Israeli ipo Bara la Asia, katika ukanda wa Asia Magharibi (au ukanda wa Mashariki ya kati). tofuati na inavyodhaniwa na baadhi ya watu kuwa Israeli ipo bara la Ulaya.
Ikumbukwe kuwa Bara la Asia ndio bara lililokubwa kuliko yote duniani, na limegawanyika katika maeneo makuu sita (6),
Kwa maelezo marefu juu ya mataifa hayo unaweza kuyasoma Wikipedia fungua link hii >> https://sw.wikipedia.org/wiki/Asia
Sasa katika huo ukanda wa Asia Magharibi /Asia ya kati ambao ndio unaundwa na nchi kama Jordan, Siria, Lebanoni, Palestina, Saudi Arabia, Oman, Yemen n.k Ndio huko sasa nchi ya Israeli nayo inapatikana.
Hivyo ni vema pia kujua juu ya historia ya muhimu zaidi ihusulo taifa hili,. Kwani huko ndiko alipotokea mkombozi wa huu ulimwenguni, ajulikanaye kama YESU KRISTO wa Nazareti. Ambaye kwa kupitia yeye mimi na wewe tumepokea uzima wa milele bure kama tukimwamini.
Hakuna mwadamu aliyewahi kutokea mwenye malengo, na mkamilifu kama Yesu Kristo..Huyu alitumwa na Mungu mwenyewe ili kuja kutuokosa sisi tulio katika shida na vifungo na mateso ya dhambi.
Na siku akirudi, miguu yake itatua tena kwa mara ya kwanza katika taifa hili hili la Israeli, juu ya milima ujulikanao kama mlima wa mizeituni (Zekaria 14:4), na taifa hili ndilo litakalokuwa makao yake makuu, ambapo atatawala kama BWANA WA MABWANA na MFALME WA WAFALME juu ya dunia nzima katika Yerusalemu yake mpya atakayoifanya.
Wakati huo dunia haitakuwa kama ilivyo sasa, kwani itakuwa imeshatengenezwa na kurudishwa katika katika hali ambayo haielezeki kwa jinsi ya kibinadamu. Tutatawala Pamoja naye kwa muda wa miaka 1000 ni kisha baada ya hapo tutaingia katika umilele.
Kwa maelezo marefu, fungua vichwa vya masomo mengi hapo chini ufahamu kalenda yote ya ki-Mungu kwetu sisi wanadamu duniani..
Shalom.
Mada Nyinginezo:
KWANINI YESU KRISTO ALIKUJA DUNIANI?
UTAWALA WA MIAKA 1000.
MAPIGO YA VITASA SABA, NA SIKU YA BWANA.
UNYAKUO.
CHUKIZO LA UHARIBIFU
Nabii Malaki alikuwa ni nabii kama walivyo manabii wengine katika biblia kama nabii Yeremia, nabii Isaya, nabii Samweli, Nabii Danieli..Biblia haijaeleza maisha yake kama ilivyoelezea kwa baadhi ya manabii wengine kama Samweli, Yeremia na Danieli. Nabii Malaki ni nabii ambaye maisha yake hayapatikani katika vitabu vingine vya biblia. Na ndiye nabii wa mwisho aliyeandika kitabu cha mwisho katika agano la kale. Kitabu cha Malaki kiliandikwa kati ya mwaka 441-400KB. Na kina Sura nne tu, lakini zilizoshiba Jumbe nzito.
Sasa tunaposema ni nabii wa mwisho haimaanishi kwamba hawakutokea manabii wengine baada yake..la!..walitokea wengine waliotumwa na Mungu, katikati ya hicho kipindi cha miaka 400 lakini Bwana Mungu hakuruhusu jumbe zao ziwe miongoni mwa orodha ya vitabu hivyo vya agano la kale. Na kama havijaruhusiwa kuwekwa kwenye orodha na Roho Mtakatifu mwenyewe hatupaswi sisi kuvitafuta na kuvipachika, wala hatupaswi kutafuta majina ya hao manabii ni wakina nani..Tukifanya hivyo tutafungua mlango wa roho ya Ibilisi kutupotosha…Roho Mtakatifu alikuwa na maana yake kubwa kuzuia visiwekwe kwenye orodha.
Hivyo kitabu cha Malaki ndio kitabu cha mwisho katika vitabu vya agano la kale, vingine vinavyochomekwa sasa ni batili.
kitabu cha malaki
Sasa tukirudi kwa huyu Nabii Malaki, ndiye Nabii pekee aliyepewa ufunuo wa kurudi kwa Roho ya Eliya duniani tena….hakuna Nabii mwingine yeyote aliyefunuliwa ufunuo huo zaidi yake yeye,
Malaki 4:5 “Angalieni, nitawapelekea Eliya nabii, kabla haijaja siku ile ya Bwana, iliyo kuu na kuogofya.
6 Naye ataigeuza mioyo ya baba iwaelekee watoto wao, na mioyo ya watoto iwaelekee baba zao, ili nisije nikaipiga dunia kwa laana”.
Na unabii huo wa Ujio wa Eliya, ulikuja kutimia kwa Yohana Mbatizaji .
Mathayo 17:10 “Wanafunzi wake wakamwuliza, wakisema, Basi kwa nini waandishi hunena ya kwamba imempasa Eliya kuja kwanza?
11 Naye akajibu, akawaambia, Kweli Eliya yuaja kwanza, naye atatengeneza yote,
12 ila nawaambia, ya kwamba Eliya amekwisha kuja, wasimtambue, lakini wakamtenda yote waliyotaka. Vivyo hivyo Mwana wa Adamu naye yuaenda kuteswa kwao.
13 Ndipo wale wanafunzi walipofahamu ya kuwa amesema nao habari za Yohana Mbatizaji”.
Nabii Malaki pia kwa ufunuo wa Roho ndiye nabii aliyezungumzia ZAKA kwa kina, Bwana alimfunulia kuwa wote wanaokwepa kulipa zaka, ni kama wezi mbele zake.
Malaki 3:8 “Je! Mwanadamu atamwibia Mungu? Lakini ninyi mnaniibia mimi. Lakini ninyi mwasema, Tumekuibia kwa namna gani? Mmeniibia zaka na dhabihu.
9 Ninyi mmelaaniwa kwa laana; maana mnaniibia mimi, naam, taifa hili lote.
10 Leteni zaka kamili ghalani, ili kiwemo chakula katika nyumba yangu, mkanijaribu kwa njia hiyo, asema Bwana wa majeshi; mjue kama sitawafungulia madirisha ya mbinguni, na kuwamwagieni baraka, hata isiwepo nafasi ya kutosha, au la”.
Nabii Malaki ndiye nabii pekee ambaye alifunuliwa hisia za Mungu kipekee sana tofauti na manabii wengine…Mungu alimfunulia ni vitu gani vinavyomchosha yeye kutoka kwa wanadamu, na vitu vinavyomchukiza ambavyo wengi hawajui kama vinamchukiza Mungu. Kwamfano suala la kuachana, wengi hawajui kwamba linamchukiza Mungu kwa kiwango kikubwa sana…
Malaki 2:16 “Maana mimi nakuchukia kuachana, asema Bwana, Mungu wa Israeli; naye aifunikizaye nguo yake kwa udhalimu namchukia, asema Bwana wa majeshi; basi jihadharini roho zenu, msije mkatenda kwa hiana”.
Na pia kuna mambo tuyafanyayo yanayomchosha Mungu wetu pasipo sisi kujua..
Malaki 2:17 “Mmemchokesha Bwana kwa maneno yenu. Lakini ninyi mwasema, Tumemchokesha kwa maneno gani? Kwa kuwa mwasema, Kila atendaye mabaya ni mwema machoni pa Bwana, naye huwafurahia watu hao, au, Mungu mwenye kuhukumu yuko wapi?”
Na pia Nabii Malaki alionyeshwa kuwa kuna maneno tuyazungumzayo ambayo ni magumu kwa Mungu wetu, ambayo hatupaswi kuyasema…
Malaki 3:13 “Maneno yenu yamekuwa magumu juu yangu, asema Bwana. Lakini ninyi mwasema, Tumesema maneno juu yako kwa namna gani?
14 Mmesema, Kumtumikia Mungu hakuna faida; na, Tumepata faida gani kwa kuyashika maagizo yake, na kwa kwenda kwa huzuni mbele za Bwana wa majeshi?
15 Na sasa twasema ya kwamba wenye kiburi ndio walio heri; naam, watendao uovu ndio wajengwao; naam, wamjaribuo Mungu ndio waponywao.
16 Ndipo wale waliomcha Bwana waliposemezana wao kwa wao. Naye Bwana akasikiliza, akasikia; na kitabu cha ukumbusho kikaandikwa mbele zake, kwa ajili ya hao waliomcha Bwana, na kulitafakari jina lake.
17 Nao watakuwa wangu, asema Bwana wa majeshi, katika siku ile niifanyayo; naam, watakuwa hazina yangu hasa; nami nitawaachilia, kama vile mtu amwachiliavyo mwanawe mwenyewe amtumikiaye”.
Hivyo Neno la Mungu ni taa..kuna mambo mengi ya kujifunza katika kitabu cha Malaki, hayo ni baadhi tu machache…lakini kila mmoja wetu akitenga muda kukisoma, huku akimruhusu Roho Mtakatifu awe mwalimu wake, yapo makubwa ya kunufaika na ya kulinufaisha kanisa la Kristo, Bwana atusaidie katika kulisoma Neno lake na kulitendea kazi.
Maran atha!
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312
Mada Nyinginezo:
“Mithali” na “Methali” ni neno lenye maana moja.. ambalo maana yake ni kipande cha sentensi chenye kubeba ujumbe halisi wa kimaisha…Methali/Mithali zinaweza kuwa ni sentensi zenye ujumbe wa wazi au zenye ujumbe wa fumbo.
Kwa mfano methali inayosema “akufaaye kwa dhiki ndiye rafiki wa kweli” hii ni methali iliyo wazi kabisa yenye ujumbe wa kwamba…mtu Yule ambaye wakati wa dhiki yupo na wewe huyo ndiye rafiki wa kweli tofauti na Yule ambaye wakati wa dhiki anakukimbia lakini wakati wa raha ndio anakukaribia.
Lakini pia kuna mithali kama “mtaka cha uvunguni sharti ainame” methali hii inahitaji kutafakari sana ndipo upate ujumbe… “Kwamba ili upate jambo Fulani huna budi kuingia gharama” Na nyingine zote ni hivyo hivyo.
Sasa katika biblia pia zipo methali/Mithali…Mithali hizi Roho Mtakatifu karuhusu ziandikwe na wenye hekima ili ziwape hekima watoto wa Mungu.
Katika biblia tunamsoma mtu mmoja anayeitwa Sulemani, ambaye alimwomba Mungu Hekima badala ya Mali, na hivyo Mungu alimpa hekima nyingi sana, mpaka wafalme na mamalkia wa dunia wakawa wanamwendea kusikiliza hekima zake. Na nyingi ya hekima alizojaliwa aliziandika kwa mfumo huo wa Methali na nyimbo.
1Wafalme4: 29 “Mungu akampa Sulemani hekima, na akili nyingi sana, na moyo mkuu, kama mchanga ulioko pwani.
30 Hekima ya Sulemani ikapita hekima ya wana wote wa mashariki, na hekima zote za Misri.
31 Kwa kuwa alikuwa na hekima kuliko watu wote; kuliko Ethani Mwezrahi, na Hemani, na Kalkoli, na Darda, wana wa Maholi; zikaenea sifa zake kati ya mataifa yote yaliyozunguka.
32 NAYE AKANENA MIFANO ELFU TATU, NA NYIMBO ZAKE ZILIKUWA ELFU MOJA NA TANO.
33 Akanena habari za miti tangu mwerezi ulioko Lebanoni hata hisopo umeao ukutani; pia akanena habari za wanyama, na za ndege, na vitambaavyo, na samaki.
34 Wakaja wa mataifa yote ili waisikie hekima ya Sulemani, toka wafalme wote wa ulimwengu, waliokuwa wamepata habari za hekima yake”.
Kwahiyo biblia ni kitabu kilichojitosheleza..asilimia 100, kina faraja, kina wasaa, kina elimu, kina Mithali, na hekima na maarifa. Kama mtu mmoja alivyowahi kusema “kama nikipatiwa biblia na mshumaa katika chumba chenye giza, basi nitaweza kukuelezea kila kitu kinachoendelea katika dunia”. Na hiyo ni kweli kabisa..
Sasa hebu tusikilize baadhi ya Mithali za biblia, kama methali tu methali ya kidunia inayosema “akufaaye kwa dhiki ndiye rafiki wa kweli” inaweza kutusaidia kutambua marafiki wa kweli, basi biblia ni dhahiri kuwa ina mithali nyingi zinazofanana na hizo ambazo zimejaa hekima kuliko mithali hizi zetu za kidunia..
Mithali juu ya wanaokuchukia/kukuwazia mabaya:
Mithali 24: 17 “Usifurahi, adui yako aangukapo; Wala moyo wako usishangilie ajikwaapo;
18 Bwana asije akaliona hilo, likamkasirisha; Akageuzia mbali naye hasira yake.
19 Usikasirike kwa sababu ya watenda mabaya; Wala usiwahusudu wabaya;
20 Kwa maana mtu mbaya hapati thawabu; Taa ya mtu mbaya itazimika”.
Hiyo ni Methali ya maisha, kamwe usifurahi…adui yako anapopatwa na mabaya!..bali uhuzunike!, na kumhurumia na Bwana atakuongezea amani na furaha, na kukupenda!…
Na mithali nyingine ni hii..
Mithali 25: 21 “Adui yako akiwa ana njaa, mpe chakula; Tena akiwa ana kiu, mpe maji ya kunywa;
22 Maana utatia makaa ya moto kichwani pake; Na Bwana atakupa thawabu”.
Mithali ya Njia unayoiendea:
Mithali 14: 12 “Iko njia ionekanayo kuwa sawa machoni pa mtu, Lakini mwisho wake ni njia za mauti”.
Maana yake ni kwamba kuwa makini na ile njia ambayo unaweza kuiona ni sawa machoni pako…. “chunguza sana njia zako, hususani zile unazoziona zipo sawa, nyingi zinaishia upotevuni”. Njia zinazofuatwa na watu wengi zinaishia upotevuni.
Zipo methali nyingi sana katika kitabu cha Mithali, Mhubiri, Zaburi na Ayubu, hatuwezi kuziandika zote hapa, lakini hizi chache ni ili kukukumbusha wewe ndugu kwamba Biblia ni neno la Mungu lililojitosheleza… anza kutenga muda kusoma biblia, kuna mambo mengi ambayo ulikuwa huyajui utayajua, kuna hekima nyingi ambazo zitakufumbua macho katika hali unayopitia sasa…Mambo ambayo ulikuwa huna majibu nayo, basi utayapata ndani ya biblia.
Anza leo kusoma vitabu hivyo vya mithali na vingine vyote, na Bwana atakuwa na wewe, zipo ambazo zina ujumbe wa wazi na zipo zenye ujumbe wa mafumbo, zenye ujumbe wa kimafumbo, yupo Roho Mtakatifu kutusaidia kuyafumbua mafumbo hayo.
Ubarikiwe.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312
Mada Nyinginezo:
https://wingulamashahidi.org/2020/07/03/kutomzuia-kutombana-mtoto-wako-ni-dhambi/
JIBU: Moja ya vitu vilivyokuwepo ndani ya hekalu la Mungu, ni kinara cha Taa, vingine vilivyokuwepo ni sanduku la agano, madhabahu ya dhahabu ya kuvukizia uvumba, na sanduku la agano.
Sasa kama tunavyojua nyumba ikijengwa na kisha haina chanzo cha Nuru ndani yake, nyumba hiyo bado haijakamilika…Hiyo ndio maana kila nyumba ikijengwa ni lazima iwekwe na mfumo wa taa ili kwamba wakati wa usiku ndani kusiwe giza shughuli zikakwama…
Na ndani ya Hema lililotengenezwa na Musa, Bwana aliagiza kuwepo na chanzo cha mwanga ndani ya lile hema, ili shughuli za kikuhani ziweze kufanyika, kama kuvukiza uvumba na kuhani mkuu kuweza kufanya upatanisho (Hivyo Bwana aliagiza pawepo kinara cha taa chenye matawi saba)….
Hali kadhalika mpaka wakati wa hekalu lilipokuja kujengwa na Sulemani jambo ni lile lile, nyumba ya Mungu haiwezi kuwa giza ndani ni lazima kuwepo na Nuru…na kwasababu nyumba ile Sulemani aliyoijenga ilikuwa ni kubwa kuliko hema la Musa, ilihitajika vinara vingi zaidi kule ndani ili pawe na mwanga wa kutosha…Hivyo vikaongezeka kutoka kinara kimoja na kuwa vinara 10…Na kila kinara kilikuwa na taa 7…Hivyo kwa ujumla ndani tu ya ile nyumba kulikuwa na taa 70..(Hivyo kulikuwa na mwanga wa kutosha).
Sasa biblia inasema sisi ni NURU ya Ulimwengu…Maana yake ni kwamba wakristo wa kweli au kanisa la Kristo linafananisha na Taa. Maana yake linamulika na kuangaza kote kote..
Mathayo 5: 14 “Ninyi ni nuru ya ulimwengu. Mji hauwezi kusitirika ukiwa juu ya mlima.
15 Wala watu hawawashi taa na kuiweka chini ya pishi, bali juu ya kiango; nayo yawaangaza wote waliomo nyumbani.
16 Vivyo hivyo nuru yenu na iangaze mbele ya watu, wapate kuyaona matendo yenu mema, wamtukuze Baba yenu aliye mbinguni”.
Hivyo basi kanisa la Kristo ndilo linalofananishwa na “kile kinara cha taa ndani ya Nyumba ya Mungu” Siri hiyo haikujulikana tangu zamani mpaka wakati Bwana Yesu alipokuja kuifichua siri hiyo tukisoma katika..
Ufunuo 1:20 “Siri ya zile nyota saba ulizoziona katika mkono wangu wa kuume, na ya vile vinara saba vya dhahabu. Zile nyota saba ni malaika wa yale makanisa saba; na vile VINARA SABA NI MAKANISA SABA”.
Unaona? Na kama ukifuatilia kwa makini maagizo Musa aliyopewa kuhusu kile kinara cha taa ni kwamba…kinapaswa kiwake daima!…(hakuna siku kinapaswa kiwe kimezima kwa kuishiwa mafuta), hivyo hilo lilikuwa ni agizo la Mungu kwahiyo wana wa Israeli walikuwa wanahakikisha kuwa hakizimi kwa gharama zozote zile…hivyo kwa mamia ya miaka viliendelea kuwaka tu hivyo hivyo…hakuna siku kilizima, wakati wa Mfalme Sulemani.
Na sisi hatupaswi Nuru yetu izime kama biblia inavyosema hapo katika Mathayo 5:16, Na nuru yetu ni matendo yetu..Yanapaswe yawe yanaangaza muda wote..Na tunapaswa tutoe mwanga mweupe na si mwekundu wala wa blue…tunapokuwa wauaji, wazinzi, watukanaji na bado tujajiita wakristo hapo ni tonatoa mianga ya rangi nyingine…
Bwana atubariki na atujalie Neema yake siku zote.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312
Mada Nyinginezo:
FAHAMU JINSI KRISTO ANAVYOPONYA WATU ROHO.
UUMBAJI BORA WA MUNGU, UPO NDANI YA MWANADAMU.
IMANI NI KUWA NA UHAKIKA WA MAMBO YATARAJIWAYO.
Je kupiga miayo ni ishara ya mapepo?
MJUMBE WA AGANO.
WANA JUHUDI KWA AJILI YA MUNGU, LAKINI SI KATIKA MAARIFA.
Ni kwanini wakati mwingine tunaona kama kuna mambo hayaendi sawa katika kanisa la Kristo, kwasababu tunafiri mambo yote yanatatuliwa na mchungaji, au mwalimu au mwinjilisti peke yake..
Kila kiungo katika mwili wa Kristo kinayo kazi yake, hivyo kimoja kisipowajibika ipasavyo ni lazima tu mapungufu yataonekana haijalishi vile vingine vitawajibika kiasi gani…
Leo hii utajiuliza ni kwanini wanawake wengi wanayo malezi mabaya ya watoto.. utakuta mwanamke anaye mtoto lakini hana heshima au maadili, au anaye mtoto lakini kichwani pamejaa miziki ya kidunia na wakati huo huo hajui hata mstari mmoja wa biblia..Unadhani hiyo inatokana na nini? Inatokana na mtu mmoja kushindwa kutimiza jukumu lake katika kanisa la Kristo.
Au utakuta mwanamke hamuheshimu mume wake, anajibizana naye kama mtoto, hajui kuwa ni agizo la Mungu kila mke amuheshimu mume wake, kama vile sisi tunavyomuheshimu Kristo na kila mume ampende mke wake, kama vile Kristo anavyotupenda sisi..Lakini yeye hilo si kitu kwake, anaona ni kawaida tu, na bado anafahamika kama mkristo, unadhani kilichomfanya awe na tabia hizo ni nini? ni kwasababu mtu Fulani hakutimiza jukumu lake katika kanisa, alimwachia mchungaji, au mtumishi Fulani afanye yeye kila kitu.
Au kwanini wanawake wengine, hawatulii katika shughuli zao, majumbani mwao, kinyume chake, ni kujizungusha mitaani, kutafuta habari za wengine, wanakosa staha, wanavaa mavazi yasiyo na heshima, nusu uchi wanakatiza barabarani, na bado ni waimba kwaya,…Unadhani hiyo inatokana na nini wakati mwingine? Ni kwasababu mtu Fulani hakutimiza jukumu lake katika mwili wa Kristo..
Paulo alimwandikia Timotheo maneno haya, akamwambia..
Tito 2:3 “Vivyo hivyo na wazee wa kike wawe na mwenendo wa utakatifu; wasiwe wasingiziaji, wasiwe wenye kutumia mvinyo nyingi, bali wafundishao mema;
4 ILI WAWATIE WANAWAKE VIJANA AKILI, wawapende waume zao, na kuwapenda watoto wao;
5 na kuwa wenye kiasi, kuwa safi, kufanya kazi nyumbani mwao, kuwa wema, kuwatii waume zao wenyewe; ili neno la Mungu lisitukanwe”.
Unaona hapo biblia inaeleza wazi kabisa huduma ya mwanamke mzee ni ipi kanisani…Kumbuka mwanamke mzee sio lazima awe ni mzee kikongwe, lakini walau mwanamke ambaye ameshafikia umri wa makamo, ameshapitia mambo mengi hususani katika ndoa, anajua jinsi gani ya kuishi na mume katika Kristo..
Ikiwa wewe ni mmojawapo na upo katika kanisa, basi fahamu kuwa unalo jukumu zito la kuwasimamia ipasavyo wanawake vijana, ukijionyesha kwanza wewe mwenyewe kama kielelezo, kwa mwenendo wako wa utakatifu na tabia. Kisha ndio uwafundishe na kuwasimamia mabinti, na wanawake vijana jinsi ya kuishi kama mwanamke wa Kikristo..
Vinginevyo usipofanya hivyo, ujue kuwa jina la Mungu linatukanwa kwa ajili yako.
Hi ni huduma kubwa sana katika kanisa, lakini cha kushangaza ni kwamba mwanamke huyu huyu mzee na yeye anataka awe mchungaji kwasababu anaona huduma aliyopewa kama vile ni ndogo haijulikani.. Hafahamu kuwa hata katika kanisa wanawake huwa ndio wengi kuliko wanaume, hivyo kama huduma basi yeye ndio mwenye huduma kubwa ya kuwaangalia watu kuliko mwanaume, lakini hilo halitaki, anataka yeye naye asimame mimbarani, ahubiri kama askofu mkuu Fulani, au mwalimu Fulani au nabii fulani..Na matokeo yake ndio unakuta migogoro mingi ya kifamilia mara mwanaume huyu kagombana na mkewe kwasababu hamuheshimu mara Yule kapigwa na memewe n.k..mwisho wa siku jina la Mungu linatukanwa kwasababu tu kiungo Fulani kanisani kilishindwa kutimiza kusudi lake.
Ikiwa wewe ni mama, leo hii tambua jukumu lako. Na ufahamu kuwa Kristo anaiheshimu sana huduma yako kama tu anavyoliheshimu lile la mchungaji, na askofu…na kama utafanya vizuri ina thawabu kuliko hata hizo zinazoonekana ni kubwa kuliko nyingine.
Bwana akubariki.
Shalom
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312
Mada Nyinginezo:
NAFASI YA MWANAMKE KATIKA KANISA
JE NI DHAMBI KUWA NA MAHUSIANO KABLA YA NDOA?
MAMBO YA KUJIFUNZA KATIKA WARAKA WA PILI WA YOHANA.
TUJIFUNZE JAMBO KWA WANAWAKE HAWA WAWILI:
USHAURI KWA MWANAMKE WA KIKRISTO.
Shalom, karibu tujifunze Biblia…
Nimewahi kukutana na watu kadha wa kadha ambao ukijaribu kuwaeleza tu habari za msalaba na wokovu ulioletwa na mwokozi wetu Yesu Kristo, wanasema Bwana Yesu alikuwa ni mzungu, hivyo hawawezi kumfuata mzungu, wala dini iliyoletwa na wazungu…Huko ni kutawaliwa na wazungu na wanahitimisha kwa kusema kwanini sisi waafrika tusidumishe Imani zetu, kwanini mpaka tuige vitu tulivyoletewa na wazungu? Kwanini tusifuate vya kwetu, huo ni ukoloni mamboleo?..kwanini hatujikubali?.
Hii ni hoja kubwa sana ambayo inawasumbua watu wengi….. na inatokana na kutojiamini na uchungu moyoni…Sasa kabla ya kwenda kwenye swali letu la msingi hapo juu linalouliza “Je Bwana Yesu alikuwa ni mzungu au la!” hebu tutafakari kwanza vipengele vifuatavyo.
Mtu unayehoji kwamba “hatupaswi kufuata kitu chochote cha mzungu” bali tudumishe vya kwetu…basi anapaswa akatae vyote vilivyoletwa na watu hao pia wa magharibi bila kuacha hata kimoja…ikiwemo simu anayoitumia, asiitumie tena, nguo anazovaa asizivae tena (kwasababu hata nguo anazovaa zimetengenezwa na viwanda vya hao hao anaowaita wazungu)..hivyo anapaswa aendelee kuvaa mavazi yake ya asili waliokuwa wanavaa waafrika wa zamani kama ni Kamba au makuti au nyuzinyuzi.
Hali kadhalika hapaswi kuishi kwenye nyumba za kisasa zenye umeme, kwasababu hata huo mfumo wa ujenzi ni kutoka kwa hao hao anaowaita wazungu na umeme pia, hapaswi kutumia dawa ya meno, pasi, hatakiwi kutumia hata trekta kulimia, hapaswi pia kuangalia wala kutumia TV, hapaswi pia kutumia jiko la gesi, wala sufuria,wala hapaswi kumiliki gari wala chombo chochote cha usafiri wa moto kwasababu vyote vimeletwa na hao hao anaowaita wazungu, akitaka kusafiri kutoka mji mmoja kwenda mwingine hana budi kutumia punda…na pia hapaswi kwenda hospitali yoyote wala kutumia aina yoyote ya matibabu ya kisasa na mwisho hapaswi kupeleka Watoto wake shule….Kama hivyo vyote atakuwa amefanikiwa kuacha kuvitumia basi atakuwa sio mnafiki kuikataa pia na Imani iliyoletwa na wazungu…lakini kama hawezi kuacha hivyo vyote na anavipenda basi atakuwa ni MNAFIKI kuchukia Imani ambayo imeletwa na hao anaowaita Wazungu, kwa kisingizio kwamba imeletwa na watu weupe!.
Sasa baada ya kutafakari hayo twende mbele Zaidi….
Ni ukweli usiopingika kwamba Imani ya Kikristo iliingia barani Afrika kupitia Wamisionari waliotoka nchi za Ulaya…Hao wamisionari hawakuwa waafrika bali walikuwa watu weupe (wazungu)….kwa njia yeyote ile waliyokuja nayo huku, lakini mwisho tunajua kuwa ilikuwa ni mpango wa Mungu wao kufika huku kuleta Habari za Mwokozi.
Sasa swali la msingi la kujiuliza ni kwamba hawa Wazungu/wamisionari je waliitolea wapi Imani ya Kikristo?…Kama unasoma biblia utakuwa unalo jibu tayari kwamba Imani ya kikristo chanzo chake ni Taifa la Israeli. Taifa la Israeli ndio taifa pekee ambalo Mungu alilichagua liwe mwanzo wa kupitisha kusudi lake hapa duniani… Hivyo hilo pekee ndio lilikuwa taifa teule la Mungu…na mataifa mengine yaliyosalia duniani yaliitwa “MATAIFA”….sasa hili neno “mataifa” ni neno la ki-ujumla ambalo lilikuwa linawakilisha makundi ya nchi zote ulimwenguni mbali na Israeli ambazo hazikuwa zinamwabudu Mungu mmoja wa mbingu na nchi (Yehova)…Ni Taifa moja tu pekee ambalo ndilo lililokuwa linamwabudu Mungu wa mbingu na nchi kulingana na jinsi yeye anataka!…na hilo si lingine Zaidi ya Taifa la Israeli.
Na waisraeli hawakuwa wazungu!…walikuwa ni watu wanaokaribia kufanana sana na “waarabu”.. Hivyo kama wewe unajua vyema jamii za watu unaweza kujua tofauti ya mzungu na mwarabu kimwonekano, hawafanani, na hata waarabu si weupe kama wazungu! Na hawana macho ya blue kama wazungu!, na nywele zao ni nyuesi na si za gold kama za wazungu!….
Sasa mwokozi wetu Yesu Kristo ndiko alikozaliwa (yaani huko Israeli) hivyo kwa mwonekano alikuwa anafanana na hawa wa Israeli…Na waisraeli hawakuwa watu hodari wa kimaendeleo wakati wa mwokozi kuishi ulimwenguni..ndio maana utaona wakati Kristo akiwa duniani, Warumi(ambao sasa ndio walikuwa wazungu) walikuwa waitawala Israeli. Na Mungu aliwafanya Israeli kuwa wadogo mpaka kufikia hatua ya kutawaliwa, kutoka na makosa yao waliomuasi. Hivyo hawakuwa na maendeleo yoyote ya kushangaza ukilinganisha na mataifa mengine ya kizungu kama Rumi na Ugiriki(Uyunani).
Sasa tukirudi kwenye swali letu.. “je Bwana Yesu alikuwa ni mzungu?”..Jibu utakuwa umelipata kulingana na maelezo hayo hapo juu….hakuwa mzungu bali mtu wa Taifa la Israeli..Waliokuwa wazungu ni wakina Pilato, Herode ambao ndio walikuwa Warumi.
Kwahiyo kimwonekano Kristo hakuonekana kama Mzungu bali kama Mwisraeli…..
Sasa hawa wazungu ilitokeaje wakamwamini Bwana Yesu ambaye hakuwa mzungu?…Habari hizo unaweza kuzipata katika historia, lakini kwaufupi ni kwamba nao pia walipelekewa habari za Yesu kama sisi tu tulivyoletewa . Wale waliozipokea ipasavyo walijua kabisa kwamba na wao ni watu wa Mataifa ambao hawakustahili kuitwa watu wa Mungu lakini kwa kupitia mkombozi mmoja Yesu Kristo waliingizwa katika neema hiyo..ambayo iliwastahili Waisraeli tu peke yao!.
Hivyo wao nao wakatuletea sisi Injili, kwasababu huku Afrika kulikuwa ni giza nene, watu walikuwa wanaabudu miungu na imani potofu….na katika zama hizi za siku za mwisho, mambo yamebadilika ni wakati wa Afrika sasa nao kuipeleka Injili kwa wazungu kwasababu huko kwao sasa kumeoza, kile kizazi kilichomtumaini Mungu kimeshaondoka kimezuka kizazi cha watu wasiomwogopa Mungu huko kwao ndio kitovu cha watu mashoga, watu wanaokufuru, watu wanaotembea uchi mabarabarani n.k. Hivyo injili inahitajika sana sasa kwa wazungu Zaidi ya kwa waafrika, kama wao walivyotuletea ni wakati sasa wa sisi kuwapelekea wao watubu, wamwamini mwokozi.
Kwahiyo ndugu, kamwe usikae uliingize suala la wokovu wa mwokozi wetu Yesu Kristo na “Rangi” Mungu wa Israeli hana ubaguzi wa rangi na anaabudiwa na watu wa rangi zote…ili awe Mungu wa mbingu na nchi ni lazima apatikane kwa watu wote…Ukiona unamwabudu Mungu anayepatikana Afrika tu, au anayepatikana Ulaya tu!…basi huo ni uthibitisho tosha kwamba huyo sio Mungu wa kweli wa mbingu na nchi..Kwasababu Mungu wa kweli wa dunia yote ni lazima aabudiwe na kutangazwa ulimwenguni kote na watu wa rangi zote!.
Na usisahau jambo hili mwokozi Yesu Kristo, alikufa, akafufuka na akapaa mbinguni na atarudi tena mara ya pili, hivyo kama umeisikia injili na bado hujamwamini, au ulikuwa unafikiri labda ukimwamini utakuwa umetimiza matakwa ya watu weupe, au ni ukoloni!..basi hilo wazo lifute kuanzia leo… hukumu inakuja, hivyo tubu leo kama hujatubu,vilevile ukabatizwe ili dhambi zako ziondolewe na Bwana atakupa kipawa cha Roho wake mtakatifu atakayekusadia kushinda dhambi na kukusaidia kuelewa mambo ambayo ulikuwa huyaelewi kuhusu yeye.
Bwana atubariki.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312
Mada Nyinginezo:
DHIKI KUU INAKUJA NA UNYAKUO UPO KARIBU.
JE! PAKA KULIA USIKU NI ISHARA YA UCHAWI?
Je! Ni kweli kuna samaki mtu (Nguva) Baharini.
Tofuati kati ya Myahudi, Mwisraeli na Muebrania ni ipi?
KWA VILE ALIVYOKUWA MTU WA HAKI.
KRISIMASI (CHRISTMAS) NI NINI? JE IPO KATIKA BIBLIA?
Makedonia ni mojawapo ya mataifa tunayoyasoma sana katika biblia, hususani katika ziara za mtume Paulo za kuhubiri injili katika mataifa. Makedonia ni taifa ambao mpaka sasa lipo, na linajulikana kwa jina hilo hilo makedonia (kwa kiingereza Macedonia), taifa hili lipo kusini mashariki mwa bara la Ulaya.
Tunaweza kusoma habari zake, katika biblia na kuona kuwa taifa hili lilikuwa ni miji mikuu mitatu, nayo ni Filipi, Beroya na Thesalonike, ambayo Mtume Paulo aliiendea kuhubiri injili. Kabla ya kupita na kwenda katika taifa lingine lijulinalo kama Akaya mji wa Athene.
Sifa mojawapo ya mji huu ni kwamba watu wake walikuwa na kiu sana ya kujua habari za Mungu tofauti na watu wa miji mingine, licha ya kwamba walikuwa ni maskini kuliko makanisa mengine,(soma 2Wakoritho 8:1-3) jambo ambalo lilipelekea mpaka Paulo kuzuiliwa kwanza na Roho Mtakatifu kuhubiri katika miji mingine iliyokuwa Asia ndogo wakati ule, kama vile Galatia na Frigia, Utasoma hilo katika..
Matendo 16:6 “Wakapita katika nchi ya Frigia na Galatia, wakikatazwa na Roho Mtakatifu, wasilihubiri lile neno katika Asia.
7 Walipofika kukabili Misia wakajaribu kuenda Bithinia, lakini Roho wa Yesu hakuwapa ruhusa,
8 wakapita Misia wakatelemkia Troa.
9 PAULO AKATOKEWA NA MAONO USIKU; ALIMWONA MTU WA MAKEDONIA AMESIMAMA, AKIMSIHI, NA KUMWAMBIA, VUKA, UJE MAKEDONIA UTUSAIDIE.
10 Basi alipokwisha kuyaona yale maono, mara tukataka kutoka kwenda Makedonia, kwa kuwa tuliona hakika ya kwamba Mungu ametuita tuwahubiri Habari Njema”.
Hivyo nasi pia tunalo la kujifunza juu ya watu hawa wa makedonia,. Kwamba tuwe na bidii katika kumtafututa Mungu, na pia tuwe watu wa kupenda kuyachunguza maandiko kwanza kabla ya kubisha pale tunapohubiriwa mfano wa watu wa Beroya walivyofanya (Maendo 17:10). Ndivyo Mungu atakavyotuona na sisi tunastahili kupokea neema ya wokovu.
Ubarikiwe.
Mada Nyinginezo:
VUKA UJE MAKEDONIA UTUSAIDIE.
WINGU KUBWA LA MASHAHIDI.
JE KUNA UISLAMU KATIKA BIBLIA?
JE! UMEPOKEA KWELI ROHO MTAKATIFU?
KUMBUKA, VIVUKO VYA YORDANI VINAKUNGOJA MBELENI.
UFALME WAKO UJE.
IKIMBIE DHAMBI KWA GHARAMA ZOZOTE ZILE!
Kuna wakati Israeli ilikuwa inapitia majira tofauti tofauti, Si kila wakati Mungu alikuwa anazungumza nao, ana kwa ana au kwa kupitia manabii au waamuzi, hapana Kuna wakati Mungu alikuwa hasemi chochote kabisa kwa kipindi fulani, Lakini hiyo haikumaanisha kuwa Mungu amewaacha au hafuatilii mienendo yao kabisa, bali ni jinsi tu yeye, alivyopenda na anafanya hivyo wakati mwingine ili tu kupima uaminifu wa watu wake.
Kipindi kimojawapo kilikuwa ni kile cha Nabii Samweli, na kingine ni kipindi cha kati ya Nabii Malaki hadi wakati wa Yohana mbatizaji ambapo inakadiriwa ni Zaidi ya miaka 300. Sasa kwa mfano tukirudi katika kipindi cha Samweli, tunaona ulifika wakati biblia inasema Neno la Bwana lilikuwa ni adimu sana, na kulikuwa hakuna mafunuo Dhahiri, hii ikiwa na maana kuwa Mungu hakuwa anajifunua moja kwa moja kwa watu wake, aidha kwa kupitia manabii au makuhani, au kitu chochote tusome..
1Samweli 3:1 “Basi, mtoto Samweli akamtumikia Bwana mbele ya Eli. Na neno la Bwana lilikuwa adimu siku zile; hapakuwa na mafunuo dhahiri.”
Unaona, sasa matokeo yake ni kuwa watu wengi walipoona hivyo, kwanini Mungu hasemi chochote, hazungumzi chochote, hapigi popote, wakadhani kuwa hawatazamwi mienendo yao na matendo yao, hapo ndipo baadhi ya watumishi wake wakaanza kupoa na kukengeuka mpaka kufikia hatua ya kufanya mambo ya ajabu madhabahuni pake…Kama vile tu ilivyo leo..
Mfano ukisoma pale utaona kulikuwa na Watoto wawili wa Kuhani aliyeitwa Eli, ambaye wa kwanza aliitwa Hofni, na wa pili aliitwa Finehasi, hawa walifikia hatua ya kuidharau sadaka ya Bwana,kwa kuchukua kiwango ambacho hawajaamuriwa kwa nguvu na Zaidi ya yote walikuwa wanazini na wanawake ambao walikuwa wanatumika katika nyumba ya Bwana.. Hofu ya Mungu ilikuwa imeshaondoka ndani yao, kwasababu tu waliona Mungu hafanyi lolote, wala hachukui hatua yoyote kwao..
Lakini siku ya siku ilipofika ya Mungu kuanza kusema tena Dhahiri..Hapo ndipo walipojua Mungu tangu zamani alikuwa anawatazama, na kuwalipa mema wale waliostahili mema, na mabaya wale waliostahili mabaya..
Siku moja kijana Samweli alipokuwa amelala usiku Bwana alimtokea na kumwambia..
1Samweli 3:11 “Bwana akamwambia Samweli, Angalia, nitatenda tendo katika Israeli, ambalo kila atakayelisikia masikio yake yatamwasha.
12 Siku hiyo nitayatimiza maneno yale yote niliyoyasema juu ya Eli katika habari za nyumba yake, tangu mwanzo hata mwisho.
13 Kwa maana nimemwambia ya kwamba nitaihukumu nyumba yake milele, kwa ajili ya ule uovu alioujua; kwa kuwa wanawe walijiletea laana, wala yeye hakuwazuia.
14 Na kwa hiyo nimeapa juu ya nyumba ya Eli, ya kwamba uovu wa nyumba ya Eli hautasafika kwa dhabihu wala kwa sadaka hata milele”.
Ujumbe huo ulikuwa ni mzito sana hata kwa Samweli ambaye haumuhusu, itakuwaje kwa wale wahusika?, Ukifuatilia Habari ile utaona ndani kipindi kifupi sana, zaidi ya watu elfu 80 walikufa kwa kupigwa na Mungu.. ikiwemo wale wana wawili wa Eli.
Hata sasa, upo wakati utaonekana kama Bwana amekaa kimya (Nikimaanisha kwa mapigo, yanaonekana kama adimu), lakini hilo lisitufanye tudhani kuwa haoni yanayoendelea katika kanisa lake..Tujue kuwa lipo kusudi analitekeleza na mojawapo ndio hilo la kuwapima walio waaminifu ni wapi …
Lakini wakati utafika, ambao utakuja kwa ghafla, atazungumza hukumu zake, lakini atakapozungumza safari hii ujue kuwa sikio lako litawasha . Leo hii unapata ujasiri wa kuvaa nusu uchi kanisani, unadhani Mungu kuwa kimya, inainajisi madhabahu yake ni kwamba anapendezwa na wewe, unashiriki meza ya Bwana halafu ukitoka hapo unakwenda kuzini, unadhani Mungu hakuoni.
wewe ni mchungaji lakini kuzini na washirika wako mfano wa Hofni na Finehasi ni kitu cha kawaida kwako, kwa kuwa huoni kitu chochote kikitokea katika Maisha yako, sasa unadhani ndivyo itakavyokuwa hivyo siku zote.
Unafanya mambo ya ajabu madhabahuni pa Mungu, wala huogopi, unafanya comedy, na siasi, ili upendwe na watu ukijiona wewe ni mjanja, nataka nikuambie wakati utafika wa mwenye madhabahu kuzungumza..
Wengine wanasema tunaishi chini ya neema, Mungu hawezi kuwaadhibu watu aliowakomboa kwa damu ya mwanawe.. Ndugu, Kasome Habari za Hanania na Safira na mke wake, halafu useme lile ni agano la kale au jipya?..Watu wale walikufa kwa kutotimiza tu viapo vyao kwa Mungu vya kumtolea sadaka, jiulize wewe ambaye ni mzinzi, halafu unashiriki meza ya Bwana, utakuwaje?
Tufahamupo hukumu za Mungu, basi tuchukue tahadhari kabla mabaya hayajatukuta mimi na wewe. Nyakati hizi ni za nyakati za hatari.
Maran Atha!
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312
Mada Nyinginezo:
https://wingulamashahidi.org/2020/07/03/kutomzuia-kutombana-mtoto-wako-ni-dhambi/
Uovu unapoongezeka sana na kufikia kiwango ambacho watu hawataki tena kubadilika..biblia inatuambia Mungu huwa anaachilia nguvu ya upotevu ili waendelee kuuamini UONGO. Ile nguvu ya kumfanya mtu aone njia anayoiendea sio sawa inaondoka ndani yake na inakuja nguvu nyingine mpya ya kumfanya aone na kuamini asilimia mia kwamba yupo katika njia sahihi.
Mstari huo tunausoma katika kitabu cha..
2Wathesalonike 2:10 “na katika madanganyo yote ya udhalimu kwa hao wanaopotea; kwa sababu hawakukubali kuipenda ile kweli, wapate kuokolewa.
11 Kwa hiyo Mungu awaletea nguvu ya upotevu, wauamini uongo;
12 ili wahukumiwe wote ambao hawakuiamini kweli, bali walikuwa wakijifurahisha katika udhalimu”.
Leo tutaangalia mifano baadhi katika biblia ya watu ambao hawakutaka kudumu katika kweli na hivyo Mungu akawatumia nguvu ya kuamini uongo, ili wakaangamia katika huo.
Huyu ni mtu, Bwana alimuonya asiende kuwalaani Israeli lakini akawa hataki kusikiliza sauti ya Mungu, kinyume chake akawa analazimisha kwenda kuwalaani watu wa Mungu ili apate fedha na umaarufu kutoka kwa Mfalme wa Moabu..alionywa lakini hakusikia…matokeo yake Mungu akamwambia aende! Na yeye kudhani kwamba Mungu tayari kampa kibali alienda pasipo kujua kuwa tayari ile nguvu ya upotevu ya kuuamini uongo inampeleka pabaya…kama sio yule punda kumsaidia angeshakufa..(kasome kitabu cha Hesabu 22).
Huyu Mungu alimwonya mara nyingi sana juu ya uovu wake, ageuke atubu lakini hakusikia, mpaka ilipofika siku ambayo Mungu aliiachia nguvu ya upotevu ishuke juu yake, auamini uongo…Siku hiyo alitaka kwenda vitani na Mungu akatuma pepo la uongo liwaingie manabii wake ili wamwambie uongo…Kwani hao manabii wake kila siku walikuwa wanamwambia ukweli lakini siku hiyo waliingiwa na pepo pasipo wao kujua na kujikuta wanaona maono ya uongo, na kumpotosha mfalme..
1Wafalme 22: 20 “Bwana akasema, Ni nani atakayemdanganya Ahabu, ili akwee Ramoth-Gileadi akaanguke? Basi huyu akasema hivi; na huyu hivi.
21 Akatoka pepo, akasimama mbele za Bwana, akasema, MIMI NITAMDANGANYA.
22 Bwana akamwambia, Jinsi gani? Akasema, Nitaondoka, na kuwa pepo wa uongo kinywani mwa manabii wake wote. Akasema, Utamdanganya, na kudiriki pia; ondoka ukafanye hivyo.
23 Basi angalia, Bwana ametia pepo wa uongo kinywani mwa manabii wako hawa wote; naye Bwana amenena mabaya juu yako”.
Mfalme Ahabu akaenda kwenye vita, akiwa amedanganywa na pasipo kujua kuwa amedanganywa…na akafa!
Mfalme huyu naye njia zake hazikumpendeza Mungu..kwani aliwasumbua sana wana wa Israeli , na wakati ule ambao njaa ilipokuwa kubwa Samaria mpaka kufikia kiwango mavi ya njiwa na kichwa cha punda kuuzwa kwa bei kubwa mjini kutokana na njaa iliyosababishwa na mfalme huyu..Na ndiye aliyemdharau Mungu wa Israeli na kusema ni Mungu wa milimani na si wa nchi tambarare. Na japokuwa Mungu aliyanusuru Maisha yake mara nyingi ili atubu…lakini hakuwahi kutubu Zaidi ya yote alizidi kufanya vita na Israeli. Lakini ilifika siku moja akaugua sana, na akatuma watu wamwendee Elisha Nabii ili aulize kwa Mungu kama atapona au la!…Na kilichotokea ni nguvu ya upotevu kuachiliwa juu yake ili auamini Uongo..
Tusome..
2Wafalme 8:7 “Kisha, Elisha akaenda Dameski; na Ben-hadadi, mfalme wa Shamu, alikuwa hawezi; akaambiwa ya kwamba, Yule mtu wa Mungu amefika hapa
8 Mfalme akamwambia Hazaeli, Chukua zawadi mkononi mwako, ukaende ili kumlaki yule mtu wa Mungu, ukamwulize Bwana kwa kinywa chake, kusema, Je! Nitapona ugonjwa huu?
9 Basi Hazaeli akaenda kumlaki, akachukua zawadi mkononi mwake, za kila kitu chema kilichopatikana Dameski, kiasi cha mizigo ya ngamia arobaini, akaenda, akasimama mbele yake akasema, Mwana wako Ben-hadadi, mfalme wa Shamu, amenituma kwako, kusema, Je nitapona ugonjwa huu?
10 Elisha akamwambia, Enenda, ukamwambie, BILA SHAKA UTAPONA; LAKINI BWANA AMENIONYESHA YA KWAMBA BILA SHAKA ATAKUFA.
…………..14 Ndipo akamwacha Elisha, akarudi kwa bwana wake; naye akamwambia, Elisha alikuambiaje? Akajibu, Aliniambia ya kuwa BILA SHAKA UTAPONA.
15 Ikawa siku ya pili yake, akatwaa tandiko la kitanda, akalichovya katika maji, akalitandaza juu ya uso wake, HATA AKAFA. Na Hazaeli akatawala badala yake”.
Umeona hapo?..Bwana alimwonyesha Elisha kuwa huyo mfalme atakufa lakini alimpa maagizo Elisha amdanganye Ben-hadadi kwamba atapona lakini kumbe atakufa!..
Hiyo ni baadhi ya mifano tu!, ndugu mpendwa saa tunazoishi ni za hatari sana….Tujitahidi sana tuupende na kuufuata ukweli ambao upo katika Neno la Mungu, ili Nguvu hii ya upotevu iliyoachiwa duniani sasa ya kuuamini uongo isije ikatumeza, na ghafla tukajikuta kwenye ziwa la Moto.
Hususani katika kipindi hichi cha siku za Mwisho, uongo umezagaa kila mahali…
Nimewahi kuona muhubiri maarufu akihubiri na kutetea dhambi madhabahuni, hali kadhalika nimeona mwingine akitumia maandiko kabisa kusapoti uvaaji wa suruali na vimini, na kama mtu huyajui maandiko vizuri anakuchukua!..kama ni wa kusoma tu mstari mmoja bila kujua mingine unakwenda na maji! Na maelfu tayari wamechukuliwa!. Hiyo ni mifano tu ya nguvu ya upotevu iliyoachiliwa nyakati hizi ili watu waamini uongo.
2Timotheo 3:13 “lakini watu wabaya na wadanganyaji wataendelea, na kuzidi kuwa waovu, wakidanganya na kudanganyika”.
Tutubu dhambi, na kujitenga na uovu kwa kadiri tuwezavyo..Bwana atusaidie, tukimwamini yeye, tukimtegemea yeye ni mwaminifu, hawezi kutuacha tukadanganyika au kuchukuliwa na hizo nguvu..Hivyo ni wajibu wetu kumpenda Mungu siku zote kwa nguvu zetu zote, kwa roho zetu zote na kwa akili zetu zote.
Bwana atubariki.
Maran atha!
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312
Mada Nyinginezo:
1 Wathesalonike 5:1 “Lakini, ndugu, kwa habari ya NYAKATI NA MAJIRA, hamna haja niwaandikie.
2 Maana ninyi wenyewe mnajua yakini ya kuwa SIKU YA BWANA yaja kama vile mwivi ajavyo usiku”.
Shalom.
Katika mistari hiyo miwili, yapo mambo mawili pia ninataka uyaone. Jambo la kwanza ni “Nyakati na Majira” na Jambo la pili ni “Siku ya Bwana”..Mtume Paulo ameitenganisha hiyo mistari miwili, kwasababu inazungumziwa vitu viwili tofauti,
Kwamfano tukianzana na huo mstari wa Kwanza, unazungumzia Nyakati na Majira ya kurudi kwake Bwana, lakini huo wa pili unazunguzia siku yenyewe ya Bwana itakavyokuwa..
Sasa mpaka mtu anaposema kwa habari ya nyakati na majira sina haja ya kuwaandikia..anamaanisha kuwa suala la majira na nyakati ambayo Kristo atarudi ni jambo ambalo kila mtu anajua, sio siri lipo wazi!, limeshaelezwa kila mahali, sio jambo jipya..na ndio maana hawezi kuandika tena kuwakumbusha watu..
Nataka nikuambie ndugu yangu ikiwa wewe ni mkristo na mpaka sasa bado hujui majira na nyakati za kurudi kwa Yesu duniani kulinyakuwa kanisa lake, basi ujue kuwa kuna tatizo kubwa sana katika Imani yako tena sana ambalo utanatakiwa ulichukulie ‘seriously”…
Biblia imetuweka wazi kabisa na kutuambia tukishaona majira Fulani au nyakati zimebadilika basi tujue ndani ya hicho kipindi siku yoyote Kristo anarudi..Ili kuelewa vizuri tafakari mfano huu,
Leo hii labda unatafuta Kazi mahali fulani, kwenye shirika Fulani la utafiti wa kilimo, halafu ukapata, ukaitwa kwenye interview, ukafanikiwa kupita, lakini wakakwambia kazi yetu rasmi itaanza kipindi cha msimu wa masika, hivyo tutakupigia simu wakati huo ukifika hakikisha tu unakuwa hewani wakati wote, ili tusikukose pindi kazi zitakapoanza. Lakini ukiangalia wewe leo hii upo mwezi wa 9 na umeshajua masika huwa inaanza kuanzia mwezi wa 2-5 mwakani..
Sasa kwa namna ya kawaida hichi kipindi cha katikati utakuwa kawaida tu, lakini itakapofika mwakani kuanzia mwezi huo wa 2 hadi wa 5, utakuwa makini sana, utakuwa karibu na simu yako kwasababu unajua wakati wowote, utapigiwa simu ukaanze kazi,.Unaona hapo! hujapewa tarehe lakini umepewa majira na Nyakati..inaweza ikawa mwezi wa pili mwanzoni, au wa tatu mwishoni, au wa nne katikati hujui..bali utajiweka tayari muda wowote..
Vivyo hivyo na sisi wakristo, tumepewa majira ya kurudi kwa Bwana Yesu, lakini hatujapewa siku, wala saa. Na majira yenyewe ndio haya tunayoyaishi sasa.. Ndugu katika wakati ambao tungepaswa tuwe makini sana na wokovu wetu basi ni katika majira haya.. Kwasababu Bwana Yesu alituambia, mtakapoanza kuona milipuko ya magonjwa yenye mfano wa Tauni yanaipiga dunia (Corona) Luka 21:11 basi mjue yupo mlangoni, mtakapoona matetemeko ya nchi, basi mjue mpo ndani ya wakati huo, mtakapoona wimbi la manabii wa uongo wengi wakizuka duniani, mtakapoona watu wanapenda anasa kuliko kumpenda Mungu, watu wanapenda fedha, basi mjue hayo ndio majira yenyewe.
Mtakapoona maasi yanayongezeka kwa kasi (ushoga na uuajji), upendo wa watu wengi kupoa, kutokea kwa wimbi kubwa la watu wenye kudhihaki wakisema mbona huyo Yesu haji, dunia ipo vilevile wakati wote,(2Petro 3:3) basi tujue tupo katika hayo majira kabisa…
Na ndio pale sasa tukirudi katika ule mstari wa Pili anasema..
2 Maana ninyi wenyewe mnajua yakini ya kuwa SIKU YA BWANA yaja kama vile mwivi ajavyo usiku.
3 Wakati wasemapo, Kuna amani na salama, ndipo uharibifu uwajiapo kwa ghafula, kama vile utungu umjiavyo mwenye mimba, wala hakika hawataokolewa.
Tukiwa katikati ya majira hayo, ghafula wakati wowote, muda wowote, Bwana atatokea kama mwizi ajavyo usiku.. Kwa bahati mbaya kwa upande wao watasema mbona duniani tupo salama na kuna amani, Hapo ndipo Unyakuo unapita kwa ghafla sana na kwa haraka..wafu wanafufuliwa, na watakatifu wachache sana wanatoweka duniani..
Wakati baadhi ya watu wakipigwa butwaa kufikiri ni nini kimetokea mbona watu wachache hatuwaoni duniani..(wengi watajua ni kawaida watu kupotea potea na kuja kupatikana baada ya siku/miaka kadhaa hivyo watapuuzia) hapo ndipo mpinga-kristo ataanza kufanya kazi..wakati huo dunia haitakuwa na zaidi ya miaka 7, usitamani wakati huo ukukute kwasababu kutakuwa ni vilio na kusaga meno kwa watakaobaki.
Embu jiulize, ni kitu gani kinakufanya uishi maisha ya kubahatisha-bahatisha wakati huu wa siku za mwisho? Neema tuliyonayo haitakuwa hivi sikuzote, upo wakati utatamani ungerudi siku moja nyuma utengeneze mambo yako lakini haitawezekana, wakati huo wenzako wakiwa wanakula karamu ya mwana kondoo mbinguni wewe utakuwa umebaki halafu kibaya zaidi uliujua ukweli lakini hukuukubali kwa wakati.
Ndugu tubu dhambi zako, mgeukie mkuu wa uzima YESU KRISTO, azifute dhambi zako..Achana na mambo ya ulimwengu hayakufikishi popote, wala hayakupi faida yoyote wewe mwenyewe unajua. Hivyo fanya uamuzi mwema wa kugeuka na kumfuata Yesu ili uwe na amani katika kipindi cha maisha yako ulichobakiwa nacho hapa duniani.
Ni matumaini yangu utafanya hivyo. Na Kristo awe pamoja na wewe, na pamoja na sisi sote.
Maran Atha.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312
Mada Nyinginezo:
SIKU YA UNYAKUO ITAKUKUTAJE?
Amin, nawaambia, Kizazi hiki hakitapita, hata hayo yote yatakapotimia..!!
MKUMBUKE MKE WA LUTU.
CHUKIZO LA UHARIBIFU
MAPIGO YA VITASA SABA, NA SIKU YA BWANA.