagizwa mule na Mungu Kila siku..Ndivyo itakavyokuwa rahisi kuliishi Neno la Mungu, kinyume na hapo usijidanganye Utasahau…kwasababu mwisho wa siku yatatoka moyoni mwako, na hivyo dhambi yoyote itakayokatisha mbele Yako, utashindwa kukabiliana nayo mapema. Mungu hapendi tuwe na tabia hii ya kusahau sahau Neno lake.
Kumbukumbu la Torati 6:6-9
[6]Na maneno haya ninayokuamuru leo, yatakuwa katika moyo wako; [7]nawe uwafundishe watoto wako kwa bidii, na kuyanena uketipo katika nyumba yako, na utembeapo njiani, na ulalapo, na uondokapo. [8]Yafunge yawe dalili juu ya mkono wako, nayo yatakuwa kama utepe katikati ya macho yako. [9]Tena yaandike juu ya miimo ya nyumba yako, na juu ya malango yako.
Piga vita kusahau Neno la Mungu.
Bwana akubariki.
Shalom.
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
Mada Nyinginezo:
Wivu ni nini na kuna aina ngapi za Wivu? Na je ni dhambi kuwa na Wivu?
Utii ni nini? na ni nani tunayepaswa kumtii au kutokumtii?
NINI MAANA YA SISI KUWA WATOTO WA MUNGU?
JE NI KUTII AU KUPATA KWANZA MAARIFA?
Karibu tujifunze biblia,
Mathayo 6:22 “Taa ya mwili ni jicho; basi jicho lako likiwa safi, mwili wako wote utakuwa na nuru.
23 Lakini jicho lako likiwa bovu, mwili wako wote utakuwa na giza. Basi ile nuru iliyomo ndani yako ikiwa giza; si giza hilo”
Umewahi kujiuliza ni kwa namna gani “Jicho” limefananishwa na “Taa ya mwili”?
Siku zote taa ikiwa inaangaza basi nyumba yote inakuwa na Nuru na ndipo vitu vyote vilivyomo ndani vinaweza kuonekana, lakini ikizima nyumba yote inakuwa giza na hakuna kitakachoonekana.
Hali kadhalika na jicho likiwa halioni, au likiwa limefumbwa basi kinachoonekana ni giza, huwezi kuona chochote, huwezi kuona mikono yako, wala miguu yako, wala kiungo kingine chochote, huwezi kuona mbele wala nyuma wala kitu kingine chochote. Kwa ufupi unakuwa ni kipofu!. Hayo ni matokeo ya jicho kuharibika!.
Sasa Bwana Yesu analinganisha Nuru iliyopo ndani yetu na jicho.. Kwamba Nuru iliyopo ndani yetu, kazi yake ni kutuongoza njia, kama vile Jicho linaloona linavyoongoza njia na kuusaidia mwili wote kusonga mbele, vile vile Nuru iliyopo ndani yetu kazi yake ni kuongoza maisha yetu katika njia sahihi.
Sasa Nuru iliyopo ndani yetu au inayopaswa uwe ndani yetu ni nini?.
Mathayo 5:16 “Vivyo hivyo NURU YENU NA IANGAZE mbele ya watu, wapate kuyaona MATENDO YENU MEMA, wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni”.
Umeona hapo?.. kumbe Nuru ni “Matendo yetu mema” .. kwamba matendo yetu yanapokuwa mema, basi ni sawa na macho yanayoona!.. Kumbe matendo yetu yakiwa mabaya sisi ni sawa na vipofu!, wala hatujui tunapokwenda!…kama Bwana Yesu alivyosema katika…
Mathayo 15:14 “Waacheni; hao ni viongozi vipofu wa vipofu. Na kipofu akimwongoza kipofu mwenzake, watatumbukia shimoni wote wawili”.
Je unataka kuona mambo yaliyopo mbele yako? na njia unayoielekea? kama ni salama?.. je! Unataka kuona hatari inayokuja na kuepukana nayo?.. Basi fanya matendo mema!!…usiende kwa waganga wala wasoma nyota wala manabii, wewe yasafishe matendo yako tu!, na utaona mambo yajayo!..
Hiyo ndio siri nyingine iliyopo nyuma ya “Matendo yetu mazuri”.. sio tu yanaupendeza moyo wa Mungu na kutupa baraka.. bali pia yanatuongoza na kutufanya tuone mambo yajayo (yaliyopo mbele yetu).
Na unayasafishaje matendo yako?.. Si kwa nguvu zako bali kwa Neema iliyopo ndani ya damu ya Yesu, ambayo hiyo inakuja kwa njia ya kutubu dhambi na kumaanisha kuziacha pamoja na kupata ubatizo sahihi..
Hapo Roho Mtakatifu ataingia ndani yako na kukupa uwezo wa wewe kufanya matendo yampendezayo Mungu, na hivyo macho yako ya kiroho yatakuwa angavu… Utakuwa na uwezo wa kuona hatari zilizopo mbele yako na kuepukana nazo, utakuwa na uwezo mkubwa wa kuona hasara zilizopo mbele yako na kuzikwepa, utakuwa unauwezo wa kuona mema yaliyopo mbele yako na kuyafuata na vile vile utakuwa na uwezo wa kuona hatari inayokufuata nyuma yako n.k
Lakini kanuni ni hiyo moja tu!..Ifanye Nuru yako (matendo yako) yaangaze!
Bwana akubariki.
Maran atha!
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
Mada Nyinginezo:
TWAENENDA KWA IMANI NA SI KWA KUONA.
Kama ulimwengu ujao utakuwa na watakatifu tu, sasa hao watakaotawaliwa watatoka wapi?
RUHUSU TOHARA IPITE JUU YA KARAMA YAKO.
ITII SAUTI ILIYOPO NYUMA YA KILA ISHARA YA MUNGU!
Mambo ya Walawi 11:9-12
[9]Katika hao wote walio ndani ya maji mtakula hawa; kila aliye na mapezi na magamba, ndani ya hayo maji, na ndani ya bahari, na ndani ya mito, mtakula hao.
[10]Na hao wote wasio na mapezi na magamba, ndani ya bahari, na ndani ya mito, katika hao waendao majini, na katika wote wenye uhai, waliomo majini, hao ni machukizo kwenu,
[11]watakuwa machukizo kwenu; msiile nyama yao, na mizoga yao itakuwa machukizo kwenu.
[12]Kila asiye na mapezi wala magamba aliye ndani ya maji ni machukizo kwenu.
Mapezi ya samaki, ni vile vitu kama mbawa ngumu zenye mfano wa miiba zinazokaa Kwa juu, au pembeni au nyuma mwa mwili wa samaki.Ukitazama samaki kama perege, sato au sangara utaona mapezi Yao.Na faida za mapezi hayo ni kuwa yanasaidia kuogelea, kuelea vema kwenye maji, kukunja Kona, kuongeza kasi na kusimama au kugeuka Kwa haraka.
Halikadhalika samaki waliokuwa na magamba ndio tu walioruhusiwa kuliwa. Na magamba yaliwasaidia kujilinda na maadui au wadudu wavamiaji kwenye mwili. Kwani ngozi ya samaki ni laini hivyo isipofunikwa na magamba magumu kama yale, meno makali ya maadui yanapopita ni rahisi kujeruhiwa, Yanakaa kama dirii kifuani mwa askari.
Lakini si samaki wote walikuwa na haya mapezi na magamba, Bali wengine hawakuwa nayo mfano wa Hawa ni kama kambale, papa, pomboo, pwezi.
Kama tunavyofahamu agano la kale ni kivuli Cha agano jipya, sio kwamba viumbe hivyo vikiliwa vitamkosesha mtu mbingu, au vitamnajisi roho , hapana. Bali vilifanywa vile kwa makusudi ili kutupitishia sisi ujumbe wa Rohoni katika agano letu jipya. Kwamba na sisi kama tutafanana na mojawapo wa viumbe hivyo Rohoni basi tunakuwa najisi mbele za Mungu.
Samaki mwenye magamba ni mwenye ulinzi wa kutosha dhidi ya mashambulizi ya maadui. Na sisi tunapokosa ulinzi wa Rohoni mfano wa yule askari anayezungumziwa katika Waefeso 6, mwenye dirii ya haki kifuani, ngao ya Imani mkononi na chepeo ya wokovu kichwani. Tunakuwa ni wadhaifu, kiasi Cha kutoweza simama mbele ya adui yetu shetani. Hivyo ni kuhakikisha kuwa umesimama imara katika wokovu wako, lakini pia utambue haki uliyopewa katika msalaba wa Yesu Kristo na Imani Yako timilifu ndani ya wokovu wako. Hapo utakuwa umejidhatiti vya kutosha mfano wa samaki mwenye gamba gumu, au mamba aliyefunikiwa na ngozi yenye gamba.
Ayubu 41:13 “Ni nani awezaye kumbambua magamba yake? Ni nani atakayepenya dirii yake maradufu? 14 Ni nani awezaye kuifungua milango ya uso wake? Meno yake yatisha kandokando yake. 15 Magamba yake yenye nguvu ndiyo fahari yake, Yamefungamana pamoja kama kwa kufungwa kwa muhuri. 16 Jinsi yalivyoshikamana Hata upepo hauwezi kupita kati. 17 Yamefungamana pamoja; Yameshikamana, hata hayawezekani kutengwa”
Vilevile samaki aliyekuwa na mapezi alikuwa ni mwepesi kukatiza katika maji. Ni sawa na mabawa Kwa ndege, au miguu na kwa mtu. Hivyo na sisi katika ulimwengu huu wa dhambi ili tusionekane kuwa najisi tuvae mapezi yetu ambayo maandiko yanasema .Ndio ule utayari wa kuihubiri injili.
Waefeso 6:15
[15]na kufungiwa miguu utayari tupatao kwa Injili ya amani;
Tusienende Kama watu wasio na kusudi maalumu la kufanya duniani, tuvae utayari, ndio mapezi yetu tutembee ulimwengu kote kiuhubiri/ kushuhudia habari njema.Kwasababu tukikosa haya, siku ile ya mwisho, tutatengwa samaki wema na waovu..Kisha wale waovu watatupwa nje.
Mathayo 13:47 ‘Tena ufalme wa mbinguni umefanana na juya, lililotupwa baharini, likakusanya samaki wa kila namna;
48 hata lilipojaa, walilivuta pwani; wakaketi, wakakusanya walio wema vyomboni, bali walio wabaya wakawatupa. 49 Ndivyo itakavyokuwa katika mwisho wa dunia; malaika watatokea, watawatenga waovu mbali na wenye haki’
Tusiwe samaki najisi.
Shalom.
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
Mada Nyinginezo:
Injili iliyopo kwa Samaki aina ya Eeli.
Pomboo ni nini katika biblia?(Kutoka 25:5, Ezekieli 16:10)
Mjombakaka ni nani kwenye maandiko? (Walawi 11:29)
Je! Ni kweli kuna samaki mtu (Nguva) Baharini.
Je! Ni dhambi kumpiga au kumuua mnyama bila sababu yoyote?
Nakusalimu katika jina la Yesu Kristo Bwana Yesu. Karibu katika kujifunza maneno ya uzima ya mwokozi wetu.
Leo tutaona jinsi “moyo wa toba ya kweli” unavyopokelewa kitofauti sana na Mungu. Kama tunavyoifahamu ile habari ya mwana mpotevu, jinsi alivyoingiwa na tamaa, ya kwenda kuanzisha maisha yake ya anasa mbali na baba yake. Na siku zilipozidi kwenda, mali zilipoisha, njaa kali ikamkuta Akaanza kula vyakula vya majalalani ambavyo viliwastahili tu nguruwe. Lakini Biblia inasema, hakung’ang’ania tu kuendelea kutaabika katika hali ile ile milele mpaka kufa kwake. Bali alijinyenyekeza akazingatia kurudi kwa baba yake akiwa na moyo wa toba, ili baba yake amfanye tu mtumwa. Na alipofanya vile, akiwa njiani anarudi, biblia inatumbia kuna tukio lilitokea.
Na tukio lenyewe ni “kuonekana kwake tokea mbali” . Tusome;
Luka 15:17 “Alipozingatia moyoni mwake, alisema, Ni watumishi wangapi wa baba yangu wanaokula chakula na kusaza, na mimi hapa ninakufa kwa njaa. 18 Nitaondoka, nitakwenda kwa baba yangu na kumwambia, Baba, nimekosa juu ya mbingu na mbele yako; 19 sistahili kuitwa mwana wako tena; nifanye kama mmoja wa watumishi wako. 20 Akaondoka, akaenda kwa babaye. Alipokuwa angali mbali, baba yake alimwona, akamwonea huruma, akaenda mbio akamwangukia shingoni, akambusu sana. 21 Yule mwana akamwambia, Baba, nimekosa juu ya mbingu na mbele yako; sistahili kuitwa mwana wako tena. 22 Lakini baba aliwaambia watumwa wake, Lileteni upesi vazi lililo bora, mkamvike; mtieni na pete kidoleni, na viatu miguuni; 23 mleteni ndama yule aliyenona mkamchinje; nasi tule na kufurahi; 24 kwa kuwa huyu mwanangu alikuwa amekufa, naye amefufuka; alikuwa amepotea, naye ameonekana. Wakaanza kushangilia”
Embu tafakari, iweje, Baba yake ndio awe wa kwanza kumwona tokea mbali na sio watumwa ambao sikuzote wao ndio wanaosimama mlangoni mwa nyumba au kuzunguka zunguka huku na huko, au kwanini isiwe hata ndugu zake wengine, badala yake baba yake ndio anayekuwa wa kwanza kumwona?
Sio kana kwamba hao wengine walikuwa hawali mboga za majani, hawaoni mbali mambo yao kuwa hafifu, hapana, bali Baba yake alikuwa na jicho lingine la rohoni kama DARUBINI. Hilo lilikuwa linaona mahangaiko, na manyanyaso ya mwanaye tokea mbali, kiasi kwamba alipofanya geuko moyoni mwake, tayari baba yake alishahisi, na akiwa njiani anakuja tayari baba yake alishajua kuwa mwanawe yupo njiani. Hivyo kabla hata mtoto hajamwona Baba, kabla hata hajaifikia nyumba yao akiwa kilomita kadhaa mbali, tayari baba alikwenda kukutana naye na kukumbatia na kumbusu sana.
Ndivyo ilivyo kwa Mungu wetu. Pale mtu anapokuwa na moyo wa toba ya kweli rohoni, haihitaji wewe kwenda kusema maneno mengi sana mbele za Mungu, kana kwamba ndio utasikiwa. Yeye anayo darubini yake, Lakini kule kuzingatia tu kurudi kwa Baba yako wa mbinguni, ukaanza kuchukua hatua. Hiyo ni toba kubwa sana ambayo itamfanya Mungu, kabla ya wewe kumfikia tayari ameshakufikia, haraka sana na kukupa tiba ya moyo wako, na raha nafsini mwako.
Hii ni kuonyesha kuwa toba ya kweli, ni ule moyo uliogeuka. Sio tu kuongozwa sala maalumu. Ndio tunajua sala ikiambatana na geuko ni vema sana, lakini ikiwa utasalishwa sala hizo elfu 10 halafu ndani yako, ni vilevile tu, hapo unapoteza muda wako ndugu.
Alikuwepo Yule mwanamke mwenye dhambi nyingi sana, alipokwenda kwa Bwana Yesu saa ile ile akaanza kulia akitubia dhambi zake, akidondosha machozi yake miguu pa Yesu, huku akiyapangusa kwa nywele zake. Lakini Yesu alipomwona akasema ‘Umesamehewa dhambi zako nyingi’, mwanamke Yule hakusalishwa sala yoyote.(Luka 7:36-50).
Ili Mungu afike kwako upesi, kuwa na toba ya kweli, ili upate kibali cha haraka kwa Mungu, sio wingi wa maombi yako, bali geuko la dhati. Na Bwana mwenyewe atakufikia kabla hujamfikia yeye.
Bwana akubariki.
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
Mada Nyinginezo:
WALA HAKUACHA MTU ACHUKUE CHOMBO KATI YA HEKALU.
Kwanini Nuhu alimlaani Kaanani badala ya mtoto wake Hamu,
UMUHIMU WA KUISHI MAISHA YAMPENDEZAYO MUNGU SASA.
MUME / MKE BORA KUTOKA KWA BWANA UTAMWONA UKIWA KATIKA MAZINGIRA GANI?
Jina la Mwokozi Mkuu Yesu Kristo libarikiwe, karibu tujifunze biblia.
Mithali 2:10 “Maana hekima itaingia moyoni mwako, Na maarifa yatakupendeza nafsi yako;
11 Busara itakulinda; Ufahamu utakuhifadhi.
Haya ni mambo manne ambayo ni muhimu sana kuwa ndani yetu.
Mambo haya manne ni Bwana pekee anayeweza kuyatoa.. Mithali 2:6 “Kwa kuwa Bwana huwapa watu hekima; Kinywani mwake hutoka maarifa na ufahamu” .
Zifuatazo ni faida kuu tatu (3) za kupata Hekima, Maarifa, ufahamu na busara.
Hii ni faida ya kwanza ya kupata Hekima, Ufahamu, busara na Maarifa; “Kumwokoa mtu na njia ya uovu”
Mithali 2:10 “Maana hekima itaingia moyoni mwako, Na maarifa yatakupendeza nafsi yako;
11 Busara itakulinda; Ufahamu utakuhifadhi.
12 ILI KUKUOKOA NA NJIA YA UOVU, Na watu wanenao yaliyopotoka;
13 Watu waziachao njia za unyofu, Ili kuziendea njia za giza;
14 Wafurahio kutenda mabaya; Wapendezwao na upotoe wa waovu;
15 Waliopotoka katika njia zao; Walio wakaidi katika mapito yao”
Njia ya Uovu ni njia yoyote ile ambayo itampelekea mtu kufanya maovu, mfano wa hayo ni yale yanayotajwa katika Wagalatia 5:19-21 “uasherati, uchafu, ufisadi, ibada ya sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, fitina, faraka, uzushi, husuda, ulevi, ulafi, na mambo yanayofanana na hayo”.
2. KUKUOKOA NA MALAYA:
Mithali 2:16 “…Ili kuokoka na malaya, Naam, malaya mwenye kubembeleza kwa maneno yake..”
Mtu aliye Malaya ni yule anayefanya uasherati aidha kwa lengo la kutafuta pesa au kujifurahisha, na hili ni neno linalotumika kuwakilisha jinsia zote mbili za watu wenye tabia hizo. Na Malaya anaweza kuwa ni mtu aliye ndani ya ndoa au nje ya ndoa.
Mtu mwenye busara (Maana yake anayeona mbele), hawezi kunaswa na mtego wa Malaya.. Mfano wa mtu aliyekuwa na busara katika biblia ambaye aliokoka na mtego wa Malaya ni Yusufu, ambaye alitegewa mtego na mke wa Potifa, lakini aliushinda mtego ule wa ibilisi.
Lakini kama Yusufu hangekuwa na Busara akilini mwake, basi angenaswa katika mtego ule wa uasherati alipobembelezwa na mke wa Potifa, na hivyo angekuwa amejiingiza katika matatizo makubwa sana, ambayo yangehatarisha hata maisha yake ya kimwili na kiroho.. kama biblia inavyosema hapa..
Mithali 2:16 “Ili kuokoka na malaya, Naam, malaya mwenye kubembeleza kwa maneno yake;
17 Amwachaye rafiki wa ujana wake, Na kulisahau agano la Mungu wake.
18 Maana nyumba yake inaelekea mauti, Na mapito yake yanakwenda kwenye wafu.
19 Katika hao wamwendeao harudi hata mmoja, Wala hawazifikilii njia za uzima”
Soma tena maandiko mengine yanayohusu tabia za Malaya, jinsi anavyobembeleza katika Mithali 7:7-23, Mithali 22:14 na Mithali 23:27.
Ukiona mtu kanaswa na mtego basi ni matokeo ya kupungukiwa Hekima, busara, maarifa na ufahamu.. kama biblia inavyosema katika Mithali 6:32 “Mtu aziniye na mwanamke hana akili kabisa; Afanya jambo litakalomwangamiza nafsi yake” .Kwasababu mtu aliyejaa mambo hayo hawezi kunaswa na mitego hiyo.
3. KUKUPELEKA KATIKA NJIA YA WATU WEMA
Faida ya kwanza tuliona ni “kumwokoa mtu katika njia ya uovu” lakini Hii ya tatu na ya mwisho, ambayo ni “Kukupeleka mtu katika njia ya watu wema”.. Hekima, busara, Maarifa na ufahamu haviishii tu kumwokoa mtu na njia mbaya na kumwacha hapo katikati bali pia kumpeleka/kumwongoza katika njia nzuri.
Mithali 2:20 “Ili upate kwenda katika njia ya watu wema, Na kuyashika mapito ya wenye haki.
21 Maana wanyofu watakaa katika nchi, Na wakamilifu watadumu ndani yake.
22 Bali waovu watatengwa na nchi, Nao wafanyao hila watang’olewa”.
Watu wema wana Njia yao, wapo katika mkondo wao, si kila mahali wanapita, na hao ndio wanaodumu katika nchi, … Sasa ili kuiona hiyo njia waliyopo basi Hekima, Busara, Maarifa na ufahamu vinahitajika. Na vyote hivyo vinatoka kwa Mungu.
Sasa swali? Mtu anapataje Hekima, Ufahamu, Busara na Maarifa ili kuepukana na hayo yote, na kupata faida hizo.
Tukitaka Hekima, Maarifa, Ufahamu na Busara biblia imetupa kanuni rahisi katika kitabu cha Ayubu.
Ayubu 28:20 “Basi hekima yatoka wapi? Na mahali pa ufahamu ni wapi?
21 Kwa kuwa imefichwa mbali na macho ya wote walio hai, Na kusitirika na ndege wa angani.
22 Uharibifu na Mauti husema, Tumesikia habari zake kwa masikio yetu.
23 Mungu ndiye aijuaye njia yake, Naye anajua mahali pake.
24 Maana anatazama hata miisho ya nchi, Na kuona chini ya mbingu nzima.
25 Apate kuufanyia upepo uzito wake; Naam, anayapima maji kwa kipimo.
26 Hapo alipoiwekea mvua amri, Na njia kwa umeme wa radi.
27 Ndipo alipoiona na kuitangaza; Aliithibitisha, naam, na kuichunguza.
28 Kisha akamwambia mwanadamu, Tazama, KUMCHA BWANA NDIYO HEKIMA, NA KUJITENGA NA UOVU NDIO UFAHAMU”.
Kumcha Bwana na kuepukana na Uovu ndio chanzo cha Hekima, maarifa, busara na ufahamu.
Maana yake Jishughulishe sana na masuala ya kiMungu sana, Jifunze Neno la Mungu, kusanyika na wengine katika maombi, ibada na kufanya uinjilisti na mambo mengine yote yanayofanana na hayo, kwa kufanya hivyo ndivyo Hekima, na hayo mambo mengine yatakayoingia ndani yako na kujaa.
Maran atha!
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
Mada Nyinginezo:
HEKIMA NI NINI? NA UFAHAMU UNAPATIKANA WAPI?
Bali mke mwenye busara, mtu hupewa na Bwana.
Mjombakaka ni nani kwenye maandiko? (Walawi 11:29)
Nini maana ya “Mwenye hekima huvuta roho za watu”
Nakusalimu katika jina kuu la Bwana wetu Yesu Kristo. Nakukaribisha tuyatafakari maneno ya uzima ya Bwana wetu.
Leo nataka tujifunze asili ya ushujaa wa rohoni, ambao wakati mwingine tunadhani mpaka tuwe na uzoefu ndio tuweze kufanya makuu kwa Mungu. Wakati Fulani Taifa la Israeli liliingia katika hali mbaya ya njaa isiyokuwa ya kawaida, mpaka kufikia hatua ya baadhi ya watu kuchinja watoto wao na kuwala (2Wafalme 6:28-29), Na hiyo ilikuwa ni kwasababu ya kuzungukwa na maadui zao wenye nguvu kwa muda mrefu walioitwa washami. Hivyo wakashindwa kuingiza au kutoa chochote ndani ya mji kwa muda usiokuwa mchache.
Hivyo hali ikiwa mbaya sana, mfalme akafunga mji, hawajui cha kufanya, watu wamepaniki, wanakula vitu visivyopaswa kulikwa, kiasi kwamba hata ‘mavi ya njiwa’ tu yalikuwa yanauzwa kama chakula. Tengeneza picha taifa kubwa kama hilo, linakumbwa na janga la njaa kali namna hiyo, hadi askari wake wazoefu wa vita, wanatetemeka na kujificha ndani ya mji, kwasababu walijua wakitoka tu ni kifo.
Na ndicho maadui zao walichokuwa wanakisubiria kwao, aidha watoke wawaue, au wafe na njaa ndani. Hivyo hali ilikuwa ni ya kutisha sana. Lakini tunaona siku moja Nabii Elisha, akapewa unabii na Mungu, na kuambiwa kuwa chakula kitapatikana na kuuzwa kwa bei ya chini kiasi ambacho hakijawahi kuuzwa hapo kabla siku ya kesho yake, ni sawa na uambiwe siku ya kesho, gunia la mahindi, linauzwa kwa Tsh1, wakati unatambua kuwa halipungui wastani wa bei ya Tsh,70,000. Ndivyo ilivyokuwa kwa Israeli, Mungu alipompa Elisha unabii huo akaambiwa siku ya kesho yake, chakula kitauzwa kwa bei ile.
Sasa kulikuwa na wakoma wanne(4), waliokuwa nje ya mji, wakoma hawa walitengwa na taifa, kwasababu ilikuwa ni kuwa watu walioathirika na ugonjwa huu watengwe mbali na makazi ya watu wao wasije kuleta maafa hayo ndani ya jamii, ni sawa na ugonjwa wa Ebola tunavyouona sasa, ndivyo ilivyokuwa ukoma kwa wakati ule.
Tengeneza picha watu hawa walikuwa ni wagonjwa, hawana wa kuwatazama, na zaidi sana wamekuwa dhaifu kwa njaa kali. Lakini tunaona walishauriana jambo kisha wakafanya maamuzi, ambao ndio ulikuwa ukombozi wa taifa la Israeli; Tusome hapo;
2Wafalme 7:1 Elisha akasema, Lisikieni neno la Bwana; Bwana asema hivi, Kesho panapo saa hii, kipimo cha unga mzuri kitauzwa kwa shekeli, na vipimo viwili vya shayiri kwa shekeli, langoni pa Samaria.
2 Basi yule akida, ambaye mfalme alikuwa akitegemea mkono wake, akamjibu yule mtu wa Mungu, akasema, Tazama, kama Bwana angefanya madirisha mbinguni, je! Jambo hili lingewezekana? Akamwambia, Angalia, wewe utaliona kwa macho yako, lakini hutakula
3 Basi walikuwapo watu wanne wenye ukoma, penye lango la mji; wakasemezana, Mbona tunakaa hapa hata tufe?
4 Tukisema, Tutaingia mjini, mjini mna njaa, nasi tutakufa humo; nasi tukikaa hapa, tutakufa vile vile. Haya! Twende tukaliendee jeshi la Washami; wakituhifadhi hai tutaishi; wakituua, tutakufa tu.
5 Basi wakaondoka kabla ya mapambazuko, ili waende mpaka kituo cha Washami; na walipofika mwanzo wa kimo cha Washami, kumbe! Hapana mtu.
6 Kwa maana Bwana alikuwa amewasikizisha Washami kishindo cha miendo ya magari, na kishindo cha farasi, kama kishindo cha jeshi kubwa; wakaambiana, Tazama, mfalme wa Israeli amewaajiri wafalme wa Wahiti, na wafalme wa Wamisri, waje wapigane nasi.
7 Kwa hiyo wakaondoka, wakakimbia kungali giza bado, wakaziacha hema zao, na farasi zao, na punda zao, na kimo chao vile vile kama kilivyokuwa, wakakimbia wapate kujiponya nafsi zao.
8 Basi wale wenye ukoma walipofika mwisho wa kituo, waliingia katika hema moja, wakala, na kunywa, wakachukua fedha, na dhahabu, na mavazi, wakaenda wakavificha; wakarudi, wakaingia katika hema ya pili, vile vile wakachukua vitu, wakaenda, wakavificha.
9 Ndipo wakaambiana, Mambo haya tufanyayo si mema; leo ni siku ya habari njema, na sisi tunanyamaza; mkingoja hata kutakapopambazuka, madhara yatatupata; basi twende tukawaambie watu wa nyumba ya mfalme.
10 Basi wakaenda, wakawaita mabawabu wa mji; wakawaambia, Tulifika kituo cha Washami, na tazama, hapana mtu ye yote huko, wala sauti ya mtu, ila farasi wamefungwa, na punda wamefungwa, na hema zao kama walivyoziacha.
11 Na mabawabu wakaita wakawaambia watu wa nyumba ya mfalme.
Ni nini kimejificha hapa?
Siri nayotaka uone ambayo imejificha nyuma ya hawa wakoma wanne, ni kwamba, pindi tu walipoamua kufanya uamuzi, wa kujitoa muhanga kwa ajili ya maisha yao, na kuanza mwendo, kuelekea kambi ya maadui, kumbe kule kwenye kambi ya washami, wanasikia kama JESHI kubwa sana la maaskari linawafuata. Hivyo wakakimbia kwa kasi sana, na kuacha kila kitu nyuma. Lakini wale maaskari wa kiisraeli waliokuwa wazoefu wakati huo wamejifungia ndani ya mji hawadhubutu kuchukua hatua..
Watu waliokuwa dhaifu na wagonjwa, ndio waliowafukuza washami na kuleta ukombozi Israeli. Watu wanne tu, waligeuka kuwa jeshi la maaskari elfu rohoni.
Hiyo ni kutufundisha nini?
Na sisi pia pale tunapoamua kufanya jambo kwa ajili ya Mungu, bila kujali hali zetu au udhaifu wetu, tufahamu kuwa jeshi la shetani linaogopa na kutetemeka kushinda hata sisi tunavyoweza kudhani. Daudi alijijua kuwa yeye si mtu wa vita, hajazoea vita, hawezi kutumia upanga wala mkuki, lakini yeye ndiye aliyesimama, kinyume na Goliathi, na kulifukuza jeshi lake lote.
Hivyo, hupaswi kujidharau, ikiwa umeokoka leo, au jana, usiseme mimi sina uzoefu, au sijui biblia vizuri, kama kushuhudia watu wenye dhambi ambao wengine wameshindwa, wewe nenda, usisubiri mpaka mchungaji wako afanye hivyo, hujui kuwa wakati huo ndio Mungu kakuchagua kuwa sababu ya ukombozi kwa wengine.
Hivyo, popote unapojiona hukidhi vigezo, fahamu kuwa rohoni ndio unakidhi. Unajiona hustahili, jua tu kwa Mungu unastahili, kuwa na imani, chukua hatua, usingoje ngoje. Tumia karama uliyopewa ndani yako kuujenga ufalme wa Mungu. Popote pale unapojiona unafaa, basi tumia nafasi hiyo kumtangaza Kristo kwa wengine. Na hakika rohoni shetani atatoweka kama jeshi la washami.
Bwana akubariki.
Shalom.
Je, umeokoka? Kama bado basi fungua hapa kwa ajili ya mwongozo huo wa kumwalika Yesu maishani mwako.
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Mada Nyinginezo:
Hazina za gizani ni zipi? (Isaya 45:3).
BWANA AWEZA KUKUPA ZAIDI SANA KULIKO HIZO.
YANAYOENDELEA SASA KATIKA MADHABAHU YA MUNGU ROHONI.
JINSI YA KUPIGANA MAOMBI YA VITA.
Karibu tujifunze biblia.
Leo tutajifunza moja ya taratibu illiyokuwa inaendelea katika Hekalu la Mungu ambayo haikuwa inampendeza Mungu.
Tusome,
Marko 11:15 “Wakafika Yerusalemu, naye akaingia ndani ya hekalu, akaanza kuwafukuza wale waliokuwa wakiuza na kununua ndani ya hekalu, akazipindua meza za wabadili fedha, na viti vyao wauzao njiwa;
16 WALA HAKUACHA MTU ACHUKUE CHOMBO KATI YA HEKALU”.
Maandiko haya ni maarufu tunapoyasoma husuani mahali hapo Bwana alipowafukuza waliokuwa wanauza njiwa na waliokuwa wanabadili fedha.
Lakini tukizidi kujifunza, tutaona sio kundi hilo tu Bwana alilolifukuza na kuliadhibu. Bali kulikuwa na kundi lingine pia ambalo lilikuwa linapandisha harufu mbaya mbele za Mungu. Na kundi hilo ni lile la watu waliokuwa WANACHUKUA CHOMBO NDANI YA HEKALU.
Sasa kuchukua Chombo kunakozungumziwa hapo si “KUIBA VYOMBO VYA HEKALUNI au KUHAMISHA CHOMBO NDANI YA HEKALU” Hapana! Bali ni KUPITA au KUKATISHA na Chombo ndani ya Hekalu, Na chombo ni kitu chochote cha kubebea bidhaa au kurahisisha kazi kama makapu, au matenga au baiskeli.
Sasa mahali hekalu lilipojengwa lilikuwa linatengenisha sehemu mbili, sehemu ya kwanza ni Bethsaida (mahali palipokuwa na soko kubwa la kondoo) na Sehemu ya juu ya “Mji wa juu”. Hivyo watu waliotoka Mjini kuelekea Bethsaida sokoni walianza tabia ya kukatiza katika ukumbi wa hekalu kama njia ya mkato (shortcut) ya wao kufika Bethsaida.
Kwahiyo kulikuwa na kundi kubwa la watu wanaokatiza pale wakiwa na vyombo vyao kila siku, Kwaufupi paligeuzwa kuwa njia, mtu yeyote alipita, wezi walikatiza, wahuni walipita, wasengenyaji walikatiza na stori zao za kuwasema wengine, waliotaka kwenda sokoni kuweka vimeza vya Kamari walikatiza kila siku na meza zao, matapeli ndio shortcut yao hiyo n.k
Tabia ambayo Bwana Yesu hakupendezwa nayo!. Hivyo akasimama pia katika maingilio na matokeo ya Hekalu akawazuia wote waliokuwa wanakatiza!.. Huenda pia nao walitandikwa na kile kikoto!!.
Sasa tabia kama hiyo pia inaendelea katika nyumba za Mungu leo (Makanisani), utakuta kuna miingiliano ya watu wanaokatiza katiza na wanaozunguka zunguka!, wasio na fikra habari na mambo ya kiMungu… Wengi wa hao hawapiti kwa lengo la kumsogelea Mungu bali kwasababu ya shughuli zao, na biashara zao na ajenda zao, wanaouza chakula wanaingia wanavyotaka, wanaouza viatu wanaingia wanavyotaka, watoto wanaotaka kucheza kutoka huko nje basi eneo la kanisa ndio ukumbi wao n.k.. ni muhimu kuwa makini sana!!
Ni lazima, kuifanya Nyumba ya Mungu kuwa nyumba ya Mungu… kama tu sisi hatupendi watu wakatize kwenye maeneo ya Nyumba zetu, tena tunawaza wakati mwingine tuzungushe uzio vipi kwa Mungu??. Kama tu sisi tunapenda watu waziheshimu nyumba zetu vipi kwa Mungu?..
Na pia nyumba ya Mungu si jengo tu bali pia miili yetu, maandiko yanasema miili yetu ni hekalu la Roho Mtakatifu (1Wakorintho 3:16, na 1Wakorintho 6:19). Ikiwa na maana kuwa pia miili yetu sio NJIA YA KILA MTU KUKATIZA!!!!.. (Maana yake si chombo cha zinaa wala kuchezewa).
1Wakorintho 6:15 “Je! Hamjui ya kuwa miili yenu ni viungo vya Kristo? Basi nivitwae viungo vya Kristo na kuvifanya viungo vya kahaba? Hasha!
16 Au hamjui ya kuwa yeye aliyeungwa na kahaba ni mwili mmoja naye? Maana asema, Wale wawili watakuwa mwili mmoja.
17 Lakini yeye aliyeungwa na Bwana ni roho moja naye.
18 Ikimbieni zinaa. Kila dhambi aitendayo mwanadamu ni nje ya mwili wake; ila yeye afanyaye zinaa hutenda dhambi juu ya mwili wake mwenyewe”.
Itunze na kuiheshimu nyumba ya Mungu (Mwili wako mwenyewe pamoja na Jengo unalokusanyikia).
Bwana akubariki.
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Mada Nyinginezo:
NI NANI ALIYEKUPA MAMLAKA HII UYATENDE HAYA?
TOFAUTI KATI YA HEKALU, SINAGOGI NA KANISA NI IPI?
Mlango uitwao “Mzuri” Unaozungumziwa katika Matendo 3:2 ndio upi?
Ni nani aliyemshawishi Daudi akawahesabu Israeli? Ni Mungu au shetani?
Hii ni Orodha ya Mitume 12 wa Bwana YESU.
Orodha hii inapatika katika Kitabu cha Mathayo 10:2-4, na kitabu cha Marko 3:18, na Luka 6:13-16.
Katika Vitabu hivyo inaonekana Mitume kutajwa kwa jina Zaidi ya Moja katika injili nyingine, kwamfano Mtume aliyeitwa Thadayo (Mathayo 10:3), kitabu cha Luka 6:16 anaonekana akitajwa kama “Yuda wa Yakobo”, Hiyo ni kuonyesha kuwa Mtume huyo alikuwa anajulikana kwa jina Zaidi ya moja. Vile vile Mtume anayeonekana kuitwa Nathanaeli katika Yohana 1:45 ndio huyo huyo anayekuja kuonekana akiitwa kwa jina la Bartholomeo katika Mathayo 10:3.
Lakini pia baada ya Yuda kumsaliti Bwana na kwenda kujinyonga, maandiko yanaonyesha kuwa Mtu aliyeitwa Mathiya alichukua nafasi yake na kuhesabiwa miongoni mwa mitume 11 wa Bwana Yesu.
Matendo 1:26 “Wakawapigia kura; kura ikamwangukia Mathiya; naye akahesabiwa kuwa pamoja na mitume kumi na mmoja”.
Hiyo ndiyo Orodha ya Mitume 12 wa Bwana Yesu Kristo, ambao Bwana aliwaweka kuwa kama Mashahidi wa kufufuka kwake (Matendo 10:39-42 na Matendo 1:22), na baada ya hawa Bwana alinyanyua mitume wengine mfano wa hawa, ambao miongoni mwao alikuwa Mtume Paulo.
Na Mitume wanatajwa katika Agano jipya tu na wao ndio walioweka msingi wa Imani kwa kanisa, katika Agano la kale walioweka msingi wa kumjua Mungu kama Yehova ni Manabii, hivyo kwa muunganiko wa Mafunuo waliopewa Mitume wa agano jipya na Manabii wa agano la kale, kanisa la Kristo linajegwa juu ya Msingi wao.
Waefeso 2:20 “Mmejengwa juu ya msingi wa mitume na manabii, naye Kristo Yesu mwenyewe ni jiwe kuu la pembeni”.
Je unajua jinsi Bwana alivyowachagua Mitume wake? na ni kigezo gani alikitumia?.. kufahamu zaidi fungua hapa >>JINSI BWANA ALIVYOWACHAGUA MITUME WAKE.
Bwana akubariki.
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Mada Nyinginezo:
Je ni kweli Tumejengwa juu ya Mitume na Manabii? (Waefeso 2:20)
Orodha ya mistari ya biblia kuhusu watoto
ORODHA YA IMANI POTOFU- Sehemu ya 1
Jina la Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo libarikiwe, karibu tujifunze biblia Neno la Mungu wetu lililo taa ya miguu yetu na mwanga wa njia yetu. (Zab. 119:105).
Kuna tofauti ya Msamaha wa dhambi na Ondoleo la dhambi.
Mtu anapokukosea labda amekutukana au kukuibia na akikuomba msamaha unaweza kumsamahe (ukamwachilia kabisa moyoni mwako) lakini kumsamehe kwako hakumfanyi yeye kuacha ile tabia.. Maana yake ni kwamba kama ile tabia haitaondoka ndani ya huyo mtu basi ni wazi kuwa atarudia lile kosa siku nyingine. Atapumzika siku mbili au tatu na baadaye atarudia lile kosa. Sasa mtu kama huyu kapata msahama lakini si ondoleo la ile tabia.
Vile vile kwa Mungu tunaweza kupata msamaha wa makosa yetu na dhambi zetu, lakini kama hatutapata Ondoloe la dhambi hizo (Maana yake kama ule mzizi wa dhambi ndani yetu hautang’olewa) basi tutabaki vile vile, kila mara tutarudia makosa yale yale. Na mzizi wa dhambi ni lazima uondoke maishani mwetu kwasababu ndicho kitu kilichomleta Bwana Yesu duniani.
Bwana Yesu hakuja tu kuleta msamaha wa dhambi bali pia ondoleo la dhambi..Kwasababu msamaha wa dhambi ulikuwepo hata kabla ya Bwana Yesu kuja duniani, watu waliomba msamaha mbele za Mungu na wakasamehewa makosa yao, lakini Ondoleo la dhambi halikuwepo, Dhambi hazikuondolewa katika kumbukumbu za Mungu (zilifunikwa tu) na vile vile hazikuondolewa ndani ya mtu, bado watu waliendelea kurudia makosa yale yale, baada ya Bwana Yesu kuja watu ndipo wakapata ondoleo la dhambi, ndani yao (utumwa wa dhambi ukakoma kwa wale wote waliompokea).
Sasa tunapataje ondoleo la dhambi?.. kiasi kwamba dhambi haitupelekeshi tena wala kututawala?
Kwanza ni kwa kutubu mbele za Mungu, na kukiri kwamba sisi ni wakosaji, (hapa unatubia makosa yako yote ambayo umeyafanya kwa kujua, na kwa kutokujua mbele za Mungu, kwa tendo hilo Bwana atakusamehe ikiwa toba hiyo imetoka kweli ndani ya moyo na kwamba umekusudia kubadilika kabisa..)
Sasa hatua inayofuata ili Dhambi zako ziondolewe (ule mzizi wa dhambi ndani yako uondoke) baada ya kutubu ni wewe kwenda kubatizwa katika ubatizo sahihi… Hiki ni kipengele cha muhimu sana ambacho si cha kupuuzia hata kidogo..
Matendo 2:37 “Walipoyasikia haya wakachomwa mioyo yao, wakamwambia Petro na mitume wengine, Tutendeje, ndugu zetu?
38 Petro akawaambia, TUBUNI MKABATIZWE KILA MMOJA KWA JINA LAKE YESU KRISTO, MPATE ONDOLEO LA DHAMBI ZENU, NANYI MTAPOKEA KIPAWA CHA ROHO MTAKATIFU”
Ubatizo sahihi unakamilisha toba na hivyo mtu anayefanya hayo Mungu anampa zawadi ya Roho Mtakatifu pamoja na Ondoleo la dhambi, jambo ambalo ni muhimu sana.
Mtu huyu kama toba yake imetoka ndani ya moyo kabisa basi ule uzinzi uliokuwa unamsumbua mara kwa mara unakufa, anajikuta anaushinda uasherati na haurudii tena, kwasababu dhambi imeondolewa ndani yake, zile tabia zilizokuwa zinamwendesha mara kwa mara zinaondoka ndani yake kwasababu ule mzizi wa dhambi umeondolewa ndani yake n.k n.K
Na kumbuka ni muhimu sana kubatizwa ubatizo ulio sahihi, kwasababu si kila batizo zinaondoa dhambi.. nyingine utabatizwa lakini utabaki vile vile. Na ubatizo sahihi ni ule wa maji mengi (Yohana 3:23) na kwa jina la Bwana Yesu Kristo (Matendo 19:10)!.
Je unataka usiendelee kuwa mtumwa wa dhambi?.. Tumia kanuni hiyo ya Matendo 2:27-37. Na Mungu ni mwaminifu atafanya sawasawa na Neno lake.
Maran atha.
Ikiwa hujabatizwa bado na unahitaji msaada wa kupata ubatizo sahihi, basi waweza kuwasiliana nasi kwa namba zetu na tutakusaidia kwa hilo.
Shalom
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
Mada Nyinginezo:
AGIZO LA TOBA LINAENDANA NA UBATIZO!.