Jina la Bwana Yesu libarikiwe, karibu tujifunze biblia, Neno la Mungu wetu.
Leo tutajifunza, mambo Matatu ambayo, kama Mkristo ukiyarekebisha hayo basi uchumi wako utaimarika zaidi.
1. KUWA MWAMINIFU KWA MUNGU WAKO.
Dawa ya kwanza ya mafanikio yoyote yale, yawe ya kimwili au kiroho, ni kuwa MWAMINIFU KWA BWANA.
Mithali 3:7
“ Usiwe mwenye hekima machoni pako;
Mche BWANA, ukajiepushe na uovu.8 Itakuwa afya mwilini pako,
Na mafuta mifupani mwako.
Kumcha Bwana ni kuishi maisha matakatifu na yanayompendeza yeye, ambayo Nuru yako inakuwa inaangaza kila mahali.
Jambo moja kubwa wakristo wengi wasilolijua ni kwamba, tumewekwa ulimwenguni ili tuhubiri injili, licha ya kwamba Mungu anataka sisi tupate faida katika mambo yetu kutoka kwake, lakini pia Mbingu inategemea kupata faida kutoka kwetu.. Na faida yenyewe ni sisi kuwavuta wengine waingie katika ufalme.
Kwahiyo maana yake ni kwamba kama wewe unafanya biashara, au kazi yoyote ya kuajiriwa au kujiajiri.. Mungu anategemea maisha yako yawe sababu ya kuwavuta wengine.
Hivyo Bwana akikuamini, atakuvutia watu wengi kwako, kama ni wateja au watu wa fursa wakujie, lengo si tu waje kununua bidhaa zako, au kukupa wewe fursa, bali Mungu anawasogeza kwako ili wapate kuiona nuru yako na wamgeukie Mungu na kutubu..Hivyo wewe unafanyika daraja la wao kumfikia Mungu zaidi.
Lakini kama wewe maisha yako hayana ushuhuda wowote,maana yake ni maisha ya uzinzi, ya wizi, ya ulevi, utukanaji, umbea, usengenyaji n.k.
maana yake Mungu akikuletea watu, ni sawa na kampelekea shetani kondoo..Hivyo ili awalinde watu wake wasizidi kupotea, anazuia wateja wasije kwako, kwasababu utawaharibu kwa tabia zako..na Mungu hapendi watu wake wapotee.
Atawazuia wasije kwako, na atawapeleka kwa watu wengine wenye staha zaidi..Huku nyuma wewe utabaki kufikiri umelogwa, kumbe ni wewe mwenyewe umejiharibu kwa kutokuwa mwaminifu kwa Mungu wako.
Mathayo 5:14
“Ninyi ni nuru ya ulimwengu. Mji hauwezi kusitirika ukiwa juu ya mlima.15 Wala watu hawawashi taa na kuiweka chini ya pishi, bali juu ya kiango; nayo yawaangaza wote waliomo nyumbani.
16 Vivyo hivyo nuru yenu na iangaze mbele ya watu, wapate kuyaona matendo yenu mema, wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni”.
Angaza Nuru yako ili milango ifunguke.
2. KUWA MWAMINIFU KATIKA KAZI UNAYOIFANYA.
Hili ni jambo la pili ambalo, ni muhimu kulijua.
Wengi wetu hatujui kuwa Mungu si Mungu wa kuwadhuru watu, bali wa kuwapatia watu mema.. Mteja yeyote Mungu anayemleta kwako, ni kwasababu Mungu anataka apate huduma bora ya viwango, ili aweze kumshukuru Mungu baada ya hapo, na Mungu apokee shukrani zake..
lakini hawezi kumleta kwako wewe unayeuza kitu kilichoisha muda wake wa matumizi (kime-expire). Hapo Mungu atakuwa muuaji na mkatili na si Mungu mwenye fadhili..
Alisema..
Mathayo 7:9
“9 Au kuna mtu yupi kwenu, ambaye, mwanawe akimwomba mkate, atampa jiwe?10 Au akiomba samaki, atampa nyoka?
11 Basi ikiwa ninyi, mlio waovu, mnajua kuwapa watoto wenu vipawa vyema, je! Si zaidi sana Baba yenu aliye mbinguni atawapa mema wao wamwombao?”
Hiyo ndio maana watu wateja hawawezi kuja kwako, kwasababu Mungu hawezi kuwaongoza watoto wake kwenda kula sumu, au vitu vilivyo chini ya ubora..vinginevyo atakuwa mwongo hapo aliposema.. “Basi ikiwa ninyi, mlio waovu, mnajua kuwapa watoto wenu vipawa vyema, je! Si zaidi sana Baba yenu aliye mbinguni atawapa mema wao wamwombao?”.
Hebu tengeneza picha wewe umeamka asubuhi, na kumwomba Baba akulinde na yule mwovu na pia akupe riziki njema..halafu unatoka hapo Mungu anakuongoza kwenda kununua Soda iliyo-expire! Kwenye duka la mtu fulani…huyoo Mungu si atakuwa mkatili sana?..
Hivyo ili Mungu kumpa mtoto wake kipawa chema sawasawa na Neno lake hilo, atamwepusha kuja kwenye duka lako, au kukupa wewe ajira..badala yake anampeleka kwenye duka lingine au kumpa mtu mwingine ajira ambaye atatoa huduma iliyo bora na kuleta faida katika ufalme wa mbinguni.
Hiyo ndio sababu wakristo wengi Mungu anaifunga milango ya riziki katika biashara zao, au katika mambo yao mengine na kuishia kudhani wamelogwa, na kuzunguka huku na huko kutafuta maombezi kumbe ni kwasababu wao wenyewe sio waaminifu katika kazi zao na hawatoi huduma iliyo bora!.
Na vile vile kuwa mwaminifu katika kumtolea Mungu, maandiko yanasema wote wasiomtolea Mungu zaka ni wezi, wanamwibia Mungu..hivyo Mungu hawezi kuwabariki wezi.
Malaki 3:8 “Je! Mwanadamu atamwibia Mungu? Lakini ninyi mnaniibia mimi. Lakini ninyi mwasema, Tumekuibia kwa namna gani? Mmeniibia zaka na dhabihu.
9 Ninyi mmelaaniwa kwa laana; maana mnaniibia mimi, naam, taifa hili lote”
Mithali 3:9 “Mheshimu BWANA kwa mali yako,Na kwa malimbuko ya mazao yako yote.
10 Ndipo ghala zako zitakapojazwa kwa wingi, Na mashinikizo yako yatafurika divai mpya”.
3. IMARISHA KAZI YAKO, AU UJUZI WAKO.
Hili ni jambo lingine pia la muhimu kujua.
Wengi wetu hatupendi kuziimarisha kazi zetu, au ni walegevu katika kuziimarisha, wakati mwingine tukidhani si mpango wa Mungu.
Lakini leo nataka nikuambie kuwa kuiimarisha kazi yako, ni jambo la muhimu sana na la kimaandiko.
Kila siku buni na tafuta mbinu mpya na ongeza ujuzi katika shughuli unayojishughulisha nayo au unayoifanya..hayo ni mapenzi ya Mungu pia!
Bwana Mungu baada ya kuimaliza kazi yake ya uumbaji pale Edeni, alipumzika, lakini baada ya kipindi fulani alinyanyuka tena na kusema..”Si vyema mtu huyu awe peke yake nitamfanyizia msaidizi wa kufanana naye”.Ndipo akamletea Hawa kama msaidizi.
Kadhalika na sisi hatuna budi kusema siku zote “si vyema kazi hii ikabaki yenyewe, basi niongeze nyingine kama hii, na nyingine na nyingine”.
Si vyema kazi hii iwe kama ilivyokuwepo mwaka jana, basi nitaiimarisha hivi na hivi..si vyema ujuzi huu nilionao nikaendelea nao, basi nitauongeza tena na tena..
Kwa kufanya hivyo, Bwana atakubariki kwasababu na yeye pia anafanya matengenez kila siku katika maisha yetu.
Haya ndiyo mambo makuu matatu yanayozuia uchumi wetu kusonga mbele.
Na yaliyo ya muhimu zadi ni hayo mawili ya kwanza.
Tofauti na wengi wanaofikiri kwamba matatizo mengi yanasababishwa na uchawi.
Uchawi wa kwanza shetani anaologa nao mtu sio kuifanya biashara yake isifanikiwe..anachokifanya cha kwanza, na tena anakifanya kwa bidii ni kumfanya MTU AWE MTENDA DHAMBI!.
Kwasababu anajua Dhambi ndio mzizi na chanzo chaatatizo yote na shida na dhiki.
Mtu aliyejitenga na dhambi kamwe shetani hamwezi, na wala hakuna uchawi mwingine wowote utakaoweza kufanya kazi juu yake.
Lakini kama mtu hajajitenga na dhambi, basi uchawi mwingine wowote utafanya kazi juu yake na kumletea madhara.
Swali ni je?
WEWE NI MWAMINIFU KWA MUNGU?…NA JE! NI MWAMINIFU KATIKA KAZI YAKO?..NA JE UMEJITENGA NA DHAMBI?
Kumbuka hakuna mtu yeyote kwa nguvu zake anaweza kuishinda dhambi, Bali tunaishinda dhambi kwa Kumwamini kwanza Bwana Yesu, kwamba yeye ni Bwana na Mwokozi na anaweza kutusamehe dhambi zetu na kutuosha..
Kwa kumwamini huko, na kubatizwa basi yeye mwenyewe anaingia ndani yetu, na kutupa huo UWEZO WA KIPEKEE WA KUSHINDA DHAMBI, ambao unatufanya kuwa Wana wa Mungu.
Yohana 1:12 “ Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu, ndio wale waliaminio jina lake”.
Uwezo huo unatufanya tuwe watu wengine tofauti na tulivyokuwa hapo kwanza..Ndio hapo zile pombe tulizokuwa hatuwezi kuziacha ghafla tunajikuta tunaweza kuziacha, ule uasherati tuliokuwa tunaona ni mgumu kuuacha tunajikuta tunaushinda, yale matusi ambayo tulikuwa tunaona ni mepesi kuyatamka ulimini mwetu tunajikuta hatuyatoi tena vinywani mwetu n.k.
Bwana atubariki.
Maran atha!
Jiunge na magroup yetu ya whatsapp kwa kubofya hapa > Group-whatsapp
Tafadhali washirikishe na wengine habari
hizi njema,
Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
Jiunge na kundi letu la mafundisho ya Biblia whatsapp kwa kubofya hapa > Group-whatsapp
Mada Nyinginezo:
Lumbwi ni jina lingine la mnyama anayeitwa KINYONGA.
[29]Tena katika vitu vile vitambaavyo, vitambaavyo juu ya nchi, hivi ni najisi kwenu; kicheche, na panya, na mjombakaka, kwa aina zake,[30]na guruguru na kenge, na mjusi na goromoe, na lumbwi.[31]Wanyama hao ndio walio najisi kwenu katika hao watambaao; awaye yote atakayewagusa, wakiisha kufa, atakuwa ni najisi hata jioni.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,
Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.
Mada Nyinginezo:
Biblia inamaanisha nini inaposema “Mwenye haki huufikiri uhai wa mnyama wake”?
Ni kweli mizimu ipo?, Na tunawezaje kujihadhari nayo?.
Katika tafsiri inayojulikana na wengi ni kwamba Mzimu/Mizimu ni roho za watu waliokufa ambazo zinaweza kurudi na kuwatokea wengi.
Roho hizo zinaweza kurudi zenyewe au kurudishwa na mtu, kwa lengo fulani, aidha kutatua tatizo lililoshindikana katikati ya mtu au jamii ya watu, au kujilipiza kisasi kwa mambo aliyofanyiwa mtu huyo kabla ya kufa.
Lakini je! Kibiblia MIZIMU ni kweli ipo?
Jibu ni la! Hakuna roho yoyote ya mtu aliyekufa, inayoweza kurudi yenyewe au kurudishwa na mtu, na kisha kutatua jambo fulani la kimaisha.
Jambo hilo liliwezekana kwa sehemu katika agano la kale kabla ya Bwana Yesu kuja, shetani alikuwa na uwezo wa kuzipandisha juu za watu waliokufa. Utaona katika maandiko aliweza kumpandisha juu nabii Samweli (1Samweli 28:11-14).
Lakini katika agano jipya, baada ya Bwana Yesu kushuka kuzimu na kuzichukua zile funguo za mauti na kuzimu, ambazo mara ya kwanza zilikuwa mikononi mwa shetani, kukawa kuanzia huo wakati na kuendelea hakuna yeyote anayeweza kuzipandisha juu roho za watu waliokufa..
Hata shetani mwenyewe hawezi tena, kwasababu funguo za kuzimu na mauti anazo Kristo mwenyewe..yeye ndiye anayewamiliki wafu wote, wema na waovu.
Warumi 14:9 “Maana Kristo alikufa akawa hai tena kwa sababu hii, awamiliki waliokufa na walio hai pia”.
Sasa swali linakuja, kama wafu hawawezi kurudi kama mizimu, hivyo tunavyoviona, au tunavyovisikia vikiwatokea watu vikiwa na sura za wapendwa wao waliowahi kuishi ni vitu gani?
Jibu rahisi ni MAPEPO yaliyojigeuza na kuvaa sura za watu waliokufa.
Maandiko yanasema shetani anaweza kujigeuza akawa kama Malaika wa Nuru, atashindwaje kujigeuza na kuvaa sura ya mtu fulani aliyekufa?. Ni kitu kirahisi sana kwake.
2 Wakorintho 11:14
“Wala si ajabu. Maana Shetani mwenyewe hujigeuza awe mfano wa malaika wa nuru”.
Kwahiyo shetani na mapepo yake wanachokifanya ni kuvaa sura za watu waliokufa na sauti zao, na kuigiza kama ndio wale watu halisi, na watu wanapowaona au kuwasikia wanaamini ni wafu wao wamerudi (Mizimu).. lakini kiuhalisia kumbe sio, bali ni mapepo yaliyojigeuza.
Na kwasababu shetani ni yule yule, anapenda kukaa nyuma ya kitu na kutafuta kuabudiwa..anakaa nyuma ya wote wanaoabudu sanamu, wanaoabudu miti wakidhani ni Mungu, wanaoabudu mizimu, wanaoabudu jua n.k
Hivyo hatuna budi tuwe macho na tujihadhari na kumwabudu shetani bila kujua, kwa kukosa maarifa.
Kadhalika kama bado tupo nje ya wokovu, hakuna namna yoyote tunaweza kujiepusha na madhara ya roho hizo chafu, ambazo zinazunguka huku na huko, kuuharibu ulimwengu.
Bwana atubariki.
Maran atha!
Jiunge na magroup yetu ya whatsapp kwa kubofya hapa > Group-whatsapp
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,
Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.
Mada Nyinginezo:
Je! Mtishbi ni jina la Baba yake au?
Jibu: Tishbi sio jina la mtu bali la mji, kama vile ulivyo mji wa Samaria au Nazareti.
Kwahiyo kama vile mtu aliyetoka mji wa Nazareti anavyoitwa Mnazareti, au aliyetokea mji wa Samaria anavyoitwa Msamaria, kadhalika mtu yeyote aliyetokea mji huo wa Tishbi aliitwa Mtishbi.
Mji huo wa Tishbi, ulikuwepo katika nchi ya Gileadi, iliyopo ng’ambo ya pili ya mto Yordani. Kwasasa ni maeneo ya nchi ya Yordani (Jordan).
Na katika mji huo mdogo wa Tishbi ndiko Nabii Eliya alikokulia na kuishi sehemu kubwa ya maisha yake.
1 Wafalme 17:1
“Basi Eliya Mtishbi, wa wageni wa Gileadi, akamwambia Ahabu, Kama BWANA, Mungu wa Israeli, aishivyo, ambaye ninasimama mbele zake, hakutakuwa na umande wala mvua miaka hii, ila kwa neno langu”
Maandiko hayajaeleza kwa undani maisha ya Nabii Eliya, ya utotoni, na ujanani, na vile vile hayajaeleza kama alikuwa na mke au watoto.
Lakini kikubwa tunachoweza kujifunza kwa Nabii huyu, ni roho ya kuomba kwa bidii..mbali na kwamba Mungu alimtumia kwa viwango vya juu sana, lakini pia alikuwa ni mtu wa kuomba kwa bidii sana, maandiko yanasema hivyo..
Yakobo 5:16
“Ungameni dhambi zenu ninyi kwa ninyi, na kuombeana, mpate kuponywa. Kuomba kwake mwenye haki kwafaa sana, akiomba kwa bidii.17 Eliya alikuwa mwanadamu mwenye tabia moja na sisi, akaomba kwa bidii mvua isinyeshe, na mvua haikunyesha juu ya nchi muda wa miaka mitatu na miezi sita.
18 Akaomba tena, mbingu zikatoa mvua, nayo nchi ikazaa matunda yake”.
Na sisi tunajifunza tuwe watu wa kuomba kwa bidii kwasababu Eliya alikuwa ni MTU tu! Kama sisi na si malaika, au mtu fulani aliyeumbwa kipekee tofauti na sisi..alichokuwa na cha ziada ni bidii ya kuomba.
Hivyo na sisi tunajifunza tuwe watu wa kuomba kwa bidii, na sio tu kuomba bali pia kuombeana. Kwasababu kuomba kwake mwenye haki kwafaa sana kama akiomba kwa bidii.
Bwana atujalie tuwe na bidii kama za hawa mashujaa wa Imani.
Maran atha!
Jiunge na magroup yetu ya whatsapp kwa kubofya hapa > Group-whatsapp
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,
Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.
Mada Nyinginezo:
Baali alikuwa ni aina ya mungu aliyekuwa anaabudiwa na watu wa kaanani na nchi za Tiro na Sidoni, ambaye kulingana na historia za wakaanani, anatajwa kuwa mwana wa mungu aliyeulikana kwa jina la El na mkewe aliyejulikana kwa jina la Ashera..hawa ndio waliomzaa huyu Baali ambaye baadaye alikuja kuabudiwa kama mungu.
Tafsiri ya jina “Baali” ni “bwana” na aliaminika kama mungu wa rutuba na wa uzao.
Aliaminika kusaidia kuongeza rutuba ya nchi, pale ambapo chakula hakikupatikana kutokana na ardhi kutozaa..basi walimwomba huyu mungu baali, ili nchi iweze kuzaa mazao.
Kadhalika pale ambapo mtu au watu walipatwa na matatizo ya kutokupata watoto, walimwomba na kumtegemea mungu huyu kwaajili ya kupata uzao.
Mungu huyu aliabudiwa sana na watu wa kimataifa, lakini ulifika wakati hata wana wa Israeli wakaanza kumwabudu.
Wana wa Israeli walianza kumwabudu baali kwa mara ya kwanza katika kile kipindi cha Waamuzi.
Waamuzi 2:11 “Wana wa Israeli walifanya yaliyokuwa ni maovu mbele za macho ya BWANA, nao wakawatumikia Mabaali.
12 Wakamwacha BWANA, Mungu wa baba zao, aliyewaleta kutoka katika nchi ya Misri, wakafuata miungu mingine, baadhi ya miungu ya watu wale waliokaa karibu nao pande zote, wakajiinamisha mbele yao; wakamkasirisha BWANA, akaghadhibika.
13 Wakamwacha BWANA, wakamtumikia Baali na Maashtorethi”.
Waliendelea hivyo na ibada hizo za mabaali, lakini si kwa kiwango kikubwa..
Hali ilikuja kuwa mbaya zaidi ulipofika wakati wa Mfalme mmoja wa Israeli aliyeitwa Ahabu, ndipo kipindi hicho ibada hizo zilishika hatamu mpaka Bwana Mungu akamtuma Eliya Nabii.
Mfalme Ahabu aliabudu baali kwa kiwango ambacho hakuna mfalme yeyote alikifikia.
1 Wafalme 16:30“ Ahabu mwana wa Omri akafanya yaliyo mabaya machoni pa BWANA kuliko wote waliomtangulia.
31 Ikawa, kama ingalikuwa neno dogo tu kuyaendea makosa ya Yeroboamu mwana wa Nebati, akamwoa Yezebeli binti Ethbaali, mfalme wa Wasidoni, akaenda akamtumikia Baali, akamsujudia.
32 Akamjengea Baali madhabahu katika nyumba ya Baali, aliyoijenga huko Samaria.
33 Ahabu akaifanya Ashera; Ahabu akazidi kumghadhibisha BWANA, Mungu wa Israeli, kuliko wafalme wote wa Israeli waliomtangulia”.
Lakini je! Baali alikuwa ni mungu kweli?
Jibu ni la!.
Mungu ni mmoja tu, aliyeziumba mbingu na nchi, jina lake YEHOVA. Hao wengine sio miungu bali ni roho za mapepo..BAALI ni pepo!..
Ndio maana haikuweza kujibu chochote mbele za uwepo wa Bwana wa majeshi, wakati ule wa Eliya.
1 Wafalme 18:26
“ Wakamtwaa yule ng’ombe waliyepewa, wakamtengeza, wakaliitia jina la Baali tangu asubuhi hata adhuhuri, wakisema, Ee Baali, utusikie. Lakini hapakuwa na sauti, wala aliyejibu. Nao wakaruka-ruka juu ya madhabahu waliyoifanya”.
Hiyo inatufundisha kuwa ibada zote za miungu na za sanamu ni chukizo kwa Bwana.
Na wote wanaoabudu sanamu, na miungu hawataurithi uzima wa milele, maandiko yanasema hivyo.
Bwana atubariki.
Jiunge na magroup yetu ya whatsapp kwa kubofya hapa > Group-whatsapp
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,
Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.
Mada Nyinginezo:
Bwana aliposema kuwa yeye ni “Mungu wa miungu” alikuwa na maana gani?..je! yeye ni Mungu wa sanamu?
Mlima Gerizimu na Ebali ni ipi, na umuhimu wao rohoni ni upi?
Jina la Bwana Yesu libarikiwe, karibu katika kuyatafakari maandiko..
2Wakorintho 11:4 “Maana yeye ajaye akihubiri YESU MWINGINE ambaye sisi hatukumhubiri, au mkipokea ROHO NYINGINE msiyoipokea, au INJILI NYINGINE msiyoikubali, mnatenda vema kuvumiliana naye”!
Hapo katika sentensi hiyo, Mtume Paulo aliposema “mnatenda vema kuvumiliana naye”..hakuwa anawasifu watu wa Korintho kwa wao kupokea roho nyingine, au kumkubali Yesu mwingine, bali kinyume chake! Alikuwa ANAWASHUTUMU!.
Sentensi hiyo ili ieleweke vizuri tunaweza kuiweka hivi ….“Mnachukuliana na mtu anayekuja kwenu na kuwahubiria yesu mwingine au injili nyingine msiyoikubali)” yaani “mnaona ni sawa na tena mnakubaliana naye”.
Hapo Mtume Paulo, alimaanisha kwamba, hawapaswi kuchukuliana na mtu yeyote anayekuja kwao na kuwaletea yesu Mwingine au roho nyingine au injili nyingine ambayo hawakuhubiriwa na mitume..kinyume chake wawakatae watu hao na wakatae injili yao na kuipuuzia…lakini hawa watu Wa Korintho walikuwa hawafanyi hivyo!.. walikuwa wanakaa na kuwasikiliza!..jambo ambalo ni hatari kwa roho zao.
Na hata sasa kuna yesu mwingine anayehubiriwa tofauti na Yule Yesu wa kwenye biblia, kadhalika kuna roho nyingine tofauti na Yule Roho Mtakatifu anayehubiriwa katika biblia, na vile vile kuna injili nyingine tofauti na injili halisi ya kwenye biblia..
yesu mwingine ni yupi?
Bwana Yesu halisi anasema wa kwenye biblia anasema.. “Yesu akamwambia, Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi (Yohana 14:6)”…lakini yesu mwingine anasema “zipo njia nyingi za kufika kwa baba, ikiwemo kupitia mtakatifu Fulani au kupitia maombi ya mtakatifu Fulani aliyekufa, au kupitia kanisa Fulani au kupitia dini nyingine yeyote”
Kadhalika Bwana Yesu halisi wa kwenye biblia alisema… “mtu yeyote akitaka kunifuata ajikane mwenyewe ajitwike msalaba wake anifuate(Mathayo 16:24) na tena anasema “itamfaidia mtu nini kuupata ulimwengu wote, akipata hasara ya nafsi yake? Ama mtu atoe nini badala ya nafsi yake?(Marko 8:36)”..lakini yesu mwingine anasema.. “sio lazima kujikana nafsi, sio lazima kuacha dhambi, sio lazima kubadilika kimwonekano, Mungu anatazama roho hatazami mwili” n.k
Huyo ndio mfano wa yesu Mwingine ambaye Paulo, aliwaonya watu wa Korintho kwamba wasimkubali,na wala wasichukuliana naye kwasababu ni shetani.
Kadhalika ipo roho Nyingine.
Roho Mtakatifu wa kweli wa kwenye biblia, akija juu ya mtu, jambo la kwanza analolifanya ni kumgeuza Yule mtu na kuwa mtakatifu, kama jina lake lilivyo.. “Roho Mtakatifu”..sifa yake ni utakatifu, na kazi ya pili ni kutuongoza na kututia katika kweli yote ya maandiko, na ya tatu ni kutukumbusha maandiko ..
lakini zipo roho ambazo mtu anapozipokea hazimfanyi kuwa mtakatifu, badala yake ndio zinampa kibali cha kutenda dhambi, kuvaa vibaya,(nusu uchi), kutukana, kuwa na kinyongo na visasi..kadhalika hazimwongozi mtu katika kusoma Neno na kulijua katika ukweli wote. Badala yake ndio zinamletea uvivu wa kuisoma biblia na kuijua..Hizo roho ni roho nyingine, ambazo sio Roho Mtakatifu, ni roho za adui, ambazo zinajigeuza na kujifananisha na Roho Mtakatifu.
Kadhalika kuna Injili nyingine.
Injili maana yake ni “habari njema za Yesu Kristo” ambazo zinaleta WOKOVU kwa mtu.(Warumi 1:16). Na wokovu ni kupata kuokoka kutoka katika hatari Fulani ijayo, au iliyopo.
Zipo injili ambazo hazimfanyi mtu aokoke kutoka katika hatari ya adhabu ya milele (katika Jehanamu ya moto), badala yake zinamfanya astahili kwenda Jehanamu.
Mfano wa injili hizo ni “injili za kutokusamehe, vinyongo na visasi”. Siku hizi hadi makanisani zinahubiriwa. Bwana Yesu alisema, msipowasamehe watu makosa yao, hata baba yenu wa mbinguni hatawasamehe (Mathayo 6:15)..Kwahiyo kutokusamehe tayari ni tiketi ya kwenda jehanamu moja kwa moja..Na injili yeyote inayohubiri kutokusamehe ni injili nyingine ya kuzimu.
Leo hii utakuta mkristo kajaa uchungu, na vinyongo..kwa mambo baadhi tu aliyofanyiwa mabaya..na anakwenda kanisani anakutana na injili ya kupiga adui zake, na kuipokea akidhani yupo salama..kumbe yupo hatarini?
Jiulize ndugu, Umempokea Yesu yupi? Wa kwenye biblia au Yule mwingine?..na umeipokea roho ipi?, Ni Roho Mtakatifu au ya adui?.. na ni Injili gani umeipokea?..ile iletayo wokovu, au ikupelekayo kuzimu?
Maandiko yanatuasa kuwa “tuzipime roho”, na sio roho tu!, bali pia tumpime Bwana yupo tumempokea Yesu Kristo au yesu kristo, na ni injili ipi tumeipokea.
Maran atha!
Jiunge na magroup yetu ya whatsapp kwa kubofya hapa > Group-whatsapp
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,
Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.
Mada Nyinginezo:
Je! Watu ambao hawajawahi kusikia injili kabisa siku ya mwisho watahukumiwa?
Ni kwa namna gani malaika wa mbinguni wanaweza kutuhubiria sisi injili?
Tofauti kati ya uchafu wa mwilini na rohoni ni ipi?
Matoazi na Matari ni nini? (Kutoka 15:20)
Katika 2Samweli 24:1 tunaona maandiko yanasema ni Mungu ndiye aliyemtia Daudi nia, lakini tukirudi katika 1Nyakati 21:1, tunaona maandiko yanasema ni shetani.
Tuanze na 2Samweli 24:1..
2Samweli 24:1 “Tena hasira ya BWANA IKAWAKA JUU YA ISRAELI, AKAMTIA DAUDI NIA JUU YAO, AKISEMA, NENDA, UKAWAHESABU ISRAELI NA YUDA”.
Tusome pia…
1Nyakati 21:1 “TENA SHETANI AKASIMAMA JUU YA ISRAELI, AKAMSHAWISHI DAUDI KUWAHESABU ISRAELI.
2 Basi Daudi akamwambia Yoabu, na wakuu wa watu, Nendeni kawahesabu Israeli toka Beer-sheba mpaka Dani; mkanipashe habari, nipate kujua jumla yao”.
Hapo tukiangalia tunaona ni kweli sentensi mbili zinajichanganya..lakini je! Ni kweli zinajichanganya?
Jibu ni la! Hazijichanganyi..fahamu zetu ndizo zinazojichanganya..lakini biblia siku zote itabaki kuwa Neno la Mungu, lililohakikiwa na Roho Mtakatifu na lisiloweza kukosewa.
Ili tuelewe vizuri maana ya mistari hiyo, hebu tutafakari katika mfano wa kawaida wa kimaisha.
Watu wawili tofauti wameshuhudia ajali barabarani.. Mmoja akatoa ushuhuda akasema “Yule mtu alipokuwa anavuka gari lilimgonga na halikusimama”…Na mwingine akatoa ushuhuda akasema.. “Yule mtu alipokuwa anavuka, Yule dereva alimgonga na hakusimama..akakimbia ”. Je! Katika hao mashuhuda wawili kuna ambaye hayupo sahihi?.. Bila shaka wote wapo sahihi!!.. aliyesema “gari limemgonga” na aliyesema “dereva kamgonga”..wote wapo sahihi..
Kwasababu Yule aliyesema gari limemgonga, hajahusisha dereva aliyekuwa analiendesha lile gari, kadhalika Yule aliyesema ni dereva kamgonga hajahusisha kifaa kilichotumika kumgongea Yule mvuka barabara, ambacho ni gari.
Kadhalika katika mistari hiyo hapo juu..Tunaona mmoja kamtaja kuwa ni Bwana Mungu ndiye aliyemtia nia Daudi, bila kuhusisha chombo alichokitumia (yaani shetani)..kadhalika mwandishi mwingine wa kitabu cha Mambo ya Nyakati, kakitaja chombo tu (yaani shetani)na bila kumhusisha aliyekitumia hicho chombo (yaani Mungu).
Kwahiyo kwa ujumla aliyeleta hayo yote ni Mungu, na shetani katumika tu kama chombo!..na hiyo yote ni kwasababu ya makosa ya Israeli. Na pia ilikuwepo sababu kwanini iwe ni kosa Daudi kwenda kuwahesabu Israeli kama utapenda kujua zaidi juu ya hilo, unaweza kufungua hapa >>>> USIZITEGEMEE NGUVU ZAKO
Kwahiyo tunachoweza kujifunza ni kwamba, Mungu anaweza kutumia chombo chochote kile kutimiza kusudi lake.
Kwamfano utaona Mungu alipotaka kuwatoa Israeli kuwapeleka Babeli, hakushuka yeye mwenyewe na kuwaondoa, bali utaona alimtumia Nebukadneza kama chombo chake cha kufanya hiyo kazi.
Kadhalika Bwana Mungu anaweza kumtumia shetani kutimiza kusudi lake.
Kwamfano mtu anayemkataa Mungu kwa makusudi, anaweza kuruhusu shetani ayaharibu maisha yake, mpaka atakapofikia hatua ya kujitambua.. Na hata wakati mwingine kama mtu huyo kama bado anazidi kushupaza shingo, basi Mungu anaweza kumweka chini milki ya shetani moja kwa moja.
Hivyo hatuna budi kukaa katika neema ya Mungu, na kuishi maisha yampendezayo, ili tusimkasirishe Bwana Mungu wetu aliyetuumba. Kwasababu maandiko yanasema.. yeye mwenyewe hapendi kumtesa mwadamu wala kumhuzunisha.. (Maombolezo 3:34).
Hivyo kwa hitimisho ni kwamba kama bado hujampokea Yesu, fahamu kuwa hizi ni siku za mwisho. Na Kristo yupo mlangoni kurudi, unyakuo wa kanisa ni wakati wowote. Je akija leo na kukukuta katika hali hiyo ya dhambi, utakuwa mgeni wa nani?
Maran atha!
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,
Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.
Mada Nyinginezo:
Ni miaka mingapi ya njaa Daudi aliyoambiwa achague? Ni miaka 7 au miaka 3?
Ni miaka mingapi ya njaa Daudi aliyoambiwa achague? Ni miaka 7 au miaka 3?
Ndoto za ajali zinaweza kuja katika maumbile mengi tofauti tofauti, wengine wanaota ajali za pikipiki, wengine za magari, wengi ndege, wengine meli, wengine treni, katika namna tofauti tofauti. Wengine wanaota mtu kagongwa na gari, au magari yanagonga gongana n.k… kwa vyovyote vile, ndoto hizo zinabeba maudhui moja nayo ni “AJALI”
Sasa ili kupata tafsiri sahihi ya ndoto hiyo ni vizuri ukajitambua wewe upo katika kundi gani.
1.) Kundi la kwanza ni waliookoka.
2) Kundi la pili ni wenye dhambi.
Tukianzana na kundi la kwanza: Ikiwa wewe, umeokoka (yaani unao uhakika umesimama ndani ya Kristo). Basi fahamu kuwa ni Mungu anakutahadharisha tukio lililopo mbele yako, aidha kuna ajali utakutana nayo, au itatokea kwa mtu mwingine, au mahali fulani. Hivyo unachopaswa kufanya, ni kuingia katika maomba ya kuvunja hiyo mipango ya adui. Ambayo pengine imepangwa kwako au kwa mtu mwingine..kemea kwa bidii kwa mamlaka uliyopewa katika jina la Yesu. Na Mungu ataisambaratisha hiyo mipango yote.
Ikiwa ndoto hiyo imekuja kwa uzito usiipuuzie, kwasababu Mungu kukuonyesha hivyo, ni ili usimame kama askari wa Mungu kushindana na hizo nyakati mbaya kabla hazijafika.( Soma Ayubu 33:14-15)
Kundi la Pili: Mwenye dhambi.
Ikiwa wewe ni mwenye dhambi(yaani hujaokoka, Kristo hayupo ndani yako). Ujue ndoto hiyo ni ishara ya tahadhari kubwa sana kwako. Kwamba kipindi si kirefu Mungu atakuadhibu, na kuadhibu kwake, kunaweza kukawa ni kifo cha ghafla, au kunaswa katika dhambi zako unazozifanya, na ukashindwa kutoka huko milele.
Soma hii Habari kwa makini;
Ezekieli 7: 6 “Mwisho umekuja, mwisho huu umekuja; unaamka ukupate; angalia, unakuja.
7 AJALI YAKO IMEKUJIA, wewe ukaaye katika nchi hii; majira yamewadia, siku ile inakaribia; siku ya fujo, wala si ya shangwe milimani.
8 BASI HIVI KARIBU NITAMWAGA GHADHABU YANGU JUU YAKO, nitazitimiza hasira zangu juu yako, nami nitakuhukumu sawasawa na njia zako; nami nitakupatiliza machukizo yako yote.
9 Jicho langu halitaachilia, wala sitaona huruma; nitakupatiliza njia zako na machukizo yako yote yatakuwa katikati yako; nanyi mtajua ya kuwa mimi, Bwana, napiga.
10 ANGALIA, SIKU HIYO; ANGALIA, INAKUJA; AJALI YAKO IMETOKEA; fimbo imechanua, kiburi kimechipuka”.
Umeona? Hayo maandiko yenyewe yanajieleza, ikiwa wewe ni mzinzi, fahamu kubwa ajali ya Ukimwi ipo mbele yako, wewe ni fisadi ajali ya vifungo ipo mbele yako, wewe ni mwizi ajali ya kifo ipo mbele yako, wewe ni mshirikina ajali ya jehanum ipo mbele yako.
Kwa ujumla kama wewe ni mwenye dhambi ujue mwisho wako upo karibuni sana. Na ukifa ni motoni. Ndio tafsiri ya ndoto hiyo.
Unasubiri nini mpaka hayo yote yakukute, ikiwa upo tayari leo kutubu dhambi, basi, Bwana Yesu atakusamehe, na kukuepusha na madhara hayo yote aliyokuonyesha mbele yako. Angeweza kukaa kimya tu, hayo mambo yakukute kwa ghafla, lakini kwasababu hataki uangamie ndio maana amekutahadharisha mapema.. Hivyo leo hii fungua moyo wako, kubali kugeuka, na uache dhambi zako zote, ili Kristo ayatengeneze tena Maisha yako.
Ikiwa upo tayari kutubu leo, basi fungua hapa, kwa ajili ya mwongozo wa SALA YA TOBA. >>> KUONGOZWA SALA YA TOBA
Bwana akubariki.
Angalia pia Kuota Unajenga nyumba
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,
Kwa mgawanyo bora wa masomo download App hapa>> App wingu la mashahidi
Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.
Mada Nyinginezo:
Nakusalimu katika jina kuu, la Bwana wetu Yesu Kristo karibu katika sehemu ya pili ya Makala hii inayohusu migogoro katika ndoa. Sehemu ya kwanza tuliona Upande wa mwanaume, Leo tutaangazia upande wa mwanamke. Kwa kurejea mgogoro uliozuka katika ndoa ya kwanza ya Adamu. Kama hukupata sehemu ya kwanza tutumie msg inbox tukutumie uchambuzi wake.
Wewe kama mke.
Unapaswa utambue kuwa mume ndio kichwa cha Familia, Ndoa ya kwanza ulitikiswa na mwanamke, kuonyesha kuwa vyanzo vya migororo ya ndoa nyingi hadi sasa ni WANAWAKE.
Na hiyo yote ni kwasababu wepesi kufungua milango kwa shetani kuwadanganya kirahisi. Kwamba wao pia wajione wanauwezo wa kujiamulia tu mambo yao bila hata ya waume zao au kumshirikisha Mungu ? Hiyo ni hatari kubwa sana.
Usijaribu kufanya hivyo mwanamke, utaiharibu ndoa yako kwa mikono yako mwenyewe. Kinyume chake, anza kuwa MTIIFU kwa mume wako kama biblia inavyosema katika..
Waefeso 5:22 “ENYI WAKE, WATIINI WAUME ZENU KAMA KUMTII BWANA WETU.
23 Kwa maana mume ni kichwa cha mkewe, kama Kristo naye ni kichwa cha Kanisa; naye ni mwokozi wa mwili.
24 Lakini kama vile Kanisa limtiivyo Kristo vivyo hivyo wake nao wawatii waume zao katika kila jambo”.
Kuwa mtiifu, mume wako anapokutakana uwahi kurudi nyumbani, TII, anapokuambia nipikie chakula, Tii, anapokuambia nifulie nguo, usimwambie housegirl si yupo, anapokuambia fanya hivi, au fanya vile wewe tenda, anapokushauri usifanye shughuli Fulani, sio nzuri, tii pia, kwasababu yule ndio kichwa chao. Ondoa kiburi ndani yako, wewe sio kichwa, ukijaribu kufanya hivyo, ndipo hapo shetani atakupa mbinu mbadala, utafute marafiki/wanaume wengine nje ya ndoa yako wenye pesa, ili kumkomoa mume wako, kumbe hujui kuwa ndio unajiangamiza wewe mwenyewe. Ndicho alichokiwaza Hawa alipokwenda kutafuta mashauri kwa nyoka.
Kwahiyo, simama katika nafasi yako, ya utiifu. Mbinu aliyotumia shetani kumwangamiza Hawa, ndio hiyo hiyo ataitumia na kwako, isiposimama katika nafasi yako kama mwanandoa. Na majuto utayaona baadaye sio sasa wakati una kiburi.
Kumbuka, mwanamke hutakaa ufanikiwe kwa kujitenga na mume wako? Kamwe halitawezekana. Mwanaume anaweza kujaribu kuishi, japo itakuwa kwa shida sana, lakini wewe sahau kuishi kwasababu Ubavu hauna ubongo,wala mikono, wala miguu, wala pua, wala macho,. Ni kipande cha nyama tu. Ndivyo ilivyo kwako wewe, ujue kuwa huna Maisha nje ya mume wako wa ndoa. Ukimwacha leo, haijalishi, una kipato kikubwa kuliko yeye, au ni mjanja kuliko yeye, nataka nikuambie hauna Maisha wewe duniani.
Na mwisho kabisa, hayo yote unaweza kuyafikia, ikiwa tu upo ndani ya Kristo, Haiwezekani kuwa mtiifu, au mwombaji, au mtakatifu, au mtu wa kusamehe, kama hutakuwa ndani ya Kristo. Kwahiyo hatua ya kwanza ni kumpa Kristo Maisha yako.
Ikiwa upo tayari kufanya hivyo leo. Basi unaweza kufuatisha sala hii kwa Imani. Ukiifuatisha kwa kumaanisha kabisa ujue kabisa Bwana Yesu atakusamehe leo na kuja ndani yako….Tafuta sehemu ya utulivu kisha piga magoti, na useme sala hii kwa sauti.
“EE MUNGU BABA, NAJA MBELE ZAKO, NIKIWA NINAJITAMBUA KUWA MIMI NI MKOSAJI NA NIMEKUTENDA DHAMBI NYINGI, NA KWAMBA NIMESTAHILI HUKUMU, (KWA KUIJERUHI NDOA YANGU). LAKINI WEWE MUNGU WANGU ULISEMA KATIKA NENO LAKO KUWA WEWE NI MUNGU WA REHEMA UNAYEWAREHEMU MAELFU ELFU YA WATU WANAOKUPENDA WEWE. NA LEO HII NINAKUJA MBELE ZAKO NAHITAJI MSAMAHA WAKO NA MSAADA WAKO MUNGU WANGU, NINATUBU DHAMBI ZANGU ZOTE KWA KUMAANISHA NA KWA MOYO WANGU WOTE, NINAKIRI KUWA YESU KRISTO NI BWANA, NA YEYE NDIYE MWOKOZI WA HUU ULIMWENGUNI. HIVYO NAOMBA DAMU YA MWANAO TAKATIFU INISAFISHE UOVU WANGU WOTE SASA NIFANYIKE KUWA KIUMBE KIPYA KUANZIA LEO NA HATA MILELE.
ASANTE BWANA YESU KWA KUNIPOKEA NA KUNISAMEHE.
AMEN.”
Ikiwa umefuatisha sala hiyo kwa Imani, ujue kuwa Kristo ameshakusamehe na kuanzia sasa anza kuwajibika kwa ajili ya ndoa yako. Na kama hujabatizwa, na unahitaji kubatizwa katika ubatizo sahihi wa kuzamishwa katika maji mengi, na kwa jina la Yesu Kristo, basi wasiliana na sisi kwa namba hizi, +255693036618 au +255789001312 Tukusaidie.
Mungu akubariki sana.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,
Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.
Mada Nyinginezo:
KWANINI NDOA NYINGI ZINAVUNJIKA? (Sehemu ya 2: Upande wa wanawake)
Nini maana ya..“wakiwazuia watu wasioe” (1Timotheo 4:1)
Kwanini wajane vijana hawakupaswa kuandikwa?
NDOA NA TALAKA:
NINI TUNAJIFUNZA KWA THEOFILO MTUKUFU?
Katika siku hizi za mwisho, migogoro ya kindoa imekuwa ni mingi sana, kiasi kwamba ndoa kudumu hata mwaka mmoja, ni jambo la kushukuru sana. Kila kukicha mikwaruzano, hakuna amani, kila mmoja amemchoka mwenzake. Mpaka wengine kudhani huyo mwenzi aliyemuoa au aliyeolewa naye halikuwa chaguo sahihi kutoka kwa Mungu, hivyo suluhisho pekee ni kuachana.
Nataka nikuambie, kabla hujafikiria kuachana na huyo mwenzi wako, Tafuta kwanza kama kuna watu walishapitia tatizo kama hilo la kwako, na uone walilitatuaje tatuaje, au mwisho wao ulikuwaje..
Kumbuka kuvunjika kwa ndoa, ni kushindwa kwa pande zote mbili (au moja), kujua wajibu wake katika ndoa kama Neno la Mungu linavyoagiza..
Ndoa inafananishwa na safari ya Maisha/ ya wokovu, si wakati wote, itakuwa ni “HONEY MOON”, si wakati wote mtakuwa ni vijana, si wakati wote mtakuwa Pamoja, na si wakati wote mambo yataenda sawa.. Haijalishi ndoa hiyo, atakuwa ameifungishwa Mungu mwenyewe Kanisani au la. Kushuka na kupanda kutakuwa ni sehemu ya Maisha yenu.
Leo hii tutajifunza, mfano wa ndoa moja maarufu katika biblia, na jinsi ilivyokumbana na migogoro mikubwa sana, ambayo naamini ni Zaidi ya migogoro ya ndoa zote zilizowahi kutokea ulimwenguni, lakini Pamoja na hayo bado iliendelea kudumu hadi dakika ya mwisho, naamini kwa kupitia hiyo itakuponya na wewe pia ambaye kwenye ndoa yako zimeshaanza kuonekana dalili za nyufa.
Na ndoa hiyo si nyingine Zaidi ya ile ya ADAMU.
Adamu alichaguliwa mke na Mungu mwenyewe, tena aliyeumbwa kutoka katika ubavu wake kabisa,kuonyesha kuwa ni wake kweli kweli,. Lakini waliishi kwa kipindi Fulani kirefu kwa raha na furaha bila taabu wala shida yoyote, hadi siku mambo yalipoanza kubadilika,
Na yalibadilika, kwa kukengeuka kwa mwanamke kwanza, pale ambapo aliacha kusikiliza maagizo ya mume wake(aliyopewa na Mungu), ya kutokula matunda ya mti wa ujuzi wa mema na mabaya, lakini yeye akayala kwa tamaa ya kutaka kuwa kama Mungu, ya kutaka kuwa kichwa (yaani kumzidi hata mume wake),ya kutaka kumiliki, akayala bila kumshirikisha mume wake, lakini kinyume chake ni kuwa tamaa hiyo Mungu aliipindua na kuihamishia kwa mume wake badala yake, na ndio maana utaona leo hii kwanini wanaume wanauchu wa kutawala, kuwa vichwa, hiyo tamaa mwanzoni haikuwepo kwao bali ilikuwa kwa mwanamke, baada ya kuasi Mungu ndio akamuadhibu mwanamke kwa kosa hilo la kumuhamishia mwanaume.
Mwanzo 3:16 “Akamwambia mwanamke, Hakika nitakuzidishia uchungu wako, na kuzaa kwako; kwa utungu utazaa watoto; na tamaa yako itakuwa kwa mumeo, naye atakutawala”.
Sasa na baadaye Adamu alipoona, mke wake kaharibu, ameasi, akakubali na yeye, kuingia katika matatizo ya mke wake kwa hiari yake yeye mwenyewe (kwasababu yeye hakudanganywa), na baada ya hapo, Mungu akamlaani naye pia.
Tangu huo wakati, Maisha yakawa magumu kweli, kwasababu dhambi imeshaingia, kulima kwa shida kukanza, magonjwa yakazuka, vifo vikaingia, kila aina ya shida ikazuka tangu huo wakati na kuendelea, kila kukicha hali ndio ilizidi kuwa mbaya, hadi kwa Watoto waliowazaa, hakuna amani katikati yao, wakawa wanauana.. Embu tengeneza picha ingekuwa wewe ni Adamu ungemfanyaje huyo mwanamke baada ya hapo?
Ni wazi kuwa ungempa talaka siku ile ile ya kwanza alipofanya kosa lile si ndio?. Tena baada ya hapo ungekuwa ni wa kulaumu Maisha yako yote, kwamba Mungu amekupa mkosi na balaa, ni heri ungebakia tu peke yako bila kuoa, lakini tangu ulipompata huyo mwanamke, mambo yako ndio yameenda kombo kabisa kabisa…
Lile kampuni amelifilisi, mali zote zimepukutika umerudia umaskini ambao ulikuwa umeshauaga zamani, amekuletea gonjwa la ukimwi kwa kutanga tanga kwake, amekufanya utengane sio tu na ndugu zako, bali hata na Mungu wako. Mwanzoni ulikuwa ukifanya ibada vizuri, lakini tangu umuoe yule mwanamke, muda kusali haupo! Kila kitu unakipata kwa shida, tofauti na ulivyokuwa ‘Single’.
Lawama kama hizo Adamu angestahili kuwa nazo kwa mke wake, Lakini hatuoni mahali popote Adamu alimwacha mke wake, na kutamani kuishi na wanyama kama hapo mwanzo, bali alimkumbatia, akakubaliana na hali, akamsamehe, akayapanga tena upya. Akijua kuwa ule tayari ni ubavu wake. Na Mungu hakukosea kumpa, lilikuwa ni chaguo sahihi.
Mwanaume,
Kumbuka kuwa, mpaka umefikia hatua ya kumwoa huyo binti/ mwanamke, ujue kuwa ndio UBAVU wako huo Mungu aliokupa, usidhani kumtambua mke mwema ni mpaka uishi naye bila migogoro, sikuzote za Maisha yako, si kweli. Huyo ambaye upo naye katika migogoro, ni wako, na atabakia kuwa wako mpaka kifo kitakapowatenganisha.
Unachopaswa kufanya ni wewe kusimama katika nafasi yako kama ADAMU.
Suluhisho sio kumwacha, kumbuka ukimwacha huyo maana yake, unataka kurudia kuishi na Wanyama, Mpende mke wako, kwasababu hakuna kitu kinachojenga Zaidi ya upendo, mkumbatie, msamehe, mjenge upya, mvumilie, pale anapokosa, hata kama alikuletea balaa kubwa namna gani, mkumbuke Adamu, alivyoweza kuwa mvumilivu, kwa kunyang’anywa kila kitu na Mungu lakini hakumwacha Hawa. Kwani biblia inasema aliishi miaka 930, na unajua mara nyingi wanawake huwa wanakuwa na umri mrefu kuliko wanaume, kwahiyo si ajabu kuona Adamu aliishi na mke wake kwa Zaidi ya miaka hata 800, lakini sisi miaka 3 tu tumeshachokana.
Biblia inasema..
Waefeso 5:25 “Enyi waume, WAPENDENI WAKE ZENU, kama Kristo naye alivyolipenda Kanisa, akajitoa kwa ajili yake;
26 ili makusudi alitakase na kulisafisha kwa maji katika neno;
27 apate kujiletea Kanisa tukufu, lisilo na ila wala kunyanzi wala lo lote kama hayo; bali liwe takatifu lisilo na mawaa.
28 Vivyo hivyo imewapasa waume nao kuwapenda wake zao kama miili yao wenyewe. Ampendaye mkewe hujipenda mwenyewe.
29 Maana hakuna mtu anayeuchukia mwili wake po pote; bali huulisha na kuutunza, kama Kristo naye anavyolitendea Kanisa.
30 Kwa kuwa tu viungo vya mwili wake.
31 Kwa sababu hiyo mtu atamwacha baba yake na mama yake, ataambatana na mkewe na hao wawili watakuwa mwili mmoja”.
UPENDO KWA MKE wako, ni agizo kutoka kwa Mungu, na sio ihari yako tu mwenyewe. Ukiwa mwanaume wa namna hii, nataka nikuambie utaiponya ndoa yako, na itadumu sana. Wanawake kukengeuka haraka, ni jambo la kawaida, lakini wakisharudi, wanakuwa ni lulu nzuri kwako. Jifunze kusamehe, na vilevile kumpenda.
Lakini hayo yote huwezi kuyafikia kama upo nje ya Kristo. Hivyo Okoka, mkaribishe Yesu katika Maisha yako, tubu dhambi zako, kwa kumaanisha kabisa, kisha ubatizwe, upokee Roho Mtakatifu, na Kristo atakupa uwezo huo, wa kumpenda mkeo kama alivyokuwa Adamu.
Bwana akubariki.
Usikose, sehemu ya pili ya Makala hii.. Ambayo inamlenga mwanamke, kama chanzo cha migogoro ndani ya ndoa, na afanye nini ili aweze kuiponya ndoa yake.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,
Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.
Mada Nyinginezo: