DON’T BE AFRAID WHEN YOU GO DOWN.

MAOMBOLEZO YA HADADRIMONI.

SWALI: Naomba kufahamu maombolezo ya Hadadrimoni tunayoyasoma katika Zekaria 12:11 ni maombolezo gani hayo?

Zekaria 12:11 “Siku hiyo kutakuwa na maombolezo makuu huko Yerusalemu, kama maombolezo ya Hadadrimoni katika bonde la Megido”.


JIBU: Hadadrimoni ni eneo lililokuwa sehemu ya bonde lijulikanalo kama Megido huko Israeli. Bonde hili lilisifika kwa vita, na Zaidi sana kuuawa kwa baadhi ya viongozi wakubwa. Hivyo kupelekea maombolezo makubwa sana kwa watu waliouliwa viongozi wao.

Mfano katika Habari hii, inamlenga mfalme Yosia, ambaye ndiye aliyekuwa tumaini la mwisho la Taifa la Israeli. Kama wewe ni msomaji wa biblia utakumbuka, Yosia alikuwa mfalme aliyemcha Mungu sana kuliko wafalme wote wa Israeli,tukimwondoa Daudi, na  yeye ndiye aliyefanikiwa kuondoa sanamu zote Israeli kipindi kile, Na ndiye mfalme ambaye kuzaliwa kwake kulitabiriwa miaka mingi sana kabla hajazaliwa.

Hivyo waisraeli walimwona kama ndiye tumaini pekee waliobakiwa nalo.

Lakini siku moja alitoka kwenda kupigana vita na mfalme wa Misri aliyeitwa Neko. Na kinyume na matazamio yake, aliuliwa, na mahali alipouliwa palikuwa ni hapo Hadadrimoni katika bonde la Megido.

Israeli nzima iliposikia, ilimwombolezea maombolezo makubwa sana,  taa ya Israeli kuzima ghafla, mpaka wakamwekea kumbukumbuku lake la kila mwaka akumbukwe.

2Wafalme 23:29 “Katika siku zake, Farao-neko, mfalme wa Misri, akakwea ili kupigana na mfalme wa Ashuru, akafika mto Frati; naye mfalme Yosia akaenda kupigana naye; naye mfalme wa Misri akamwua huko Megido, hapo alipoonana naye”.

2Nyakati 35:25 “Naye Yeremia akamlilia Yosia; na waimbaji wote waume kwa wake wakamtaja Yosia katika maombolezo yao, hata leo; hata wakayafanya kuwa ada kwa Israeli; nayo, tazama, yameandikwa katika maombolezo”.

Hivyo Mungu akatumia kivuli hicho kueleza jinsi taifa la Israeli litakavyokuja kuomboleza huko mbeleni, siku watakapopewa neema ya kumtambua Kristo. Biblia inasema wayahudi watamwombolezea Yesu waliyemchoma, watalia kama vile mtu aliyefiwa na mwana wake wa pekee, mfano wa pigo la wamisri la kuuliwa wazaliwa wao wa kwanza, jinsi walivyokuwa na maombolezo makuu.

Kama vile, maombolezo ya Yosia katika bonde la Hadadrimoni, Waisraeli walivyombolezea mfalme wao, kwa uchungu mwingi, ndivyo itakavyokuwa siku hiyo watakapomwagiwa neema ya kumtambua Kristo..

Zekaria 12:10 “Nami nitawamwagia watu wa nyumba ya Daudi, na wenyeji wa Yerusalemu, roho ya neema na kuomba; nao watamtazama yeye ambaye walimchoma; nao watamwombolezea, kama vile mtu amwombolezeavyo mwanawe wa pekee; nao wataona uchungu kwa ajili yake, kama vile mtu aonavyo uchungu kwa ajili ya mzaliwa wake wa kwanza.

11 Siku hiyo kutakuwa na maombolezo makuu huko Yerusalemu, KAMA MAOMBOLEZO YA HADADRIMONI KATIKA BONDE LA MEGIDO.

12 Nayo nchi itaomboleza, kila jamaa peke yake; jamaa ya nyumba ya Daudi peke yao, na wake zao peke yao; jamaa ya nyumba ya Nathani peke yao, na wake zao peke yao;

13 jamaa ya nyumba ya Lawi peke yao, na wake zao peke yao; jamaa ya nyumba ya Shimei peke yao, na wake zao peke yao.

14 Jamaa zote zilizosalia, kila jamaa peke yake, na wake zao peke yao”.

Ndugu, Kipindi si kirefu hii neema inayochezewa leo hii, itageuka na kuwarudia wayahudi. Kipindi hicho unyakuo utakuwa umeshapita, na Roho Mtakatifu hayupo tena kwetu sisi watu wa mataifa, bali kwa watu wake Israeli. Dunia itastaajabia, kuona watu hawa wametolea wapi moyo huo wa kujuta kwa ajili ya Yesu ambaye leo hii wanamkataa.

Kwani wayahudi hawa wakati huo, biblia inasema watajitenga, familia kwa familia, ukoo kwa ukoo, kila moja atakuwa na maombolezo yake makuu sana haradharani na sirini, kudhihirisha kazi ya Roho Mtakatifu juu yao. Sasa wakati huo ndio Mungu atakuwa anawaandaa ili kuwarudishia  ufalme ambao waliutazamia kutoka kwa masihi wao, sawasawa na lile ulizo la mitume (Matendo 1:6)

Ndugu, ukishaona mabadiliko haya kwa wayahudi, ujue umeshaachwa katika unyakuo, vilevile hii dunia itakuwa na kipindi kifupi sana kisichozidi miaka 7 hadi iishe. Leo hii tumeshaona Israeli imekuwa taifa, wote wamesharudi kwao. Unadhani wanachosubiria ni nini kama sio kurudiwa wakati wowote.

Bwana Yesu alisema,

Mathayo 24:32 “Basi kwa mtini jifunzeni mfano; tawi lake likiisha kuchipuka na kuchanua majani, mwatambua ya kuwa wakati wa mavuno u karibu”;

Mtini unawakilisha taifa la Israeli (Yer 24), Hivyo tuonapo Israeli leo hii inachipuka, tujue kuwa wakati wa mavuno umeshafika.

Je!, unalitambua hilo? Bado unaipuuzia hii neema ambayo hatuna nayo muda mrefu?. Una Habari kuwa unyakuo ni wakati wowote, na hatua zake tayari zimeshaanza?. Wakati tulionao sasa si wakati wa kubembelezewa wokovu, Injili imeshazagaa kila mahali, watu wote wameshasikia, ni wakati wa kujitakasa, wewe ambaye tayari umeshaokoka. Lakini kama bado upo nje ya neema kipindi hichi? Utakuwa ni wa ajabu kweli.

Unasubiria siku Fulani, neema ikufikie? wakati neema ya wokovu ipo tayari kila mahali, unasubiria ikufikieje tena? Tambua kuwa  njia imeshasonga, na wengi wanatamani waingie wanashindwa, kwasababu upotofu mwingi upo duniani, na wewe bado tu unaisubiri.. Ni kuwa makini sana. Neema inakimbilia Israeli sasa, jicho la Bwana linaelekea kule sasa, kwani muda wetu umeshakwisha.

Bwana atusaidie.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

SIKU YA TAABU YA YAKOBO.

DHIKI KUU INAKUJA NA UNYAKUO UPO KARIBU.

JE KANISA LITAPITIA DHIKI KUU?

MAPIGO YA VITASA SABA, NA SIKU YA BWANA.

Amin, nawaambia, Kizazi hiki hakitapita.

Uru wa Ukaldayo ni nini?

Rudi nyumbani

Print this post

Uru wa Ukaldayo ni nini?

Neno “Uru” kama lilivyo katika Mwanzo 11:28, lina maana gani?.

Jibu: Tusome,

Mwanzo 11:28 “Harani akafa kabla ya baba yake Tera katika nchi aliyozaliwa, yaani, katika URU wa Wakaldayo.

29 Abramu na Nahori wakajitwalia wake. Jina la mkewe Abramu aliitwa Sarai, na jina la mkewe Nahori aliitwa Milka, binti Harani, ambaye alikuwa baba wa Milka na wa Iska”.

Neno “Uru”. Maana yake ni ARDHI/HIMAYA.. Kwahiyo hapo biblia iliposema “Harani akafa kabla ya baba yake Tera katika nchi aliyozaliwa, yaani, katika URU wa Wakaldayo”.. Maana yake ni kwamba “Tera alikufa katika Nchi/Himaya ya Wakaldayo”.

Kulingana na historia zilikuwepo “Uru” nyingi, enzi za kale, zilikuwepo Uru za Waashuri, Uru za Waajemi n.k.. Lakini iliyotajwa kwenye biblia ni moja tu ambayo ni Uru ya wakaldayo. (Kujua Wakaldayo walikuwa ni watu gani fungua hapa >> Wakaldayo)

Lakini kikubwa tunachoweza kujifunza ni kuwa Abramu aliambiwa atoke katika  nchi aliyozaliwa “Uru wa Wakaldayo”, aende nchi nyingine.

Ikifunua kuwa Mungu anapomwita mtu anapaswa atoke pale alipo na kwenda sehemu nyingine kiroho.

Mwanzo 12:1 “Bwana akamwambia Abramu, Toka wewe katika nchi yako, na jamaa zako, na nyumba ya baba yako, uende mpaka nchi nitakayokuonyesha;

 2 nami nitakufanya wewe kuwa taifa kubwa, na kukubariki, na kulikuza jina lako; nawe uwe baraka

 3 nami nitawabariki wakubarikio, naye akulaaniye nitamlaani; na katika wewe jamaa zote za dunia watabarikiwa”.

Je tangu ulipomwamini Yesu umetoka katika himaya ya ulevi?, umetoka katika himaya za wazinzi?, umetoka katika himaya za wachawi na washirikina, kama bado, ni Dhahiri kuwa bado hujaanza safari ya Wokovu. Anza leo kwa kujitenga na mambo hayo.

Maran atha!

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312


Mada Nyinginezo:

JUMA LA SABINI (70) LA DANIELI

TUMEFANYIKA KUWA WANA WA MUNGU!

JINSI YA KUSOMA BIBLIA.

VIPINDI VINNE VYA MAISHA VILIVYO VIGUMU MTU KUMKUMBUKA MUUMBA WAKE.

Nini maana ya mtakayoyafunga duniani, yatakuwa yamefungwa mbinguni?

Rudi nyumbani

Print this post

Je Mungu huwa anadhihaki watu?

Je Mungu huwa anadhihaki watu kulingana na Mithali 1:26 na Zaburi 59:8?.

Jibu ni ndio!!..Mungu anadhihaki!!.. na sio tu kudhihaki, bali pia anafadhaisha, na vilevile anahuzunisha watu..

Lakini lengo la kudhihaki watu, au kuhuzunisha watu, au kufadhaisha watu ni tofauti na lengo kama tulilonalo sisi..

Sisi tunawadhihaki watu ili tuwakomoe, au ili tuwakomeshe, au ili  tuwatese.. Lakini Mungu lengo lake si hilo, yeye hatudhihaki ili atukomoe, au atukomeshe….Lengo lake yeye ni sisi tutubu, tugeuke, tuone aibu kwa njia zetu mbaya, kisha tutubu na kuacha njia zetu mbaya. Na tukishatubu basi anatufurahisha na kutufariji.

Ndio maana maandiko yanasema..

Mithali 1:23 “GEUKENI KWA AJILI YA MAONYO YANGU; Tazama, nitawamwagia roho yangu, Na kuwajulisheni maneno yangu.

24 Kwa kuwa nimeita, nanyi mkakataa; Nimeunyosha mkono wangu, asiangalie mtu;

25 Bali mmebatilisha shauri langu, Wala hamkutaka maonyo yangu;

26 Mimi nami nitacheka siku ya msiba wenu, NITADHIHAKI HOFU YENU IFIKAPO”.

Je! Unataka kudhihakiwa na Mungu siku ya msiba wako, au tabu yako..je unataka kuchekwa siku na shida yako?.

Kama hutaki basi jitenge na ulimwengu, na dhambi… Hizo ndizo zinazotuficha uso wa Mungu mbali nasi. Lakini habari njema ni kwamba, Bwana hafurahii misiba yetu, wala tabu zetu, lengo lake ni sisi tuone aibu,  tuache dhambi zetu… ili atupe faraja na furaha.

Maombolezo 3:31 “Kwa kuwa Bwana hatamtupa mtu Hata milele.

32 Maana AJAPOMHUZUNISHA atamrehemu, Kwa kadiri ya wingi wa huruma zake.

33 Maana moyo wake hapendi kuwatesa wanadamu. Wala kuwahuzunisha”.

Maran atha!

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312


Mada Nyinginezo:

BASI, IWENI NA HURUMA, KAMA BABA YENU ALIVYO NA HURUMA

Nini maana ya Hukumu haina huruma kwake yeye asiyeona huruma?

JE! NI WAPI UTAPOKEA HISIA ZA KWELI ZA KI-MUNGU?

NDIPO HUENDA AKACHUKUA PEPO WENGINE SABA.

Biblia inamaanisha nini inaposema “Mwenye haki huufikiri uhai wa mnyama wake”?

Rudi nyumbani

Print this post

Je! Mtu ambaye hajaoa anaruhusiwa kulichunga kundi?

SWALI: Shalom… Pastor naomba kuuliza je ni sahihi mtumishi kuongoza kanisa hajafunga ndoa? na anaweza kubatiza washirika? Amina.


JIBU: Kigezo cha mtu kuwa Kiongozi wa kanisa, na kufanya kazi zote za madhabahuni, ikiwemo kubatiza, kuwawekea watu mikono ya utumishi, n.k. vimetolewa katika kitabu cha 1Timotheo 3:1-7

1 Timotheo 3 : 1-16

1 Ni neno la kuaminiwa; mtu akitaka kazi ya askofu, atamani kazi njema.

2 Basi imempasa askofu awe mtu asiyelaumika, mume wa mke mmoja, mwenye kiasi na busara, mtu wa utaratibu, mkaribishaji, ajuaye kufundisha;

3 si mtu wa kuzoelea ulevi, si mpiga watu; bali awe mpole; si mtu wa kujadiliana, wala asiwe mwenye kupenda fedha;

4 mwenye kuisimamia nyumba yake vema, ajuaye kutiisha watoto katika ustahivu;

5 (yaani, mtu asiyejua kuisimamia nyumba yake mwenyewe, atalitunzaje Kanisa la Mungu?)

6 Wala asiwe mtu aliyeongoka karibu, asije akajivuna akaanguka katika hukumu ya Ibilisi.

7 Tena imempasa kushuhudiwa mema na watu walio nje; ili asianguke katika lawama na mtego wa Ibilisi.

Askofu maana yake ni mwangalizi wa kanisa, Hivyo yeyote anayelichunga kanisa, awe ni mchungaji, mwalimu, Mtume, maana yeye ndio mwangalizi basi vigezo hivyo vinamuhusu.

Lakini katika vigezo hivyo vyote, hakuna hata kimoja, kinachosema, ni lazima aoe.. Isipokuwa anasema Askofu ni lazima awe ni mume wa mke mmoja..Akiwa na maana kwamba ikiwa ni mwana-ndoa basi, anapaswa awe ni mume wa mke mmoja, na si Zaidi, kama anao wake wawili au watatu, tayari ameshakidhi vigezo vya kutostahili kuitwa mchungaji.

Lakini ikiwa ni mtu ambaye, hajaoa lakini ameshika vigezo vyote, hivyo, yaani, ni mtu asiyelaumika, si mlevi, mpole, si mpenda fedha, aliyeshuhudiwa na watu ni mwema, amekomaa kiroho. Basi huyo anavigezo vyote vya kuwa mchungaji, au kiongozi yoyote wa kanisa.

Mtume Paulo hakuwa ameoa, lakini alikuwa ni mwangalizi wa makanisa yote yaliyokuwa Asia, na mataifa mengine, Na Zaidi sana yeye ndiye aliyetoa mwongozi wa mafundisho ya ndoa.

Hivyo kuoa/ kutokuoa, si takwa, la kuwa askofu.

Kinyume chake mtume Paulo,alishauri  watu wote wawe kama yeye (yaani wasioe), kwasababu watu wasiooa inawapa wigo mpana wa kumtumikia Mungu bila kuvutwa na mambo mengine, ikiwa wamemaanisha kweli kujikita kwa Bwana.

1Wakorintho 7:32 “Lakini nataka msiwe na masumbufu. Yeye asiyeoa hujishughulisha na mambo ya Bwana, ampendezeje Bwana;

33 bali yeye aliyeoa hujishughulisha na mambo ya dunia hii, jinsi atakavyompendeza mkewe”.

Lakini ikiwa huwezi kuishi Maisha hivyo, kwa jinsi ulivyoitwa, basi hakikisha unatumika kiuaminifu, hapo utakuwa umekidhi vigezo vya kulichunga kundi , kubatiza, n.k.

Bwana akubariki.

Shalom.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

Ndoa na Talaka

Ndoa ya serikali ni halali?

Je! Shetani anao uwezo wa kuumba, kama Mungu?

Uvuvi bora hauchagui wa kuvua.

Askofu na mchungaji mkuu ni nani?

WANA-NDOA: Baba Mkwe, Na mama Mkwe.

Rudi nyumbani

Print this post

Wayebusi walikuwa ni watu gani?

Wayebusi walikuwa ni “wana wa Kaanani”. Kujua Wakaana walikuwa ni watu gani unaweza kufungua hapa >> Wakaanani.

Lakini Watoto wa Kaanani ndio walikuwa hawa “Wayebusi”. Hivyo Wayebusi hawakuwa kabila kubwa, ukilinganisha na Kaanani, baba yao, na waliishi katika sehemu ndogo tu ya nchi ya Kaanani.

Mwanzo 10:15 “Kanaani akamzaa Sidoni, mwanawe wa kwanza, na Hethi,

16 na MYEBUSI, na Mwamori, na Mgirgashi ”.

Wayebusi kama walivyokuwa Wakaanani na Wahivi, na Wahiti, walikuwa ni watu wanaoabudu miungu, na kufanya mambo ambayo yalikuwa ni machukizo mbele za Bwana, kwani walikuwa wanafanya uchawi, wanaloga, wanawapitisha wana wao kwenye moto kama sadaka kwa miungu yao n.k

Kumbukumbu 18:9 “Utakapokwisha kuingia katika nchi akupayo Bwana, Mungu wako usijifunze kutenda kwa mfano wa machukizo ya mataifa yale.

10 Asionekane kwako mtu ampitishaye mwanawe au binti yake kati ya moto, wala asionekane mtu atazamaye bao, wala mtu atazamaye nyakati mbaya, wala mwenye kubashiri, wala msihiri,

11 wala mtu alogaye kwa kupiga mafundo, wala mtu apandishaye pepo, wala mchawi, wala mtu awaombaye wafu.

12 Kwa maana mtu atendaye hayo ni chukizo kwa Bwana; kisha ni kwa sababu ya hayo Bwana, Mungu wako, anawafukuza mbele yako.

13 Uwe mkamilifu kwa Bwana, Mungu wako.

14 Maana mataifa haya utakaowamiliki huwasikiliza wanaoshika nyakati mbaya na kutazama bao; bali wewe, Bwana, Mungu wako, hakukupa ruhusa kutenda hayo”.

Kutokana na machukizo hayo, Mungu aliwaondoa katika nchi ya Kaanani, kama alivyowaondoa wakaanani wenyewe Pamoja na Wahivi na Wahiti.

Lakini hata baada ya kuondolewa na Yoshua, walisalia wachache waliokaa katika baadhi ya miji..na mojawapo ya mji waliokuwa wanakaa ni Yerusalemu.

Yoshua 15:63 “Tena katika habari ya Wayebusi, hao wenye kukaa Yerusalemu, wana wa Yuda hawakuweza kuwatoa; lakini hao Wayebusi walikaa pamoja na wana wa Yuda huko Yerusalemu hata hivi leo”.

Mji wa Yerusalemu hapo kwanza, kabla haujaitwa Yerusalemu, ulikuwa unaitwa YEBUSI, kufuatia jina la hawa Wayebusi, na ulikuwa unakaliwa na hawa Wayebusi, lakini baadaye kipindi cha wafalme, Daudi alikuja kuutwaa na kuwaondoa katika mji huo na kuuita Yerusalemu..

Waamuzi 19:10 “Lakini huyo mtu hakukubali kukaa usiku huo, ila akainuka, akaenda zake, akafika mkabala wa Yebusi (huo ndio Yerusalemu); nao walikuwako pamoja naye punda wawili waliotandikwa; suria yake naye alikuwa pamoja naye”.

2Samweli 5:6 “Kisha mfalme na watu wake wakaenda Yerusalemu ili kupigana na Wayebusi, wenyeji wa nchi ile; hao ndio waliomwambia Daudi, wakisema, Usipowaondoa vipofu, na viwete, hutaingia humu kamwe; huku wakidhania ya kuwa Daudi hawezi kuingia humo”.

Jamii ya Wayebusi, sasa haipo tena, imepotea kabisa..Na Bwana ndiye aliyeipoteza, kutokana na Machukizo waliyokuwa wanayafanya!.

Na kama maandiko yanavyosema, Bwana Mungu ni yule yule, jana, leo na hata milele, habadiliki..Maana yake ni kwamba aliyokuwa anayachukia enzi hizo ndiyo anayoyachukia mpaka leo. Kama aliwatowesha Wayebusi na wakaanani, basi atawatowesha pia watu wafanyayo hayo, katika siku za mwisho.

Na nyakati hizi za mwisho, maasi yamekuwa makubwa kuliko hata waliokuwa wanayafanya Wayebusi na Wakaanani.

Hadi leo watu wanaua Watoto wao, (kwa kutoa mimba na kafara), hadi leo watu wanafanya uchawi na ushirikina n.k, mambo hayo ndio yanayotujulisha kuwa tunaishi katika siku za Mwisho, na ghadhabu ya Mungu inakaribia kumwagwa duniani kote.

Lakini hekima ya Mungu inatuonya tutoke katika vifungo vya dhambi, kwa kumpokea Mwana wa Mungu, Yesu Kristo, na kubatizwa kwa jina lake na kwa Roho wake, ili tuokoke na ghadhabu ijayo.

Matendo 2:40 “Akawashuhudia kwa maneno mengine mengi sana na kuwaonya, akisema, Jiokoeni na kizazi hiki chenye ukaidi”.

Maran atha

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312


Mada Nyinginezo:

Wakaanani walikuwa ni watu gani?

Wahiti ni watu gani?

Ni kweli Paulo alipuuzia maonyo aliyopewa ya kwenda Yerusalemu?

Ni wayahudi wa aina gani wanaotajwa kuwa sinagogi la shetani? (Ufunuo 2:9, Ufunuo 3:9)

Nini maana ya ombeni kukimbia kwenu kusiwe wakati wa baridi wala siku ya sabato?.

Rudi nyumbani

Print this post

JIHUDHURISHE, ILI AANZISHE MAZUNGUMZO NA WEWE

Nakusalimu katika jina la mwokozi wetus Yesu Kristo, sifa na utukufu vina yeye milele na milele. Amina.

Unafahamu kuwa shetani ambaye ni adui yetu, si kila wakati anafanya mambo yake kwa kutegemea jitihada zake tu, anajua  kabisa mambo mengine huwa hayatoki isipokuwa kwa kufuata kanuni ambazo tayari Mungu alishaziweka.

Na huwa anazitumia hizo kanuni, kutuharibu sana, lakini sisi kama wana wa ufalme, hatuzitumii kumuharibu yeye.

Kwamfano madhara aliyopanga kumletea  Ayubu, alitambua kuwa haiwezekani kwa njia ya kawaida kuyatekeleza ,. Ndipo akatumia njia ya juu Zaidi ya kujishusha, kwa kwenda KUJIHUDHURISHA mbele za Mungu,.

Akashusha kiburi chake hadi chini kabisa, akaungana na Malaika watakatifu wa Mungu, kupanda mbinguni, akaenda mbele ya uwepo wa Mungu, kwa unyenyekevu wote, akitumaini kuwa kwa kutenda kule, ni lazima tu Mungu atamwangalia, kwasababu Mungu ni Mungu wa uumbaji wote.

Na kweli baadaye Mungu alipomwona anatembea tembea mbele ya uwepo wake kwa muda mrefu, akaanzisha mazungumzo naye, Akamuuliza unatoka wapi shetani, akasema duniani, katika mizunguko yangu, ndipo shetani akatumia fursa hiyo ya mazungumzo, kupeleka na mashataka yake yote. Na mwisho wa siku akapatiwa haja yake.

Akashuka chini, akamfanya Ayubu kama alivyoweza kumfanya..

Ayubu 1:6 “Ilikuwa, siku moja ambayo hao wana wa Mungu walikwenda kujihudhurisha mbele za Bwana, Shetani naye akaenda kati yao.

7 Bwana akamwuliza Shetani, Umetoka wapi wewe? Ndipo Shetani akamjibu Bwana, na kusema, Natoka katika kuzunguka-zunguka duniani, na katika kutembea huku na huku humo.

8 Kisha Bwana akamwuliza Shetani, Je! Umemwangalia huyo mtumishi wangu Ayubu? Kwa kuwa hapana mmoja aliye kama yeye duniani, mtu mkamilifu na mwelekevu, mwenye kumcha Mungu na kuepukana na uovu”.

Tunachopaswa tujue ni nini, Ikiwa mungu wa dunia hii, anajua siri ya mafanikio ya uharibifu wake, haitegemei tu nguvu zake mwenyewe, bali pia kwa kujihudhurisha mbele za Mungu ..Unategemea vipi wewe na mimi tusiwe watu wa namna hiyo?

Shetani anatushangaa sana, tunapomkimbia Mungu, anatushangaa sana tunapokwenda mbali na uwepo wa Mungu, kwa visingizio visivyokuwa na maana, hatutaki kwenda kumfanyia Mungu ibada hata mara moja kwa wiki tunasema tumechoka, kwasababu jumatatu tunakwenda kazini hivyo hatuna budi tulale!! Ndugu ukitegemea nguvu zako kuyaongoza haya Maisha jihesabie tu wewe ni MKIA Maisha yako yote. Ndivyo ilivyo..

Hilo shetani alijaribu akaona halifai, na wewe unalijaribu, alijua si kila wakati nitajiamulia tu mimi mwenyewe, kwa nguvu zangu..Lazima niwe na muda wangu wa kwenda kujinyenyekeza, tena kwa muda mrefu mbele za Mungu.

Ikiwa tunaona mikesha ni shida, hata mara moja kwa mwezi, tusahau Mungu kuanzisha mazungumzo yoyote na sisi. Ikiwa hatujizoezi kusali mara kwa mara, na kuutafuta uso wa Mungu hata kwa mifungo wakati mwingine, tujue tu mambo mengi sana tutafeli kuyatimiza maishani mwetu.

Faida za kujihudhurisha mbele za Bwana ni zipi?.

Tunapokuwa uweponi mwa Bwana muda mrefu, Mungu mwenyewe ataanzisha mazungumzo na sisi, atatuuliza, unasumbukia nini, una haja gani, unatafuta nini? Kama tu alivyofanya kwa shetani…Lakini akitutazama hatupo uweponi mwake, Tunazunguka zunguka tu duniani, na masumbufu ya Maisha haya kila wakati, siku saba kwa juma, siku 365 za mwaka, na yeye ataendelea na mambo yake, atatuacha tutaabike wenyewe..

Biblia inasema..

Yakobo 4:8 “Mkaribieni Mungu, naye atawakaribia ninyi..”

Ndugu tujizoezi, kumkaribia Mungu kila siku, ibada inayotoka rohoni iwe ni sehemu ya Maisha yetu, Na bila shaka tutaanza kumuona Mungu akisema na roho zetu.

Kumbuka uanzapo kufanya mambo kama hayo kwa bidii, hutasikia sauti kama sauti ikisema na wewe, bali rohoni Mungu atakuwa anazungumza na Maisha yako. Na mara utaona yote uliyokuwa unamwomba, au unayatamani yatendeke tangu zamani, Mungu anakufanikisha kwa njia ambazo hujazitazamia. Hivyo ndivyo Mungu anavyozungumza na watu.

Tukiijua kanuni hii, shetani atatuchukia sana, kwasababu tutakuwa tumeshajua siri ya mafanikio yetu, kama yalivyokuwa yake katika huu ulimwengu.

Kama wewe ni mtakatifu, anza sasa kumpa Mungu muda wako wa kutosha, huko ndiko kujihudhurisha mbele zake, usiwe na udhuru wa kutokwenda ibadani, usiwe na udhuru wa kutohudhuria mikesha na wenzako, usiwe na udhuru wa kutokufunga na kuomba, na kujifunza Neno kila siku. JIHUDHURISHE kwa kadiri uwezavyo mbele za Mungu.

Ndivyo Mungu atakavyoanzisha mazungumzo na wewe.

Bwana akubariki.

Ikiwa bado upo nje ya Kristo, kumbuka kuwa, hatuna muda mrefu hapa duniani, Unyakuo ni wakati wowote, kulingana na kutimia kwa dalili zote zilizotabiriwa katika maandiko, na kama hilo halitoshi fahamu kuwa mlango wa neema, umeshaanza kufungwa, usipoiamini injili, leo, kesho itakuwa ni ngumu Zaidi, na siku moja hutaiamini kabisa. Kwasababu neema haidumu milele, maandiko yanasema hivyo!.

Hivyo tubu dhambi zako kwa kumaanisha leo, mgeukie Kristo, injili tuliyobakiwa nayo sasa sio ya kubembelezwa, ni wewe mwenyewe uone hali halisi, umgeukie muumba wako.

Maran Atha.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

TUSIRUHUSU MAMBO YA KUSUBIRISHA, YAVURUGE MUDA WETU NA MUNGU.

Amin, nawaambia, Kizazi hiki hakitapita..

Je! Shetani anao uwezo wa kuumba, kama Mungu?

“Vya Kaisari mpeni kaisari”  ni vipi hivyo tunavyopaswa tumpe?.

Rudi nyumbani

Print this post

Wakaanani walikuwa ni watu gani?

Wakaanani walikuwa ni watu wanaoishi katika nchi ya Kaanani. Kumbuka Kaanani alikuwa ni mtu, ambaye tunamsoma katika Mwanzo 9:18, kuwa alikuwa ni mwana wa Hamu, ambaye aliuona utupi wa baba yake.

Mwanzo 9:18 “Wana wa Nuhu waliotoka katika safina, ni Shemu, na Hamu, na Yafethi; na HAMU ndiye BABA WA KANAANI”.

Wakaanani ndio watu waliokuwa wanamiliki sehemu kubwa ya Israeli, kabla wa nawa Israeli hawajaingia nchi hiyo, ndio maana nchi ya Israeli hapo kwanza ilikuwa inaitwa nchi ya Kaanani, kwasababu hao wakaanani, ndio walikuwa wameshikilia sehemu kubwa ya nchi hiyo, Zaidi ya mataifa mengine machache kama Wahiti, Wahivi na Wayebusi.

Wakaanani walitawala ardhi ile kuanzia Kusini mwa nchi ya Lebanoni, mpaka karibia na mipaka ya nchi ya Misri.

Wakaanani walikuwa ni watu waliokuwa wanaabudu miungu, hivyo desturi zao zilifarakana na sheria wa Mungu wa Israeli, kwani walikuwa ni wachawi, watu wanaobashiri, wanaojichora, wanaotazama nyakati za hatari, wanaowapitisha Watoto wao kwenye moto kwaajili ya sadaka kwa miungu yao. N.k.

Kwasababu ya machukizo hayo, ambayo pia yalichangiwa na laana Mungu aliyomlaani Hamu, kwa kosa la kuuona uchi wa Baba yake, ndipo Mungu akawaondoa katika nchi hiyo na kuwapa wana wa Yakobo (yaani wana wa Israeli).

Kumbukumbu 18:9 “Utakapokwisha kuingia katika nchi akupayo Bwana, Mungu wako usijifunze kutenda kwa mfano wa machukizo ya mataifa yale.

10 Asionekane kwako mtu ampitishaye mwanawe au binti yake kati ya moto, wala asionekane mtu atazamaye bao, wala mtu atazamaye nyakati mbaya, wala mwenye kubashiri, wala msihiri,

11 wala mtu alogaye kwa kupiga mafundo, wala mtu apandishaye pepo, wala mchawi, wala mtu awaombaye wafu.

12 Kwa maana mtu atendaye hayo ni chukizo kwa Bwana; kisha ni kwa sababu ya hayo Bwana, Mungu wako, anawafukuza mbele yako.

13 Uwe mkamilifu kwa Bwana, Mungu wako.

14 Maana mataifa haya utakaowamiliki huwasikiliza wanaoshika nyakati mbaya na kutazama bao; bali wewe, Bwana, Mungu wako, hakukupa ruhusa kutenda hayo”.

Mbali na kwamba Wakaanani walikuwa ni watu WASIOFAA, lakini pia biblia inarekodi kuwa walikuwa ni watu Hodari, wakubwa kimwili na walioendelea sana. Ndio maana utaona Musa alipowatuma watu wakaipeleleze ile nchi yao, wale wapelelezi walikuja na ripoti za kuogopesha, kwani walijiona nafsi zao kama mapanzi mbele ya hao Wakaanani.

Hesabu 13:32 “Wakawaletea wana wa Israeli habari mbaya ya ile nchi waliyoipeleleza, wakasema, Ile nchi tuliyopita kati yake ili kuipeleleza, ni nchi inayowala watu wanaoikaa; na watu wote tuliowaona ndani yake ni watu warefu mno.

33 Kisha, huko tuliwaona Wanefili, wana wa Anaki, waliotoka kwa hao Wanefili; tukajiona nafsi zetu kuwa kama mapanzi; nao ndivyo walivyotuona sisi”.

Jamii ya Wakaanani sasahivi haipo tena, imepotea (Bwana ndiye aliyeitowesha).

Ni nini tunachoweza kujifunza kwa Wakaanani?

Kikubwa tunachoweza kujifunza ni kwamba mafanikio ya mtu au Taifa, sio kigezo cha kukubaliwa na Mungu.

Wakaanani walikuwa wameendelea kuliko Israeli, walikuwa na sayansi kubwa kuliko Israeli na mataifa mengi, lakini Mungu aliwaondoa katika ile nchi na kuwatowesha kabisa kwasababu walikuwa wanafanya machukizo.

Hiyo ni kutukumbusha na sisi watu wa siku za mwisho kuwa, Mafanikio ya kimwili sio kigezo cha kukubaliwa na Mungu. Leo hii kipimo cha kwanza cha mtu aliyebarikiwa na Mungu ni kiwango cha mali alicho nacho, na fedha alizonazo.. lakini Si utakatifu tena..

Bwana Yesu alisema..

Marko 8:36 “KWA KUWA ITAMFAIDIA MTU NINI KUUPATA ULIMWENGU WOTE, AKIPATA HASARA YA NAFSI YAKE?

37 Ama mtu atoe nini badala ya nafsi yake?

38 Maana kila mtu atakayenionea haya mimi, na maneno yangu, katika kizazi hiki cha uzinzi na dhambi, Mwana wa Adamu atamwonea haya mtu huyo, atakapokuja katika utukufu wa Baba yake pamoja na malaika watakatifu”.

Na Zaidi sana Neno la Mungu linatuhimiza tuutafute Utakatifu kwa gharama zote, kwasababu pasipo huo hatutamwona Mungu (Waebrania 12:14), Na utakatifu tunaupata kwa kumpokea Roho Mtakatifu ndani yetu.

Maran atha.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312


Mada Nyinginezo:

Wahiti ni watu gani?

Moabu ni nchi gani kwasasa?

Wasamaria walikuwa ni watu gani?

TUMEFANYIKA KUWA WANA WA MUNGU!

Je Adamu na Hawa, walikuwa hawafanyi mema kabla ya kula tunda?

Rudi nyumbani

Print this post

Je vazi alilovikwa Bwana Yesu lilikuwa la Zambarau au Jekundu?

Swali: Tunasoma katika Marko 15:17,na Yohana 19:2  kuwa Bwana alivikwa Vazi la rangi ya Zambarau, lakini tukirudi kwenye Mathayo 27:28 tunaona ni vazi Jekundu, Sasa vazi lipi ni sahihi hapo?.

Jibu: Tusome,

Marko 15:16 “Nao askari wakamchukua ndani ya behewa, ndiyo Praitorio (yaani, nyumba ya uliwali), wakakusanya pamoja kikosi kizima.

17 Wakamvika VAZI LA RANGI YA ZAMBARAU, wakasokota taji ya miiba, wakamtia kichwani;

18 wakaanza kumsalimu, Salamu, Mfalme wa Wayahudi!”.

Tusome tena..

Mathayo 27:27 “Ndipo askari wa liwali wakamchukua Yesu ndani ya Praitorio, wakamkusanyikia kikosi kizima.

28 WAKAMVUA NGUO, WAKAMVIKA VAZI JEKUNDU.

29 Wakasokota taji ya miiba, wakaiweka juu ya kichwa chake, na mwanzi katika mkono wake wa kuume; wakapiga magoti mbele yake, wakamdhihaki, wakisema, Salamu, Mfalme wa Wayahudi!”

Sasa kwa mistari hii miwili ni rahisi kusema kuwa biblia inajichangaya.. lakini biblia kamwe haijichanganyi, kinachojichanganya ni fahamu zetu.

Sasa tukirudi kwenye hiyo mistari ni kwamba zamani mavazi waliyokuwa wanavaa watu wenye heshima, au mamlaka Fulani, yalikuwa ni ya rangi ya zambarau iliyochanganyikana na rangi nyekundu. Sehemu kubwa ilikuwa ni rangi ya Zambarau na sehemu ndogo ni nyekundu. Hivyo mtu atakayelitaja kama vazi la Zambarau au kama vazi jekundu, anakuwa hajakosea..

Kwa mfano unaweza kusoma…

Ufunuo 17:4 “Na mwanamke yule alikuwa AMEVIKWA NGUO YA RANGI YA ZAMBARAU, NA NYEKUNDU, amepambwa kwa dhahabu, na kito cha thamani, na lulu, naye alikuwa na kikombe cha dhahabu mkononi mwake, kilichojawa na machukizo, na machafu ya uasherati wake”.

Pia unaweza kusoma Ufunuo 18:16, Luka 16:19.

Kwahiyo Marko na Mathayo…wote walikuwa sahihi..isipokuwa kila mmoja kaelezea rangi, iliyokuja ya kwanza kichwani mwake.

Lakini Zaidi sana tunachoweza kujiuliza ni kwanini Bwana wamvike vazi lile la Zambarau na nyekundu? Na si la rangi nyingine?.. Jibu ni kama tulivyojifunza hapo juu kuwa mavazi hayo yalivaliwa na watu wenye cheo au wafalme au mamalkia.. Kwahiyo walipomvika vazi hilo lengo lake ni ili wamdhihaki “mfalme wa wayahudi”..kwahiyo ni vazi kama la kumdhihaki ndio maana wakamvika na taji ya miiba, kwasababu watu wanaovaa mavazi kama hayo wanakuwa pia na taji za utukufu!.. Lakini Bwana Yesu walimvika Taji ya miiba.

Sasa kwa urefu juu ya Taji ya miiba, unaweza kufungua hapa >> Taji ya Miiba.

Maran atha!

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312


Mada Nyinginezo:

VAZI LA YESU HALIGAWANYWI.

AKAJIFUNGA VAZI LAKE, AKAJITUPA BAHARINI.

PINDO LA VAZI LAKE SASA LIMEREFUSHWA.

Wale Nyoka wa Moto jangwani, walikuwa ni wa namna gani?

Maana Ya Maneno Katika Biblia.

Rudi nyumbani

Print this post

Wahiti ni watu gani?

Wahiti ni watu gani, na wa Taifa gani kwa sasa?

Biblia haijaeleza kwa urefu, Habari ya Wahiti, lakini kulingana na maandiko, walikuwa ni watu Hodari na waliotawala sehemu ya nchi ya Israeli, katika upande wa kaskazini. Kumbuka Nchi ya Israeli hapo kwanza ilikuwa inakaliwa na watu wa mataifa, ambao ndio hao Wahiti, wengine ni Wayebusi, Wahivi, waperizi na Wakaanani.

Kulingana na historia, Wahiti, hawakumiliki tu sehemu ya nchi ya Israeli, enzi za zamani, bali pia historia inaonyesha walimiliki sehemu ya nchi ya Syria kwa sasa na mashariki mwa nchi ya Uturuki, ambayo zamani ilijulikana kama Asia ndogo.

Wahiti hawakuwa watu waliomwabudu Mungu wa Israeli, bali walikuwa wanaabudu miungu na walikuwa wanaishi katika desturi za kipagani; Na katika biblia kipindi cha Ibrahimu na Isaka, Wahiti walikuwepo tayari katika nchi ile, wanamiliki sehemu ya ardhi, ndio maana utaona Esau mwana wa Isaka alikwenda kujitwalia wake kutoka kwa hawa Wahiti.

Mwanzo 26:34 “Esau alipokuwa mwenye miaka arobaini, akamwoa Yudithi, binti Beeri, MHITI, na Basemathi, binti Eloni, Mhiti.

35 Roho zao Isaka na Rebeka zikajaa uchungu kwa ajili yao”.

Wahiti Pamoja na kwamba waliondolewa katika nchi ya Israeli, wakati waisraeli wanaingia katika nchi hiyo ya ahadi, lakini bado waliendelea kuwepo na kumiliki sehemu nyingine za dunia, na ndio maana utaona wakitajwa hata baada ya wana wa Israeli kurudi kutoka katika uhamisho wa Babeli.

Ezra 9:1 “Na mambo hayo yalipokwisha kutendeka, wakuu wakanikaribia, wakisema, Watu wa Israeli, na makuhani, na Walawi, hawakujitenga na watu wa nchi hizi, wamefanya sawasawa na machukizo yao, yaani, ya Wakanaani, na WAHITI, na Waperizi, na Wayebusi, na Waamoni, na Wamoabi, na Wamisri, na Waamori.

2 Maana wametwaa binti zao kuwa wake zao, na wake za watoto wao; basi mbegu takatifu wamejichanganya na watu wa nchi hizi; naam, mkono wa wakuu na mashehe umetangulia katika kosa hili”.

Wahiti waliondolewa katika nchi ya ahadi na Mungu, kwasababu ya matendo yao ya kipagani, ambayo yalikuwa kinyume na mapenzi ya Mungu.

Kumbukumbu 9:4 “Usiseme moyoni mwako, Bwana, Mungu wako, atakapokwisha kuwasukumia nje mbele yako, ukasema, Ni kwa haki yangu alivyonitia Bwana niimiliki nchi hii; KWANI NI KWA AJILI YA UOVU WA MATAIFA HAYA BWANA AWAFUKUZA NJE MBELE YAKO.

5 Si kwa haki yako, wala kwa unyofu wa moyo wako, hivi uingiavyo kuimiliki nchi yao; LAKINI NI KWA UOVU WA MATAIFA HAYA BWANA, MUNGU WAKO, AWAFUKUZA NJE MBELE YAKO; tena apate kuliweka imara hilo neno Bwana alilowaapia baba zako Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo”.

Wahiti, waliendelea kuwepo miaka mingi, lakini nyakati za agano jipya hatuwaoni wakitajwa tena, ni wazi kuwa jamii hiyo ya watu ilipotea kabisa, mpaka leo hakuna jamii ya Wahiti duniani, kama vile walivyo Israeli.

Ikifunua kuwa wote wasiomcha Mungu, watapotea lakini wote wamtumainio Bwana watadumu milele.

Zaburi 125:5 “Wamtumainio Bwana ni kama mlima Sayuni, Ambao hautatikisika, wakaa milele.

2 Kama milima inavyouzunguka Yerusalemu, Ndivyo Bwana anavyowazunguka watu wake, Tangu sasa na hata milele”.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312


Mada Nyinginezo:

MUME / MKE BORA KUTOKA KWA BWANA UTAMWONA UKIWA KATIKA MAZINGIRA GANI?

MBINGU MPYA NA NCHI MPYA. (Sehemu ya 1)

SOMO no.02 (BINTI WA YEFTHA).

Rudi nyumbani

Print this post

 SWALI: Ni njia gani itumike kuwaongoza mabubu sala ya toba?

JIBU: Tukumbuke kuwa “sala ya Toba” sio wokovu, Sala ya toba ni njia mojawapo, inayotumiwa kuukaribisha wokovu ndani ya mtu, lakini sala kama sala yenyewe sio wokovu, Ikiwa na maana zipo njia nyingine, Na ndio maana huwezi kuona mahali popote mitume waliwaambia watu wafuatisha sala fulani, kwamba kwa hiyo ndio wataokoka..Huwezi kuona.

Wokovu unatoka moyoni. Pale mtu anapojitambua kuwa ni mwenye dhambi, na hivyo anahitaji kukombolewa kutoka katika mauti na Yesu Kristo, kitendo kinachompelekea kuyasalimisha maisha yake yote kwa Bwana Yesu ayaongoze, na kuachana na mambo ya ulimwengu, Huo ndio wokovu.

Sasa jambo kama hili likishatokea ndani ya mtu, udhihirisho wa nje ndio unafuata, ambao mojawapo ndio kukiri kwa kinywa chako, na cha pili ni Matendo yako.

Kutimiza lile andiko la Warumi 10:9

“Kwa sababu, ukimkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu, utaokoka”.

Sasa mabubu, hawajajaliwa kuongea, hawawezi kumkiri Kristo kwa vinywa vyao..Lakini wanaweza kuonyesha kuwa wamemwanini Kristo kwa matendo yao. Wakifanya hivyo tayari huo ni wokovu tosha, kutoka kwa Bwana.. Hivyo mtu kama huyu ikiwa tayari ameshamwani Bwana muhimize tu, aanze kuenenda sawasawa na kuamini kwake.

Tutakumbuka kisa kile cha Yule mwanamke ambaye Bwana Yesu alisema alikuwa na dhambi nyingi, jinsi alivyomwendea na kulia sana miguuni pake, kudhihirisha majuto ya makosa yake, kisha kumpangusa kwa nywele zake, Utaona pale Bwana Yesu hakuzungumza naye maneno yoyote, kwamba njoo nikuongoze sala ya toba, au sema maneno haya au yale, hapana isipokuwa alipoona tu moyo wake wa toba ulivyomaanisha kwelikweli alimwambia.. “Mwanamke umesamehewa dhambi zako”

Luka 7:36-48

 “36 Mtu mmoja katika Mafarisayo alimwalika ale chakula kwake; akaingia katika nyumba yake yule Farisayo, akaketi chakulani.

37 Na tazama, mwanamke mmoja wa mji ule, aliyekuwa mwenye dhambi, alipopata habari ya kuwa ameketi chakulani katika nyumba ya yule Farisayo, alileta chupa ya marimari yenye marhamu.

38 Akasimama nyuma karibu na miguu yake, akilia, akaanza kumdondoshea miguu machozi yake, na kuipangusa kwa nywele za kichwa chake, akiibusu-busu miguu yake na kuipaka yale marhamu.

39 Basi, yule Farisayo aliyemwalika alipoona vile, alisema moyoni mwake, Mtu huyu kama angekuwa nabii, angemtambua mwanamke huyu amgusaye, ni nani, naye ni wa namna gani, ya kwamba ni mwenye dhambi…..

44 Akamgeukia yule mwanamke, akamwambia Simoni, Wamwona mwanamke huyu? Niliingia nyumbani kwako, hukunipa maji kwa miguu yangu; bali huyu amenidondoshea machozi miguu yangu, na kuipangusa kwa nywele za kichwa chake

45 Wewe hukunibusu; lakini huyu tangu nilipoingia hakuacha kunibusu sana miguu yangu.

46 Hukunipaka kichwa changu mafuta; bali huyu amenipaka miguu yangu marhamu.

47 Kwa ajili ya hayo nakuambia, Amesamehewa dhambi zake ambazo ni nyingi, kwa kuwa amependa sana; lakini asamehewaye kidogo, huyo hupenda kidogo.

48 Kisha alimwambia mwanamke, Umesamehewa dhambi zako.

Hii kuonyesha kwamba, pale unaoonyesha geuko la kweli moyoni mwako, kabla hata hujazungumza chochote tayari umeshasamehewa.

Ndivyo ilivyo kwa mabubu, haijalishi hawataweza kukiri sala yoyote kwa vinywa vyao, lakini ikiwa moyoni mwao wameonyesha mabadiliko, hicho ndicho Mungu anachokitaka. Imekuwa desturi leo hii kuona kundi kubwa la watu wanasema wameongozwa sala ya toba na kumkiri Yesu , lakini ukitazama matendo yao hayaendani na walichokikiri. Huo ni unafki ambao unamchukiza Bwana sana.

Mathayo 15:7 “Enyi wanafiki, ni vema alivyotabiri Isaya kwa habari zenu, akisema,

8 Watu hawa huniheshimu kwa midomo; Ila mioyo yao iko mbali nami”.

Bwana anataka tumfuata na tumwabudu katika Roho na kweli. Na sio katika maneno matupu. Ikiwa mtu asiweza kuongea, amesimama katika wokovu, huyo mtu ni wa thamani sana mbele za Mungu

Swali ni je wewe, uliyemkiri Bwana, unayemsifu, unayemuhubiri, unayemtangaza. Je! Ni kweli kitokacho mdomoni mwako, kimeambatana na badiliko la ndani?

Majibu tunayo.

Bwana atusaidie.

Shalom.

Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;

Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

Utasi ni ugonjwa gani? (Marko 7:32).

Kiungo chako kimoja kikikukosesha kikate. Ina maana gani?

Kuongozwa sala ya toba.

Dusumali ni nini katika biblia?

Matoazi na Matari ni nini? (Kutoka 15:20)

Je Malaika Mikaeli ndiye Yesu mwenyewe?

Tofauti kati ya mbinguni, peponi, Kuzimu, Jehanamu, na Paradiso ni ipi?

Rudi nyumbani

Print this post