Title October 2020

Je! Wana wenu huwatoa kwa nani? maana yake ni nini?

SWALI: Bwana Yesu alimaanisha nini kusema “je! Wana wenu huwatoa pepo kwa uweza wa nani?” pale Mafarisayo walipomwambia kuwa yeye anatoa pepo kwa Beelzebuli mkuu wa pepo?


JIBU: Tusome kuanzia juu kidogo habari yenyewe,

Mathayo 12:24 “Lakini Mafarisayo waliposikia, walisema, Huyu hatoi pepo, ila kwa Beelzebuli mkuu wa pepo.

25 Basi Yesu akijua mawazo yao, akawaambia, Kila ufalme ukifitinika juu ya nafsi yake, hufanyika ukiwa; tena mji au nyumba yo yote ikifitinika juu ya nafsi yake, haitasimama.

26 Na Shetani akimtoa Shetani, amefitinika juu ya nafsi yake; basi ufalme wake utasimamaje?

27 Na mimi nikitoa pepo kwa Beelzebuli, JE! WANA WENU HUWATOA KWA NANI? KWA SABABU HIYO HAO NDIO WATAKAOWAHUKUMU.

28 Lakini mimi nikitoa pepo kwa Roho wa Mungu, basi ufalme wa Mungu umekwisha kuwajilia”.

Tukumbuke kuwa neema ya Mungu ya uponyaji ilikuwepo tangu zamani za agano la lake, isipokuwa tu haikuwa imefunuliwa katika utimilifu wote kama ilivyokuwa kwetu sisi wa agano jipya kwa kupitia Yesu Kristo mwokozi wetu. Utaona kuna wakati Mungu alikuwa anawaponya wayahudi pale walipokuwa wanamwomba, japo halikuwa jambo la papo kwa papo kama alivyokuja kufanywa na Bwana Yesu mwenyewe, mti wa uzima.

Kwa mfano ukisoma Yohana 5, utaona kulikuwa na birika moja mashuhuri lililoitwa Bethzatha huko Yerusalemu, ambapo kuna wakati Mungu analikuwa anamtuma malaika wake, kuyatibua maji kisha yule mtu wa kwanza kutumbukia alikuwa anaponywa ugonjwa wake saa ile ile .Haijalishi alikuwa anasumbuliwa na vifungo vya magonjwa au mapepo ya udhaifu mengi kiasi gani,  ilikuwa akiingia tu mule ni lazima atoke mzima, na ndio maana utaona yule mtu ambaye alikuwa anasumbuliwa na ule ugonjwa wa udhaifu kwa muda wa miaka 38, (na bila shaka lilikuwa ni pepo la udhaifu)? Bwana Yesu alimfungua badala yake, Utauliza tumejuaje alikuwa na pepo la udhaifu? Ni kwasababu mwishoni kabisa Bwana Yesu alimwambia asifanye dhambi tena yasiye yakamkuta yaliyo mabaya zaidi ya yale aliyokuwa nayo..Kumbuka hilo ndio lile Yesu alilolisema katika Luka 11:24 kwa habari ya mapepo, ambayo hayo yana tabia ya kufanya hali ya mtu kuwa mbaya zaidi pale yanaporudi na kukuta nyumba yao imefagaliwa.

Kwahiyo ni wazi kuwa mtu Yule alikuwa na mapepo ya udhaifu, na kwamba kama angeingia tu kwenye yale maji, basi mapepo hayo yangemwondoka. Hivyo huo ni mfano tu mmojawapo wa Mungu alioutumia kuwafungua wayahudi, zipo njia nyingine pia walizomwombea Mungu, na Mungu akawasikia na kuponywa hata na mapepo. Hivyo jambo la kutoa pepo lilikuwa linafanywa na wayahudi hata kabla ya kuja kwa Bwana Yesu, utalithibitisha hilo kwa wale wayahudi wapunga pepo, (Matendo 19:13), ambao walikurupuka tu na wao wakajaribu kulitaja jina la Yesu, bila kujua linahitaji mamlaka ili kulitaja. Lakini wao wakajaribu kufanya kwa njia zao, na huku matendo yao maovu, yakawakuta yaliyowakuta.

Lakini sasa tukirudi kwenye ile habari, tunaona walipokuja kwa Yesu na kuona mambo mapya yanafanyika, yaani kitendo cha Neno moja tu, mapepo yanatoka, magonjwa yanatoweka, wafu wanafufuliwa, tofauti na wao walivyokuwa wanaomba, au wanafanya, wakahitimisha kuwa huyu atakuwa anatumia nguvu za giza. Na ndio hapo Yesu akawauliza swali tu la kufikirikika, ikiwa mnasema mimi ninatoa pepo kwa beelzebuli, Je! Hao wana wenu (wanafunzi wenu), huwatoa kwa nani?, wanapoingia katika lile birika la Bethzatha na kufunguliwa ni kwa uweza wa pepo gani? Wanapomwomba Mungu wakati mwingine juu ya mapepo na mapepo yanawatoka, je! Ni kwa uwezo wa pepo wa namna gani?  Lakini Kama mnaamini ni kwa msaada wa Mungu wa Ibrahimu wanafanya hivyo na sio mapepo, kwanini mnahitimisha kuwa na mimi ninatoa pepo kwa uwezo wa mashetani?. Kumbukeni hao ndio watakaowahukumu.

Unaona? Nasi tunapaswa tuwe makini, palipo na nguvu za Mungu za kweli zinawaponya watu, hatupaswi kuhitimishi na kusema ule ni uchawi, hiyo ni dhambi ya kumkufuru Roho Mtakatifu, ambayo haiwezekaniki kusameheka, sio kila mtumishi unayemwona ni mchawi, hivyo tuchunge vinywa vyetu. Tuzungumze tu pale ambapo tumethibitisha kuwa hizi ni nguvu za giza, lakini sio kuhitimisha kila mahali unapoona nguvu za Mungu zinadhihirika kuwa ni nguvu za giza. Hapo tutakuwa tumejiweka vitanzini wenyewe.

Bwana atusaidie.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255 789001312

Mada Nyinginezo:

KUNA UMUHIMU WA KUWA MTU WA KURIDHIKA.

Zaburi maana yake nini, katika Biblia?

ONDOKA YESU, TUACHIE MAPEPO.

UTENDAJI KAZI WA MPINGA-KRISTO.

Amin, nawaambia, Kizazi hiki hakitapita, hata hayo yote yatakapotimia..!!

Rudi Nyumbani:

Print this post

KUNA UMUHIMU WA KUWA MTU WA KURIDHIKA.

Jina la Bwana wetu Yesu Kristo libarikiwe.

Karibu tujifunze biblia,

Neno la Mungu linasema..

1Timotheo 6:7 “Kwa maana hatukuja na kitu duniani, tena hatuwezi kutoka na kitu;

8  ila tukiwa na chakula na nguo tutaridhika na vitu hivyo”..

Hili ni moja la andiko linalochukiwa na wengi..Hususani watu wenye uchu wa kupata mali. Lakini wanalisahau pia hili neno..

Mhubiri 5:10 “Apendaye fedha hatashiba fedha, Wala apendaye wingi hatashiba maongeo. Hayo pia ni ubatili”.

Maana yake ni kwamba kama wewe ni mtu wa kuzipenda fedha mno, usifikiri utafika wakati utasema sasa sizihitaji tena.. Hata upate nyingi kiasi gani, bado utazidi kuzitafuta tu!.. Hekima ndio inasema hivyo..Siku zote mwenye fedha nyingi ndio yupo busy kuzitafuta kuliko yule asiyekuwa nazo. Matajiri wote wakubwa ulimwenguni ndio wapo bize kuliko watu wasio na fedha nyingi.

Ndivyo hekima inavyosema.. Mhubiri 5:12 “Usingizi wake kibarua ni mtamu, kwamba amekula kidogo, au kwamba amekula kingi; lakini kushiba kwake tajiri hakumwachi kulala usingizi”.

Rafiki yangu mmoja mwenye kazi nzuri na mshahara mzuri sana, (ambaye ni kama boss tu huko kazini kwake) siku moja alinifuata huku akiwa amenyong’onyea, isivyo kawaida..Wakati naanza kuzungumza naye tu, akaniambia leo nimejifunza kitu kikubwa sana nikiwa kazini,

Akaniambia kazini, mahali anapofanya kazi kuna watu ambao kazi yao ni kufanya usafi, ambao mishahara yao ni laki moja, aliyezidi sana analipwa laki moja na nusu. Akasema kilichomshangaza zaidi ni kwamba siku hiyo kawakuta wamejikusanya wanasheherekea na kufurahi na kucheka pamoja mwisho wa mwezi, hivyo wamenunua soda na kukata keki, wakifurahi. Nikazidi kumuuliza kwani wao kufanya hivyo kumekuathiri nini wewe?. Akasema alipowaona wanafurahi huku wanamishahara midogo, ambayo kwa kiwango hicho, cha laki moja yeye anaweza kukitumia kwa siku moja tu na kinaweza kisimtoshe…..Akashangaa inakuwaje wao wenye mishahara midogo wana furaha na raha, na yeye hana raha na ana mshahara mkubwa!….. akasema “Hilo jambo kwa kweli limenigusa sana na nahisi kuna kitu natakiwa nijifunze”.

Sasa huyu alikuwa hajui kama hicho anachokisema tayari biblia ilishakise,a miaka mingi sana huko nyuma …. Mhubiri 5:12 “Usingizi wake kibarua ni mtamu, kwamba amekula kidogo, au kwamba amekula kingi; lakini kushiba kwake tajiri hakumwachi kulala usingizi”.

Ndugu hatuna budi kila siku kujifunza kuridhika… Kwa kusema hivi sio kwamba nasema tuwe masikini au nauunga mkono umasikini hapana!..Ni mapenzi ya Mungu tutajirike, lakini hata katika utajiri pia tunaweza kujifunza kuridhika.

Kuridhika katika hali ya utajiri ni huku… “Aidha siku imepata kingi au vichache, kumshukuru kwako Mungu kupo palepale, kumfurahia kuko pale pale, kutenda kwako mema kupo pale pale”..Kwaufupi moyo wako haupo kwenye mali kabisa.. Na hata ukikosa au ukipata, vyote kwako ni sawasawa tu wewe utabaki kuwa yule yule, kama Ayubu.

Ayubu 31:25 “Kama nilifurahi kwa kuwa mali yangu yalikuwa mengi, Na kwa sababu mkono wangu umepata vitu vingi”

ZIFUATAZO NI FAIDA CHACHE ZA KURIDHIKA.

  1. Unapata nafasi ya kumtafakari Mungu:

Hii ni faida ya kwanza ya kuridhika, unaporidhika unakuwa unafungua mlango  mkubwa katika ufahamu wako wa kufanya jambo lingine ambalo linaweza kuwa la muhimu. Na jambo la muhimu kuliko yote ni muda wa kumtafuta Mungu. Lakini unapoingia katika tamaa ya mali zinazotokana na kutokuridhika, kamwe muda wako siku zote unakuwa umebana, hutapata hata nafasi ya kushika biblia, wala kulisoma Neno lake.

  1. Unapata Furaha:

Unaporidhika, na huku Mungu akiwa moyoni mwako, utapata furaha ya kudumu, kwasababu hutaingia kwenye mashindano na Mtu na wala hutaendeshwa na mali, hivyo hutakuwa mtumwa wa vitu hivyo, na hivyo utakuwa ni mtu wa furaha siku zote.

  1. Utajiepusha na Mitego na Vitanzi vya shetani:

Biblia inasema katika hiyo 1Timotheo 6: 9  “Lakini hao watakao kuwa na mali huanguka katika MAJARİBU NA TANZİ, na tamaa nyingi zisizo na maana, zenye kudhuru, ziwatosazo wanadamu katika upotevu na uharibifu.

Wote wanaojiingiza katika mauaji, ni kwasababu ya tamaa ya mali, inayotokana na kutokuridhika na hali walizonazo, wanaojiingiza katika ukahaba na wizi ni kwasababu ya tamaa ambayo inatokana na kutokuridhika..

  1. Hutafarakana na Imani:

1Timotheo 6: 10  “Maana shina moja la mabaya ya kila namna ni kupenda fedha; ambayo wengine hali wakiitamani hiyo WAMEFARAKANA NA IMANİ, na kujichoma kwa maumivu mengi”.

Ukiridhika na mshahara, hutamdhulumu mtu wala kusaka njia za kando kando kutafuta mali..Na hivyo Imani yako haiwezi kuathirika.

Kumbuka biblia inatuambia kwamba “Hatukuja na kitu wala hatutaondoka na kitu” na pia Bwana Yesu alisema… “itatufaidia nini (au kwa lugha rahisi, tutapata faida gani), tukiupata ulimwengu mzima halafu tukapata hasara ya nafsi zetu”?. Hilo ni swali tumepewa mimi na wewe na Bwana, la kutafakari!..

Bwana akubariki.

Kama hujampokea Yesu lakini upo bize na shughuli za ulimwengu huu, nakushauri, simamisha kwanza shughuli zako, tafuta uhakika wa usalama wa roho yako, ukishaupata rudi endelea na shughuli zako kama zinampendeza Mungu.

Maran atha!

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255 789001312


Mada Nyinginezo:

TAFUTA KUWA NA AMANI NA WATU WOTE.

SALA YA ASUBUHI

Jiepushe na tamaa ya Mali/kupenda fedha.

JE! MTUMISHI KUTOKUWA NA FEDHA NI ISHARA KUWA KUNA TATIZO KATIKA IMANI YAKE?

Rudi Nyumbani:

Print this post

Zaburi maana yake nini, katika Biblia?

Zaburi maana yake ni “nyimbo takatifu”. Hivyo kitabu cha Zaburi katika biblia, ni kitabu cha Nyimbo takatifu. Zimeitwa nyimbo takatifu kwasababu zimetungwa kwa lengo la kumrudisha mtu kwa muumba wake, kwa njia hiyo ya kusifu na kumwimbia. Pia Pamoja na kwamba zilikuwa ni nyimbo, lakini ndani yake pia zilikuwa zimejaa unabii wa mambo yanayokuja.

Katika agano la kale nyimbo hizo ziliimbwa na wayahudi (yaani waisraeli) wakati wa kuabudu katika masinagogi yao, na hata leo wakristo tunatumia baadhi ya mashairi hayo kutengeneza nyimbo nzuri za kumwimbia Mungu wetu na kumshukuru na kumsifu.

Kitabu  cha Zaburi katika biblia kimeandikwa sehemu kubwa na Mfalme Daudi, wapo wengine wachache walioshiriki kuandika kitabu hicho kizima, lakini sehemu kubwa imeandika na Daudi. Na Daudi alianza kumwimbia Mungu tangu udogoni, biblia inasema hivyo.

Pia wapo wengine walioandika Zaburi (Nyimbo) katika biblia, ambazo mashairi yao hayawekwa katika kitabu cha Zaburi. Mfano wa watu hao ni Musa na Sulemani.  Kwamfano Zaburi za Musa unaweza kuzisoma katika kitabu cha Kumbukumbu la Torati 32.

Jambo dogo tunaloweza kujifunza ni kwamba..Zaburi hizi zilizoandikwa na Daudi, zimewezwa kutukuzwa na Mungu mwenyewe mpaka leo, kwasababu zimejaa maneno ya sifa kwa Mungu, na ya kumtukuza sana. Kwamfano hebu tafakari maneno ya mistari hii..

Zaburi 145:1 “Ee Mungu wangu, Mfalme, nitakutukuza, Nitalihimidi jina lako milele na milele.

 2 Kila siku nitakuhimidi, Nitalisifu jina lako milele na milele.

 3 Bwana ndiye mkuu mwenye kusifiwa sana, Wala ukuu wake hautambulikani.

 4 Kizazi kwa kizazi kitayasifu matendo yako, Kitayatangaza matendo yako makuu.

 5 Nitaifikiri fahari ya utukufu wa adhama yako, Na matendo yako yote ya ajabu.

 6 Watu watayataja matendo yako ya kutisha, Nami nitausimulia ukuu wako.

 7 Watalihubiri kumbukumbu la wema wako mkuu. Wataiimba haki yako.

8 Bwana ana fadhili, ni mwingi wa huruma, Si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa rehema,

9 Bwana ni mwema kwa watu wote, Na rehema zake zi juu ya kazi zake zote”.

Hivyo na sisi pia inapendeza kama tukimwimbia Mungu wetu, wimbo wa sifa za kweli za kumtukuza yeye na kumpa yeye utukufu, kwasababu Mungu anaketi katika sifa, na ni vizuri kabisa tukamwimbia kwa vinanda vya zote,

Zaburi 147:1 “Haleluya. Msifuni Bwana; Maana ni vema kumwimbia Mungu wetu, Maana kwapendeza, kusifu ni kuzuri”

 Zaburi 149:1 “Haleluya. Mwimbieni Bwana wimbo mpya, Sifa zake katika kusanyiko la watauwa”

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255 789001312


Mada Nyinginezo:

TENZI ZA ROHONI

SIKU YA HUKUMU ITAKUWAJE?

JE KUHUDUMU KWA NYIMBO ZA INJILI KUKOJE?

YOTE NAMTOLEA YESU_Tenzi za Rohoni.

MWAMBA WENYE IMARA

Rudi Nyumbani:

Print this post

USIKATE TAMAA UNAPOPITIA MAGONJWA.

Unaweza kuwa umempokea Yesu, na unapitia ugonjwa ambao ni mbaya sana, na pengine usio na tiba, Na unajiuliza inawezekanikaje mimi mtu wa Mungu niwe na ugonjwa kama huu?, au mwanangu? Na mimi namcha Mungu sana na kujitahidi kwenda katika njia zake?.

Ukishafikia hali kama hiyo usianze kunung’unika, badala yake huo ndio uwe wakati wa kutafuta kulijua Neno la Mungu zaidi, kwasababu Neno la Mungu ndio dawa ya kutibu hali unayoipitia.

Sasa kama wewe unadhani ni mtumishi wa Mungu na unapitia hilo tatizo, hebu mtafakari Ayubu, labda yeye alimpendeza Mungu kuliko wewe, lakini aliponywa shida yake wakati wa Bwana ulipofika.

Tukimwacha huyo, yupo mtumishi mwingine wa Mungu, mkubwa sana katika biblia…ambaye Mungu alikuwa anazungumza naye uso kwa uso. Na biblia inasema baada yake hakukuwahi kutokea nabii kama huyo..

Kumbukumbu 34:10 “Wala hajainuka tena katika Israeli NABII KAMA MUSA, ambaye Bwana alimjua uso kwa uso;

 11 katika ishara zote na maajabu yote, ambayo Bwana alimtuma kuyatenda katika nchi ya Misri, kwa Farao, na kwa watumishi wake wote, na kwa nchi yake yote”

Huyo ni Musa ambaye wengi wetu tunamjua. Lakini Pamoja na Nabii huyu kupata kibali  hicho cha kipekee mbele za Mungu, lakini siku moja alishawahi kupata ugonjwa wa laana usio na tiba. Siku moja alishawahi kupata UKOMA tena ule mweupe unaowaka kama theluji.

Kutoka 4: 6 “Bwana akamwambia tena, Sasa tia mkono wako kifuani mwako. Akautia mkono wake kifuani mwake; naye alipoutoa, kumbe! MKONO WAKE ULIKUWA UNA UKOMA, umekuwa mweupe kama theluji”

Huyo ni mtumishi wa Mungu kapata ukoma, ugonjwa ambao ulikuwa ni mbaya kuliko wote nyakati za hizo, na ulikuwa ni ugonjwa wa laana na pigo na usiokuwa na tiba. Hivyo Musa aliupata huu ugonjwa mbele za Mungu. Unaweza kujiuliza kwanini Mungu hakufanya ishara nyingine, mfano wa hizo za nyoka, badala yake akampa hiyo ya Ugonjwa?.

Kwanini asingemwambia tu, tia mkono wako kifuani na ghafla kutokee katika mkono wake dhahabu au almasi, lakini kinyume chake mkono wake uligeuka kuwa mauti,

Na kwanini aitumie hiyo ishara kwenye mwili wa Musa mtumishi wake, na wala si kwa mtu mwingine asiye wake au mnyama?.

Hiyo ni kuonyesha kwamba hata watu wanaompendeza Mungu wakati mwingine watapitia pia magonjwa, tena yale hatari kabisa yasiyo na uwezekano wa kupona, lakini Bwana atayaondoa kama alivyoondoa kwa Ayubu na Musa..

Zaburi 34: 18 “Bwana yu karibu nao waliovunjika moyo, Na waliopondeka roho huwaokoa.

19 Mateso ya mwenye haki ni mengi, Lakini Bwana humponya nayo yote”.

Na ndio maana Bwana akamwonyesha Musa ile ishara ya kuugua na kuponywa, kuonyesha kwamba yeye ni Mungu atuponyaye..

“Akasema, Tia mkono wako kifuani mwako tena. Akautia mkono wake kifuani mwake tena, na alipoutoa kifuani mwake, kumbe! Umerudia hali ya mwili wake”.

Hivyo magonjwa, na dhiki za kitambo zisituogopeshe, na kutufanya tunung’unike, au moto wako wa kumtafuta Mungu uzime!.. ni za muda tu! Na zitaisha, Usiache kumwamini Mungu wala usipunguze kumtumikia, kwasababu Mungu atakuponya tu kwa wakati wake..na kila kitu kitarudi kama kilivyokuwa. Wala usiruhusu mawazo yako kila dakika yafikirie ugonjwa wako, mawazo kama hayo yakija yakatae na yapeleke kutafakari vitu vingine, kwasababu vita vikubwa vya shetani vipo katika akili zetu na mawazo yetu.

Mwisho, Neno la Mungu ndio silaha kama tulivyotangulia kusema..usipotaka kusoma Neno binafsi, na mara kwa mara, huwezi kamwe kumshinda shetani, hata uwe mwombaji kiasi gani.. Kwasababu shetani kinachomwogopesha sana, ni jinsi tunavyoyaelewa maandiko. Akijua unayaelewa maandiko vizuri, anakuwa anakuhofu sana..lakini akijua Neno hulielewi vizuri, wewe ndio unakuwa rafiki yake, atakutesa kwa kila aina ya mateso anayoyajua yeye. Na kama hujampokea Kristo neema inakuita leo, mpokee Yesu ufanyike kiumbe kipya.

Bwana akubariki sana.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255 789001312


Mada Nyinginezo:

USIWE NA HOFU, USHUKAPO CHINI.

NI JAMBO GANI LINALOMTAMANISHA SANA BWANA TUMWOMBE BILA KUKATA TAMAA?

RUDIA, TENA NA TENA KUMWOMBA MUNGU USIKATE TAMAA.

UTAFIKA WAKATI WA WEWE KUACHWA NYIKANI.

RUDI KUMPA MUNGU UTUKUFU.

Rudi Nyumbani:

Print this post

Kongwa ni nini kwenye biblia?(Wagalatia 5:1)

Kongwa ni kifungo cha shingoni. Kwa jina lingine ni nira. Tazama picha.

Hivi ni baadhi ya vifungu vinavyolitaja neno hilo;

Kumb 28:48 “kwa hiyo utawatumikia adui zako atakaowaleta Bwana juu yako, kwa njaa, na kwa kiu, na kwa uchi, na kwa uhitaji wa vitu vyote; naye atakuvika kongwa la chuma shingoni mwako, hata atakapokwisha kukuangamiza”.

Matendo 15:10 “Basi sasa mbona mnamjaribu Mungu na kuweka kongwa juu ya shingo za wanafunzi, ambalo baba zetu wala sisi hatukuweza kulichukua”.

Wagalatia 5:1 “Katika ungwana huo Kristo alituandika huru; kwa hiyo simameni, wala msinaswe tena chini ya kongwa la utumwa”.

1 Timotheo 6:1 “Wo wote walio chini ya kongwa, hali ya utumwa, na wawahesabie bwana zao kuwa wamestahili heshima yote, jina la Mungu lisitukanwe wala mafundisho yetu.

Walawi 26:13 “Mimi ndimi Bwana, Mungu wenu, niliyewaleta mtoke katika nchi ya Misri, ili msiwe watumwa wao; nami nimeivunja miti ya kongwa lenu, nikawaendesha mwende sawasawa”.

1Wafalme12:4 “Baba yako alilifanya zito kongwa letu; basi sasa utupunguzie utumwa mzito tuliotumikishwa na baba yako, na lile kongwa zito alilotutwika, nasi tutakutumikia”.

Swali ni je! sisi tupo chini ya kongwa la nani? La Mungu au la shetani?. Mtu yeyote ambaye hajaokoka, haijalishi atakuwa na mafanikio makubwa kiasi gani, tayari yupo chini ya kongwa la shetani, na anaongozwa kuelekea kuzimu. Lakini aliyemwamini Yesu na kuoshwa dhambi zake, yupo chini ya kongwa/Nira ya Kristo, akiongozwa kuelekea uzimani (Mathayo 28:11).

Hivyo tujitathimini sisi tupo upande gani, na kama hatujaokoka, basi tumpe Bwana leo maisha yetu ayaokoe, kwasababu hizi ni nyakati za mwisho.

Shalom

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255 789001312

Mada Nyinginezo:

Hori ni nini kibiblia (Waamuzi 5:17, Luka 2:7)?

Nyungu ni nini kibiblia?(Ayubu 41:20,31, Waamuzi 6:19)

Areopago ni nini? Kwanini mtume Paulo walimpeleka huko?

Arabuni maana yake ni nini?

Nyama zilizosongolewa ni zipi?Je kunywa damu ni dhambi?

Rudi Nyumbani:

Print this post

Hori ni nini kibiblia (Waamuzi 5:17, Luka 2:7)?

Neno hori lina maana mbili, maana ya kwanza ni ile inayofahamika na wengi, kuwa eneo la kulishia mifugo.

Biblia inatuambia Bwana Yesu alipozaliwa, alilazwa katika hori la kulia ng’ombe, hivyo maana ya kwanza ya neno hili ndio hiyo.

Luka 2:7 “akamzaa mwanawe, kifungua mimba, akamvika nguo za kitoto, akamlaza katika hori ya kulia ng’ombe, kwa sababu hawakupata nafasi katika nyumba ya wageni”.

Maana ya pili ya neno hori ni mkono wa bahari. Yaani eneo la bahari au ziwa lililoingia nchi kavu, tazama picha juu.

Neno hilo utalipata katika vifungu hivi;

Yoshua 15:4 “kisha ukaendelea hata Azmoni, na kutokea hapo penye kijito cha Misri; na matokeo ya huo mpaka yalikuwa baharini; huu ndio mpaka wenu wa upande wa kusini.

5 Na mpaka wa upande wa mashariki ulikuwa Bahari ya Chumvi, hata mwisho wa mto wa Yordani. Na mpaka wa upande wa kaskazini ulikuwa kutoka pale penye hori ya baharini mwisho wa mto wa Yordani;

6 na huo mpaka ukaendelea hata Beth-hogla, kisha ukaendelea upande wa kaskazini wa Beth-araba; kisha mpaka ukaendelea hata jiwe la Bohani mwana wa Reubeni”;

Yoshua 18:19 “kisha mpaka ukaendelea mbele ubavuni mwa Beth-hogla upande wa kaskazini; na matokeo ya mpaka yalikuwa katika ile hori ya kaskazini ya Bahari ya Chumvi, mwisho wa kusini wa mto wa Yordani; huo ndio mpaka wa upande wa kusini”.

Waamuzi 5:17 “Gileadi alikaa ng’ambo ya Yordani, Na Dani, mbona alikaa katika merikebu? Asheri alikaa kimya penye bandari ya bahari, Alikaa katika hori zake”.

Matendo 27:38 “Walipokwisha kushiba wakaipunguza shehena ya merikebu, wakiitupa ngano baharini.

39 Kulipokucha hawakuitambua ile nchi, ila waliona hori yenye ufuo, wakashauriana kuiegesha merikebu huko, kama ikiwezekana”.

Lakini tukirudi kwenye ile maana ya kwanza.

Ni kwanini Yesu alizaliwa katika hori la kulishia ng’ombe na si kwenye majumba ya kifahari? Ni kwasababu alikuwa ni sadaka iliyoandaliwa kuja kuchinjwa kwa ajili ya upatanisho wa dhambi za watu mbeleni, mfano wa ng’ombe au kondoo, hivyo ilimpasa na yeye azaliwe kule, kama ishara ya utumishi wake duniani.

Isaya 53:5 “Bali alijeruhiwa kwa makosa yetu, Alichubuliwa kwa maovu yetu; Adhabu ya amani yetu ilikuwa juu yake, Na kwa kupigwa kwake sisi tumepona.

6 Sisi sote kama kondoo tumepotea; Kila mmoja wetu amegeukia njia yake mwenyewe; Na Bwana ameweka juu yake Maovu yetu sisi sote.

7 Alionewa, lakini alinyenyekea, Wala hakufunua kinywa chake; Kama mwana-kondoo apelekwaye machinjoni, Na kama vile kondoo anyamazavyo Mbele yao wakatao manyoya yake; Naam, hakufunua kinywa chake”.

Shalom.

Tazama maana za maneno mengine ya biblia.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255 789001312

Mada Nyinginezo:

Baghala ni nini katika maandiko?(2Wafalme 5:16).

Konzi ni nini?(Mhubiri 4:6)

Shokoa ni nini katika biblia?

https://wingulamashahidi.org/2020/09/24/rangi-ya-kaharabu-ni-ipi-kibiblia/https://wingulamashahidi.org/2020/09/24/rangi-ya-kaharabu-ni-ipi-kibiblia/

Marijani ni nini katika biblia(Ayubu 28:18,Mithali 8:11)?

SIKU YA UNYAKUO ITAKUKUTAJE?

Rudi Nyumbani:

Print this post

ONDOKA YESU, TUACHIE MAPEPO.

Shalom karibu tuyatafakari maandiko, leo tutaangazia kile kisa cha Yesu na yule mtu aliyekuwa na mapepo kule makaburini. Pengine ulishawahi kuisoma hii habari mara nyingi, lakini naomba tuisome tena kwa mara nyingine, kwasababu Neno la Mungu halina mwisho wa kujifunza (Zab 12:6). Hivyo usomapo zingatia hususani hivyo vipengele vilivyowekwa katika herufi kubwa.

Marko 5 : 1-19

“ 1 Wakafika ng’ambo ya bahari mpaka nchi ya Wagerasi.

2 Na alipokwisha kushuka chomboni, mara alikutana na mtu, ambaye ametoka makaburini, mwenye pepo mchafu;

3 makao yake yalikuwa pale makaburini; wala hakuna mtu ye yote aliyeweza kumfunga tena, hata kwa minyororo;

4 kwa sababu alikuwa amefungwa mara nyingi kwa pingu na minyororo, akaikata ile minyororo, na kuzivunja-vunja zile pingu; wala hakuna mtu aliyekuwa na nguvu za kumshinda.

5 Na sikuzote, usiku na mchana, alikuwako makaburini na milimani, akipiga kelele na kujikata-kata kwa mawe.

6 Na alipomwona Yesu kwa mbali, alipiga mbio, akamsujudia;

7 akapiga kelele kwa sauti kuu, akasema, Nina nini nawe, Yesu, Mwana wa Mungu aliye juu? Nakuapisha kwa Mungu usinitese.

8 Kwa sababu amemwambia, Ewe pepo mchafu, mtoke mtu huyu.

9 Akamwuliza, Jina lako nani? Akamjibu, Jina langu ni Legioni, kwa kuwa tu wengi.

10 AKAMSIHI SANA ASIWAPELEKE NJE YA NCHI ILE.

11 Na hapo milimani palikuwa na kundi kubwa la nguruwe, wakilisha.

12 Pepo wote wakamsihi, wakisema, Tupeleke katika nguruwe, tupate kuwaingia wao.

13 Akawapa ruhusa. Wale pepo wachafu wakatoka, wakaingia katika wale nguruwe; nalo kundi lote likatelemka kwa kasi gengeni, wakaingia baharini, wapata elfu mbili; wakafa baharini.

14 Wachungaji wao wakakimbia, wakaieneza habari mjini na mashambani. Watu wakatoka walione lililotokea.

15 Wakamwendea Yesu, wakamwona yule mwenye pepo, ameketi, amevaa nguo, ana akili zake, naye ndiye aliyekuwa na lile jeshi; wakaogopa.

16 Na wale waliokuwa wameona waliwaeleza ni mambo gani yaliyompata yule mwenye pepo, na habari za nguruwe.

17 WAKAANZA KUMSIHI AONDOKE MIPAKANI MWAO.

18 Naye alipokuwa akipanda chomboni, yule aliyekuwa na pepo akamsihi kwamba awe pamoja naye;

19 lakini hakumruhusu, bali alimwambia, Enenda zako nyumbani kwako, kwa watu wa kwenu, kawahubiri ni mambo gani makuu aliyokutendea Bwana, na jinsi alivyokurehemu”.

Utaona katika habari hiyo, mapepo hayo yalipokutana tu na Yesu, na kuambiwa wamtoke yule mtu, biblia inatuambia yalianza “kumsihi sana Yesu” Yalianza kumlilia na kumwomba kwa nguvu sana na kwa bidii, kwamba Bwana asiyafukuze nje ya nchi ile?.

Ulishawahi kujiuliza ni kwanini hayakutaka kupelekwa nje ya nchi ile?. Sio kwasababu yangeshindwa kuishi, hapana lakini ni kwasababu tayari yalikuwa yameshawezeka mambo yao mengi ya uharibifu katika mji ule, hivyo kuondolewa pale na kwenda kuanzisha uharibifu mwingine ugenini, si jambo dogo itakuwa ni hasara kubwa kwao.

Hiyo inatupa picha kuwa mapepo yamejigawanya kulingana na maeneo ya kijeografia, hivyo yale mapepo yaliyokuwa ndani ya yule mtu, yalijua mchoro mzima wa mji ule, yalijua takribani watu wote waliokuwa katika ule mji, na mipango ya kuwaangamiza.

Sasa tukirudi kwenye habari tunaona, kulikuwa na wale watu wanaochunga nguruwe pembezoni wakitazama kila kitu kinachoendelea, wakayasikia kabisa yale mapepo yakimsihi sana Bwana pale, pengine kwa nusu saa, au lisaa hatujui lakini yalikuwa yanamlilia Bwana kweli kweli, Na mwisho wa siku Bwana hakuyaondoa, aliyaacha yaendelee kubaki tu katika ule mji isipokuwa tu yamtoke yule kichaa.

Hivyo wale watu walipoona vile, wakaenda kuitana kule mijini na vijijini, sasa badala wamsihi Yesu aendelee kubaki katika ule mji ili awasaidie kwasababu maadui zao bado wapo mjini, kinyume chake wao ndio wakaanza kumsihi Yesu aondoke mipakani mwao.?

Unaona hilo? Ni sawa na kusema Ondoka Yesu, tuachie mapepo. Cha ajabu nao pia wakaiga mbinu ya mapepo, ya kusihi, wakamsihi Bwana pale pengine kwa dakika kadhaa..Na mwisho wa siku Yesu akawasikia nao pia, akapanda zake chomboni mwake akaondoka, hawakumpa hata nafasi ya kulala siku moja wala kuingia mjini maili moja, alifika pale ufukweni na kugeuza siku hiyo hiyo.

Tunajifunza nini?

Mashetani nayo yanamwomba Mungu, na Mungu anayasikia. Ukitaka kuthibitisha hilo kasome (1Wafalme 22:20-23, na Ayubu 1:9).

Hivyo yanakuwa na kibali maalumu cha kuendelea kubaki mahali fulani, au ndani ya mtu fulani. Sasa kama sisi tutakuwa ni watu wa kuukataa wokovu, ni watu wa kupinga njia za Mungu pale anapotujia kwa lengo la kutuponya roho zetu..Kamwe usitazamie kama utaweza kushindana na majeshi ya mapepo wabaya.

Wale watu waliona jinsi mapepo yale yalivyokuwa mabaya, kwanza yanawafanya watu kuwa vichaa, pili yanafanya kazi ya kuua, ndio maana utaona yalienda kuwauwa wale nguruwe ziwani, kuonyesha kuwa kazi yao kubwa ni uuaji, lakini walimkataa, Sasa kwa kuwa walimkataa Yesu wakamfukuza, yale mapepo pengine yalirudi kazini yakaenda kuwafanya vichaa wengine hata elfu kumi kwa namna ile, na kusababisha vifo vingi.

Hivyo nasi tujue kuwa tusipomsihi Yesu, mapepo yatamsihi kwa niaba yetu, na yatakuwa na haki kabisa ya kukaa ndani yetu, au katika jamii yetu, au koo zetu, kwasababu Yesu hayupo katikati yetu. Tumemfukuza atoke mjini kwetu.

Mpokee Bwana, hii dunia pasipo yeye hakuna ushindi. Shetani kazi yake ni kuharibu (1Petro 5:8-9).

Kama upo bado nje ya Kristo ni vema ukatubu dhambi zako, umrudie yeye leo, Na kama hujabatizwa basi tafuta pia kufanya hivyo mapema sana.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255 789001312


Mada Nyinginezo:

MAPEPO NI NINI?

Je kupiga miayo ni ishara ya mapepo?

AKAMSHIKA MKONO YULE KIPOFU, AKAMCHUKUA NJE YA KIJIJI.

PALE UNAPOKUWA NA SABABU ZA KUMLAUMU MTU, UFANYE NINI?

MAJINI WAZURI WAPO?

Rudi Nyumbani:

Print this post

Je tunapaswa tushiriki Meza ya Bwana mara ngapi?

SWALI: Je tunapaswa tushiriki Meza ya Bwana mara ngapi kwa Mwezi, au kwa Mwaka?


Jina la Bwana wetu Yesu Kristo libarikiwe. Ni neema ya Mungu tumeiona siku mpya ya leo, hivyo nakukaribisha tujifunze Biblia pamoja.

Kutokana na mkanganyiko mkubwa wa kila mmoja kusema ratiba yake, na kuiona kuwa ndio ipo sahihi, imesababisha kuzalika kwa madhehebu mengi, na hivyo kuzidi kuufanya ukristo uwe mgumu kueleweka zaidi kwa wale walio nje. Lakini maandiko yanasema..

2Timotheo 2;19  “Lakini msingi wa Mungu ulio imara umesimama, wenye muhuri hii, Bwana awajua walio wake…”.

Hivyo haijalishi kuna mkorogo mkubwa kiasi gani duniani, lakini walio wa Mungu, hawatapotea kamwe.

Tukirudi katika Maandiko tunasoma mstari ufuatao…

Luka 22:19  “Akatwaa mkate, akashukuru, akaumega, akawapa, akisema, [Huu ndio mwili wangu unaotolewa kwa ajili yenu; fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu”.

Hapo biblia imesema “fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu”.. Maana yake wafanye mara kwa mara ndio maana kaongezea neno “kwa ukumbusho wangu”, mbele yake. Sasa katika hali ya kawaida hata nikikupa picha yangu, nikakwambia ichukue hii kwa ukumbusho wangu..haimaanishi kwamba uichukue iangalie mara moja kisha ukaitupe.. la! Bali nimemaanisha uihifadhi, kila unaitazama unikumbuke..na hiyo inaweza kuwa kwa wiki mara moja, au kwa mwezi mara moja..lakini ni ngumu kuwa kwa mwaka mara moja..Kama ukiitazama picha yangu kwa miaka 3 mara moja, ni wazi kuwa mimi sipo moyoni mwako kwa kiwango kikubwa, ndio maana hata hamu ya kunikumbuka huna. Lakini kama nipo moyoni mwako kikweli kweli, ile picha haiwezi kupita siku mbili, au wiki hujaitazama.

Sasa katika kushiriki meza ya Bwana ni hivyo hivyo, Bwana hajaweka kwamba ni mara ngapi kwa wiki, au kwa mwezi au kwa mwaka tunapaswa tuishiriki. Lakini kwa mkristo kweli aliyezaliwa mara ya Pili, ambaye anajua umuhimu wa kuishiriki meza ya Bwana, hawezi kusubiria kulifanya hilo tendo mara moja kwa mwaka, au mara mbili au mara tatu?

Ni sawa na biblia ilivyosema katika Waebrania 10:25  “wala tusiache kukusanyika pamoja, kama ilivyo desturi ya wengine; bali tuonyane; na kuzidi kufanya hivyo, kwa kadiri mwonavyo siku ile kuwa inakaribia”.

Hapo biblia imesema “tusiache kukusanyika” lakini haijasema ni mara ngapi kwa wiki tukusanyike, au mara ngapi kwa mwezi au mwaka. Hivyo kwa mtu aliyezaliwa mara ya pili, na anayejua umuhimu hasa wa kukusanyika pamoja..haiwezi ikapita wiki bila kuhudhuria kwenye kusanyiko pamoja na wenzake. Kanisa la kwanza walijua umuhimu wa kukusanyika na hivyo wakaona kiwango cha chini cha kukusanyika pamoja angalau kiwe mara moja kwa wiki.Na sisi tunafuata utaratibu huo huo, angalau tukusanyike mara moja kwa wiki, ili kujinoa sisi kwa sisi. Lakini Bwana Yesu hakuwapa masharti wala ratiba ya siku za kukusanyika pamoja.

Kadhalika biblia inasema “ Ombeni bila kukoma (1Wathesalonike 5:17)”.  Haijatoa ratiba ya kwamba tuombe mara ngapi kwa wiki, au mwezi au mwaka.. Lakini kwa mtu aliyezaliwa kweli mara ya pili na ambaye Roho Mtakatifu anaugua ndani yake, hawezi kupitisha siku mbili hajaingia kabisa magotini…Lakini yule asiyejua umuhimu wa maombi katika maisha yake, anaweza kupitisha hata mwezi au miezi kadhaa bila kuomba kabisa.

Hivyo hata katika kushiriki meza ya Bwana, kama kweli umezaliwa mara ya pili, na unampenda Bwana, na umepata kujua umuhimu wa kushiriki meza ya Bwana, na jinsi gani tendo hilo lina madhara makubwa sana katika ulimwengu wa roho, huwezi kulifanya kwa mwaka mara moja au mara mbili.

Zipo dini ambazo ibada za kushiriki meza ya Bwana ni mara moja kwa mwaka. Na zinatumia andiko la kwamba Kristo alishiriki na wanafunzi wake mara moja tu, msimu ule wa pasaka. Hivyo na dini hizo zinasema kushiriki meza ya Bwana ni mara moja tu, na tena ni ile siku ya Pasaka.

Ndugu usidanganyike!, Meza ya Bwana tunaweza kushiriki mara kwa mara kwa kadiri tupatavyo nafasi ya kukutanika. Na sio tu meza ya Bwana ndio agizo la msingi.. Yapo na maagizo mengine yaliyo ya muhimu hivyo hivyo, kama KUTAWADHANA MIGUU. Ni lazima sisi kwa sisi tutawadhane miguu mara kwa mara tunapokusanyika pamoja, kama Bwana alivyotupa maagizo hayo. Na pia ni lazima tuwe waombaji wa mara kwa mara, angalau kila siku. Hayo yote ni kwa faida yetu wenyewe.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255 789001312

Mada Nyinginezo:

MEZA YA BWANA, NA KUTAWADHANA MIGUU.

DAKIKA MOJA TU, INAKUFANYA UMWAMINI SHETANI?

Ni kwa nini tunasema tunamwabudu MUNGU aliye hai ,Je! wale wanaomwabudu shetani sio mungu wao aliye hai?

UPENDO WA KRISTO WATUBIDISHA;

Rudi Nyumbani:

Print this post

Konzi ni nini?(Mhubiri 4:6)

Konzi ni kiasi cha kujaa mkono.

Kama vile ilivyo kiasi cha kujaa ndoo kinavyoitwa debe, vivyo hivyo na kiasi cha kujaa mkono kinaitwa konzi. Tazama picha juu.

Hivi ni baadhi ya vifungu ambavyo utakutana na Neno hilo;

Mithali 30:4 “Ni nani aliyepanda mbinguni na kushuka chini? Ni nani aliyekamata upepo kwa makonzi yake? Ni nani aliyeyafunga maji ndani ya nguo yake? Ni nani aliyefanya imara ncha zote za nchi? Jina lake ni nani? Na ni nani jina la mwanawe, kama wajua”?

Mhubiri 4:6 “Heri konzi moja pamoja na utulivu, Kuliko konzi mbili pamoja na taabu; na kujilisha upepo”.

Isaya 40:12 “Ni nani aliyeyapima maji kwa konzi ya mkono wake, na kuzikadiri mbingu kwa shubiri, na kuyashika mavumbi ya dunia katika pishi, na kuipima milima kwa uzani, na vilima kama kwa mizani”?

Kutoka 9:8 “Bwana akawaambia Musa na Haruni, Jitwalieni konzi za majivu ya tanuuni, kisha Musa na ayarushe juu kuelekea mbinguni mbele ya Farao”.

Soma pia, Ezekieli 13:19, Walawi 2:2

Lakini biblia inatuambia pia..

Mhubiri 4:6 “Heri konzi moja pamoja na utulivu, Kuliko konzi mbili pamoja na taabu; na kujilisha upepo”.

Tunapokuwa na kidogo lakini kinatupa amani, ni bora kuliko kuwa na vingi lakini vya malalamiko,manung’uniko, vinyongo, hasira, au  wivu.n.k. Bwana atusaidie.

Shalom.

Tazama tafsiri ya maneno mengine ya biblia chini.

Ikiwa utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255 789001312

Mada Nyinginezo:

Baghala ni nini katika maandiko?(2Wafalme 5:16).

Mavyaa ni nani kibiblia?(Mika 7:6)

SIFONGO NA SIKI NI NINI?

VITABU VYA BIBLIA: Sehemu ya 1

Amin, nawaambia, Kizazi hiki hakitapita, hata hayo yote yatakapotimia..!!

Rudi Nyumbani:

Print this post

Baghala ni nini katika maandiko?(2Wafalme 5:16).

Baghala kwa jina lingine ni nyumbu, lakini sio Yule nyumbu wa porini, bali ni mnyama chotara anayezalishwa kwa kukutanishwa Farasi na Punda. Tazama picha juu.

Utalisoma Neno hilo (Baghala) katika kifungu hichi.

2Wafalme 5:16 “Lakini akasema, Kama Bwana aishivyo, ambaye nimesimama mbele yake, sipokei kitu. Akamshurutisha apokee; lakini akakataa.

17 Naamani akasema; Kama sivyo, lakini mtumwa wako na apewe mzigo wa udongo wa BAGHALA wawili; kwa maana mtumwa wako hatatoa tena sadaka ya kuteketezwa wala dhabihu kwa miungu mingine, ila kwa Bwana”.

Zamani wana wa Israeli walikuwa wanatumia aidha punda au farasi, lakini baadaye tunakuja kuona sehemu nyingi walianza kuwatumia nyumbu katika shughuli zao nyingi, badala ya punda au farasi, kwasababu waligundua  ni wavumilivu, na wagumu, na aanabeba mizigo mikubwa zaidi kuliko punda, na wanaishi  mara zaidi ya farasi, japo ni wafupi kidogo ya farasi.

Hivyo sehemu zote utakazokutana nazo kwenye biblia zinamzungumzia nyumbu, basi ujue ni mnyama huyu chotara. Vifuatavyo ni baadhi ya vifungu vinavyomwelezea;

Zaburi 32:9 “Msiwe kama farasi wala nyumbu, Walio hawana akili. Kwa matandiko ya lijamu na hatamu Sharti kuwazuia hao, au hawatakukaribia”.

Ezra 2:66 “Farasi zao walikuwa mia saba thelathini na sita; nyumbu zao, mia mbili arobaini na watano”;

2Samweli 18:9 “Na kwa bahati Absalomu akakutana na watumishi wa Daudi. Naye Absalomu alikuwa amepanda nyumbu wake, na yule nyumbu akapita chini ya matawi manene ya mwaloni mkubwa, hata kichwa chake kikakwama katika mwaloni huo, akanyakuliwa juu kati ya mbingu na nchi; na yule nyumbu aliyekuwa chini yake akaenda mbele”.

1Wafalme 10:25 “Wakaleta kila mtu zawadi yake, vyombo vya fedha, na vyombo vya dhahabu, na mavazi, na silaha, na manukato, na farasi, na nyumbu, hesabu yake ya mwaka kwa mwaka”.

Soma pia Nehemia 7:68.

Hivyo kwa kuhitimisha, ni kwamba Baghala ndio huyu nyumbu, tunaliyemsoma. Tofauti na farasi na Punda.

Ubarikiwe.

Tazama maana ya maneno mengine ya biblia chini.

Pia ikiwa utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255 789001312

Mada Nyinginezo:

Daawa ni nini kama tunavyosoma katika biblia?

Njuga ni nini (Isaya 3:16, Zekaria 14:20)?

Shokoa ni nini katika biblia?

USIPIGE MATEKE MCHOKOO!

NJONI, NUNUENI MLE NA MNYWE.

Kulabu ni nini katika biblia?(2Wafalme 19:27)

Rudi Nyumbani:

Print this post

UTAPENDA KUCHANGIA HUDUMA HII?

Tutamshukuru Mungu kwa ajili yako, kwa mchango wako, ili kuifanya injili hii isonge mbele Tuma sadaka yako kwa namba hizi:
Airtel:+255789001312 -Devis Magembe
Mpesa: +255767992434-Denis Magembe


This will close in 315 seconds