SWALI: Tukisoma Mathayo 5:19 Inasema..
“Basi mtu ye yote atakayevunja AMRI MOJA katika hizi ZILIZO NDOGO, na kuwafundisha watu hivyo, ataitwa mdogo kabisa katika ufalme wa mbinguni; bali mtu ATAKAYEZITENDA na KUZIFUNDISHA, huyo ataitwa MKUBWA katika ufalme wa mbinguni”.
Swali langu 👆Amri ndogo zinazozungumziwa hapo ni zipi? Ningependa kuzijua!
Kama kuna Amri ndogo ,bila shaka na Amri kubwa au kuu zitakuwepo pia ningependa kufahamu hilo.
Asante na Mungu awabariki kwa majibu yenu.
JIBU: Ukisoma maneno ya juu yake yaliyotangulia utaona anasema.. sikuja kuitangua torati bali kuitimiliza, Hii ikiwa na maana kuwa vipo vipengele vya torati ambavyo havikukamilika, au havikueleweka kwa wengi ndio sasa yeye akaja kuviweka sawa, na kuvimalizia..
Sasa kwa wayahudi (Yaani mafarisayo na waandishi) waliona kama ni sheria mpya Yesu anawaletea watu, sheria ambazo Musa hakuziandika, visheria vidogo vidogo ambavyo si lazima mtu kuvishika, japo vinaelezea uhalisia.
Kwa mfano Musa aliwaagiza wasizini, lakini jambo lingine lolote linalohusiana na uzinzi, kama vile kutazama pornography, au kufanya masturbation ni sawa, lakini Yesu alipokuja na sheria mpya kwamba kila amtazamaye mwanamke kwa kumtamani ameshakwisha kuzini naye.. Waliona kama ni jambo la ziada (kama sheria ndogo tu), lakini hawajui kuwa mtu ambaye atazishika hizo ndizo zitakazomfanya awe mkubwa sana katika ufalme wa mbinguni.
Vilevile Musa alisema usiue, lakini Bwana Yesu akasema mtu atakayemwonea ndugu yake hasira tayari ni muuaji. Hivyo hatupaswi kuwekeana vinyongo sisi kama ndugu, haijalishi tumeudhiana sana kiasi gani. Sasa ikitokea unapuuzia maneno haya, ujue kuwa katika ufalme wa mbinguni unaonekana ni mdogo sana, haijalishi kuwa hujawahi kufikiria hata kuua.
Musa alisema Jicho kwa jicho, na jino kwa jino, lakini Yesu alisema, tusishindane na watu waovu, mtu akupigaye shavu la kuume mgeuzie na la kushoto.
Musa alisema, usiape uongo, lakini Yesu alisema usiape kabisa kwa kiapo chochote.
Alisema tena mpende jirani yako, mchukie adui yako, lakini Yesu alisema wapendeni adui zenu waombeeni wanaowaudhi..n.k n.k.
Sasa amri kama hizo za Yesu zilionekana ni ndogo hivyo zikadharauliwa, wengi wakawa hawazishiki, ni sawa na leo hii tu, mtu akuambie umuombee adui yako, ni jambo ambalo unaweza ukalidharau, na ndio maana huwezi kulisikia kwenye vinywa vya watumishi, vilevile ni ngumu kuviona watu wakiviishi, zinapuuziwa lakini ndizo zinazotupa ukubwa mbinguni.
Ndio maana Yesu alisema pale juu.. “Haki yenu isipozidi hiyo haki ya waandishi na Mafarisayo, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni”(Mathayo 5:20).
Akiwa na maana tukiyatenda tu yale ambayo watu wa dini wanayatenda kwa desturi na mazoea, hatuna cha ziada ndani yetu, tujue kuwa mbinguni hatutaingia.
Nasi tunafundishwa, tuyashike kwa kuyaishi na kuyafundisha, sana hayo maagizo ya Yesu, ambayo ndio yanayokamilisha torati nzima. Soma kitabu Mathayo sura ya 5 mpaka ya 7 utapata maagizo hayo yote kwa urefu.
Bwana akubariki.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,
Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
Jiunge na kundi letu la mafundisho ya Biblia whatsapp kwa kubofya hapa > Group-whatsapp
Mada Nyinginezo:
Shalom, nakukaribisha katika kuyatafakari maneno ya uzima, biblia inatuambia..
Mithali 16:31 “KICHWA CHENYE MVI NI TAJI YA UTUKUFU, Kama kikionekana katika njia ya haki”.
Wengi wetu tunatafuta wokovu ili tu tuende mbinguni, tunadhani wokovu ni kumkiri tu Yesu na kubatizwa, basi imeishia hapo, tunachosubiria tu ni kufa na kwenda mbinguni.. Ndugu Mawazo kama hayo ndiyo yanatufanya kila siku tuwe watu wa kulegea legea watu wa kusubiri subiri,tukisema siku moja wataokoka, siku tunayokaribia kufa, siku ambayo tukishatimiza malengo yetu ndio tutakayomtumikia Mungu, hatujui kuwa kuchelewa kwetu kunatupotezea nafasi nyingi na kubwa sana mbinguni.
Ndugu yangu, maisha ya mwilini ni kivuli tosha cha maisha ya rohoni. Kama vile katika mwili kuna hatua, ya utoto, utu uzima na uzee, na kwamba ili mtu afikie ile ya mwisho ni lazima azipitie hizi za kwanza zote, vivyo hivyo na rohoni..
Kumbuka Uzee siku zote una kibali, una heshima, na una utukufu,
Biblia inasema..
Walawi 19:32 “Mwondokeeni mtu mwenye mvi; heshimuni uso wa mtu mzee; nawe mche Mungu wako, Mimi ndimi Bwana”.
Unaona na utukufu wake unadhihirishwa kwa zile mvi zinazotokea juu ya kichwa chake. Hali kadhalika rohoni, kwa jinsi mtu anavyokua kiroho, anavyodumu katika wokovu, anavyomtumikia sana Bwana, ndivyo mvi zake zinavyoongezeka kidogo kidogo, na kwa jinsi atakavyoendelea kung’ang’ana na Bwana atafikia hatua kichwa chake chote kinajaa mvi, kinakuwa cheupe pe chote.
Ukishafikia hatua hiyo rohoni, ujue wewe ni mtu ambaye utakuwa karibu sana na Mungu utakapofika mbinguni.
Ukisoma kitabu cha Ufunuo, utawaona kuna wazee 24 mbinguni, Wale ni malaika wa Mungu, ambao wanafanana na wanadamu wazee, utajiuliza ni kwanini Mungu kawaweka pale kama wazee na si vijana au watoto ili wakizunguke kiti chake cha enzi, tena wakiwa katika idadi yao hiyo ndogo ya 24?. Hiyo ni kuonyesha kuwa watu wa namna hiyo, ndio watakaokuwa karibu sana na Mungu hata wakati ule ukifika.
Ufunuo 4:3 “na yeye aliyeketi alionekana mithili ya jiwe la yaspi na akiki, na upinde wa mvua ulikizunguka kile kiti cha enzi, ukionekana mithili ya zumaridi.
4 Na viti ishirini na vinne vilikizunguka kile kiti cha enzi, na juu ya vile viti naliona wazee ishirini na wanne, wameketi, wamevikwa mavazi meupe; na juu ya vichwa vyao walikuwa na taji za dhahabu”.
Na kama tunavyojua ili kumtambua mzee utaona mvi nyeupe katika kichwa chake. Katika biblia tunamwona Bwana wetu Yesu Kristo akiwa kama mzee wetu wa kwanza rohoni mwenye nywele hizo nyeupe..
Ufunuo 1:14 “Kichwa chake na nywele zake zilikuwa nyeupe kama sufu nyeupe, kama theluji; na macho yake kama mwali wa moto”;
Sasa kama tulivyosema, mpaka mtu afikie hatua ya uzee, ni sharti kwanza apitie utoto na ujana,..Vivyo hivyo rohoni ili tufikie ukomavu Mungu anaoutarajia kwetu hatuna budi kuukulia wokovu vya kutosha angali tukiwa hapa hapa duniani.
Inashangaza kuona mtu anayachukulia maisha yake ya rohoni, kirahisi rahisi tu, leo inapita bado yupo katika dhambi, kesho nayo hivyo hivyo, mwezi unapita, miaka inapita, anasikia tu injili anapuuzia, bado hajali maisha yake ya milele yatakuja kuwaje huko atakapokwenda, yeye anajitaabisha tu na haya maisha ya kitambo ya miaka 80, lakini yale ya mabilioni ya miaka hayaangalii. Anadhani kule ni kufa na kuingia tu, hajua kuwa zipo nafasi na vyeo, ambavyo si watu wote watapewa na Mungu.
Mwingine atasema ameokoka, lakini miaka nenda rudi, bado ni mchanga kiroho, hakui yupo pale pale, maisha yake hayana ushuhuda, ukimuuliza ni nini umefanya kwa Mungu wako, hana, yeye ni kusikiliza tu, basi, akidhani ndicho Mungu alichotuitia hapa duniani.
Tunapaswa tukifika kule tutambuliwe kwa mvi zetu rohoni, tumemtumikia Mungu wetu kweli kweli, sio tunatambuliwa kama vitoto vichanga tena.
Unapoyasikia maneno haya, usiyapuuzie, kumbuka unapaswa uwe ndani ya Kristo ukimtumikia kwa muda wa kutosha ukiwa hapa duniani, ili ujijengee daraja zuri kule unapokwenda, usidhani wokovu ni kuamini tu basi..wokovu ni maisha, kila siku unajenga maisha yako ya baadaye, kama vile unavyojijengea maisha yako ya mwilini.
Hivyo mimi na wewe kuanzia sasa, tutamani kuwa karibu na Mungu, kwasababu tukifa kule tutatambuliwa kwa idadi ya mvi zetu rohoni.
Maran Atha.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,
Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
Jiunge na kundi letu la mafundisho ya Biblia whatsapp kwa kubofya hapa > Group-whatsapp
Mada Nyinginezo:
SWALI : Shalom .. Tukisoma Mathayo 5:43-45 Inazungumzia juu ya mtu ili awe mkamilifu hana budi kumjali mwingine hata kama Anatukosea,kwamba sisi tumeambiwa tuwaombee tuwapende N.K..Sasa tukisoma tena Mathayo 18:6..Inasema Hivi..
“Bali atakayemkosesha mmojawapo wa wadogo hawa waniaminio, yamfaa afungiwe shingoni jiwe kubwa la kusagia, na kutoswa katika kilindi cha bahari.”..Sasa Hapa mtumishi Sjaelewa kwenye Haya maneno aliyoyazungumzia Bwana katika huu mstari, Kwasababu Mathayo 5:43-45 inasema tuwaombee ila hapa Mathayo 18:6 inasema afadhali Afungiwe jiwe ikiwa na maana Aangamizwe..Naona pananitatiza kidogo
JIBU: Bwana Yesu alisema hivi katika Mathayo 5:43-44
“43 Mmesikia kwamba imenenwa, Umpende jirani yako, na, Umchukie adui yako;
44 lakini mimi nawaambia, Wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi,”
Bwana alimaanisha kweli kusema hivyo, kwa namna ya kawaida ukishakuwa mwanadamu tu, mwenye kitu Fulani kipekee ndani yako, ni lazima utakuwa tu na maadui, wengine watakuwa maadui zao kutokana na wivu, aidha wa utumishi wako, au ndoa yako, au mafanikio yako, au cheo chako, au kipawa chako, au mwonekano wako, n.k. Na wivu huo unaweza kufikia hatua hata ya hao watu kutaka kukuua.
Lakini ukijikuta katika hali kama hiyo wewe kama mkristo unapaswa ufanyaje? Je na wewe uwalipizie kisasi, jibu ni la hapo unapaswa tuwe kama Bwana Yesu alivyokuwa, pale ambapo walimtundika msalabani aliwaombea msamaha, pale ambapo Stefano anauliwa kwa kupigwa mawe mbele ya Paulo aliwaombea na kusema Bwana asiwahesabie kosa lile.
Umeona ni jukumu letu kuwaombea rehema.
Lakini pamoja na hayo kuna wakati mtu anafanya makosa kinyume na Mungu mwenyewe, na hiyo ni hatari zaidi, kwasababu japo Mungu kasema yeye ni mwingi wa rehema lakini pia ni mwingi wa hasira, Na ndio maana utasoma hapo, Bwana Yesu akisema..
Mathayo 18:6 “bali atakayemkosesha mmojawapo wa wadogo hawa waniaminio, yamfaa afungiwe shingoni jiwe kubwa la kusagia, na kutoswa katika kilindi cha bahari”
Unapaswa uwe makini sana na Watu waliomwamini Bwana Yesu, hususani wale ambao ni wachanga kiroho, watu waliotubu dhambi zao na kumwelekea Bwana, kwa mioyo yao yote, halafu wewe unakwenda kuwaondoa katika mstari wa wokovu kwa namna moja au nyingine, ukifanya hivyo ujue hukumu yako ni kubwa sana.
Katika biblia utamwona mtu mmoja anaitwa Balaamu, huyu alijua kabisa wana wa Israeli wanaenda sawa na Mungu wao, sasa akatafuta njia ya kuwakosesha kwa makusudi ili wafarakane na Mungu ili waadhibiwe.. Hivyo akabuni njia ya kuwakosesha, kwa kuwaletea wanawake wa kimataifa ili wazini nao, (jambo ambalo Mungu aliwakataza wana wa Israeli) kisha baada ya hapo Mungu awaadhibu na kuwaacha..Na kweli adhma yake ilifanikiwa, na matatizo yakawakumba kweli wana wa Israeli (Ufunuo 2:14).
Leo hii wapo watumishi wanaozini na washirika wao, mpaka imepelekea, wale wengine ambao walikuwa wameanza kuamini wameuacha wokovu, kutokana na matendo mabaya ya viongozi wao. Sasa watu kama hawa wanamudhi sana Mungu, hawajui tu. Mpaka kufikia hatua kama hiyo ya Mungu kusema..ingemfaa zaidi mtu kama huyo jiwe la kusagia lifungwe shingoni mwake akatupwe baharini… Ni Kuonyesha kuwa hukumu yake ni kubwa sana…Hata akifungiwa jiwe kubwa na kwenda kutupwa kwenye vilindi vya bahari kwa tendo hilo bado Mungu anaona ni sawa tu, amestahili.
Lakini swali ni je! Kwa ruhusu hiyo, tukawafungue watu mawe shingoni? Jiulize Wewe unaweza kufanya hivyo? Unaweza kudhubutu kumtupa mwanadamu mwenzako baharini? Au ulishawahi kufanya hivyo?. Kuna wakati Mungu alikuwa anamwambia Musa kwa hasira kwamba ajitenge na wana wa Israeli ili awaangamize kwasababu wamemwacha upesi na kugeukia kuabudu masanamu. Na yeye atamfanya kuwa taifa kubwa.
Lakini Musa alizituliza hasira za Bwana, akawaombea rehema, Sio kwamba angekubali Mungu asingetimiziwa aliyoahidiwa, angetimiza kweli, Mungu angeenda kumfanya kuwa taifa kubwa, na yeye angekuwa mfalme juu yao, lakini bado asingekuwa mkamilifu mbele za Mungu. Na ndio maana mtu kama Musa alipata kibali cha kipekee sana mbele za Mungu.
Kumbukumbu 9:12 “Bwana akaniambia, Ondoka huko, shuka upesi; kwa kuwa watu wako uliowatoa Misri wamejiharibu; wamekengeuka mara katika njia niliyowaamuru; wamejifanyia sanamu ya kusubu.
13 Tena Bwana akasema nami zaidi, akaniambia, Nimeliona taifa hili; na tazama, ni taifa lenye shingo ngumu;
14 niache, nipate kuwaangamiza, na kulifuta jina lao chini ya mbingu; nami nitakufanya wewe uwe taifa kubwa lenye nguvu kuwapita wao”.
Nasi pia, Tunapaswa tuitulize hasira ya Mungu, kwa kuwaombea rehema, na Sio kwa kuitekeleza.
Maombi ya kuwaangamiza maadui zetu, tunapaswa tujue kwa mkristo, hayana nafasi.
Bwana akubariki.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,
Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.
Mada Nyinginezo:
Kwanini wale dubu waliowauwa vijana wa Elisha walikuwa wa kike?
Maana ya Neno “kuruzuku” ni “kutoa Riziki”. Unapompa mtu mwingine riziki hapo umemruzuku. Katika biblia tunaona neno hilo limetokea mara kadhaa Mungu akiwaruzuku watu.
Katika kitabu cha Nehemia tunaona Neno hilo likitajwa..
Nehemia 9: 21 “Naam, muda wa miaka arobaini uliwaruzuku jangwani, wasihitaji kitu; nguo zao hazikuchakaa, wala miguu yao haikuvimba”.
Na pia tunaliona neno hilo katika kitabu cha Zaburi.
Zaburi 65:9 “Umeijilia nchi na kuisitawisha, Umeitajirisha sana; Mto wa Mungu umejaa maji; Wawaruzuku watu nafaka Maana ndiwe uitengenezaye ardhi”.
Na mwisho tunaona neno hilo katika kitabu hicho hicho cha Zabur 68,
Zaburi 68:10 “Kabila yako ilifanya kao lake huko; Ee Mungu, kwa wema wako uliwaruzuku walioonewa”.
Kama Bwana alivyowaruzuku wana wa Israeli Jangwani, mahali ambapo hapakuwa na kilimo wala maji, lakini Mungu wa mbingu na nchi akawapa MANA kutoka mbinguni na maji kutoka mwambani, na nyama kimiujiza, akakupe na wewe mtu wa Mungu uliyempokea na kumwamini Yesu Kristo, riziki zote za mwilini na rohoni. Akakuruzuku kwa riziki nyingi katika jina la Yesu.
Amen
Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.
Mada Nyinginezo:
Nini maana ya “Uchungu wa mauti ni dhambi, na nguvu za dhambi ni torati”
1Petro 2:1 “Basi, wekeni mbali uovu wote na hila yote, na unafiki na husuda na masingizio yote. 2 Kama watoto wachanga waliozaliwa sasa yatamanini maziwa ya akili yasiyoghoshiwa, ili kwa hayo mpate kuukulia wokovu”;
Kughoshi ni kugeuza, au kutia dosari, lengo likuwa ni kukifanya kionekane kama kile cha kwanza, leo hii utasikia maneno kama ‘vyeti vimeghoshiwa’, maana yake ni kuwa wametengeza vyetu bandia ili waonekane kama na wao ni wahitimu kumbe ni uongo. Utasikia tena watu pia ‘wanaghoshi fedha’, maana yake ni kuwa wanatengeneza fedha bandia ili zionekane kama zile halisi, zifae kwa manunuzi.
Sasa mtume Petro aliposema yatamanini maziwa ya akili yasiyoghoshiwa, alitumia mfano wa maziwa yanyonywao na watoto wachanga kufananisha na Neno la Mungu. Kwamba maziwa yale kwa asili huwa hayagoshiwi, hayatiwi kitu kingine chochote, wala hayaingiliwi na uchafu wowote, kwani mtoto hujafyonza moja kwa moja kutoka kwa mama yake.
Lakini kama vile leo hii utaona mambo yamebadilika watoto wachanga hawapewi tena maziwa yanayotoka moja kwa moja katika matiti ya mama zao, badala yake wanakwenda kuletewa maziwa mengine ya kwenye makopo, ya ng’ombe, ambayo kwa kutazama unaweza kuona yanafanana sana na yale ya mama, lakini kumbe yapo mbali sana kiubora na kiafya kwa mtoto mchanga. Utakuta hayo ya kwenye makopo yamechanganywa na vitu vingine wanavyoviita virutubisho, na kemikali baadhi za kuyafanya yasiharibike mapema..Sasa maziwa hayo ni maziwa yaliyoghoshiwa. Mtoto ananyweshwa kama mbadala wa maziwa halisi ya mama yake, na kamwe hayawezi kuwa na ubora ule ule kama wa yale ya mama.
Vivyo hivyo na sisi kama wakristo, tunapaswa tuyafyonze maziwa yanayotoka moja kwa moja kwa Mungu wetu mwenyezi, yanayotoka katika maandiko matakatifu (yaani BIBLIA), hayo ndio matiti yetu. Ili tuukulie wokovu katika afya njema za rohoni Mungu anazozihitaji. Lakini kama tutataka tuikulie injili nyingine ambayo si ile tunayoisoma katika maandiko tufahamu, tunajidhohofisha wenyewe.
Na ndio hapo, utashangaa kwanini mkristo anashindwa kusimama vema katika Imani, leo yupo sawa kesho kaanguka katika dhambi, utakuta mwingine yupo katika kanisa kwa miaka mingi, lakini ukitafuta matunda yoyote kwa Mungu wake hana, ukitafuta ni wangapi alishawahi waleta kwa Kristo, hupati, hayo yote ni matokeo ya kunywa maziwa ya aina nyingine yasiyomtia mtu nguvu rohoni.
Ukiona unakaa mahali na kuhubiriwa injili ya mafanikio tu wakati wote, auhubiriwi utakatifu, au mambo ya ufalme wa mbinguni na siku za mwisho, ujue kuwa hayo ni maziwa ya kughoshiwa, yanayofanana na yale halisi, hayatakusaidia chochote katika kuushinda ulimwengu.
Lakini mtume Paulo anasisitiza kwa kusema..‘Kama watoto wachanga waliozaliwa sasa yatamanini maziwa ya akili yasiyoghoshiwa, ili kwa hayo mpate kuukulia wokovu’
Unaona ni wajibu wetu kuitamani injili ya kweli, injili ile iliyoandikwa na mitume kwenye biblia, ili kwamba tuweze kuukulia wokovu wetu vema inavyostahili, tusishindwe na shetani kivyepesi, pia ili tuwe watu wa kumzalia Mungu matunda katika ukristo wetu.
Kumbuka hizi ni siku za mwisho, mafundisho mengi ya uongo yameenea sasa ulimwengu mzima, na ndio maana Bwana Yesu alituonya na kusema .ANGALIE JINSI MSIKIAVYO (Luka 8:18)..Akiwa na maana tuwe makini na yale tunayohubiriwa kwasababu si yote yanajenga roho zetu.Mengi ya hayo ni feki, yanatia ubovu roho zetu.
Shalom.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,
Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.
Mada Nyinginezo:
Je ni kweli imani ya mtu ndiyo itakayomuokoa, na si kitu kingine?
JIBU: Kama ulishawahi kuwahubiria watu kadha wa kadha habari za wokovu, naamini ulishawahi kukutana na watu baadhi wakikueleza, maneno haya, kwamba haijalishi wewe ni dini gani, au unaamini nini, imani yako ndiyo itakayokuokoa, ukiwa na imani kuwa Mungu yupo, hilo tu, linakutosha, hayo mengine si ya muhimu sana.
Atakuambia hata anayeabudu kupitia mti, au anayeabudu kupitia ng’ombe Mungu anamsikia hata, anayeabudu kupitia Rozari Mungu anamsikia kinachojalisha ni imani yake tu wala si kingine.
Ni kweli kabisa mawazo yao ni sahihi, kwamba imani ni daraja la kumfikia Mungu, kama vile maandiko yanavyosema katika..
Waebrania 11:6 “Lakini pasipo imani haiwezekani kumpendeza; kwa maana mtu amwendeaye Mungu lazima aamini kwamba yeye yuko, na kwamba huwapa thawabu wale wamtafutao”.
Lakini hawajui kuwa Imani ambayo haijakamilishwa haikufikishi popote, nikiwa na maana imani ambayo haijulikana msingi wake ni upi, imejengwa katika nini haikupeleki popote.. Kitendo cha kuamini tu Mungu yupo, hata wachawi wanaamini hivyo, na ukiwauliza watakuambia ndio namwamini Mungu na pia ananisaidia, mapepo nayo yatakuambia sisi nasi tunamwamini Mungu na pia tunatetemeka tunapolisikia jina lake..
Utalithibitisha hilo katika..
Yakobo 2:19 “Wewe waamini ya kuwa Mungu ni mmoja; watenda vema. Mashetani nao waamini na kutetemeka”.
Sasa kama unasema mimi naamini Mungu, na namwogopa, ujue kuwa huna tofauti na mashetani. Kama unadhani utakwenda mbinguni kwa imani ya namna hiyo, basi ujue mashetani watakutangulia kwanza mbinguni kisha wewe utayafuata baadaye.
Bwana Yesu alisema wazi kabisa katika Yohana 14:6..”mimi ndio njia na kweli na uzima, mtu hafiki kwa Baba isipokuwa kwa njia yangu mimi.” Akiwa na maana hakuna imani yoyote itayokufikisha mbinguni isipokuwa ile ya kumwamini yeye (Yesu Kristo).
Ni sawa na leo useme unayo simu, yenye line nzuri, yenye salio la kutosha, hivyo unaweza sasa kuwasiliana na mimi wakati wowote.. Jibu ni la! kama hutakuwa na namba yangu ya simu, kamwe hutakaa uwasiliane na mimi.. Haijalishi utakuwa na simu nzuri, au salio la kutosha au namba za watu wengine elfu kwenye kitabu chako cha kumbukumbu, kama huna namba yangu mimi binafsi, kamwe huwezi kuwasiliana na mimi.
Leo hii watu wanataka kuwasiliana na Mungu, kwa njia zao wenyewe walizojitungia, wanajaribu kupiga kila namba wanayoibuni tu vichwani mwao, wengine wanamtafuta Mungu kupitia dini zao, wengine wadhehebu yao, wengine wanyama, wengine miti,sanamu, jua, mwezi, n.k. wakidai kuwa wanamtafuta Mungu Yule Yule mmoja, ukiwaeleza dini au dhehebu halikufikishi popote, watakuambia usitupotoshe, imani yako ndio itakayokuokoa..
Ndugu, usipomuamini Yesu, hutafika popote. Na kumwamini Yesu sio kusema mimi ni mkristo, au mimi namwamini Yesu, hapana, bali kunakuja kwa kutubu kwanza dhambi zako kwa kumaanisha kuziacha, pili kwa kubatizwa katika ubatizo sahihi wa kuzamishwa katika maji tele katika jina lake sawasawa na Matendo 2:38, Kisha kupokea Roho Mtakatifu. Na kuanzia hapo kuishi maisha matakatifu yanayoendana na Neno lake,(yaani BIBLIA). Sasa Kwa kufanya hivyo imani yako itakuwa imekamilishwa mahali sahihi. Hapo ndipo utakuwa na uhakika unamwabudu Mungu kweli, kupitia mwana wake Yesu Kristo.
Lakini kwa kusema tu mimi namwamini Mungu, imani yangu itaniokoa na huku hujui Mungu kakuagiza nini katika Neno lake, au anakutaka ufanye nini..Ujue kuwa umepotea, na ukifa leo utakwenda kuzimu. Vilevile ukijivunua dhehebu lako, na hutaki kumtafuta Kristo Yesu aliye njia, ujue kuwa kuzimu itakuwa pia ni sehemu yako. Hakuna njia za kubuni buni katika kumfikia Mungu.. Ni sharti umwamini Yesu, na kuoshwa dhambi zako na yeye.
Maran Atha.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,
Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.
Mada Nyinginezo:
Nini maana ya “kila tendo lisilotoka katika imani ni dhambi?”
SWALI: Isaya 4:1 na siku hiyo wanawake saba watamshika mtu mume mmoja wakisema, tutakula chakula chetu na kuvaa nguo zetu wenyewe lakini tuitwe tu kwa jina lako; utuondolee aibu yetun. Je; andiko hili linamaanisha nini?
Kwanini wanawake? Kwanini wawe saba? Kwanini chakula chao na nguo zao na sio za mume wao? maanake mume akioa moja ya majukumu ya kwake kufanya kwa mkewe ni kumlisha na kumvika sasa hawa wanakula na kuvaa vya kwao ni kitu gani hawa wanawake?
JIBU: ufunuo wa mstari huo ni huu..wanawake saba ni makanisa saba (katika vipindi saba vya kanisa kama inavyooneka katika ufunuo 2 & 3)..
Mtu mume mmoja ni Yesu Kristo,.Lakini hao wanawake wote 7 wanasema watakula chakula chao wenyewe na kuvaa nguo zao wenyewe bali waitwe tu kwa jina la yule mtu mume mmoja ambaye ni Yesu Kristo.Jambo hili la kusema tutakula chakula chetu na kuvaa nguo zetu wenyewe ni tabia za hayo makanisa yote 7 yalivyokuwa, kila kanisa lilikuwa na tabia yake pekee, na yote yanatafuta kumpendeza Yesu Kristo lakini kwa njia zao wenyewe,
kwahiyo hicho “chakula” kinachozungumziwa hapo ni mapenzi yao wenyewe, na mienendo yao wenyewe hawataki chakula cha Bwana wao,(ambalo ni neno la Kristo lisiloghoshiwa), wala hawataki “mavazi” ya Bwana wao (Ambao ni utakatifu na matendo mema soma ufunuo 19:8,) bali waitwe tu kwa Jina la Bwana Yesu aibu yao iwaondoke hii aibu ina maana waiepuke hukumu itakayokuja na ndio maana yale makanisa yote hayakuweza kuoana na Kristo kikamilifu yalikuwa na mapungufu yake, na sisi pia tupo katika kanisa la mwisho la saba la LAODIKIA ni kanisa vuguvugu,na ndilo lililomkinai Bwana wake kuliko mengine yote yaliyotangulia soma..
ufunuo 3:14-22,”14 Na kwa malaika wa kanisa lililoko Laodikia andika; Haya ndiyo anenayo yeye aliye Amina, Shahidi aliye mwaminifu na wa kweli, mwanzo wa kuumba kwa Mungu.
15 Nayajua matendo yako, ya kuwa hu baridi wala hu moto; ingekuwa heri kama ungekuwa baridi au moto.
16 Basi, kwa sababu una uvuguvugu, wala hu baridi wala moto, nitakutapika utoke katika kinywa changu.
17 Kwa kuwa wasema, Mimi ni tajiri, nimejitajirisha, wala sina haja ya kitu; nawe hujui ya kuwa wewe u mnyonge, na mwenye mashaka, na maskini, na kipofu, na uchi.
18 Nakupa shauri, ununue kwangu dhahabu iliyosafishwa kwa moto, upate kuwa tajiri, na mavazi meupe upate kuvaa, aibu ya uchi wako isionekane, na dawa ya macho ya kujipaka macho yako, upate kuona.
19 Wote niwapendao mimi nawakemea, na kuwarudi; basi uwe na bidii, ukatubu.
20 Tazama, nasimama mlangoni, nabisha; mtu akiisikia sauti yangu, na kuufungua mlango, nitaingia kwake, nami nitakula pamoja naye, na yeye pamoja nami.
21 Yeye ashindaye, nitampa kuketi pamoja nami katika kiti changu cha enzi, kama mimi nilivyoshinda nikaketi pamoja na Baba yangu katika kiti chake cha enzi.
22 Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo Roho ayaambia makanisa.”
Lakini tunapaswa wote tushinde ili tuvuke kutoka kuwa masuria na kuwa bibi-arusi safi wa Yesu Kristo waliokubaliwa tayari kwenda kwenye arusi ya mwanakondoo itakayofanyika mbinguni kwa Baba.Kumbuka bibi-arusi sio sawa na suria.Kwahiyo ndugu watakaoshiri karamu ya mwanakondoo ni bibi-arusi tu, je! wewe ni bibiarusi? umepokea Roho Mtakatifu? umejiweka tayari kumpokea Bwana wako atakaporudi? matendo yako yanastahili wokovu? jibu lipo moyoni mwako. Tubu sasa umgeukie Bwana kumbuka tunaishi kizazi ambacho kitashuhudia kuja kwa pili kwa Kristo.
ufunuo 19: 7 Na tufurahi, tukashangilie, tukampe utukufu wake; kwa kuwa arusi ya Mwana-Kondoo imekuja, na mkewe amejiweka tayari.
8 Naye amepewa kuvikwa kitani nzuri, ing’arayo, safi; kwa maana kitani nzuri hiyo ni matendo ya haki ya watakatifu.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,
Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.
Mada Nyinginezo:
SWALI: Katika Ezra 9:12 na Kumbukumbu 7:3, Tunaona Bwana Mungu aliwakataza waisraeli kuoana na watu wa mataifa. Je watumishi hawa walioolewa au kuoa mataifa walifanya dhambi?.
2. Boazi kumwoa Ruthu
Na kama ni dhambi mbona Miriamu Mungu alimpiga kwa ukoma baada ya kuhoji kwanini kaka yake, Musa alioa mwanamke wa kimataifa?
Jibu: Esta hakufanya jambo lililo sahihi kuolewa na mfalme wa kimataifa asiyemjua Mungu wa Israeli, kulingana na sheria za Mungu, lakini Mungu aliruhusu jambo hilo litokee, kwa makusudi maalumu, kwamba Esta aolewe na Mfalme Ahasuero (ambaye ni mtu wa kimataifa) ili Mungu awaokoe watu wake dhidi ya maadui zao.
Utaona jambo kama hilo hilo lilitokea wakati wa Samsoni, pale ambapo Samsoni alikuwa ni Mwisraeli lakini akaenda kutafuta kuoa wanawake wa kimataifa (wakina Delila). Utaona walikuwepo wanawake wengi wa kiisraeli wenye sifa zote, lakini Samsoni hakwenda kwa hao bali kwa Delila aliyekuwa mfilisti, na biblia inasema jambo lile lilitoka kwa Bwana. (Yaani Mungu aliruhusu liwe hivyo)
Waamuzi 14:3 “Ndipo baba yake na mama yake wakamwambia, Je! Hapana mwanamke hata mmoja katika ndugu zako, au katika jamaa zangu zote, hata uende kumwoa mwanamke kwa hawa Wafilisti wasiotahiriwa? Samsoni akamwambia baba yake; Mnipatie huyo, kwa maana ananipendeza sana.
4 Lakini baba yake na mama yake HAWAKUJUA YA KUWA JAMBO HILI NI LA BWANA; MAANA ALITAKA KISA JUU YA WAFILISTI. Basi wakati ule Wafilisti walikuwa wakiwatawala Israeli”.
Unaona?..Mungu aliruhusu Samsoni atafute mke wa kimataifa, ili tu kutafuta kisa cha kuwaokoa waisraeli watu wake, chini ya utawala wa wafilisti.
Na ndio hivyo hivyo kwa Esta, Mungu aliruhusu Esta aolewe na mwanaume wa kimataifa (Mfalme Ahasuero), lengo na madhumuni ni kutafuta tu kisa cha kuwaokoa Israeli dhidi ya maadui zao ambao walikuwa wanawanyanyasa chini ya utawala huo. Na kilipopatikana kisa, Maadui za Israeli wote walikufa na Israeli wakapata raha. Lakini hayakuwa mapenzi kamili ya Mungu, Esta aolewe na mwanaume wa kimataifa, wala Samsoni aoe mwanamke wa kimataifa, ilikuwa ni kinyume cha sheria za Mungu.
Lakini pamoja na hayo tunaona pia mtu mwingine akioa mke wa kimataifa, na huyo si mwingine zaidi ya Boazi, aliyemwoa Ruthu, aliyekuwa mwanamke wa kimataifa.
Sasa ni kwanini iwe hivyo?
Ni kwasababu Ruthu tayari alikuwa ameshaacha miungu ya kwao, na kumgeukia Mungu wa kweli wa Israeli, kwasababu lengo kuu la Mungu kuwaambia wana wa Israeli wasioe wanawake wa mataifa ni kuepuka kugeuzwa mioyo. (1Wafalme 11:2). Na si lengo lingine.
Hivyo Ruthu tayari alikuwa ameshaiacha miungu ya kwao, na amemgeukia Mungu wa kweli wa Israeli kwa moyo wake wote, tofauti na Delila au Mfalme Ahasuero aliyemwoa Esta, hao walikuwa bado hawajaiacha miungu yao.
Ruthu 1:16 “Naye Ruthu akasema, Usinisihi nikuache, Nirejee nisifuatane nawe; Maana wewe uendako nitakwenda, Na wewe ukaapo nitakaa. Watu wako watakuwa watu wangu, Na Mungu wako atakuwa Mungu wangu;
17 Pale utakapokufa nitakufa nami, Na papo hapo nitazikwa; Bwana anitende vivyo na kuzidi, Ila kufa tu kutatutenga wewe nami”.
Kwahiyo unaweza kuona, Ruthu tayari moyo wake ulikuwa umeshahamia kwa Mungu wa Israeli, akili yake yote ilikuwa inamwaza Mungu wa Israeli, na watu wa Israeli, na kwa Imani hiyo akahesabika kuwa kama mmojawapo wa mwanamke wa kiisraeli, japokuwa ni mwanamke wa kimataifa.
Sawa tu na yule Rahabu kahaba, ambaye naye pia kwa Imani, alihesabiwa kuwa mwanamke wa kiisraeli, ingawa alikuwa ni Myeriko, kwasababu aliiacha miungu ya kwao na kumwamini Mungu wa Israeli na kumkiri.
Yoshua 2: 11 “Na mara tuliposikia hayo mioyo yetu iliyeyuka, wala haukusalia ujasiri wo wote katika mtu awaye yote, kwa sababu yenu; kwa kuwa Bwana, Mungu wenu, yeye ndiye Mungu, katika mbingu juu na katika nchi chini”
Waebrania 11: 30 “Kwa imani kuta za Yeriko zikaanguka, zilipokwisha kuzungukwa siku saba
31 Kwa imani Rahabu, yule kahaba, hakuangamia pamoja na hao walioasi; kwa kuwa aliwakaribisha wale wapelelezi kwa amani”..
Na swali la mwisho ni kwanini Musa alimwoa Siphora, mkushi? Na ilihali yeye ni myahudi?
Kumbuka sheria ililetwa na Mungu kwa mkono wa Musa, hivyo Musa tayari alikuwa ameshaoa kabla ya hiyo sheria kuja. Kwahiyo haikuwa sahihi kumwacha mke wake huyo wa kimataifa na kuoa mwingine ilihali ameshapata naye watoto. Hivyo Mungu alimbariki na huyo huyo mkewe, maadamu alikuwa naye pia anamcha Mungu wa Israeli. Na sio tu Musa peke yake aliyekuwa na mke wa kimataifa, bali hata Yusufu, biblia inasema mke wake alikuwa ni binti wa kuhani wa Oni (Mwanzo 41:45), ambaye hakuwa myahudi. Lakini Mungu hakumpa maagizo amwache, kwasababu sheria hiyo bado ilikuwa haijaja.
Na sisi wakristo wa agano jipya, hatupaswi kuoa, wala kuoelewa na mtu ambaye hajamkabidhi Yesu maisha yake (Mpagani), hiyo ni kulingana na maandiko. Ni sharti kwanza awe amemwamini Yesu na kusimama katika imani ndipo ndoa ifuate. (kwa urefu juu ya somo hili unaweza kufungua hapa >> Je Ni sahihi kuolewa/kuoa mtu wa imani nyingine?)
Bwana akubariki.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,
Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.
Mada Nyinginezo:
Je! Ni halali kuoa/kuolewa na mtu ambaye tayari anao watoto?
JIFUNZE KUELEWA MAANA YA KUOA/KUOLEWA KABLA YA KUINGIA HUKO.
Je! Ni sahihi kwa mkristo kuoa/kuolewa na mtu wa imani nyingine?
Shalom, nakusalimu katika jina kuu la Bwana wetu Yesu Kristo, karibu tuyatafakari maneno ya uzima pamoja.
Muda mfupi kabla ya Bwana Yesu kwenda kutukuzwa na maelfu ya watu kule Yerusalemu lipo agizo ambalo aliwapa wanafunzi wake wawili, na agizo lenyewe lilikuwa ni kwenda kumletea mwana punda aliyekuwa amefungwa mahali Fulani. Wengi wetu tunaweza kuona lile lilikuwa ni agizo jepesi, lakini kiuhalisia halikuwa jepesi kama tunavyodhani, kwani walipotumwa walioambiwa sio wakaombe wapewe, hapana bali wakachukue, kana kwamba hao punda walikuwa ni wa kwao.
Embu tusome kidogo;
Luka 19:29 “Ikawa alipokaribia Bethfage na Bethania, kwenye mlima uitwao wa Mizeituni, alituma wawili katika wale wanafunzi,
30 akisema, Nendeni mpaka kijiji kile kinachowakabili, na mtakapoingia ndani mtaona mwana-punda, amefungwa, ambaye hajapandwa na mtu ye yote bado, mfungueni mkamlete hapa.
31 Na kama mtu akiwauliza, Mbona mnamfungua? Semeni hivi, Bwana anamhitaji.
32 Na wale waliotumwa wakaenda wakaona kama alivyowaambia.
33 Na walipokuwa wakimfungua mwana-punda, wenyewe waliwaambia, Mbona mnamfungua mwana-punda?
34 Wakasema, Bwana ana haja naye”.
Utajiuliza ni kwanini, Bwana atumie kauli hiyo, mfungue na sio waombeni mniletee? Unadhani hakujua kanuni za kuchukua mali za watu wengine? Alijua sana, lakini si kila wakati aliruhusu hilo, pengine wale wanafunzi walisema kwanini Bwana asituambie tukaanze na kuomba kwanza, si tutapewa tu, kuliko kwenda na kufungua wanyama ambao si wetu, si tutaitwa wezi?
Ni sawa na leo hii mtu akuambie, nenda pale mlimani city, utakuta gari limepakiwa, ingia kisha piga ufunguo, endesha uniletee, bila shaka utasema huyu mtu hanitakii mema bali mabaya.. anataka nikachomwe moto kama mwizi.
Lakini Kristo alikuwa na sababu kufanya vile, alijua mwisho wake utakuwaje..Vilevile alijua madhara ya kutanguliza kuomba omba vibali kwenye kazi yake, alijua milolongo ambayo wangekutana nayo, alijua vikwazo ambavyo shetani angevizusha mahali pale..pengine nyie ni wakina nani, mmesajiliwa wapi, shughuli yenu ni nini, hatuwatambui hapa mtaani, msimgolee yule punda, elimu yenu ni ipi, leta uthibitisho kwanza wa barua kutoka kwa huyo Bwana wenu, n.k. vinginevyo tutawashitaki..
Lakini wao hawakuongea chochote walipofika, badala yake walianza kufanya kama Yesu alivyowaagiza, kufungua punda na pengine katika hatua ya mwisho kabisa pale walipoanza kuondoka, ndipo wahusika walipowaona, na kuwauliza nyie mnafanya nini hapo? Mnawapeleka wapi hao punda?..Wakasema Bwana anawahitaji..
Sasa wale kuona tayari punda wao wameshafunguliwa na gharama imeshaingiwa, kuwarudisha itakuwa ni hatua ndefu sana wakaona ni bora wawache tu, pengine wawape masharti Fulani madogo ya kuwatumia, au walipie gharama Fulani kidogo tu. Hilo halijalishi maadamu punda wameshapatikana.
Vivyo hivyo na hata sasa, usitegemee kwanza ruhusu za watu kufanya jambo lolote la ki-Mungu, ni ngumu sana kusikilizwa au kusapotiwa, fanya kwanza kisha baadaye wakikuuliza kwanini ulifanya waambie ni kwababu Yesu aliniagiza..hata wakikasirika lakini tayari ulishafanya, lile agizo la Yesu litakulinda.
Vikwazo vya shetani ni vingi sana, unaweza ukajikuta haumfanyii Mungu lolote kisa, visheria Fulani vidogo vidogo, au viutaratibu Fulani vinakubana. Wewe fanya tu agizo lake litakulinda mbele ya safari. Unaweza hata usifanya huduma kisa hujakamilisha taratibu hii au ile, hayo tumeyaona sana sehemu nyingi, usingojee kukamilisha taratibu za wanadamu kwanza, endelea na taratibu za Mungu, kisha hizo za wanadamu zitafuata baadaye watakapokuuliza..kwasababu ukisema uanzie kwao, utavunjika moyo mapema mpendwa. Vikwanzo ni vingi kila kukicha.
Bwana Yesu alishatoa agizo, enendeni ulimwenguni kote, mkuhubiri injili kwa kila kiumbe. Hilo agizo halisemi, mkaombe kwanza kuhubiri, hapana, wewe kahubiri kwa jinsi Mungu alivyokujalia kisha wakikufuata, waeleze hilo ni agizo la Yesu. Kwa kufanya hivyo Yesu mwenyewe atafungua njia ya kukusaidia, atakuwekea wepesi, au kupewa kibali cha kuendelea na kazi ya Bwana.
Bwana akubariki.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,
Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.
Mada Nyinginezo:
Kuna swali limeulizwa na wasomaji wetu hapa..
“Bwana Yesu asifiwe mtumishi, pole na hongera na majukumu, mtumishi Mimi nilitaka kufahamu kuhusu Yohana mbatizaji, yeye ndiye aliyembatiza Yesu mwana wangu tena akasema nalishuhudia Roho wa Mungu akishuka kama hua toka mbinguni akatua juu yake tena yeye aliyempeleka yaani Mungu akamwambia yule utakayeona Roho akishuka juu yake huyo ndiye atakayebatiza kwa Roho mtakatifu na kwa Moto, tena Yohana anawahakikishia kwamba ajaye nyuma yake huyo ni mkubwa kuliko yeye na ya kwamba alikuwako kabla yake…..Sasa swali kwanini alipokuwa gerezani anatuma wanafunzi wake wakamuulize kuwa yeye ndiye Yesu au tumtazamie mwingine? Ina maana alichotushuhudia mwanzo kuwa ajaye ni mkuu na alimuona Roho akishuka juu yake bado hakuamini kuwa ni yeye? Asante, Mungu akusaidie katika kujibu”.
Jibu:
Ni kawaida ya mwanadamu pale anapoahidiwa kitu au anapoonyeshwa jambo fulani na Mungu, wakati huo huo kuanza kuundia matarajio yake mwenyewe juu yake jinsi ahadi hiyo itakavyotimia.. Sasa pale maono hayo yanapotimia nje ya hayo matarajio yake mwenyewe, inakuwa ni rahisi sana kutetereka kama sio kuiacha Imani kabisa.
Katika mazingira ya Yohana mbatizaji, Sio kwamba hakuamini alichoonyeshwa, aliamini na kujua kabisa Yesu Kristo ndio yule aliyekuwa anatarajiwa kwa muda mrefu,. Lakini shida ilianza kutokea pale alipoanza kubuni matarajio yake mwenyewe, ambayo wakati mwingine sio kwamba yalikuwa sio sahihi, hapana pengine yalikuwa ni ya kutimia baadaye kabisa, sio kwa wakati ule.
Sasa alipoona Yesu hajaja kama mfalme, akiwa na pepeto mikononi mwake kukusanya ngano ghalani na makapi kuyachoma motoni, kama alivyoonyeshwa (Mathayo 3:12) kinyume chake amekuja katika upole na unyonge, anakataliwa na watu hiyo ikampelekea baadaye aanze kutilia shaka.. Labda pengine atakuwa sio huyu..
Umeona, hata leo hii, Mungu anawapa watu wengi ahadi ya mambo fulani, na wanajua kabisa ni Mungu amewajibu pengine walijibiwa kwa ndoto, au maono, au sauti, au ishara n.k. lakini kwa bahati mbaya, wameyatilia shaka, kama sio kuyaacha kabisa maono hayo kutokana na kuwa waliyaruhusu matarajio yao yatawale maono hayo Mungu aliyowapa.
Kwa mfano utakuta mwanamke Fulani, ameahidiwa na Mungu kwamba kabla ya miaka mitano atakuwa na watoto watatu. Sasa badala asubiri maajabu ya Mungu , yeye muda huo huo anaanza kujiundia matarajio yake, kwamba mwaka wa kwanza atapata mmoja, kisha baada ya miaka miwili atapata mwingine , na mingine atakuja baada ya miaka mingine miwili ya mwisho kupita ili kutimiza mitano.
Sasa matarajio hayo sio mabaya, lakini yana athari pale ambapo atakapoona wakati huo unapita bila ya yeye kuona chochote, mwaka wa kwanza unapita, wa pili nao hivyo hivyo haioni chochote, watatu, na wanne hivyo hivyo.. hapo ndipo mtu huyo anapoanza kutilia shaka kudhani pengine Mungu hakusema naye, pengine Mungu hakumjibu, pengine maono yale yalimaanisha kitu kingine, pengine hivi, pengine vile, pengine kuna mahali alimkosea Mungu..
Unaona? Mwisho wa siku anayaacha kabisa, na kuanza kuhangaika tena. Lakini kama angekuwa mtulivu na kuamini kuwa ni Mungu aliyemjibu, angesubiria matarajio ya Mungu yatende kazi, pengine Mungu amempangia mwaka wa tano ule wa mwisho apate ujauzito wa watoto mapacha watatu.
Ndicho kilichotokea kwa Yohana mbatizaji, hiyo inatufundisha kuwa Pale Mungu anapotuahidi kitu, basi tumwamini vile vile alivyotuonyesha, bila kuongezea matarajio yetu juu yake, na hapo ndipo tutakapoweza kuishi maisha ya kutotilia shaka maneno yote ya Mungu.
Bwana akubariki.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,
Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.
Mada Nyinginezo:
Ni vitu vipi hivyo viwili visivyoweza kubadilika? (Ebr 6:18)